Saturday 17 July 2010

TEMBELEA: www.sokainbongo.com

Arsenal, Chelsea zashinda mechi za kujipima
Katika mechi za kirafiki na za matayarisho kwa ajili ya Msimu mpya, leo Chelsea na Arsenal zilicheza na kushinda mechi zao.
Chelsea iliifunga Crystal Palace kwa bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Michael Essien kwenye dakika ya 60.
Nao Arsenal waliichabanga Barnet FC kwa bao 4-0 na hadi mapumziko Arsenal walikuwa mbele kwa bao 3-0.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Andre Arshavin, dakika ya pili, Simpson, mabao mawili dakika za 16 na 45, na Samir Nasri akafunga dakika ya 75.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Mascherano hana mawasiliano na Liverpool
Meneja mpya wa Liverpool, Roy Hodgson, amesema hana mawasiliano na Kiungo wao Javier Mascherano ambae kwa sasa yuko likizo baada ya kutoka Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia alipokuwa na Nchi yake Argentina.
Hodgson amekuwa akitaka kuongea na Mascherano hasa kwa vile kumekuwa na uvumi mkali anataka kuhama kwenda Inter Milan kuungana na aliekuwa Meneja wa Liverpool, Rafael Benitez.
Pia inadaiwa Klabu nyingine kama vile Chelsea, Manchester City na FC Barcelona zinamuwinda.
Hodgson amesema: “Nimejaribu kuwasiliana na Mascherano lakini hapatikani kwa simu na pia hajibu ujumbe wa simu.”
Mascherano ana Mkataba na Liverpool hadi 2012.
Wakati huo huo, Hodgson amesema ameshakutana na kuongea na Steven Gerrard na Fernando Torres na Wachezaji hao hawauzwi.
Kumekuwa na uvumi pia kuwa Mastaa hao wawili wanataka kuondoka.
Makamu Mwenyekiti wa Kanisa hilo, Win Bijman, amesema: “Watu hawaelewi kwa nini amesimamishwa. Kanisa hapa linajaa kwa ajili yake na Makanisa mengine ni matupu!”
Hata hivyo, sala za Padre Paul Vlaar hazikupokewa kwani Holland ilifungwa 1-0 na Spain waliotwaa Kombe la Dunia.
CHEKI: www.sokainbongo.com
Man United 3 Celtic 1
Mabao ya Berbatov, Danny Welbeck na Tom Cleverly jana yamewapa ushindi Manchester United wa 3-1 dhidi ya Celtic ya Scotland Uwanjani Rogers Centre huko Toronto, Canada katika mechi yao ya kwanza ya ziara yao ya huko Canada, Marekani na Mexico.
Man United ndio walikuwa wa kwanza kupata bao Mfungaji akiwa Dimitar Berbatov dakika ya 34 kufuatia pasi ya Mame Biram Diouf.
Celtic walisawazisha kwa penalti ya Georgios Samaras dakika ya 61 baada ya Wes Brown kumwangusha Straika wa Celtic.
Danny Welbeck alifunga bao la pili dakika ya 74 baada ya kupokea pasi toka kwa Berbatov na dakika ya 86 Cleverly akapachika bao la 3 kwa shuti lililombabatiza Beki na kumbabaisha Kipa Lukasz Zaluska.
Kikosi cha Man United kilichoanza kilikuwa:
Edwin van der Sar, Ryan Giggs, Paul Scholes, Darren Fletcher, Berbatov, Fabio, Rafael, Jonny Evans, Smalling, Obertan, Diouf.
Mechi inayofuata kwa Man United ni huko Philadelphia, Marekani hapo Julai 21 dhidi ya Philadelphia Union.

Friday 16 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com
Barca wakata tamaa kwa Fabregas
Rais wa FC Barcelona, Sandro Rosell, amekiri huenda wasiweze kumchukua Cesc Fabregas kutoka Arsenal kabla Msimu mpya wa 2010/11 kuanza kwa vile Arsenal hawataki kusikia lolote kuhusu kumuuza Nahodha wao.
Rosell ametamka: “Arsenal wanaona kama wanaonewa. Hawataki kusikiliza ofa na wala kumuuza!”
Mwezi uliokwisha, Barca walitoa ofa ya Pauni Milioni 33 kumnunua Fabregas, mwenye umri wa Miaka 23 ambae alianza Soka akiwa mtoto kwenye Chuo cha Barca na kuhamia Arsenal akiwa na Miaka 16, lakini Arsenal waliikataa ofa hiyo.
Rosell alimaliza kwa kusema: “Atatua hapa kama si sasa ni baadae! Tutaona! Lakini hatuwezi kuwa wehu na kulipa pesa ambazo si thamani yake!”
Mkataba wa Fabragas Klabuni Arsenal unakwisha 2015.
Rooney kupandishiwa Mshahara
Mazungumzo ya kuuboresha Mkataba wa Wayne Rooney unaomalizika 2012 yatafanyika mapema Mwezi ujao baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United David Gill kurudi Manchester kutoka ziarani na Timu hiyo huko USA, Canada na Mexico.
Mazungumzo hayo yatafanyika kati ya Gill na Wakala wa Wayne Rooney, Paul Stretford.
Kwa sasa Rooney analipwa Pauni 90,000 kwa wiki na katika Mkataba mpya atakuwa akilipwa Pauni 130,000 kwa wiki na kumfanya awe ndie anaelipwa juu zaidi kupita Mchezaji yeyote hapo Manchester United.
Kabla, Cristiano Ronaldo, aliekuwa akilipwa Pauni 120,000, ndie alikuwa anaongoza akifuata Rio Ferdinand anaepata Pauni 110,000 kwa wiki.
Man City kumnasa Difenda toka Lazio
Manchester City wako mbioni kumchukua Beki wa Lazio kutoka Serbia, Aleksandar Kolarov, kwa Pauni Milioni 17.
Man City wanamtaka Fulbeki huyo wa kushoto anaesifika kucheza kama Gwiji Roberto Carlos ili pia kuchukua nafasi ya Wayne Bridge ambae Kocha Roberto Mancini anahisi si imara sana.
Huyo atakuwa Mchezaji wa nne kwa Man City kumnasa kabla Msimu mpya haujaanza wengine wakiwa David Silva toka Valencia, Yaya Touré toka Barcelona na Jerome Boateng kutoka Hamburg.
Inaaminika hao si Wachezaji wa mwisho kununuliwa kwani juhudi zipo za pia kuwabeba James Milner kutoka Aston Villa na Straika wa Wolfsburg ya Ujerumani, Edin Dzeko.
CHEKI: http://www.sokainbongo.com/


UEFA CHAMPIONS LIGI: Droo Raundi ya 3 yatoka!!
Waliowahi kuwa Mabingwa wa Ulaya mara 4, AFC Ajax, wamepangwa kucheza na PAOK FC ya Ugiriki katika Raundi ya 3 ya Mtoano.
Celtic ya Scotland imepangwa kucheza na FC Braga ya Ureno.
Mechi za Raundi hii zitachezwa Julai 27 na 28 na marudio ni Agosti 3 na 4.
Droo inayofuata:
Droo hii itafanywa Agosti 6 ili kupata Timu zitakazocheza Raundi ya Mchujo kuingia kwenye Makundi na Droo hii itazijumuisha pia Timu za AJ Auxerre, Sevilla FC, Tottenham Hotspur FC, UC Sampdoria na Werder Bremen.
Mechi za Raundi hii ya Mchujo zitachezwa Agosti 17 na 18 na marudio ni Agosti 24 na 25.
Washindi 10 wa Raundi hiyo ya Mchujo wataungana na Timu 22 zitakazoingizwa moja kwa moja kwenye Droo ya kupanga Makundi 8 ya Timu nne nne kila moja.
Miongoni mwa Timu hizo 22 ni pamoja na Manchester United, Chelsea, Mabingwa wa Ulaya Inter Milan, Real Madrid, Bayern Munich, FC Barcelona na kadhalika.
Steji hiyo ya Makundi itaanza kuchezwa tarehe 14 na 15 Septemba na kumalizika Desemba 8.
Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI itachezwa Uwanja wa Wembley, London hapo tarehe 28 Mei 2011.
EUROPA LIGI: Droo ya Raundi ya 3 yatoka, Liverpool kilingeni!
Liverpool itaanza kinyang’anyiro cha kugombea UEFA EUROPA LIGI katika hatua ya Raundi ya 3 ya Mtoano na watakutana na Mshindi kati ya FK Rabotnicki ya Macedonia au FC Mika ya Armenia.
Mechi za Liverpool zitachezwa Julai 29 Uwanjani Anfield na marudiano ni Agosti 5 ugenini.
FK Rabotnicki wameifunga FC Mika 1-0 na marudio ni nyumbani kwa FC Mika huko Armenia.
Waliowahi kuwa Mabingwa mara mbili wa Ulaya, Juventus, wamepangiwa kucheza na Mshindi kati ya Timu ya Ireland Shamrock Rovers FC v Bnei Yehuda Tel Aviv FC ya Israel.
Nao Sporting Clube de Portugal watacheza na FC Nordsjaelland ya Denmark.
Droo inayofuata:
Washindi 35 wa Raundi ya 3 ya Mtoano wataunganishwa na Timu 15 zitakazotolewa Raundi ya 3 ya Mtoano wa UEFA CHAMPIONS LIGI pamoja na Timu nyingine 24 zikiwemo FC Porto, PFC CSKA Moskva, PSV Eindhoven na Aston Villa FC.
Hii itakuwa ni Raundi ya Mchujo kuingia kwenye Makundi na Droo yake itafanywa hapo Agosti 6.
Fainali ya EUROPA LIGI itachezwa Lansdowne Road, Dublin, Ireland hapo tarehe 18 Mei 2011.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Ole amwaga sifa kwa Forlan
Shujaa Veterani wa Manchester United ambae sasa ni Meneja wa Timu ya Rezevu huko Old Trafford, Ole Gunnar Solskjaer, amesema hakushangazwa kwa Diego Forlan kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini.
Ole alikuwepo wakati Staa huyo wa Uruguay anaingia Man United 2002 na kuondoka 2004 ambako alicheza mechi 63 na kufunga bao 10.
Ole Gunnar Solskjaer amenena: “Alipokuwa hapa Diego alikuwa mzuri.  Bahati mbaya wakati huo tulikuwa na Ruud van Nistelrooy akifunga magoli kibao! Na Scholes alikuwa akicheza nyuma tu ya Ruud na yalitengenezwa magoli mengi sana. Na mimi pia nilikuwa wakati mwingine nacheza kama patna wa Ruud. Hayo yote yalimfanya yeye asipate nafasi za kucheza!”
Lakini Solskjaer amekiri Diego Forlan alikuwa Mchezaji mzuri ambae hata Sir Alex Ferguson alikubali aondoke kwenda Spain kwa shingo upande.
Bafana ina Kocha mpya
Msaidizi wa Kocha toka Brazil wa Timu ya Afrika Kusini, Carlos Alberto Parreira, Pitso Mosimane, ameteuliwa kuwa Kocha mpya wa Bafana Bafana kwa Mkataba wa Miaka minne.
Ni Parreira aliewashawishi Chama cha Soka kumteua Mosimane kama Kocha na sasa kazi kubwa mbele yake ni kuiwezesha Afrika Kusini kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazochezwa huko Gabon na Equatorial Guinea kwa pamoja Mwaka 2012 na zile zinazofuata 2013 huko Libya pamoja na kuiingiza Bafana Bafana Fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitachezwa mfululizo 2012 na 2013 kwa vile mfumo utabadilika na kuanzia 2013 zitakuwa zikichezwa Miaka tasa [kila baada ya Miaka miwili] ili zisigongane na Fainali za Kombe la Dunia.
Mosimane amewataka wasaidizi waliokuwa chini ya Parreira kutoka Brazil wabaki ili kumsaidia.
Wasaidiza hao ni Jairo Leal na Francisco Gonzalez.

Thursday 15 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Anelka atoboa mpasuko ndani ya France
Nicolas Anelka, ambae alitimuliwa toka Kikosi cha Ufaransa kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini baada kugombana na Kocha Raymond Domenech, ametoboa kuwa Wachezaji wote walikubaliana kugomea mazoezi baada ya yeye kufukuzwa.
Anelka amepasua hali ndani ya kambi ya France ilikuwa tete na kama isingekuwa yeye basi ni lazima Mchezaji mwingine angelipuka kwa hasira.
Pia, alisema ni Wachezaji wote kwa pamoja walikubaliana kugoma na hakuwepo kiongozi wa mgomo kwani kila mtu aliunga mkono.
Kauli hiyo ya Anelka iliungwa mkono na Mchezaji mwingine, Jeremy Toulalan, ambae alisema kuwa hakukuwa na kiongozi wa mgomo kwa vile hatua hiyo ilikuwa ya pamoja.
Msimamo huo wa Toulalan umepata pongezi toka kwa Anelka alietamka: “Ni ushujaa kwake kusimama na kusema ukweli! Ninasikia fahari kubwa kucheza nae Ufaransa!”
Hata hivyo, Anelka aligeuka mbogo kwa Bixente Lizarazu, Mchezaji wa zamani wa Ufaransa aliekuwemo France iliyochukua Kombe la Dunia 2008, ambae alikaririwa akimponda Anelka kwa kuwa mbinafsi na asiejituma huko Afrika Kusini wakati wa mechi.
Anelka alihoji: “Lizarazu- ni nani? Yeye ni Mchezaji wa zamani tu , aliekosa sifa na kutambuliwa, kwa vile alikuwa kivuli tu mbele ya kina Zinedine Zidane na Christophe Dugarry. Amesahau alikuwa Kombe la Dunia 2002? Sikuchukuliwa na sikusema lolote! Asizungumze kuhusu heshima, haijui huyo!”
Henry….huyooo aaga Ufaransa!!!
Thierry Henry ametangaza kujiuzulu kucheza Ufaransa.
Henry, ambae juzi tu ametangaza kuihama FC Barcelona kujiunga na MLS huko Marekani na Klabu ya New York Red Bulls, ameamua kung’atuka baada ya Miaka 13 ya kuwa na Timu ya Taifa ya Ufaransa.
Mchezaji huyo mwenye Miaka 32 alianza kucheza Ufaransa Mwaka 1997 na alikuwemo kile Kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia Mwaka 1998 na EURO 2000 lakini alikumbwa na kashfa ya kushika mpira na mkono kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Ireland iliyozua bao la kusawazisha kwa Ufaransa na kuifikisha Fainali huko Afrika Kusini.
Na huko Afrika Kusini, hakuwa na wakati mzuri na hakuanza hata mechi moja ya Kikosi cha Ufaransa kilichokumbwa na mzozo mkubwa wa kufukuzwa Anelka, Wachezaji kugoma na kisha kutupwa nje ya Kombe la Dunia wakiwa mkiani chini ya New Zealand kwenye hatua ya kwanza tu ya Makundi.
Henry ameichezea Ufaransa mara 123 na kufunga bao 51 na ndie Mfungaji Bora katika historia ya Timu ya Ufaransa.
Katika taarifa fupi, Henry ametamka: “Huu ndio mwisho wangu kwa Timu ya Taifa.”
CHEKI: www.sokainbongo.com

Maradona apewa dili mpya
Diego Maradona atapewa Mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha Argentina hadi Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2014 zitakazochezwa huko Brazil.
Maradona aliifanikisha Argentina kufika Robo Fainali ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini hivi majuzi na kutolewa na Germany waliposhindiliwa bao 4-0.
Mwenyewe Maradona amekuwa akidokeza ataacha kuifundisha Argentina lakini Rais wa Chama cha Soka, AFA, Julio Grondona, amesema watakutana nae wiki ijayo ili wampe ofa ya Mkataba wa Miaka minne.
Licha ya Wadau wengi Duniani kumwona Maradona kama si Kocha stadi lakini huko kwao Argentina ni kipenzi kikubwa.
Rooney ashinda kesi
Wayne Rooney ameshinda kesi ya madai iliyokuwa ikimtaka alipe Pauni Milioni 4.3 kama fidia kwa kutolipa kamisheni ya mapato yake kwa Kampuni ya Proactive ambao waliwahi kuwa Wakala wake.
Jaji wa Mahakama ya Biashara huko Manchester, Jaji Brendan Hegarty, ametupilia mbali madai ya Proactive.
Proactive walikuwa wakimuwakilisha Rooney tangu 2002 wakati Mwanzilishi wa Kampuni hiyo, Paul Stretford, alipomsaini lakini Stretford alitoka Kampuni hiyo kwa ugomvi Mwaka 2008 na Rooney akaiacha Proactive na kuanza kuwakilishwa na Stretford binafsi.
Mwaka huo 2002, Stretford alipokuwa Proactive alipomsaini Rooney, Mchezaji huyo alikuwa na Miaka 17 na alikuwa akilipwa Pauni 80 kwa Wiki na Everton kwa vile alikuwa bado yupo kama Mwanafunzi Chuo cha Soka na alikuwa bado akiishi nyumba ya Serikali na Wazazi wake.
Lakini, Rooney akaibuka kuwa Staa na kuchukuliwa na Manchester United na kugeuka kuwa Milionea huku akiwa na Mikataba minono ya Matangazo ya Biashara na Kampuni kubwa kama Nike na Coca Cola.
Jaji Hegarty akitoa hukumu yake alisema Mkataba wa Rooney na Proactive ulikuwa ni Miaka minane na ni kinyume na FA ambao hutaka Mikataba kati ya Mawakala na Wachezaji iwe na kikomo cha Miaka miwili tu.
Baada ya hukumu hiyo, Rooney, ambae yuko Barbados vakesheni, alitoa tamko la kutoa shukrani zake na furaha yake kwa ushindi huo.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Heskey ang’atuka England
Straika wa Aston Villa Emile Heskey ametangaza kustaafu kuichezea Timu ya England.
Mchezaji huyo mwenye Miaka 31, aliechezea England mara 62 na kufunga goli 7 tu, alikuwemo Kikosi cha England huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia na kucheza mechi ya kwanza dhidi ya USA na ile na Algeria kisha kupigwa benchi mechi na Slovenia.
Hata hivyo uteuzi wake kwenye Kikosi hicho cha England ulizua mshangao kwa vile Msimu mzima uliopita akiwa na Aston Villa alifunga bao 3 tu.
Fergie adai Wachezaji watarudi bila ‘hengiova’
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema haamini kuwa Wayne Rooney na wenziwe waliocheza bila mafanikio Kombe la Dunia huko Afrika Kusini watarudi Klabuni wakiwa na ‘hengiova’ ya kutofanya vizuri kwenye Mashindano hayo makubwa.
Rooney alikuwa na England huko Afrika Kusini lakini hakung’ara na hakufunga hata bao moja katika mechi nne alizocheza ya mwisho ikiwa kipigo cha 4-1 toka kwa Germany.
Wachezaji wengine wa Man United waliokuwa kwenye Kombe la Dunia ni Michael Carrick [England], Patrice Evra [France], Nemanja Vidic [Serbia], Park Ji-sung [South Korea] na Javier ‘Chicharito’ Hernandez [Mexico].
Wachezaji hao wote wataripoti tena Julai 28 wakitokea likizo.
Ferguson amesema: “Sitegemei huzuni na kuvunjika moyo toka kwao. Watahisi wamekosa kitu lakini hawataathirika.”
Lakini Ferguson akasema anahisi Mchezaji pekee ambae ataridhika na uchezaji wake huko Afrika Kusini ni Mchezaji mpya Chipukizi Hernandez aliechezea Mexico na kufunga bao mbili.
Wigan yamchota Kipa Al Habsi
Wigan Athletic imemsaini Kipa wa Kimataifa wa Oman Ali Al Habsi kwa mkopo wa Mwaka mmoja kutoka Bolton Wanderers.
Kipa huyo mwenye Miaka 28 amekuwa hana namba huko Bolton lakini katika mechi chache alizocheza amekuwa akifanya vizuri na Kocha wa Wigan, Roberto Martinez, amesema Al Albsi ataleta ushindani kwa Kipa wao Nambari Wani Chris Kirkland.
Al Absi ameichezea Oman mara 70 katika mechi za Kimataifa.
Wigan imekuwa haina Makipa wa Akiba baada ya kuondoka kwa Richard Kingson na Vladimir Stojkovic.
Wigan watacheza mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England kwa Msimu mpya wakiwa nyumbani DW Stadium dhidi ya Blackpool, Timu ambayo imepanda Daraja.

Wednesday 14 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Torres kukosa mwanzo wa Msimu
Baada ya Chama cha Soka cha Spain kuthibitisha kuwa Fernando Torres ameumia kiwango kikubwa kupita ilivyodhaniwa kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Holland, Liverpool wanangoja wamchunguze wenyewe lakini dalili zote zinaonyesha Straika huyo ataukosa mwanzo wa Msimu mpya wa Ligi Kuu England utakaoanza Agosti 14.
Liverpool imewapa Wachezaji wake wote waliocheza Kombe la Dunia likizo hadi mwanzoni mwa Agosti.
Torres amekuwa akiandamwa na majeruhi mfululizo Msimu uliokwisha ambapo aliumia musuli Mwezi Desemba Mwaka jana kisha akafanyiwa operesheni ya goti iliyomfanya asicheze Januari na Februari na ikafuata operesheni nyingine kwenye goti hilo hilo iliyomfanya azikose mechi 4 za mwisho za Ligi Kuu na Nusu Fainali ya EUROPA LIGI dhidi ya Atletico Madrid.
Hata hivyo, ingawa alikaa nje ya uwanja kwa wiki 6, Spain ilimchukua acheze Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ambako alipwaya sana.
Kwenye mechi hiyo ya Fainali huko Johannesburg alingizwa toka benchi na kucheza dakika 10 tu na kuumia tena bila kuguswa na mtu.
Henry rasmi MLS USA
Thierry Henry amejiunga na Timu ya New York Red Bulls inayocheza Major League Soccer, MLS, huko Marekani akitokea FC Barcelona kwa Mkataba ambao utamzalishia Mamilioni.
Henry ameondoka Barcelona kama Mchezaji huru ingawa Mkataba wake ulibakiwa na Mwaka mmoja.
Henry, Miaka 32, huenda akacheza mechi yake ya kwanza kwa Red Bulls Julai 22 na Tottenham ya England kwenye mechi ya kirafiki.
LIGI YA MABINGWA CAF hatua ya Makundi
LIGI YA MABINGWA YA CAF ambayo ndio hutoa Klabu Bingwa Afrika inaendelea Wikiendi hii ikiwa inaingia hatua ya Makundi mawili yenye Timu 4 kila moja na Washindi wawili toka kila Kundi ndio wataingia Nusu Fainali.
KUNDI A lina Timu za:
-Esperance Sportive de Tunis [Tunisia]
-ES Setif [Algeria]
-TP Mazembe Englebert [Congo DR]
-Dynamos [Zimbabwe]
KUNDI B:
-El Ismaily [Egypt]
-El Ahly [Egypt]
-JS Kabylie [Algeria]
-HeartlandFC [Nigeria]
RATIBA:
Ijumaa Julai 16: ES setif v Esperance
Jumamosi Julai 17: Dynamo v Mazembe
Jumapili Julai 18: Heartland v El Ahly
El Ismaily v JS Kabylie
Ijumaa Julai 30: Mazembe v ES Setif
CHEKI: www.sokainbongo.com


FIFA yatoa Listi ya Ubora Duniani, Spain juu…Bongo yaporomoka ni wa 112!!
Leo FIFA imetoa Listi ya ubora Duniani kwa Timu za Taifa na kama ilivyotegemewa, Mabingwa wapya wa Dunia, Spain, ndio wanaongoza wakifuatiwa na Holland, Brazil na Germany.
England wapo nafasi ya 7.
Tanzania imeporomoka nafasi 4 na sasa wako nafasi ya 114.
Timu za juu ni:
1 Spain
2 Holland
3 Brazil
4 Germany
5 Argentina
6Uruguay
7 England
8 Portugal
9 Egypt
10 Chile
11 Italy
12 Greece
13 USA
14 Serbia
15 Croatia
Tanzania imezungukwa na:
110 Zimbabwe
111 Georgia
112 Tanzania
113 Rwanda
114 Cuba
115 Kenya

Tuesday 13 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Real haimtaki Gerrard, umri na bei vyawatisha!!
Real Madrid imesema haina nia ya kumchukua Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard na hilo limetamkwa na Mshauri wa Ununuzi wa Wachezaji Ernesto Bronzetti.
Kumekuwa na tetesi kuwa baada ya Liverpool kukosa kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao, Gerrard hatabaki Liverpool na pia matamshi ya Meneja mpya wa Real Madrid, Jose Mourinho, kuwa anataka Wachezaji kama Gerrard kwenye Timu yake, yalileta dhana kuwa Gerrard yuko njiani kwenda Real.
Bronzetti amepasua kuwa Rais wa Real, Florentino Perez, hana nia na Gerrard kwa vile ana Miaka 30 na pia Liverpool wametaka dau kubwa la Pauni Milioni 58 kumuuza.
Redknapp asaini Mkataba mpya Spurs
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp ameongeza Mkataba hadi 2013 kutoka uliopo sasa ambao ungekwisha Mwakani.
Redknapp, Miaka 63, akielezea hatua hiyo, alitamka: “Sasa Nipo Spurs kwa Miaka mitatu mingine na nina furaha! Nani anajua, naweza kukaa Miaka mingi zaidi!”
Meneja huyo alijiunga na Spurs akitoka Portsmouth Oktoba 2008 na Spurs ilikuwa ipo mkiani na akaipandisha hadi nafasi ya 8 lakini Msimu uliofuata, ule wa 2009/10 uliokwisha Mwezi Mei, aliiwezesha kumaliza nafasi ya 4, hivyo itacheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu unaoanza Mwezi Agosti na hilo lilimfanya ateuliwa Meneja Bora wa Msimu wa Ligi Kuu England.
Akiongelea kuhusu kuongeza Mkataba wake, Redknapp alisema: “Hatujui nini kitatokea baadae lakini ukiwa bado na afya unaendelea. Ukiwaona Ferguson [Miaka 68], Capello [64], Wenger [60] na Roy Hodgson [62], unadhani naweza kufanya kama wao!”
CHEKI: www.sokainbongo.com

Kombaini Bora ya Kombe la Dunia 2010 yatajwa
Mara baada ya Kombe la Dunia 2010 kumalizika kimetajwa Kikosi cha Wachezaji 11 Bora waliong’ara kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kinaundwa na Wachezaji watano kutoka kwa Mabingwa Dunia, Spain, watatu toka Germany na mmoja mmoja kutoka Holland, Ureno na Uruguay.
Kikosi kamili ni kifuatacho:
-Kipa: Iker Casillas [Spain]
-Beki wa Kulia: Sergio Ramos [Spain]
-Sentahafu: Arnie Friedrich [Germany]
-Sentahafu: Carles Puyol [Spain]
-Beki wa Kushoto: Fabio Coentrao [Ureno]
-Kiungo: Bastian Schweinsteiger [Germany]
-Kiungo: Xavi [Spain]
-Kiungo: Wesley Sneijder [Holland]
-Winga Kulia: Thomas Mueller [Germany]
-Winga Kushoto: Andres Iniesta [Spain]
-Straika: Diego Forlan [Uruguay]
Makocha wa Timu 32 za Kombe la Dunia 2010: WAPI WAENDA?
Fainali za Kombe la Dunia 2010 ndio hizo zimeaga hapo Jumapili Julai 11 kwa Spain kuifunga Holland 1-0 na kutwaa Ubingwa wa Dunia na baadhi ya Makocha walioongoza Timu 32 kwenye Fainali hizo tayari washang’oka, wengine kwa hiari na baadhi kwa kufukuzwa, huku wengine hawajui hatma zao.
Ifuatayo ni Listi yao na nini kimewajiri:
FRANCE: Raymond Domenech, baada ya kuiongoza France iliyokumbwa na migogoro na aibu huko Afrika Kusini, hayupo tena na nafasi yake imechukuliwa na Laurent Blanc.
ENGLAND: Fabio Capello bado yumo mzigoni ingawa England ilisulubiwa na Germany kwa bao 4-1 kwenye Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia.
ITALY: Marcello Lippi, aliiongoza Italy kutwaa Kombe la Dunia 2006, lakini 2010 imetolewa Raundi ya Kwanza tu. Bado haijajulikana nini kitatokea kwake ingawa huenda akaondoka.
SLOVENIA: Matjaz Kek bado yumo mzigoni na nusura waingie Raundi ya Pili Kombe la Dunia kama si USA kuifunga Algeria dakika ya mwisho.
SLOVAKIA: Vladimir Weiss aliingiza Timu yake Raundi ya Pili na hiyo ni historia hivyo kubaki kwake si tatizo.
PORTUGAL: Carlos Queiroz amesema haondoki ingawa walitolewa Raundi ya Pili na Spain kwa bao 1-0 na ikafuata vita ya maneno kati yake na Cristiano Ronaldo.
SERBIA: Radomir Antic anabaki licha ya kushindwa kusonga mbele toka Raundi ya Kwanza.
HOLLAND: Bert van Marwijk aliipeleka Holland Fainali na kufungwa na Spain 1-0 na inasadikiwa bado atashika hatamu.
SPAIN: Ni lazima Vicente del Bosque atabaki kibaruani baada ya Spain kunyakua Ubingwa wa Dunia.
GERMANY: Mkataba wa Joachim Low umekwisha na hajaamua kama aendelee.
GREECE: Otto Rehhagel ameondoka baada ya kukaa Miaka 8 na kuisaidia Greece kunyakua EURO 2004 na kuiingiza EURO 2008 na Kombe la Dunia 2010 Mashindano ambayo yote walitolewa Raundi ya Kwanza tu.
USWISI: Ottmar Hitzfeld huenda akabaki na wao ndio Timu pekee iliyowafunga Spain huko Afrika Kusini.
DENMARK: Morten Olsen ana Mkataba hadi 2012.
GHANA: Milovan Rajevac huenda akaendelea na nusura aingize Ghana Nusu Fainali kama si mkono wa Luis Suarez wa Uruguay.
SOUTH AFRICA: Carlos Alberto Parreira anaondoka kwa vile Mkataba haupo tena.
CAMEROON: Paul Le Guen, ingawa anatakiwa abaki, pia Australia inamtaka na huenda akaondoka.
ALGERIA: Rabah Saadane bado anaheshimika huko Algeria na ni wazi hang’olewi labda atoke mwenyewe.
IVORY COAST: Sven-Goran Eriksson alikuwa na Timu hii kwa Mkataba wa muda mfupi tu.
NIGERIA: Lars Lagerback amepewa nyongeza ya Mkataba wa Miaka miwili.
AUSTRALIA: Pim Verbeek ameondoka.
NORTH KOREA: Licha ya kufungwa 7-0 na Ureno, kwa Kocha Kim Jong-Hun haijulikana ni nini kitamkuta sababu ya usiri wa Nchi hiyo.
SOUTH KOREA: Huh Jung-Moo amejiuzulu.
JAPAN: Takeshi Okada amejiuzulu.
NEW ZEALAND: Ricki Herbert bado yupo mzigoni kwa kuiwezesha Timu yake kutofungwa katika mechi 3 za Kundi lao walizotoka sare na kumaliza nafasi ya 3 juu ya Italy walioshika mkia.
USA: Bob Bradley ana uchu wa kuendelea na hamna presha kumng’oa.
HONDURAS: Reinaldo Rueda anaendelea.
MEXICO: Javier Aguirre ameamua mwenyewe kuondoka licha ya kutokuwa na shinikizo lolote la kumtoa.
BRAZIL: Dunga amefukuzwa.
ARGENTINA: Diego Maradona, licha ya kudharauliwa na Dunia juu ya uwezo wake kama Kocha, kwao ni kipenzi kikubwa na hivyo haitegemewi kuondolewa.
CHILE: Marcelo Bielsa atadumu.
URUGUAY: Oscar Tabarez aliipeleka Timu hadi kuchukua nafasi ya 4 na mwenyewe anataka kubaki.
PARAGUAY: Gerardo Martino yupo ofisini hadi baada ya Copa America Mwakani.
CHEKI: www.sokainbongo.com

FIFA yatoa Listi ya Ubora kwa Timu za Kombe la Dunia
FIFA imetangaza Listi ya Ubora kwa Timu 32 zilizocheza Fainali za Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini ambazo zilimalizika Jumapili Julai 11 kwa Fainali ya Holland v Spain na Spain kutwaa Ubingwa wa Dunia kwa kuifunga Holland 1-0.
Timu inayoshika Nambari Wani ni Spain, ikifuatiwa na Holland, Germany na Urugay.
Brazil wamechukua nafasi ya 6, Ghana ya 7 na England ya 13.
Akizungumzia kuhusu England na Brazil, Rais wa FIFA, Sepp Blatter, amesema: “England ndio Mama wa Soka, Brazil ndio moyo lakini siku hizi hakuna Taifa dogo kwenye Soka. Kuna Nchi ndogo lakini Timu zao za Taifa ni imara sana kwani Soka limepanda!”
Listi kamili:
1 Spain, 2 Netherlands, 3 Germany, 4 Uruguay, 5 Argentina, 6 Brazil, 7 Ghana, 8 Paraguay 9 Japan, 10 Chile, 11 Portugal, 12 United States, 13 England, 14 Mexico, 15 South Korea, 16 Slovakia 17 Ivory Coast, 18 Slovenia, 19 Switzerland, 20 South Africa, 21 Australia, 22 New Zealand, 23 Serbia, 24 Denmark, 25 Greece, 26 Italy, 27 Nigeria, 28 Algeria, 29 France, 30 Honduras, 31 Cameroon, 32 North Korea
Mastaa Man United kukosa mwanzo wa Ligi
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema baadhi ya Wachezaji wake waliokuwa huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia huenda wakaikosa mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu na Newcastle hapo Agosti 16 kwa sababu wanatakiwa waanze mazoezi Julai 28 baada ya kupewa likizo.
Kikosi cha Wachezaji 22 cha Man United kipo Chicago kwa mazoezi na ziara ya mechi za kirafiki huko Marekani, Canada na Mexico, ziara ambayo inamalizika Julai 30.
Manchester United wanategemewa kucheza ile mechi ya kufungua pazia Msimu mpya kugombea Ngao ya Hisani na Mabingwa wa Ligi Kuu Chelsea Uwanjani Wembley, London hapo Agosti 8.

Monday 12 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Mabingwa wa Dunia Spain watua kwao!
Kikosi cha Spain kikiwa na Kombe la Dunia kibindoni, baada ya kuifunga Holland 1-0 hapo jana Uwanjani Soccer City, Soweto, Johannesburg, leo mchana wametua Mjini Madrid, Spain.
Goli la Andres Iniesta la dakika ya 116 ndio limewapa Spain Ubingwa wa Dunia kwa mara ya kwanza katika histori yao.
Nahodha Iker Casillas akifuatana na Kocha Vicente del Bosque ndio walikuwa wa kwanza kushuka kwenye Ndege Uwanja wa Ndege wa Barajas huku Kundi kubwa la Watu likiwapokea.
Inategemewa Timu yote ya spain baadae itahudhuria sherehe kwa Waziri Mkuu wa Spain Jose Luis Rodriguez Zapareto.
Baada ya sherehe hizo Timu itazungushwa Mitaa ya Madrid ili Raia wawapokee na kuwashangilia Mashujaa wao.
Blatter aziponda Spain, Holland kwa uchezaji wa rafu!!
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, amezilaumu Timu za Spain na Holland kwa kucheza mchezo wa rafu katika Fainali ya Kombe la Dunia hapo jana huko Johannesburg ambako Spain walitwaa Kombe kwa kuifunga Holland 1-0.
Mechi hiyo ilijaa rafu na mchezo usioridhisha uliomfanya Refa Howard Webb kutoka England aweke rekodi kwa kutoa Kadi 15 ikiwemo Nyekundu kwa Beki wa Holland Heitinga.
Blatter alilalamika: “Fainali haikuwa nilivyotegemea. Siwezi kuwalaumu Marefa kwani walikuwa na wakati mgumu mno kuchezesha na hawakusaidiwa na Wachezaji.”
Pia Blatter aliipongeza Spain kwa kuwa Mabingwa wa Dunia.
Forlan atwaa Mpira wa Dhahabu
Straika wa Uruguay Diego Forlan ametwaa Mpira wa Dhahabu kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini baada ya kuchaguliwa ndie Mchezaji Bora.
Forlan, Miaka 31, anaechezea Atletico Madrid na aliewahi kucheza Manchester United, alifunga bao 5 kwenye Fainali hizo na kuiwezesha Uruguay, bila kutegemewa, kufika Nusu Fainali.
Thomas Mueller, Miaka 20, wa Germany alishinda Tuzo ya Mchezaji bora Kijana.
Mueller pia alifunga bao 5.
Kipa na Nahodha wa Spain, Iker Casillas, ametwaa Tuzo ya Kipa Bora kwenye Fainali baada ya kufungwa bao mbili tu katika mechi 7 walizocheza huko Afrika Kusini.
CHEKI: www.sokainbongo.com

SPAIN BINGWA WA DUNIA!!!
Ilichukua muda wa nyongeza, dakika ya 116, kwa Iniesta kuipatia Spain bao la ushindi, baada ya dakika 90 za mpira usiokuwa na hadhi ya Fainali ya Kombe la Dunia kwa rafu na uongo wa kujirusha ovyo uliomfanya Refa Howard Webb toka England awe na wakati mgumu wa kuchagua Kadi ipi atoe na kufanya zitoke Kadi nyingi kupita Fainali yeyote ile.
Kila Mtu alijua Kadi Nyekundu itatolewa dakika yeyote na kweli ilitoka dakika ya 110 hivi kwa Heitinga wa Holland kupata Kadi ya Njano ya pili.
Ni mechi iliyokuwa na nafasi chache za wazi ingawa Holland walipata mapema nafasi mbili ‘klia’ kupitia Robben na Spain kupitia Fabregas.
Timu:
SPAIN: Casillas, Sergio Ramos, Pique, Puyol, Capdevila, Busquets, Alonso, Xavi, Iniesta, Pedro, Villa.
Akiba: Valdes, Albiol, Marchena, Torres, Fabregas, Mata, Arbeloa, Llorente, Javi Martinez, Silva, Jesus Navas, Reina.
HOLLAND: Stekelenburg, Van Der Wiel, Heitinga, Mathijsen, Van Bronckhorst, Van Bommel, De Jong, Sneijder, Robben, Kuyt, van Persie.
Akiba: Vorm, Boulharouz, Ooijer, De Zeeuw, Braafheid, Elia, Schaars, Babel, Afellay, Huntelaar, Van der Vaart, Boschker.

Sunday 11 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Suarez aililia Ligi Kuu England!!
Mchezaji wa Ajax ya huko Uholanzi, Luis Suarez, ambae pia aliichezea Uruguay kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kujizolea sifa kubwa, nzuri na mbaya, amedai anapenda kucheza Ligi Kuu England hasa Manchester United au Tottenham.
Suarez, Miaka 23, Msimu uliokwisha aliifungia Ajax mabao 50 na kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini alipachika bao 3 kwa Uruguay lakini pia alijizolea sifa mbovu ya kuudaka mpira kwenye mstari wa goli dakika ya mwisho ya mechi na kuinyima Ghana ushindi wa wazi kitendo ambacho alitwangwa Kadi Nyekundu.
Huko nyuma Suarez aliwahi kuhusishwa na kuhamia Manchester United lakini mwenyewe amekiri huu ni wakati muafaka kuhamia England kwa jinsi Ligi Kuu ilivyokuwa na timu Bora.
Amesema: “Kuna Timu kama 5 zipo kiwango cha juu! Zitazame Man City na Liverpool zina kina Torres, Gerrard, Mascherano, Silva, Yaya Toure lakini hazimo UEFA CHAMPIONS LIGI!! Hii inaonyesha kuna Timu Bora huko!”
Suarez akamalizia: “Man United ni Timu bomba sana pamoja na Real Madrid na ndizo zinazosifika kupita zote Duniani! Unajua kabisa ukijiunga na Man United na kukaa kwa muda mrefu lazima utashinda Vikombe tu!”
Benayoun amponda Benitez
Kiungo wa zamani wa Liverpool Yossi Benayoun amemshambulia vikali aliekuwa Meneja wake huko Liverpool Rafael Benitez na kudai ndie aliesababisha yeye kuhama kwenda Chelsea.
Benayoun alidumu Liverpool Misimu mitatu lakini alikuwa akitumika kama Mchezaji wa Akiba.
Kiungo huyo amedai Benitez, ambae ameondoka Liverpool na sasa amejiunga na Inter Milan ya Italia, alimkosesha raha na alikuwa akimtendea vibaya.
Benayoun amesema: “Nikicheza vizuri hanipi pongezi, hata nikiingizwa na kafunga goli najua fika mechi ijayo sina namba! Msimu uliokwisha nilicheza mechi dhidi ya Fulham na ile na Lyon na akaamua kunibadilisha na Washabiki wakachukizwa na hilo na kuzomea! Yeye akadai nlicheza ovyo!”
Mchezaji huyo akaendelea kusema Benitez alikuwa akimwambia yeye ni Mchezaji mzuri akitokea benchi.
CHEKI: www.sokainbongo.com

PWEZA PAULO AENDELEZA LIBENEKE!!
Utabiri wa Pweza aitwae Paulo alie huko Oberhausen, Ujerumani umeendelea kutimia pale Germany walipoifunga Uruguay mabao 3-2 hapo jana Jumamosi, Julai 10 na kutwaa nafasi ya 3 kwenye Kombe la Dunia 2010.
Lakini macho ya Dunia nzima yapo kwenye mechi ya leo ya Fainali ya Kombe la Dunia kati ya Holland na Spain ambayo Pweza Paulo ameshatabiri kuwa Mshindi ni Spain.
Je Pweza Paulo ataendeleza libeneke?
Fergie akanusha kumtaka Sneijder!!
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amezikataa ripoti kwamba wametoa ofa kwa Inter Milan ili kumnunua Wesley Sneijder ambae anang’ara mno kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini akiwa na Nchi yake Uholanzi ambayo leo inacheza Fainali na Spain.
Ripoti hizo pia zilimnukuu Rais wa inter Massimo Moratti akidai ni kweli Man United inamtaka Sneijder.
Hata hivyo Ferguson ametamka: “Sijui ripoti hizo zinatoka wapi! Inawezekanaje waikatae ofa yangu wakati sijatoa ofa yeyote? Kwanza nina Kikosi kizuri tu na Vijana wangu wadogo sasa wamepata uzoefu wa Mwaka mmoja zaidi tangu Msimu uliopita!”
Ferguson pia amekanusha ripoti kuwa baada ya kukataliwa Sneijder sasa anataka kumchukua Kiungo wa Germany Mesut Ozil ambae pia aling’ara huko Afrika Kusini kwenye Kombe la Dunia.
CHEKI: www.sokainbongo.com

Kiatu cha Dhahabu Kombe la Dunia: Leo Mshindi ni Villa au Sneijder?
Leo ni kitimtim cha nani atakuwa Bingwa wa Dunia kati ya Holland na Spain zitakazokwaana kuanzia saa 3 na nusu usiku [bongo] huko Uwanja wa Soccer City, Soweto, Johannesburg lakini pia kwa Wachezaji kuna kitimtim cha nani atatwaa Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora wa Kombe la Dunia 2010.
Ingawa kuna Wachezaji wanne wamefungana juu kwa kufunga bao 5 kila mmoja lakini wenye nafasi kubwa ya kunyakua Tuzo hii, kwa vile Timu zao zinacheza leo, ni David Villa wa Spain na Wesley Sneijder wa Holland.
WAFUNGAJI BORA:
-Villa bao 5 [Spain]
-Sneijder bao 5 [Holland]
-Forlan bao 5[Uruguay]
-Muller bao 5 [Germany]
-Klose bao 4 [Germany]
-Higuain bao 4 [Argentina]
-Vittek bao 4 [Slovakia]
-Donovan bao 3 [USA]
-Gyan bao 3 [Ghana]
-Fabiano bao 3 [Brazil]
-Suarez bao 3 [Uruguay]
Klose akosa kuifikia rekodi ya Ronaldo
Miroslav Klose wa Germany jana alishindwa kuifikia rekodi ya Ronaldo de Lima wa Brazil ya kufunga jumla ya mabao 15 katika mechi za Fainali ya Kombe la Dunia.
Klose, mwenye jumla ya mabao 14, jana alishindwa kucheza mechi kutafuta Mshindi wa 3 wa Kombe la Dunia ambayo Germany iliifunga Uruguay kwa bao 3-2.
Klose alishindwa kuchezeshwa kwa vile alikuwa anakabiliwa na maumivu ya mgongo.
Germany 3 Uruguay 2
Sami Khedira alifunga bao la 3 na kuwapa Germany ushindi wa ba0 3-2 dhidi ya Uruguay na hivyo kunyakua ushindi wa 3 wa Kombe la Dunia huko Afrika Kusini.
Germany ndio walikuwa wa kwanza kupata bao pale shuti la Mita 30
la Schweinsteiger kutemwa na Kipa Fernando Muslera na kumwangukia Muller aliefunga.
Uruguay walisawazisha kupitia Edinson Cavani aliepokea pasi ya Suarez na dakika 6 ndani ya Kipindi cha Pili Forlan alifunga bao la pili baada ya pasi ya Suarez.
Germany wakasawazisha kwa kichwa cha Marcell Jensen baada Kipa Muslera kuikosa krosi.
Timu:
URUGUAY: 1-Fernando Muslera; 2-Diego Lugano, 3-Diego Godin, 4-Jorge Fucile, 16-Maximiliano Pereira, 15-Diego Perez, 17-Egidio Arevalo, 7-Edinson Cavani, 22-Martin Caceres, 9-Luis Suarez, 10-Diego Forlan.
GERMANY: 22-Hans-Joerg Butt; 2-Marcell Jansen, 3-Arne Friedrich, 17-Per Mertesacker, 20-Jerome Boateng, 13-Thomas Mueller, 4-Dennis Aogo, 6-Sami Khedira, 7-Bastian Schweinsteiger, 19-Cacau, 8-Mesut Ozil.
Refa: Benito Archundia (Mexico)
Powered By Blogger