Nafasi ya pili imechukuliwa na Timu Kongwe Bayern Munich waliowafunga Vfb Stuttgart mabao 2-1. Licha ya kufungwa, Stuttgart wameshika nafasi ya 3 huku Hertha Berlin nafasi ya 4.
Mechi za leo za Bundesliga ndizo zilikuwa mechi za mwisho za msimu wa Ligi.
Saturday, 23 May 2009
Ronaldo de Lima [32] atafikishwa mbele ya Tume ya Michezo huko Sao Paulo, Brazil baada ya kugundulika alimfinya na kumvuta nywele Beki wa Botafogo aitwae Fahel [pichani].
Ronaldo,ambae aliwahi kuwa Mchezaji Bora Duniani mara 3 na alieiwezesha Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1994 na 2002, hakuonekana na Refa wa pambano hilo la Klabu ya Ronaldo iitwayo Corinthians waliocheza na Botafogo.
Lakini picha za video zilionyesha tukio hilo ambalo lilianza baada ya Beki wa Botafogo Fahel kumvuta jezi Ronaldo na kumchezea rafu na Ronaldo akalipiza kisasi kwa kumfinya na kumvuta nywele Fahel.
Mwendesha Mashtaka wa Tume hiyo ya Michezo Paulo Schmitt amesema ingawa Ronaldo ni supastaa lakini kwenye Tume hiyo kila mtu ni sawa.
Akipatikana na hatia Ronaldo atafungiwa mechi 3.
Lakini kitu cha kushangaza kabisa ni ile hatua ya Mchezaji wa Botafogo Fahel ambae alitendewa makosa hayo kusema yuko tayari kutoa ushahidi ili kumtetea Ronaldo.
Fahel amesema: 'Nadhani alichukizwa wakati ule!! Lakini kinachotokea uwanjani bora kiachwe uwanjani!'
Ronaldo alianza kucheza tena mwezi Machi mwaka huu akichezea Corinthians ya Brazil baada ya kukaa mwaka mmoja nje kwa kuwa majeruhi na tangu wakati huo ameifungia Corinthians mabao 10 hali iliyowafanya mashabiki wengi kumtaka Bosi wa Timu ya Taifa ya Brazil, Dunga, amrudishe tena Kikosini.
Hata hivyo, Dunga juzi aliteua Kikosi cha Brazil bila Ronaldo ambacho kitacheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia mwanzoni mwa Juni na baadae kusafiri hadi Afrika Kusini kucheza kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara [FIFA CONFEDERATION CUP] yanayoanza Juni 14.
Kiungo Boateng wa Hull City ashangazwa na zogo la Kikosi cha Man U watakachocheza nacho kesho!!!
George Boateng, Mchezaji Kiungo wa Hull City ambao kesho wanakutana na Manchester United KC Stadium nyumbani kwa Hull katika mechi ambayo inabidi washinde ili wajinusuru kushushwa Daraja, amesema anashangazwa sana na jinsi mzozo ulivyoibuka wa Kikosi kipi kichezeshwe na Manchester United hapo kesho.
Manchester United, baada ya kuuchukua Ubingwa wa LIGI KUU wiki iliyopita na kukabiliwa na Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE Jumatano ijayo watakapocheza Roma, Italia na Barcelona, wanategemewa kuwapumzisha mastaa wao kwenye mechi ya kesho isiyo na umuhimu wowote kwao.
Boateng anaamini Klabu zenyewe zilizo hatarini kushushwa ndio zijilaumu kwa kuwa katika hali hiyo na sio kutafuta visingizio. Anasema: 'Sir Alex Ferguson msimu wote amekuwa akibadilisha Kikosi chake na wameshinda mechi nyingi. Nilitazama ile Nusu Fainali ya FA CUP na Everton walipopumzisha mastaa wao wengi na wakatolewa kwa penalti na hakuna mtu alielaumu isipokuwa Mashabiki wa Man U waliotaka kwenda Fainali.'
Boateng aliongeza: 'Tunajua Hull City ni Timu ndogo na Nchi nzima inataka Klabu kubwa Newcastle inayoongozwa na Shujaa wa England Alan Shearer ibaki LIGI KUU. Ndio maana hizi kelele za visingizio vya ajabu!!'
Ligi ya Ujerumani inaisha leo jioni kwa Timu zote kucheza mechi zao za mwisho kuanzia saa 10 na nusu, bongo taimu, na, ingawa Wolfsburg yuko kileleni akiwa na pointi 66 nyuma yake ipo Timu Kongwe Bayern Munich na pia Vfb Stuttgart, waliofungana pointi 64 huku Hertha Berlin wakishika nafasi ya 4 wakiwa na pointi 63. Vinara Wolfburg wanahitaji suluhu tu wachukue Ubingwa huku Bayern Munich na Vfb Stuttgart, wanaokutana pamoja, inabidi kwanza wapate ushindi na pili waombee matokeo mabaya kwa Wolfsburg.
MECHI ZA LEO ZA VINARA:
Bayern Munich v VfB Stuttgart,
Wolfsburg v Werder Bremen,
Karlsruhe v Hertha Berlin,
CHELSEA YATOA TAMKO KUHUSU MASHTAKA YA UEFA!!
===YASIKITISHWA KUSHTAKIWA!!!
===MENEJA WAO HIDDINK ADAI UEFA IMENUFAIKA KWA FAINALI KUTOKUWA YA TIMU MBILI ZA ENGLAND!!
Klabu ya Chelsea imetoa tamko rasmi kufuatia hatua ya UEFA, Chama cha Soka Ulaya, kuwashitaki kama Klabu kwa kushindwa kudhibiti Wachezaji wake wasifanye utovu wa nidhamu na pia kushindwa kuwazuia Washabiki wake wasitupe vitu uwanjani huku Wachezaji wake Didier Drogba na Jose Bosingwa wakiwemo kwenye mashtaka kwa kutuhumiwa kumkashifu Refa Tom Henning Ovrebo kutoka Norway aliechezesha pambano lao la Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE dhidi ya Barcelona lililoisha 1-1 lakini Chelsea wakatupwa nje kwa goli la ugenini.
Taarifa ya Chelsea ilisema: ‘Chelsea itajibu tuhuma za UEFA leo kwa niaba ya Klabu na Wachezaji waliotuhumiwa. Tunapenda kuweka wazi, kama tulivyofanya wakati ule, matukio yale yanasikitisha na yalitokea tu baada ya kupandwa na munkari kufuatia kushindwa katika mazingara yenye utata katika mechi muhimu.’
Taarifa hiyo ilimaliza kwa kukumbusha kuwa Wachezaji wake Drogba na Bosingwa walishaomba msamaha kwa vitendo vyao.
Chelsea na Wachezaji wao wamepewa mpaka Ijumaa ijayo Mei 29 kutoa utetezi na UEFA itakaa Juni 17 kusikiliza kesi hiyo.
Wakati huohuo, Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, amekoleza moto katika sakata hilo la kushindwa Chelsea kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona na sasa kuzikutanisha Fainali Manchester United na Barcelona hapo Jumatano huko Roma, Italia.
Guus Hiddink amedai UEAFA inapata manufaa makubwa kwa Barcelona kucheza na Manchester United Fainali badala ya Timu mbili za England kukutana tena Fainali kama ilivyokuwa msimu uliopita huko Moscow, Urusi Chelsea walipotolewa na Manchester United.
Hiddink anasema: ‘Ni ngumu kusema kama kulikuwa na njama kwa sababu hatuna ushahidi!! Lakini mimi ni binadamu na nadhani UEFA, ingawa hawawezi kusema hilo, wana furaha kubwa hamna Fainali ya Timu za England tupu kwa mara ya pili!! Lakini kosa ni letu!! Tungefunga goli nyingi mechi ile!! Ila Refa Yule ni mzoefu ingawa ashawahi kuwa na matatizo hapo nyuma! Sijui nini kilimtokea usiku ule!!
Katika mechi hiyo kitu kilichowakera Chelsea ni kunyimwa penalti kadhaa za wazi.
RAFA: ‘ALONSO HAUZWI!!’
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, ameibuka na kung’ang;ania Kiungo wake Xabi Alonso atabaki Anfield baada ya Magazeti kadhaa huko England na Spain kubeba mabango kuwa Kiungo huyo yuko njiani kuelekea Real Madrid kufuatia kauli za Mgombea Urais wa Real Madrid Florentino Perez kudai atamsaini.
Msimu uliopita Xavi Alonso alikuwa bado kidogo auzwe kwani Liverpool ilionyesha nia ya wazi kabisa kutaka kumchukua Nahodha wa Aston Villa Greth Barry dili ambayo baadae ilikwama baada ya mvutano wa bei kati ya Klabu hizo mbili. Wakati huo, Xavi Alonso alikuwa majeruhi lakini alipopona, msimu huu, Alonso ameng’ara sana kwenye mechi alizochezea Liverpool.
Benitez amesema: ‘Xavi bado ana miaka mitatu kwenye mkataba wake na hatutaki kumuuza.’
UTATA KIKOSI CHA MAN U KITAKACHOPANGWA MECHI YA KESHO NA HULL CITY!!!!
===Ferguson alifikiria awapigie simu Mameneja wa Sunderland, Newcastle na Middlesbrough ili kuwapoza!!!!!
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amewahakikishia Mameneja wa Klabu za Sunderland, Newcastle na Middlesbrough kwamba siku ya Jumapili watakapocheza mechi ya mwisho ya LIGI KUU England huko KC Stadium na wenyeji Hull City atapanga Kikosi imara chenye uwezo wa kushinda mechi hiyo.
Huko England, huku Manchester United tayari keshaunasa Ubingwa wa LIGI KUU na Jumatano ana ‘BIGI MECHI’ na Barcelona ikiwa Fainali ya Ubingwa wa Ulaya, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu Kikosi kitakachopangwa na Ferguson kwenye mechi hiyo na Hull City ambayo inapigania kufa na kupona ishinde ili inusurike kushushwa Daraja wakati Timu za Sunderland, Newcastle na Middlesbrough zinaomba Hull City afungwe ili na wao wapone kushushwa Daraja.
Ili kupoza mjadala huo na kuwaondolea wasiwasi wahusika, Ferguson amesema: ‘Kitu muhimu tuwe na Ligi yenye uaminifu na uadilifu mkubwa duniani na sisi tutatimiza wajibu wetu Jumapili! Timu yeyote itayoshuka uwanjani itaiwakilisha Manchester United na kama kawaida sisi tutacheza tushinde tu! Mtu yeyote asiwe na wasiwasi kuhusu dhamira yetu safari hii!’
Ferguson akaongezea: ‘Nilifikiria niwapigie simu Mameneja watatu wahusika-Gareth Southgate [Middlesbrough], Ricky Sbragia [Sunderland] na Alan Shearer [Newcastle]. Lakini nikafikiria Ricky Sbragia alifanya kazi hapa Man U na anaijua Klabu hii na lazima atajua nini tutafanya! Southgate na Shearer mara nyingi sana washacheza na sisi na wanajua wazi Man U ikicheza inatafuta nini!!’
Lakini, Ferguson akakubali anaweza kupeleka Kikosi cha Wachezaji Chipukizi kama kile kilichocheza Wembley kwenye Nusu Fainali ya FA CUP na kutolewa kwa matuta na Everton ambacho baadhi ya Wachezaji wake walikuwa Darron Gibson, Federico Macheda na Danny Welbeck.
Ferguson akaongeza: ‘Ikiwa niliwaamini kucheza Nusu Fainali ya Kombe muhimu, kwa nini nisiwaamini kucheza mechi ya mwisho ya Ligi wakati tushachukua Ubingwa?’
Hata hivyo, Ferguson akamalizia kwa kuiponda FA: ‘Barcelona wamecheza mechi yao ya mwisho ya Ligi Jumamosi na sisi Jumapili! Timu ya England imeingia Fainali sasa mara ya 5 mfululizo, sidhani FA hawajui hilo! Ni rahisi kwao kuzipanga hizi mechi za mwisho za Ligi ziwe Jumamosi badala ya Jumapili. Hata ingekuwa Jumamosi, nisingepanga Kikosi changu chote bora ila labda Wachezaji wawili au watatu wangekuwemo!’
Friday, 22 May 2009
UEFA, Chama cha Soka Ulaya, kimeifungulia Chelsea na Wachezaji wake Didier Drogba na Jose Bosingwa mashitaka kufuatia utovu wa nidhamu ulioonyeshwa mara baada ya mechi ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyofanyika Stamford Bridge kati ya Chelsea na Barcelona matokeo yakiwa 1-1 lakini Barcelona akaingia Fainali kwa goli la ugenini.
Chelsea kama Klabu imeshitakiwa kwa kosa la utovu wa nidhamu wa Wachezaji wake na kwa washabiki wake kutupa vitu uwanjani.
Wachezaji Didier Drogba na Jose Bosingwa wameshitakiwa kwa kumkashifu Refa Tom Henning Ovrebo kutoka Norway.
Washtakiwa wote wanatakiwa wajibu tuhuma hizo ifikapo 29 Mei 2009 na UEFA itatoa uamuzi Juni 17.
RATIBA YA MECHI ZA JUMAPILI 24 Mei 2009 [saa 12 jioni saa za bongo]
Arsenal v Stoke
Aston Villa v Newcastle
Blackburn v West Brom
Fulham v Everton
Hull v Man U
Liverpool v Tottenham
Man City v Bolton
Sunderland v Chelsea
West Ham v Middlesbrough
Wigan v Portsmouth
Ronaldo: 'Sijali kinachotokea Real Madrid!!'
Mshambuliaji wa Manchester United, Cristiano Ronaldo, amesema yanayotokea Real Madrid hayamuhusu kwani yeye ni Mchezaji wa Manchester United na anachokijali ni nini kinachotokea Manchester United tu.
Ronaldo, ambae ndie Mchezaji Bora Duniani, amesema: 'Kwa sasa ninafikiria Fainali ya Jumatano ya Ubingwa wa Ulaya!! Sijali chochote kitatokea Real Madrid, ninachojali ni nini kitatokea Man U!!'
Kila mara, hasa mwishoni mwa msimu, huwa kunazuka stori kutoka Spain kuwa Ronaldo ataenda Real Madrid na safari hii zimeanza kwani ni ajenda kubwa ya Wagombea Urais wa Real Madrid. Uchaguzi wa Rais wa Klabu hiyo ya Spain, ambao ni kawaida wagombea wake kutoa ahadi kibao, utafanyika hivi karibuni.
Ronaldo pia akazikandya taarifa kuwa yeye na Lionel Messi wana mgongano mkubwa binafsi hasa kwa vile Timu zao Manchester United na Barcelona zinakutana Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE huko Roma, Italia Jumatano ijayo.
'Ni vita kati ya Timu mbili.' Ronaldo anasema. 'Bila ya Timu yangu sishindi na Messi bila ya Timu yake hashindi!!'
Fabregas apona adhabu ya kutema mate!!!
Kuna taarifa zisizo rasmi kuwa FA, Chama cha Soka cha England, kimetupilia mbali mashtaka ya Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, kumtemea mate Meneja Msaidizi wa Hull City, Brian Horton, mara naada ya mechi ya Kombe la FA kati ya Arsenal na Hull City ambayo Arsenal walishinda 2-1.
Fabregas hakucheza mechi hiyo kwa kuwa alikuwa majeruhi na inadaiwa akiwa amevaa kiraia aliingia uwanjani kuwapongeza wenzake na Wachezaji walipokuwa wakielekea Vyumba vya Kubadilishia Jezi, Fabregas alimtemea mate Brian Horton.
Lampard MCHEZAJI BORA CHELSEA MSIMU HUU!!!
Frank Lampard, Kiungo stadi wa Chelsea, ameshinda Tuzo ya MCHEZAJI BORA wa Chelsea kwa msimu wa mwaka 2008/9, hii ikiwa ni mara yake ya 3 mfululizo kushinda Tuzo hiyo.
Tuzo hii huendeshwa na Klabu ya Chelsea na wapigaji kura ni Mashabiki wa Chelsea.
Ronaldo na Ronaldinho nje Timu ya Taifa ya Brazil!!!
Wachezaji wa siku nyingi wa Brazil Ronaldo na Ronaldinho wameachwa katika uteuzi wa Timu ya Taifa ya Brazil itakayocheza mechi za mchujo za Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini kuwania kucheza Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 na yale Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara [Confedreation Cup] ambalo litachezwa mwezi ujao huko Afrika Kusini na litashindanisha Timu za Taifa Bingwa wa kila Bara Duniani pamoja na Bingwa wa Dunia, Italia, na Mwenyeji, Afrika Kusini.
Ronaldo, ambae hajaichezea Timu ya Taifa ya Brazil tangu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006, hivi karibuni amerudi uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu akichezea Klabu yake Corinthians Nchini Brazil.
Katika mchujo wa kuwania kuingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini 2010, Brazil watacheza na Uruguay Juni 6 na siku nne baadae watapambana na Paraguay, Nchi ambayo mpaka sasa ndio inayoongoza Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini.
Mara baada ya mechi hizo mbili, Brazil wataelekea Afrika Kusini kushindana Kombe la Mabara.
Kocha wa Brazil, Dunga, ameteua Wachezaji wapya watatu ambao ni Kipa Viktor kutoka Klabu ya Gremio, Mlinzi Andres Santos na Kiungo Ramires wote wakicheza soka lao huko huko Brazil.
Vile vile amemchukua Kipa wa Tottenham, Gomes, ili kuwa Kipa namba mbili kuziba pengo la Kipa Doni wa AS Roma ambae ni majeruhi. Kipa nambari moja ni Julio Cesar anaedakia Juventus.
Dunga amesema amemtema Ronaldinho ili kumpa muda zaidi wa kurudi kwenye fomu kwa vile mpaka sasa hana namba ya kudumu Klabuni kwake AC Milan. Dunga pia ametoa sababu hiyo hiyo kwa Ronaldo.
Brazil mpaka sasa wako nafasi ya pili katika Kundi la Nchi 10 za Marekani ya Kusini, nyuma ya Paraguay, baada ya mechi 12 na kila Nchi itacheza jumla ya mechi 18. Timu 4 za juu zitaingia moja kwa moja Fainali ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na Timu ya 5 itakwenda kucheza na Timu ya 4 ya Kundi la Nchi za CONCACAF ili kupata Timu moja itakayoingia Fainali.
Kikosi kamili cha Brazil tutawaletea baadae.
Thursday, 21 May 2009
Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis, amesisitiza Meneja wao Arsene Wenger lazima atabaki Emirates Stadium na kauli hii inafuatia ile ya Wenger mwenyewe hapo jana alipotamka hamna ishu ya yeye kuondoka.
Wenger amekuwa akihusishwa kuhamia Real Madrid baada ya misimu minne kupita huku Arsenal ikiambulia patupu na kutoka bila Kombe lolote. Hali hii imezua manung’uniko toka kwa Wadau na Washabiki wa Klabu.
Gazidis amethibitisha Wenger atabakia na mkataba wake utakapoisha 2011 ataongezewa.
Bosi wa LIGI KUU atetea Klabu kubadilisha Vikosi vyao!!!
Bosi wa LIGI KUU England, Richard Scudamore, amesisitiza Timu ya Manchester United ikiongozwa naSir Alex Ferguson wana kila haki ya kukishusha uwanjani Kikosi chenye Wachezaji wowote wale waliosajiliwa katika mechi yao ya mwisho ya LIGI KUU wakatakapoumana na Hull City Jumapili ijayo.
Wakati mechi hii haina umuhimu wowote kwa Manchester United kwani washatwaa Ubingwa wa LIGI KUU, kwa Hull City mechi hii ni ya kufa na kupona ili kujinusuru kushushwa Daraja.
Timu nyingne ambazo zinaitolea macho mechi hii ni Newcastle na Middlesbrough ambao wanaomba Hull City afungwe ili nao wanusurike kushushwa Daraja.
Manchester United wiki ijayo Jumatano huko Roma, Italia watavaana na Barcelona kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambayo Man U wanataka kuwa Timu ya kwanza kabisa kutetea vyema taji lake kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE. Hivyo, Wadau wengi wanaona ni busara kubwa kwa Manchester United kuwapumzisha Mastaa kama Ronaldo, Rooney, Vidic, Van Der Sar na kadhalika katika mechi ‘uchwara’ ya LIGI KUU ya Jumapili ambao wao tayari wameshautwaa Ubingwa.
Richard Scudamore, Mkurugenzi Mtendaji wa LIGI KUU, anaelezea: ‘Lazima tuwe wakweli! Wao washashinda LIGI KUU na Jumatano wana mechi kubwa na Barcelona! Wana Kikosi kikubwa cha Wachezaji wengi sasa kuna ubaya gani kubadilisha Timu? Wao wakishusha Timu yeyote lazima watakuwa wanaamini itashinda!!’
RIO: 'NTACHEZA FAINALI NA BARCELONA!!!'
Beki mahiri wa Manchester United, Rio Ferdinand, ambae yuko nje ya uwanja kwa karibu mwezi sasa baada ya kuumia kwenye mechi kule Emirates Stadium Manchester United ilipoitoa Arsenal 3-1 kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, amesema ana imani kubwa atakuwa fiti kucheza Fainali ya Kombe hilo Jumatano ijayo huko Roma, Italia dhidi ya Mabingwa wa Spain, Barcelona.
Jana, Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, alionyesha wasiwasi kuwa huenda Rio akaikosa Fainali hiyo na kudokeza ikiwa atafanya mazoezi vizuri basi inabidi acheze mechi ya LIGI KUU Jumapili na Hull City ili kujipa mazoezi.
Rio Ferdinad alizungumza: ‘Nipo fiti. Nishaanza mazoezi makali. Na Meneja akinichagua ntacheza Jumapili. Sina wasiwasi niko fiti kucheza Fainali na Barcelona.’
Shakhtar Donetsk 2 Werder Bremen 1
Bao la muda wa nyongeza la Rodrigues Jadson liliwalaza Werder Bremen ya Ujerumani na kuhakikisha Shakhtar Donetsk ya Ukraine wanaondoka na Kombe la UEFA ambalo ni la mwisho kushindaniwa kwani msimu ujao mashindano haya yataitwa UEFA EUROPA LEAGUE. Fainali hii ilichezwa Istanbul, Uturuki Uwanja wa Sukru Saracoglu ambao ni mali ya Klabu maarufu ya huko Uturuki Fernebahce.
Luiz Adriano aliifungia Shakhtar bao la kwanza dakika ya 25 lakini Werder Bremen wakasawazisha kabla ya hafutaimu mfungaji akiwa Ronaldo Naldo kwa frikiki ya mbali ambayo Kipa wa Shaktar Andriy Pyatov aliisindikiza wavuni.
Timu hizi zilikuwa 1-1 hadi mwisho wa dakika 90 ndipo ukaingia muda wa nyongeza wa dakika 30 na dakika 7 tu toka muda wa nyongeza uanze Shakhtar wakapata bao lao la ushindi.
Vikosi vilikuwa:
Shakhtar Donetsk: Pyatov, Srna, Kucher, Chigrinsky, Rat, Lewandowski, Fernandinho, Ilsinho (Gai 99), Jadson (Duljaj 112), Willian , Luiz Adriano (Gladkyy 89). Akiba hawakucheza: Khudzamov, Ischenko, Chyzhov, Moreno.
Kadi: Srna, Lewandowski, Ilsinho.
Magoli: Luiz Adriano 25, Jadson 97.
Werder Bremen: Wiese, Fritz (Pasanen 94), Prodl, Naldo, Boenisch, Niemeyer (Tziolis 103), Frings, Baumann, Ozil, Pizarro, Rosenberg (Hunt 78). Akiba hawakucheza: Vander, Tosic, Vranjes, Harnik.
Kadi: Frings, Fritz, Tziolis, Boenisch.
Goli: Naldo 35.
Watazamaji: 53,100.
Refa: Luis Medina Cantalejo (Spain).
Wednesday, 20 May 2009
Wenger asisitiza atabaki Arsenal!!!!
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesisitiza atabaki Arsenal kufuatia minong'ono kuwa anataka kuhamia Real Madrid.
Kufuatia kutokushinda Kombe lolote kwa miaka minne sasa na manung'uniko ya Wadau wa Arsenal na pia kauli yake mwenyewe Wenger kuwa anavutiwa kwenda Real Madrid, dhana ya kuwa mwisho wa utawala wa Wenger wa miaka 13 Arsenal umewadia ilitawala Emirates kwa siku kadhaa.
Lakini baada ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis, Wenger amethibitisha anabaki Arsenal.
Wenger, baada ya mkutano huo, alisema kwa ufupi: 'Hamna haja ya kuwa na wasiwasi, hii si ishu kwangu. Mie nabaki hapa.'
Wakati Wenger asisitiza kubaki, Mchezaji wake Adebayor ataka kung'oka!!!!!
Wakala wa Mshambuliaji wa Arsenal Emmanuel Adebayor, Stephane Courbis, ametoa tamko kuwa mwishoni mwa msimu watafanya mazungumzo na Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ili kujua nini hatima ya Mchezaji huyo.
Baada ya kupondwa na washabiki wengi wa Arsenal, inasemekana Adebayor amekerwa na anataka kuhama na wengi wa Washabiki hao wanakumbuka kwa kero kubwa kwamba msimu uliopita ilibaki kidogo tu Adebayor kuhamia AC Milan Klabu ambayo hadi leo inamtaka.
Ferguson anaomba Rio apone!!! Wenger asema Defensi ya Man U ndio itawapa ushindi kwa Barcelona!!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amedai Beki wake mahiri Rio Ferdinand yuko kwenye hatihati ya kucheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona Jumatano ijayo na, ili kuthibitisha yuko fiti, inabidi acheze mechi ya LIGI KUU England Jumapili watakapokuwa ugenini KC Stadium kucheza na Hull City wanaogombea kufa na kupona wasishushwe Daraja.
Rio Ferdinand aliumia kwenye mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa Emirates Stadium na Manchester United kuwafunga Arsenal mabao 3-1. Baada ya hapo amekosa mechi 3 mfululizo.
Ferguson amesema: 'Rio anahitaji mechi ya mazoezi baada ya kutocheza wiki tatu!! Hii mechi na Hull City ni muhimu kwake.'
Akizungumzia Fainali na Barcelona, Ferguson amesema itakuwa mechi ya wazi kwani Timu zote huwa zinapenda kushambulia. Ferguson aliongeza: 'Kila Klabu ina staili yake. Barca wana yao sisi tuna yetu. Ukitazama Wachezaji walioko Barca na wale ambao tunao bila shaka itakuwa Fainali murua!!!'
Nae Arsene Wenger wa Arsenal amesema anaamini uchezaji wa Defensi ya Manchester United ndio utakaoamua kama Man U wanaweza kulitetea Kombe hilo.
Wenger amesema anategemea mechi kati ya Manchester United na Barcelona itakuwa na mfumo na mtindo ule ule kama ulivyoonekana kwenye mechi ya LIGI KUU Jumamosi iliyopita Old Trafford kati ya Manchester United na Arsenal ambayo ilikuwa 0-0 na Man U kuutwaa Ubingwa wa LIGI KUU.
Wenger anasema: 'Tulimiliki mipira mingi na wao walitegemea mashambulizi ya kushtukiza. Hii ndio itakuwa hivyo siku ya Barcelona.'
Golikipa nambari wani wa England, David James, miaka 38, anaedakia Portsmouth amefanyiwa operesheni ya bega na hivyo atazikosa mechi za England za mchujo kuwania nafasi ya kwenda Afrika Kusini mwaka 2010 kwenye Fainali za Kombe la Dunia za mwezi Juni ambapo England watacheza na Kazakhstan na Andorra. Kipa nambari mbili wa England ni Yule Kipa rizevu wa Manchester United, Ben Foster, ambae pia imetangazwa anahitaji operesheni kurekebisha kidole gumba na atazikosa mechi za Klabu yake ile ya mwisho ya LIGI KUU Jumapili na Hull City na Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona. Hivyo Ben Foster nae atazikosa mechi za mwezi ujao za England.
Sasa nafasi iko wazi kwa Kipa wa West Ham Robert Green na hata Kipa wa zamani wa England Paul Robinson wa Blackburn kushika hatamu. Wengine wanaonyatia nafasi hiyo ni Chris Kirkland wa Wigan na Joe Hart wa Manchester City
Wakala wa Mchezaji Antonio Valencia athibitisha Real Madrid wametoa ofa!!!
Mchezaji kutoka Ecuador anaechezea Wigan, Antonio Valencia, inasemekana anatakiwa na Real Madrid na Klabu hiyo ya Spain imeshatoa ofa rasmi ili kumchukua.
Habari hizo zimethibitishwa na Wakala wake, Diego Herrera, na sasa Wigan wanasubiri ofa toka Klabu nyingine ili kumnadi kwa bei poa.
Mwenyekiti Arsenal adai Wenger atabaki Arsenal!!!
Kufuatia utata uliozuka baada ya mgongano kati ya Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, na baadhi ya Wadau wenye hisa Klabuni hapo kwenye mkutano wa hadhara kati ya Wadau na Menejimenti wiki iliyokwisha ambapo Wadau hao walihoji na kumkandya Wenger hasa kwa vile Arsenal haijachukua Kombe lolote tangu mwaka 2005, Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood, imebidi aibuke na kutuliza ngoma.
Mzozo huo ulifuatiwa na taarifa zilizogaa kuwa Mgombea Urais wa Real Madrid, Florentino Perez, ambae inasemekana ana uhusiano mzuri na Wenger, ametoa ahadi kuwa akichaguliwa Rais basi Arsene Wenger atatua Santiago Bernabeue.
Habari hizo zikashika mizizi pale Arsene Wenger mwenyewe kuhojiwa na TV Stesheni moja kutoka huko Ufaransa na kukiri kuwa kuhamia Real Madrid kuna mvuto na huko kuna mradi mkubwa.
Mwenyekiti Hill-Wood amewaponda Wadau hao, ambao wengine walidiriki kuhoji hata mbinu za Uchezaji anazotumia Wenger, kwa kuwaambia vitendo hivyo ni makosa na kuhujumu Timu.
Hata hivyo Hill-Wood amethibitisha Wenger ana mkataba na Arsenal hadi 2011 na hategemei kuwa ataondoka.
Beki Cannavaro ahama Real na kurudi Klabu yake ya zamani Juventus!!!
Nahodha wa Timu ya Taifa ya Italia, Fabio Cannavaro, miaka 35, amehama Real Madrid na kurudi kwao Italia kuchezea Juventus kwa mkataba wa mwaka mmoja. Cannavaro alienda Real mwaka 2006 na sasa ataichezea Juventus kuanzia Julai 1, 2009.
Cannavaro, aliyekuwa Mchezaji Bora wa Dunia mwaka 2006, aliihama Klabu ya Juventus mwaka huo huo mara tu baada ya Klabu hiyo kushushwa Daraja baada ya kubainika ilishiriki kwenye njama za kupanga matokeo na Mashabiki wa Juventus walikasirika kwa kuhama kwake. Kurudi kwa Cannavaro Juventus kumetangazwa siku moja tu baada ya kufukuzwa kazi Meneja Claudio Ranieri.
Kikosi cha Man U kitakachocheza na Hull City LIGI KUU Jumapili ijayo chazua mjadala mkali England!!!!
Sir Alex Ferguson ametoa fununu kuwa Kikosi cha Manchester United kitakachocheza mechi ya mwisho ya LIGI KUU England na Hull City Jumapili ijayo, mechi ambayo haina umuhimu wowote kwa Man U kwani kisha uchukua Ubingwa lakini ni ya kufa na kupona kwa Hull City, kitakuwa cha mchanganyiko.
Hull City watawakaribisha Man U KC Stadium huku wakitaka ushindi ili kuepuka kushushwa Daraja na wakati huohuo kuwakandamiza Newcastle na Middlesbrough kuungana na West Bromwich ambao tayari washashushwa Daraja.
Phil Brown, Meneja wa Hull City, amesema: 'Sidhani kama Ferguson atatusaidia!! Ni kweli siku tatu baadae atakuwa na Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona na akili yake yote iko huko lakini ukweli ni kwamba Manchester United wana Kikosi Bora LIGI KUU na wanaweza kuchagua Timu mbili tofauti na kushinda mechi yeyote ile!!! Si rahisi kwetu ni kazi ngumu!!!!'
Baadhi ya watu wameuhusisha uhusiano mzuri wa Sir Alex Ferguson na Phil Brown kuwa huenda ukamsaidia tena Phil Brown na wametaja jinsi Ferguson alivyomsaidia Brown kupata kazi ya Umeneja huko Derby County mwaka 2005.
Alan Shearer, Meneja wa Newcastle, Timu ambayo inagombea kunusurika kushushwa na huenda hatua ya Ferguson ya kuchezesha Kikosi hafifu inaweza kumuathiri, amesema: 'Ningependa Man U wasingekuwa na Fainali ile siku tatu baadae!! Lakini siwezi kumwambia chochote Ferguson!! Lakini hali kama hii ishatokeo hapo nyuma na Ferguson amekuwa mkweli kwani alitazama mazingara ya msimamo wa ligi na kuchagua Kikosi kilichomridhisha kila mtu!!! Huo ndio ubora wa Ferguson!!!'
Ferguson mwenyewe amesema: 'Hiki ni Kikosi bora nilichonacho!! Jumamosi na Arsenal ningeweza kuteua Timu mbili tofauti na Jumapili ijayo ntateua Timu inayostahili. Nina Kikosi cha Wachezaji 28 au 29 wakiwemo chipukizi Macheda, Webeck, Possebon na mapacha Da Silva. Najua ni vijana lakini ni Wachezaji wazuri sana!!!
Tuesday, 19 May 2009
- =HII NI FAINALI YA MWISHO UEFA CUP
- =MSIMU UJAO KUITWA 'UEFA EUROPA LEAGUE'
Kwenye Nusu Fainali Werder Bremen waliwabwaga wenzao wa Ujerumani Hamburg kwa goli la ugenini baada ya mechi zao mbili kumalizika kwa jumla ya bao 3-3.
Shakhtar Donetsk aliwatoa wenzao wa Ukraine Dynamo Kiev kwa jumla ya bao 3-2 kwenye mechi zao mbili za Nusu Fainali.
Pambano la kesho ni la kihistoria kwani hii ndio Fainali ya mwisho ya Kombe la UEFA baada ya kushindaniwa kwa miaka 38.
Kamati Kuu ya UEFA iliamua kuubadilisha mfumo wa Kombe hili kuanzia msimu ujao wa 2009/10 na pia kuupa jina jipya pamoja na Wadhamini wapya.
Mashindano haya ya UEFA CUP kuanzia msimu ujao yatachezwa kwa mtindo wa Makundi kwa mechi za nyumbani na ugenini ukifanana na mfumo wa UEFA CHAMPIONS LEAGUE. Jina jipya la mashindano hayo litakuwa 'UEFA EUROPA LEAGUE.'
Sunderland wafungwa na Portsmouth 3-1, bado mashakani kushushwa Daraja!!!!
Wakiwa ugenini Fratton Park, Sunderland walipata bao la utangulizi likifungwa na Kenwyne Jones dakika ya 59 lakini Portsmouth wakasawazisha dakika moja baadae kupitia Mnigeria John Utaka. Dakika ya 68 Beki wa Sunderland Bardsley akajifunga mwenyewe kuwapa uongozi Portsmouth na kosa kubwa alilofanya Anthon Ferdinand wa Sunderland, mdogo wake Rio Ferdinand wa Manchester United, liliwazawadia Portsmouth bao la 3 alilofunga Traore dakika ya 88.
Ingawa Sunderland wako nafasi ya 16 wakiwa na pointi 36 lakini wakifungwa mechi yao ya mwisho watashushwa ikiwa Newcastle na Hull City watashinda mechi zao za mwisho.
Ikiwa Newcastle watashinda na Hull City kutoka droo basi Sunderland [IKIWA HATOFUNGWA ZAIDI YA BAO 5] na Newcastle watapona na badala yake Hull City wataporomoka.
Ili Middlesbrough apone itabidi kwanza ashinde mechi yake na kuomba Hull City na Newcastle wafungwe lakini nani atashushwa kati ya Middlesbrough na Hull City itategemea Middlesbrough kafunga bao ngapi na Hull City kafungwa ngapi.
Hizo, kwa ufupi, ndizo hesabu kali za nani atasalimika kubaki LIGI KUU.
Msimamo kwa Timu za chini zilizo kwenye VITA KUU ya KUJINUSURU KUSHUSHWA DARAJA ni [West Bromwich tayari shashushwa]: [TIMU ZA NAFASI YA 18 HADI 20 HUSHUSHWA]
-Nafasi ya 16: Sunderland pointi 36
-Nafasi ya 17: Hull City pointi 35
-Nafasi ya 18: Newcastle pointi 34
-Nafasi ya 19: Middlesbrough pointi 32
-Nafasi ya 20: West Brom pointi 31
MECHI ZA MOTO ZA MWISHO KWA TIMU HIZI ZA CHINI JUMAPILI IJAYO 24 MEI 2009:
Aston Villa v Newcastle
Hull v Man U
Sunderland v Chelsea
West Ham v Middlesbrough
Monday, 18 May 2009
KITIMTIM KWA SUNDERLAND LEO: Portsmouth v Sunderland
- Sunderland watajinusuru kushuka Daraja leo??
Portsmouth na Sunderland leo saa 4 usiku, saa za bongo, wanavaana Uwanjani Fratton Park nyumbani kwa Portsmouth kwenye mechi ya LIGI KUU England ambayo haina umuhimu kwa Portsmouth kwani matokeo ya mechi za juzi na jana zimewaepusha kushuka Daraja lakini kwa Sunderland ni mechi ya kufa na kupona.
Sunderland, ambao wako pointi mbili juu ya zile Timu tatu za mwisho zilizo eneo la kuporomoka Daraja, wakishinda leo basi watajihakikishia kubaki LIGI KUU lakini wakifungwa au kutoka suluhu itabidi wasubiri hadi Jumapili ijayo kujua usalama wao wakati Timu zote za LIGI KUU zitacheza mechi za funga dimba za LIGI KUU msimu huu wa mwaka 2008/9.
Timu tatu za mwisho na ambazo ziko kwenye eneo la kuteremshwa Daraja ni Newcastle, Middlesbrough na ile ya mkiani, West Bromwich Albion, ambayo jana iliaga rasmi LIGI KUU baada ya kupigwa 2-0 na Liverpool.
Beki mahiri wa Mabingwa Manchester United, Nemanja Vidic, ametunukiwa Tuzo mbili Klabuni kwake Manchester United baada ya kushinda kura na kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Msimu anaechaguliwa na Wachezaji Wenzake na nyingine Mchezaji Bora wa Msimu anaechaguliwa na Washabiki.
Vidic, miaka 27, kutoka Nchi ya Serbia aliehamia Manchester United kutoka Spartak Moscow miaka mitatu iliyopita akishirikana na Beki mwenzake Rio Ferdinand, walipewa pongezi za dhati kwa kuweka ngome imara katika Chakula cha Usiku kilichotayarishwa ili kutoa Tuzo hizo.
Cristiano Ronaldo, Mshindi wa Tuzo hizo Msimu uliopita, safari hii alishinda Tuzo ya Goli la Mwaka kwa goli alilofunga kwenye mechi ya Man U na FC Porto ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE alipoachia kigongo cha mita kama 40.
RANIERI AFUKUZWA JUVENTUS!!!
Claudio Ranieri, aliewahi kuwa Meneja wa Chelsea, leo ametimuliwa kazi na Bodi ya Juventus baada ya kutoridhika na uongozi wake.
Ranieri alipewa kazi ya Umeneja Juventus Juni 2007 lakini hakuna mafanikio yeyote yaliyopatikana na huu ni msimu wa 7 sasa Juventus haijatwaa Ubingwa wa Italy na hata msimu huu, huku kukiwa kumaebaki mechi 2 ligi kwisha, wako nafasi ya 3 wakiwa mbele ya Fiorentina kwa pointi moja tu na wakipitwa watapoteza nafasi ya kuingia moja kwa moja ya Makundi ya kugombea UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu ujao.
Sunday, 17 May 2009
WEST BROMWICH TIMU YA KWANZA KUSHUSHWA LIGI KUU MSIMU HUU!!
- Wafungwa 2-0 na Liverpool!!!
- Almanusura Wachezaji wa Liverpool kutwangana uwanjani!!!!
West Bromwich Albion imeteremshwa Daraja na kurudishwa Daraja la chini liitwalo COCA COLA CHAMPIONSHIP baada ya kupigwa mabao 2-0 na Liverpool.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Steven Gerrard na Dirk Kuyt.
Mechi hii nusura iingie doa kubwa pale Wachezaji wa Liverpool Jamie Carragher na Alvaro Arbeloa walipovaana na kusukumana na ikabidi mwenzao Xabi Alonso aingilie kati kuamulia na pia Refa kuwaonya.
Mchezaji wa West Bromwich asimamishwa kwa tuhuma za kununua Madawa ya Kulevya!!
Mchezaji wa West Bromwich, Roman Bednar kutoka Czech, amesimamishwa na Klabu yake baada ya Gazeti liitwalo 'News of the World' kuandika ripoti kuwa walimfuma akinunua Madawa ya Kulevya.
Chelsea 2 Blackburn 0
Nicolas Anelka alifunga bao moja na kumtengenezea Florent Malouda kufunga bao la pili kayika mechi ya LIGI KUU England iliyochezwa Stamford Bridge ambayo ndiyo ya mwisho kwa Meneja wao Guus Hiidink uwanjani hapo kwani mwishoni mwa msimu anarudi kwenye kazi yake ya kudumu ya kuwa Meneja wa Timu ya Taifa ya Urusi.
STAA WA URENO FIGO KUSTAAFU SOKA!!!
Kiungo Luis Figo ametangaza kustaafu Soka mwishoni mwa msimu huu mara tu baada ya kuisaidia Klabu yake ya Inter Milan kunyakua Ubingwa wa Italia kwa mara ya 4 mfululizo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 ambae mwaka 2001 ndie alikuwa Mchezaji Bora Duniani alijitengenezea jina lake alipozichezea Barcelona na Real Madrid za Spain.
Figo alihama Barcelona na kwenda Real Madrid mwaka 2000 na mwaka 2002 alichukua Klabu Bingwa Ulaya akiwa na Real.
Mwaka 2005 akahamia Inter Milan ya Italia.
Figo ndie Mchezaji anaeshikilia rekodi ya kuchezea Timu ya Taifa ya Ureno mechi nyingi kwa kucheza mechi 127 na kufunga magoli 32.
Baada ya vita kati ya Manchester United na Liverpool kumalizika rasmi jana kwa Manchester United kuchukua Kombe la Ubingwa wa LIGI KUU England, sasa Liverpool yuko kwenye vita yake nyingine ya kuhakikisha anamaliza nafasi ya 2 mbele ya Chelsea. Liverpool yuko nafasi ya 2 na ana pointi 80 na Chelsea ni wa 3 akiwa na pointi 77 huku Timu zote zimebakisha mechi 2.
Leo Liverpool mgeni wa West Bromwich ambao wako kwenye balaa la kushushwa Daraja wakiwa wako mkiani na Chelsea yuko kwake Stamford Bridge kucheza na Blackburn ambayo matokeo ya mechi za jana yamemhakikishia yuko salama LIGI KUU.
RATIBA LIGI KUU ENGLAND-LEO NA KESHO:
Jumapili, 17 Mei 2009
[saa 9 na nusu mchana]
West Brom v Liverpool
[saa 12 jioni]
Chelsea v Blackburn
Jumatatu, 18 Mei 2009
[saa 4 usiku]
Portsmouth v Sunderland
MATOKEO KAMILI MECHI ZA JANA:
Jumamosi, 16 Mei 2009
Man U 0 v Arsenal 0
Bolton 1 v Hull 1
Everton 3 v West Ham 1
Middlesbrough 1 v Aston Villa 1
Newcastle 0 v Fulham 1
Stoke 2 v Wigan 0
Tottenham 2 v Man City 1
AC Milan afungwa, Inter Milan atwaa Ubingwa!!!
Baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Villareal, Real Madrid wameupeleka Ubingwa wa Spain kwa Watani wao wa Jadi Barcelona ambao jana hawakucheza.
Ubingwa huu ni wa 19 kwa Barcelona ambao wiki iliyopita pia walishinda Kombe la Mfalme Spain kwa kuifunga Atletic Bilbao 4-1.
Barcelona watacheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE hapo Mei 27 mjini Rome, Italia na Mabingwa wa Watetezi wa Ulaya Manchester United ambao jana walitwaa kwa mara ya 18 Ubingwa wa England.
Huko Italia, mambo yalikuwa kama Spain pale AC Milan, Klabu yenye uhasama na na Inter Milan, ilipopigwa 2-1 na Udinese hapo jana na kuwazawadia mahasimu wao Inter Milan Ubingwa wa Italia wa ligi ya Serie A bila ya Inter Milan kuwa na mechi jana.
Mara baada ya mechi hiyo ya Udinese na AC Milan kwisha, mashabiki wa Inter Milan [pichani] walifurika katikati ya jiji la Milan kusheherekea ushindi wao.
Inter Milan, wanaoongozwa na Meneja wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho, sasa wametwaa 'SCUDETTO' kwa mara ya 4 mfululizo.