Saturday, 28 February 2009

Refa Peter Walton aiomba Sheffield United msamaha kwa makosa katika uchezeshaji yalioipa Hull City ushindi!!

Refa Peter Walton ambae ni mmoja wa Marefa wanaochezesha LIGI KUU England amempigia simu Bosi wa Sheffield United Kevin Blackwell ili kumuomba msamaha kufuatia makosa makubwa yaliyofanywa kwenye mechi ya Kombe la FA kati ya Hull City na Sheffield United iliyochezwa Alhamisi na Hull City wakaibuka washindi 2-1.
Mshika Kibendera aliashiria kwa Mwamuzi Peter Walton kuwa bao la kwanza mpira ulivuka mstari kufuatia kichwa kibovu cha Mlinzi wa Sheffield United Kyle Naughton kugonga mwamba wa juu wa goli na kudunda mstarini na kutoka nje ya goli.
'Tulipoteza mechi ambayo hatukufungwa! Lile goli la kwanza mpira haukuvuka mstari!' Kevin Blackwell alilalamika. 'Na Refa alitunyima penalti ya wazi! Lakini huyu Refa ni mwungwana kwani amenipigia simu kuomba radhi baada ya kuona marudio ya mechi kwenye video na kuungama walikosea! Hakutakiwa kuomba radhi lakini ameomba, ni utu wa hali ya juu!'
CARLING CUP: Jumapili Fainali- Manchester United v Tottenham
Mabingwa Watetezi Kombe la Carling, Tottenham, Jumapili saa 12 jioni [bongo taimu] watajitupa Uwanjani Wembley, mjini London, kupambana na Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia, Manchester United, kuwania Kombe la Carling.
Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson, kawaida huchanganya kikosi chake kwenye Kikombe hiki Chipukizi na Maveterani na tayari ameshaambia Vijana Danny Welbeck na Darron Gibson kuwa wataanza Fainali hiyo ila amepata pigo baada ya kugundulika Chipukizi Rafael Da Silva hawezi kucheza kwa kuwa ana ufa mdogo kwenye mfupa wa enka na atakuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja.
Wachezaji wa Tottenham Robbie Keane, Wilson Palacios, Carlo Cudicini na Pascal Chimbonda wote hawaruhusiwi kucheza kwani walishacheza Kombe hili na Timu zao za zamani kabla ya kuhamia Tottenham msimu huu.
Vilevile, Mshambuliaji Chipukizi Frazier Campbell, haruhusiwi kucheza kwani bado ni Mchezaji wa Man U na yupo Tottenham kwa mkopo tu.
Akizungumzia mechi hii, Ferguson alisema: 'Bila shaka tunataka kushinda Fainali hii lakini ukweli ni kwamba umuhimu kwetu ni LIGI KUU na UEFA CHAMPIONS LEAGUE. Jumatano tunacheza LIGI KUU ugenini na Newcasle na hiyo ni mechi muhimu sana kuliko hii Fainali! Hivyo ntachaguwa Kikosi Jumapili huku nikifikiria Jumatano pia!'
Nae Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp amesema: 'Tunacheza na Timu Bora! Juzi walipocheza na Inter Milan walitisha! Lakini tuna Wachezaji wazoefu na bahati ikituangukia, tutacheza vizuri!'

MECHI ZA LIGI KUU England WIKIENDI:
Jumamosi, Februari 28
[saa 9.30 mchana bongo taimu]
Everton v West Bromwich
[saa 12]
Arsenal v Fulham
Chelsea v Wigan
Middlesbrough v Liverpool
Jumapili, Machi 1
[saa 9.30]
Hull v Blackburn
West Ham v Man City
[saa 10.00]
Bolton v Newcastle
[saa 12]
Aston Villa v Stoke City

Friday, 27 February 2009

Villa, Tottenham nje, Man City wasonga!!!

Aston Villa, wakipumzisha nusu ya kikosi chao thabiti, walipigwa goli 2-0 na CSKA Moscow mjini Moscow na hivyo kutolewa nje ya UEFA CUP kwa jumla ya mabao 3-1. Mechi ya kwanza ilikuwa 1-1.
Nao Tottenham walitoka suluhu 1-1 na Shakhtar Donetsk na kuyaaga mashindano kwani walifungwa 2-0 mechi ya kwanza.
Timu pekee ya England iliyofuzu ni Manchester City iliyoshinda 2-1 na kuitoa FC Copenhagen kwa jumla ya mabao 4-3.
Raundi ijayo Manchester City itakutana na Aalborg ya Denmark.

Thursday, 26 February 2009

Man City, Aston Villa na Tottenham leo wanajimwaga UEFA CUP kuwania nafasi ya Timu 16

Leo usiku Timu za LIGI KUU England Manchester City, Aston Villa na Tottenham wanajitupa uwanjani kuwania kuingia Raundi ya Timu 16 kwenye Kombe la UEFA mechi za leo zikiwa marudiano ya mechi za duru la kwanza lililochezwa wiki iliyokwisha.
Manchester City leo wako nyumbani kurudiana na FC Copenhagen na timu hizi zilitoka sare 2-2 katika mechi ya kwanza.
Aston Villa wako ugenini kurudiana na CSKA Moscow na mechi kati yao ya kwanza iliisha droo 1-1.
Tottenham, ingawa leo wako nyumbani, ndio wenye kibarua kikubwa kwani kwenye mechi ya kwanza walikutwa mabao 2-0 na Timu ya Ukraine Shakhtar Donetsk.
Mbali ya mechi hizi zinazohusu Timu za LIGI KUU England pia kuna mechi nyingine za UEFA CUP zinazohusisha timu 26 kwani raundi hii ina jumla ya timu 32.
Baadhi ya mechi za kuvutia za leo ni zile za marudiano kati ya Ajax na Fiorentina, AC Milan v Werder Bremen, Depotivo La Coruna v Aab, Galatasaray v Bordeaux, Valencia v Dynamo Kiev.
Liverpool waidonyoa Real kwao, Chelsea wapiga kimoja nyumbani, Bayern aua ugenini na Villareal, Panathinaikos ngoma droo!!!!

Jana UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliendelea kunguruma Ulaya huku Timu za England zikipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na karamu ya magoli iliwaangukia Bayern Munich pale walipoiangushia kipigo kikali Sporting Lisbon cha mabao 5-0 kulekule kwao Ureno.

Chelsea wakiwa ngomeni kwao Stamford Bridge waliwafunga Juventus bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Didier Drogba dakika ya 13 ya mchezo.

Liverpool, wakicheza ugenini Uwanja wa Santiago Bernabeu na wenyeji Real Madrid, walicheza mchezo wa kujihami lakini wakaondoka na ushindi wa bao 1-0 pale Yossi Benayoun alipopachika kwa kichwa dakika ya 82.

Villareal na Panathinaikos walitoka suluhu 1-1 na bila shaka Wagiriki hao Panathinaikos watafurahia matokeo hayo kwa kuwa wamefunga goli ugenini na hilo ni muhimu sana watakaporudiana baada ya wiki mbili huko Ugiriki kwani goli la ugenini huhesabiwa mawili endapo mechi itaisha suluhu.

Timu hizi zitarudiana tarehe 10 Machi 2009 wakati Liverpool atakuwa kwake Anfield kucheza na Real Madrid na Chelsea atasafiri hadi Italia kurudiana na Juventus.

FA CUP: Middlesbrough 2 West Ham 0

Middlesbrough imefanikiwa kusonga mbele Kombe la FA pale walipowafunga West Ham ba0 2-0 katika mechi ya marudiano na sasa wataivaa Everton kwenye Robo Fainali.
Timu hizi zilitoka sare 1-1 na ilibidi zirudiane kupata mshindi.
Mabao ya Middlesbrough, ambayo ilikuwa haijashinda mechi 5 za nyuma katika mechi zote ilizocheza, yalifungwa na Stewart Downing kwa frikiki murua na Tuncay Sanli.

MECHI ZA FA CUP ZIJAZO:

Raundi ya 5:
26 Februari 2009 Hull City v Sheffield United [marudiano]
8 Machi 2009 Arsena v Burnley
Robo Finali:
7 Machi 2009
Coventry v Chelsea
Fulham v Manchester United
8 Machi 2009
Everton v Middlesbrough
[Tarehe itajulishwa]
Arsenal au Burnley v Hull City au Sheffield United

Majambazi yavamia nyumbani kwa Mchezaji wa Man U na kupora!!

Wakati Darren Fletcher [pichani akiwa na Rio Ferdinand] akiwa Milan, Italia na Timu yake Manchester United ilipoenda kupambana na Inter Milan huku nyuma siku ya Jumatatu jioni nyumba yake iliyoko mji wa Manchester kitongoji cha Bowdon ilivamiwa na majambazi waliovunja mlango wa mbele na kumtishia Mchumba wake pamoja na Mama Mzazi wa huyo Mchumba kwa visu na kuwapora vito vya thamani.
Inaaminika Majambazi watatu walishiriki tukio hilo.
Hili ni tukio la kwanza kumhusisha Mchezaji wa Man U ingawa huko Liverpool yameshawakuta Wachezaji kadhaa wa Liverpool kwa familia zao kuvamiwa wakati wao wanapokuwa nje ya nchi kwa mechi za kimataifa.

Wednesday, 25 February 2009

Wenger astushwa Timu yake kuanza kipindi cha pili ikiwa na Wachezaji 9 tu uwanjani!!!
Mourinho amkacha Ferguson baada ya mechi!!!

Leo, Liverpool ugenini, Chelsea nyumbani!!!

Vioja kwenye mechi za jana vilivyoacha gumzo kubwa kwa Wadau wa Soka ni pale Arsenal waliokuwa nyumbani Emirates wakicheza na AS Roma kukianza kipindi cha pili cha mchezo wakiwa na Wachezaji 9 tu ndani ya uwanja baada ya Mabeki Kolo Toure na William Gallas kuchelewa kuingia uwanjani wakati mechi inaanza kipindi cha pili.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, alihojiwa juu ya tukio hilo la ajabu alilielezea hivi: 'Ni kosa letu. Kengele inapolia lazima muwe tayari kutoka nje ya vyumba vya kubadilishia nguo. Tatizo lilikuja pale ile desturi na imani ya Kolo Toure ya kila siku kuwa wa mwisho kutoka chumbani na wa mwisho kuingia uwanjani! Kolo Toure ilibidi amsubiri Gallas aliekuwa anapatiwa matibabu na hilo lilimchelewesha Gallas kuvaa buti zake na kufunga vizuri gadi za ugoko. Toure ilibidi amsubiri Gallas atangulie ili yeye awe wa mwisho! Hawakujua kama mechi ilishaanza!'
Walipoibuka uwanjani wakakuta mechi ishaanza na Kolo Toure kwa pupa akaingia ndani bila ruhusa ya Refa na ikabidi Refa amtwange Kadi ya Njano.

Na huko San Siro, mara baada ya mechi kati Inter Milan na Manchester United kumalizika, Meneja wa Inter Milan hakuonekana kwenda kupeana mkono na mwenzake Sir Alex Ferguson kama ilivyo desturi mechi ikiisha.
Alipohojiwa, Mourinho alijitetea: 'Benchi letu la akiba lilipo tuna mlango maalum ambao hunipeleka moja kwa moja vyumba vya kubadilishia nguo! Sikumkimbia Ferguson na sisi ni marafiki! Mbona nimempelekea hotelini kwake chupa ya mvinyo wa Dola 300?'

Leo usiku ni zamu ya Liverpool na Chelsea kuingia vitani kupambana kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE huku Liverpool wakiwa wageni wa Real Madrid ndani ya Uwanja wa Santiago Bernabeu na Chelsea akimkaribisha aliekuwa Meneja wa zamani wa Chelsea Claudio Ranieri akiongoza Timu yake Juventus ya Italy.

Mechi zingine za leo ni kati ya Sporting Lisbon ya Ureno na Bayern Munich ya Ujerumani na Villareal ya Spain na Panathinaikos ya Ugiriki.
FA CUP: Matokeo mechi za jana
Coventry 1 Blackburn o
Fulham 2 Swansea 1
Timu ya daraja la chini Coventry jana iliibwaga Blackburn iliyopo LIGI KUU na sasa watapambana na Chelsea kwenye Raundi inayofuata ya Kombe la FA mechi itakayochezwa tarehe 7 Machi.
Nao Fulham waliwabwaga Swansea na sasa watakutana na Manchester United hapo tarehe 7 Machi.
Arsenal washinda nyumbani, Man U droo ugenini!

Arsenal wakicheza nyumbani Emirates waliwafunga AS Roma bao 1-0 bao la penalti lililofungwa na Robin van Persie baada ya Philippe Mexes kumchezea rafu van Persie.

Nao Manchester United wakiwa ugenini ndani ya San Siro walitoka suluhu ya 0-0 na wenyeji Inter Milan.

Mechi zitarudiwa tarehe 11 Machi wakati Arsenal atakapokuwa ugenini na Man U atakuwa kwake Old Trafford.

MATOKEO MECHI NYINGINE:
Atletico Madrid 2 FC Porto 2
Lyon 1 Barcelona 1

MECHI ZA Jumatano Februari 25:
Chelsea v Juventus
Real Madrid v Liverpool
Sporting Lisbon v Bayern Munich
Villaral v Panathinaikos

Tuesday, 24 February 2009

Arsenal v AS Roma na Inter Milan v Manchester United
Wenger alia Arshavin kutocheza, Ferguson asema goli ni muhimu leo na Mourinho adai mshindi atajulikana Old Trafford na si leo!!

Beckham alikuwa na Man U mazoezini San Siro ili kuwapa moyo!!

Leo usiku Arsenal wanajimwaga uwanjani kwao Emirates kupambana na AS Roma ya Italia huku Meneja wao Arsene Wenger akishangazwa na sheria za UEFA zinazomzuia Mchezaji wake mpya Andrei Arshavin kucheza leo kwa vile hapo awali alicheza mashindano haya akiwa na Zenit St Petersburg ambayo kwa sasa haipo tena mashindanoni baada kutolewa nje kwenye Makundi.
Wenger, ambayo Timu yake ina ubutu kufuatia kuumia kwa Washambuliaji kadhaa akiwemo Nyota Adebayor, alilalama: 'Sheria zinashangaza lakini tulipomnunua tulijua hilo!
Nae Mchezaji wa Brazil aliewahi kuchezea Arsenal kwa mkopo akitokea Real Madrid ambae kwa sasa yuko AS Roma, Julio Baptista ametamba wao ndio wanaostahili kushinda leo.
Baptista alikaririwa akisema: 'Sie ndio tunategemewa kushinda! Arsenal wana upungufu mkubwa kwa kuwakosa Fabregas, Adebayor, Eduardo, Walcot na hata Rosicky! Tunajua Arsenal ni hatari bila ya hata hao Wachezaji lakini ukweli kuwakosa hao ni pigo kubwa kwao!'
Huko Milan, Italia, vita ya kisaikolojia iliyojulikana sana wakati Mourinho akiwa na Chelsea, iliendelea tena kati ya Mourinho safari hii akiwa na Inter Milan ambao leo wanakutana na Manchester United uwanjani San Siro huku Mourinho akidokeza mechi ya leo itakuwa suluhu kwa vile Manchester United watajihami ili washinde marudiano yatayochezwa Old Trafford wiki mbili zijazo.
Hata hiyo mechi ya marudiano, Mourinho amedokeza huenda ikaamuliwa katika muda wa nyongeza!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ambayo Timu yake inakabiliwa na uhaba wa Walinzi baada ya Nemanja Vidic kufungiwa mechi hii na kina Wes Brown, Neville, O'Shea na Evans kuwa majeruhi, amekataa maoni ya Morinho na kusisitiza wao wanaingia uwanjani kushinda na kwamba bao la ugenini ni muhimu sana kwao.
Ferguson amesema: 'Man U siku zote hushambulia! Siku zote tunatafuta ushindi!'
Man U leo asubuhi walifanya mazoezi San Siro na David Beckham aliechezea Man U tangu akiwa mtoto na kwa sasa yupo Milan akiwa Timu ya AC Milan wapinzani wakubwa wa Inter Milan, alikuwepo mazoezini kuwapa moyo marafiki zake na aliongea na Wachezaji na Sir Alex Ferguson.
Baada ya mazoezi hayo ya Man U, Beckham alienda Hotelini walikofikia Man U kwa maongezi zaidi.

LIGI KUU England: Hull City 1 Tottenham Hotspurs 2

Beki Jonathan Woodgate alifunga bao kwa kichwa dakika ya 86 na kuipa Tottenham ushindi muhimu ulioifanya kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa pointi 5 juu ya timu zilizo kwenye nafasi ya timu zinazo poromoka daraja.
Tottenham walipata bao la awali kupitia Winga Aaron Lennon aliefunga kwa shuti la mita 20 dakika ya 17 lakini Hull City wakiwa kwao KC Stadium walisawazisha dakika ya 27 kupitia Turner.

Monday, 23 February 2009

NI Wakati mwingine tena wa UHONDO wa MABINGWA ULAYA!!!

Baada ya miezi miwili ya 'mapumziko' LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA', yaani UEFA CHAMPIONS LEAGUE, inarudi tena dimbani na safari hii zipo jumla ya Timu 16 zikicheza mechi za mtoano, nyumbani na ugenini, kupata Timu 8 zitakazoingia Robo Fainali.

Mechi za kwanza zitachezwa kesho Jumanne na nyingine kesho kutwa Jumatano na marudiano ni wiki mbili baadae.
Ifuatayo ni tathmini na utabiri Timu ipi itaibuka kidedea baada ya mechi mbili:

MANCHESTER UNITED v INTER MILAN
Ni mechi ya kutoa ute kwa mashabiki na hata wale wasiokuwa na upande.
Ni mechi inayokutanisha Mabingwa Watetezi wa Kombe hili na moja ya Timu Bora Italia ingawa haijawahi kushinda Kombe hili tangu mwaka 1965.
Ni mechi ngumu inayowakutanisha tena Sir Alex Ferguson na Jose Mourinho wakikumbushana 'vita vyao' vya tangu Mourinho akiwa FC Porto hadi Chelsea.
Inter Milan ingawa ni Timu ya Italia ina Wachezaji wawili tu toka Italia na imesheheni Wachezaji wa nje hasa Marekani ya Kusini na nguzo yao kubwa ni Washambuliaji wao wenye nguvu Zlatan Ibrahimovic na Adriano huku Man U wakitegemea ufundi, wepesi na ushirikiano wa kina Rooney, Ronaldo, Berbatov, Carrick na kikosi chao kizima.
UTABIRI: MAN U

AS ROMA v ARSENAL
Ni mechi ya Timu zinazocheza 'Soka Tamu' Ulaya ingawa Timu hizi kwenye ligi zao zipo chini ya kiwango na zimo hatarini kushindwa kuingia LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA msimu ujao kutokana na kuwa nafasi za chini kwenye ligi za nchini kwao.
Arsenal wanakabiliwa na majeruhi kwa Mastaa wao kama Fabregas, Adebayor na Eduardo na hivyo wana ubutu. Mchezaji mpya Andrei Arshavin haruhusiwi kucheza kwa vile aliichezea Timu yake ya zamani Zenit St Petersburg awali kwenye Kombe hili.
Nguzo ya AS Roma ni, bila shaka, Francesco Totti na kwa sababu mechi ya kwanza inachezwa uwanja wa AS Roma Olympic Stadium, Totti atawika na hili ni tatizo kubwa kwa Arsenal.
UTABIRI: AS ROMA

FC BARCELONA v LYON
Kwa sasa, wachezesha kamari wote wa Ulaya wanawapa Barcelona nafasi ya kwanza kutwaa Ubingwa huu huku Mabingwa Watetezi Manchester United wakipewa nafasi ya pili.
Hilo ndio tatizo kubwa kwa Lyon ingawa wanae Mchezaji nyota na kipaji kikubwa Karim Benzema.
UTABIRI: BARCELONA

FC PORTO v ATLETICO MADRID
Kimaandishi Atletico Madrid wangestahili kushinda mpambano huu lakini Atletico Madrid wana migogoro na walimtimua Meneja wao huku Mastaa wao Diego Forlan na Sergio Aguero viwango vyao vimeshuka mno.
FC Porto nyumbani kwao Ureno ni wababe na hawajafungwa hata mechi moja tangu Novemba mwaka jana.
UTABIRI: FC PORTO

LIVERPOOL v REAL MADRID
Hili, kama lile la MAN U v INTER MILAN, ni pambano linalotoa udenda kwa mashabiki na vyombo vya habari.
Hili ni pambano ambalo unahitaji 'Mtabiri wa Kulipwa' ili utabiri nani atashinda!
Real wanaongozwa na Meneja Mhispania Juande Ramos aliefukuzwa kazi hivi karibuni huko England alipokuwa na Tottenham.
Liverpool inaongozwa na Meneja Mhispania Rafael Benitez.
Hii ni vita ya Spain!
UTABIRI: REAL MADRID

JUVENTUS v CHELSEA
Baada ya MAN U v INTER MILAN, hii ni mechi ya pili baina ya ENGLAND v ITALY!
Wakati Juventus ikiendeleza mapambano yake bila ya sokomoko lolote chini ya Meneja Claudio Ranieri aliekuwa Meneja wa kwanza wa Chelsea kutimuliwa na Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovic mwaka 2004, Chelsea wanaingia vitani ikiwa ni mechi ya pili tu tangu Meneja mpya Guus Hiddink apewe wadhifa baada ya kufukuzwa Mbrazil Luiz Felipe Scolari.
Kuyumba kwa Chelsea kunaipa matumaini Juve ya Mchezaji Mkongwe Alessandro Del Piero.
UTABIRI: JUVENTUS

BAYERN MUNICH v SPORTING LISBON
Ndiyo ni mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE lakini kwa vyovyote vile haiwezi kushika bango kubwa Ulaya kote na duniani kote!
Wengi wanaamini mbali ya Bayern Munich kumkosa Mshambuliaji wao mkuu Luca Toni alieumia, waliobaki kina Miroslav Klose, Franck Ribery na Lucas Podolski ni bunduki tosha kwa Meneja wao Jurgen Klinsman kushangilia ushindi!
UTABIRI: BAYERN MUNICH

PANATHINAIKOS v VILLAREAL
Hizi ni Timu mbili zisizo na ubavu kuwa Mabingwa wa Ulaya lakini ondoa shaka zina uwezo wa kumtetemesha hata huyo atakaechukua Ubingwa kwani ni Timu ngumu kufungika.
Villareal waliweza kuwasimamisha Mabingwa Watetezi Man U kwenye mechi mbili za Makundi awali kwenye Kombe hili na kutoka sare ya bila kufungana.
Nao Panathinaikos, kwenye Makundi, waliwabamiza Inter Milan iliyokuwa kwake San Siro na kumaliza wakiwa juu yao kwenye msimamo wa Makundi.
Lakini Villareal wakiwa na Mkongwe wa Arsenal Robert Pires na Chipukizi alietokea Man U Giussepe Rossi wana uwezo wa kuwabwaga hao Wagiriki.
UTABIRI: VILLAREAL
INTER MILAN v MAN U: Ronaldo: 'Ni kuua au kuuawa!!!'
-Nae Beckham ashabikia Man U: 'Watashinda! Ntaenda uwanjani kuongea na timu!'


Mchezaji Bora Duniani, Cristiano Ronaldo, anaamini timu yake Manchester United ni bora na ina uzoefu mkubwa kupita wapinzani wao wa kesho kwenye pambano la mtoano la UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Inter Milan ya Italia, litakalochezwa huko Milan, Italia.
'Litakuwa pambano gumu kwani wao wanaongoza ligi ya kwao SERIE A lakini sisi ni bora na tuna uzoefu mkubwa,' Ronaldo alisema. 'Sisi ni Mabingwa watetezi na tuna Wachezaji wazuri sana! Sasa tupo hatua ya kuua au kuuawa!'
Nae Mchezaji wa zamani wa Man U ambae kwa sasa yuko AC Milan ya Italia ambao ni wapinzani wa jadi wa Inter Milan, David Beckham, ambae alicheza mechi kati ya wapinzani hao wiki mbili zilizopita mechi ambayo Inter iliifunga AC Milan 2-1, amesema: 'Inter wana Wachezaji wazuri wenye nguvu na kasi na hasa Fowadi yao ni hatari na inamudu vyema kumiliki mpira. Ukiidhibiti Fowadi hiyo basi una nafasi! Man U kwa sasa wana timu nzuri, Defensi yao ni ngome kubwa na Fowadi yao hatari sana!'
Beckham aliongeza: 'Kama mpenzi wa Man U, nipo upande wao na kama Mchezaji wa AC Milan, nipo upande wa Man U! Nitaenda kwenye mechi na nitaongea na Wachezaji wa Man U na Sir Alex Ferguson.'
Beckham alimalizia: 'Man U wanastahili kushinda lakini pengine ninawapendelea kwani mie ni shabiki mkubwa na naipenda!'
Inter Milan kwa sasa inaongozwa na Meneja Jose Mourinho ambae alikuwa Chelsea na kuwepo kwake kunaleta kumbukumbu ya mapambano akiwa Chelsea na misuguano yake na Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson. Akiwa Chelsea aliiwezesha timu hiyo kuwa Mabingwa wa LIGI KUU mara mbili mfululizo.
Inter Milan ina Wachezaji mahiri na maarufu kama kina Toldo, Cordoba, Zanetti, Maicon, Marco Materazzi, Chivu, Luis Figo, Patrick Viera, Cambiasso, Sulley Muntari, Alesandro Mancini, Zlatan Ibrahimovic, Adriano.
Kikosi cha Man U kilichosafiri leo kwenda Italia ni: Van der Sar, Kuszczak, Ferdinand, Evra, O'Shea, Evans, Fabio, Eckersley, Giggs, Park, Carrick, Nani, Scholes, Possebon, Gibson, Fletcher, Ronaldo, Rooney, Bebatov, Tevez, Welbeck

LIGI KUU England: Baada ya Man City kuwavuta jezi, Benitez bado aota Ubingwa lakini Mark Hughes wa Man City awapa ukweli!!

Meneja wa Liverpool, Rafael Benitez, baada ya jana timu yake kutoka droo 1-1 na Man City na hivyo kubaki nyuma ya Manchester United kwa pointi 7 huku zimebaki mechi 12, bado hajakata tamaa na anaamini wanaweza kutwaa ubingwa wakishinda mechi zao zote zilizobaki ikiwemo ile watakayokwenda Old Trafford nyumbani kwa Man U kupambana na Mabingwa hao tarehe 14 Machi 2009.
'Si rahisi' Benitez alikiri na kuongeza. 'Kitu muhimu tushinde mechi zetu pamoja na ile ya Old Trafford!'
Lakini Meneja wa Man City Mark Hughes ambae aliwahi kuwa Straika hatari wa Man U, mbali ya timu yake jana kuipunguza kasi Liverpool kwa droo ya 1-1, pia amewakatisha tamaa kwa kutamka: 'Si kitu rahisi Liverpool kuwa Bingwa! Inabidi Man U ateleze na hicho si kitu rahisi! Inabidi wapoteze mechi 3 na Liverpool ashinde zote!'

Sunday, 22 February 2009

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Yarudi tena kilingeni, Jumanne na Jumatano Viwanja Ulaya kuwaka moto!!!

Mashindano ya kugombea Klabu Bingwa Ulaya yanarudi tena uwanjani kuanzia Jumanne ikiwa sasa ni hatua ya Mtoano kati ya Timu 16 zilizobaki ambazo zitacheza nyumbani na ugenini.
Mabingwa Watetezi Manchester United watakuwa wageni wa Inter Milan huko Italia, Timu inayoongozwa na aliekuwa Meneja wa Chelsea Jose Mourinho.
Timu nyingine za LIGI KUU England zilizokuwemo kwenye hatua hii ya mtoano ni Chelsea, Liverpool na Arsenal.
Arsenal watakuwa kwao Emirates kuwakaribisha AS Roma ya Italia, Chelsea yuko nyumbani Stamford Bridge kumkaribisha Juventus ya Italia na Liverpool watakuwa huko Spain Uwanja wa Bernabeau nyumbani kwa Real Madrid.
RATIBA KAMILI:
Jumanne, Februari 24
Arsenal v AS Roma

Atletico Madrid v FC Porto

Inter Milan v Man U

Lyon v Barcelona

Jumatano, Februari 25
Chelsea v Juventus

Real Madrid v Liverpool

Sporting v Bayern Munich

Villareal v Panathinaikos
Liverpool chupuchupu, waambulia sare!!! Sasa wako nyuma ya Man U kwa pointi 7!!!!

Liverpool wakiwa ngomeni kwao Anfield walipigana kufa na kupona kujinusuru wasifungwe na Manchester City timu ambayo haijawahi kushinda ugenini tangu Agosti mwaka jana baada ya Craig Bellamy kuifungia Man City bao dakika ya 4 kipindi cha pili.
Liverpool wakijitutumua walisawazisha kupitia Dirk Kuyt dakika ya 78.
Matokeo hayo yanawafanya Liverpool wawe na pointi 55 wakiwa pointi 7 nyuma ya Manchester United wenye pointi 62.

Fulham 2 West Bromwich Albion 0

Mabao ya Bobby Zamora na Andy Jonhson yamewapa ushindi wa 2-0 Fulham dhidi ya timu ya mwisho kwenye LIGU KUU West Bromwich Albion.
Man U 2 Blackburn 1: Man U wako pointi 8 mbele, Liverpool wacheza leo!!!

Jana Manchester United wakiwa nyumbani Old Trafford waliifunga Blackburn, timu ambayo siku zote huwawekea ngumu, mabao 2-1 kwa mabao ya Wayne Rooney na Cristiano Ronaldo.
Bao la Blackburn, ambalo ni la kwanza Man U wanafungwa kwenye LIGI KUU tangu Sami Nasri wa Arsenal atoboe nyavu zao Novemba 8 mwaka jana, lilifungwa na Mshambuliaji wao hatari Roque Santa Cruz.
Refa Howard Webb aliiacha mechi hii ikiwa na malumbano baada ya kulikataa bao la wazi la Man U lililofungwa na Johnny Evans kwa kichwa kufuatia kona na 'kuwanyima' penalti Blackburn pale ilipodaiwa Pedersen alivutwa na Rafael.
Hata hivyo Man U wangeweza kutoka na ushindi mnono endapo nafasi za wazi zilizotua kwa Ronaldo, Rooney na Berbatov zingetumiwa vilivyo.
Leo Liverpool wanajimwaga uwanjani kwao Anfield kupambana na mahasimu wakubwa wa Man U, Manchester City, wakipigania kupunguza pengo lilopo la pointi 8 kati yao na Man U.
Liverpool wataingia uwanjani bila ya tegemezi Steven Gerrard ambae ni majeruhi na Xabi Alonso aliefungiwa mechi hii.
MECHI NYINGINE ZA LEO NI:
Fulham v West Ham
Newcastle v Everton
Powered By Blogger