UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Mechi za mwisho za MAKUNDI!!!Jumanne tarehe 9 Desemba 2008 na Jumatano mechi za mwisho za Makundi ya kugombea Klabu Bingwa Ulaya 2008/9, yaani UEFA CHAMPIONS LEAGUE, zitamalizika.
Awamu hii iligawiwa kwenye Makundi manane yenye timu 4 kila moja huku mbili za juu zikisonga mbele kuingia Raundi inayofuata ya Mtoano itakayokuwa na jumla ya timu 16.
Timu zitakazokuwa nafasi ya 3 toka kila Kundi zitaingizwa kwenye Kapu la Dro yenye Timu 32 kugombea Kombe la UEFA.
Mpaka sasa Timu 13 kati ya 16 tayari zimeshafuzu kuingia Raundi hiyo ya Mtoano.
Timu hizo 13 ni pamoja na Mabingwa Watetezi wa Kombe hili Manchester United, Liverpool, Inter Milan, Atletico Madrid, Villareal , Barcelona, Sporting Lisbon, Lyon, Bayern Munich, Arsenal, FC Porto, Juventus na Real Madrid.
Timu 3 zilizobaki zitakazokamilisha idadi ya Timu 16 moja itatoka Kundi B, ambako tayari Inter Milan kashafuzu, hivyo nafasi hiyo moja itaamuliwa kwenye mechi ya mwisho ya Jumanne kati ya Panathinaikos na Anorthosis Famagusta na mshindi ndie ataendelea.
Nafasi mbili za mwisho kukamilisha jumla ya Timu 16 ni za Timu za Kundi A ambamo kukiwa kumesalia mechi moja kwa kila Timu, AS Roma, anaongoza Kundi hili akiwa na pointi 9, Chelsea, ni wa pili akiwa na pointi 8 na Bordeaux wa tatu akiwa na pointi 7 huku CFR Cluj wa mwisho akiwa na pointi 4.Katika mechi za mwisho, AS Roma anamkaribisha Bordeaux na Chelsea atakuwa nyumbani Stamford Bridge kupambana na CFR Cluj. Timu mbili za juu toka Kundi hili zitaendelea.
Vilevile, mechi hizi za mwisho kwa baadhi ya Makundi zitaamua nani atashika nafasi ya uongozi na nani wa pili kitu ambacho ni muhimu sana kwenye upigaji kura timu zipi zinakutana kwenye Raundi hiyo ya Mtoano yenye jumla ya timu 16 zitakazopangwa kucheza nyumbani na ugenini kuanzia tarehe 24 na 25 Februari 2009.
Umuhimu huo unakuja kutokana na Timu iliyoshika uongozi kupangiwa kukutana na mshindi wa pili toka kundi jingine na kwamba timu zilizokuwa Kundi moja kwenye awamu ya Makundi na zile zinazotoka Nchi moja haziwezi kupangwa kukutana kwenye Raundi hiyo ya Mtoano.
Hivyo, kwenye Raundi ijayo, Man U, Arsenal, Liverpool na Chelsea haziwezi kukutana kwani zote zinatoka England.
Dro ya kuamua nani wanakutana kwenye Mtoano itafanyika tarehe 19 Desemba 2008.
KUNDI A
Kundi hili ndilo lenye kasheshe kubwa.
Mahesabu yake ni kwamba ni CFR Cluj pekee ndio imeshatolewa nje na ina uhakika wa kumaliza nafasi ya mwisho. Chelsea wanawakaribisha CFR Cluj hapo Jumanne.
Chelsea wanahitaji ushindi ili wasonge mbele ingawa wanaweza kusonga mbele hata wakifungwa endapo tu Bordeaux hawatowafunga AS Roma timu inayoongoza Kundi hili kwenye mechi itakayochezwa Rome, Italia.
Nao AS Roma wanaweza kusonga mbele hata kama wakifungwa ikiwa Chelsea atafungwa.
Bordeau hana ujanja. Lazima amfunge AS Roma ili asonge mbele.
KUNDI B
Inter Milan, ambao washafuzu, watashika uongozi Kundi hili wakiifunga Werder Bremen walio nafasi ya mwisho na ambao wanahitaji ushindi angalau wamalize wa tatu na kucheza Kombe la UEFA. Na hata huo ushindi unaweza usitosheleze kwa Werder Bremen kwani ikiwa Anorthosis Famagusta ya Cyprus ikiifunga Panathinaikos ya Ugiriki hukohuko Ugiriki basi Anorthosis Famagusta watasonga mbele na Panathinaikos watacheza UEFA.
Lakini droo kwa Panathinaikos ni vilevile nzuri kuwafanya wasonge mbele ingawa ushindi unaweza kuwapa nafasi ya kuongoza Kundi.
KUNDI C
Kila kitu kimekamilika toka Kundi hili huku Barcelona wako wa kwanza na Sporting Lisbon wako wa pili na ndio timu zinazosonga mbele.
Timu toka Ukraine Shakhtar Donetsk iko ya 3 na itacheza UEFA.
FC Basel ya Uswisi wako mkiani na nje ya mashindano na wanacheza mechi ya mwisho na Sporting Lisbon kukamilisha ratiba tu.
KUNDI D
Atletico Madrid na Liverpool wameshafuzu lakini nani ndie wa kwanza ndio kitaamuliwa kwenye mechi zao za Jumanne. Timu zote hizi zina pointi 11 lakini Atletico Madrid wanaongoza kwa tofauti ya magoli.
Atletico Madrid atacheza ugenini na Olympique de Marseille ambao wanahitaji ushindi ili wacheze UEFA.
Liverpool watakuwa wageni wa PSV Eindhoven ambao nao wanahitaji ushindi wa nguvu ili kuwapiku Marseille kucheza UEFA.
KUNDI E
Mabingwa Watetezi wa Kombe hili Manchester United wanaoongoza ingawa wako pointi sawa na Villareal, wote wakiwa wameshapita, wanawakaribisha Aaalborg ya Demark ambao nao washaingia UEFA CUP.
Man U wanajua wazi wakishinda mechi hii basi watashika uongozi Kundi hili labda Villareal aifunge Celtic magoli mawili zaidi ya yale Man U watawafunga Aalborg.
Celtic ya Scotland, timu iliyotupwa nje, itaikaribisha Villareal.
KUNDI F
Lyon wanawakaribisha Bayern Munich katika mechi itakayoamua nani anachukua hatamu za Kundi hili kwani timu zote zimeshafuzu.
Ushindi kwa Lyon au suluhu ya bila magoli itawapa uongozi Lyon.
Ili wacheze UEFA, wenyeji Steau Bucharest lazima wawafunge Fiorentina na matokeo mengine yeyote Fiorentina ataonja UEFA.
KUNDI G
Arsenal wanasafiri hadi Ureno kupambana na FC Porto na ingawa timu zote zimefuzu ni pambano ambalo litaamua nani ataongoza Kundi hili huku Arsenal anahitaji suluhu tu ili aongoze.
Nao Fenerbahce watasafiri hadi nyumbani kwa Dynamo Kiev na inabidi washinde ili wacheze UEFA.
KUNDI H
Juventus wanaongoza Kundi hili na wakicheza nyumbani wanahitaji sare tu katika mechi na timu iliyotupwa nje ya FC Bate.
Real Madrid, nao washafuzu ingawa wakishinda na Juventus akifungwa basi wao watashika hatamu.
Real anacheza na timu ya FC Zenit St Petersburg ambao sasa watacheza UEFA baada ya kukosa nafasi kusonga mbele na hii ni nafasi nzuri kwao kutetea Taji lao la UEFA kwani wao ndio Mabingwa wa UEFA CUP msimu uliopita.
RATIBA KAMILI NI:
Jumanne, 9 Decemba 2008
KUNDI A
Chelsea v CFR
Roma v Bordeaux,
KUNDI B
Werder Bremen v Inter Milan,
Panathinaikos v Anorthosis Famagusta,
KUNDI C
Barcelona v Shakhtar Donetsk,
Basle v Sporting,
KUNDI D
Marseille v Atletico Madrid,
PSV vLiverpool,
Jumatano, 10 Decemba 2008
KUNDI E
Celtic v Villarreal,
Man U v AaB,
KUNDI F
Steaua Bucuresti v Fiorentina
Lyon v Bayern Munich
KUNDI G
Dynamo Kiev v Fenerbahce,
FC Porto vArsenal,
KUNDI H
Juventus v BATE
Real Madrid v Zenit St Petersburg