Saturday 22 November 2008

LIGI KUU: Vinara Chelsea & Liverpool wabanwa mbavu, Arsenal apigwa vibaya!!

Vinara wa LIGI KUU Chelsea na Liverpool, wote wakicheza nyumbani kwao, leo wamevutwa jezi na kutoka suluhu na 'timu dhaifu'!!

Chelsea amelezimishwa sare ya 0-0 na Newcastle wakati Liverpool ameenda dro ya 0-0 na Fulham.

Nao Arsenal, ambao wako kwenye mgogoro baada ya kumbwaga chini Nahodha wao William Gallas kufuatia kitendo chake cha kuanika hadharani matatizo ya ndani ya klabu, leo ilishuka City of Manchester Stadium kupambana na timu nyingine inayosuasua, Manchester City, huku Kipa Manuael Almunia akiwa Nahodha.
Arsenal wakajikuta waking'utwa mabao 3-0 katika mechi hii kikiwa kipigo cha pili mfululizo kwa Arsenal baada ya wiki iliyopita kulazwa mabao 2-0 na Aston Villa.
Mabao ya Man City yalifungwa na Stephen Ireland, Robinho na Daniel Sturridge akafunga la 3 kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na Beki Johan Djourou.

MATOKEO KAMILI MECHI ZA LEO NI:

Portsmouth 2-2 Hull

Chelsea 0-0 Newcastle

Liverpool 0-0 Fulham

Man City 3-0 Arsenal

Stoke 1-0 West Brom
Middlesbrough 1-3 Bolton
WAJUE MAREFA WANAOONGOZA KWA KUWAPA WACHEZAJI KADI!!!

Wakati kila timu kwenye LIGI KUU imeshacheza mechi 13 [isipokuwa Man U na Fulham waliocheza 12] jumla ya Marefa 18 ndio waliochezesha mechi zote hizo huku Refa Mike Dean [pichani] aliechezesha jumla ya mechi 11 ndie anaeongoza kwa kutoa kadi nyingi.

Mike Dean ameshatoa Kadi Nyekundu 5 na za Manjano 47.

Anaefuata ni Refa Mike Riley aliechezesha mechi 10 na kugawa Kadi Nyekundu 2 na za Njano 45.

Steve Bennet ana mechi 9 na hajatoa Nyekundu hata moja ingawa amegawa Njano 37.

Rob Styles ana mechi 9, Nyekundu 3 na Njano 33.

Andre Marriner mechi 9, Nyekundu 4 na Njano 32.

Kati ya Marefa hao 18 waliochezesha LIGI KUU mpaka sasa hakuna hata mmoja ambae ametoka uwanjani bila kutoa kadi.

Anaeshika mkia kwa kutoa kadi chache kabisa ni Mark Halsey aliechezesha mechi 6 na kutoa Nyekundu 1 na Njano 6.
TATHMINI: MECHI ZA VIGOGO ZA LEO ZA LIGI KUU!!

Vinara wa LIGI KUU Chelsea na Liverpool leo wanajimwaga viwanjani huku macho ya wengi yakitazama kama Steven Gerrard wa Liverpool na Frank Lampard wa Chelsea watacheza baada ya kujitoa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uingereza iliyoifunga Ujerumani katika mechi ya kirafiki mabao 2-1 siku ya Jumatano mjini Berlin, Ujerumani.
Wachezaji hao walijitoa kwa madai ni majeruhi na kitendo hicho kilimkera Meneja wa Uingereza Fabio Capello na akalazimisha Wachezaji hao waende kwenye kambi ya Timu ya Uingereza ili wachunguzwe na Madaktari wa timu hiyo.
Leo Chelsea inawakaribisha Stamford Bridge Newcastle ambao hawajawahi kushinda hapo katika mechi za LIGI KUU.
Liverpool nao wanawakaribisha Fulham uwanjani Anfield ambako katika mechi 7 za LIGI KUU walizocheza hapo, Fulham hawajashinda hata moja na wameweza kufunga bao 2 tu.
Mabingwa wa LIGI KUU, Man U, ambao wako nafasi ya 3 nyuma ya Chelsea na Liverpool, wanashuka uwanjani Villa Park kucheza na wenyeji wao Aston Villa ambao wako nafasi ya 5.
Man U aliecheza mechi moja pungufu ana pointi 24 akifuatiwa na Arsenal na Aston Villa wenye pointi 23.
Aston Villa, ambao waliwabamiza Arsenal mabao 2-0 huko Emirates Stadium katika mechi iliyokwisha, hawajawahi kuwafunga Man U katika mechi 11 zilizopita.
Huenda leo Man U ikamkosa Dimitar Berbatov alieumia siku ya Jumatano wakati akiichezea Timu yake ya Taifa ya Bulgaria ilipocheza na Serbia ingawa Wachezaji Rio Ferdinand na Wayne Rooney waliokosa mechi ya wiki iliyopita ya ushindi wa 5-0 dhidi ya Stoke City wanaweza kuwemo dimbani.
Manchester City leo watawakaribisha Arsenal ambao wako kwenye kipindi kigumu sana hasa baada ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani Emirates na Aston Villa wiki iliyopita, kisha kumpoteza nyota chipukizi Theo Walcott alepasuliwa bega na jana Klabu ilithibitisha haina Nahodha baada ya Nahodha William Gallas kutimuliwa kwa kuanika 'chupi chafu' hadharani!
RIO FERDINAND & ASHLEY COLE WAUNGANA NA RAPA 50 CENT KUTOA FILAMU!

Mastaa wa Uingereza Rio Ferdinand wa Manchester United na Ashley Cole wa Chelsea wamejitosa kwenye utengenezaji filamu baada ya kuchangia dau la kutengeneza filamu iitwayo 'DEAD MAN RUNNING' ambayo itachezwa na mkali wa Rap 50 Cent na Mcheza sinema wa Uingereza aitwaye Danny Dyer.
Filamu hii imeshaanza kutengenezwa huku picha zikichukuliwa mjini London na Manchester.
Katika picha hii Danny Dyer anaekti kama mtu anayedaiwa na kukabwa koo na 50 Cent ili amlipe Pauni laki moja ndani ya masaa 24.
50 Cent ambae ni mwanamuziki mahiri wa kizazi kipya ameshacheza sinema maarufu kama 'Get Rich or Die Tryin' na 'Righteous Kill'.
Rio Ferdinand anamiliki kampuni yake ya kufyatua rekodi iitwayo White Chalk Records na hivi karibuni ilitoa singo yake ya kwanza 'Black Ice' iliyoimbwa na kimwana Nia Jai huku Rio mwenyewe akionekana ndani ya video hiyo.
MPASUKO ARSENAL: Baada ya kuanika 'chupi chafu' hadharani, Nahodha Gallas anyang'anywa Unahodha!!!!!

Taarifa zilizozagaa kila kona ya ulimwengu wa soka zimebaini Nahodha wa Arsenal William Gallas amevuliwa Unahodha wa timu hiyo mara tu baada ya kutamka hadharani kuwa mambo si shwari ndani ya kambi ya 'Washika Bunduki'.
Gallas, mwenye umri wa miaka 31 aliejiunga Arsenal Septemba 2006 na kuteuliwa kuwa Nahodha Agosti 2007, alisema kuwa Timu ya Arsenal ina mgawanyiko, kiburi na waoga.
Vilevile alimtuhumu Mchezaji mmoja, anaesadikiwa kuwa ni Robin Van Persie, ndie kiini cha mzozo huu.
Arsenal ambayo leo jioni inacheza ugenini ikikabiliana na Manchester City imemuacha Gallas kwenye msafara wa timu hiyo iliyoondoka London jana kuelekea Manchester.
Wadau wengi walianza kumponda Gallas tangu msimu uliopita pale alipoonyesha dhahiri uwanjani kuwa hawezi kuwa kiongozi, wakati timu yake ikicheza na Birmingham, Refa alipoipa Birmingham penalti dakika ya mwisho ya mchezo na Gallas badala ya kuwahamasisha wenzake kama Nahodha anavyotakiwa yeye aliamua kwenda kukaa chini kwenye duara la kati ya uwanja na kuanza kulia.
James McFadden wa Birmingham alifunga penalti hiyo ya dakika ya mwisho na mechi ikaisha suluhu na kufanya uongozi wa Arsenal kwenye ligi wakati huo upungue na kuwa pointi mbili tu.
Mara baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo Gallas, huku akibubujikwa machozi, alilipiga mateke bango la matangazo pembezoni mwa uwanja.
Kuanzia hapo Arsenal ikaporomoka na katika mechi 10 zilizofuata ikashinda 2 tu na kuwaachia Man U kunyakua ubingwa.

Friday 21 November 2008

MPASUKO NDANI YA ARSENAL: Nahodha Gallas apasua jipu hadharani!!!

Nahodha wa Arsenal, William Gallas, ametoboa hadharani kuwa timu yao ya Arsenal haina umoja, kuna mgawanyiko na Wachezaji hawana ushujaa na wala si wapiganaji.
Gallas amepasua jipu hilo huku Arsenal ikiendelea kusuasua kwenye LIGI KUU ikiwa pointi 9 nyuma ya vinara Chelsea na Liverpool na pointi moja nyuma ya Man U ambayo imecheza mechi moja pungufu.
Mpaka sasa, baada ya mechi 13 za LIGI KUU, Arsenal imeshapoteza mechi 4. Pia, hivi juzi tu imepita pigo jingine baada ya kuthibitishwa staa na chipukizi wao Theo Walcott atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 8 baada ya kuumia bega ambalo linahitaji kupasuliwa.
Gallas anaripotiwa kutamka: 'Wachezaji wa Arsenal si mashujaa vitani. Sasa timu haziogopi kuja Emirates na kucheza mpira kwani washajua sisi ni waoga. Vilevile tuna Wachezaji kiburi. Katika mechi unaambiwa kama Nahodha kuna Mchezaji analalamikiwa na wenzake, unamfuata na anaanza kukukashifu! Hii haikubaliki! Tena Mchezaji huyo ni mdogo kwangu kwa miaka 6!'
Gallas ana umri wa miaka 31 na Wachezaji ambao wana umri wa miaka 25 ndani ya Arsenal ni Robin Van Persie, Emmanuel Eboue, Eduardo na Bacary Sagna.
Wachunguzi wanahisi Mchezaji anaetuhumiwa na Gallas ni Robin Van Persie.
RATIBA: MECHI ZIJAZO ZA LIGI KUU & UEFA CHAMPIONS LEAGUE

LIGI KUU UINGEREZA:

Jumamosi, 22 Novemba 2008

[saa 12 jioni bongo taimu]

Chelsea v Newcastle

Liverpool v Fulham

Man City v Arsenal

Middlesbrough v Bolton

Portsmouth v Hull City

Stoke City v West Brom

[saa 2 na nusu usiku]

Aston Villa v Man U

Jumapili, 23 Novemba 2008

[saa 10 na nusu jioni]

Sunderland v West Ham

[saa 1 usiku]

Tottenham v Blackburn

Jumatatu, 24 Novemba 2008

[saa 5 usiku]

Wigan v Everton

UEFA CHAMPIONS LEAGUE:

JUMANNE, 25 Novemba 2008
[saa 4 dak 45 usiku]

AaB v Celtic,

Arsenal v Dynamo Kiev,

BATE Borisov v Real Madrid,

Bayern Munich v Steaua Bucuresti,

Fenerbahce v FC Porto,

Fiorentina v Lyon,

Villarreal vMan U

Zenit St Petersburg v Juventus,

Jumatano, 26 Novemba 2008

[saa 4 dak 45 usiku]

Anorthosis Famagusta v Werder Bremen,

Atletico Madrid v PSV,

Bordeaux v Chelsea

CFR 1907 Cluj-Napoca v Roma,

Inter Milan v Panathinaikos,

Liverpool v Marseille,

Shakhtar Donetsk v Basle,

Sporting v Barcelona,

Thursday 20 November 2008

HABARI MBALIMBALI ZA LIGI KUU:

Theo Walcott kupasuliwa bega!

Chipukizi wa Arsenal, Theo Walcott, atafanyiwa operesheni ya bega baada ya kuteguka bega hilo juzi katika mazoezi ya kikosi cha Timu ya Taifa ya England kilichokuwa kikijitayarisha kucheza mechi ya kirafiki na Ujerumani.
Theo Walcott ana historia ya kuwa na matatizo ya bega hilo kwani mwaka 2007 alifanyiwa operesheni na kuwekewa pini. Hii majuzi katika mechi ya LIGI KUU dhidi ya Stoke City aliumia tena bega hilohilo.
Inatarajiwa chipukizi huyo atakosa mechi zote za Arsenal kwa mwaka huu 2008.


Benayoun atishia kuhama Liverpool

Myahudi Yossi Benayoun ametishia itabidi ahame Liverpool kwa sababu hapangwi na Meneja Rafa Benitez na badala yake humtumia kwa nadra kama mchezaji wa akiba.
Benayoun alijiunga Lierpool mwaka 2007 akitokea West Ham na mpaka sasa ameshacheza mechi 41 tu nyingi zikiwa kutokea benchi la akiba.

Luka Modric wa Spurs nje wiki 2!

Luka Modric atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki 2 ili kuuguza musuli wa nyonga baada ya kuumia katika mechi Tottenham waliyofungwa na Fulham mabao 2-1 wikiendi iliyokwisha.

MATOKEO MECHI ZA KIMATAIFA ZA JUMATANO 19 NOVEMBA 2008

Germany 1 England 2

Scotland 0 Argentina 1

Denmark 0 Wales 1

N Ireland 0 Hungary 2

Republic of Ireland 2 Poland 3

Brazil 6 Portugal 2

Colombia 1 Nigeria o

Venezuela o Angola 0

France 0 Uruguay 0
Powered By Blogger