Saturday, 8 May 2010

Redknapp Meneja Bora Ligi Kuu 2009/10
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amenyakua Tuzo ya kuwa Meneja Bora wa Msimu.
Redknapp, miaka 63, amepewa Tuzo kwa kutambua mafanikio yake kwa kuiongoza Tottenham inyakue nafasi ya 4 Ligi Kuu na hivyo kuiwezesha kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Mwenyewe Redknapp amesema: “Nimefurahi kuzawadiwa lakini bila ya wenzangu Makocha, kina Kevin Bond, Joe Jordan, Clive Allen, Tony Parks, Tim Sherwood, Les Ferdinand na lile jopo la Wakufunzi wa Stamina na Viungo, nisingepata Tuzo hii!”
Redknapp alichukua hatamu Tottenham Oktoba 2008 huku Timu ikiwa mkiani kwenye Ligi Kuu na Msimu huu ipo nafasi ya 4 na inawezekana hata kuipiku Arsenal na kushika nafasi ya 3 ikiwa wataifunga Burnley na Arsenal kufungwa na Fulham siku ya Jumapili.
Redknapp amekuwa Meneja wa pili kushinda Tuzo hii tangu Ligi Kuu ianzishwe bila Timu yake kuwa Bingwa.
Meneja wa kwanza kuikwapua Tuzo bila ya kuwa Bingwa ni George Burley alietunukiwa baada ya kuiwezesha Ipswitch Town ishike nafasi ya 5 Msimu wa mwaka 2000/01.
Tuzo hii ya Meneja Bora hutolewa na Wadhamini wa Ligi Kuu, Barclays, na jopo la uteuzi huwa ni Vyama vya Soka, Vyombo vya Habari na Mashabiki.
Motta kuikosa Fainali UEFA CHAMPIONS LIGI
• Afungiwa Mechi 2
Bodi ya Nidhamu na Udhibiti ya UEFA imemfungia Mchezaji wa Inter Milan Thiago Motta kwa mechi mbili ikiwa ni adhabu baada ya kupewa Kadi Nyekundu mechi ya Nusu Fainali ya pili Inter waliporudiana na FC Barcelona Uwanjani Nou Camp Aprili 28.
Kifungo hicho kinamaanisha Motta hataruhusiwa kucheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI hapo Mei 22 Inter watakapoikwaa Bayern Munich.
Inter wamepewa siku tatu kukata rufaa lakini kawaida ya UEFA ni kuwa rufaa siku zote hutupiliwa mbali.
Motta anaungana na Mchezaji wa Bayern Munich Franck Ribery kukosa Fainali hiyo kwa kufungiwa na UEFA.
Ribery yamemkuta kama ya Motta alipotolewa kwa Kadi Nyekundu kwenye Nusu Fainali Bayern walipocheza na Lyon na UEFA ikampa adhabu ya kufungiwa mechi zaidi.
Bayern walimkatia rufaa Ribery lakini UEFA ikaitupa rufaa hiyo na sasa Bayern wamekwenda CAS [Court of Arbitration for Sports], Mahakama ya Usuluhisho kwa Michezo ili kumwezesha kucheza Fainali.
Togo huru!!
 -Blatter wa FIFA aokoa jahazi!!
Kufuatia usuluhishi wa Sepp Blatter, Rais wa FIFA, Togo itafutiwa adhabu yake ya kufungiwa na CAF, Shirikisho la Soka Afrika, kucheza Mashindano mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika waliyopewa kwa kujitoa Fainali za mashindano kama hayo yaliyofanyika Nchini Angola mwezi Januari baada ya Basi lao kushambuli kwa risasi na Waasi wa Jimbo la Angola la Cabinda na kumuua Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa Togo.
Blatter ametamka: “Nina furaha kusema tumepata ufumbuzi ulioridhisha pande zote. Mafanikio haya ni kwa Jamii yote ya Soka hasa ya Afrika.”
Rais wa CAF, Issa Hayatou, amekubali kuiomba Kamati Kuu ya CAF kuifuta adhabu kwa Togo ambayo ingewafanya wasicheze Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 na 2014.
Baada ya kufungiwa, Togo walikata rufaa kwa CAS [Court of Arbitration for Sports], Mahakama ya Usuluhisho kwa Michezo, na Mahakama hiyo ikamwomba Sepp Blatter kusuluhisha.
Hatua hii ya kuifungulia Togo itawalazimu CAF kurekebisha Ratiba ya Mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 ambayo ilishapangwa mwezi Februari bila Togo kushirikishwa.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 zitafanyika kwenye Nchi mbili kwa pamoja ambazo ni Gabon na Equatorial Guinea na zile za mwaka 2014 zitakuwa Libya.
KWINGINEKO ULAYA:
La Liga: Barca na Real zafukuzana!!!
Huko Spain kwenye La Liga ni mbio kati ya Vigogo wawili huku Mabingwa Watetezi, Barcelona wakiongozwa na Lionel Messi, ndio wako kileleni kwa pointi moja dhidi ya Mahasimu wao wakubwa Real Madrid wanaoongozwa na Cristiano Ronaldo.
Kila Timu imebakiwa na mechi mbili na wikiendi hii Real wanacheza na Athletic Bilbao na Barca watakwaana na Sevilla.
Barcelona wanaweza kuutwaa Ubingwa wikiendi hii ikiwa watashinda na Real kutoka sare.
Serie A: Inter wanyemelea Ubingwa
Huku kila Timu zimebakiwa na mechi mbili, Inter Milan ndio wanaongoza Serie A na AS Roma ni wa pili.
Inter, wanaocheza na Chievo Verona Jumapili, wanaweza kuutwaa Ubingwa hiyo Jumapili wakishinda na AS Roma kutoka sare au kufungwa na Cagliari.
Ligue 1: Olympique MAarseille tayari Bingwa
Olympique Marseille tayari washautwaa Ubingwa wa Ligue 1 hii ikiwa ni mara yao ya kwanza baada ya miaka 18.
Bundesliga: Bayern Munich anusa Ubingwa!
Bayern Munich anaongoza Ligi akiwa pointi 3 mbele ya Schalke na ana tofauti kubwa ya magoli [goli 17] na hivyo labda itokee balaa kubwa lisiloelezeka ili aukose Ubingwa.
Bayern wako ugenini kucheza na Hertha Berlin.
LIGI KUU England: Jumapili Msimu kwisha!
Timu zote za Ligi Kuu Jumapili saa 12 jioni, saa za bongo, zinashuka dimbani kucheza mechi zake za mwisho za Msimu huu huku tayari zishajulikana Timu 4 za kwanza zitakazocheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao na Timu 3 zinazoshushwa Daraja.
Lakini mpaka baada ya dakika 90 za mechi kati ya Chelsea v Wigan na Manchester United v Stoke City kumalizika ndipo Bingwa wa Msimu wa 2009/10 atajulikana huku Chelsea akitaka ushindi tu kuwa Bingwa na Man United anaomba Chelsea atoke sare au afungwe ili wao waifunge Stoke na kuwa Bingwa.
Timu 4 zitakazocheza UEFA CHAMPIONS LIGI ni Chelsea, Man United, Arsenal na Tottenham.
Timu 3 zilizoshuka Daraja ni Hull City, Burnley na Portsmouth.
RATIBA:
Jumapili, 9 Mei 2010
[saa 12 jioni]
Arsenal v Fulham
Aston Villa v Blackburn
Bolton v Birmingham
Burnley v Tottenham
Chelsea v Wigan
Everton v Portsmouth
Hull v Liverpool
Man United v Stoke
West Ham v Man City
Wolves v Sunderland
MSIMAMO LIGI KUU:
[Kila Timu imecheza Mechi 37 na kubakisha moja]
1. Chelsea pointi 83===KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
2. Man United pointi 82=KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
3. Arsenal pointi 72===KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
4. Tottenham 70=====KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
--------------------------------------
5. Man City 66====EUROPA LIGI
6. Aston Villa 64==EUROPA LIGI
7. Liverpool 62===EUROPA LIGI
---------------------------------------
8. Everton 58
9. Birmingham 50
10.Stoke City 47
11.Blackburn 47
12.Fulham 46
13.Sunderland 44
14.Bolton 36
15.Wigan 36
16.Wolves 35
17.West Ham 34
----------------------------------------------------
18.Hull 29=======IMESHUSHWA DARAJA
19.Burnley 27====IMESHUSHWA DARAJA
20.Portsmouth 19 =IMESHUSHWA DARAJA
[FAHAMU: Newcastle United na West Bromwich Albion zimepandishwa Daraja kutoka Coca Cola Championship kuingia Ligi Kuu baada ya Newcastle kuutwaa Ubingwa wa Daraja hilo na WBA kumaliza nafasi ya 2.
Timu ya tatu itakayoungana na hizo mbili itapatikana baada ya Michuano maalum itayoshirikisha Timu zilizomaliza nafasi ya 3 hadi ya 6.
Timu hizo ni Nottingham Forest, Cardiff City,Leicester City na Blackpool.
Michuano hiyo ni [Nyumbani na Ugenini]:
Mei 8 Blackpool v Nottingham Forest
Mei 9 Leicester City v Cardiff City
Marudio:
Mei 11 Nottingham Forest v Blackpool
Mei 12 Cardiff City v Leicester City
[WASHINDI KUKUTANA FAINALI WEMBLEY KUPATA TIMU MOJA ITAKAYOPANDA DARAJA]

Friday, 7 May 2010

Ancelotti aomba Wachezaji wake kuwa Kul!!
Bosi wa Chelsea Carlo Ancelotti amewataka Wachezaji wake kuwa watulivu watakapocheza Jumapili na Wigan Uwanjani Stamford Bridge katika mechi ya mwisho ya Msimu wa Ligi Kuu England ambayo Chelsea wakishinda tu wao ni Mabingwa wa 2009/10 na wakipata matokeo mengine zaidi ya hayo na Manchester United, watakaocheza nyumbani kwao Old Trafford na Stoke City kushinda, basi Man United watatwaa tena Ubingwa kwa mara ya 4 mfululizo.
Ancelotti amekiri Timu yake iko nafasi nzuri ya kuuchukua Ubingwa lakini ujumbe kwa Wachezaji wake umekuwa ni kuwataka waondoe hofu na kutulia.
Ancelotti amesema: “Kuwa Bingwa, lazima tucheze kama tulivyocheza na Stoke na Liverpool. Lazima tuwe na utulivu, tuwe na ukakamavu na nia ile ile!”
Safari hii, Ancelotti ataomba Chelsea iwe na bahati tofauti na ile iliyowapa kipigo cha 3-1 na Wigan walipokutana huko Uwanja wa DW mwezi Septemba katika mechi ya kwanza ya Ligi.
Fergie: ‘Wiki moja mbaya ilitugharimu!’
Sir Alex Ferguson ameungama kuwa wiki moja mbaya ndio imewaweka njia panda ya kuutetea Ubingwa wao wa Ligi Kuu kwa mara ya 4 mfululizo na pia kutoendelea kuwemo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wiki hiyo, mwezi Aprili, walifungwa na Chelsea 2-1 na wakatolewa na Bayern Munich kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI kwa magoli ya ugenini.
Ferguson amesema: “Ilikuwa wiki mbaya na imetupotezea kila kitu!”
Baada ya kufungwa 2-1 huko Ujerumani na Bayern Munich, wakatoka sare 0-0 na Blackburn kwenye Ligi Kuu na kuwapa mwanya Chelsea kuongoza Ligi na hatimaye Chelsea kuishinda Man United kiutata bao 2-1 wiki hiyo hiyo.
Nae Kiungo wa Man United, Darren Fletcher, yeye anaamini uhakika wa wao kutwaa Ubingwa ulipata dosari pale walipokumbwa na majeruhi wengi na hata kubakiwa na Difenda mmoja tu alie fiti na kuwalazimu yeye mwenyewe, Michael Carrick na Chipukizi Ritchie De Laet kucheza Difensi na kufungwa 3-0 na Fulham.
Fletcher amesema: “Bila ya dosari ile mambo yangekuwa mengine! Tulicheza gemu 3 au 4 tukiwa na Difensi ya kuungaunga!”
LA LIGA: Pellegrini adai Ubingwa ni Wikiendi hii!
Kocha wa Real Madrid, Manuel Pellegrini, amedai Ubingwa wa Spain utaamuliwa wikiendi hii kutokana na mechi za Real Madrid v Athletic Bilbao na Sevilla v Barcelona ambazo zitafanya kila Timu ibakiwe na mechi moja tu Ligi kwisha.
Mpaka sasa Mabingwa Watetezi Barcelona wanaongoza Ligi hiyo kwa pointi moja mbele ya Mahasimu wao wakubwa Real Madrid.
Obi kuikosa Fainali ya FA CUP
Kiungo kutoka Nigeria anaechezea Chelsea, John Mikel Obi, atazikosa mechi za mwisho za Klabu yake ikiwemo Fainali ya Kombe la FA Mei 15 na Portsmouth baada ya kufanyiwa operesheni ndogo ya goti.
Obi pia itaikosa mechi ya Chelsea Jumapili watapomaliza Ligi Kuu kwa kucheza na Wigan.
Mchezaji huyo aliumia goti Chelsea walipocheza na Bolton.
Man United kuzuru Marekani na Canada Majira ya Joto
Manchester United watacheza gemu nne huko USA na Canada katika ziara ya kabla kuanza Msimu mpya.
Man United kwanza wataenda Chicago ambako ni nyumbani kwa wadhamini wao wapya wa Jezi, AoN, hapo Julai 12 kwa mazoezi na kisha watacheza na Celtic ya Scotland Julai 16 Uwanja wa Rogers Centre huko Toronto, Canada.
Julai 21 watacheza na Philadelphia Union na Julai 25 wataivaa Kansas City Wizards.
Julai 28, Manchester United watacheza na Kombaini ya Mastaa wa Ligi ya MLS Mjini Houston.
Hii itakuwa ziara ya tatu kwa Man United Nchini Marekani baada ya kuzuru mwaka 2003 na 2004.
Man City yasisitiza Mancini kubaki!
Manchester City imetangaza haina nia ya kumtimua Meneja wake Roberto Mancini aliemrithi Mark Hughes mwezi Desemba mwaka jana baada ya kukosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao walipofungwa na Tottenham 1-0 hapo juzi.
Msimu ujao, England itawakilishwa na Chelsea, Manchester United, Arsenal na Tottenham kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI kwa vile zitamaliza Ligi Kuu zikiwa nafasi 4 za juu.
Man City imesisitiza Mancini ataendelea kuijenga Klabu hiyo na wanategemea Msimu ujao kufanya vyema zaidi chini yake.

Thursday, 6 May 2010

LIGI KUU waigomea Fulham kupanga upya mechi na Ze Gunners
Wasimamizi wa Ligi Kuu England wamelikataa ombi la Fulham la kutaka mechi yao ya mwisho na Arsenal itakayochezwa Jumapili isogezwe mbele na kuchezwa Jumamosi ili wapate muda mrefu zaidi wa kujitayarisha kwa ajili ya Fainali ya EUROPA LIGI ambayo watacheza Jumatano ijayo na Atletico Madrid huko Hamburg, Ujerumani.
Ligi Kuu imelitupa ombi hilo kwa kusema kuwa kwa vile Jumapili ni siku ya mwisho ya Ligi mechi zote zimepangwa kuanza muda mmoja na haitakuwa vyema mechi ya Arsenal v Fulham itakayochezwa Uwanja wa Emirates isogezwe.
Redknapp: “Ni sahihi sisi kucheza UEFA!”
Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp, anaamini Timu yake inastahili kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao baada ya kuinyakua nafasi ya 4 walipoifunga Manchester City bao 1-0 hapo jana Uwanjani City of Manchester kwa bao la dakika ya 82 la Peter Crouch.
Redknapp ametamka: “Ulikuwa usiku mwema! Tumecheza vizuri na tulistahili kushinda!”
Tottenham wanamalizia ligi Jumapili kwa kucheza na Burnley na upo uwezekano wa kushika nafasi ya 3 ikiwa watashinda na Arsenal, ambao wako nafasi hiyo, wafungwe na Fulham.
Mkataba wa Rooney kujadiliwa baadae
Manchester United na Wawakilishi wa Wayne Rooney wamekubaliana kufanya mazungumzo ya kuuboresha Mkataba wa Mchezaji huyo baada ya kumalizika Fainali za Kombe la Dunia.
Mkataba wa sasa wa Rooney bado una miaka miwili kumalizika na unampa Mshahara wa Pauni Elfu 90 kwa wiki na huo mpya unategemewa kumpatia Pauni 150,000 kwa wiki na kumfanya awe na Mshahara wa juu kupita Wachezaji wengine hapo Man United.
Kwa sasa Rio Ferdinand, anaepata Pauni 110,000 kwa wiki, ndie anaelipwa juu zaidi.
Marseille watwaa Ubingwa Ufaransa
Marseille waliwafunga Rennes bao 3-1 na kutwaa Ubingwa wa Ufaransa na hii ni mara ya kwanza kuwa Bingwa tangu mwaka 1992.
Huku Ligue 1 ikiwa imabekisha mechi mbili kumalizika, Marseille wako pointi 8 mbele na hakuna Timu inayoweza kuwakamata.
Marseille ina Wachezaji wengi kutoka Afrika wakiwemo Mamadou Niang kutoka Senegal, Taye Taiwo kutoka Nigeria, Souleymane Diawara toka Senegal, Charles Kabore wa Burkina Faso , Stephane Mbia wa Cameroun na Bakari Kone wa Ivory Coast.
Tottenham washinda Fainali ya Nafasi ya 4
Man City 0 Spurs 1
Peter Crouch aliwapa furaha Tottenham alipofunga bao dakika ya 82 na kuwapa ile nafasi ya nne ya kucheza Ulaya Msimu ujao na kuwatosa Man City.
Katika mechi nyingine ya Ligi Fulham walifungwa 1-0 na Stoke City.

Wednesday, 5 May 2010

Bayern kwenda kwa Pilato kwa ajili ya Ribery
Bayern Munich imesema itakata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi katika Michezo, CAS [Court for Arbitration for Sports] baada ya UEFA kuitupilia mbali rufaa yao kupinga kufungiwa kwa Mchezaji wao Franck Ribery mechi 3 ikimaanisha ataikosa Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ambayo Bayern Munich watakutana na Inter Milan Uwanjani Santiago Bernabeau Mei 22.
Ribery alipewa Kadi Nyekundu kwenye mechi ya Bayern v Lyon ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI alipomtimba Straika wa Lyon Lisandro na UEFA ikamwongezea adhabu ya kifungo cha mechi 3.
Chamakh ahesabu siku za kutua Ze Gunners
Straika kutoka Morocco ambae anachezea Bordeaux ya Ufaransa, Marouane Chamakh, amesema sasa anahesabu siku tu ili uhamisho wake kwenda Arsenal uwe rasmi.
Chamakh, miaka 26, anategemewa kusaini Mkataba na Arsenal utakaompa Mshahara wa Pauni Elfu 50 kwa wiki.
Mchezaji huyo ambae ameifungia Bordeaux bao 15 Msimu huu amesema: “Nahesabu siku, ni siku 11! Napatwa na mawazo mengi kwani nimekuwa hapa Bordeaux miaka 10! Lakini nina furaha kwenda Arsenal, wanacheza soka tamu!”
Uhamisho wa Chamakh kwenda Arsenal ni wa bure kwa vile Mchezaji huyo anamaliza Mkataba wake na Bordeaux mwishoni mwa Msimu huu utakaomalizaka wiki ijayo.
Fergie kutembeza shoka United
Kuna taarifa toka Manchester United kuwa Meneja wao, Sir Alex Ferguson, ameidhinisha Wachezaji wawili wauzwe ili kuleta msukumo mpya ndani ya Klabu na inadhaniwa Wachezaji hao ni Dimitar Berbatov na Kipa Ben Foster.
Ferguson akiongea na TV ya Man United, MUTV, amesema: “Inabidi uchukue uamuzi ili kuimarisha Timu. Ukiwa unapigania Vikombe vinne kwa Msimu mmoja lazima ujue wakati upi wa kuimarisha Timu.”
Hata hivyo Ferguson hakutaja Wachezaji gani watapelekwa sokoni ila alichosema ni kuwa hamna mabadiliko makubwa kwa sababu Timu inao Chipukizi wengi.
Ferguson ametamka: “Watu hawatambui tumesaini Wachezaji watatu wadogo kwa Pauni Milioni 20 tu! Nao ni Chris Smalling toka Fulham, Mame Diouf na Javier Hernandez toka Mexico.”
Ferguson alikumbushia pia Timu yake inao Chipukizi wengi ambao watakuwepo kwa muda mrefu na aliwataja hao kuwa ni Jonny Evans, Federico Macheda, Gabriel Obertan, Danny Welbeck na Darron Gibson.
Matamshi ya Ferguson yanafuatia kauli za Mkurugenzi Mtendaji wa Man United, David Gill, aliethibitisha Klabu itasajili Wachezaji wapya.
Gill alitamka: “Naweza kukutazama moja kwa moja machoni na kukwambia tunazo fedha kibao za kununua Wachezaji. Tushaongea na Meneja Ferguson na tunajua nani tunamtaka lakini si tabia yetu kuzungumzia majina!”
LEO NI FAINALI NAFASI YA 4!!!
Leo saa 4 usiku, saa za bongo, Uwanja wa City of Manchester utazikutanisha Timu za Manchester City na Tottenham Hotspurs zinazogombea ile nafasi lulu, nafasi ya 4 kwenye Msimamo wa Ligi Kuu, ili kuungana na Timu 3 za juu, Chelsea, Manchester United na Arsenal, kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Hadi sasa nafasi hiyo ya 4 imekaliwa na Tottenham wenye pointi 67 na Man City wako nafasi ya 5 wakiwa na pointi 66 na Timu zote hizi zimecheza mechi 36 na wakikutana leo watabakisha mechi moja.
Tottenham wakishinda leo watajihakikishia nafasi hiyo ya 4 lakini wakishinda Man City itabidi Timu hizo zisubiri hadi mechi za mwisho Jumapili ili ipatikane Timu ya 4.
Tottenham wana rekodi nzuri kwa Man City kwani katika mechi ya kwanza ya Ligi waliifunga City bao 3-0.
Msimu uliokwisha Tottenham walishinda mechi zote mbili za Ligi kwa bao 2-1 kila mechi.
Katika mechi ya leo kila Timu itamkosa Kipa nambari wani ambao wameumia na Man City watamchezesha Kipa wa ‘kuazima’ kutoka Sunderland, Martin Fulop.
Kipa wa Tottenham anategemewa kuwa Ben Alnwick kufuatia kuumia kwa Kipa Mbrazil Heurelho Gomes.
Vikosi vinategemewa kuwa:
Manchester City (Fomesheni 4-4-2): Fulop; Zabaleta, Toure, Kompany, Bridge; A Johnson, De Jong, Vieira, Bellamy; Adebayor, Tévez.
Tottenham Hotspur (Fomesheni 4-4-1-1): Gomes; Kaboul, Dawson, King, Assou-Ekotto; Bentley, Huddlestone, Bale; Modric; Crouch.
Refa: Steve Bennett
Fergie: Sijuti wala sikasiriki!
Sir Alex Ferguson ametamka hawezi kukaa chini ajute au kukasirika wapi Manchester United walifanya kosa na pengine kuwapa Ubingwa Chelsea Jumapili ijayo.
Jumapili Ligi Kuu inamalizika kwa Chelsea kucheza na Wigan na Manchester United kuikwaa Stoke City.
Ikiwa Chelsea wataifunga Wigan wao ni Mabingwa lakini wakishindwa hilo na Man United wakiifunga Stoke basi Man United watautetea Ubingwa wao.
Ferguson amesema: “Nilikuwa nautazama tena kila mchezo lakini huko ni kujitesa tu! Msimu ulipoanza tulifungwa na Biurnley tukakosa penalti mechi hiyo na hizo ni pointi 3 tumepoteza! Mechi zote na Chelsea Marefa waliwabeba!”
Ferguson amedokeza atafanya mabadiliko kwa ajili ya Msimu ujao na tayari ameshawachukua Wachezaji chipukizi Chris Smalling toka Fulham na Javier Hernandez  toka Mexico.

Tuesday, 4 May 2010

Liverpool kumong’onyoka?
Kufuatia Msimu mbovu na kutoambulia chochote kuna kila dalili Timu ya Liverpool huenda ikasarambatika na Watu kutimkia kila upande wakiongozwa na Meneja wao Rafa Benitez ambae ametamka kuwa wiki hii anakutana na Mwenyekiti wa Klabu Martin Broughton ili kuamua nini hatima yake.
Kuna uvumi mzito Benitez yuko njiani kwenda Juventus Msimu ukiisha.
Mbali ya Benitez kuna tetesi baadhi ya Wachezaji, kama vile Nahodha Steven Gerrard na Fernando Torres, wamo mbioni kuhama.
Lakini, ukiacha tetesi, Mchezaji ambae amesimama wazi na kutamka huenda akahama ni Yossi Benayoun ambae amesema hana uhakika kama atakuwepo Msimu ujao kwa vile ndani ya Klabu kuna utata.
Inasemekana Benayoun yuko mbioni kwenda Urusi kuchezea CSKA Moscow.
Utata wa Liverpool umeshamiri hasa pia kwa sababu Wamiliki wake Wamarekani wawili, George Gillet na Tom Hicks, wameshatundika bango la kuiuza Klabu ambayo imekabwa nna madeni kibao.
Blanc apewa ofa ya Umeneja Ufaransa
Laurent Blanc amepewa ofa na Chama cha Soka cha Ufaransa kuchukua nafasi ya Raymond Domenech ya kuwa Meneja wa Timu ya Taifa ya Ufaransa mara baada ya Fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Blanc, ambae alikuwa Nahodha wa Ufaransa ilipotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na aliewahi kuichezea Manchester United kati ya mwaka 2001 na 2003, hajathibitisha kukubali ofa hiyo kwa vile bado yumo kwenye kinyang’anyiro cha kutetea Ubingwa wao kwenye Ligue 1 akiwa na Klabu yake Bordeaux iliyobakisha mechi 4 kumaliza Msimu.
Kocha wa sasa wa Ufaransa, Domenech, ataondoka kwa hiari baada ya Kombe la Dunia kumalizika.

Monday, 3 May 2010

Ze Gunners yapigwa!!
Blackburn 2 Arsenal 1
Huko Ewood Park, kwenye mechi ya Ligi Kuu, Blackburn Rovers wamewafunga Arsenal kwa bao 2-1 katika mechi ya pili na ya mwisho ya Ligi kwa leo.
Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kufunga kupitia Robin van Persie na Blackburn wakasawazisha Mfungaji akiwa David Dunn.
Bao la ushindi la Blackburn liliingizwa na Beki Chris Samba kufuatia kona.
Hiki ni kipigo cha 3 kwa Arsenal katika mechi zao nne za mwisho za Ligi lakini bado yuko nafasi ya 3.
Timu hizi zimebakisha mechi moja ili kumaliza Ligi Jumapili ijayo.
Hull City rasmi wameshuka Daraja!!!
Wigan 2 Hull City 2
Sare ya 2-2 na Wigan katika mechi ya Ligi Kuu ya leo imehitimisha rasmi kushuka Daraja kwa Hull City na kuungana na Timu nyingine mbili, Portsmouth na Burnsley, kwenda kucheza Ligi ya Coca Cola Championship Msimu ujao.
Kwa sare ya leo, Hull City wamefikisha pointi 29 na Timu iliyo juu yao, West Ham, ina pointi 34 na mechi imebaki moja tu hivyo hawawezi kuwafikia West Ham.
Hull City waliongoza 2-1 hadi dakika za majeruhi na hivyo walikuwa wana uwezo, kimahesabu, kurefusha kutoshuka Daraja hadi mechi ya mwisho lakini bao la lala salama la Steve Gohouri wa Wigan la kusawazisha ndio liliwamaliza Hull City.
Katika mechi hii, Wigan walitangulia kupata bao kupitia Moses kwenye dakika ya 30 lakini Hull wakasawzisha dakika ya 42 kupitia Atkinson na Cullen akawafungia bao la pili dakika ya 64.
Ndipo kwenye dakika ya 93 Gohouri alipowakata maini Hull City kwa kusawazisha na kuwaporomosha chini.

Sunday, 2 May 2010

Fergie aizungumza Liverpool!!
Mara baada ya Liverpool kupigwa 2-0 kwao Anfield na Chelsea na hivyo kufuta matumaini ya Manchester United ya kutaka Chelsea watibuliwe, Sir Alex Ferguson alipohojiwa alisema: “Si kitu tulichokitaka-hiyo ni kweli! Nilidhani Liverpool wanaweza kufanya kitu. Lakini ni ngumu kutegemea wangewafunga Chelsea. Goli la kwanza? Inaweza kutokea na nina hakika Gerrard atajuta, lakini imetokea. Sisi inabidi tutimize wajibu wetu- na hilo ndio fahari na historia ya Klabu hii!! Hatuwezi kushinda kila kitu. Lakini tukiifunga Sunderland leo, kinyang’anyiro kitaenda hadi siku ya mwisho! Huo ndio ukweli.”
Ubingwa hadi Jumapili ijayo!!!!
Sunderland 0 Man United 1
Manchester United leo wamehakikisha vita vya Ubingwa kati yao na Chelsea vinaendelea hadi Jumapili ijayo wakati mechi za mwisho kabisa za Ligi Kuu zitapochezwa baada ya kuifunga Sunderland huko Stadium of Light kwa bao 1-0.
Kabla ya mechi hii ya Man United, hivi leo Chelsea waliwafunga Liverpool 2-0 na hivyo kuwa mbele ya Man United kwa pointi 4 na kama wangefungwa na Sunderland, leo hii Chelsea angekuwa Bingwa.
Bao la ushindi la Man United lilifungwa na Nani kwenye dakika ya 28.
Mechi za mwisho, Chelsea na Man United wote watachezea Viwanja vya nyumbani kwa Chelsea kuikaribisha Wigan Timu ambayo iliitandika Chelsea bao 3-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi na Man United kuwakaribisha Old Trafford vibonde wa Chelsea, Stoke City, waliokung’utwa goli 7-0 na Chelsea.
Ili kuwa Bingwa, Chelsea anahitaji kuifunga Wigan na akishindwa kufanya hilo na Man United wakaifunga Stoke City, Ubingwa utabaki Old Trafford.
Liverpool 0 Chelsea 2
-Zawadi toka kwa Gerrard yawasogezea Ze Bluzi Ubingwa!!!!!!
Chelsea leo wamejisafishia njia ya kuuchukua Ubingwa walipoifunga Liverpool bao 2-0 huko Anfield na hivyo kujikita kileleni wakiwa pointi 4 mbele ya Manchester United ambao watacheza na Sunderland muda si mrefu.
Chelsea wamebakisha mechi moja watakayocheza kwao Stamford Bridge Jumapili ijayo na Wigan Timu ambayo iliitwanga Chelsea bao 3-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu na ushindi dhidi ya Wigan utawapa Chelsea Ubingwa bila ya kujali Manchester United watapata matokeo gani katika mechi zao.
Bao la kwanza kwa Chelsea hivi leo lilikuwa zawadi nono toka kwa Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, ambae alirudisha pasi nyuma kizembe, au makusudi ikiwa ni Man United na unaamini mechi hii ni njama, na kumpasia Dider Drogba aliefunga kilaini dakika ya 33.
Bao la pili lilipachikwa Na Frank Lampard kwenye dakika ya 54.
Fulham 3 West Ham 2
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Fulham imeipiga West Ham kwa bao 3-2 na mabao ya Fulham yalifungwa na Clint Dempsey, Carlton Cole [kajifunga mwenyewe] na Stefano Okaka.
Mabao ya West Ham yalipachikwa na Carlton Cole na Guillermo Franco.
Powered By Blogger