Monday 9 February 2009

Scolari afukuzwa Chelsea!!!

Klabu ya Chelsea imetangaza kupitia tovuti yake kuwa Meneja wao Luiz Felipe Scolari amefukuzwa kazi ili Klabu ipate changamoto mpya ya kugombea Vikombe ambavyo Timu hiyo ina nafasi ya kuvichukua.
Scolari, ambae alishinda Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa Meneja wa Brazil, aliteuliwa kuwa Meneja wa Chelsea mwaka jana kabla msimu huu haujaanza na alichukua nafasi ya Avram Grant ambae nae alitimuliwa.
Chelsea imetangaza atakaekaimu nafasi hiyo ni Meneja Msaidizi Ray Wilkins.

Tony Adams atimuliwa toka Portsmouth!!

Klabu ya Portsmouth imethibitisha kuwa imemwachisha kazi aliekuwa Meneja wao Tony Adams kufuatia mwenendo mbaya wa Timu.
Tony Adams, aliekuwa Nahodha wa zamani wa Arsenal na Timu ya Taifa ya England, aliteuliwa kuwa Meneja wa Portsmouth mwishoni mwa Oktoba mwaka jana kufuatia kuondoka kwa Harry Redknapp aliehamia Tottenham.
Lakini tangu wakati huo Portsmouth imecheza mechi 16 za LIGI KUU na kushinda 2 tu na kuifanya Timu iwe pointi moja tu juu ya timu zilizo kwnye zoni ya kushuka daraja.
Vilevile, Portsmouth ambao ndio walikuwa Mabingwa Watetezi wa Kombe la FA walitolewa nje ya Mashindano hayo walipofungwa na Timu ya Daraja la chini Swansea kwa bao 2-0.
Jumamosi Portsmouth walifungwa nyumbani kwao na Liverpool kwa bao 3-2 katika mechi waliyokuwa wakiongoza 2-1 huku zimesalia dakika 5 tu!
Portsmouth imetangaza aliekuwa Mkurugenzi wa Vijana Paul Hart ndie atakuwa Meneja wa muda wa klabu wakati wakianza kusaka mtu mpya.

Shaun Wright-Phillips afungiwa Mechi 3!!!

Mchezaji wa Manchester City Shaun Wright-Philips amefungiwa kucheza Mechi 3 na FA baada ya kupatikana na hatia ya kulipiza kisasi kwa kumpiga teke Rory Delap wa Stoke katika mechi Man City walifungwa 1-0.
Kwenye mechi hiyo Rory Delap alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu kumpiga na mpira Shaun Wright-Phillips lakini Refa hakuona jinsi Mchezaji huyo wa Man City alivyolipa kisasi lakini baada ya mechi Refa Martin Atkinson alikiri kama angemwona Shaun Wright-Phillips basi angempa Kadi Nyekundu.
Sasa Shaun Wright-Phillips atazikosa mechi za Timu yake dhidi ya Portsmouth, Liverpool na West Ham

No comments:

Powered By Blogger