Saturday 11 July 2009

Campbell wa Man U aenda Sunderland!
Kijana wa Manchester United Frazier Campbell, miaka 21, ambae alikuwa akicheza kwa mkopo Tottenham msimu uliokwisha ikiwa ni mapatano yaliyomfanya Dimitar Berbatov kusaini Man U, hatimaye amenunuliwa na Steve Bruce, Meneja mpya wa Sunderland, na kufanya Campbell awe Mchezaji wake wa kwanza Bruce kumnunua.
Campbell alitegemewa sana kwenda Hull City Timu ambayo aliichezea kwa mkopo msimu wa 2007/8 na kuisaidia kupanda kuingia LIGI KUU lakini ameichagua Sunderland ya Steve Bruce aliewahi kuichezea Man U.
Mchezaji wa Man City akwaa ‘Mafua ya Kitimoto’, akwama Cyprus!!!
Mchezaji wa Timu ya England na Klabu ya Manchester City, Micah Richards, umri miaka 21, amezuiwa kuondoka Kisiwa cha Cyprus alikokuwa mapumzikoni baada ya kuupata ugonjwa wa ‘Mafua ya Nguruwe’ na sasa anaendelea na matibabu.
Richards, ambae amepewa dawa ya Tamiflu ili kuutibu ugonjwa huo, anaelezea: ‘Kwanza nilidhani ninaumwa kifua au nimepata sumu kutokana na pombe nyingi kwani nilikuwa siwezi kuinuka na hata kula! Nilipoambiwa nina ‘Mafua ya Nguruwe’ nilistuka! Unaskia watu wanakufa kwenye Taarifa za Habari!’
Inategemewa Jumapili ataruhusiwa kuondoka kurudi England.
Richards mwenyewe anasema akirudi mazoezini bila shaka Wachezaji wenzake watamletea vitimbwi na mzaha mwingi! Richards anasema: ‘Najua wengine watakuja mazoezini wamejiziba sura kama Madaktari wako kwenye opersheni!’
Man City wakiri kushindwa na Eto'o!!
Manchester City wamekiri kushindwa kumchukua Eto’o kutoka Barcelona na wametamka hawajishughulishe tena kuhusu suala hilo. Man City na Barca zilikuwa zikijadiliana juu ya Mshambuliaji huyo kutoka Cameroun ili ahame kwa Pauni Milioni 25.
Bosi Mkuu wa Man City, Garry Cook, amekiri: ‘Dili imeshindikana!’ Inaelekea kuna utata kuhusu mkataba wa Eto’o na Barcelona ambae alijiunga Barca mwaka 2004 kutoka Mallorca kwa Pauni Milioni 16 na mpaka sasa ameshaifungia Klabu hiyo mabao zaidi ya 100.
Mpaka sasa Man City imeshawanunua Mshambuliaji Roque Santa Cruz kutoka Blackburn kwa Pauni Milioni 18 na Kiungo Gareth Barry kutoka Aston Villa kwa Pauni Milioni 12.
Alonso bado anawindwa na Real, Fabregas hayumo kwenye ‘Listi ya Manunuzi!’
Real Madrid wamesema bado wana nia ya kumnunua Kiungo Xabi Alonso kutoka Liverpool ingawa inasemekana Liverpool wamepandisha dau lake hadi Pauni Milioni 50.
Mkurugenzi wa Michezo wa Real, Miguel Pardeza, ametamka: ‘Real haiachi kufuatilia kitu hadi tujue hakiwezekani. Mpaka sasa kuna vipingamizi lakini tunaweza kubadilisha hilo.’
Hata hivyo, Pardeza amekanusha taarifa kuwa bado wanamtaka Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas kwa kusema hayumo katika ‘Listi yao ya Manunuzi’.
Mdau Kroenke aongeza hisa Arsenal!
Mkurugenzi wa Arsenal Stan Kroenke, mwenye hisa nyingi Klabuni Arsenal, ameongeza hisa zaidi na sasa anamiliki karibu aslimia 29 ya hisa zote na kumfanya akaribie hisa za aslimia 30 ambazo, kisheria, zitamlazimisha atoe ofa ya kununua hisa zote Klabuni hapo.
Kroenke, ambae ni Mmarekani anaemiliki Klabu ya Mpira wa Vikapu ya NBA Denver Nuggets, Klabu ya Mpira wa Magongo Colorado Avalanche na Klabu ya Soka ya Colorado Rapids zote za Marekani, mwezi Mei alinunua hisa nyingine na kumpiku Mrusi Alisher Usmanov kama mtu mwenye hisa nyingi.
Hivi karibuni kumekuwa na mvutano katika Bodi ya Arsenal huku Mdau Usmanov akitaka Wenger apewe fedha nyingi kununua Wachezaji lakini Bodi ikagoma.
Jermaine Pennant ahamia Zaragoza!
Winga wa Liverpool, Jermaine Pennant, aliekuwa akichezea Portsmouth kwa mkopo sasa amehamia Real Zaragoza baada ya mkataba wake na Liverpool kumalizika mwanzoni mwa mwezi huu.
Pennant pia alipata ofa kujiunga na AC Milan lakini akaikataa kwa sababu anaelewa Klabu hiyo itamchukua David Beckham na hivyo kumfanya akose namba ya kudumu.
Real Zaragoza iliyokuwa Daraja la chini msimu huu imerudi tena Daraja la juu La Liga.

Thursday 9 July 2009

Ziara ya Man United kabla msimu kuanza!!!
Mabingwa Manchester United wameanza mazoezi kwenye Kituo chao cha mazoezi huko Carrington, Manchester wakijitayarisha kwa ziara ya Asia watakayoianza Juali 16 kwa kuruka hadi Kuala Lumpur, Malaysia ambako watacheza mechi ya kwanza Uwanja wa Bukit Jalil Julai 18 na Kombaini ya Malaysia.
Baada ya hapo watakwenda Jakarta, Indonesia kucheza na Timu ya Mchanganyiko wa Wachezaji wa Ligi Kuu ya Indonesia Julai 20.
Julai 24 watakuwa Mji Mkuu wa Korea ya Kusini, Seoul, kucheza na Klabu ya FC Seoul kwenye Uwanja wa Kombe la Dunia Seoul.
Kisha, Man U wataruka hadi Uchina kucheza na Hangzhou Greentown Julai 26 Uwanjani Huanglong Sports Center.
Kutoka China, Man U wataenda moja kwa moja hadi Ujerumani kushiriki kwenye Kombe la Audi na tarehe 29 Julai watakwaana na Vigogo wa Argentina Boca Juniors kwenye Uwanja wa Klabu ya Bayern Munich uitwao Allianz Arena.
Siku ya pili, Man U watacheza na na Bayern Munich au AC Milan ikiwa ama ni mechi ya Fainali ya Kombe hilo la Audi au ya kutafuta Mshindi wa tatu ikitegemea matokeo kati ya mechi za Man U na Boca Juniors na ile ya Wenyeji Bayern Munich na AC Milan.
Manchester United watakuwa nyumbani Old Trafford Agosti 5 kucheza mechi ya kirafiki na Klabu ya Spain, Valencia.
Jumapili, Agosti 9, ndani ya Uwanja wa Wembley, ile mechi ya ‘Fungua Pazia la Msimu Mpya’ ijulikanayo kama Ngao ya Hisani itachezwa, na Manchester United, wakiwa Mabingwa wa Ligi Kuu, watapambana na Chelsea, Mabingwa wa Kombe la FA.
Wiki inayofuata, Jumapili Agosti 16, siku moja baada ya LIGI KUU England kuanza rasmi, Manchester United wataanza rasmi kutetea Ubingwa wao katika Ligi hiyo kwa kuikaribisha Timu iliyopanda Daraja, Birmingham, Uwanjani kwake Old Trafford.
Mdau adai Arsenal haina pesa kununua Wachezaji!!!
Mrusi Alisher Usmanov, anaemiliki hisa Arsenal ambazo kiidadi zinamfanya yeye kuwa wa pili kwa kumiliki hisa nyingi, amedai kuwa Arsenal haina mtaji wa kuiwezesha kununua Wachezaji wapya.
Usmanov, aliejaribu kuishawishi Bodi ya Klabu hiyo kumpa pesa Arsene Wenger kununua Wachezaji, ametoa kauli inayosema: ‘Bodi imesema ina uwezo wa kununua Wachezaji lakini sisi wadau tunajua pesa hizo hamna!’
Mpaka sasa Arsenal imemununua Mchezaji mmoja tu Mlinzi wa Ajax, Thomas Vermaelen, waliemchukua kwa Pauni Milioni 10.
Hata hivyo alichokifanya Meneja Arsene Wenger ni kuimarisha Mikataba ya Wachezaji wake Chipukizi waliokuwa nao kama vile Lukasz Fabianski, Kieran Gibbs, Aaron Ramsey, Theo Walcott, Jack Wilshere na Robin van Persie ambao wote Mikataba yao imeboreshwa na kurefushwa na wote wamesisitiza kubaki Arsenal kwa muda mrefu.
FIFA yarekebisha sheria za Soka!
Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke ametangaza marekebisho kadhaa ya baadhi ya Sheria za Kandanda na marekebisho hayo yameanza kutumika Julai 1.
Kitu kikubwa katika marekebisho hayo ni ile Sheria Namba 11 inayohusu Ofsaidi na hasa hili limekuja baada ya kuibuka utata mkubwa kwenye EURO 2008 katika mechi ya Holland na Italy baada ya Ruud van Nistelrooy wa Holland kufunga goli huku akionekana ofsaidi lakini wakati alipopewa pasi Beki wa Italy alitoka uwanjani kwa kujiangusha nje ya uwanja ili kufanya van Nistelrooy aonekane ofsaidi lakini Refa akamhesabu kama vile alikuwa uwanjani na kulikubali goli.
Wakati huo, Sheria ilimtaka Refa amwonye Mchezaji huyo aliyejitoa Uwanjani na haikutamka lolote kuhusu kumhesabu kama bado yuko uwanjani na hivyo Mfungaji anahesabiwa sio ofsaidi.
Sasa FIFA imefuta utata huo na sheria hiyo ya ofsaidi inasema kuwa endapo Mchezaji atajitoa uwanjani ili kumfanya Mpinzani aonekane kazidi basi atahesabiwa yuko uwanjani na baada ya mpira kusimama Mchezaji aliejitoa uwanjani atapewa onyo kali.
Copa Libertadores Fainali: Estudiantes 0 Cruzeiro 0!
Katika mechi ya kwanza ya Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa za Nchi za Marekani ya Kusini, ambayo ni Fainali ya 50 ya Mashindano hayo maarufu kwa jina la COPA LIBERTADORES, jana Timu za Nchi Mahasimu Kisoka Argentina na Brazil , Klabu ya Estudiantes ya Argentina na Cruzeiro ya Brazil zilitoka suluhu 0-0.
Fainali hii inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na mechi ya jana ilichezwa Argentina na marudiano yatafanyika Brazil wiki ijayo tarehe 15 Julai.
‘Uhamisho wa Kiwehu’ wamtia uchizi Benitez!
Meneja wa Liverpool Rafael Benitez ametoboa kuwa Klabu yake imeshindwa kushindana katika Soko la kununua Wachezaji kwa vile bei ni za ‘kiwehu!’.
Hivi juzi tu Liverpool ilitoa Pauni Milioni 17 kumnunua Beki wa Kulia wa Portsmouth Glen Johnson lakini ikamkosa Mchezaji waliekuwa wakimwania kwa muda mrefu Gareth Barry aliechukuliwa na Manchester City.
Vilevile, inabidi Benitez apigane ili kunusuru Xabi Alonso na Javier Mascherano wasimponyoke kwani kuna imani kubwa wanatakiwa na Vigogo wa Spain Real Madrid.
Benitez amegomba: ‘Soko ni la kiwehu! Sasa ni pesa, pesa, pesa tu sasa!’
Hata hivyo ameonya Timu zinazotumia pesa nyingi kununua Wachezaji kwamba kitabu cha hundi hakihakikishi Timu inapata mafanikio.
Rais wa Barca aikandya Real!!!
Rais wa Barcelona, Joan Laporta, amewaponda Mahasimu wao wakubwa huko Spain, Real Madrid kwa kutumia pesa nyingi sana kununua Wachezaji.
Real Madrid imewanunua Ronaldo, Kaka, Albiol na Benzema yuko njiani na jumla ya pesa zilizotumika kuwapata Wachezaji hao wanne ni zaidi ya Euro Milioni 200.
Laporta amekaririwa akisema: ‘Sisi Tunatengeneza Wachezaji wanaoshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Duniani, sisi hatununui Mchezaji Bora Duniani! Real wamejikita sokni na la kulipotosha Soko la Wachezaji duniani! Sisi hatuko hivyo!’
Wakati huohuo, Laporta amethibitisha kuwa Mchezaji wa Cameroun, Samuel Eto,o, ambae anawaniwa na Manchester City, amepewa nyongeza ya mkataba wa miaka miwili lakini mpaka sasa hajapatikana kuthibitisha.
Laporta amesema: ‘Nimempigia Eto’o mara kadhaa lakini simu yake ya mkononi haipokelewi. Sijui kama kabadilisha namba au kaipoteza!’
Boro yawatwanga faini Wachezaji Mido na Alves!!!
Meneja wa Middlesbrough Timu iliyoporomoka kutoka Ligi Kuu England msimu uliokwisha, Gareth Southgate, amethibitisha Wachezaji wao Mido kutoka Misri na Alfonso Alves wa Brazil wamechukuliwa hatua za kinidhamu na Klabu hiyo ikiwa pamoja na kukatwa mishahara ya wiki mbili kwa kuchelewa kuripoti kwenye mazoezi ya kujitayarisha na mwanzo wa msimu mpya wa Daraja la chini liitwalo Coca Cola Championship unaoanza mwezi Agosti.
Wachezaji hao wawili walitakiwa waanze mazoezi Jumatatu lakini hawakuonekana na ingawa Alves amesharipoti Mido bado yuko mitini.

Wednesday 8 July 2009

PELE ABASHIRI NCHI YA AFRIKA INAWEZA KUTINGA FAINALI KOMBE LA DUNIA AFRIKA KUSINI 2010!!
Edson Arantes Do Nascimento, maarufu Duniani kote kama Pele [pichani akimkabidhi Ronaldo Tuzo ya Mchezaji Bora Duniani], ametabiri mojawapo ya Nchi za Afrika inaweza ikaingia Fainali ya Kombe la Dunia mashindano hayo yakichezwa mwakani huko Afrika Kusini.
Pele alitoa utabiri huo alipokuwa Abuja, Nigeria akiisaidia Nchi yake Brazil ili ipate Uenyeji wa Mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 kwenye Baraza Kuu la Vyama vya Olimpiki vya Afrika.
Pele alisema kauli yake inaungwa mkono na uwezo walioonyesha Afrika Kusini kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Mabara wiki mbili zilizoisha na pia Marekani kucheza Fainali ya Kombe hilo.
Pele alisema: ‘Kwa sasa hamna Timu ndogo au Nchi ndogo.’
Alipoulizwa kwa sasa anashughulika na nini Pele alijibu: ‘Nipo na FIFA na pia na watoto shuleni. Nipo kwenye Kamati mojawapo ya FIFA. Miaka 6 iliyokwisha nilikuwa Waziri wa Michezo Brazil na nilipata Marafiki wengi duniani.’
Copa Libertadores leo Fainali: Estudiantes v Cruzeiro!
Leo ni Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa za Nchi za Marekani ya Kusini na ni Fainali ya 50 ya Mashindano hayo maarufu kwa jina la COPA LIBERTADORES na leo inazikutanisha Timu za Nchi Mahasimu Kisoka Argentina na Brazil wakati Argentina watawakilishwa na Klabu ya Estudiantes na Brazil ni Cruzeiro.
Fainali hii inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na mechi ya leo itachezwa Argentina na marudiano yatafanyika Brazil wiki ijayo tarehe 15 Julai.
Hii ni mara ya pili kwa Klabu hizi mbili kukutana kwenye Kombe hili msimu huu kwani walikuwa Kundi moja katika mechi za awali ambapo mechi ya kwanza Cruzeiro iliifunga Estudiantes 3-0 huko Brazil na marudiano huko Argentina, Estudiantes ilishinda 4-0.
Cruzeiro inae Mchezaji, Kleber, ambae wengi watamkumbuka kwani alicheza hivi juzi Kombe la Mabara huko Afrika Kusini na kuisaidia Brazil kutwaa Kombe hilo.
Nao, Estudiantes wanae Mkongwe Juan Sebastian Veron ambae aliwahi kuichezea Manchester United.
Mechi hii itanza saa 7 na nusu usiku saa za kibongo.
Zokora ahama Spurs kwenda Sevilla
Sevilla wamemsaini Mchezaji wa Tottenham anaetoka Ivory Coast Kiungo Didier Zokora kwa ada ambayo haikutajwa.
Zokora, 28, ameichezea Spurs mechi 134 na sasa amesaini mkataba wa miaka minne na Sevilla ya Spain. Sevilla inategemea kumtambulisha Zokora mbele ya Washabiki wao leo jioni.
Arsenal itajenga Timu, si kununua Timu!!
Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal Ivan Gazidis amesisitiza wao watajenga Timu na si kununua Timu wakati wakijitahidi kupata mafanikio ambayo wameyakosa tangu mwaka 2005 walipochukua Kikombe kwa mara ya mwisho walipolinyakua Kombe la FA.
Wakati Manchester United, Chelsea, Liverpool na Manchester City zinategemewa kutumia Mamilioni kununua Wachezaji, Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, hana bajeti kubwa ya kuingia Soko la Wachezaji na alichokifanya ni kuimarisha Mikataba ya Wachezaji wake Chipukizi waliokuwa nao kama vile Lukasz Fabianski, Kieran Gibbs, Aaron Ramsey, Theo Walcott, Jack Wilshere na Robin van Persie ambao wote Mikataba yao imeboreshwa na wote wamesisitiza kubaki Arsenal kwa muda mrefu.
Hata Nahodha Cesc Fabregas, anaevumishwa sana kwenda Barcelona, amesisitiza atabaki Arsenal.
Gazidis ametamka: ‘Sisi tunafuata njia nyingine. Sisi tunajenga Timu na hatununui Timu! Ndio maana Wachezaji wetu wanafuatwa fuatwa na Klabu nyingine!’
Inaelekea Real wasalimu amri kwa Ribery!!
Real Madrid, baada ya kumwaga ‘vijisenti’ kwa kuwachukua Ronaldo na Kaka, sasa inaelekea wameanza kuosha mikono kwa kukubali kushindwa kumbabadua Franck Ribery kutoka Klabu ya Ujerumani Bayern Munich.
Mkurugenzi Mtendaji wa Real, Jorge Valdano, akionyesha kukata tamaa, amesema: ‘Tunahisi Ribery haondoki Bayern msimu huu. Bayern wametumia njia nyingi kusema hawataki ahame! Wakati mwingine wanakataa moja kwa moja, wakati mwingine wanatamka dau kubwa sana, kama Euro Milioni 80, ambayo ni njia nyingine ya kusema hapana! Basi, tutasubiri kwani amebakisha miaka miwili na Bayern!’
Hata hivyo kunu fununu kuwa, baada ya Real Madrid kunyosha mikono, huenda Chelsea wakaingia mtamboni kumwania Ribery ingawa inaweza kuwa ngumu kumchukua kwani Ribery mwenyewe, kufuatia urubuni wa Balozi wa Real, Zinedine Zidane, ameweka bayana yeye anataka kwenda Real tu.
MAN U wasaini Mchezaji wa tatu!!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amemsaini Mchezaji wa Bordeaux ya Ufaransa, Gabriel Obertan, miaka 20, [pichani] kwa mkataba wa miaka minne na kumfanya awe ni Mchezaji wa 3 kusainiwa baada ya kuwachukua Luis Antonio Valencia na Michael Owen.
Ferguson, akizitangaza habari hizo, amesema: ‘Ni muda mrefu tumekuwa tukimfuatilia na tulichelewa kumchukua kwa sababu ya programu yake ya mafunzo. Tunapenda kuwachukua Wachezaji Vijana na kuwaendeleza na tutajua baada ya miaka miwili kafikia wapi.’
Gabriel Obertan, Mchezaji mrefu sana [Futi 6 Inchi 1]anaechezea Timu ya Taifa ya Vijana wa Ufaransa chini ya Maiaka 21 na ambae anazimudu nafasi za Kiungo na Ushambuliaji, ametamka: ‘Nina furaha kucheza Manchester United. Hii ni nafasi kubwa kwangu.’
Hata hivyo, kwa sababu Mchezaji huyo ameumia kidogo hatakuwemo kwenye msafara wa Manchester United utakaoelekea Asia wiki ijayo.
Van Persie asaini mkataba mpya Arsenal!!
Robin van Persie amesaini mktaba mpya na Klabu yake Arsenal wa muda mrefu ingawa muda huo haukutajwa.
Mdachi huyo mwenye miaka 25 ndie Mfungaji Bora wa Klabu hiyo kwa msimu uliopita kwa kufunga magoli 20 katika mechi 44 alizocheza na inasemekana sasa Mshahara wake utakuwa Pauni Elfu 80 kwa wiki.
Van Persie alichukuliwa kutoka Klabu ya Feyenoord mwaka 2004.
Birmingham wamchota Lee Bowyer
Meneja wa Birmingham Alex McLeish amemsaini Lee Bowyer kwa mkataba wa miaka miwili na kwa uhamisho wa bure tu kutoka West Ham ambako mkataba wake ulimalizika Julai 1.
Lee Bowyer, miaka 32, alikuwepo Birmingham kwa mkopo mwishoni mwa msimu uliopita na alisaidia sana Birmingham kupanda Daraja kuingia Ligi Kuu msimu utakaoanza mwezi ujao.
Bowyer anaungana na Wachezaji Christian Benitez, Stephen Carr, Scott Dann, Roger Johnson, Joe Hart na Giovanny Espinoza waliosaini kuichezea Birmingham msimu ujao.
Lee Boywer, ambae ni Kiungo mwenye vituko vingi, alianza kucheza Soka la juu alipokuwa na Charlton kisha akahamia Leeds mwaka 1996 na baadae kwenda West Ham mwaka 2003 na miezi sita baadae kuhamia Newcastle ambako alikaa miaka mitatu na kurudi tena West Ham.

Tuesday 7 July 2009

Kipa Ben Foster asaini mkataba mpya Man U!!
Kipa Ben Foster, miaka 26, amesaini mktaba mpya wa miaka minne na Klabu yake Manchester United ambao utamuweka Old Trafford hadi 2013.
Foster, ambae pia anachezea Timu ya Taifa ya England, ndie anaeonekana ni mrithi wa Edwin van der Sar anaestaafu mwakani na alichukuliwa na Man u kutoka Stoke City mwaka 2005.
Kupanda chati kwa Foster kumekuwa kwa hati hati kwani amekuwa akikumbwa na majeruhi ya mara kwa mara ikiwa na pamoja kuukosa mwisho wa msimu uliopita baada ya kuumia kidole gumba cha mkono na kufanyiwa operesheni
Kipa Paddy Kenny wa Sheffield United agundulika katumia madawa yaliyopigwa marufuku!
Kipa Paddy Kenny wa Sheffield United amesimamishwa na Klabu yake Sheffield United baada ya kugundulika amefeli vipimo vya uchunguzi na kuonekana ametumia madawa ambayo hayaruhusiwi.
Ugunduzi huo uliotokea baada ya kupimwa kwenye mechi ya mchujo wa kupanda Daraja mwezi Mei ambayo Sheffield United walicheza na Preston na kuonekana ana chembe chembe za dawa ‘Ephedrine’ ambayo ni marufuku kwa Wanamichezo kwa sababu huongeza nguvu.

Dawa hiyo hutumika kutibu mafua na kutuliza pumu.
Kipa Kenny sasa atachunguzwa na FA na huenda akatumikia kifungo cha miaka miwili.
Bosi wa Chelsea adai Terry hauzwi!!
Bosi wa Chelsea, Peter Kenyon, ametangaza kuwa Nahodha wao John Terry hauzwi licha ya kufukuziwa kwa karibu sana na Manchester City.
Kenyon anaungana na Meneja mpya, Carlo Ancelotti,aliedai jana kuwa Nahodha huyo atabaki Stamford Bridge.
Kenyon ametamka: ‘Ana mkataba wa miaka mitatu. Mwenyewe amesema hataki kuondoka na sisi hatutaki aondoke. Mwisho wa hadithi!’
Winga Chipukizi wa Ufaransa apimwa afya Man U!!!!
Gabriel Obertan, miaka 20, anaechezea Timu ya Taifa ya Vijana wa Ufaransa wa chini ya miaka 21 na Klabu ya Bordeaux, leo amepimwa afya yake Manchester United ili anunuliwe.
Obertan, aliekuwa pia akitakiwa na Klabu za AC Milan, Inter Milan na Arsenal, ameichagua Manchester United na Meneja wake huko Bordeaux, Laurent Blanc, aliewahi kuichezea Man U, ameonyeshwa kushtushwa kwa Man U kumtaka Mchezaji huyo ingawa amesema ni nafasi bora kwa Winga huyo.
Mrusi Yuri Zhirkov njiani kwenda Chelsea!!
Mchezaji wa Kiungo wa Timu ya Urusi na Klabu ya CSKA Moscow, Yuri Zhirkov, amefanyiwa upimaji wa afya Klabuni Chelsea ili wamsajili.
Zhirkov, miaka 25, anathaminiwa kuwa ada yake itakuwa kwenye Pauni Milioni 18.
Mbrazil Jo kubaki Everton kwa mkopo!!
Straika wa Manchester City kutoka Brazil, Jo, ataendelea kubaki Everton kwa mkopo wa mwaka mmoja zaidi baada ya Klabu hizo kufikia makubaliano.
Msimu uliokwisha Jo alichezea Everton kwa mkopo na kucheza mechi 12 na kufunga bao 5.
Jo alinunuliwa na Manchester City kutoka CSKA Moscow lakini hakupata mafanikio Klabuni hapo.
Kwa sasa, Man City wanawawinda Samuel Eto’o kutoka Barcelona na Carlos Tevez ambae hana Klabu.
Ronaldo atambulishwa mbele ya Mashabiki 80,000 Uwanjani Bernabeau!!!
Cristiano Ronaldo ameanuliwa rasmi kama Mchezaji wa Real Madrid mbele ya Mashabiki 80,000 waliofurika Uwanjani Santiago Bernabeau.
Ronaldo amehamia Real kwa ada ambayo ni rekodi ya dunia ya Pauni Milioni 80.
Lakini mwishoni mwa sherehe hizo Washabiki hao walivamia Uwanja na ilibidi Polisi wamkimbize Ronaldo ili kumuokoa.

Monday 6 July 2009

Glenn Hoddle: Owen ni bora kupita Tevez kwa Man U!
Kocha wa England mwaka 1998 Glenn Hoddle aliempa Jezi Michael Owen kuchezea England kwa mara ya kwanza na kuifunga Argentina mwaka huo huo kwa goli la ajabu sana kwenye Kombe la Dunia, wakati Owen ni Kinda tu, amepasua na kusema Sir Alex Ferguson amefanya uamuzi busara na wa akili kubwa kumchota Michael Owen kucheza Old Trafford.
Hoddle ametamka: ‘Ni biashara nzuri Ferguson kafanya! Nina uhakika kama Michael atabaki fiti na atacheza mechi 30 au zaidi atafanya vizuri sana kupita Tevez! Jinsi Man U wanavyocheza Owen atakuwa bora tu!’
Glenn Hoddle akaongeza: ‘Man U wanamiliki na kutawala mpira, wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga na hio ni bora kwa Owen ambae ni mmaliziaji hatari! Owen atang’ara Man U!’
Hoddle akawakumbusha watu kuhusu Eric Cantona, Teddy Sherigham na Henrik Larsson ambao wote maisha yao Kisoka yalielekea ukingoni lakini Ferguson akawavuta Man U na wakawika na pia kuiletea mafanikio Man U.

Sunday 5 July 2009

Sunderland wanamfukuzia Mlinzi Da Silva toka Paraguay!!
Meneja wa Sunderland, Steve Bruce, yuko mbioni kumsaini Mlinzi wa Klabu ya Deportivo Toluca, Paulo Da Silva kutoka Paraguay ili awe Mchezaji wake wa kwanza kumsajili.
Steve Bruce amehamia Sunderland kutoka Wigan mara tu baada ya Ligi Kuu kumalizika katikati ya mwezi Mei.
Paulo Da Silva, umri miaka 29, ni Mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika na Klabu yake Deportivo Toluca iliyothibitisha kuwa baada ya Sunderland kuonyesha nia ya kumchukua Mchezaji huyo mwenyewe aligoma kuongeza mkataba.
Inasadikiwa Da Silva atasafiri kwenda England wiki ijayo ili kukamilisha taratibu za uhamisho.
Mkongwe Mark Viduka atathmini ofa toka Klabu mbili za Ligi Kuu
Mchezaji wa zamani wa Newcastle, Veterani Mark Viduka, ambae mkataba wake na Klabu hiyo ulimalizika wiki iliyokwisha anatafakari ofa toka Klabu mbili za Ligi Kuu ambazo hazikutajwa ingawa mojawapo inaaminika ni Fulham.
Viduka, mwenye umri wa miaka 33, anapenda abaki England ili ajiongezee matumaini ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani akiwa na Nchi yake Australia ambayo tayari imefuzu kuingia Fainali hizo.
Wakala wa Mark Viduka, Steve Kutner, amekiri kuwa zipo Klabu mbili kubwa za Ligi Kuu zenye nia ya kumchukua Viduka ingawa hakuzitaja.
Redknapp akiri Man City imempiku kuwachukua Barry na Santa Cruz!
Bosi wa Tottenham, Harry Redknapp, amekiri kuwa Manchester City waliwashinda ubavu kwa kuwa na uwezo mkubwa na ndio maana wakaweza kuwachukua Wachezaji Gareth Barry kutoka Aston Villa na Roque Santa Cruz kutoka Blackburn Rovers ambao wao pia walikuwa wanawawania.
Redknapp amesema uwezo wa Man City kulipa ada kubwa na kuwalipa Wachezaji mishahara minono ndio unaowawezesha kuchukua Wachezaji kwa bei mbaya.
Hata hivyo Redknapp amesema Tottenham hawana papara ya kukurupuka kununua Wachezaji na hata kama hawakupata mtu msimu huu ana imani na Kikosi kilichopo.
Beckenbauer aisapoti England kuwa Mwenyeji Fainali za Kombe la Dunia
Mchezaji wa zamani wa Ujerumani na Mshindi wa Kombe la Dunia Franz Beckenbauer anaamini bila wasiwasi kuwa England ina uwezo wa kuendesha Fainali za Kombe la Dunia kwa sababu wana Viwanja vingi vya kisasa na pia Washabiki wengi sana.
Franz Beckenbauer, Nahodha wa zamani wa Ujerumani, yumo kwenye Kamati ya FIFA itayoamua nani Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.
Beckenbauer amekaririwa akisema: ‘Hata wakiambiwa wawe Wenyeji kesho, England wanao uwezo kwa sababu wana miundo mbinu ya kisasa, Washabiki, Viwanja na kila kitu kinachotakiwa kwa Fainali hizo.’
England ni miongoni mwa Nchi 9 zinzogombea Uenyeji wa Fainali za 2018 na wapo katika Nchi 11 zinazogombea zile za 2022.
FIFA itaamua Desemba nani watakuwa Wenyeji.
Tevez: ‘Mimi sio msaliti!’
Carlos Tevez amewakikishia Mashabiki wa Manchester United kuwa akijiunga na Wapinzani wa Manchester United, Manchester City, atakuwa haisaliti Klabu hiyo aliyochezea misimu miwili kwa kuwa sababu ya kuondoka yeye ni Man U na si yeye.
Hata hivyo, Manchester United walikuwa tayari kulipa pesa za kumnunua Tevez toka Kampuni inayommliki na pia walishampa ofa ya mkataba wa miaka mitano na mshahara mkubwa tu ambao ungemfanya Tevez awe mmoja wa Wachezaji wa Man U wanaolipwa donge nono sana, lakini Tevez aligoma kwa madai kuwa msimu uliokwisha alidharauliwa kwa kutopangwa mara kwa mara.
Mkataba wa Tevez na Manchester United ulimalizika Juni 30.
Powered By Blogger