Friday 22 May 2009

LIGI KUU ENGLAND: TAMATI NI JUMAPILI!!!
LIGI KUU England inamalizika Jumapili huku Bingwa Manchester United tayari kavikwa Taji ila vita kubwa iiyobaki ni Timu ngapi mbili zinaungana na West Bromwich Albion kuporomoka na kucheza Daraja la chini la Coca Cola Championship msimu ujao. Timu zitakazocheza kufa na kupona hiyo Jumapili ili kuepuka kuungana na West Bromwich Albion kwenda Daraja la chini ni Sunderland, Hull City, Newcastle na Middlesbrough.
RATIBA YA MECHI ZA JUMAPILI 24 Mei 2009 [saa 12 jioni saa za bongo]
Arsenal v Stoke
Aston Villa v Newcastle
Blackburn v West Brom
Fulham v Everton
Hull v Man U
Liverpool v Tottenham
Man City v Bolton
Sunderland v Chelsea
West Ham v Middlesbrough
Wigan v Portsmouth
Ronaldo: 'Sijali kinachotokea Real Madrid!!'
Mshambuliaji wa Manchester United, Cristiano Ronaldo, amesema yanayotokea Real Madrid hayamuhusu kwani yeye ni Mchezaji wa Manchester United na anachokijali ni nini kinachotokea Manchester United tu.
Ronaldo, ambae ndie Mchezaji Bora Duniani, amesema: 'Kwa sasa ninafikiria Fainali ya Jumatano ya Ubingwa wa Ulaya!! Sijali chochote kitatokea Real Madrid, ninachojali ni nini kitatokea Man U!!'
Kila mara, hasa mwishoni mwa msimu, huwa kunazuka stori kutoka Spain kuwa Ronaldo ataenda Real Madrid na safari hii zimeanza kwani ni ajenda kubwa ya Wagombea Urais wa Real Madrid. Uchaguzi wa Rais wa Klabu hiyo ya Spain, ambao ni kawaida wagombea wake kutoa ahadi kibao, utafanyika hivi karibuni.
Ronaldo pia akazikandya taarifa kuwa yeye na Lionel Messi wana mgongano mkubwa binafsi hasa kwa vile Timu zao Manchester United na Barcelona zinakutana Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE huko Roma, Italia Jumatano ijayo.
'Ni vita kati ya Timu mbili.' Ronaldo anasema. 'Bila ya Timu yangu sishindi na Messi bila ya Timu yake hashindi!!'
Fabregas apona adhabu ya kutema mate!!!
Kuna taarifa zisizo rasmi kuwa FA, Chama cha Soka cha England, kimetupilia mbali mashtaka ya Nahodha wa Arsenal, Cesc Fabregas, kumtemea mate Meneja Msaidizi wa Hull City, Brian Horton, mara naada ya mechi ya Kombe la FA kati ya Arsenal na Hull City ambayo Arsenal walishinda 2-1.
Fabregas hakucheza mechi hiyo kwa kuwa alikuwa majeruhi na inadaiwa akiwa amevaa kiraia aliingia uwanjani kuwapongeza wenzake na Wachezaji walipokuwa wakielekea Vyumba vya Kubadilishia Jezi, Fabregas alimtemea mate Brian Horton.
Lampard MCHEZAJI BORA CHELSEA MSIMU HUU!!!
Frank Lampard, Kiungo stadi wa Chelsea, ameshinda Tuzo ya MCHEZAJI BORA wa Chelsea kwa msimu wa mwaka 2008/9, hii ikiwa ni mara yake ya 3 mfululizo kushinda Tuzo hiyo.
Tuzo hii huendeshwa na Klabu ya Chelsea na wapigaji kura ni Mashabiki wa Chelsea.
Ronaldo na Ronaldinho nje Timu ya Taifa ya Brazil!!!
Wachezaji wa siku nyingi wa Brazil Ronaldo na Ronaldinho wameachwa katika uteuzi wa Timu ya Taifa ya Brazil itakayocheza mechi za mchujo za Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini kuwania kucheza Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 na yale Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara [Confedreation Cup] ambalo litachezwa mwezi ujao huko Afrika Kusini na litashindanisha Timu za Taifa Bingwa wa kila Bara Duniani pamoja na Bingwa wa Dunia, Italia, na Mwenyeji, Afrika Kusini.
Ronaldo, ambae hajaichezea Timu ya Taifa ya Brazil tangu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006, hivi karibuni amerudi uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu akichezea Klabu yake Corinthians Nchini Brazil.
Katika mchujo wa kuwania kuingia Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini 2010, Brazil watacheza na Uruguay Juni 6 na siku nne baadae watapambana na Paraguay, Nchi ambayo mpaka sasa ndio inayoongoza Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini.
Mara baada ya mechi hizo mbili, Brazil wataelekea Afrika Kusini kushindana Kombe la Mabara.
Kocha wa Brazil, Dunga, ameteua Wachezaji wapya watatu ambao ni Kipa Viktor kutoka Klabu ya Gremio, Mlinzi Andres Santos na Kiungo Ramires wote wakicheza soka lao huko huko Brazil.
Vile vile amemchukua Kipa wa Tottenham, Gomes, ili kuwa Kipa namba mbili kuziba pengo la Kipa Doni wa AS Roma ambae ni majeruhi. Kipa nambari moja ni Julio Cesar anaedakia Juventus.
Dunga amesema amemtema Ronaldinho ili kumpa muda zaidi wa kurudi kwenye fomu kwa vile mpaka sasa hana namba ya kudumu Klabuni kwake AC Milan. Dunga pia ametoa sababu hiyo hiyo kwa Ronaldo.
Brazil mpaka sasa wako nafasi ya pili katika Kundi la Nchi 10 za Marekani ya Kusini, nyuma ya Paraguay, baada ya mechi 12 na kila Nchi itacheza jumla ya mechi 18. Timu 4 za juu zitaingia moja kwa moja Fainali ya Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na Timu ya 5 itakwenda kucheza na Timu ya 4 ya Kundi la Nchi za CONCACAF ili kupata Timu moja itakayoingia Fainali.
Kikosi kamili cha Brazil tutawaletea baadae.

No comments:

Powered By Blogger