Saturday, 22 November 2008

MPASUKO ARSENAL: Baada ya kuanika 'chupi chafu' hadharani, Nahodha Gallas anyang'anywa Unahodha!!!!!

Taarifa zilizozagaa kila kona ya ulimwengu wa soka zimebaini Nahodha wa Arsenal William Gallas amevuliwa Unahodha wa timu hiyo mara tu baada ya kutamka hadharani kuwa mambo si shwari ndani ya kambi ya 'Washika Bunduki'.
Gallas, mwenye umri wa miaka 31 aliejiunga Arsenal Septemba 2006 na kuteuliwa kuwa Nahodha Agosti 2007, alisema kuwa Timu ya Arsenal ina mgawanyiko, kiburi na waoga.
Vilevile alimtuhumu Mchezaji mmoja, anaesadikiwa kuwa ni Robin Van Persie, ndie kiini cha mzozo huu.
Arsenal ambayo leo jioni inacheza ugenini ikikabiliana na Manchester City imemuacha Gallas kwenye msafara wa timu hiyo iliyoondoka London jana kuelekea Manchester.
Wadau wengi walianza kumponda Gallas tangu msimu uliopita pale alipoonyesha dhahiri uwanjani kuwa hawezi kuwa kiongozi, wakati timu yake ikicheza na Birmingham, Refa alipoipa Birmingham penalti dakika ya mwisho ya mchezo na Gallas badala ya kuwahamasisha wenzake kama Nahodha anavyotakiwa yeye aliamua kwenda kukaa chini kwenye duara la kati ya uwanja na kuanza kulia.
James McFadden wa Birmingham alifunga penalti hiyo ya dakika ya mwisho na mechi ikaisha suluhu na kufanya uongozi wa Arsenal kwenye ligi wakati huo upungue na kuwa pointi mbili tu.
Mara baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo Gallas, huku akibubujikwa machozi, alilipiga mateke bango la matangazo pembezoni mwa uwanja.
Kuanzia hapo Arsenal ikaporomoka na katika mechi 10 zilizofuata ikashinda 2 tu na kuwaachia Man U kunyakua ubingwa.

No comments:

Powered By Blogger