Liverpool kumong’onyoka?
Kufuatia Msimu mbovu na kutoambulia chochote kuna kila dalili Timu ya Liverpool huenda ikasarambatika na Watu kutimkia kila upande wakiongozwa na Meneja wao Rafa Benitez ambae ametamka kuwa wiki hii anakutana na Mwenyekiti wa Klabu Martin Broughton ili kuamua nini hatima yake.
Kuna uvumi mzito Benitez yuko njiani kwenda Juventus Msimu ukiisha.
Mbali ya Benitez kuna tetesi baadhi ya Wachezaji, kama vile Nahodha Steven Gerrard na Fernando Torres, wamo mbioni kuhama.
Lakini, ukiacha tetesi, Mchezaji ambae amesimama wazi na kutamka huenda akahama ni Yossi Benayoun ambae amesema hana uhakika kama atakuwepo Msimu ujao kwa vile ndani ya Klabu kuna utata.
Inasemekana Benayoun yuko mbioni kwenda Urusi kuchezea CSKA Moscow.
Utata wa Liverpool umeshamiri hasa pia kwa sababu Wamiliki wake Wamarekani wawili, George Gillet na Tom Hicks, wameshatundika bango la kuiuza Klabu ambayo imekabwa nna madeni kibao.
Blanc apewa ofa ya Umeneja Ufaransa
Laurent Blanc amepewa ofa na Chama cha Soka cha Ufaransa kuchukua nafasi ya Raymond Domenech ya kuwa Meneja wa Timu ya Taifa ya Ufaransa mara baada ya Fainali za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Blanc, ambae alikuwa Nahodha wa Ufaransa ilipotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na aliewahi kuichezea Manchester United kati ya mwaka 2001 na 2003, hajathibitisha kukubali ofa hiyo kwa vile bado yumo kwenye kinyang’anyiro cha kutetea Ubingwa wao kwenye Ligue 1 akiwa na Klabu yake Bordeaux iliyobakisha mechi 4 kumaliza Msimu.
Kocha wa sasa wa Ufaransa, Domenech, ataondoka kwa hiari baada ya Kombe la Dunia kumalizika.
No comments:
Post a Comment