Thursday 26 February 2009

Liverpool waidonyoa Real kwao, Chelsea wapiga kimoja nyumbani, Bayern aua ugenini na Villareal, Panathinaikos ngoma droo!!!!

Jana UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliendelea kunguruma Ulaya huku Timu za England zikipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na karamu ya magoli iliwaangukia Bayern Munich pale walipoiangushia kipigo kikali Sporting Lisbon cha mabao 5-0 kulekule kwao Ureno.

Chelsea wakiwa ngomeni kwao Stamford Bridge waliwafunga Juventus bao 1-0 kwa bao lililofungwa na Didier Drogba dakika ya 13 ya mchezo.

Liverpool, wakicheza ugenini Uwanja wa Santiago Bernabeu na wenyeji Real Madrid, walicheza mchezo wa kujihami lakini wakaondoka na ushindi wa bao 1-0 pale Yossi Benayoun alipopachika kwa kichwa dakika ya 82.

Villareal na Panathinaikos walitoka suluhu 1-1 na bila shaka Wagiriki hao Panathinaikos watafurahia matokeo hayo kwa kuwa wamefunga goli ugenini na hilo ni muhimu sana watakaporudiana baada ya wiki mbili huko Ugiriki kwani goli la ugenini huhesabiwa mawili endapo mechi itaisha suluhu.

Timu hizi zitarudiana tarehe 10 Machi 2009 wakati Liverpool atakuwa kwake Anfield kucheza na Real Madrid na Chelsea atasafiri hadi Italia kurudiana na Juventus.

FA CUP: Middlesbrough 2 West Ham 0

Middlesbrough imefanikiwa kusonga mbele Kombe la FA pale walipowafunga West Ham ba0 2-0 katika mechi ya marudiano na sasa wataivaa Everton kwenye Robo Fainali.
Timu hizi zilitoka sare 1-1 na ilibidi zirudiane kupata mshindi.
Mabao ya Middlesbrough, ambayo ilikuwa haijashinda mechi 5 za nyuma katika mechi zote ilizocheza, yalifungwa na Stewart Downing kwa frikiki murua na Tuncay Sanli.

MECHI ZA FA CUP ZIJAZO:

Raundi ya 5:
26 Februari 2009 Hull City v Sheffield United [marudiano]
8 Machi 2009 Arsena v Burnley
Robo Finali:
7 Machi 2009
Coventry v Chelsea
Fulham v Manchester United
8 Machi 2009
Everton v Middlesbrough
[Tarehe itajulishwa]
Arsenal au Burnley v Hull City au Sheffield United

Majambazi yavamia nyumbani kwa Mchezaji wa Man U na kupora!!

Wakati Darren Fletcher [pichani akiwa na Rio Ferdinand] akiwa Milan, Italia na Timu yake Manchester United ilipoenda kupambana na Inter Milan huku nyuma siku ya Jumatatu jioni nyumba yake iliyoko mji wa Manchester kitongoji cha Bowdon ilivamiwa na majambazi waliovunja mlango wa mbele na kumtishia Mchumba wake pamoja na Mama Mzazi wa huyo Mchumba kwa visu na kuwapora vito vya thamani.
Inaaminika Majambazi watatu walishiriki tukio hilo.
Hili ni tukio la kwanza kumhusisha Mchezaji wa Man U ingawa huko Liverpool yameshawakuta Wachezaji kadhaa wa Liverpool kwa familia zao kuvamiwa wakati wao wanapokuwa nje ya nchi kwa mechi za kimataifa.

No comments:

Powered By Blogger