Wednesday, 5 May 2010

Chamakh ahesabu siku za kutua Ze Gunners
Straika kutoka Morocco ambae anachezea Bordeaux ya Ufaransa, Marouane Chamakh, amesema sasa anahesabu siku tu ili uhamisho wake kwenda Arsenal uwe rasmi.
Chamakh, miaka 26, anategemewa kusaini Mkataba na Arsenal utakaompa Mshahara wa Pauni Elfu 50 kwa wiki.
Mchezaji huyo ambae ameifungia Bordeaux bao 15 Msimu huu amesema: “Nahesabu siku, ni siku 11! Napatwa na mawazo mengi kwani nimekuwa hapa Bordeaux miaka 10! Lakini nina furaha kwenda Arsenal, wanacheza soka tamu!”
Uhamisho wa Chamakh kwenda Arsenal ni wa bure kwa vile Mchezaji huyo anamaliza Mkataba wake na Bordeaux mwishoni mwa Msimu huu utakaomalizaka wiki ijayo.
Fergie kutembeza shoka United
Kuna taarifa toka Manchester United kuwa Meneja wao, Sir Alex Ferguson, ameidhinisha Wachezaji wawili wauzwe ili kuleta msukumo mpya ndani ya Klabu na inadhaniwa Wachezaji hao ni Dimitar Berbatov na Kipa Ben Foster.
Ferguson akiongea na TV ya Man United, MUTV, amesema: “Inabidi uchukue uamuzi ili kuimarisha Timu. Ukiwa unapigania Vikombe vinne kwa Msimu mmoja lazima ujue wakati upi wa kuimarisha Timu.”
Hata hivyo Ferguson hakutaja Wachezaji gani watapelekwa sokoni ila alichosema ni kuwa hamna mabadiliko makubwa kwa sababu Timu inao Chipukizi wengi.
Ferguson ametamka: “Watu hawatambui tumesaini Wachezaji watatu wadogo kwa Pauni Milioni 20 tu! Nao ni Chris Smalling toka Fulham, Mame Diouf na Javier Hernandez toka Mexico.”
Ferguson alikumbushia pia Timu yake inao Chipukizi wengi ambao watakuwepo kwa muda mrefu na aliwataja hao kuwa ni Jonny Evans, Federico Macheda, Gabriel Obertan, Danny Welbeck na Darron Gibson.
Matamshi ya Ferguson yanafuatia kauli za Mkurugenzi Mtendaji wa Man United, David Gill, aliethibitisha Klabu itasajili Wachezaji wapya.
Gill alitamka: “Naweza kukutazama moja kwa moja machoni na kukwambia tunazo fedha kibao za kununua Wachezaji. Tushaongea na Meneja Ferguson na tunajua nani tunamtaka lakini si tabia yetu kuzungumzia majina!”

No comments:

Powered By Blogger