Saturday 7 February 2009

Liverpool wachukua uongozi 'kwa muda', Villa wa tatu, Chelsea adoda!!!

Liverpool sasa anaongoza LIGI KUU England, pengine mpaka kesho tu, baada ya kupata ushindi wa ajabu kwa kupata mabao ya kushangaza walipocheza na timu inayodidimia Portsmouth.
Liverpool walipata bao la tatu dakika za mwisho likifungwa na Nyota Fernando Torres aliengizwa mwishoni na kuwapa ushindi wa 3-2.
Portsmouth walikuwa wakiongoza kwa bao 2-1 hadi dakika 5 zikisalia lakini Kuyt akasawazisha na Torres akawaua Portsmouth dakika za majeruhi.
Liverpool yuko kinarani akiwa na pointi 54 kwa mechi 25, wa pili ni Man U pointi 53, mechi 23 huku Chelsea aliebanwa leo na Hull City kwa kutoka sare ya 0-0, akiporomoka hadi nafasi ya 4.
Aston Villa kwa kuifunga leo Blackburn 2-0 wamepanda hadi nafasi ya 3 wakiwa na pointi 51 kwa mechi 25.
Chelsea ana pointi 49, mechi 25.
Arsenal wapo nafasi ya 5 na wana pointi 43 na wanacheza kesho ugenini na jirani na mahasimu wao, watoto wa jiji moja London, tena London ya Kaskazini, Tottenham ambao watakuwa kwao White Hart Lane.
Timu hizi kwenye mzunguko wa kwanza wa LIGI KUU walitoka 4-4.
Mabingwa Man U watakuwa Upton Park nyumbani kwa West Ham na wakitoka sare tu watachukua tena uongozi wa ligi huku wakiwa na mechi moja mkononi.

MATOKEO YA MECHI ZOTE:

Blackburn 0-2 Aston Villa
Chelsea 0-0 Hull
Everton 3-0 Bolton
Man City 1-0 Middlesbrough
Portsmouth 2-3 Liverpool
Sunderland 2-0 Stoke
West Brom 2-3 Newcastle
Wigan 0-0 Fulham
MECHI ZA LIGI KUU:

Jumamosi, 7 Februari 2009

Man City v Middlesbrough [saa 9 dak 45 mchana]
[saa 12 jioni]
Blackburn v Aston Villa
Chelsea v Hull
Everton v Bolton
Portsmouth v Liverpool
Sunderland v Stoke
West Brom v Newcastle
Wigan v Fulham

Jumapili, 8 Februari 2009

[saa 10 na nusu jioni]
Tottenham v Arsenal

[saa 1 usiku]
West Ham v Man U

Endapo leo Liverpool, anaesafiri kwenda Portsmouth, atawafunga wenyeji wao hao ambao wako nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi ikiwa ni pointi moja tu juu ya timu zilizo nafasi ya kushuka daraja, basi atachukua uongozi wa LIGI KUU kwa kumpita Manchester United ambae mechi yake inachezwa kesho.
Hata hivyo, Liverpool atakuwa amecheza mechi 2 zaidi ya Man U.
Ushindi kwa Liverpool ni muhimu hasa kufuatia kipigo cha Jumatano walichopewa na mahasimu wao wakubwa Everton kwa bao 1-0 na kuwatoa nje ya Kombe la FA.
Katika mechi hiyo Liverpool walipata pigo kubwa baada ya Nahodha wao Steven Gerrard kuumia na sasa atakuwa nje ya kwa wiki 3.
Wengi wanajua bila ya Gerrard Liverpool inapwaya mno na ndio maana macho ya wengi yapo kwenye mechi hii.
Kwa upande mwingine, Portsmouth wakiwa chini ya Meneja Tony Adams, Nahodha wa zamani wa Arsenal, wako taabani wakiwa wamepata pointi moja katika mechi 7 za LIGI KUU zilizopita na hii ni presha kubwa kwa Tony Adams kutimuliwa.
Leo, Timu iliyo nafasi ya 3, nyuma ya Liverpool, Chelsea, inawakaribisha Hull City na ikiwa watashinda na Liverpool kufungwa mechi yake ya leo, basi watafungana kwa pointi na Chelsea atakuwa juu ya Liverpool kwa ubora wa tofauti ya magoli.

Ferguson na Vidic watwaa Tuzo ya Barclays kwa Januari!!!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, na Beki wake, Nemanja Vidic, wamepewa Tuzo za Barclays za Meneja na Mchezaji bora wa Januari kwa kila mmoja na hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Vidic kutunukiwa tuzo hiyo lakini ni mara ya 22 kwa Sir Alex Ferguson kushinda.
Barclays ndio wadhamini wakuu wa LIGI KUU England na wamewazadia Manchester United kwa kushinda mechi zao zote 5 za LIGI KUU kwa mwezi Januari bila ya kufungwa hata goli moja.
Man U walianza Januari kwa kuziwasha Chelsea 3-0 na West Brom 5-0 na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wigan, Bolton na Everton.
Kwa sasa Man U ndie kinara wa ligi.

Materazzi ashinda kesi, alipwa Mamilioni ya Pauni kama Fidia!!!

Marco Materazzi, Mtaliani aliejizolea umaarufu wa kuchukiwa, hasa baada ya Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006 kati ya Italy na France pale 'alipokula ndosi' na kusababisha kipenzi Zinedine Zidane 'aone Nyekundu', ameshinda kesi yake Mahakama Kuu England na sasa Gazeti la SUN itabidi limlipe fidia ambayo inaaminika ni Mamilioni ya Pauni.
Gazeti hilo inasemekana lilidai Materazzi alimwambia Zidane ni 'mtoto wa malaya wa haramia' na ndio maana Zidane, ambae asili yake ni Mwarabu wa Algeria, alikasirika na kumtwanga kichwa ambacho Refa hakuona ila tukio hilo lilionwa na Refa wa Akiba aliembonyeza mwenzake na kumpa Kadi Nyekundu.
Mechi hiyo ya Fainali Kombe la Dunia iliisha 1-1 lakini Italia waliibuka Mabingwa baada ya kushinda kwa tombola ya penalti.
Hii ni kesi ya 3 kwa Materazzi kuyashinda Magazeti ya England, mengine yakiwa Daily Star na Daily Mail, yote yakimlipa fidia kuhusu ishu ya Zidane.

N'Zogbia na Kinnear waendelea kuchambana magazetini!!!

Bosi wa Newcastle, Joe Kinnear na aliekuwa Mchezaji wake, Charles N'Zogbia, ambae sasa amehamia Wigan, wameendelea kuwakiana magazetini huku kila mmoja akimkandya mwenzake.
Vita hii iliianza kama wiki moja sasa na ndio ilisababisha N'Zogbia kudai ahamishwe na hatimaye kuhamia Wigan siku chache zilizopita.
Chanzo kilikuwa pale Joe Kinnear akiwa kwenye mahojiano na Waandishi wa Habari kurekodiwa akimwita Charles N'Zogbia 'Charles Insomnia', Imsomnia likiwa neno la Kiingereza lenye maana kukosa usingizi, kitu ambacho kilimkasirisha sana N'Zogbia ingawa Kinnear alijitetea alikosea tu kutamka jina hilo na hakuwa na nia ya dhihaka.
N'Zogbia, baada ya kuhama, ameibuka na kudai: 'Kinnear hana uwezo wa kuongoza Klabu. Ukimsikia Meneja akisema vitu vile ujue hakuheshimu na kama hana heshima kuna faida gani kucheza timu yake? Sikuwa na furaha kuchezea Newcastle, Meneja alikuwa haongei na mimi!!!'
Nae Kinnear amejibu: 'Maneno yake ni vichekesho!! Yeye alitaka kuhama tu na kila siku ananifuata mara Arsenal, mara Man U, mara Real wanamtaka na sasa kaishia Wigan!! Alikuwa kwenye dunia ya Abunuwasi!!'

Friday 6 February 2009

Mchezaji mwingine wa Man City mbaroni!!!

Baada ya Robinho kujikuta mikononi mwa Polisi na huku uchunguzi wa kesi yake ya 'shambulio la ngono' ukiendelea, Mchezaji mwingine wa Manchester City amejikuta mikononi mwa Polisi wa Manchester baada kutokea ugomvi nje ya Naiti Klabu siku ya Mkesha wa Krismas.
Mchezaji huyo ni Mlinzi Micah Richards [20] ambae alihojiwa na Polisi na kuachiwa kwa dhamana mpaka tarehe 8 Aprili 2009 huku uchunguzi ukiendelea.


Steven Gerrard nje wiki 6!!!

Nahodha na 'Mbeba Timu' wa Liverpool, Steven Gerrard, atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 3 baada ya uchunguzi kuthibitisha amechanika musuli mguuni.
Gerrard aliumia na kutolewa kwenye dakika ya 16 tu ya mechi kuwania Kombe la FA ambayo Liverpool alifungwa 1-0 na mahasimu wao wakubwa Everton.
Gerrard atazikosa mechi za Liverpool dhidi ya Portsmouth, Man City na hata ile ya UEFA Champions League na Real Madrid hapo Februari 25. Pia ataikosa mechi ya kirafiki ya England watakapocheza na Spain wiki ijayo.

Thursday 5 February 2009

FA CUP: Everton waibwaga Liverpool!!!

Everton wakiwa nyumbani kwao Goodison Park waliwatoa nje ya Kombe la FA Watani wao wa Jadi Liverpool kwa bao 1-0 bao alilofunga chipukizi wa miaka 19 Dan Gosling katika dakika 120 za muda wa nyongeza baada ya mechi kwisha 0-0 katika dakika 90.
Timu hizi zilitoka suluhu ya 1-1 katika mechi iliyochezwa Anfield wiki iliyokwisha na mechi hii ni marudiano.
Dan Gosling aliingizwa kama Mchezaji wa Akiba na alipachika bao la ushindi dakika ya 118 zikiwa dakika mbili tu kabla gemu haijaenda tombola ya penalti.
Liverpool ilishusha kikosi chake kamili kilichombamiza Chelsea lakini walipata pigo kubwa dakika ya 16 tu baada ya Nahodha na 'Mbeba Timu' Steve Gerrard kuumia na kutolewa na inasadikiwa atakuwa nje kwa wiki hadi 4.
Pigo jingine kwa Liverpool ni pale Leiva Lucas alipolambwa Kadi Nyekundi kipindi cha pili baada ya kupewa Njano mbili.
Kwenye mechi yote hii Mfungaji wao stadi Fernando Torres alionekana ni abiria tu na ilibidi atolewe aingizwe Babel.
Sasa Everton wamesonga mbele na watacheza na Aston Villa Raundi ya 5 ya Kombe hili la FA.


MATOKEO MECHI NYINGINE ZA LEO ZA MARUDIANO NI:
Aston Villa 3-1 Doncaster
Blackburn 2-1 Sunderland [BAADA YA DAKIKA 120]
Nottm Forest 2-3 Derby

RATIBA YA MECHI ZA RAUNDI YA 5:

Jumamosi, 14 Februari 2009
[SAA 9:45 MCHANA]
Swansea v Fulham
[SAA 12 JIONI]
Sheffield United v Hull
Blackburn v Coventry
West Ham v Middlesbrough
[SAA 2:30 USIKU]
Watford v Chelsea
Jumapili, 15 Februari 2009
[SAA 11:30 JIONI]

Everton v Aston Villa
[SAA 1:30 USIKU]
Derby v Man U
Jumatatu, 16 Februari 2009
[SAA 4:45 USIKU]

Arsenal v Cardiff [Marudiano ya Raundi ya 4 Mshindi anacheza na Burnley kwenye Raundi ya 5]

Wednesday 4 February 2009


LIGI KUU England: Wabongo wafarijika baada ya DSTV kuokoa jahazi!!!

Tangu wikiendi iliyokwisha, baada ya kukosa kuona matangazo ya moja kwa moja, yaani laivu, ya mechi za LIGI KUU England kufuatia kufilisika kwa Kampuni iliyokuwa ikimiliki GTV waliokuwa na haki ya asilimia 80 kuonyesha mechi za LIGI KUU, Wabongo walikuwa na majonzi makubwa lakini leo wameibuka kidedea na kushangilia kufuatia taarifa rasmi kutoka DStv kuwa wamefanikiwa kupata leseni ya kuonyesha laivu mechi zote za LIGI KUU msimu huu na kazi hiyo wataianza kwa mechi zote za wikiendi hii zitakazoonyeshwa kwenye Chaneli zake za Supersport na vilevile leseni hiyo imewaruhusu kuonyesha mechi zote za msimu ujao.
Awali, DStv walipewa haki ya kuonyesha asilimia 20 tu za mechi za LIGI KUU kwa Nchi za Kusini mwa Sahara, ikiwemo Tanzania, ingawa huko Makao Makuu yao Afrika Kusini na Nigeria walipewa haki ya kuonyesha mechi zote.
Kabla ya kuibuka kwa GTV mwaka uliokwisha, DStv ndio walikuwa pekee wakionyesha mechi zote na walijenga sifa kubwa, umaarufu na uaminifu mkubwa kwa umahiri wao miongoni mwa Washabiki wa Bongo.

FIFA yatangaza Nchi zinazogombea Uenyeji wa Fainali Kombe la Dunia 2018

England, ambae ndie anapewa nafasi kubwa kunyakua Uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia 2018, atapata upinzani toka kwa Wapinzani 10 wakiwa ni Spain na Portugal, wanaoomba kwa pamoja kuwa Wenyeji kwa kushirikiana, sawa na Uholanzi na Ubelgiji ambao nao watashirikiana.
Nchi zinazoomba kila moja kivyake ni Urusi, Australia, USA, Mexico, Qatar, Indonesia, Japan na Korea.
Ingawa mwaka 2002, Japan na Korea walishirikiana kuwa Wenyeji safari hii kila nchi imeomba kivyake.
Kura ya kumchagua mwenyeji itafanywa na FIFA Desemba mwaka huu.
Mwenyeji wa Fainali zijazo za 2010 ni Afrika Kusini na zile za 2014 zitafanyika Brazil.

Shaun Wright-Phillips ashtakiwa na FA!!!

Chama cha Soka cha England, FA, kimemshtaki Mchezaji wa Manchester City Shaun Wright- Phillips kwa kuleta vurugu mbaya kwenye mechi ya Jumamosi ambayo Man City walifungwa na Stoke.
Shaun Wright-Phillips alibabatizwa na mpira kwa makusudi na Mchezaji wa Stoke Rory Delap wakati filimbi ishalia na Refa Martin Atkinson akampa Kadi Nyekundu Delap lakini hakumwona Shaun Wright-Philips akilipiza kisasi kwa kumpiga teke Delap.
Lakini baada ya mechi, alipoona video ya tukio lote, Refa Martin Atkinson akakiri endapo angeliona tukio hilo basi Shaun Wright-Phillips angepewa Kadi Nyekundu pia.
Shaun Wright-Phillips amepewa hadi kesho Alhamisi saa 3 usiku [bongo taimu] kutoa utetezi wake.

Nao Middlebrough wakiri kosa kwa FA la kushindwa kudhibiti Wachezaji wao!!!

Middlesbrough wamekubali kosa waliloshitakiwa na FA la kushindwa kudhibiti Wachezaji wao kwenye mechi waliyobamizwa 3-0 na West Brom Januari 17 kufuatia vitendo vya Wachezaji wake kumzonga Refa Mark Halsey alipomtoa nje Mchezaji wa Middlesbrough Didier Digard kwa Kadi Nyekundu alipomchezea rafu Borja Valero na kumsababisha Refa huyo adondoshe chini Kadi yake.
Mbali ya kukubali kosa, Klabu ya Middlesbrough imeomba iende mbele ya kikao kitakachotoa adhabu ili iwakilishe ombi la kupunguziwa adhabu.

Tottenham yampa Mchezaji 'mpya' Robbie Keane Unahodha!!!

Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp, amemteua Robbie Keane kuwa Nahodha wake mara tu baada ya Mchezaji huyo kununuliwa kutoka Liverpool hapo juzi.
Robbie Keane ndie aliekuwa Nahodha wa Tottenham kabla hajauzwa kwenda Liverpool miezi 6 iliyokwisha.
Harry Redknapp ametamka: 'Nahisi kurudi kwa Keane hapa kutatuletea msukumo mpya! Yeye ni mtu mwenye mvuto mkubwa na kila sifa ya ushujaa na uongozi!!'
Kwa sasa Tottenham iko kwenye patashika ya kujikwamua toka nafasi za mwisho kwenye msimamo wa ligi zinazohatarisha timu kushuka daraja.
FA CUP: BURNLEY 3 WEST BROM 1

Katika mechi ya marudiano ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA jana, timu ya daraja la chini Burnley imeiadhiri West Brom kwa kuinyuka mabao 3-1 na hivyo kuingia Raundi ya 5 na itakutana na mshindi kati ya Arsenal na Cardiff mechi iliyokuwa pia ichezwe jana lakini ikaahirishwa kwa sababu ya hali ya hewa kufuatia dhoruba ya barafu nyingi kuanguka Uingereza.
Sasa Arsenal na Cardiff watacheza Februari 16.

MECHI ZA MARUDIANO ZA FA CUP LEO 4 Februari 2009:

[Saa 4 dak 45 usiku]
Aston Villa v Doncaster
Nottingham Forest v Derby
[Saa 5 usiku]
Blackburn v Sunderland
Everton v Liverpool

Kadi Nyekundu ya Lampard yafutwa!!

Kadi Nyekundu aliyopewa Frank Lampard na Refa Mike Riley kwa kumchezea rafu Xabi Alonso wa Liverpool kwenye mechi ya Jumapili ilyopita ambayo Liverpool aliifunga Chelsea 2-0 imefutwa na FA baada ya Rufaa ya Chelsea.
Sasa Lampard yuko huru kucheza mechi zijazo.

PILIKAPILIKA ZA UHAMISHO ZILIVYOISHA!!

Baada ya dirisha la uhamisho kufungwa, chini ndio listi kamili ya biashara kamili iliyofanywa na Klabu za LIGI KUU ENGLAND.

Arsenal
Kuingia: Andrei Arshavin (Zenit St Petersburg,)
Kuhama: Gavin Hoyte (Watford mkopo); Jay Simpson (West Brom, mkopo)
Aston Villa
Kuingia:Emile Heskey (Wigan dau, £3.5m)
Kuhama: Wayne Routledge (QPR, £300,000)
Blackburn Rovers
Kuingia: Gael Givet (Marseille, mkopo); El-Hadji Diouf (Sunderland, £2m)
Kuhama:Matt Derbyshire (Olympiacos, mkopo); Robbie Fowler (huru); Eddie Norlan (Preston NE,); Sergio Peter (Sparta Prague,)
Bolton Wanderers
Kuingia: Ariza Makukula (Benfica, mkopo); Sebastien Puygrenier (Zenit St Petersburg, mkopo); Mark Davies (Wolves, )
Kuhama: Kevin Nolan (Newcastle, £4m); Ian Walker (huru); Heidar Helguson (QPR)
Chelsea
Kuingia: Ricardo Quaresma (Inter Milan, mkopo)
Kuhama: Carlo Cudicini (Tottenham, bure); Ben Sahar (De Graafschap, mkopo); Jack Cork (Wolves, mkopo); Wayne Bridge (Manchester City, £10m); Scott Sinclair (Birmingham, mkopo)
Everton
Kuingia: Jo (Manchester City mkopo)
Kuhama: Hamna
Fulham
Kuingia: Olivier Dacourt (Inter Milan, mkopo); Giles Barnes (Derby, mkopo)
Kuhama: Jimmy Bullard (Hull, £5m); Andranik Teymourian (Barnsley, mkopo); Leon Andreasen (Hannover, mkopo); Soel Ki-Hyeon (Al-Hilal, mkopo); Hameur Bouazza (Birmingham, mkopo); Lee Cook (QPR, £1.9m)
Hull City
Kuingia: Jimmy Bullard (Fulham, £5m); Kevin Kilbane (Wigan); Manucho (Manchester United, mkopo); Kamil Zayatte (Young Boys, £2.5m alikuwa akichezea kwa mkopo sasa amekuwa wa kudumu)
Kuhama: Stelios Giannakopolous (Larissa); Dean Windass (Oldham, mkopo); Marlon King (Middlesbrough)
Liverpool
Kuingia: Hamna
Kuhama: Robbie Keane (Tottenham); Jermaine Pennant (Portsmouth, mkopo)
Manchester City
Kuingia: Shay Given (Newcastle, £6m); Nigel De Jong (Hamburg, £19m); Craig Bellamy (West Ham, £14m); Wayne Bridge (Chelsea, £10m)
Kuhama: Jo (Everton, mkopo); Tal Ben Haim (Sunderland)
Manchester United
Kuingia:
Zoran Tosic na Adem Ljajic (wote Partizan Belgrade, dau halikutajwa); Ritchie de Laet (Stoke)
Kuhama: Manucho (Hull, mkopo)
Middlesbrough
Kuingia: Marlon King (Hull, mkopo)
Kuhama: Mido (Wigan, mkopo)
Newcastle United
Kuingia: Ryan Taylor (Wigan); Kevin Nolan (Bolton, £4m); Peter Lovenkrands (huru)
Kuhama: Shay Given (Man City); Charles N'Zoigbia (Wigan)
Portsmouth
Kuingia: Angelo Basinas (AEK); Theofanis Gekas (Werder Bremen); Jermaine Pennant (Liverpool, mkopo); Nadir Belhadj (Lens, alikuwa mkopo sasa wa amenunuliwa); Hayden Mullins (West Ham, bure); Pele (Porto, mkopo)
Kuhama: Jermaine Defoe (Tottenham, £15m); Lassana Diarra (Real Madrid, £20m); Ben Sahar (Chelsea, mwisho wa mkopo)
Stoke City
Kuingia: Mathew Etherington (West Ham); James Beattie (Sheffield United, £3.5m); Henri Camara (Wigan, mkopo)
Kuhama: Ritchie de Laet (Man U); Tom Soares (Charlton, mkopo), Liam Lawrence (Derby)
Sunderland
Kuingia:
Tal Ben Haim (ManCity, mkopo); Calum Davenport (West Ham, mkopo)
Kuhama: Michael Chopra (Cardiff, mkopo); El-Hadji Diouf (Blackburn, £4m); Roy O'Donovan (Blackpool, mkopo); Ross Wallace (Preston, £100k); Liam Miller (QPR); Pascal Chimbonda (Tottenham)
Tottenham Hotspur
Kuingia: Robbie Keane (Liverpool, £12m); Wilson Palacios (Wigan, £15m); Jermaine Defoe (Portsmouth, £15m); Carlo Cudicini (Chelsea, bure); Pascal Chimbonda)
Kuhama: Hossam Ghaly (Al Nasar); Paul Stalteri (huru); Kevin Price-Boateng (Borussia Dortmund, mkopo); Cesar Sanchez (Valencia, mkopo)
West Bromwich
Kuingia: Juan Carlos Menseguez (San Lorenzo); Youssouf Mulumbu (Paris St-Germain, mkopo); Pele (Porto, mkopo); Marc-Antoine Fortune (Nancy, mkopo); Jay Simpson (Arsenal, mkopo)
Kuhama: Sherjill MacDonald (Roeselare, mkopo)
West Ham
Kuingia: Savio Nsereko (Brescia, £10m)
Kuhama: Julien Faubert (Real Madrid, mkopo); Craig Bellamy (Man City, £14m); Calum Davanport (Sunderland, mkopo); Mathew Etherington (Stoke); Nigel Quashie (Wolves, mkopo); Lee Bowyer (Birmingham, mkopo); Hayden Mullins (Portsmouth, bure); Kyel Reid (Wolves, mkopo)
Wigan Athletic
Kuingia: Charles N'Zoigbia (Newcastle); Mido (Middlesbrough, mkopo); Ben Watson (Crystal Palace, £2m); Hugo Rodallega (Necaxa, £4.5m)
Kuhama: Ryan Taylor (Necwastle); Wilson Palacios (Tottenham); Kevin Kilbane (Hull),
Emile Heskey (Aston Villa, £3.5m); Marlon King (Middlesbrough, mkopo); Henri Camara (Stoke, mkopo)


Monday 2 February 2009

Robbie Keane arudi Tottenham!!!

Tottenham imemsaini tena aliekuwa Nahodha wao miezi 6 tu tangu wamuuze kwa Liverpool kwa Pauni Milioni 20.3 na safari hii dau la kuuzwa kwa Keane na Liverpool halikutajwa lakini inaaminika ni Pauni Milioni 15.
Robbie Keane akiwa hapo Liverpool alicheza mechi 19 na kufunga mabao matano.
Keane ambae alikuwa Tottenham tangu Agosti 2002 hadi Julai 2008 alicheza mechi 254 na kufunga mabao 107 hapo Tottenham.
Keane ni Mchezaji wa tatu aliewahi kuchezea Tottenham na kurudishwa tena hapo na Meneja Harry Redknapp ndani ya huu mwezi mmoja wengine wakiwa Jermaine Defoe alierudi toka Portsmouth na Pascal Chimbonda kutoka Sunderland.

Dili ya Arshavin kwenda Arsenal hatihati, N'Zogbia yuko Wigan na Dacourt arudi tena England!!

Huku muda ukiyoyoma na dirisha likikaribia kubamizwa komeo, ile vuta nikuvute kati ya Arsenal na Klabu ya Kirusi Zenit St Petersburg kuhusu uhamisho wa Andrei Arshavin inaendelea.
Taarifa zinasema huenda dili hiyo imekufa baada ya pande zote mbili kushindwa kukubaliana dau la uhamisho na nini walipwe hao Warusi kama fidia kwa Nyota Arshavin aliewika kwenye EURO 2008 kuvunja mkataba na Klabu yake Zenit.
Klabu za Wigan na Newcastle zimekubaliana kubadilishana Wachezaji huku Mlinzi Ryan Taylor [24] akienda Newcastle na Charles N'Zogbia akitoka Newcastle kwenda Wigan ingawa Wigan imebidi pia watoe Pauni Milioni 6 ili kumchukua N'Zogbia.
N'Zogbia alijiunga Newcastle kutoka Le Havre ya Ufaransa mwaka 2004 na Taylor alijiunga na Wigan mwaka 2006 kutoka Tranmere.
Nae Mchezaji wa Kimataifa wa Ufaransa, Olivier Dacourt [34], aliewahi kuchezea LIGI KUU akiwa na Everton na Leeds, ametua Fulham kwa mkopo akitokea Inter Milan.
Dirisha la Uhamisho Wachezaji halifungwi leo saa 2 usiku [saa za bongo]!!!

Uongozi wa LIGI KUU England umetangaza kuwa Vilabu vitaruhusiwa kukamilisha taratibu za uhamisho hata baada ya Dirisha la Uhamisho Wachezaji kufungwa leo saa 2 usiku saa za bongo ikiwa ni kuvisaidia Vilabu hasa baada ya Uingereza yote kukumbwa na kuanguka kwa barafu nyingi iliyoleta matatizo nchi nzima hasa kwenye usafiri ambako barabara, reli na viwanja vya ndege kufungwa [Tizama picha kushoto Polisi akiwa barabarani alivyoganda kwa barafu!!].
Uongozi wa LIGI KUU umetamka kuwa baada ya kujadiliana na FA pamoja na FIFA wameruhusiwa kuongeza muda ili Klabu zikamilishe makubaliano na Vilabu vingine pamoja na Wachezaji husika ili mradi tu Vilabu vinavyohusika kwenye uhamisho vinatuma barua pepe kwa LIGI KUU kwamba Vilabu hivyo vina makubaliano na vilevile Klabu inayomnunua Mchezaji iwaridhishe kuwa hali ya hewa ndio imechelewesha kutosainiwa Mchezaji kabla ya saa 2 usiku saa za bongo.
Wakati kuna taarifa hizo za kuongeza muda, tayari Klabu kadhaa zimekamilisha uhamisho wa Wachezaji kabla ya dirisha kufungwa kama tunavyowaletea hapa chini.

Jo ahamia Everton kwa mkopo

Klabu ya Everton imemsaini Mbrazil wa Manchester City Jo kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu huu.
Jo mwenye umri wa miaka 21 alitua Man City akitokea CSKA Moscow Julai 2008 ingawa mpaka sasa anashindwa kupata namba ya kudumu hapo Man City alikochezea mechi 18 na kufunga magoli matatu tu.
Everton kwa sasa ina uhaba mkubwa wa Washambuliaji baada ya Mastraika wao wote, wakiwemo
Ayegbeni Yakubu, Louis Saha na James Vaughan kuumia.
Jo, ambae ana urefu wa Futi 6 Inchi 3 na jina lake kamili ni Joao Alves de Assis Silva, alifunga magoli 44 katika mechi 77 alizochezea CSKA Moscow.

Portsmouth wamsaini Kiungo Basinas

Mgiriki aliekuwemo kwenye Timu ya Ugiriki iliyoshinda Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 2004 na anaechezea Klabu ya Ugiriki AEK Athens, Angelos Basinas [33] amejiunga na Portsmouth kwa mkataba wa miezi 18.
Huyo ni Mgiriki wa pili kuchukuliwa na Portsmouth kwenye Dirisha hili la Uhamisho mwingine akiwa Theofanis Gekas ambae kachukuliwa kwa mkopo kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani hadi mwishoni mwa msimu huu.

Camara yuko Stoke kwa mkopo

Mshambuliaji kutoka Senegal, Henri Camara [31], amehamia Stoke kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu akitokea Klabu yake Wigan.
Camara msimu huu amefunga goli 6 akiwa na Wigan.

Mechi ya marudiano Kombe la FA Arsenal v Cardiff hapo kesho yaahirishwa

Ile mechi ya marudiano ya Kombe la FA kati ya Arsenal v Cardiff iliyokuwa ichezwe kesho Emirates Stadium imeahirishwa kwa sababu ya hali ya hewa mbaya iliyoandamana na kuanguka barafu nyingi iliyoikumba England na hasa Jiji la London.
Ingawa kiwanja cha Emirates kinachezeka kwa kuwa kina hita chini ya ardhi zinazoyeyusha barafu mechi hii itapangwa baadae kwa hofu ya usalama wa Washabiki na vilevile wasiwasi pengine usafiri utakuwa mgumu.
Timu hizi zilitoka suluhu 0-0 zilipocheza Januari 25.
Dirisha la Uhamisho Wachezaji kufungwa leo saa 2 usiku [saa za bongo]!!!

Dirisha la Uhamisho Wachezaji litafungwa leo saa 2 usiku, saa za kibongo, ingawa kuna habari zisizothibitishwa huenda likasogezwa mbele kidogo ili kutoa nafasi zaidi kwa sababu Uingereza yote imekumbwa na hali mbaya ya hewa hasa kufuatia kuanguka barafu nyingi kulikovuruga usafiri nchi nzima.
Mara baada ya kufungwa dirisha hilo tutawaletea taarifa kamili za Wachezaji gani wamehama dakika hizi za mwisho kwani kuna taarifa nyingi kuhusu mbio za dakika za mwisho .


FA England imepokea rufaa ya Lampard wa Chelsea kupinga Kadi Nyekundu.

Chama cha Soka England, FA, kimethibitisha kupokea rufaa toka Klabu ya Chelsea inayohusu Kadi Nyekundu aliyopewa Frank Lampard na Refa Mike Riley kwenye mechi ambayo Chelsea alifungwa bao 2-0 na Liverpool uwanjani kwa Liverpool Anfiled katika mechi ya LIGI KUU hapo jana.
Ingawa Refa Mike Riley alikuwa kama mita 2 tu toka walipovaana Lampard na Alonso na ingawa marudio ya video yameonyesha Lampard aliucheza mpira na hakukusudia kucheza rafu, Refa huyo alitoa Kadi Nyekundu moja kwa moja.
Hii si mara ya kwanza kwa Lampard na Alonso kukwaana uwanjani kwani mwaka 2005 Lampard alimvunja enka Alonso.
Endapo rufaa ya Lampard itatupwa basi atazikosa mechi za LIGI KUU dhidi ya Hull na Aston Villa na ile ya Raundi ya 5 ya Kombe la FA dhidi ya Watford.
FA itaisikiliza Rufaa hiyo siku ya Jumanne ijayo.


MECHI ZIJAZO ZA LIGI KUU ENGLAND [saa ni za bongo]

Jumamosi, 7 Februari 2009
Man City v Middlesbrough [saa 9 dak 45 mchana]
[saa 12 jioni]
Blackburn v Aston Villa
Chelsea v Hull
Everton v Bolton
Portsmouth v Liverpool
Sunderland v Stoke
West Brom v Newcastle
Wigan v Fulham
Jumapili, 8 Februari 2009
[saa 10 na nusu jioni]
Tottenha v Arsenal
[saa 1 usiku]
West Ham v Man U
Jumamosi, 14 Februari 2009
[saa 12 jioni]

Portsmouth v Man City
Jumatano, 18 Februari 2009
[saa 5 usiku]

Man U v Fulham
Refa Mike Riley 'aihujumu' Chelsea!!!!

Kadi Nyekundu, ambayo Timu nzima ya Chelsea ililalamikia, kwa Kiungo Frank Lampard kwenye dakika ya 60 iliwakata maini na kuruhusu Liverpool kuwachosha Chelsea na kupata mabao 2 dakika za mwishoni.
Lampard waziwazi kabisa aliucheza mpira lakini Refa Mike Riley akadhani amemchezea Rafu mbaya Xabi Alonso.
Uamuzi huu uliidhoofisha sana Chelsea mbayo tayari ilionekana kuzidiwa kila kitu.
Torres alifunga bao la kwanza dakika ya 88 na la pili dakika za majeruhi.

Newcastle 1 Sunderland 1

Djibril Cisse aliipatia Sunderland dakika ya 32 lakini Refa Howard Webb aliwapa Newcastle penalti tata iliyofungwa na Shola Ameobi dakika ya 69.
Powered By Blogger