Saturday, 23 January 2010

KOMBE LA FA: Muuaji wa Man U aitoa nishai Spurs!!
Jermaine Beckford ambae ndie aliefunga bao moja na la ushindi lililoitupa nje ya FA Cup Manchester United leo tena ameibuka shujaa wa Leeds United alipowafungia mabao mawili huko White Hart Lane na kulazimisha sare ya 2-2 na Wenyeji wao Tottenham Hotspurs kwenye mechi ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA.
Mwanzoni mwa mechi hii, Tottenham walikosa kufunga penalti iliyopigwa na Jermaine Defoe na kuokolewa na Kipa wa Leeds Ankergren.
Peter Crouch aliwapa uongozi Tottenham alipofunga bao la kwanza dakika mbili kabla ya mapumziko lakini Leeds wakasawazisha kipindi cha pili dakika ya 52 kupitia mashine yao ya magoli Jermaine Beckford.
Tottenham wakapata bao la pili kupitia Mchezaji alietoka benchi la akiba Roman Pavlyuchenko dakika ya 74 na kuifanya gemu kuwa 2-1.
Ndipo dakika 90 zikakatika na kukaongezwa dakika 5 na ndipo kwenye dakika ya 94 pasi ndefu ikamkuta shujaa Jermaine Beckford ndani ya boksi aliekontroli vizuri na kumchomoka Beki Dawson ambae akamkata Beckford na Refa Alan Wiley hakusita kutoa penalti.
Beckford akafunga penalti hiyo na sasa mechi hiyo itabidi irudiwe nyumbani kwa Leeds Uwanjani Elland Road hapo tarehe 2 Februari.
Rooney aipaisha Man U kileleni!!
• Apachika bao 4!!!
Wayne Rooney leo ameiwezesha Manchester United ikae kileleni mwa LigI Kuu England alipofunga bao zote 4 katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Hull City kwenye mechi pekee ya Ligi iliyochezwa Old Trafford.
Kwa ushindi wa leo, Man United wana pointi 50 kwa mechi 23, Arsenal pointi 48 kwa mechi 22 na Chelsea pointi 48 kwa mechi 21.
Arsenal na Chelsea zote hazitacheza mechi za Ligi wikiendi hii kwa vile wana mechi za Kombe la FA.
Baadhi ya Washabiki wa Manchester United waliohudhuria mechi hiyo walivaa na kupepea skafu za rangi ya kijani na njano ikiwa ishara ya kuwapinga Wamiliki wa Man U Familia ya Glazer kwa kuiingiza Klabu hiyo kwenye madeni na kutosajili Wachezaji wapya.
Rangi hizo za njano na kijana zilikuwa ndizo rangi za Timu ya Newton Heath iliyoanzishwa mwaka 1878 na baadae kubadilishwa jina kuitwa Manchester United.
Bila shaka Mashabiki hao na wengine wote watakuwa wamepozwa roho baada ya kumuona Beki wao stadi Rio Ferdinand akicheza kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kupona maumivu yake na uchezaji wake ulimfurahisha kila mtu.
Hadi mapumziko, Man United walikuwa mbele kwa bao la kwanza la Rooney aliemalizia baada ya mkwaju wa Paul Scholes kutemwa na Kipa Myhill.
Rooney alipachika bao nyingine 3 dakika za 82, 86 na 90.
Vikosi:
Man United: Van der Sar, Rafael, Ferdinand, Evans, Evra [Fabio, 87], Park, Nani, Scholes [Gibson, 72], Fletcher, Owen [Berbatov, 72], Rooney.
Hull City: Myhill, Dawson, Gardner, McShane, Zayatte, Barmby [Mendy, 57], Geovanni [Kilbane, 74], Hunt, Boateng, Fagan, Garcia [Ghillas, 70].
Refa: Steve Bennett
FA CUP: Leo Vigogo wapeta!! 
MATOKEO
[RAUNDI YA 4]
Accrington Stanley 1 v Fulham 3
Aston Villa 3 v Brighton 2
Bolton 2 v Sheffield United 0
Cardiff 4 v Leicester City 2
Derby County 1 v Doncaster 0
Everton 1 v Birmingham 2
Notts County 2 v Wigan 2
Portsmouth 2 v Sunderland 1
Preston 0 v Chelsea 2
Reading 1 v Burnley 0
Southampton 2 v Ipswich 1
West Bromwich 4 v Newcastle 2
Wolves 2 v Crystal Palace 2
[INAANZA saa 2 na robo usiku]
Tottenham v Leeds United
FA CUP: Jumapili Januari 24
[RAUNDI YA 4]
Scunthorpe v Man City [saa 1 usiku]
Stoke City v Arsenal [saa 10 na nusu jioni]
Man U wakusanya Pauni Milioni 504 kwa mauzo ya Hati za Dhamana
Manchester United wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Pauni Milioni 504 kutokana na mauzo ya Hati za Dhamana na makusanyo hayo yatasaidia ulipaji wa deni la Pauni Milioni 509 linaloikabili Klabu na pia kuwasaidia Wamiliki wa Klabu hiyo Familia ya Glazer kulipia deni lao la Pauni Milioni 202.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United David Gill amekuwa kwenye ziara ya Dunia nzima wiki za hivi karibuni ili kutangaza Hati hizo za Dhamana ambazo zitaendelezwa hadi Februari 2017 na sasa ziara hiyo ya Gill imezaa mafanikio makubwa kwani Hati hizo zimeuzwa kupindukia na kupita matarajio.
Msemaji wa Familia ya Glazer amesema biashara hiyo italeta uwazi hapo Klabuni kwa miaka 7 ijayo na pia kurahisisha uendeshwaji wa Klabu na hivyo kuweza kusajili Wachezaji wapya.

Kesho dabi ya Milan: Inter Milan v AC Milan
Inter Milan na AC Milan kesho saa 4 dakika 45 usiku saa za bongo zitaingia Uwanja uitwao Stadio Giuseppe Meazza, nyumbani kwa Inter, katika pambano la Timu za Mji mmoja la Serie A huku Timu zote hizo zikiwa zinafukuzana kileleni mwa Ligi hiyo ya Serie A.
Inter Milan ndie nambari wani akiwa na pointi 46 kwa mechi 20 na AC Milan ni wa pili akiwa na pointi 40 kwa mechi 19.
Katika mechi ya awali mwanzoni mwa Ligi, Inter iliinyuka AC Milan mabao 4-0 lakini hivi karibuni Inter ikiwa chini ya Meneja machachari Jose Mourinho imekuwa ikiyumba mno na katika mechi zake mbili za mwisho dhidi ya Timu dhaifu Bari na Siena iliponea chupuchupu kufungwa na kuambulia sare.
AC Milan, chini ya Meneja Leonardo, na Ronaldinho aliefufuka tena na Washambuliaji wao hatari , Marco Borriello na Alexandre Pato wakisaidiwa na David Beckham, wamekuwa wakipata mafanikio makubwa hivi karibuni kwa Soka lao zuri.
FA Cup: Ferguson Mtoto kuivaa Chelsea!!

Darren Ferguson, miaka 37, ni Meneja wa Klabu ndogo sana iliyo Daraja la Championship ambalo liko chini ya Ligi Kuu iitwayo Preston North End na pia ni Mtoto wa Meneja maarufu na mwenye mafanikio makubwa kwenye historia ya Uingereza, Sir Alex Ferguson wa Manchester United.
Darren Ferguson leo ataiongoza Preston North End Uwanjani kwao Deepdale kucheza na Vigogo Chelsea kwenye Raundi ya 4 ya Kombe la FA.
Baada ya Chelsea kuifumua Sunderland mabao 7-2 hivi juzi, wengi hawawapi Preston nafasi hata chembe.
Lakini Darren Ferguson anasema: “Reading walikwenda Liverpool wakashinda! Leeds walikuwa Old Trafford wakaifunga Man United! Chelsea hawawezi kuwa wanacheza vizuri kila siku!”
Darren Ferguson alianza kazi ya Umeneja Misimu mitatu iliyopita akiwa na Peterborough Timu aliyoipandisha Madaraja mawili mfululizo hadi kuifikisha Championship Msimu huu na akajiuzulu toka Timu hiyo mwezi Novemba mwaka jana.
Amejiunga na Preston mwanzoni mwa Januari.
Kuhusu Baba yake, Darren Ferguson amekiri anaongea nae kila siku na humpa ushauri lakini amesisitiza yeye hutoa maamuzi peke yake.
Steve Bruce aishambulia Liverpool!!!
Bosi wa Sunderland Steve Bruce ameishambulia vikali Liverpool kwa kumrubuni Straika wao Kenwyne Jones na kutangaza kuwa watamchukua kwa mkopo.
Bruce ameziita habari hizo ni utovu wa nidhamu na zina lengo za kumchanganya Mchezaji wao ili apate matumaini mabovu.
Bruce amesema: “Wao hawajoangea na mtu yeyote wa Klabu hii kuhusu Jones. Wanatangaza kwa umma kumchukua yeye na bila shaka washaongea nae kinyemela! Hivi watafikiriaje sisi tukisema tunamchukua Steven Gerrard kwa mkopo?”
Neville & Tevez waonywa na FA
Nahodha wa Manchester United Gary Neville na Mchezaji wa Manchester City Carlos Tevez wametakiwa wajitahadharishe ili wasichukuliwe hatua na kuadhibiwa kufuatia msuguano kati yao uliotokea kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Carling Cup wiki iliyopita huko City of Manchester Stadium ambako Man City waliifunga Man United 2-1 Mfungaji wa bao 2 za City akiwa Tevez.
Kabla ya mechi Neville alikaririwa akisema kuwa Tevez, ambae aliichezea Man United kwa mkopo kabla ya kuhamia City na ilitakiwa ilipwe Pauni Milioni 25 ili awe Mchezaji wa kudumu wa Man U, hakuwa na thamani ya Pauni Milioni 25 na inaelekea hilo lilimkera Tevez na alipofunga mabao yake kwenye mechi kati ya Timu hizo wiki iliyopita alikuwa akienda kushangilia mbele ya benchi la Man U. Ilidaiwa kuwa wakati Tevez anashangilia Neville alionekana akitoa ishara ya kidole kimoja ambayo wengi hutafsiri ni matusi.
Baada ya matukio hayo kwenye mechi hiyo iliripotiwa kuwa Tevez akihojiwa na TV ya kwao Argentina alimwita Neville ni ‘zuzu’ na ‘mlamba viatu’ na ndio maana kila alipofunga goli alikuwa akienda mbele yake kumkejeli.
FA, ikishirikiana na Polisi wa Manchester, wamekuwa wakijaribu kutuliza na kuipoza hali kabla ya marudiano ya Nusu Fainali ya Carling Cup kati ya Vilabu hivyo vya Jijini Manchester Uwanjani Old Trafford Jumatano ijayo.

Friday, 22 January 2010

Van Nistelrooy kutua West Ham?
Inasemekana West Ham imetoa ofa ya Mshahara wa Pauni Laki 1 kwa wiki ili Straika wa Real Madrid Ruud van Nistelrooy ajiunge kwa mkopo na Klabu hiyo ya Jijini London.
Taarifa hizo zimeenezwa na mmoja wa Wamiliki wapya wa West Ham David Sullivan ingawa hakumtaja kwa jina Straika huyo lakini wadau wanahisi ni Van Nistelrooy ambae kwa sasa hana namba ya kudumu huko Real.
Fergie anataka ushindi kesho ili aukwae uongozi Ligi Kuu
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, anahisi sasa Ligi inaingia hatua muhimu na ushindi kwa Timu yake inayocheza na Hull City huko Old Trafford kwenye mechi pekee ya Ligi Kuu hapo kesho ni muhimu sana kwa vile utawafanya waongoze Ligi kwa pointi 2 mbele ya Arsenal na Chelsea wanaofungana kwa pointi kileleni mwa Ligi hiyo.
Ferguson amesema: “Ukishinda mechi zako, uko kileleni! Ni nafasi nzuri kuwepo! Itazame Arsenal, wameshinda mechi zao za hivi karibuni, sasa wako juu wakati watu wengi waliwafuta kwenye Ligi!”
Ferguson pia aliongeza kuwa ushindi kwao ni muhimu hasa kwa vile wikiendi inayofuata watakuwa Emirates kupambana na Arsenal na amesema: “Ni nafasi nzuri kwetu kesho kwani Jumapili ijayo tuko na Arsenal na hiyo ni mechi kubwa! Kisha wiki inayofuata Arsenal wanacheza na Chelsea!! Hizi ni nyakati zinazovutia!!”
Ferdinand kesho ndani ya Old Trafford!!
Hajacheza Miezi mitatu sasa lakini kesho Beki mahiri wa Manchester United na England, Rio Ferdinand, atashuka na Klabu yake kupambana na Hull City kwenye mechi ya Ligi Kuu kama ilivyothibitishwa na Meneja wake Sir Alex Ferguson.
Ferguson ametamka: “Rio amekuwa akifanya vizuri mazoezini. Atacheza Jumamosi.”
Ferdinand amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo yaliyokuwa pia yakiathiri misuli za miguu na ilibidi apelekwe Jijini London kwa Speshelisti.
Ferguson vile vile amesema Majeruhi mwingine wa muda mrefu, Owen Hargreaves, kwa sasa yupo kwenye mazoezi makali na Kikosi cha Akiba na jina lake litakuwemo kwenye Listi ya Wachezaji 25 wanaotakiwa kusajiliwa UEFA kwa ajili ya Mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambako Man U watacheza na AC Milan kwenye Raundi ya Mtoano ya Timu 16 mwezi Februari.
KOMBE LA AFRIKA: Ufafanuzi mechi za Robo Fainali ni Misri v Cameroun na Zambia v Nigeria!!!
Sheria za kujikanganya za CAF jana zilijitokeza na kuwapoteza Wadau wengi wakiwemo Waandishi wa Habari na hata Timu ya Gabon ambao mara baada ya mechi yao waliyofungwa 2-1 na Zambia walishangilia wakijua wao ndio wameingia Robo Fainali kwa vile Cameroun walitoka sare 2-2 na Tunisia lakini wakalizwa walipofafanuliwa wao ni ‘auti’!
Awali ilitangazwa Robo Fainali ni Msiri v Zambia na Nigeria v Cameroun ikimaanisha Kundi D Mshindi wa Kwanza ni Cameroun na Mshindi wa Pili ni Zambia lakini sasa CAF imefafanua kuwa katika Kundi hilo Zambia, Cameroun na Gabon zote zilifungana kwa kuwa na pointi 4 kila mmoja na hivyo kilichoamua nafasi ni hizo sheria za kushangaza za CAF za kuchukua matokeo ya mechi za uso kwa uso za Timu zilizofungana ili kuamua nani mshindi.
Hivyo, Zambia ameibuka kama Mshindi wa 1, Cameroun wa 2 na Gabon wa 3 kwa vile katika mechi za kwa uso kwa uso kati ya Timu hizo 3, Zambia ndie alikuwa na magoli mengi ya kufunga.
Matokeo mechi kati yao:
-Gabon 1 Cameroun 0
-Cameroun 3 Zambia 2
-Zambia 2 Gabon 1
Magoli ya kufunga:
-Zambia 4
-Cameroun 3
-Gabon 2
RATIBA ROBO FAINALI:
Jumapili Januari 24:
Angola v Ghana
Ivory Coast v Algeria
Jumatatu Januari 25:
Misri v Cameroun
Zambia v Nigeria
Arsenal yupo kileleni lakini kimbembe chao kinakuja!!!
Wiki 3 zijazo, Mechi 6 zijazo kuamua MBIVU au MBICHI!!!!
Baada ya kuwatungua Bolton mabao 4-2 hapo juzi huku wakipata ‘msaada mkubwa’ wa Refa Alan Wiley na hivyo kukaa kileleni mwa Ligi Kuu, Arsenal sasa ndio wanaingia hatua ngumu mno kwao kwa kukumbana na Vigingi na Vigogo vya kila aina ambavyo wakivishinda basi wanaweza wakatwaa Mataji yao ya kwanza tangu Mwaka 2005 walipotwaa FA Cup kwa mara ya mwisho.
RATIBA YAO YA WIKI 3 ZIJAZO NI:
Jumapili, Januari 24
FA Cup: Stoke v Arsenal
Jumatano, Januari 27
LIGI KUU: Aston Villa v Arsenal
Jumapili, Januari 31
LIGI KUU: Arsenal v Man United
Jumapili, Februari 7
LIGI KUU: Chelsea v Arsenal
Jumatano, Februari 10
Arsenal v Liverpool
Jumatano, Februari 17
UEFA CHAMPIONS LEAGUE: FC Porto v Arsenal
Wikiendi hii ni FA CUP, LIGI KUU ni Mechi 1
Wikiendi hii ni mahsusi kwa Kombe la FA lakini itakuwepo mechi moja tu ya Ligi Kuu ambayo ilipangwa upya baada ya Timu za Manchester United na Hull City kutolewa kwenye Kombe hilo na hivyo Timu hizo zitakutana Old Trafford siku ya Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Jumamosi, 23 Januari 2010
[saa za bongo]
LIGI KUU:
Man United v Hull City [saa 12 jioni}
FA CUP
[RAUNDI YA 4]
[saa 12 jioni isipokuwa ikitajwa]
Accrington Stanley v Fulham
Aston Villa v Brighton
Bolton v Sheffield United
Cardiff v Leicester City
Derby County v Doncaster
Everton v Birmingham
Notts County v Wigan
Portsmouth v Sunderland
Preston v Chelsea [saa 9 dak 45 mchana]
Reading v Burnlaey [saa 9 dak 45 mchana]
Southampton v Ipswich
Tottenham v Leeds United [saa 2 na robo usiku]
West Bromwich v Newcastle
Wolves v Crystal Palace
Jumapili, 24 Januari 2010
FA CUP
[RAUNDI YA 4]
Scunthorpe v Man City [saa 1 usiku]
Stoke City v Arsenal [saa 10 na nusu jioni]

Thursday, 21 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Ni Zambia na Cameroun Robo Fainali!!!
• Timu zakamilika Robo Fainali!!
Zambia wameweza kuwafunga Gabon 2-1 na hivyo kutinga Robo Fainali na huko watakutana na Misri.
Katika mechi nyingine ya Kundi D, Cameroun wametoka sare 2-2 na Tunisia na hivyo nao wameungana na Zambia kuingia Robo Fainali na watakutana na Nigeria.
RATIBA KAMILI YA ROBO FAINALI:
Jumapili Januari 24:
Angola v Ghana
Ivory Coast v Algeria
Jumatatu Januari 25:
Misri v Zambia
Cameroun v Nigeria
O’Shea nje Msimu wote!!
Beki kiraka wa Manchester United John O'Shea atakuwa nje ya uwanja kwa msimu wote baada ya kugundulika tatizo lake la mguu ni kubwa kupita ilivyodhaniwa hapo awali.
O’Shea aliumia mwezi Novemba alipokuwa akiichezea Nchi yake Ireland kwenye mechi ya Mtoano wa Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa.
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amethibitisha habari hizo kuhusu tatizo la John O’Shea na kusema hilo ni pigo kubwa kwa Timu yake hasa ikizingatiwa Mchezaji huyo ni ‘kiraka’ anaecheza nafasi nyingi na kwa sasa alikuwa akihitajika sana kwa vile Man U ina majeruhi wengi hasa safu ya ulinzi.
Gallas kutoadhibiwa!!
Beki wa Arsenal William Gallas amepona kuadhibiwa na FA kwa rafu mbaya aliyochemchezea Mark Davies wa Bolton hapo jana na ambayo ililalamikiwa sana na Meneja wa Bolton Owen Coyle hasa kwa vile tukio hilo lilifuatia Arsenal kusawazisha bao wakati walikuwa nyuma 2-1.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Arsenal walishinda 4-2.
Owen Coyle aliielezea rafu hiyo ya Gallas kuwa ni ‘shambulizi’ lakini Refa Alan Wiley inasemekana amechukulia rafu hiyo kama ni kugongana kwa Wachezaji wawili kwa bahati mbaya na ndio maana hakutoa rafu na wala hakusimamisha mpira wakati Mark Davies akigalagala chini na ndipo Arsenal wakaendelea kwenda kufunga.
Hata Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, alikiri kuwa hiyo ni rafu na pia Refa alipaswa kusimamisha mpira.
Baada ya mechi hiyo Mark Davies alionekana akitoka nje ya uwanja kwa msaada wa magongo.
Carling Cup: FA kuongea na klabu za Manchester ili kupoza mechi ya Nusu Fainali!
Chama cha Soka cha England, FA, kitakutana na Klabu za Manchester United na Manchester City ili kupoza hali tete iliyotawala Mji wa Manchester hasa baada ya mechi ya juzi ya Nusu Fainali kati ya Klabu hizo ambayo Man City iliishinda Man U 2-1 huko City of Manchester Stadium na sasa zitarudiana kwenye mechi ya pili ya Nusu Fainali hiyo huko Old Trafford Jumatano ijayo.
Mbali ya ushabiki wa kawaida wa Mahasimu hao wanapokutana safari hii hali imetiwa chachu na kugombea nafasi ya kwenda Fainali Wembley na pia Mchezaji Carlos Tevez kuihama Man U na kwenda Man City huku akizua mgogoro uliogubikwa na maneno makali tangu ahame.
Tevez huyo huyo ndie aliefunga bao zote mbili katika ushindi huo wa juzi wa Man City na wakati akishangilia alienda mbele ya benchi la Man U na inadaiwa Nahodha wa Man U Gary Neville aliekuwa benchi alimwonyesha Tevez ishara ya kidole kimoja.
Hata hivyo FA imesema haitomchukulia hatua yeyote Gary Neville kwa kukosekana ushahidi madhubuti.
K ufuatia hali hiyo na pia kama tahadhari FA imeamua kuchukua hatua thabiti ili kudhibiti mlipuko wowote.
Arsenal watwaa uongozi wa Ligi Kuu
• Refa azua mzozo!!
Jana Arsenal walikwea kilele cha Ligi Kuu baada ya kuipiga Bolton mabao 4-2 huko Uwanja wa Emirates lakini ilibidi watoke nyuma baada ya kupigwa bao 2-0 katika 28 za kwanza za mchezo.
Bolton walifunga kupitia Gary Cahill na Matthew Taylor kwa penalti.
Arsenal walipata mabao yao kupitia Tomas Rosicky na Cesc Fabregas aliesawazisha kisha Thomas Vermaelen akafunga bao la 3 na Andrey Arshavin akaweka la nne.
Lakini mechi hii ilizua utata mkubwa kwa goli la pili la Arsenal la kusawazisha ambalo lilianza kwa Beki wa Arsenal Gallas kumchezea rafu mbaya na kumuumiza Mark Davies lakini Refa Alan Wiley hakupiga filimbi ya rafu wala kusimamisha mpira na Arsenal wakaenda mbele na kufunga bao lao la pili la kusawazisha.
Meneja wa Bolton Owen Coyle ameiita rafu ya Gallas si rafu bali ni ‘shambulizi!’
Kwa ushindi huo sasa Arsenal wamefungana pointi na Chelsea wote wakiwa na pointi 48 lakini Arsenal yuko mbele kwa tofauti ya magoli.
Hata hivyo Chelsea wamecheza mechi moja pungufu.
Nyuma yao kwa pointi moja yuko Manchester United.
VIKOSI Vilivyoanza:
Arsenal: Almunia, Sagna, Gallas, Vermaelen, Clichy, Fabregas, Denilson, Diaby, Rosicky, Arshavin, Eduardo.
Akiba: Fabianski, Vela, Walcott, Silvestre, Traore, Eastmond, Emmanuel-Thomas.
Bolton: Jaaskelainen, Steinsson, Cahill, Knight, Robinson, Lee, Mark Davies, Muamba, Cohen, Taylor, Kevin Davies.
Akiba: Al Habsi, Samuel, Elmander, Klasnic, Ricketts, McCann, Andrew O'Brien.
Refa: Alan Wiley
Carling Cup: Villa ipo Fainali Wembley!!
• Villa 6 Blackburn 4!!
• Refa pia azua mgogoro!!!
Katika mechi ya pili ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling iliyochezwa jana Park, Aston Villa wameweza tena kuifunga Blackburn safari hii ikiwa ni mabao 6-4 na hivyo kuingia Fainali itakayochezwa Wembley Februari 28 na watakutana na mshindi wa mechi kati ya Manchester United na Manchester City.
Katika mechi ya kwanza, Villa waliishinda Blackburn bao 1-0 huko Ewood Park.
Jana Blackburn walikuwa mbele kwa bao 2-0 ndani ya dakika 26 za kwanza kwa mabao yaliyofungwa na Klasnic lakini Villa wakasawazisha kupitia Warnock na Milner huku bao moja likiwa la utata mkubwa.
Kisha Beki wa kutumainiwa wa Blackburn, Chris Samba, akapewa Kadi Nyekundu na kipindi cha pili Villa wakaongeza mabao kupitia Agbonlahor, Heskey, Young na moja Nzonzi wa Blackburn alijifunga mwenyewe.
Meneja wa Blackburn, Sam Alladyce, amemponda Refa Atkinson kwa kuchangia Timu yake kufungwa.
Alladyce amedai Refa huyo alifumbia macho rafu ya Agbonlahor kwa Ryan Nelsen iliyomfanya Warnock apate mwanya kufunga na pia kumpa Kadi Nyekundu Samba kulikuwa ni uamuzi mkali kupindukia.
Kuyt aipa ushindi Liverpool!!
Mabao mawili yaliyofungwa na Mshambuliaji wa Liverpool ambae siku zote anajituma kupindukia, Dirk Kuyt, yameleta ahueni huko Anfield baada ya kuandamwa na mikosi ya kufungwa na matokeo mabaya kwa Liverpool na hata watu kuanza kumsakama Meneja wa Liverpool Rafa Benitez.
Kuyt aliipa ushindi Liverpool dhidi ya Tottenham katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa jana usiku huko Anfield.

Wednesday, 20 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Nigeria yaungana na Misri Robo Fainali!!
Leo Nigeria wameinyuka Msumbiji mabao 3-0 na kuungana na Misri kutoka Kundi C kuingia Robo Fainali.
Mabao ya Nigeria yalifungwa na Osaze Odemwingie, bao 2, na Obafemi Martins, bao moja.
Misri ndio Washindi wa Kundi hili na Nigeria wamechukua nafasi ya pili.
Nao, Misri, katika mechi yao ya kukamilisha ratiba tu, waliipiga Benin 2-0 kwa mabao yaliyofungwa na Al Muhammad na Emad Moteab.
Robo Fainali zitachezwa Jumapili na Jumatatu ijayo.
Kesho ni Kundi D linacheza mechi zake za mwisho na Gabon ndio wanaongoza Kundi hilo wakiwa na pointi 4, Cameroun pointi 3, Tunisia 2 na Zambia moja tu.
Ili kuingia Robo Fainali, Gabon na Cameroun wanahitaji suluhu tu wakati Tunisia na Zambia ni lazima washinde.
MECHI ZA KESHO Januari 21:
[KUNDI D]
Gabon v Zambia
Cameroun v Tunisia
ROBO FAINALI:
Jumapili Januari 24:
Angola v Ghana
Ivory Coast v Algeria
Jumatatu Januari 25:
Misri v Mshindi wa 2 Kundi D
Mshindi wa 1 Kundi D v Nigeria
Soka England leo:
LIGI KUU: Arsenal wanataka kukaa kileleni!!!
MECHI ZA LEO:
Arsenal v Bolton
Liverpool v Tottenham
Ndani ya siku 3, Arsenal wanakutana tena na Bolton baada ya kuwafunga huko kwao mabao 2-0 siku ya Jumapili na leo wapo nyumbani Emirates Stadium na ushindi wa mabao mawili utawapa Arsenal uongozi wa Ligi Kuu na kuzipiku Manchester United na Chelsea.
Msimamo [Timu zimecheza mechi 21 isipokuwa inapotajwa]
1 Chelsea pointi 48
2 Man Utd pointi 47 [mechi 22]
3 Arsenal pointi 45
4 Tottenham pointi 38
5 Man City pointi 38
Katika mechi ya pili ya Ligi Kuu ya leo, Liverpool wanawakaribisha Tottenham na hii ni mechi ngumu mno kwa Liverpool hasa kwa vile itawakosa Mastaa wao Steven Gerrard na Fernando Torres ambao ni majeruhi.
CARLING CUP: Marudiano ya Nusu Fainali Aston Villa v Blackburn
Leo huko Villa Park, nyumbani kwa Aston Villa, Blackburn wanarudiana na Aston Villa na wanawania kulipiza kisasi baada ya kufungwa kwao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Carling uliochezwa wiki iliyopita.
Mshindi wa leo atatinga Fainali kukutana na Mshindi wa Manchester United au Manchester City hapo Februari 28.
Blackburn, ambao wanasota chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pia walitolewa nje na Aston Villa kwenye Kombe la FA.
Mechi hii itaanza saa 4 dakika 45 usiku saa za bongo.
KOMBE LA AFRIKA leo: Nani kuungana na Misri Robo Fainali?
Leo kuna mechi mbili za Kundi C, Misri v Benin na Msumbiji v Nigeria, zitakazoanza kwa pamoja saa 1 usiku hizi zikiwa ndizo mechi za mwisho za Kundi hili huku tayari Misri ashaingia Robo Fainali na pia kujihakikishia kuwa yeye ni Mshindi wa kwanza wa Kundi.
Ili Nigeria afuzu kuingia Robo Fainali wanahitaji sare tu dhidi ya Msumbiji ambao wao ni lazima washinde ili wajipe matumaini ya kusonga .
Ili Benin wasonge mbele kwanza ni lazima waifunge Misri kisha waombe Mungu Nigeria wafungwe na Msumbiji.
Carling Cup: Kipigo cha mechi ya kwanza, Fergie hajavunjika moyo, aahidi kisago Old Trafford!!!
• Refa kuibeba Man City, Fergie asema: “Kila mtu kaona!!”
Sir Alex Ferguson amegoma kuvunjika moyo kufuatia kipigo cha 2-1 hapo jana katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling iliyochezwa nyumbani kwa Mahasimu wao Manchester City Uwanjani City of Manchester ambako Carlos Tevez alipachika bao 2 na kuwapa ushindi.
Marudiano ni wiki ijayo huko Old Trafford siku ya Jumatano Januari 27.
Fergie amesisitiza: “Tutacheza nyumbani! Itakuwa ni ujinga ikiwa hujipi matumaini kwani tutakuwa ndani ya Uwanja wetu, mbele ya Mashabiki wetu na wao ni Mahasimu wetu na kila Mchezaji wetu anajua hilo!!”
Fergie akazungumzia mechi ya jana na kusema: “Tulicheza vizuri na tulitawala mchezo! Waliposawazisha tiulipoteana kwa robo saa hivi kisha tukatawala kabisa!!”
Kuhusu Tevez, ambae alikuwa Man U kabla kwenda Man City, kufunga bao zote mbili, Ferguson amesema: “Hilo ni soka!! Kuna Wachezaji wengi wamehama kwetu na wakaja kutufunga! Sisi tunaridhika na Wachezaji wetu!”
Katika mechi ya jana, Manchester United ndio walipata bao la kwanza kupitia Ryan Giggs lakini Manchester City wakasawazisha dakika mbili kabla haftaimu baada ya Refa Mike Dean kuwapa penalti wakati rafu yenyewe ilichezwa wazi kabisa nje ya boksi wakati Beki wa Man U Rafael alipomvuta jezi Bellamy.
Tevez alifunga penalti hiyo na kipindi cha pili Tevez tena akafunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 65 kufuatia kona.
Ferguson alikataa kuzungumzia kwa undani kuhusu Refa Mike Dean kuwabeba Man City na akasema kwa mkato: “Sizungumzii hilo! Kila mtu aliona mwenyewe!! Leo maamuzi hayakuwa kwetu, siku nyingine yatakuwa kwetu!!”

Tuesday, 19 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Ghana iko Robo Fainali!!!
Bao la dakika ya 30 la Mwana wa Abedi Ayew Pele, aitwae Ayew, limeifikisha Ghana Robo Fainali baada ya kuwatoa Burkina Faso kwa bao hilo moja.
Burkina Faso walikuwa wakitaka sare tu ili wao ndio wasonge mbele.
Sasa Januari 24 ndio zitakuwa Robo Fainali za kwanza kwa Angola kucheza na Ghana huku Ivory Coast kukutana na Algeria.
Robo Fainali nyingine zitachezwa Januari 25 na tayari Misri yuko huko huku ameshajihakikishia kuwa Mshindi wa kwanza wa Kundi C na hivyo atacheza na Mshindi wa Pili wa Kundi D ambalo wapo Cameroun, Gabon, Zambia na Tunisia.
Mechi nyingine ya Robo Fainali ya hiyo Januari 25 ni kati ya Mshindi Kundi D na Mshindi wa Pili Kundi C ambae pengine ni Nigeria, Benin au Zambia.
MECHI ZA KESHO Januari 20:
[saa 1 usiku, bongo taimu]
[KUNDI C]
Egypt v Benin
Nigeria v Mozambique
KOMBE LA AFRIKA: Burkina Faso v Ghana
Mjini Luanda, Uwanja wa Novemba 11, Ghana leo watajitupa na Burkina Faso ili kuwania nafasi ya kuungana na Ivory Coast toka Kundi B kuingia Robo Fainali.
Lakini baada ya kupigwa 3-1 na Ivory Coast, Ghana hawana njia ila lazima waifunge Burkina Faso ili wasonge mbele.
Burkina Faso, baada ya kutoka droo 0-0 na Ivory Coast, wao sare tu inawatosha kusonga mbele.
Kundi hili limebakiwa na Timu 3 tu kufuatia kujitoa kwa Togo baada ya kupata maafa makubwa ya kushambuliwa risasi kwa Basi lao na kuwaua Kocha Msaidizi na Afisa Habari wao pamoja na Dereva wa Basi hilo walipokuwa njiani kwenda Cabinda.
Mbali ya lazima kupata ushindi tu, Ghana wana matatizo Kambini kwao kufuatia kuumia kwa Nyota wao Michael Essien na Wachezaji kadhaa wengine wakiwa kwenye hati hati.
CARLING CUP: Manchester kuwaka moto leo!!!
Jiji la Manchester leo litakuwa ndani ya hekaheka kubwa kufuatia mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling kuchezwa leo usiku kuanzia saa 5 saa za bongo huko City of Manchester Stadium kati ya Wenyeji Manchester City na Manchester United.
Timu hizi zitarudiana Old Trafford wiki ijayo tarehe 27 Januari.
Hii ni mechi ya 153 kuwakutanisha Mahasimu hao na Man U wameshinda mechi 62, Man City mechi 41 na suluhu 49.
Mara ya mwisho kwa Timu hizi kupambana ilikuwa ni kwenye Ligi Kuu mwanzoni mwa Msimu huu huko Old Trafford na Man U walishinda 4-3.
West Ham yapata Wamiliki wapya!!
David Gold na David Sullivan, ambao waliwahi kuimiliki Klabu ya Birmingham, wameinunua Klabu ya West Ham kwa dau la Pauni Milioni 105.
Ingawa habari hizi hazijathibitishwa rasmi na West Ham lakini duru za karibu ya Klabu hiyo zimehakikisha ukweli wa taarifa hizo na pia kudai kibarua cha Meneja wa Timu hiyo, Gianfranco Zola, kipo salama.

Monday, 18 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Angola na Algeria Robo Fainali!!!!
Angola 0 Algeria 0
Wenyeji wa Mashindano Angola na Algeria zilitoka suluhu ya 0-0 iliyowabeba wote wawili kuingia Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika mechi iliyochezwa Mji Mkuu wa Angola Luanda Uwanjani Novemba 11 na hivyo kuwabwaga nje Mali na Malawi waliokuwa wakipambana katika mechi nyingine.
Kufuatana na sheria za Mashindano hayo, ingawa Algeria na Mali zilimaliza zikiwa sawa wakiwa na pointi 4 kila mmoja na ingawa Mali alikuwa na goli nyingi, ni Algeria amepita kwa vile tu waliifunga Mali Timu hizo zilipokutana.
Mali 3 Malawi 1
Goli mbili za haraka za Kanoute kwenye sekundi ya 40 ya mchezo na Seydou Keita kwenye dakika ya 4 tu pamoja na la 3 la Mamadou Bagayoko yaliipa ushindi Mali wa mabao 3-1 lakini hilo halikuweza kuwafinikisha kuingia Robo Fainali kwani suluhu ya 0-0 ya Angola na Algeria iliwabeba wawili hao kusonga mbele.
Bao la Malawi lilifungwa na Russell Mwafulirwa.
MECHI ZA KESHO Jumanne Januari 19:
[KUNDI B]
Burkina Faso v Ghana
Ivory Coast v Togo [HAMNA Togo imejitoa]
Henry apona rungu la FIFA
Mshambuliaji wa Ufaransa Thierry Henry hatapewa adhabu yeyote na FIFA kufuatia kitendo chake cha kuucheza mpira kwa mkono kisha kumpasia William Gallas alieisawazishia Ufaransa katika muda wa nyongeza dhidi ya Ireland na kuibeba Nchi hiyo kuingia Fainali za Kombe la Dunia.
Ufaransa ilikuwa imeshinda mechi ya kwanza 1-0.
Baada ya kitendo hicho cha Henry kuliibuka mzozo mkubwa huku kukiwa na mbiu ya mechi kurudiwa lakini FIFA iligomea hatua hiyo na badala yake ikapeleka kesi ya Henry kwenye Kamati ya Nidhamu ambayo leo imeamua kuwa hamna misingi yeyote ya kisheria kufuatana na kanuni za FIFA kumwadhibu Henry.
Kanuni za FIFA hutambua tu na huweza kuchukua adhabu ikiwa mtu anazuia kufungwa goli kwa mkono ikiwa yeye si Kipa lakini ipo kimya endapo mtu anatumia mkono kufunga goli.
Mwenyewe Henry aliomba radhi kwa kitendo chake.
HABARI KWA UFUPI:
• Rio kurudi uwanjani Jumatano!!
Beki mahiri wa Manchester United, Rio Ferdinand, ambae hajacheza miezi mitatu sasa inasemekana huenda akaingia dimbani Jumatano wakatika Man U watakapotua City of Manchester Stadium kukwaana na Mahasimu wao Manchester City katika dabi ya mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Carling Cup.
Mechi ya mwisho kwa Rio ilikuwa Oktoba 25 walipofungwa na Liverpool.
• Essien nje Angola!!
Kiungo wa Ghana, Michael Essien, hataweza kucheza tena kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika huko Angola baada ya kuumia goti mazoezini.
Madaktari wamesema Mchezaji huyo itabidi awe nje si chini ya mwezi mmoja.
• Zaki ndani ya Hull City!!!
Straika wa Zamalek ya Misri, Amr Zaki, amesaini kuichezea Timu ya Ligi Kuu England Hull City kwa mkopo hadi mwishoni mwa Msimu.
Zaki aliichezea Wigan kwa mkopo Msimu uliopita lakini hakupata mkataba wa kudumu baada ya kukwaruzana na aliekuwa Meneja wa Wigan wakati huo Steve Bruce.
Zaki ambae pia huchezea Timu ya Taifa ya Misri hayupo Angola na Timu hiyo baada ya kuumia.
• Qatar kuinunua Man U?
Kufuatia ziara yao ya siku 4 huko Doha, Qatar wiki iliyokwisha, kumeibuka stori za Magazeti ya Uingereza kuwa Nchi ya Qatar ambayo ina Utajiri mkubwa hasa wa gesi ipo mbioni kuinunua Klabu ya Manchester United kutoka kwa Wamiliki wake Ukoo wa Kimarekani wa Glazer.
Hata hivyo Mamlaki ya Rasilmali ya Qatar imekataa kuthibitisha habari hizo.
KOMBE LA AFRIKA: Leo kimbembe cha mechi za mwisho Kundi A!!!
• Angola v Algeria na Mali v Malawi
• Nani kusonga Robo Fainali?????
Mechi zote hizi za Kundi A zitachezwa leo kwa pamoja kuanzia saa 1 usiku saa za bongo kwa ile ya Angola v Algeria kuchezwa Uwanja wa Novemba 11 Luanda na Mali v Malawi kuchezwa Uwanja wa Chimandela huko Cabinda.
Angola wanaongoza Kundi hili wakiwa na pointi 4, Malawi na Algeria wana 3 na Mali wana pointi moja tu.
Ili wasonge mbele ni lazima Mali waifunge Malawi lakini hilo pia litategemea matokeo mechi ya Angola na Algeria.
Malawi akimfunga Mali basi moja kwa moja atasonga mbele.
Algeria nao wanahitaji wasifungwe ili wawe na matumaini ya kusonga lakini ushindi ndio utawapa uhakika zaidi.
Wenyeji Angola wanahitaji suluhu tu ili kusonga mbele.
JANA:
• Cameroon 3 Zambia 2
• Gabon 0 Tunisia 0
Cameroun jana wajipa uhai wa kusonga mbele Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa Zambia 3-2 katika mechi ya Kundi D huku Gabon wakizidi kujichimbia kwenye uongozi wa Kundi hili baada ya kutoka sare 0-0 na Tunisia katika mechi zilizochezwa jana.
Kwa matokeo hayo, Gabon wako juu wakiwa na pointi 4, Cameroun ana 3, Tunisia 2 na Zambia 1.
Mechi za mwisho za Kundi hili ni Januari 21 na itakuwa Cameroun v Tunisia na Zambia v Gabon huku Timu zote hizo 4 zina matumaini ya kusonga mbele.
LIGI KUU: Arsenal waipiga Bolton, Wenger ajisifia!!
Baada ya kuichapa Bolton bao 2-0 hapo jana kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa nyumbani kwa Bolton, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ametamba kuwa sasa Timu yake inaanza kukomaa na wana uwezo wa kutwaa Ubingwa.
Ushindi huo umeifanya Arsenal sasa iwe pointi 3 nyuma ya Vinara Chelsea na pointi 2 nyuma ya Manchester United huku wakiwa na mechi moja mkononi ambayo wataicheza Jumatano hii kwao Emirates kwa kucheza tena na Bolton.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Nahodha Cesc Fabregas katika kipindi cha kwanza na la pili na Fran Merida kipindi cha pili.

Sunday, 17 January 2010

Kwingineko ULAYA:
-Italia: Ronaldinho awasha 3 mguuni kwake! Juve yawashwa!! Inter sare!!
-Spain: Barca kidedea, Real kilio!!!
Ronaldinho alifunga bao 3 mguuni kwake na kuiwezesha AC Milan kuinyuka Sienna bao 4-0 leo kwenye mechi ya Serie A huko Italia na hivyo kufanya pengo na Vinara wa Ligi Inter Milan kuwa pointi 6 baada ya Inter Milan kutoka sare 2-2 na Bari hapo jana.
Inter Milan na AC Milan zitapambana kwenye dabi ya Milan wikiendi ijayo.
Nayo Juventus ilifungwa 1-0 na Chievo.
Huko Spain, Mabingwa Barcelona sasa wako pointi 5 mbele ya Real Madrid kwenye La Liga baada ya kuifumua Sevilla 4-0, bao 2 zikipigwa na Lionel Messi.
Na Mahasimu wa Barca, Real Madrid walilizwa ugenini waliponyukwa kibao kimoja na Athletic Bilbao.
LIGI KUU: Blackburn 2 Fulham 0
Blackburn waliokuwa hawajashinda katika mechi 9 zilizopita za Ligi Kuu leo wakiwa nyumbani Ewood Park wameifunga Fulham Timu inayofanya vizuri kwenye ligi kwa mabao 2-0.
Kona ya Benni McCarthy ilizua kizaazaa langoni mwa Fulham na kumdondokea Beki wa Blackburn Chris Samba aliepiga ndochi na kuandika bao la kwanza katika dakika ya 25.
Kipindi cha pili dakika ya 65 kufuatia frikiki ya Benni McCarthy Beki Ryan Nelsen aliunganisha kichwa na kufunga bao la pili.
Kwa ushindi huo Blackburn wako nafasi ya 12 wakiwa na pointi 24 kwa mechi 22 na Fulham wako nafasi ya 9 kwa mechi 21 na pointi 27.
LIGI KUU: Aston Villa 0 West Ham 0
Uwanja wa Villa Park leo umeshindwa kumpata mbabe katika mechi ya Ligi Kuu England kati ya Wenyeji Aston Villa na West Ham baada ya Timu hizi kutoka sare 0-0.
Kila Timu ilikosa mabao kadhaa ingawa hamna hata moja iliyotawala kabisa mchezo huo.
Katika mechi nyingine iliyoanza muda si mrefu uliopita kati ya Blackburn na Fulham mpaka sasa dakika ya 25 Blackburn wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Beki Christopher Samba sekunde chache zilizopita.
Mancini hana ugomvi na Robinho!
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amesisitiza Robinho bado anahitajika na Klabu hiyo licha ya kutokucheza vizuri na jana kulazimishwa kutolewa ingawa aliingizwa kumbadilisha mtu katika mechi ya Ligi Kuu waliyofungwa na Everton 2-0.
Katika mechi hiyo ya jana iliyochezwa Goodison Park, Robinho alikuwa benchi na ilibidi aingizwe dakika ya 8 tu ya mchezo baada ya kuumia kwa Roque Santa Cruz lakini alivurunda vibaya na ilibidi atolewe dakika ya 60 ya mchezo na nafasi yake ichukuliwe na Shaun Wright-Phillips.
Kitendo hicho kilimkera Robinho na alipobadilishwa tu hakuenda kukaa benchi kama ilivyo kawaida bali alienda moja kwa moja vyumba vya kubadilisha jezi.
Mancini ametamka: “Huo si mwisho wa Robinho! Ni Mchezaji mzuri lakini katika Timu hii kila mtu ni lazima afanye bidii na kucheza vizuri!”
Mancini akaongeza katika mechi hiyo na Everton kulikuwa na Mafowadi wengi kina Bellamy, Benjani na Tevez na ilibidi amtoe Robinho.
Robinho alijiunga na Man City mwezi Agosti 2008 akitokea Real Madrid kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 32.5 ambayo ni rekodi Uingereza lakini tangu Mei 2009 hajaifungia Man City hata bao moja.
Hivi karibuni kumekuwa na uvumi kuwa Barcelona itamchukua Robinho.
Mbiu ya kufukuzwa Rafa yapulizwa kwa nguvu!!
• Murphy asema hafai, aondoke!!!
Danny Murphy, Kiungo wa zamani wa Liverpool ambae sasa ni Mchezaji wa Fulham ingawa yeye mwenyewe anadai ni Shabiki wa kutupwa wa Liverpool, amesema maendeleo ya Klabu hiyo yamerudi nyuma tangu aondoke huko mwaka 2004.
Murphy, miaka 32, amesema sasa umefika wakati wa kumtimua Rafa Benitez kwa sababu anaipeleka Klabu hiyo pabaya.
Murphy amehoji kuwa licha ya kuruhusu Alonso aondoke inashangaza kuona pia akiwauza kina Crouch na Bellamy na sasa anamtegemea mtu mmoja tu na ambaye ni Torres.
Murphy amefoka: “Timu hii sasa inategemea watu watatu tu na ni Torres, Gerrard na Carragher! Katika miaka miwili sasa, amefanya maumuzi mabaya mengi ingawa historia inasema alitwaa Ubingwa wa Ulaya na FA Cup! Kwa muda aliokaa Liverpool, sasa hivi ilitakiwa watu waulize Ubingwa wa Ligi Kuu unakuja au la na si watu kugombea kumaliza katika 4 bora na kuingia UEFA CHAMPIONS LEAGUE tu! Na huo Ubingwa hamna Msimu huu! Ni wazi lazima aondoke!”
KOMBE LA AFRIKA: Leo ni leo kwa Cameroun!!!
Cameroun leo wanashuka Uwanja wa Taifa wa Tundavala Mjini Lubango kukwaana na Chipolopolo huku wakiwa wamejeruhiwa baada ya kupigwa kigoli kimoja na Gabon katika mechi ya kwanza.
Zambia wao walitoka sare ya 1-1 na Tunisia.
Hivyo, ili kuhakikisha wana nafasi ya kusonga mbele, Cameroun lazima washinde leo na Kocha wa Cameroun, Mfaransa Paul Le Guen, amesema Timu yake itakuwa makini mno ili kuhakikisha ushindi.
Kocha wa Zambia, Herve Renard, amesema Wachezaji wake watasimama imara mbele ya Cameroun.
Katika mechi ambayo itaitangulia ile ya Cameroun na Zambia hapo Uwanja wa Taifa wa Tundavala, Gabon wanacheza na Tunisia na ushindi kwa Gabon utawapeleka Robo Fainali.
Gabon waliinyuka Cameroun 1-0 katika mechi ya kwanza na Tunisia walienda sare 1-1 na Zambia.
KOMBE LA AFRIKA: Misri yatinga Robo Fainali
Mabingwa Watetezi wa Afrika, Misri, wameingia hatua inayofuata ya Kombe la Afrika baada ya kushinda mechi yao ya pili katika Kundi lao walipoifunga Msumbiji mabao 2-0 hapo jana.
Mabao ya Misri yalifungwa na Dario Khan wa Msumbiji aliejifunga mwenyewe kufuatia krosi ya Ahmed Fathi na la pili alifunga Gedo kwa fataki kali aliyoipiga nje ya boksi.
Mechi ya mwisho ya Misri ni Jumatano watakapocheza na Benin huku Nigeria wakimaliza na Msumbiji.
Powered By Blogger