Thursday 21 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Ni Zambia na Cameroun Robo Fainali!!!
• Timu zakamilika Robo Fainali!!
Zambia wameweza kuwafunga Gabon 2-1 na hivyo kutinga Robo Fainali na huko watakutana na Misri.
Katika mechi nyingine ya Kundi D, Cameroun wametoka sare 2-2 na Tunisia na hivyo nao wameungana na Zambia kuingia Robo Fainali na watakutana na Nigeria.
RATIBA KAMILI YA ROBO FAINALI:
Jumapili Januari 24:
Angola v Ghana
Ivory Coast v Algeria
Jumatatu Januari 25:
Misri v Zambia
Cameroun v Nigeria
O’Shea nje Msimu wote!!
Beki kiraka wa Manchester United John O'Shea atakuwa nje ya uwanja kwa msimu wote baada ya kugundulika tatizo lake la mguu ni kubwa kupita ilivyodhaniwa hapo awali.
O’Shea aliumia mwezi Novemba alipokuwa akiichezea Nchi yake Ireland kwenye mechi ya Mtoano wa Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa.
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amethibitisha habari hizo kuhusu tatizo la John O’Shea na kusema hilo ni pigo kubwa kwa Timu yake hasa ikizingatiwa Mchezaji huyo ni ‘kiraka’ anaecheza nafasi nyingi na kwa sasa alikuwa akihitajika sana kwa vile Man U ina majeruhi wengi hasa safu ya ulinzi.
Gallas kutoadhibiwa!!
Beki wa Arsenal William Gallas amepona kuadhibiwa na FA kwa rafu mbaya aliyochemchezea Mark Davies wa Bolton hapo jana na ambayo ililalamikiwa sana na Meneja wa Bolton Owen Coyle hasa kwa vile tukio hilo lilifuatia Arsenal kusawazisha bao wakati walikuwa nyuma 2-1.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Arsenal walishinda 4-2.
Owen Coyle aliielezea rafu hiyo ya Gallas kuwa ni ‘shambulizi’ lakini Refa Alan Wiley inasemekana amechukulia rafu hiyo kama ni kugongana kwa Wachezaji wawili kwa bahati mbaya na ndio maana hakutoa rafu na wala hakusimamisha mpira wakati Mark Davies akigalagala chini na ndipo Arsenal wakaendelea kwenda kufunga.
Hata Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, alikiri kuwa hiyo ni rafu na pia Refa alipaswa kusimamisha mpira.
Baada ya mechi hiyo Mark Davies alionekana akitoka nje ya uwanja kwa msaada wa magongo.
Carling Cup: FA kuongea na klabu za Manchester ili kupoza mechi ya Nusu Fainali!
Chama cha Soka cha England, FA, kitakutana na Klabu za Manchester United na Manchester City ili kupoza hali tete iliyotawala Mji wa Manchester hasa baada ya mechi ya juzi ya Nusu Fainali kati ya Klabu hizo ambayo Man City iliishinda Man U 2-1 huko City of Manchester Stadium na sasa zitarudiana kwenye mechi ya pili ya Nusu Fainali hiyo huko Old Trafford Jumatano ijayo.
Mbali ya ushabiki wa kawaida wa Mahasimu hao wanapokutana safari hii hali imetiwa chachu na kugombea nafasi ya kwenda Fainali Wembley na pia Mchezaji Carlos Tevez kuihama Man U na kwenda Man City huku akizua mgogoro uliogubikwa na maneno makali tangu ahame.
Tevez huyo huyo ndie aliefunga bao zote mbili katika ushindi huo wa juzi wa Man City na wakati akishangilia alienda mbele ya benchi la Man U na inadaiwa Nahodha wa Man U Gary Neville aliekuwa benchi alimwonyesha Tevez ishara ya kidole kimoja.
Hata hivyo FA imesema haitomchukulia hatua yeyote Gary Neville kwa kukosekana ushahidi madhubuti.
K ufuatia hali hiyo na pia kama tahadhari FA imeamua kuchukua hatua thabiti ili kudhibiti mlipuko wowote.

No comments:

Powered By Blogger