Monday 22 December 2008

LIGI KUU ENGLAND: Msimu huu Mameneja 6 washabwagwa!! Nani atafuata?

LIGI KUU ENGLAND inasifika ndio ligi bora duniani lakini imeshaanza kurithi mwenendo mbaya ambao zamani ulikuwa ukionekana kwenye ligi za nchi za Italy, Spain na hasa nchi za Marekani ya Kusini tu!
Mwendo huu mbovu ambao umeleta wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya wadau wa soka la England ni ile tabia ya kuwatimua au kulazimisha Mameneja wa Klabu za Soka kujiuzulu.
Tangu msimu huu uanze hapo mwezi Agosti tayari Mameneja kadhaa wa Klabu za LIGI KUU ENGLAND hawana kazi!
Ukichukulia kwamba LIGI KUU ina Klabu 20, hivyo wapo Mameneja 20, basi hiyo idadi ni kubwa mno na inatisha na kuleta mtikiso mkubwa sana ndani ya soka ya Uingereza.

Mpaka sasa mabadiliko ya Mameneja ni:

-Paul Ince: Blackburn Rovers-aliondolewa Desemba 16.

-Roy Keane: Sunderland-aliondoka 4 Desemba.

-Harry Redknapp: Portsmouth-yeye alihamia Tottenham 25 Oktoba.

-Juande Ramos: Tottenham-kafukuzwa 25 Oktoba.

-Kevin Keagan: Newcastle-mwenyewe alibwaga manyanga 4 Septemba.

-Alan Curbishley: West Ham-aliachishwa 3 Septemba.

Sasa, kwenye anga za soka, upo mdahalo mkubwa sana wa nani ataingia kwenye listi hiyo?
Wanaotarajiwa kujumuika kwenye listi hiyo ni pamoja na, amini usiamini, Luis Felipe Scolari, Meneja Mbrazil wa Klabu ya Chelsea.
Yeye anahusishwa sana hasa kwa dhana kwamba Chelsea haichezi soka la kuvutia na matokeo mengi ya mechi zake ni kama tombola kitu ambacho kinahisiwa kumkera mmiliki wa Klabu hiyo, tajiri aliekubuhu toka Urusi Roman Abramovich, ambae amwekeza mabilioni ya pesa.
Mwingine anaeingizwa kwenye listi hii ni Mark Hughes wa Manchester City.
Huyu alitolewa timu ya Blackburn Rovers na kuingizwa Manchester City na aliekuwa Waziri Mkuu wa Thailand Shinawatra Thanksin ambae alikuwa ndie mmiliki wa Klabu hiyo.
Wakati Mark Hughes anatua tu hapo Manchester City, Shinawatra, pengine kufuatia matatizo yake ya kisiasa huko kwao Thailand ambako alikimbia baada ya kuandamwa na kashfa za rushwa na kuburuzwa Mahakamani, aliamua kuiuza Klabu hiyo kwa Koo ya Kifalme tajiri sana kutoka Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.
Matajiri hao wa Kiarabu, mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, siku hiyo hiyo walipotangazwa kuwa ndio wamiliki wapya wa Manchester City na ikiwa ndio siku ya mwisho kwa dirisha la uhamisho la kuhama Wachezaji kufungwa, walikufuru kwa kumnyotoa Staa toka Brazil Robinho aliekuwa akichezea Real Madrid kwa dau la Pauni Milioni 32 ambalo ndio rekodi ya bei ghali kwa kununuliwa Mchezaji England na kumleta Manchester City!
Leo, miezi minne baadae, Manchester City wako nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi wakiwa timu ya 3 toka chini na hilo ndio eneo la timu zinazoporomoshwa daraja mwishoni mwa msimu!
Hilo ndio janga linalomkabili Mark Hughes wakati akiwa Meneja wa Klabu inayokejeliwa kuwa ndio tajiri duniani!
England kuna Chama cha Mameneja wa Ligi kiitwacho LEAGUE MANAGERS ASSOCIATION [LMA] na siku zote kimepinga maamuzi ya kuwatimua Mameneja bila ya kupewa nafasi, muda na mtaji wa kuongoza timu.
LMA siku zote imekuwa ikitoa mifano ya Sir Alex Ferguson wa Manchester United na Arsene Wenger wa Arsenal kwamba ukimpa Meneja nafasi, muda na mtaji basi lazima Klabu itakuwa na mafanikio!
Sir Alex Ferguson yuko Manchester United tangu tarehe 6 Novemba 1986 na katika miaka 22 aliyokuwa hapo ameshaweka historia ya kuwa Meneja Bora katika historia ya soka Uingereza.
Yeye ameshatwaa Makombe, Ubingwa na Tuzo ambazo listi yake ni ndefu kupita urefu wa makala hii!
Siku chache zilizopita, Sir Alex Ferguson ameiwezesha Manchester United kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Duniani hili likiwa Kombe lake kubwa la tatu mwaka huu baada ya kuutwaa Ubingwa wa LIGI KUU ENGLAND na Kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei.
Arsene Wenger yuko Arsenal kwa miaka 12 tangu alipojiunga tarehe 1 Oktoba 1996 na yeye ndie mwenye sifa ya kuwa Meneja Bora na mwenye mafanikio bora katika historia ya miaka 100 ya Klabu ya Arsenal, klabu iliyoanzishwa mwaka 1886!
Katika LIGI KUU ENGLAND, Arsene Wenger ndie mwenye rekodi pekee ya kuwa Meneja pekee ambae Klabu yake haikufungwa msimu mzima!
Huo ulikuwa msimu wa mwaka 2004!
Sasa, fanananisha na Paul Ince aliepewa madaraka Mwezi Agosti mwaka huu na wakati anaingia tu hapo Klabuni wamiliki wanauza Wachezaji bora wa timu na hapewi mtaji wala Mchezaji yeyote mpya!
Baada ya Mechi 17 za LIGI KUU, Paul Ince akiwa madarakani na kushinda mechi 3 tu, anatimuliwa!
Jambo hili limewakera wengi na Sir Alex Ferguson ashatamka: 'Kwa sasa ni vigumu kwa Mameneja wapya! Klabu zinatawaliwa na Wamiliki na Bodi zenye uroho wa pesa tu! Klabu sasa zimekuwa si mali ya Mashabiki na wapenzi-ni mali za mabwanyenye waroho wa utajiri wasiojua utu hata chembe! Inasikitisha sana!'
Wenger alinena: 'Ni upumbavu! Huwezi kumpa mtu miezi miwili ukategemea maajabu! Hii si soka sasa, hii ni kampuni za watu wenye pesa wasiojua soka!'
Inasikitisha na inaondoa ile ladha ya ushindani ndani ya kandanda!

No comments:

Powered By Blogger