Wednesday 8 July 2009

MAN U wasaini Mchezaji wa tatu!!!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amemsaini Mchezaji wa Bordeaux ya Ufaransa, Gabriel Obertan, miaka 20, [pichani] kwa mkataba wa miaka minne na kumfanya awe ni Mchezaji wa 3 kusainiwa baada ya kuwachukua Luis Antonio Valencia na Michael Owen.
Ferguson, akizitangaza habari hizo, amesema: ‘Ni muda mrefu tumekuwa tukimfuatilia na tulichelewa kumchukua kwa sababu ya programu yake ya mafunzo. Tunapenda kuwachukua Wachezaji Vijana na kuwaendeleza na tutajua baada ya miaka miwili kafikia wapi.’
Gabriel Obertan, Mchezaji mrefu sana [Futi 6 Inchi 1]anaechezea Timu ya Taifa ya Vijana wa Ufaransa chini ya Maiaka 21 na ambae anazimudu nafasi za Kiungo na Ushambuliaji, ametamka: ‘Nina furaha kucheza Manchester United. Hii ni nafasi kubwa kwangu.’
Hata hivyo, kwa sababu Mchezaji huyo ameumia kidogo hatakuwemo kwenye msafara wa Manchester United utakaoelekea Asia wiki ijayo.
Van Persie asaini mkataba mpya Arsenal!!
Robin van Persie amesaini mktaba mpya na Klabu yake Arsenal wa muda mrefu ingawa muda huo haukutajwa.
Mdachi huyo mwenye miaka 25 ndie Mfungaji Bora wa Klabu hiyo kwa msimu uliopita kwa kufunga magoli 20 katika mechi 44 alizocheza na inasemekana sasa Mshahara wake utakuwa Pauni Elfu 80 kwa wiki.
Van Persie alichukuliwa kutoka Klabu ya Feyenoord mwaka 2004.
Birmingham wamchota Lee Bowyer
Meneja wa Birmingham Alex McLeish amemsaini Lee Bowyer kwa mkataba wa miaka miwili na kwa uhamisho wa bure tu kutoka West Ham ambako mkataba wake ulimalizika Julai 1.
Lee Bowyer, miaka 32, alikuwepo Birmingham kwa mkopo mwishoni mwa msimu uliopita na alisaidia sana Birmingham kupanda Daraja kuingia Ligi Kuu msimu utakaoanza mwezi ujao.
Bowyer anaungana na Wachezaji Christian Benitez, Stephen Carr, Scott Dann, Roger Johnson, Joe Hart na Giovanny Espinoza waliosaini kuichezea Birmingham msimu ujao.
Lee Boywer, ambae ni Kiungo mwenye vituko vingi, alianza kucheza Soka la juu alipokuwa na Charlton kisha akahamia Leeds mwaka 1996 na baadae kwenda West Ham mwaka 2003 na miezi sita baadae kuhamia Newcastle ambako alikaa miaka mitatu na kurudi tena West Ham.

No comments:

Powered By Blogger