Friday, 6 March 2009

Wikiendi hii mchanganyiko LIGI KUU na FA CUP

Baada ya mechi za katikati ya wiki za LIGI KUU ambazo Timu zote vinara, yaani Man U, Chelsea, Liverpool, Arsenal na isipokuwa Aston Villa zilishinda mechi zao, wikiendi hii ni mchanganyiko wa mechi za LIGI KUU na zile za FA Cup.
RATIBA: [Taimu za Bongo]
Jumamosi, 7 Machi 2009
LIGI KUU
Sunderland v Tottenham [SAA 12 JIONI]
FA CUP
Coventry v Chelsea [SAA 9.30 MCHANA]
Fulham v Man U [SAA 2.15 USIKU]
Jumapili, 8 Machi 2009
Arsenal v Burnley [SAA 10.30 JIONI]
Everton v Middlesbrough [SAA 1 JIONI]

Monday, 2 March 2009

LIGI KUU England: Mechi za Wiki hii [taimu ni ya kibongo]
Jumanne, 3 Machi 2009
[Saa 4.45 usiku]
Portsmouth v Chelsea
West Brom v Arsenal
[Saa 5 usiku]
Liverpool v Sunderland
Jumatano, 4 Machi 2009
[Saa 4.45 usiku]
Man City v Aston Villa
Newcastle v Man U
Stoke v Bolton
Wigan v West Ham
[Saa 5 usiku]
Blackburn v Everton
Fulham v Hull
Tottenham v Middlesbrough
Wenger bado ana imani licha ya Timu kuzomewa na Washabiki wao Emirates!!!

Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, ameonyesha kustaajabu kwa nini Mashabiki wa Arsenal wamepoteza imani wakati yeye na Timu yote bado wana imani kubwa na uwezo wao.
Mara baada ya filimbi ya mwisho baada ya pambano la LIGI KUU dhidi ya Fulham lililochezwa Emirates Stadium nyumbani kwa Arsenal kuisha 0-0 ikiwa ni suluhu ya nne mfululizo ya bila magoli kwa Arsenal kwenye ligi, Mashabiki wao waliwazomea Wachezaji wao.
Arsene Wenger amesema: 'Sijui kwa nini Mashabiki hawana imani! Hilo halinisumbui! Kitu muhimu ni kuwa ninaamini tunachofanya ni sawa. Kuzomewa si tatizo, tatizo ni kuwa tunashindwa kushinda mechi tunazotakiwa kushinda!'

Ferguson aitaka Timu kuwa makini!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, baada ya kutwaa taji jingine tena safari hii ikiwa Kombe la Carling, ametaka kikosi chake kuwa makini na kutuliza akili huku wakipigania kutetea Ubingwa wao kwenye LIGI KUU England na UEFA CHAMPIONS LEAGUE pia na wakiwania kulitwaa Kombe la FA.
Ferguson amenena: 'Nina uzoefu mkubwa sana wa kujua Soka ni mchezo katili! Tunaweza kutwaa Vikombe vyote msimu huu lakini pia inawezekana wikiendi ijayo tukaenda kucheza na Fulham na mpira ukambabatiza mtu matakoni na kuingia goli, tumefungwa, tumetolewa nje ya FA Cup! Nani anajua hilo?'
Hata hivyo Sir Alex Ferguson amekiri wikiendi hii imekuwa njema sana kwao baada ya kuwaona wapinzani wao wakubwa Liverpool wakifungwa na hivyo kupoteza pointi muhimu kwenye LIGI KUU na pia Man U kutwaa Carling Cup.
Ferguson alimalizia: 'Kitu muhimu sasa ni kutilia mkazo mechi ya Jumatano tunayocheza ugenini na Newcastle LIGI KUU na kuhakikisha tunashinda'

Kipa Ben Foster wa Man U atoboa siri ya umahiri wa kuokoa penalti Fainali Carling Cup

Golikipa wa Manchester United, Ben Foster ]25], kawaida ni Kipa wa Akiba lakini alicheza Fainali ya Carling Cup dhidi ya Tottenham jana kufuatia msimamo wa Bosi wao Sir Alex Ferguson kuchezesha chipukizi na wale wasiokuwa na namba kwenye Kikosi cha Kwanza kwenye mashindano hayo ya Kombe la Carling.
Ben Foster aliibuka shujaa wa mechi hiyo na kuondoka na Tuzo Maalum ya Mchezaji Bora wa fainali hiyo na pia kuibua tena zile imani kuwa yeye ndie Kipa Bora wa England, msimamo ambao wengi walikuwa nao lakini ukafifia kwani Foster alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuumia goti.
Foster ametoboa kuwa kilichomsaidia kuukoa penalti ya kwanza ya Tottenham iliyopigwa na Jamie O'Hara ni kwa sababu yeye na Kocha wa Makipa wa Man U Eric Steele, kabla ya penalti kupigwa, walikuwa wanacheki iPod [kifaa sawa na simu ya mkononi kinachorekodi na kuchezesha video] iliyokuwa na Wachezaji mbalimbali wa Tottenham wakiwa wanapiga penalti.
Hivyo, Foster alidai, walijua O'Hara akipiga basi atapiga juu kidogo na kushoto kwake na hilo kweli lilitokea.

Sunday, 1 March 2009

Manchester United washinda Carling Cup!!

Dakika 120 hazikutoa hata bao na ikaja tombola ya penalti ndipo Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia, Manchester United, wakafunga penalti 4 huku wapinzani wao wakifunga moja tu na kukosa 2.
Wafungaji wa Man U walikuwa Giggs, Tevez, Ronaldo na Anderson.
Wapigaji wa Tottenham walikuwa Jamie O'Hara ambae penalti yake iliokolewa na Kipa wa Man U Ben Foster, Vedran Corluka alifunga na David Bentley akatoa nje.
Tottenham ndio walikuwa Mabingwa Watetezi wa Kombe hili.
Tangu msimu huu uanze Agosti mwaka jana Man U washatwaa Ngao Ya Hisani na Kombe la Klabu Bingwa Duniani. Na bado wapo kwenye vinyang'anyiro vya Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya huku wakiwa wanaongoza LIGI KUU England.

Vikosi vilikuwa:
Man U: Foster, O'Shea [Vidic dak 76], Evans, Ferdinand, Evra, Ronaldo, Scholes, Gibson [Giggs 91], Nani, Tevez, Welbeck [Anderson 56]
Tottenham: Gomes, Corluka, Dawson, King, Assou-Ekotto, Lennon [Bentley 102], Jenas [Bale 98], Zokora, Modric, Bent, Pavlyuchenko [O'Hara 65]
Refa: Chris Foy
LIGI KUU England:
Bolton 1 Newcastle o
Ricardo Gardner aliifungia Bolton bao la ushindi na kuwafanya wapande juu msimamo wa ligi na kuwadidimiza chini Newcastle.
Hull City 1 Blackburn Rovers 2
Leo Blackburn wamejinasua toka nafasi tatu za chini kabisa kwenye msimamo wa ligi kwa ushindi wa bao 2-1 ugenini dhidi ya Hull City.
Mabao ya Blackburn yalifungwa na Stephen Warnock na Keith Andrews. Bao la Hull City alifunga Ian Ashbee.
West Ham 1 Manchester City 0
Bao la kipindi cha pili lililofungwa na Jack Collison katika mechi waliyoitawala kabisa, limewafanya West Ham kupanda hadi nafasi ya 7 kwenye msimamo wa ligi.
Robinho wa Man City alikosa mabao kadhaa na mechi hii ilishuhudia kuumia vibaya kwa Mchezaji wa West Ham Behrami ambae njumu zake zilinasa kwenye majani na enka na goti lake lilionyesha kupinda kabisa na ilibidi mechi isimame kwa dakika sita huku akipewa huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na hewa ya oksijeni.
Baadae alikimbizwa hospitalini.
Aston Villa 2 Stoke City 2
Aton Villa waliongoza bao 2-0 hadi zikiwa zimebaki dakika chache mechi kwisha lakini Stoke City wakajitutumua na kusawazisha huku wakifunga bao la pili lililofungwa na GlennWhelan dakika ya 90.
Aston Villa walipata bao zao kupitia Stiliyan Petrov na John Carew na Stoke walipata kupitia Ryan Shawcross na Glenn Whelan.
Aston Villa wanabaki nafasi ya nne wakiwa pointi 3 nyuma ya Chelsea na Liverpool waliofungana pointi 55 lakini wako pointi 6 juu ya Arsenal walio nafasi ya tano.
Liverpool wazidi kuporomoka, Chelsea wachupa juu yao na Arsenal bado doro!!!

Chelsea walipata goli la ushindi la utata kwenye dakika ya 90 mfungaji akiwa Frank Lampard, goli ambalo Meneja wa Wigan Steve Bruce amelipinga na kudai Mfungaji alimchezea rafu Beki wake Melchiot, na sasa Chelsea wameweza kuwapita Liverpool ambao walifungwa 2-0 na Middlesbrough na hivyo kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa LIGI KUU England.
Chelsea walipata bao lao la kwanza kupitia Nahodha John Terry dakika ya 25 lakini Wigan walisawazisha dakika ya 82 kupitia Olivier Kapo.
Liverpool wakicheza ugenini Riverside nyumbani kwa Middlesbrough timu ambayo mwendo wake hauridhishi walijikuta wakianza kwa balaa pale Mchezaji wao Xabi Alonso alipojifunga mwenyewe kufuatia kona iliyopigwa dakika ya 32.
Tuncay Sanli alipachika bao la pili kwa Middlesbrough dakika ya 63 na kuwafanya Liverpool waporomoke toka nafasi ya pili hadi ya 3 ingawa wako pointi sawa na Chelsea, wote wakiwa na 55, lakini Chelsea ana tofauti ya magoli bora.
Timu hizi sasa zimecheza mechi 27 kila moja huku Manchester United iliyocheza mechi 26 bado inaongoza ikiwa na pointi 62.
Nao Arsenal wameendelea kudorora pale walipotoka suluhu ya 0-0 na Fulham hii ikiwa mechi yao ya nne sasa ya LIGI KUU wakimaliza bila kufunga hata goli moja.
Arsena bado wako nafasi ya 5 wakiwa wamecheza mechi 27 na wana pointi 46. Juu yao wapo Aston Villa waliocheza mechi 26 na wana pointi 51.
.............................Baada ya mechi, NINI WAMESEMA?
Rafael Benitez, Meneja wa Liverpool: 'Nusu saa ya kwanza tulipata nafasi 5 za wazi! Kabla ya mechi hii tulijua kushinda Ligi ni ngumu, sasa ni wazi ni ngumu kabisaaa!!'
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal: 'Tumeanza kupata wasiwasi! Hili ni pigo kubwa kwetu! Tuna ubutu sasa na ni ngumu kusema tatizo ni nini- ama kisaikolojia, au mbinu au ufundi! Nikiongea zaidi tatizo litakuwa kubwa zaidi!'
Powered By Blogger