Wednesday 20 May 2009

Refa atoka kifungoni, kuchezesha LIGI KUU England wikiendi!!!! Refa Mark Clattenburg, 34, ambae alisimamishwa mwezi Agosti mwaka jana na kuondolewa kuchezesha pambano la Ngao ya Hisani kati ya Manchester United na Portsmouth mwezi huo huo na kisha kufungiwa miezi minane kufuatia tuhuma Kampuni moja inayomhusu yeye ilikuwa na madeni mengi na hivyo huo ni ukiakwaji wa maadili kwa Marefa, amemaliza kifungo chake na atachezesha mechi yake ya kwanza ya LIGI KUU England siku ya Jumapili kati ya Manchester City na Bolton. Clattenburg ni Refa wa FIFA na huko England alionekana kama Refa mzuri kijana anaechipukia.
Wenger asisitiza atabaki Arsenal!!!!
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesisitiza atabaki Arsenal kufuatia minong'ono kuwa anataka kuhamia Real Madrid.
Kufuatia kutokushinda Kombe lolote kwa miaka minne sasa na manung'uniko ya Wadau wa Arsenal na pia kauli yake mwenyewe Wenger kuwa anavutiwa kwenda Real Madrid, dhana ya kuwa mwisho wa utawala wa Wenger wa miaka 13 Arsenal umewadia ilitawala Emirates kwa siku kadhaa.
Lakini baada ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis, Wenger amethibitisha anabaki Arsenal.
Wenger, baada ya mkutano huo, alisema kwa ufupi: 'Hamna haja ya kuwa na wasiwasi, hii si ishu kwangu. Mie nabaki hapa.'
Wakati Wenger asisitiza kubaki, Mchezaji wake Adebayor ataka kung'oka!!!!!
Wakala wa Mshambuliaji wa Arsenal Emmanuel Adebayor, Stephane Courbis, ametoa tamko kuwa mwishoni mwa msimu watafanya mazungumzo na Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ili kujua nini hatima ya Mchezaji huyo.
Baada ya kupondwa na washabiki wengi wa Arsenal, inasemekana Adebayor amekerwa na anataka kuhama na wengi wa Washabiki hao wanakumbuka kwa kero kubwa kwamba msimu uliopita ilibaki kidogo tu Adebayor kuhamia AC Milan Klabu ambayo hadi leo inamtaka.
Ferguson anaomba Rio apone!!! Wenger asema Defensi ya Man U ndio itawapa ushindi kwa Barcelona!!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amedai Beki wake mahiri Rio Ferdinand yuko kwenye hatihati ya kucheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona Jumatano ijayo na, ili kuthibitisha yuko fiti, inabidi acheze mechi ya LIGI KUU England Jumapili watakapokuwa ugenini KC Stadium kucheza na Hull City wanaogombea kufa na kupona wasishushwe Daraja.
Rio Ferdinand aliumia kwenye mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa Emirates Stadium na Manchester United kuwafunga Arsenal mabao 3-1. Baada ya hapo amekosa mechi 3 mfululizo.
Ferguson amesema: 'Rio anahitaji mechi ya mazoezi baada ya kutocheza wiki tatu!! Hii mechi na Hull City ni muhimu kwake.'
Akizungumzia Fainali na Barcelona, Ferguson amesema itakuwa mechi ya wazi kwani Timu zote huwa zinapenda kushambulia. Ferguson aliongeza: 'Kila Klabu ina staili yake. Barca wana yao sisi tuna yetu. Ukitazama Wachezaji walioko Barca na wale ambao tunao bila shaka itakuwa Fainali murua!!!'
Nae Arsene Wenger wa Arsenal amesema anaamini uchezaji wa Defensi ya Manchester United ndio utakaoamua kama Man U wanaweza kulitetea Kombe hilo.
Wenger amesema anategemea mechi kati ya Manchester United na Barcelona itakuwa na mfumo na mtindo ule ule kama ulivyoonekana kwenye mechi ya LIGI KUU Jumamosi iliyopita Old Trafford kati ya Manchester United na Arsenal ambayo ilikuwa 0-0 na Man U kuutwaa Ubingwa wa LIGI KUU.
Wenger anasema: 'Tulimiliki mipira mingi na wao walitegemea mashambulizi ya kushtukiza. Hii ndio itakuwa hivyo siku ya Barcelona.'

No comments:

Powered By Blogger