Thursday 22 October 2009

Chelsea waomba kifungo kisimamishwe hadi rufaa yao iishe!!
Chelsea wameiomba CAS [Court of Arbitration for Sport], Mahakama ya Usuluhishi Michezoni, isimamishe adhabu waliyopewa na FIFA ya kutosajili Wachezaji hadi 2011 kwa kosa la kumrubuni na kumsajili kinyume cha sheria Chipukizi kutoka FC Lens ya Ufaransa, Gael Kakuta, mwaka 2007 hadi hapo uamuzi wa rufaa yao kwa CAS utakapotolewa.
Kakuta, ambae sasa ana miaka 18, amefungiwa miezi minne na kutakiwa kuilipa fidia FC Lens Pauni 710,000.
Chelsea imetakiwa pia iilipe FC Lens Pauni 118000 kama fidia ya kumfundisha Kakuta.
CAS bado haijapanga lini itasikiliza rufaa hiyo ya Chelsea.
Wachezaji wa Ujerumani kuvaa Vesti za Deraya ili kuzuia risasi huko Bondeni!!
Wachezaji wa Ujerumani watakaokuwa Kikosi cha Ujerumani cha Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani kwenye Fainali wameambiwa iwatalazimu kuvaa vesti za kuzuia risasi ikiwa watataka kutoka nje ya Hoteli watakayofikia huko Afrika Kusini.
Mkuu wa Ulinzi wa Kampuni ya BaySecur ambayo huwalinda Chama cha Soka cha Ujerumani na wageni zake amesema inabidi Wachezaji wawe waangalifu zaidi Afrika Kusini hasa kwa vile ujambazi umekithiri na ikiwalazimu kutoka nje ya Hoteli yao basi inabidi wapewe eskoti yenye silaha na Wachezaji wavae vesti hizo za kuzuia risasi.
Chakula cha Man U chaharibiwa na Idara ya Forodha Urusi!!!!
Chakula cha kwenye ndege ambayo ilikwenda kuwabeba Manchester United huko Moscow, Urusi ili kuwarudisha Manchester mara baada ya kuwafunga CSKA Moscow 1-0 katika mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE hapo jana kiliamriwa kiharibiwa na Idara ya Forodha ya Uwanja wa Moscow kwani uingizwaji wake ulikiuka kanuni za Urusi.
Chakula hicho maalum kiliagizwa na Uongozi wa Manchester United na kilikuwa na lishe maalum ili kuwawezesha Wachezaji kujenga miili yao baada ya mechi yao na CSKA hasa ukichukulia wana mechi ya Lig Kuu na Mahasimu wao wakuu Liverpool siku ya Jumapili huko Anfield.
Wachezaji wa Manchester United walitegemewa kupata mlo huo wakiwa kwenye safari kutoka Moscow kurudi Manchester ambayo huchukua masaa manne.
Parreira: Afrika Kusini wakinipa ofa ntaifikiria!
Carlos Alberto Parreira amesema akipewa ofa na Afrika Kusini ili kuwa Kocha wa Bafana Bafana ataifikiria ipasavywo.
Afrika Kusini ndio Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa kuanzia Juni 11, 20010 hadi Julai 11, 2010 na kwa sasa hawana Kocha baada ya kumtimua Mbrazil mwenzake Parreira, Joel Santana ambae alishika wadhifa huo kutoka kwa Parreira alielazimika kuuacha baada ya Mke wake kuugua mwaka jana.
Hata hivyo, kipindi cha Santana, Bafana Bafana ilifungwa mechi 8 kati ya 9 ilizocheza mwisho na hilo ndilo lilimfanya atimuliwe.
Parreira, aliyekuwa Kocha wa Brazil iliyochukua Kombe la Dunia mwaka 1994, amesema: “Kuna chansi ntapewa ofa! Ntaiangalia! Wao wanataka waendelee na Kocha wa Brazil kwani wanaamini staili ya Brazil ndio inayoifaa Afrika Kusini. Kocha atakaeichukua Afrika Kusini atalazimika kuondoa balaa la kufungwa! Morali ni ndogo kwao!”
LEO EUROPA LIGI!!
Baada ya kunguruma kwa UEFA CHAMPIONS LIGI jana na juzi, leo ni zamu ya EUROPA LIGI kutawala anga za Ulaya kwa mechi kadha wa kadha.
Timu za Uingereza zitazoshuka dimbani leo ni Everton, Fulham na Celtic.
Mechi zao ni:
Benfica v Everton
Fulham v AS Roma
Celtic v Hamburger SV
MECHI NYINGINE NI:
Ajax v Dinamo Zagreb,
Athletic Bilbao v Nacional,
BATE v AEK Athens,
Club Brugge v Partizan Belgrade,
CSKA Sofia v Basle,
FC Sheriff Tiraspol v FC Twente,
FK Austria Vienna v Werder Bremen,
FK Ventspils v Sporting,
Galatasaray v Dinamo Bucharest,
Hapoel Tel-Aviv v Rapid Vienna,
Hertha Berlin v Heerenveen,
Lazio v Villarreal,
Lille v Genoa,
Panathinaikos v SK Sturm Graz,
Politehnica Timisoara v Anderlecht,
PSV v FC Copenhagen,
Shakhtar Donetsk v Toulouse,
Sparta Prague v CFR 1907 Cluj-Napoca,
Steaua Bucharest v Fenerbahce,
SV Red Bull Salzburg v Levski Sofia,
Valencia v Slavia Prague,
UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Mechi za Jana!!!
Real Madrid wabamizwa kwao, Chelsea ushindi mnono na Bayern apigwa!!
KUNDI C
Makosa ya Makipa wa pande zote mbili, jana walifanya mechi ya Real Madrid na AC Milan iwe na lundo la magoli lakini alikuwa Chipukizi toka Brazil, Pato, alieipa ushindi AC Milan wakiwa ugenini Uwanjani Santiago Bernabeu.
Mechi hii iliisha kwa ushindi wa AC Milan wa bao 3-2.
Katika mechi nyingine ya Kundi hili, Mchezaji wa zamani wa Real Madrid na Manchester United, Mlinzi Gabriel Heinze aliipa ushindi Klabu yake Marseille wa bao 1-0.
KUNDI A
Bordeaux waliifunga Bayern Munich 2-1 katika mechi iliyokuwa na goli la kujifunga, penalti 2 kukoswa na Kadi Nyekundu 2.
Bayern waliongoza kwenye dakika ya 6 baada ya Michael Ciani kujifunga mwenyewe lakini Ciani alijirekebisha na kuisawazishia Bordeaux.
Bayern wakabaki mtu 10 baada ya Thomas Mueller kupewa Kadi 2 za Njano na hivyo kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu na dakika 5 kabla mapumziko, Marcus Planus akaifungia Bordeaux bao la pili.
Kisha Yoann Gourcuff akakosa penalti ya kwanza ya Bordeaux na akafuata Daniel van Bueyten wa Bayern kupewa Kadi Nyekundu baada ya kumchezea faulo Marouane Chamakh ndani ya boksi lakini penalti iliyopigwa na Jussie haikuzaa goli kwa Bordeaux na hivyo kukosa penalti 2 katika mechi hiyo.
Katika mechi nyingine ya Kundi hili Juventus waliifunga Maccabi Haifa 1-0.
KUNDI D
Chelsea wakiwa nyumbani Stamford Bridge waliishindlia Atletico Madrid mabao 4-0 kwa mabao ya Salomon Kalou, mawili, Frank Lampard na la kujifunga mwenyewe la Luis Perea.
FC Porto waliifunga Apoel Nicosia 2-1.
KUNDI B
Wolfsburg walitoka suluhu 0-0 na Besiktas na Manchester United walishinda ugenini 1-0 dhidi ya CSKA Moscow.

Wednesday 21 October 2009

CSKA Moscow 0 Man U 1
Kwenye Uwanja wa nyasi bandia, Luzhniki Stadium, ambazo hata UEFA hawakuziruhusu kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE mwaka jana Man U walipowaua Chelsea na kutwaa Ubingwa wa Ulaya, leo Manchester United wamewafunga wenyeji wao CSKA Moscow kwa bao 1-0.
Mechi hii iliyochezwa mjini Moscow, Urusi ilianza mapema kupita mechi nyingine za leo za UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Bao la ushindi la Manchester United lilipachikwa na Winga Antonio Valencia dakika ya 86.
Manchester United yuko kileleni Kundini mwao akiwa na pointi 9.
Vikosi vilikuwa:
CSKA Moscow: Akinfeev, Semberas, Ignashevich, Alexei Berezutsky, Vasili Berezutsky, Odiah, Rahimic, Schennikov, Krasic, Dzagoev, Necid.
AKIBA: Pomazan, Daniel Carvalho, Mamaev, Aldonin, Piliev, Oliseh, Grigoriev.
Man Utd: Van der Sar, Neville, Ferdinand, Vidic, Fabio Da Silva, O'Shea, Valencia, Scholes, Anderson, Nani, Berbatov.
AKIBA: Kuszczak, Brown, Owen, Carrick, Welbeck, Jonathan Evans, Macheda.
Refa: Claus Bo Larsen (Denmark).
Misri kupasha na Bongo!!!
Timu ya Taifa ya Misri imejitoa kucheza na Ujerumani mechi ya kirafiki mwezi ujao na badala yake itacheza na Tanzania kabla ya pambano lao la kufa na kupona na Algeria la Kombe la Dunia la kuwania nani ataenda Fainali Kombe la Dunia.
Mechi hiyo kirafiki kati ya Misri na Tanzania itachezwa Novemba 5 na taarifa za mechi zimethibitishwa na Kocha Msaidizi wa Misri Shawki Gharib aliesema: “Tumeamua kucheza na Tanzania ingawa mechi hiyo haipo kwenye Kalenda ya FIFA ya mechi za Kimataifa. Hio ndio sababu kwa vile Tanzania haina Wachezaji wanaocheza nje na inakuwa rahisi kucheza nao nje ya Kalenda ya FIFA.”
Algeria wako pointi 3 mbele ya Misri kwenye Kundi lao na mechi hiyo kati ya Misri na Algeria itakayochezwa Cairo ni muhimu kwa Misri wanaohitahi ushindi wa 3-0 ili kwenda Fainali Kombe la Dunia.
Katika mechi ya mwisho ya Kundi lao, Misri waliifunga Zambia 1-0 huko Lusaka.
Fergie asusa Mkutano na Waandishi baada ya swali kuhusu Refa Wiley!!
Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson aligoma kuendelea na mkutano wa Waandishi wa Habari uliokuwa ukifanyika Uwanjani Luzhniki huko Moscow, Urusi baada ya kuulizwa swali kuhusu kesi yake na FA iliyotokana na kauli yake kuwa Refa Alan Wiley hayuko fiti.
Ferguson amepewa na FA mpaka Novemba 3 kuwasilisha utetezi wake kuhusu mashitaka yanayohusiana na kesi hiyo.
Baada ya kuulizwa swali kuhusu Refa Alan Wiley, Ferguson aliinuka na kutoka chumba cha mahojiano baada ya kutamka: “Swali la kipumbavu na halipati jibu! Nipo kwenye mkutano huu kuhusu mechi na CSKA Moscow!”
Boro yamtimua Southgate!!!
Timu iliyoshushwa Daraja toka Ligi Kuu msimu uliopita, Middlesbrough, imemfukuza kazi Meneja wao Derek Southgate ambae walikuwa nae kwa miaka mitatu na nusu.
Klabu ya Middlesbrough pia imetamka msaidizi wake Alan Smith nae ameondolewa na Makocha Colin Cooper na Steve Agnew watakaimu nafasi ya Umeneja kwa muda.
Klabu hiyo ipo Ligi ya Coca Cola Championship iliyo chini tu ya Ligi Kuu England.
Derek Southgate alichukua wadhifa wa Umeneja baada ya Meneja aliekuwepo Steve McClaren kuteuliwa kuwa Meneja wa England.
Kabla ya uteuzi huo wa kuwa Meneja wa Boro, Southgate alikuwa ni Mchezaji wa klabu hiyo akicheza kama Sentahafu.
TATHMINI-UEFA CHAMPIONS LEAGUE LEO:
RATIBA: Jumatano, Oktoba 21
Bordeaux v Bayern Munich,
CSKA Moscow v Manchester United
Chelsea v Atletico Madrid,
FC Porto v Apoel Nicosia,
FC Zurich v Marseille,
Juventus v Maccabi Haifa,
Real Madrid v AC Milan,
Wolfsburg v Besiktas,
Manchester United wako ugenini Urusi kucheza na CSKA Moscow kwenye Uwanja wa Luzhniki wenye nyasi bandia ambao huwa mgumu kuchezea kwa timu ngeni.
Mechi hii itaanza mapema kupita zote na itaanza saa 1 na nusu usiku saa za bongo.
Hata hivyo, Manchester United wanaukumbuka vyema uwanja huo kwani Mei 2008 ndipo waliponyakua Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE walipowabwaga Chelsea.
Man U wako huko Moscow bila Mastaa wao Giggs, Rooney, Evra, Fletcher na Park ambao wameachwa Manchester kwa kuwa ni majeruhi.
Mpaka sasa kwenye Kundi lao Man U ndio wako juu baada ya kuzishinda Besiktas na Wolfsburg katika mechi mbili za kwanza.
CSKA Moscow, wanafundishwa na Kocha wa zamani wa Tottenham Juande Ramos, wameshinda mechi moja na kufungwa moja. Walifungwa na Wolfsburg na wao kuifunga Besiktas.
Katika Kundi hili B mechi nyingine ya leo ni kati ya Wolfsburg na Besiktas.
Kundi D, Chelsea wanaoongoza Kundi hili wapo nyumbani Stamford Bridge na watacheza na Atletico Madrid.
Katika mechi nyingine ya Kundi hilI FC Porto watawakaribisha Apoel Nicosia huko Ureno.
Kundi C, leo ni mechi ya Miamba Real Madrid na AC Milan mechi inayochezwa nyumbani kwa Real Uwanjani Santiago Bernabeu.
Katika mechi hiyo, Nyota wa Brazil Kaka leo, kwa mara ya kwanza, atapambana na Klabu yake ya zamani AC Milan.
Mechi nyingine ya Kundi C ni kati ya FC Zurich na Marseille.
Real Madrid ndie anaeongoza Kundi C huku FC Zurich akifuatia.
Mechi za Kundi A za leo ni Bordeaux v Bayern Munich na juventus v Maccabi Haifa.
Bayern Munich ndie anaongoza Kundi hili akiwa pointi sawa na Bordeaux lakini bAyern yuko mbele kwa magoli.
JANA-USIKU WA MAAJABU ULAYA!!!
MASKINI: Liverpool ni vipigo mfululizo!!!! Barca waaibishwa Nou Camp!!!
Mechi za jana za UEFA CHAMPIONS LEAGUE zimeleta matokeo yasiyotarajiwa na magoli bwelele huku ajabu kubwa ni pale Warusi Rubin Kazan walipowakung’uta Mabingwa Watetezi wa Ulaya FC Barcelona kwa bao 2-1 tena wakiwa nyumbani kwao Nou Camp.
Liverpool wameendelea kupata vipigo mfululizo ingawa jana sio puto ndio liliwafunga bali ni goli la dakika za majeruhi wakiwa kwenye ngome yao Anfield na pia kupata athari kubwa pale mhimili wao na Nahodha wao Steven Gerrard kucheza dakika 25 tu za mwanzo na kulazimika kutoka baada ya kuumia.
Matokeo ya mechi ya jana ambayo Liverpool alifungwa 2-1 na Lyon ya Ufaransa yamedhihirisha ile imani ya wengi kuwa Liverpool bila Gerrard na Torres ni nyanya tu. Jana Torres hakucheza kabisa.
Sasa, baada ya vipigo mfululizo, Jumapili kwenye Ligi Kuuu, Liverpool wanawakaribisha Mahasimu wao wakubwa Manchester United na hilo linawatia homa Mashabiki wa Liverpool.
Arsenal wakiwa ugenini huko Uholanzi na huku wakiongoza bao 1-0 walilazimishwa sare ya 1-1 na AZ Alkmaar.
Rangers ya Scotland iliadhiriwa vibaya ikiwa nyumbani baada ya kuchapwa bao 4-1 na Unirea Urziceni.
Sevilla, baada ya mechi 3 tu, wameweka rekodi huko Ulaya baada ya kufuzu kusonga mbele Raundi nyingine baada ya mechi 3 tu.
Matokeo kamili mechi za jana Jumanne, Oktoba 20:
KUNDI E
Liverpool 1 Lyon 2
Debrecen 3 Fiorentina 4
KUNDI F
Inter Milan 2 Dynamo Kiev 2
Barcelona 1 Rubin Kazan 2
KUNDI G
Stuttgart 1 Sevilla 3
Rangers 1 Unirea Urziceni 4
KUNDI H
AZ Alkmaar 1 Arsenal 1
Olympiakos 2 Standard Liege 1

Tuesday 20 October 2009

Blatter kuwania tena Urais FIFA 2011!!!
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, ametoboa kuwa atasimama tena kwenye uchaguzi wa kugombea Urais FIFA hapo mwaka 2011.
Blatter ambae yupo kwenye wadhifa huo tangu 1998 amesema: “Bado sijakamilisha misheni yangu kwenye Soka!”
Blatter, mwenye umri wa miaka 78 na ni raia wa Uswisi, alichukua wadhifa huo toka kwa Joao Havelange wa Brazil.
Akisisitiza, Blatter ametamka: “Sijamaliza misheni yangu kwenye Soka! Nahitaji muda zaidi! Natumai mwaka 2011, Kongresi ya FIFA itanipa imani la sivyo ntarudi kijijini kwangu! Soka ni maisha yangu!”
BAADA YA GOLI LA PUTO [Mpira wa Bichi]:
Washabiki wa Man U kusachiwa, kunyang’anywa Mipira ya Bichi Anfield Jumapili ijayo!!!
Jumapili ijayo huko Uwanjani Anfield, Mashabiki wa Manchester United ambao wataingia uwanjani kwenda kushuhudia pambano la Ligi Kuu baina ya Liverpool na Manchester United watalazimika kusachiwa na kunyang’anywa Mipira ya Bichi ili kuwazuia wasishangilie kwa kebehi na pengine kusababisha goli kama alilofunga Mshambuliaji wa Sunderland Darren Bent Jumamosi iliyopita pale Liverpool walipopigwa 1-0 baada ya mpira kuugonga mpira wa bichi uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kumhadaa Kipa Pepe Reina.
Wakati huo huo, Polisi wamesema wanalichunguza tukio hilo la kurushwa mpira huo wa bichi uwanjani na mpaka sasa hawajamtambua Kijana alieurusha ingawa picha yake ilionekana waziwazi kwenye mikanda ya video.
Pia kuna taarifa kuwa Washabiki wa Liverpool wameonyesha chuki na hata kutoa vitisho kwa Kijana huyo alierusha mpira huo wa bichi ingawa nae pia ni Shabiki wa Liverpool.
Lakini baadhi ya watu wamemtetea Kijana huyo na kusema ingawa hakupaswa kurusha mpira huo wa bichi lakini alipourusha Kipa Pepe Reina aliuona na kuutoa nje ya uwanja nyuma ya goli lakini ulitulia dakika chache na kupeperushwa tena uwanjani na ndipo shuti la Darren Bent likaubabatiza na kumwacha Reina akitaka kudaka mpira huo wa bichi mwekundu huku mpira riali ukitinga wavuni.
JANA LIGI KUU: Fulham 2 Hull City 0
Kwenye mechi pekee ya Ligi Kuu hapo jana usiku, Fulham ikiwa nyumbani Craven Cottage imeitwanga Hull City mabao 2-0.
Mabao ya Fulham yamefungwa na Bobby Zamora dakik 2 kabla haftaimu baada ya shuti la Damien Duff kutemwa na Kipa Boaz Myhill na la pili alifunga Diomansy Kamara baada ya pande tamu la Zamora.
Kwa ushindi huo, Fulham imejinasua toka Timu 3 za mwisho na sasa wako nafasi ya 12 wakiwa na pointi 10 na Hull City bado wamejikita kwenye nafasi 3 za mwisho.
Fergie kwenda kujitetea mwenyewe kesi yake FA!!!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ataomba kwenda kutoa utetezi wake mwenyewe wakati kesi yake aliyoshitakiwa na FA itakaposikilizwa.
Ferguson ameshitakiwa kwa kosa la ‘kuonyesha mwenendo usioridhisha’ baada ya kutoa matamshi tarehe 3 Oktoba kwamba Refa Alan Wiley aliechezesha mechi ya Ligi Kuu kati ya Manchester United na Sunderland iliyoisha 2-2 hakuwa fiti.
Ingawa Ferguson aliomba radhi kwa kauli yake kwa Refa Alan Wiley, FA iliamua kumshitaki na amepewa mpaka Novemba 3 kuwasilisha utetezi wake.
Wiki iliyopita FA ilimpa onyo badala ya faini au kifungo au vyote Meneja wa Liverpool Rafa Benitez kwa shitaka kama la Ferguson kwa vile ana rekodi nzuri lakini Wadadisi wa mambo wanahisi Sir Alex Ferguson itakuwa ngumu kwake kukwepa adhabu kali hasa kwa vile siku za nyuma ameshawahi kupatikana na hatia kwa kosa kama hilo pale alipopigwa Faini Pauni 5000 baada ya kumvaa Refa Mark Clattenburg haftaimu kwenye mechi na Bolton misimu miwili iliyopita.
Pia ashawahi kufungiwa mechi mbili baada ya kukwaruzana na Refa Mike Dean kwenye mechi ambayo Man U waliifunga Hull City.
UEFA CHAMPIONS LEAGUE kunguruma leo Ulaya!!:
Leo ni Liverpool v Lyon na AZ Alkmaar v Arsenal
Jumanne, 20 Oktoba 2009
[saa 3 dak 45 usiku]
AZ Alkmaar v Arsenal,
Barcelona v Rubin Kazan,
Debrecen v Fiorentina,
Inter Milan v Dynamo Kiev,
Liverpool v Lyon,
Olympiakos v Standard Liege,
Rangers v Unirea Urziceni,
VfB Stuttgart v Sevilla,
KESHO:
Jumatano, 21 Oktoba 2009
Bordeaux v Bayern Munich,
CSKA Moscow v Manchester United
Chelsea v Atletico Madrid,
FC Porto v Apoel Nicosia,
FC Zurich v Marseille,
Juventus v Maccabi Haifa,
Real Madrid v AC Milan,
Wolfsburg v Besiktas,
Tathmini:
Liverpool v Lyon
Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard yuko fiti kucheza mechi ya leo ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE nyumbani Anfield lakini Straika Fernando Torres ataikosa mechi hii kwa vile bado ni majeruhi.
Wachezaji wote hao wawili hawakucheza Jumamosi kwenye kipigo cha ‘Goli la Puto” katika mechi ya Ligi Kuu waliyofungwa 1-0 na Sunderland.
Liverpool wako nafasi ya 3 kwenye KUNDI E baada ya kushinda mechi moja na kufungwa moja huku Wapinzani wao wa leo kutoka Ufaransa Lyon ndio wanaongoza kwa kushinda mechi zao mbili za kwanza.
Kipigo cha Liverpool cha Jumamosi mikononi mwa Sunderland ni kipigo chao cha 4 katika Ligi msimu huu lakini Meneja Rafa Benitez amesema: “Tukishinda leo na Lyon, Timu itapata moyo na tukishinda Jumapili ijayo na Manchester United nina uhakika hali yetu itakuwa tofauti kabisa!”
Lyon siku ya Jumamosi kwenye ligi ya kwao Ufaransa walipata kipigo chao cha kwanza msimu huu walipofungwa 2-0 na Sochaux huku wakicheza bila Mastaa wao Sidney Govou, Kim Kallstrom, Cleber Anderson, Mathieu Bodmer na Jean-Alain Boumsong ambao wote wanategemewa kucheza leo.
Kikosi cha Liverpool kitatokana na: Reina, Johnson, Carragher, Agger, Skrtel, Insua, Aurelio, Dossena, Benayoun, Riera, Gerrard, Mascherano, Lucas, Babel, Voronin, Kuyt, Ngog, Spearing, Cavalieri, Darby, Plessis.
AZ Alkmaar v Arsenal
Leo Arsenal watacheza bila Wachezaji majeruhi Tomas Rosicky na Theo Walcott watakapokuwa Uwanjani DSB Stadion huko Uholanzi kucheza na AZ Alkmaar kwenye mechi ya Kundi H ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Wachezaji wengine wa Arsenal watakaokosa mechi ya leo kwa kuwa ni majeruhi ni Samir Nasri, Kipa Lukasz Fabianski, Nicklas Bendtner, Eduardo, Denilson na Johan Djourou.
Ingawa Kipa Manuel Almunia amepona ugonjwa aliokuwa ameumwa lakini huenda akakosa namba kwa vile Kipa Chipukizi Vito Mannone ameonyesha umahiri mkubwa katika mechi alizocheza hadi sasa.
Mpaka sasa katika Kundi H, Arsenal hawajafungwa baada ya kuzishinda TImu za Olympiakos na Standard Liege katika mechi za awali na ndio wanaoongoza Kundi hili.
AZ Alkmaar inafundishwa na Staa wa zamani wa Uholanzi Ronald Koeman na ingawa wako mkiani kwenye Kundi H baada ya kutoka sare mechi moja na kufungwa moja ni wagumu mno kufungika kwao kwani katika mechi 34 za Makombe ya Ulaya walizocheza nyumbani wamefungwa mechi moja tu.
Kikosi cha Arsenal kitatokana na: Mannone, Clichy, Gallas, Vermaelen, Sagna, Eboue, Song, Fabregas, Diaby, Arshavin, van Persie, Almunia, Vela, Gibbs, Silvestre, Merida, Wilshere, Ramsey.
Santana si Kocha tena Bondeni!!!
Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini na Kocha wao Joel Santana kutoka Brazil wameafikiana kuvunja mkataba kati yao na kwa hivyo Timu ya Taifa ya Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana au ukipenda siku hizi ‘Watoto wa Vuvuzela’, sasa haina Kocha na Wasaidizi Pitso Mosimane na Jairo Leal wataiongoza Timu hiyo kwa muda.
Uamuzi wa Santana kutengana na Afrika Kusini umetangazwa jana na hilo limefuatia matokeo mabaya ya Bafana Bafana tangu Santana aanze kuifundisha Aprili, 2008 alipochukua nafasi ya Mbrazil mwenzake Carlos Alberto Parreira ambae alilazimika kuondoka kurudi kwao Brazil baada ya kuuguliwa na mkewe.
Rais wa SAFA, Chama cha Soka Afrika Kusini, Kirsten Nematandani, amesema sasa wanatafuta Kocha mwingine haraka iwezekanavyo ili wajiandae vyema kama Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa kuanzia Juni 11 hadi Julai 11 mwakani.

Monday 19 October 2009

SAKATA LA ‘GOLI LA PUTO JEKUNDU’: Ligi Kuu yasema mechi ya Sunderland na Liverpool hairudiwi!!!
Ligi Kuu England imetamka kuwa mechi ya Sunderland na Liverpool ambayo Liverpool alifungwa 1-0 kwa bao la Darrent Bent dakika ya 5 ya mchezo baada ya kufumua shuti lililougonga ‘mpira wa bichi’ uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kisha kumbabaisha Kipa wa Liverpool Pepe Reina na kutinga wavuni haiwezi kurudiwa licha ya ukweli kuwa Refa Mike Jones alifanya kosa kubwa kulikubali goli hilo.
Kufuatana na Sheria za mpira ilitakiwa Refa akatae goli hilo kwa vile mchezo uliingiliwa na kitu toka nje na kisha alitakiwa aamue mpira udondoshwe kati ya Wachezaji wawili, mmoja wa Sunderland na mwingine wa Liverpool, ili kuuanzisha tena mchezo.
Msemaji wa Ligi Kuu amesema haiwezekani mechi hiyo kurudiwa kwa vile FIFA inaamini na kufuata ile desturi kuwa ‘uamuzi wa Refa ni wa mwisho.’
Hata hivyo, FIFA, miaka minne iliyopita yenyewe ilienda kinyume na hiyo desturi yao pale ilipoamuru mechi ya Mtoano wa Kombe la Dunia kati ya Uzbekistan na Bahrain irudiwe baada ya kugundulika Refa alifanya kosa kwa kulikataa goli walilofunga Uzbekistan kwa penalti na kuamua Baharain wapige frikiki wakati uamuzi sahihi ulikuwa ni kuamua penalti ipigwe tena.
Mbali ya kuonekana wameonewa, Klabu ya Liverpool haina mpango wa kushika bango mechi irudiwe na hata Meneja wao Rafa Benitez amekiri kuwa ni suala la kiufundi ingawa inawezekana hakujua kuwa kisheria lile goli halikuwa halali.
Nae Steve Bruce, Meneja wa Sunderland, amekubali kuwa alikuwa hajui kama kisheria lile goli si halali lakini amesema mara nyingine maamuzi huenda kinyume nao.
Owen: “Sikuisaliti Liverpool kwa kujiunga Man U!!”
Mchezaji wa Manchester United Michael Owen amekubali kuwa atapata wakati mgumu sana Jumapili ijayo pale Timu yake itakapokwenda Anfield kucheza mechi ya Ligi Kuu na Wapinzani wao wa jadi Liverpool, Klabu ambayo ndiyo alianza kuichezea.
Huku akisisitiza yeye si msaliti, Michael Owen alisema: “Nikicheza na kufunga goli ntashangilia kama kawaida! Lazima wakubali mie ni binadamu. Ningependa watu watambue mchango wangu kwao nilipochezea Liverpool na watambue kuwa sasa nipo kwa Mahasimu wao Man U na nitacheza kwa nguvu zote!”
Owen ameendelea kueleza: “Watu wanazungumzia uaminifu na kwa Shabiki ni rahisi kuzungumzia hilo! Lakini mie ni Baba, Kaka na Mtoto na ni Mchezaji ambae anatafuta kula yake na ailishe Familia yake! Nilipokuwa mtoto niliishabikia Everton wapinzani wa Liverpool lakini sikuchezea Everton na nikachezea Liverpool! Nimechezea Real Madrid na mie si Shabiki wa Real! Hii ni kazi kama kazi nyingine!”
Hughes anaamini “BIGI 4” msimu huu watakwama!!!!
Mark Hughes ambae ni Meneja wa ‘Timu Tajiri’ Manchester City amesema anaamini hao wanaoitwa “BIGI 4”, yaani Manchester United, Chelsea, Liverpool na Arsenal ambao wamekuwa wakiitawala Ligi Kuu miaka ya hivi karibuni, msimu huu watakwama na kufungwa na Timu nyingine.
Mpaka sasa msimamo wa Ligi Kuu ni kama ufuatavywo:
1. Manchester United mechi 9 pointi 22
2. Chelsea mechi 9 pointi 21
3. Tottenham mechi 9 pointi 19
4. Arsenal mechi 8 pointi 18
5. Man City mechi 8 pointi 17
6. Aston Villa mechi 8 pointi 16
7. Sunderland mechi 9 pointi 16
8. Liverpool mechi 9 pointi 15
Mark Hughes amesema: “Unaweza kuhisi msimu huu hao ‘BIGI 4’ wanafungika! Hili ni nzuri kwa ligi! Wameshapoteza pointi nyingi mwanzoni na watapoteza nyingi tu!”
Refa aliekubali “GOLI LA PUTO” abwagwa kuchezesha Daraja la chini Wikiendi ijayo!!
Refa Mick Jones aliechezesha mechi ya Ligi Kuu kati ya Sunderland na Liverpool Jumamosi iliyopita na kukubali goli lililofungwa baada ya mpira kuugonga ‘mpira wa bichi’ uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kumbabaisha Kipa Pepe Reina, ameondolewa kuchezesha Ligi Kuu na badala yake atachezesha mechi ya Daraja la Chini kati ya Peterborough na Scurnthorpe.
Ingawa Kipa Pepe Reina na wenzake walilalamika Refa huyo alilikubali goli hilo kinyume na sheria.
Fergie ashitakiwa na FA!!!
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, ametakiwa ajibu mashitaka ya “kutokuwa na mwenendo wa kuridhisha” ifikapo Novemba 3 kufuatia kauli aliyoitoa hapo Oktoba 3 mara baada ya mechi ya Man U na Sunderland iliyoisha 2-2 pale alipomsema Refa Alan Wiley hayuko fiti kuchezesha mechi kwa kuwa alikuwa akichukua muda mwingi kuwaonya, kuwapa Kadi na kuwaandika Wachezaji kwenye kitabu muda ambao ulimsaidia kupumzika.
Licha ya Sir Alex Ferguson kuomba radhi kwa kauli yake na pia kuiandikia FA kujieleza, leo FA imetangaza lazima ajibu mashitaka.
Endapo Ferguson atapatikana na hatia basi anaweza kupigwa faini au kuufungiwa kukaa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi au vyote viwili kwa pamoja.
Droo ya Mitoano ya Nchi za Ulaya kuwania nafasi 4 kutinga Fainali Kombe la Dunia 2010 yafanyika!!!
Mechi za Mtoano wa Nchi 8 za Ulaya zimepangwa leo ili kupata Timu 4 zitakazoenda Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na mechi hizo zitachezwa nyumbani na ugenini hapo Novemba 14 na marudio ni Novemba 18.
RATIBA:
Novemba 14
Republic of Ireland v France
Portugal v Bosnia-Hercegovina
Greece v Ukraine
Russia v Slovenia
Novemba 18
France v Republic of Ireland
Bosnia-Hercegovina v Portugal
Ukraine v Greece
Slovenia v Russia
Man U waenda Moscow leo bila Wachezaji Watano muhimu!!!
Rooney, Giggs waachwa!!!
Kikosi cha Manchester United leo kilipanda ndege kuelekea Moscow, Urusi ambako Jumatano watacheza na CSKA Moscow kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE bila ya Wachezaji wao watano maarufu wakiwemo Ryan Giggs na Wayne Rooney ambao ni majeruhi.
Wachezaji wengine walioachwa ni Patrice Evra, Park Ji-Sung na Darren Fletcher ambao pia ni majeruhi.
Ingawa Dimitar Berbatov na Nemanja Vidic walikuwamo kwenye msafara lakini hawana uhakika kama watachezeshwa kwa vile nao pia ni majeruhi.
Kikosi kilichopanda ndege ni:
Van der Sar, Kuszczak, Foster; Neville, Rafael, O'Shea, Ferdinand, Vidic, Brown, J Evans, Fabio; Valencia, Scholes, Carrick, C Evans, Anderson, Nani; Owen, Berbatov, Macheda, Welbeck.

Sunday 18 October 2009

Wigan 1 Man City 1
Mechi ya Ligi Kuu kati ya Wigan na Manchester City ndani ya KC Stadium, nyumbani kwa Wigan iliyochezeshwa na Refa Alan Wiley ambae wiki mbili sasa yuko kwenye vichwa vya habari Magazetini baada ya mzozo unaomhusu Sir Alex Ferguson, ilimalizika kwa sare ya 1-1 na Man City kuwa mtu 10 baada ya Refa Alan Wiley kumpa Kadi 2 za Njano Mlinzi toka Argentina Pablo Zabaleta.
Wigan walitangulia kufunga bao la kwanza dakika ya 45 mfungaji akiwa Charles N'Zogbia lakini Man City walirudisha dakika moja tu baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia Martin Petrov.
VIKOSI:
Wigan: Kirkland, Melchiot, Boyce, Bramble, Figueroa, Rodallega, Thomas, Diame, N'Zogbia, Scharner, Scotland.
AKIBA: Pollitt, Cho, Koumas, Gomez, Sinclair, Kapo, King.
Man City: Given, Zabaleta, Richards, Lescott, Bridge, Wright-Phillips, De Jong, Barry, Petrov, Tevez, Adebayor. AKIBA: Taylor, Johnson, Ireland, Santa Cruz, Sylvinho, Kompany, Weiss.
Refa: Alan Wiley
Listi ya Wagombea Mpira wa Dhahabu “Ballon d’Or” yatangazwa!!!
Ronaldo, Giggs, Rooney, Gerrard, Lampard na Terry ndani ya nyumba!!!
Mchezaji wa bei mbaya ambae ndie mshindi msimu uliokwisha wa Mpira wa Dhahabu, “Ballon d’Or”, Cristiano Ronaldo, yuko kwenye listi ya Wachezaji 30 waliotajwa ndio Wagombea wa Tuzo hiyo inayosifika ambayo hutolewa kila mwaka na Gazeti la Michezo la Soka la Ufaransa na hutambulika kama ndio ya ‘Mchezaji Bora wa Ulaya”.
Ronaldo alinyakua Tuzo hiyo mwaka jana akiwa ni Mchezaji wa Manchester United.
Mshindi wa Tuzo hiyo atatangazwa Desemba 1 huko Paris, Ufaransa.
Listi kamili, ikionyesha Ligi na Klabu wanazochezea ni ifuatayo:
Ligi Kuu England
Arsenal:
Andrey Arshavin
Cesc Fabregas
Chelsea:
Didier Drogba
Frank Lampard
John Terry
Liverpool:
Fernando Torres
Steven Gerrard
Manchester United:
Ryan Giggs
Wayne Rooney
Nemanja Vidic
Primera Liga
Real Madrid:
Karim Benzema
Kaka
Iker Casillas
Cristiano Ronaldo
Barcelona:
Thierry Henry
Zlatan Ibrahimovic
Andres Iniesta
Lionel Messi
Xavi
Yaya Toure
Valencia:
David Villa
Sevilla:
Luis Fabiano
Atletico Madrid:
Diego Forlan
Serie A
Juventus:
Diego
Inter Milan:
Samuel Eto'o
Julio Cesar
Maicon
Bundesliga
Wolfsburg:
Edin Dzeko
Bayern Munich:
Franck Ribery
Ligue 1
Bordeaux:
Yoann Gourcuff

HILI NDIO GOLI LA 'PUTO JEKUNDU!!!'
Pichani Kipa Pepe Reina wa Liverpool akibabaika adake mpira au 'puto jekundu' kwenye mechi ya jana ya Ligi Kuu ambayo Liverpool ikiwa ugenini ilifungwa na Sunderland bao 1-0 kwa goli ambalo sasa limebatizwa "GOLI LA PUTO JEKUNDU!".
'Puto' hilo, hakika ni mpira wa kuchezea bichi, ulitupwa uwanjani na Shabiki mmoja wa Liverpool alieketi nyuma ya goli na sekunde chache baadae Darren Bent wa Sunderland kupiga shuti lililoubabatiza mpira huo wa bichi na kumwacha Reina akitaka kudaka 'puto' hilo na mpira kutinga wavuni.
Blackburn 3 Burnley 2
Katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England kati ya mbili za leo Jumapili Oktoba 18, Blackburn Rovers wakiwa nyumbani Ewood Park, wamejinyakulia pointi 3 baada ya kuwapiga Burnley bao 3-2.
Burnley ndio walikuwa wa kwanza kufunga bao kwenye dakika ya 5 kupitia Robbie Black lakini Blackburn wakasawazisha dakika 3 baadae mfungaji akiwa Richard Dunne.
Dakika ya 20 Blackburn wakaongeza bao la pili mfungaji akiwa Straika wa Ureno Di Santo na Pascal Chimbonda akaipatia bao la 3 dakika ya 40.
Burnley walipata bao la pili kwenye dakika ya 90 mfungaji akiwa Mchezaji wa zamani wa Man U Chris Eagles na kuifanya mechi iwe patashika katika dakika za majeruhi huku Burnley wakipigana kusawazisha.
Mechi ya pili itakayoanza muda si mrefu kuanzia sasa ni kati ya Wigan na Manchester City.
Fergie aongea kuhusu Refa Alan Wiley
Sir Alex Ferguson ametoboa kuwa alimponda Refa Alan Wiley na kumwita hayuko fiti baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Timu yake Manchester United na Sunderland kumalizika 2-2 kwa sababu alikerwa na uchezaji wa Timu yake uliokuwa chini ya kiwango na walibahatika kupata suluhu baada ya goli la kujifunga mwenyewe kwa Beki wa Sunderland Anton Ferdinand, ambae ni mdogo wake mlinzi wa Man U Rio Ferdinand, dakika za majeruhi.
Sir Alex Ferguson ameshaomba radhi kwa kauli yake hiyo na pia ameshajieleza kimaandishi kwa FA, kama alivyoamriwa, na sasa Jumatatu Oktoba 19 atajua kama FA itamfungulia mashitaka au la.
Ferguson amesema: “Niliudhika na uchezaji wetu mbovu na hasira zilinifanya nimlaumu Refa Wiley! Ndio maana nikaona ni bora niombe radhi kwake! Nadhani atakubali kuomba kwangu msamaha na na ntajaribu kuongea nae uso kwa uso!”
GOLI LA PUTO JEKUNDU LISINGEKUBALIWA!
Refa wa zamani wa Ligi Kuu, Jeff Winter, ameshangazwa kwa kukubaliwa goli la Sunderland hapo jana walipoifunga Liverpool bao 1-0 kwani mpira uliopigwa kwenye dakika ya 5 ya mchezo na Straika Darren Bent wa Sunderland uligonga ‘mpira mwekundu wa bichi’ na kumbabaisha Kipa Pepe Reina wa Liverpool na kutinga wavuni. Mpira huo wa ‘bichi’ ulitupwa na Shabiki mmoja wa Liverpool aliekaa nyuma ya goli sekunde chache kabla tukio la goli.
Jeff Winter amesema: “Sheria za Soka ziko wazi! Kama kunatokea kitu nje ya uwanja na kuingilia mchezo basi ni wajibu wa Refa kusimamisha mchezo hadi kitu hicho kinaondolewa! Nadhani Marefa wa mechi hiyo walijua hilo lakini wamekosea kwa kulikubali goli!”
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, amekataa kulaumu ‘mpira huo wa bichi’ kwa kufungwa na alikri kuwa Timu yake haikucheza vizuri.
Jana Liverpool iliwakosa nguzo yao, Nahodha Steven Gerrard na Straika Fernando Torres, ambao ni majeruhi.
Powered By Blogger