Wednesday, 24 December 2008

Ferguson: 'Sinunui Mchezaji Januari!'

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema hawana haja ya kununua Mchezaji yeyote wakati dirisha la uhamisho litakapofunguliwa Januari 2009.
Msimu ulipoanza, Manchester United ilinunua Mchezaji mmoja tu ambae ni Dimitar Berbatov waliemnunua kutoka Tottenham kwa Pauni Milioni 30 mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Ferguson ametamka: 'Tulichukuwa Wachezaji 23 kwenda Japan na tumetwaa Ubingwa wa Dunia! Sina wasiwasi kumchezesha yeyote kati ya hao wakati wowote!'

Mourinho anatamani kurudi LIGI KUU ENGLAND!

Aliekuwa Meneja machachari na mwenye vituko wa Chelsea, Jose Mourinho, amekiri ana hamu sana ya kurudi England ili aongoze Klabu ya LIGI KUU.
Mourinho kwa sasa yuko Italia na Timu ya Inter Milan ambayo ndio kinara wa Ligi huko iitwayo Serie A na ambao watakutana na Mabingwa Watetezi wa Ulaya Man U kwenye Raundi ya Mtoano ya UEFA Champions League mwezi Februari mwakani.
Akihojiwa, Mourinho: 'Sifichi. Naipenda LIGI KUU England. Lazima siku moja nirudi huko!'

Scolari ashangazwa na Kadi Nyekundu aliyopewa Nahodha wake John Terry!!

Meneja wa Chelsea Luis Felipe Scolari amesema ameshangazwa na Mwamuzi Phil Dowd kumpa John Terry Kadi Nyekundu.
Terry alipewa kadi hiyo siku ya Jumatatu usiku wakati Chelsea ilipocheza na Everton na Terry kumchezea vibaya Leon Osman kwenye dakika ya 35.
Mara baada ya mechi hiyo Scolari aligoma kufanya mahojiano na Waandishi wa Habari na vilevile alikataza mtu yeyote wa Klabu kuhojiwa.

Fabregas kuepuka kisu!!

Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas alieumizwa goti kwenye mechi kati ya Arsenal na Liverpool amethibitisha kuwa Daktari Bingwa wa mjini Barcelona, Spain ameridhia asifanyiwe upasuaji na badala yake apumzike tu ingawa muda unaokadiriwa goti lake kupona ni miezi minne.

Tuesday, 23 December 2008

IMETHIBITISHWA: Fabregas nje miezi minne!

Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, amethibitisha kuwa Nahodha wake Cesc Fabregas atakuwa nje ya uwanja hadi mwezi Aprili mwakani baada ya Madaktari kugundua ameumia vibaya ndani ya goti lake.

Cesc Fabregas hatihati kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Kiungo mahiri wa Arsenal ambae pia ndie Nahodha, Cesc Fabregas, huenda akawa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuumia goti kwenye mechi ya Arsenal na Liverpool.
Fagregas aliumia baada ya kupigana kibuyu na Xavi Alonso wa Liverpool katika kipindi cha kwanza na kutolewa nje ya uwanja hapohapo na nafasi yake kuchukuliwa na Vassiriki Diaby.
Hatma yake itajulikana leo baada ya kuchunguzwa na wataalam.

LIGI KUU ENGLAND inaingia patamu!

LIGI KUU ENGLAND sasa inaingia kwenye mechi ngumu na za mfululizo zitakazochezwa kipindi cha Sikukuu ya Krismas siku ya Boxing Day tarehe 26 Desemba 2008 na kufuatiwa na mechi nyingine baada ya mapumziko ya siku moja tu kwa baadhi ya timu.
Kihistoria kipindi hiki ndio hutoa mwanga Timu zipi zitapata mafanikio na zipi zitakumbwa na vita ya kupuruchuka kushushwa daraja.

Kimsimamo, kwa Timu za juu hali iko hivi:

-Liverpool: mechi 18 pointi 39

-Chelsea: mechi 18 pointi 38

-Aston Villa: mechi 18 pointi 34

-Man U: mechi 16 pointi 32

-Arsenal: mechi 18 pointi 31

Ijumaa, 26 Decemba 2008
[saa 9 dak 45 mchana]


Stoke v Man U

[saa 10 jioni]

Liverpool v Bolton
Portsmouth v West Ham
Chelsea v West Brom
Tottenham v Fulham

[saa 12 jioni]

Man City v Hull
Middlesbrough v Everton
Sunderland v Blackburn
Wigan v Newcastle

[saa 2 na robo usiku]

Aston Villa v Arsenal

Jumapili, 28 Decemba 2008
[saa 9 mchana]

Newcastle v Liverpool

[saa 11 jioni]

Arsenal v Portsmouth
Bolton v Wigan
Everton v Sunderland
Fulham v Chelsea
West Brom v Tottenham
West Ham v Stoke
[saa 1 na robo usiku]
Blackburn v Man City

Jumatatu, 29 Decemba 2008
[saa 5 usiku]

Man U v Middlesbrough

Jumanne, 30 Decemba 2008
[saa 5 usiku]

Hull v Aston Villa


LIGI KUU ENGLAND: Nahodha John Terry ala NYEKUNDU!

Everton 0 Chelsea 0

Nahodha wa Chelsea John Terry alitandikwa KADI NYEKUNDU na Refa Phil Dowd baada ya kumchezea rafu mbaya Winga wa Everton Leon Osman kwenye dakika ya 36 ya mechi lakini Chelsea wakajikongoja na kupata suluhu.

Monday, 22 December 2008

LIGI KUU ENGLAND: Msimu huu Mameneja 6 washabwagwa!! Nani atafuata?

LIGI KUU ENGLAND inasifika ndio ligi bora duniani lakini imeshaanza kurithi mwenendo mbaya ambao zamani ulikuwa ukionekana kwenye ligi za nchi za Italy, Spain na hasa nchi za Marekani ya Kusini tu!
Mwendo huu mbovu ambao umeleta wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya wadau wa soka la England ni ile tabia ya kuwatimua au kulazimisha Mameneja wa Klabu za Soka kujiuzulu.
Tangu msimu huu uanze hapo mwezi Agosti tayari Mameneja kadhaa wa Klabu za LIGI KUU ENGLAND hawana kazi!
Ukichukulia kwamba LIGI KUU ina Klabu 20, hivyo wapo Mameneja 20, basi hiyo idadi ni kubwa mno na inatisha na kuleta mtikiso mkubwa sana ndani ya soka ya Uingereza.

Mpaka sasa mabadiliko ya Mameneja ni:

-Paul Ince: Blackburn Rovers-aliondolewa Desemba 16.

-Roy Keane: Sunderland-aliondoka 4 Desemba.

-Harry Redknapp: Portsmouth-yeye alihamia Tottenham 25 Oktoba.

-Juande Ramos: Tottenham-kafukuzwa 25 Oktoba.

-Kevin Keagan: Newcastle-mwenyewe alibwaga manyanga 4 Septemba.

-Alan Curbishley: West Ham-aliachishwa 3 Septemba.

Sasa, kwenye anga za soka, upo mdahalo mkubwa sana wa nani ataingia kwenye listi hiyo?
Wanaotarajiwa kujumuika kwenye listi hiyo ni pamoja na, amini usiamini, Luis Felipe Scolari, Meneja Mbrazil wa Klabu ya Chelsea.
Yeye anahusishwa sana hasa kwa dhana kwamba Chelsea haichezi soka la kuvutia na matokeo mengi ya mechi zake ni kama tombola kitu ambacho kinahisiwa kumkera mmiliki wa Klabu hiyo, tajiri aliekubuhu toka Urusi Roman Abramovich, ambae amwekeza mabilioni ya pesa.
Mwingine anaeingizwa kwenye listi hii ni Mark Hughes wa Manchester City.
Huyu alitolewa timu ya Blackburn Rovers na kuingizwa Manchester City na aliekuwa Waziri Mkuu wa Thailand Shinawatra Thanksin ambae alikuwa ndie mmiliki wa Klabu hiyo.
Wakati Mark Hughes anatua tu hapo Manchester City, Shinawatra, pengine kufuatia matatizo yake ya kisiasa huko kwao Thailand ambako alikimbia baada ya kuandamwa na kashfa za rushwa na kuburuzwa Mahakamani, aliamua kuiuza Klabu hiyo kwa Koo ya Kifalme tajiri sana kutoka Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.
Matajiri hao wa Kiarabu, mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, siku hiyo hiyo walipotangazwa kuwa ndio wamiliki wapya wa Manchester City na ikiwa ndio siku ya mwisho kwa dirisha la uhamisho la kuhama Wachezaji kufungwa, walikufuru kwa kumnyotoa Staa toka Brazil Robinho aliekuwa akichezea Real Madrid kwa dau la Pauni Milioni 32 ambalo ndio rekodi ya bei ghali kwa kununuliwa Mchezaji England na kumleta Manchester City!
Leo, miezi minne baadae, Manchester City wako nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi wakiwa timu ya 3 toka chini na hilo ndio eneo la timu zinazoporomoshwa daraja mwishoni mwa msimu!
Hilo ndio janga linalomkabili Mark Hughes wakati akiwa Meneja wa Klabu inayokejeliwa kuwa ndio tajiri duniani!
England kuna Chama cha Mameneja wa Ligi kiitwacho LEAGUE MANAGERS ASSOCIATION [LMA] na siku zote kimepinga maamuzi ya kuwatimua Mameneja bila ya kupewa nafasi, muda na mtaji wa kuongoza timu.
LMA siku zote imekuwa ikitoa mifano ya Sir Alex Ferguson wa Manchester United na Arsene Wenger wa Arsenal kwamba ukimpa Meneja nafasi, muda na mtaji basi lazima Klabu itakuwa na mafanikio!
Sir Alex Ferguson yuko Manchester United tangu tarehe 6 Novemba 1986 na katika miaka 22 aliyokuwa hapo ameshaweka historia ya kuwa Meneja Bora katika historia ya soka Uingereza.
Yeye ameshatwaa Makombe, Ubingwa na Tuzo ambazo listi yake ni ndefu kupita urefu wa makala hii!
Siku chache zilizopita, Sir Alex Ferguson ameiwezesha Manchester United kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Duniani hili likiwa Kombe lake kubwa la tatu mwaka huu baada ya kuutwaa Ubingwa wa LIGI KUU ENGLAND na Kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei.
Arsene Wenger yuko Arsenal kwa miaka 12 tangu alipojiunga tarehe 1 Oktoba 1996 na yeye ndie mwenye sifa ya kuwa Meneja Bora na mwenye mafanikio bora katika historia ya miaka 100 ya Klabu ya Arsenal, klabu iliyoanzishwa mwaka 1886!
Katika LIGI KUU ENGLAND, Arsene Wenger ndie mwenye rekodi pekee ya kuwa Meneja pekee ambae Klabu yake haikufungwa msimu mzima!
Huo ulikuwa msimu wa mwaka 2004!
Sasa, fanananisha na Paul Ince aliepewa madaraka Mwezi Agosti mwaka huu na wakati anaingia tu hapo Klabuni wamiliki wanauza Wachezaji bora wa timu na hapewi mtaji wala Mchezaji yeyote mpya!
Baada ya Mechi 17 za LIGI KUU, Paul Ince akiwa madarakani na kushinda mechi 3 tu, anatimuliwa!
Jambo hili limewakera wengi na Sir Alex Ferguson ashatamka: 'Kwa sasa ni vigumu kwa Mameneja wapya! Klabu zinatawaliwa na Wamiliki na Bodi zenye uroho wa pesa tu! Klabu sasa zimekuwa si mali ya Mashabiki na wapenzi-ni mali za mabwanyenye waroho wa utajiri wasiojua utu hata chembe! Inasikitisha sana!'
Wenger alinena: 'Ni upumbavu! Huwezi kumpa mtu miezi miwili ukategemea maajabu! Hii si soka sasa, hii ni kampuni za watu wenye pesa wasiojua soka!'
Inasikitisha na inaondoa ile ladha ya ushindani ndani ya kandanda!
MABINGWA WA ENGLAND, MABINGWA WA ULAYA na sasa MABINGWA WA DUNIA: Hata Sepp Blatter wa FIFA arukaruka kwa furaha!!!
Baada ya kukabidhiwa Kombe lao na kutawazwa rasmi kuwa wao ndio MABINGWA WA DUNIA, Mabingwa wa England ambao pia ndio Mabingwa wa Ulaya, Manchester United, wakiongozwa na Nahodha wa mechi hiyo, Beki Rio Ferdinand alieshikilia Kombe hilo, waliimba, kupiga kelele, vifijo, nderemo na rapu za kila lugha maana kundi la Wachezaji wa sasa wa Man U wanatoka kila kona ya Dunia!!
Hata Rais wa FIFA Sepp Blatter aliingia uwanjani kwa furaha [pichani juu] maana NI KWELI MAN U NI TIMU YA DUNIA!
Hebu tizama baadhi tu ya Wachezaji: Park ni Mkorea, Vidic anatoka Serbia, Evra ni Mfaransa, Ronaldo na Nani ni Wareno, na ingawa Anderson na Rafael wanatoka Brazil, hawa wawili wanaweza kuongea Kireno pamoja na akina Ronaldo na Nani!
Yupo Tevez toka Argentina, Berbatov wa Bulgaria na usiwasahau Waingereza wenyewe akina Rio, Neville, Carrick, Rooney, Scholes wakisaidiwa na Wajomba zao toka Ireland O'Shea na Evans, na Giggs kutoka Wales!
Alikuwepo chipukizi Danny Welbeck ambae ingawa Mwingereza asili yake ni Ghana!
Na, yupo Manucho toka Angola! Huyu nae anaweza kuteta Kireno na kundi la Ronaldo!
Aaah, yupo Kipa stadi toka Uholanzi Edwin van der Sar, akisaidiwa na Tomasz Kuszczak toka Poland na Chipukizi Ben Amos toka Uingereza!
Juu ya wote, wapo viongozi na hao ni Sir Alex Ferguson anaetoka Scotland na Sir Bobby Charlton ambae ni Mwingereza halisi!
Mbali ya wote, ukiacha kundi la Mashabiki wachache waliotoka Uingereza kuja kuishangilia Man U, ZAIDI YA ASILIMIA 90 YA WATAZAMAJI HAPO UWANJANI YOKOHAMA, JAPAN WALIOKUWA WAKIISHANGILIA MANCHESTER UNITED WALIKUWA NI WAJAPANI HALISI!
Wakati Rooney azawadiwa gari huko Japan, Mashabiki wa Quito walia huko Ecuador!!

Wakati Wayne Rooney, nyota wa Mabingwa wapya wa Dunia Manchester United, akizawadiwa gari mpya aina ya Toyota na kukabidhiwa UFUNGUO MKUBWA WA DHAHABU baada ya kuiwezesha timu yake kunyakua Kombe la Klabu Bingwa Duniani huko Yokohama, Japan baada ya kuiua Liga de Quito kwa bao 1-0, Mashabiki wa Quito waliangua vilio waziwazi huko kwao walipokuwa wakiangalia pambano hilo moja kwa moja toka kwenye TV kubwa zilizowekwa hadharani kwenye mitaa maarufu huko nchini kwao Ecuador!!
Rooney ndie aliechaguliwa Mchezaji Bora wa mechi ya Fainali na pia Mchezaji Bora wa Mashindano hayo yote na vilevile Mfungaji Bora na hivyo kushinda Mpira wa Dhahabu.
Cristiano Ronaldo alizawadiwa Mpira wa Fedha.
Wayne Rooney alifunga jumla ya mabao matatu kwenye Mashindano hayo mawili yakiwa kwenye Nusu Fainali dhidi ya Gamba Osaka ya Japan mechi ambayo Man U walishinda 5-3.

Sunday, 21 December 2008

MAN U NI MABINGWA WA DUNIA! Rooney awapa ushindi!!

Mabingwa wa England na Ulaya, Manchester United, wamejiongezea taji lingine na sasa ni Klabu Bingwa Duniani baada ya kuipachika Liga de Quito ya Ecuador, Mabingwa wa Marekani Kusini, bao 1-0 kwa bao tamu la Wayne Rooney katika mechi ya Fainali ya Klabu Bingwa Duniani iliyochezwa Yokohama, Japan.
Wakiwa wametawala kipindi chote cha kwanza na kukosa mabao mengi, Manchester United walipata pigo pale Beki wao Nemanja Vidic alipotolewa nje kwa Kadi Nyekundu dakika ya 49 ya mchezo baada ya kumpiga kipepsi Mchezaji wa Quito Claudio Bieler.
Ikabidi Man U wamtoe Fowadi Carlos Tevez na kumwingiza Mlinzi Johnny Evans kuziba pengo la Vidic.
Hata hivyo pengo la kucheza watu 10 halikuonekana kwani Man U waliendelea kutawala na kushambulia.
Ilipofika dakika ya 73, kazi nzuri ya Cristiano Ronaldo ilimkuta Wayne Roonel aliefunga bao safi la ushindi.
Meneja Sir Alex Ferguson alikipongeza kikosi chake kwa kucheza kitimu na juhudi hasa walipokuwa 10 tu.
Nae Mchezaji aliewapa Kombe, Wayne Rooney, alietangazwa ndie Mchezaji Bora wa Mashindano, alijigamba: 'Sisi ndio bora duniani! Ushindi huu ni muhimu kwa klabu!'

LIGI KUU ENGLAND: Arsenal 1 Liverpool 1

Vinara wa LIGI KUU ya England, Liverpool walilazimisha sare ya 1-1 na Arsenal katika mechi iliyochezwa nyumbani kwa Arsenal uwanja wa Emirates.
Arsenal walipata bao lao kwenye dakika ya 24 baada ya Robin Van Persie kufunga bao la kifundi sana baada ya kupokea pasi safi toka kwa Samir Nasri.
Liverpool, wakicheza bila ya kuwa na Meneja wao Rafa Benitez aliefanyiwa operesheni kuondolewa vijiwe kwenye figo, walisawazisha kwa bao zuri pia kupitia Robbie Keane aliefumua shuti kali dakika ya 42.
Mshambuliaji nyota wa Arsenal Emmanuel Adebayor alipewa Kadi Nyekundu dakika ya 62 baada ya kupata Kadi 2 za Njano.

Matokeo mechi nyingine za LIGI KUU:

Newcastle 2 Tottenham 1

West Brom 2 Manchester City 1

MECHI INAYOFUATA: Jumatatu, 22 Desemba 2008: Everton v Chelsea

Endapo Chelsea ataifunga Everton kwenye mechi hii, basi Chelsea atachukua uongozi wa LIGI KUU.

Mpaka sasa msimamo kwa Timu 5 za juu ni kama ufuatavywo:

-Liverpool: mechi 18 pointi 39

-Chelsea: mechi 17 pointi 37

-Aston Villa: mechi 18 pointi 34

-Manchester United: mechi 16 pointi 32

-Arsenal: mechi 18 pointi 31
KLABU BINGWA DUNIANI: Leo Fainali!!!

Liqa de Quito v Manchester United

Leo saa 7 na nusu mchana saa za kibongo, Mabingwa wa Ulaya Manchester United watakutana na Mabingwa wa Marekani ya Kusini Liga de Quito, klabu kutoka Ecuador, katika Fainali ya FIFA CLUB WORLD CUP mechi itakayochezwa Yokohama International Stadium mjini Yokohama huko Japan.
Manchester United iliwahi kuchukua Kombe linalofanana na hili mwaka 1999 pale ilipoifunga Palmeiras ya Brazil iliyokuwa ikiongozwa na Meneja wa sasa wa Chelsea, Luis Felipe Scolari, kwa bao 1-0.
Wakati huo mechi zilikuwa zinashindaniwa na Klabu mbili tu, moja ikiwa Bingwa wa Ulaya na nyingine Bingwa wa Marekani ya Kusini.
Siku hizi mfumo wa Klabu Bingwa Duniani umebadilika na kila Bara la Dunia linawakilishwa na Bingwa wake.
Safari hii, Afrika iliwakilishwa na Al Ahly ya Misri.
Kocha wa Liga de Quito, Edgardo Bauza amesema mechi hii itakuwa ngumu sana lakini watacheza kufa na kupona.
Nae Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson amesema Quito wanacheza kandanda la aina ile ile ya Timu za Marekani ya Kusini na hivyo ni timu ngumu.
Nae Mchezaji Bora wa Ulaya, Cristiano Ronaldo, ametamka; 'Hakika si mechi rahisi lakini nataka kushinda kwa ajili ya timu yangu na mashabiki wa England. Hii itatupa morali tena kushinda Ligi Kuu na Klabu Bingwa Ulaya!'
LIGI KUU ENGLAND: Meneja Sam Allardyce aanza vyema utawala Blackburn!!

Meneja mpya wa Blackburn Sam Allardyce ameanza vyema utawala wake baada ya kuwakung'uta Stoke City mabao 3-0 uwanja wa nyumbani Ewood Park.
Mabao ya Blackburn yalifungwa ndani ya nusu saa ya kwanza ya mchezo wafungaji wakiwa McCarthy, dakika ya 9 kwa penalti, Roberts dakika ya 18 na Benni McCarthy akafunga tena dakika ya 27.

Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, matokeo ni:

Bolton 2 Portsmouth 1

Fulham 3 Middlesbrough 0

Hull City 1 Sunderland 4

West Ham 0 Aston Villa 1

MECHI ZA LEO NA KESHO:

JUMAPILI, 21 Desemba 2008
[saa 10 na nusu jioni]


West Brom v Man City

[saa 12 jioni]

Newcastle v Tottenham

[saa 1 usiku]

Arsenal v Liverpool

JUMATATU, 22 Desemba 2008
[saa 5 usiku]

Everton v Chelsea
Powered By Blogger