Friday, 21 November 2008

MPASUKO NDANI YA ARSENAL: Nahodha Gallas apasua jipu hadharani!!!

Nahodha wa Arsenal, William Gallas, ametoboa hadharani kuwa timu yao ya Arsenal haina umoja, kuna mgawanyiko na Wachezaji hawana ushujaa na wala si wapiganaji.
Gallas amepasua jipu hilo huku Arsenal ikiendelea kusuasua kwenye LIGI KUU ikiwa pointi 9 nyuma ya vinara Chelsea na Liverpool na pointi moja nyuma ya Man U ambayo imecheza mechi moja pungufu.
Mpaka sasa, baada ya mechi 13 za LIGI KUU, Arsenal imeshapoteza mechi 4. Pia, hivi juzi tu imepita pigo jingine baada ya kuthibitishwa staa na chipukizi wao Theo Walcott atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 8 baada ya kuumia bega ambalo linahitaji kupasuliwa.
Gallas anaripotiwa kutamka: 'Wachezaji wa Arsenal si mashujaa vitani. Sasa timu haziogopi kuja Emirates na kucheza mpira kwani washajua sisi ni waoga. Vilevile tuna Wachezaji kiburi. Katika mechi unaambiwa kama Nahodha kuna Mchezaji analalamikiwa na wenzake, unamfuata na anaanza kukukashifu! Hii haikubaliki! Tena Mchezaji huyo ni mdogo kwangu kwa miaka 6!'
Gallas ana umri wa miaka 31 na Wachezaji ambao wana umri wa miaka 25 ndani ya Arsenal ni Robin Van Persie, Emmanuel Eboue, Eduardo na Bacary Sagna.
Wachunguzi wanahisi Mchezaji anaetuhumiwa na Gallas ni Robin Van Persie.

No comments:

Powered By Blogger