Monday, 3 November 2008


Arsenal walia!!!!

Klabu ya Arsenal, inayosifika kwa kutandaza 'soka zuri', imegubikwa na majonzi makubwa kufuatia mwendo wa kusuasua kwenye LIGI KUU hasa baada ya kupoteza mechi kadhaa kutoka kwa 'vibonde'.
Arsenal wameshafungwa na Hull City na Stoke City timu ambazo zimepanda daraja msimu huu.
Kufungwa huko pamoja na kuimwaga mechi ya Jumatano iliyopita walipocheza na majirani na mahasimu wao wakubwa Tottenham wakati wakiongoza mabao 4-2 huku zikiwa zimesalia dakika mbili tu za mchezo tena wakiwa Uwanja wa nyumbani wa Emirates ndiko kulikoleta simanzi, majonzi na sasa nyufa za kutojiamini zimeanza kuonekana.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger. baada ya kufungwa na Stoke City 2-1, alikiri kuwa timu ina udhaifu mkubwa wa kucheza mipira ya juu inayodondoshwa golini kwao. Katika mechi hiyo, 'speshalisti' wa mipira ya kurusha, Rory Delap wa Stoke City, ndie aliesababisha magoli yote baada ya mipira yake ya kurusha kumaliziwa na wenzake.
Baada ya mechi na Tottenham nyota wa Arsenal Emmanuel Adebayor alikubali kuwa kwa 'mtaji huo' klabu yake haiwezi kuchukua ubingwa.
Sasa Nahodha wa timu, William Gallas, amejitokeza kwa kudai ili washinde ni bora Arsenal waachane na kucheza 'soka zuri' badala yake wagangamale kutafuta ushindi.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mchezaji mwingine wa Arsenal beki Gael Clichy aliesema wakati mwingine si vyema kucheza pasi tu ni bora pia kubutua mipira ili kulinda ushindi.
Wiki hii ni wiki muhimu sana kwa Arsenal kwani Jumatano wanacheza kwenye michuano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE watakaporudiana na Fenerbahce ya Uturuki uwanjani Emirates.
Kwenye mechi ya kwanza, Arsenal aliishinda Fenerbahce mabao 5-2 huko Uturuki.
Kisha, Jumamosi, kwenye LIGI KUU, Arsenal watawakaribisha Mabingwa wa LIGI KUU, Man U, uwanjani Emirates.
Kwenye LIGI KUU, Arsenal wanashika nafasi ya 4 wakiwa na pointi 20 kwa mechi 11, Man U wako juu yao nafasi ya 3 wakiwa na pointi 21 ingawa wamecheza mechi moja pungufu [wamecheza 10 tu].
RATIBA LIGI KUU LEO Jumanne, 3 Novemba 2008:

Newcastle v Aston Villa

St James Park, nyumbani kwa Newcastle, leo kutakuwa na mpambano wa LIGI KUU kati ya wenyeji Newcastle na Aston Villa, mechi ambayo itaanza saa 5 usiku saa za Afrika Mashariki.
Newcastle mpaka sasa wana pointi 9 tu kwa mechi 10 walizocheza na wako nafasi ya 20 kwenye msimamo wa ligi, nafasi ambayo ni ya mwisho.
Aston Villa wako nafasi ya 5 wakiwa na pointi 20 kwa mechi 10 walizocheza.
Leo Newcastle wanategemewa kuwachezesha mastaa wao Michael Owens na Nicky Butt ambao wote walikuwa majeruhi.
Refa kwenye mechi atakuwa Steve Bennet.

Bolton 2 Man City 0

Mabao mawili yaliyofungwa mwishoni kipindi cha pili yameiwezesha Bolton kuwafunga Manchester City na hivyo kujikwamua kutoka kwenye nafasi tatu za mwisho za msimamo wa LIGI KUU.
Robinho aliupoteza mpira katikati ya uwanja na Bolton wakapanda kufanya shambulizi la haraka lililomkuta Mjamaica Gardner aliepachika bao kwenye dakika hiyo ya 77. Gardner alikuwa resevu kwenye mechi hii na aliingizwa dakika ya 43 kuchukuwa nafasi ya Riga.
Zikiwa zimebaki dakika 2 mechi kuisha, Gardner alipenyeza krosi murua ambayo katika harakati za kuokoa Richard Dunne wa Manchester City akajifunga mwenyewe.

Sunday, 2 November 2008



UEFA CHAMPIONS LEAGUE: RATIBA YA MECHI ZA WIKI HII

Baada ya mechi zilizochezwa tarehe 21 na 22 Oktoba 2008, yaani wiki mbili zilizopita, LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA itawaka tena moto siku za Jumanne na Jumatano wiki hii. Mpaka sasa kila timu imeshacheza mechi 3 kati ya jumla ya mechi 6.

Timu zipo kwenye Makundi manane ya timu nne kila moja. Timu mbili za juu za kila kundi zitasonga mbele kwenye raundi nyingine ya michuano hii. Timu zitazoshika nafasi ya 3 zitaingizwa kwenye UEFA CUP.

JUMANNE, 4 Novemba 2008 [saa 4 dak 45 usiku]

Anorthosis Famagusta v Inter Milan,

Barcelona v Basle,

CFR Cluj-Napoca v Bordeaux,

Liverpool v Atletico Madrid,

Marseille v PSV,

Roma v Chelsea,

Sporting v Shakhtar Donetsk,

Werder Bremen v Panathinaikos,

JUMATANO, 5 Novemba 2008 [saa 4 dak 45 usiku]

AaB v Villarreal,

Arsenal v Fenerbahce

BATE v Zenit St Petersburg,

Celtic v Man U

Dynamo Kiev v FC Porto,

Fiorentina v Bayern Munich,

Lyon v Steaua Bucuresti,

Real Madrid v Juventus,

MECHI ZA LEO, KESHO na WIKIENDI IJAYO:

JUMAPILI 2 NOVEMBA 2008: Bolton v Man City [saa 1 usiku]

JUMATATU 3 NOVEMBA 2008: Newcastle v Aston Villa [saa 5 usiku]

JUMAMOSI 8 NOVEMBA 2008:

[saa 9 dak 45 mchana]

Arsenal v Man U

Wigan v Stoke City

[saa 12 jioni]

Hull City v Bolton

Sunderland v Portsmouth

West Ham v Everton

JUMAPILI 9 NOVEMBA 2008:

[saa 9 na nusu mchana]

Blackburn v Chelsea

[saa 12 jioni]

Aston Villa v Middlesbrough

Man City v Tottenham

[saa 1 usiku]

Fulham v Newcastle
Vinara Liverpool wapigwa !!!, Chelsea aua !!!, Arsenal auawa !!!, Man U washinda !!!

Mechi za jana za LIGI KUU zilileta msismko ambao hakika utakuwa umeusisimua ulimwengu wa soka na kuwafurahisha baadhi ya mashabiki, kuwavunja moyo wengine na kuwafanya wengine wabaki wakiomba Mungu!
Ni matokeo ambayo polepole yanaanza kuleta picha ni nani wa kuwatolea macho kwenye msimu hu, ni nani hasa wana uchu na Ubingwa.

Tottenham 2 Liverpool 1

Roman Pavlyuchenko, Mrusi aliehamia Tottenham msimu huu, alipachika bao la ushindi kwenye dakika ya 90 na kuvunja rekodi ya Liverpool ya kutofungwa kwenye LIGI KUU msimu huu na vilevile kuwasaidia Chelsea kuwang'oa toka kileleni!
Ushindi huu vilevile umeashiria himaya nzuri kwa Meneja mpya Harry Redknapp ambae ni mechi yake ya tatu tu tangu atue hapo akitokea Portsmouth.
Mechi ya kwanza waliishinda Bolton 2-0 wikiendi iliyopita na Jumatano wakatoka suluhu 4-4 na Arsenal.
Liverpool walianza mechi hii iliyochezwa White Hart Lane, nyumbani kwa Tottenham, kwa kishindo pale walipopachika bao dakika ya 3 tu ya mchezo kupitia Dirk Kuyt na walitawala mechi yote.
Lakini kipindi cha pili mambo yalienda kombo na Liverpool wakajifunga wenyewe bao kupitia Carragher kufuatia kona na akajikuta akipiga kichwa wavuni.

Chelsea 5 Sunderland 0

Chelsea wakiwa kwao Stamford Bridge waliwashindilia Sunderland mabao 5-0 na kuchukua uongozi wa LIGI KUU baada ya Liverpool kufungwa na Tottenham.
Nicolas Anelka alipachika mabao 3 kwenye dakika za 30, 45 na 53, Alex dakika ya 27 na Lampard dakika ya 51.

Stoke City 2 Arsenal 1

Rory Delap na mipira yake ya kurusha jana iliwaua Arsenal baada ya Ricardo Fuller na Seyi Olofinjana kuunganisha mipira hiyo ya kurusha na kutikisa nyavu kwenye dakika za 11 na ya 73.
Gael Clichy aliipatia Arsenal bao lake dakika ya 90 baada ya shuti lake kuwababatiza Wachezaji watatu na kutinga wavuni.

Man U Hull City 3

Man U walitawala mechi hii na kukosa rundo la mabao lilowafanya dakika za mwisho wajikaze sana ili Hull City wasisawazishe.
Man U walijikuta wako mbele 4-1 kwa mabao kupitia Ronaldo aliefunga bao la kwanza lakini Hull wakasawazisha kupitia Daniel Cousin. Michael Carrick akaipatia Man U bao la pili, Ronaldo la tatu na Nemanja Vidic akafunga la nne na kuwafanya Man U wawe burudani mbele kwa mabao 4-1.
Ndipo wakaibuka Hull City kwa kufunga bao la pili kupitia Bernand Mendy na Rio Ferdinand akatoa penalti iliyofungwa vizuri na Geovanni na kufanya gemu kuwa 4-3.

MATOKEO MECHI NYINGINE:

Everton 1 Fulham 0

Luis Saha alifunga bao lake la kwanza tangu ahamie Everton kutokea Man U kwa kichwa kwenye dakika ya 87.

Middlesbrough 1 West Ham 1

Mullins wa West Ham aliipa bao dakika ya 11 lakini Mmisri Mido aliisawazishia Middlesbrough kwenye dakika ya 83.

Portsmouth 1 Wigan 2

Amr Zaki toka Misri aliifungia Wigan bao la kwanza kwa penalti dakika ya 45 lakini Kranjcar akaisawazishia Portsmouth dakika ya 82.
Emile Heskey akaipa ushindi Wigan kwenye dakika za majeruhi.
Hiki ni kipigo cha pili mfululizo kwa timu aliyoiacha Meneja Harry Rednapp aliehamia Tottenham na Timu kuchukuliwa na Meneja mpya Tony Adams.

West Brom 2 Blackburn 2

Andrews alifunga bao la kusawazisha dakika ya 89 na kuwaokoa Blackburn toka kipigoni baada ya West Brom kuongoza kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Bednar, dakika ya 55, na Miller dakika ya 62 ingawa walikuwa ni Blackburn waliopata bao la kwanza kupitia Benni McCarthy toka bondeni Afrika Kusini aliefunga kwa penalti dakika ya 13.
McCarthy alikung'utwa kadi nyekundu baadae kwenye dakika ya 36 ya mechi hiyo baada kupewa kadi mbili za njano.

Powered By Blogger