UTATA WA KUFUTWA KADI NYEKUNDU YA JOHN TERRY: Ferguson aponda uamuzi, Scolari asema hajapata kuona maishani uamuzi wa Refa unafutwa!!
Kufuatia Chelsea kushinda rufaa iliyomfutia Nahodha wake kadi nyekundu aliyopewa Jumamosi iliyokwisha kwenye mechi ambayo Chelsea waliifunga Man City 3-1, kumezuka mzozo mkubwa huko Uingereza kuhusu uhalali wa kuifuta kadi hii.
Refa wa mechi Mark Halsey aliyotoa kadi hiyo nyekundu aliandika kwenye ripoti yake ya mechi kuwa kadi ilitoka kwa sababu ya 'rafu mbaya' na si 'faulo ya kiprofesheni' kama wengi wanavyodai.
Ili mchezaji atolewe nje kwa 'faulo ya kiprofesheni' inabidi awe beki wa mwisho anaemzuia kwa njia isiyo halali mchezaji kwenda kufunga.
Siku hiyo wakati John Terry akitenda kosa hilo nyuma yake alikuwa beki mwenzake Carvalho aliekuwa akija kukaba nyuma na vilevile beki mwingine wa Chelsea Bosingwa alikuwa tayari amefika kumsaidia Terry na Carvalho.
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ameuponda uamuzi huu na kuuita upendeleo uliotokana na shinikizo la Bosi wa Marefa Keith Hackett ambae siku za nyuma ashawahi kukwaruzana na Ferguson.
Ferguson alibwata: 'Hacket alimlazimisha Refa Mark Halsey aifute kadi nyekundu iwe njano lakini refa alipogoma sasa kashushwa na wikiendi hii hachezeshi mechi za LIGI KUU! Atachezesha mechi ya Daraja la Tatu [inaitwa LEAGUE TWO]! Angekuwa mchezaji wa Man U Hackett asingefanya hili!!!'
Wikiendi hii Refa Mark Halsey kapangiwa kuchezesha mechi ya LEAGUE TWO kati ya Chester na Shrewsbury.
Nae Meneja wa Chelsea Luis Felipe Scolari ameshangazwa na uamuzi huo wa kufuta kadi na kusema: 'Hii ni mara ya kwanza katika maisha yangu ya ukocha kuona kadi nyekundu inafutwa na uamuzi wa refa unabadilishwa!! Nadhani ni Uingereza tu hili linatokea!! Nchi nyingine refa ni Mungu!!'
Kama kadi nyekundu ya John Terry ingesimama palepale basi asingecheza mechi ya Jumapili ambapo Chelsea inaikaribisha Man U Stamford Bridge.
Kukerwa kwa Ferguson bila shaka kumezidishwa na ukweli kuwa siku hiyohiyo Jumamosi Beki wake wa kutumainiwa Nemanja Vidic alipewa kadi mbili tata za njano hivyo kupata nyekundu na kutolewa nje ya mechi waliyofungwa 2-1 na Liverpool.
Beki huyo ataikosa mechi ya Jumapili na Chelsea.
Hata hivyo Man U hawakukata rufaa.