Saturday 30 January 2010

NI FAINALI!!!!!!!
Egypt v Ghana
• Jumapili, Januari 31 Novemba 11 Stadium, Luanda, Angola saa 1 usiku [bongo taimu]
Misri, Mabingwa Watetezi wa Afrika, watakuwa wakicheza Fainali yao ya 3 mfululizo huku wakiwania kuweka rekodi ya kuwa Nchi ya kwanza kutwaa Taji la Afrika mara 3 mfululizo watakapopambana na Ghana.
Katika mechi 5 za Fainali hizi, Misri wamefunga jumla ya bao 14 na wamezitoa Timu ngumu za Cameroun, kwenye Robo Fainali, na Algeria kwenye Nusu Fainali.
Ghana ni Timu inayowakilishwa na Vijana wengi na wengi hawakuipa matumaini makubwa hasa baada ya injini yao Michael Essien kuumia na kujitoa kwenye Kikosi.
Hata hivyo wakiongozwa na Chipukizi kina Andre Ayew na Asamoah Gyan, Shujaa wao aliefunga goli moja moja za ushindi Robo Fainali na Nusu Fainali walipozibwaga Angola na Nigeria.
Kwenye Kundi lao, Ghana walifungwa na Ivory Coast 3-1 na kisha wakafunga Burkina Faso 1-0.
Wadau wanategemea Wachezaji Mohamed Zidan wa Misri anaecheza Borussia Dortmund ya Ujerumani na wa Ghana Andre Ayew wa Marseille ya Ufaransa kung’ara kwa Timu zao kwenye hiyo Fainali.
Makocha wote, Milovan Rajevac wa Ghana na Hassan Shehata wa Misri, wamekataa kuzungumzia lolote kuhusu Fainali hiyo.
VIKOSI VINATEGEMEWA KUWA:
Egypt [Fomesheni 3-5-2]
El Hadhary – Gomaa, Said, Fathallah – Mohammady, Fathi, Moawad, Hassan, Abd Rabo – Metab, Zidan
Ghana [Fomesheni 4-4-2]
Kingson - Inkoom, Sarpei, Addy, Vorsah - Agyeman-Badu, Draman, Kwadwo Asamoah, Gyan - Ayew, Agyemang
BIGI MECHI Jumapili: Arsenal v Man United
Ni mechi ambayo Sir Alex Ferguson wa Manchester United ameibatiza ‘mechi kubwa kwa msimu huu’ kwa vile Arsenal na Manchester United zipo kwenye kinyang’anyiro cha Ubingwa wa Ligi Kuu wakiwafukuza vinara Chelsea, lakini Arsene Wenger yeye anaamini matokeo yake si muhimu mno kuamua nani Bingwa kwa vile kila Timu itabaki kwenye kinyang’anyiro lolote linalokuwa.
Katika mzunguko wa kwanza huko Old Trafford, Manchester United waliifunga Arsenal 2-1 lakini Manchester United hawajaishinda Arsenal ugenini kwenye Ligi Kuu tangu Februari 2005 waliposhinda 4-2 Uwanja wa zamani Highbury.
Katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu hapo Jumatano, Arsenal walitoka suluhu 0-0 na Aston Villa huko Villa Park na hivyo kuikosa nafasi ya kuipiku Manchester United toka nafasi ya pili na pia Chelsea na kuongoza Ligi.
Vile vile katika mechi hiyo Arsenal walipata pigo pale Difenda wao wa kutumainiwa Thomas Vermaelen kuumia na huenda asicheze mechi hii na nafasi yake pengine itachukuliwa na Mkongwe Sol Campbell.
Nao Manchester United waliifunga Hull City 4-0 kwenye mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu huku Wayne Rooney akifunga bao zote 4.
Katika mechi hii, Man U watamkosa Rio Ferdinand aliefungiwa mechi 4 kwa kosa la kumpiga Craig Fagan wa Hull lakini Difenda wao wa kutumainiwa Nemanja Vidic amepona na huenda akacheza.
VIKOSI VINATEGEMEWA KUWA:
Arsenal (Fomesheni 4-3-3): Almunia; Sagna, Gallas, Campbell, Clichy; Denilson, Fabregas, Ramsey; Rosicky, Bendtner, Arshavin.
Man United (Fomesheni 4-4-2): Van der Sar; Rafael, Brown, Evans, Evra; Valencia, Fletcher, Scholes, Giggs; Rooney, Berbatov.
Refa: Chris Foy
LIGI KUU: MATOKEO MECHI ZA Jumamosi, Januari 30
Birmingham 1 v Tottenham 1
Fulham 0 v Aston Villa 2
Hull 2 v Wolves 2
Liverpool 2 v Bolton 0
West Ham 0 v Blackburn 0
Wigan 0 v Everton 1
Burnley v Chelsea [INAANZA saa 2 na nusu usiku bongo taimu]
MECHI ZA Jumapili, 31 Januari 2010
[saa 10 na nusu jioni]
Man City v Portsmouth
[saa 1 usiku]
Arsenal v Man United

CAF yaifungia Togo!!!
Togo wamefungiwa kutocheza Mashindano mawili yafuatayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kujitoa kwenye Fainali za Mashindano hayo yanayofanyika Angola kufuatia basi walilokuwa wakisafiria kushambuliwa kwa risasi na kuuliwa Dereva wake, Kocha Msaidizi na Afisa Habari wa Togo.
Baada ya maafa hayo Serikali ya Togo iliamuru Timu ya Togo irudi nyumbani.
Basi hilo la Togo lilitokea Congo na lilikuwa limeshaingia Angola kwenye Jimbo la Cabinda lenye Waasi na likashambuliwa likiwa njiani kwenda kwenye kituo chao Mji wa Cabinda walikotakiwa kuwa Kundi moja na Ghana, Ivory Coast na Burkina Faso.
Rais wa CAF, Issa Hayatou, amethibitisha kuwa Togo imefungiwa kwa vile Serikali iliingilia masuala ya soka.
LIGI KUU: Matabaka yaanza kujitokeza!
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu kumeanza kujitokeza matabaka yanayotenganisha vikundi vya Timu na kila kikundi kinaonekana wazi kugombea kitu chao.
Kundi la kwanza ni lile la Timu 3 za juu ambazo ndizo unazoweza kusema wanawania Ubingwa.
Kundi hili linaongozwa na Chelsea wenye pointi 51 kwa mechi 22, wakifuata Mabingwa Watetezi Manchester United wenye pointi 50 kwa mechi 23 na Arsenal ni wa 3 pointi 49 kwa mechi 23 pia.
Kundi la pili ni lile linalowania nafasi ya 4 ambalo lina Timu 4 nazo ni Tottenham pointi 41 kwa mechi 23, Liverpool pointi 38 kwa mechi 23, Manchester City pointi 38 kwa mechi 21 na Aston Villa pointi 37 kwa mechi 22.
Kundi la 3 ni lile lenye Timu kama 5 ambazo zinalifukuza Kundi la pili kwa mbali kidogo na hili lina Birmingham, Everton, Fulham, Blackburn na Stoke.
Pengine unaweza ukaiingiza Sunderland humo.
Mwishowe ni lile Kundi lenye nia tu ya kujinusuru wasishushwe Daraja lakini hili lina matabaka mawili ya lile lenye afueni na lile la taaban bin hoi.
Kwenye afueni unaweza kuziweka Sunderland pointi 23 na Wigan [22].
Kwenye taabani yuko yule alieshika mkia Portsmouth mwenye pointi 14 tu na juu yake yupo Hull pointi 19 wakifuatia Burnley [20], Wolves [20], West Ham [20] na Bolton [21].
MSIMAMO LIGI KUU England: [Timu zimecheza mechi 23 isipokuwa inapotajwa]
1 Chelsea pointi 51 [mechi 22]
2 Man Utd pointi 50
3 Arsenal pointi 49
4 Tottenham pointi 41
5 Liverpool pointi 38
6 Manchester City pointi 38 [mechi 21]
7 Aston Villa pointi 37 [mechi 22]
8 Birmingham pointi 33 [mechi 22]
9 Everton pointi 29 [mechi 22]
10 Fulham pointi 27 [mechi 22]
11 Blackburn pointi 27
12 Stoke pointi 25 [mechi 21]
13 Sunderland pointi 23 [mechi 22]
14 Wigan pointi 22 [mechi 21]
15 Bolton pointi 21 [mechi 21]
16 West Ham pointi 20 [mechi 22]
17 Wolves pointi 20 [mechi 22]
18 Burnley pointi 20 [mechi 22]
19 Hull pointi 19 [mechi 22]
20 Portsmouth pointi 14 [mechi 21]
SAKATA LA TERRY: FA yagoma kuzungumzia kashfa!!!
Chama cha Soka England, FA, kimekataa kuzungumza lolote kuhusu Nahodha wa England John Terry kufuatia mlipuko wa taarifa zake kwenye vyombo vya habari akihusishwa na uhusiano wa kimapenzi na gelfrendi wa Mchezaji mwenzake Wayne Bridge uliotajwa jana kufuatia Mahakamani kufutilia mbali uamuzi wa awali wa jina la Terry kutotajwa katika tuhuma hizo.
Kumekuwa na wito toka kona nyingi kuwa Terry ambae ana Mke na Watoto ajiuzulu Unahodha wa England.
Klabu ya John Terry ambayo pia ni Nahodha, Chelsea, imesema ipo pamoja na Terry kwenye matatizo yake na kwamba inachukulia kashfa hiyo kama tatizo binafsi la Mchezaji huyo na wako tayari kumpa msaada pamoja na familia yake.
UHAMISHO: Dirisha kufungwa Jumatatu!!!
Dirisha la Uhamisho wa Wachezaji linategemewa kufungwa Jumatatu na, ingawa kumekuwa hamna kikubwa mno kilichofanyika kwenye kipindi hiki, zifuatazo ni taarifa na tetesi zilizotanda kwenye dakika hizi za mwisho:
-Babel
Winga huyu wa Liverpool amehusishwa na Birmingham na inasemekana ofa ya Klabu hiyo ya Pauni Milioni 9 ilikataliwa na Liverpool lakini inadaiwa majadiliano yanaendelea.
-Dindane
Aruna Dindane kutoka Ivory Coast ambae yuko Portsmouth kwa mkopo akitokea Klabu ya Ufaransa Lens huenda nae akachukuliwa na Birmingham.
-Pavlyuchenko
Roman Pavlyuchenko ni chaguo nambari wani la Birmingham ingawa Tottenham wameweka ngumu lakini mjadala unaendelea na pengine uamuzi utatoka wakati wowote.
-Wilshere
Imeshathibitishwa kuwa Bolton Wanderers imemchukua Jack Wilshere kutoka Arsenal kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.
Arsene Wenger amesema uamuzi wa kumruhusu Kiungo huyo Chipukizi ni kumpa uzoefu wa Ligi Kuu.
-Okaka
Fulham wako hatua za mwisho kumchukua Straika kutoka AS Roma Stefano Okaka na kwa sasa anafanyiwa upimwaji afya ili ahamie Fulham kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.
-Benjani
Meneja wa Sunderland Steve Bruce amethibitisha wako kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na Wawakilishi wa Straika kutoka Zimbabwe Benjani Mwaruwaru ili wamnunue moja kwa moja kutoka Manchester City.
KOMBE LA AFRIKA: Mshindi wa 3 leo, ni Algeria v Nigeria
Leo Uwanjani Novemba 11 Mji Mkuu wa Angola, Luanda, Timu zilizofungwa Nusu Fainali hapo juzi, zinashuka dimbani kulilia nafasi ya ushindi wa 3.
Algeria ilibamizwa 4-0 na Misri na Nigeria ilitolewa na Ghana kwa bao 1-0.
Mechi hii itaanza saa 1 usiku, saa za bongo.
Fainali ni kesho.
Leo Ulaya:
SERIE A:
AS Bari v Palermo
Napoli v Genoa
LA LIGA:
RCD Espanyol v Athletic de Bilbao
Sporting Gijon v FC Barcelona
Deportivo la Coruna v Real Madrid
BUNDESLIGA:
Bayern Munich v FSV Mainz 05
Borussia Munchen Gladbach v SV Werder Bremen
Hannoverscher 1896 v FC Nurnberg
Hertha Berlin v VFL Bochum
Eintracht Frankfurt v FC Koln
Schalke 04 v TSG Hoffenheim
LIGUE 1:
FC Girondins de Bordeaux v US Boulogne
Lille OSC v Racing Club de Lens
Le Mans v Toulouse FC
AS Nancy Lorraine v Lorient
AS Monaco FC v Nice
Stade Rennais FC v Grenoble
Montpellier HSC v Olympique de Marseille
SKANDALI LA TERRY!!!
• Unahodha England kumtoka?
• Atajwa kortini baada ya kuitaka Mahakama isimtangaze!!
Ingawa kulikuwa na tetesi za muda mrefu kuwa John Terry, Nahodha wa Chelsea na England, ana ‘skandali’ ambalo kuna Gazeti la Uingereza limelivalia njuga na kutaka kulilipua, FA ilikataa kumvua Unahodha wa England na Mkuu wake, Ian Watmore, alikaririwa kabla ya Krismas mwaka jana kuwa uamuzi huo ni juu ya Fabio Capello, Kocha wa England.
Lakini jana skandali hilo limeingia hatua mpya pale Mahakama kuamua haioni sababu yoyote ya jina la John Terry kutotangazwa na hivyo Magazeti yakapata ‘sikukuu’ kumtaja Terry katika sakata hilo linalomhusisha kufanya uhusiano wa kimapenzi na Bibi Vanessa Perroncel aliekuwa Mpenzi wa Mchezaji mwenzake wa Chelsea wakati huo, Wayne Bridge, ambae sasa yuko Manchester City.
Wadau sasa wameshika bango wakidai ‘uhuni’ huo kwa mtu mwenye ndoa na pia Nahodha wa England unafedhehesha heshima hiyo hivyo ni bora Terry akavuliwa huo Unahodha hasa kwa vile imebaki miezi mitano kabla Fainali za Kombe la Dunia kuanza na pia England ipo mbioni kugombea kuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018.
Wengine walikumbusha na kufanananisha na skandali la kauli potofu ya aliekuwa Meneja wa England, Glenn Hoddle, alipodai vilema wamepewa adhabu na Mungu na kauli hiyo ilimkosti kazi yake alipolazimika kujiuzulu Umeneja wa England.
Watu wa karibu na Wayne Bridge wamedai Beki huyo wa Manchester City aliekuwa rafiki wa karibu mno na John Terry alichukizwa mno aliposikia uhusiano wa mpenzi wake Vanessa na John Tery hasa kwa vile wao walikuwa ni wageni waalikwa kwenye harusi ya Terry iliyofanyika mwaka 2007.

Friday 29 January 2010

Kitimtim cha Ligi Kuu
Bigi Mechi ni Jumapili wakati Arsenal wakiwa kwao Emirates watawavaa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Manchester United kwenye mechi inayozikutanisha Timu mbili zilizotenganishwa kwa pointi moja huku Man United wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Chelsea na juu ya Arsenal walio nafasi ya 3.
Jumamosi kutakuwa na mechi 7 za Ligi Kuu na vinara wa Ligi Chelsea watasafiri kwenda kucheza na Burnley na Timu kubwa inayosuasua Liverpool itakuwa nyumbani kuwakaribisha Bolton Wanderers.
Aston Villa wanasafiri hadi London kucheza na Fulham huku wakiwa hawajashinda mechi zao 5 za mwisho za ugenini lakini Fulham wakiwa uwanja wa nyumbani Craven Cottage ni Timu ngumu.
Tottenham watakuwa nyumbani kucheza na Birmingham na huenda Mchezaji wao mpya Eidur Gudjohnsen akaonekana. Tottenham wako nafasi ya 4 wakiwa pointi 3 mbele ya Timu ya 5 Liverpool.
Hull City wataikaribisha Wolves na Timu hizi zote ziko eneo la hatari la kuporomoka Daraja na wanatofautiana kwa pointi moja tu kati yao.
Everton, ambao wameanza kupamba moto na hawajafungwa mechi 8 sasa, wanasafiri hadi Uwanja wa DW kucheza na Wigan ambao wanapigania uhai wao kwenye Ligi Kuu.
Nyumbani kwa West Ham, Uwanja wa Upton Park, kutakuwa na mechi kali kati ya wenyeji na Blackburn Rovers ambao wako nafasi ya 11 kwenye Ligi huku West Ham
wakielea nafasi ya 4 toka mkiani.
Jumapili, kabla ya Bigi Mechi ya Arsenal v Man United, Manchester City watataka kufuta machungu ya kubamizwa na Man United 3-1 siku ya Jumatano kwa kuisulubu Timu iliyo mkiani Portsmouth wakiwa Uwanja wa nyumbani City of Manchester.
RATIBA KAMILI:
[saa za bongo]
Jumamosi, 30 Januari 2010
[saa 12 jioni]
Birmingham v Tottenham
Fulham v Aston Villa
Hull v Wolves
Liverpool v Bolton
West Ham v Blackburn
Wigan v Everton
[saa 2 na nusu usiku]
Burnley v Chelsea
Jumapili, 31 Januari 2010
[saa 10 na nusu jioni]
Man City v Portsmouth
[saa 1 usiku]
Arsenal v Man United
Jumatatu, 1 Februari 2010
[saa 5 usiku]
Jumanne, 2 Februari 2010
[saa 4 dak 45]
Hull v Chelsea
Jumatano, 3 Februari 2010
Fulham v Portsmouth
Rooney: Man United si Timu ya Mtu Mmoja!!
Wayne Rooney amepinga vikali kauli za watu kadhaa akiwemo Supastaa wa zamani England Alan Shearer kwamba Manchester United sasa inamtegemea yeye peke yake ili kupata ushindi.
Rooney juzi ndie aliefunga bao la ushindi kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Carling dhidi ya Manchester City katika mechi waliyoshinda 3-1 na hivyo kuitoa City kwa jumla ya bao 4-3 katika mechi mbili za hiyo Nusu Fainali na kuipeleka Timu yake Fainali Wembley watakapocheza na Aston Villa Februari 28.
Katika mechi ya nyuma ya hiyo, Manchester United waliishinda Hull City 4-0 kwenye Ligi Kuu na Rooney ndie aliefunga bao zote 4.
Mpaka sasa Rooney ameshafunga jumla ya mabao 21 msimu huu na kwenye Ligi Kuu yeye ndie anaeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 19.
Rooney ametamka: “Sioni kama hii ni Timu ya mtu mmoja! Kama sipewi mipira, sifungi! Na kama sifungi, wengine watafunga tu!”
Mafarao Fainali, Algeria wakikwaa kipondo!
• Misri 4 Algeria 0
• Algeria mtu 8 uwanjani baada ya Nyekundu kutembea!!!
Mbele ya Mamia ya Mashabiki wao walioruka na Ndege maalum kwenda Benguela, Angola kutoka Algeria na Misri na kufurika Uwanjani, Misri waliishushia kipigo kitakatifu Algeria cha bao 4-0 na kulipiza kisasi cha kutolewa na Algeria kushiriki Fainali za Kombe la Dunia, kipigo kilichowaacha Algeria wakisambaratika na kubaki mtu 8 tu uwanjani baada ya Wachezaji wao watatu kula Kadi Nyekundu.
Misri watacheza Fainali yao ya 3 mfululizo hapo Jumapili kwa kukutana na Ghana waliyoibwaga Nigeria 1-0 kwenye Nusu Fainali ya awali.
Kiama cha Algeria kilianzia pale Hosni Abd Rabou kufunga kwa penalti baada ya Mchezaji wa Algeria Rafik Halliche kucheza rafu ndani ya boksi iliyompa Kadi yake ya pili ya Njano na hivyo kuwashwa Nyekundu.
Mohamed Zidan alipachika bao la pili, Mohamed Abdelshafi alifunga bao la 3 na Mchezaji hodari wa Akiba, Gedo, kama kawaida yake, alifunga bao la 4.
Baadae kwenye mechi hiyo Wachezaji wa Algeria, Nadir Belhadj na Kipa Fawzi Chaouchi, walipewa Kadi Nyekundu.
Baada ya mechi Kocha Msaidizi wa Misri, Shawki Gharib, alisema: “Tunastahili kuwa Fainali! Tumezifunga timu 3 [Nigeria, Ivory Coast na Algeria] ambazo ziko Fainali Kombe la Dunia!”
Kocha wa Algeria Rabah Saadane alimlaumu Refa Codjia kutoka Benin kwa kipigo chao kwa kusema: “Refa alimpa Kadi Nyekundu Halliche ambae ni Mlinzi wetu bora kwa kosa lilsilostahili! Halafu tulicheza mtu 8 na haiwezekani kwa Timu bora kama Misri!”
Vikosi vilikuwa:
Algeria: Chaouchi, Yahia, Bougherra, Halliche, Belhadj, Yebda, Mansouri, Matmour (Abdoun dakika ya 75), Ziani, Meghni (Laifaoui dakika 67), Ghezzal (Zemmamouche dakika 89).
Akiba hawakucheza: Gaouaoui, Bezzaz, Lemmouchia, Saifi, Raho, Babouche, Zaoui, Bouazza, Ziaya.
Kadi Nyekundu: Halliche (dakika 38), Belhadj (dakika 70), Chaouchi (dakika 88).
Misri: El Hadari, El Mohamady, Gomaa, Fathallah (Gedo dak 59), Moawad (Abdelshafy dak 78), Hassan, Fathi, Said, Abd Rabou, Zidan, Moteab (Ghaly dak 52).
Akiba hawakucheza: Abdoul-Saoud, Salem, El Sakka, Eid, Tawfik, Shikabala, Raouf, Hamdy, Wahid.
Mabao: Abd Rabou dakika ya 39, Zidan dakika 65, Abdelshafy dakika 81, Gedo dakika 90.
Refa: Bonaventure Koffi Codjia (Benin).
Ghana 1 Nigeria 0
  • Nyota Nyeusi Fainali!!  
Bao la Mshambuliaji Asamoah Gyan dakika ya 21 limeiingiza Ghana Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuipiga Nigeria 1-0 hapo jana.
Gyan pia ndie aliefunga bao 1 na la ushindi Ghana walipowatoa Wenyeji Angola kwenye Robo Fainali.
Lakini shujaa wa Ghana aliehakikisha wanatinga Fainali bila shaka ni defensi yao hasa Kipa Richard Kingson waliookoa mikikimikiki yote ya akina Martins, Odemwingie, Obasi, Mikel na wenzao.
Baada ya mechi Mshindi Gyan alisema: “Inashangaza!! Sisi ni Timu ya Vijana Chipukizi na wengi hawakutegemea tutatinga Fainali!”
Vikosi vilikuwa:
Ghana: Kingson, Inkoom, Vorsah, Addy, Sarpei (Rahim Ayew dakika 53), Andre Ayew, Agyemang-Badu, Annan, Asamoah, Gyan (Amoah 84), Opoku (Draman 35).
Akiba hawakucheza: McCarthy, Osei, Mensah, Essien, Narry, Addo, Adiyah, Afful, Adjei.
Nigeria: Enyeama, Mohammed (Odiah 80), Nwaneri, Shittu, Echiejile, Kaita, Mikel, Yussuf (Obinna 67), Odemwingie (Yakubu 70), Martins, Obasi.
Akiba hawakucheza: Ejide, Yobo, Taiwo, Kanu, Olofinjana, Uche, Etuhu, Apam, Aiyenugbu.
Refa: Daniel Bennet (South Africa).
Robinho arudi kwao Brazil!!!
• Yupo Santos kwa mkopo!!
Mchezaji kutoka Brazil, Robinho, ambae kukaa kwake Manchester City kumetawaliwa na majonzi binafsi ya kutokuwa na furaha, yuko mbioni kurudi kwao Brazil kuichezea Santos kwa mkopo wa miezi 6.
Robinho, miaka 26, aliigharimu Manchester City Pauni Milioni 32 walipomnunua kutoka Real Madrid mwaka 2008 ikiwa ni rekodi kwa Uingereza, amekuwa hana namba Man City kwa kuwa kiwango chake kimeporomoka mno na mwenyewe amekuwa akililia aondoke ili kunusuru nafasi yake kwenye Timu ya Taifa ya Brazil itakayocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwezi Juni.
Robinho alikuwa Mchezaji wa Santos kabla kuhamia Real Madrid mwaka 2003.
Man U yamthibitisha Smalling
Manchester United imethibitisha kuwa Difenda Chris Smalling, miaka 20, kutoka Fulham amefaulu vipimo vya afya na amesaini mkataba wa miaka minne ingawa atabaki Fulham hadi mwisho wa msimu huu na kujiunga Old Trafford mwezi Julai.
Smalling, anaechezea Timu ya Taifa ya England ya Vijana chini ya miaka 21, ameshaichezea Fulham mechi 9 msimu huu na Sir Alex Ferguson amezungumza: “Ni mwepesi na anausoma mchezo vizuri. Tumefurahi kumchukua!”
Smalling alitoa shukrani zake kwa Meneja wake Roy Hodgson wa Fulham na kusema: “Nimejifunza mengi Fulham na nawashkuru! Kuja kwenye Klabu bora duniani ni nafasi adimu na nina furaha kubwa!”
Mutu yamkuta tena!!!
• Ni madawa yamtia matatani!!!!
Mshambuliaji wa Fiorentina Adrian Mutu amegundulika kutumia madawa yaliyopigwa marufuku na sasa yuko matatani na CONI, Kamati ya Olimpiki ya Italia, hii ikiwa ni mara ya pili kwa Mutu kukumbana na rungu la utumiaji wa madawa yaliyopigwa marufuku.
Mutu, miaka 31 kutoka Romania, aligundulika na chembechembe za dawa iitwayo ‘sibutramine’ ambayo hutumika kupunguzia unene na ambayo ipo kwenye listi ya dawa marufuku kwa Wanamichezo.
Ugundizo huo ulitokea baada ya mechi ya Serie A kati ya Klabu yake Fiorentina na Bari iliyofanyika Januari 10 na Mutu alipiga bao kwenye mechi hiyo Fiorentina waliyoshinda 2-1.
Mwaka 2004 Mutu aligundulika akitumia kokeni na kufungiwa pamoja na kufukuzwa na Klabu yake ya wakati huo, Chelsea, ambayo ilimshitaki na kumdai Mutu alipe fidia kwa kukiuka mkataba.
Mutu anatakiwa ailipe Chelsea Pauni Milioni 15 na kesi ipo Mahakamani baada ya Mutu kukata rufaa.

Thursday 28 January 2010

Rio kifungo mechi 4!!!!!!!!!

Rio Ferdinand amefungiwa mechi 4 baada ya rufaa yake ya kupinga shitaka la kushambulia kutupwa na Jopo Huru la Nidhamu.
Rio alishitakiwa kwa kumpiga Straika wa Hull City Craig Fagan katika mechi ya Ligi Kuu ya Jumamosi iliyopita na tukio hilo halikuonwa na Refa Steve Bennett.
Kawaida kosa kama hilo Mchezaji hufungiwa mechi 3 tu lakini ukikata rufaa na kushindwa hiyo rufaa ni kawaida pia kuongezewa kifungo cha mechi moja na hilo ndilo lililomkuta Rio Ferdinand.
Kwa hiyo Rio atazikosa mechi za Ligi Kuu za kuanzia Jumapili na Arsenal pia mechi za Portsmouth, Aston Villa na Everton lakini ataiwahi Fainali ya Carling na Aston Villa Februari 28.
Tottenham wamyakua Gudjohnsen kwa mkopo
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amesema Klabu yake imemchukua kwa mkopo Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na Barcelona Eidur Gudjohnsen hadi mwishoni mwa msimu.
Gudjohnsen kwa sasa ametokea Klabu ya Ufaransa Monaco.
West Ham pia walikuwa wakimuwania Mchezaji huyo mwenye miaka 31 lakini inaelekea wameshindwa kumpata.
Tottenham wanao Mastraika wanne akina Jermain Defoe, Peter Crouch, Robbie Keane na Roman Pavlyuchenko ingawa Pavlyuchenko yuko mguu nje mguu ndani kwani kuna minong’ono huenda akahama.
Gudjohnsen alipokuwa Chelsea walitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu mara 2 mwaka 2005 na 2006 na huko Barcelona aliweza kutwaa Mataji manne makubwa mwaka jana yakiwemo ya La Liga na UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Tosic wa Man United yuko FC Cologne
Manchester United wamemkopesha Winga wao kutoka Serbia Zoran Tosic kwa Klabu ya Ujerumani FC Cologne hadi mwishoni mwa msimu.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 22 alijiunga na Man United miezi 12 iliyokwisha akitokea Partizan Belgrade lakini amemudu kuchezea mechi 2 tu za Kombe la Carling dhidi ya Barnsley na Tottenham.
Tosic amesema: “Siamini kama huu ndio mwisho wangu Man U!! Nikicheza vizuri Cologne ntarudi tu Old Trafford!!”
KOMBE LA AFRIKA: Leo Watani wa Jadi wakumbana Nusu Fainali !!!
  • Ni Algeria v Misri na Ghana v Nigeria
Kihistoria, mechi za leo zinakutanisha Nchi ambazo zina ushindani wa jadi ambao mara nyingine huzua balaa hata nje ya Uwanja wa Mpira hasa kwa mechi za Misri v Algeria na mfano ni hivi karibuni Nchi hizo zilipokutana kwenye Mtoano wa Kombe la Dunia na ukazuka mtafuruku mkubwa na hata Basi la Wachezaji wa Algeria kupigwa mawe huko Cairo mwezi Novemba mwaka jana.
Vurugu hizo zilitapakaa hadi Nchini Algeria ambako Wamisri walishambuliwa na wengi kuikimbia Nchi hiyo.
Pia kulikuwa na ripoti kuwa Jamii za Raia wa Nchi hizo waishio Ufaransa walipambana baada ya mechi hiyo ya Cairo.
Lakini Wadau wanategemea mechi za leo zitaisha salama huko Angola ingawa kila Nchi imethibitisha kuwapeleka mamia ya raia zao kwa ndege maalum.
Ghana na Nigeria watacheza Uwanja wa Novemba 11 huko Luanda, Angola na mechi yao itaanza saa 1 usiku saa za bongo.
Nigeria watamkosa Mlinzi Onyekachi Apam ambae alipewa Kadi Nyekundu kwenye mechi ya Robo Fainali waliyowatoa Zambia kwa penalti.
Ghana wao wanategemea kuwa na Kikosi chao kamili.
Algeria na Misri zipo Uwanja wa Ombaka huko Benguela na mechi yao itaanza saa 4 na nusu saa za bongo.
Beki wa Misri Wail Gomaa ameeleza kuwa wao hawataki kisasi na Algeria kwa kuwabwaga nje ya Kombe la Dunia ila wanachotaka tu ni ushindi.
Washindi wa mechi za leo watakutana Fainali Jumapili.
MECHI ZA LIGI KUU JANA: Ushindi kwa Chelsea, Everton na Blackburn Rovers, Villa na Arsenal ngoma ngumu!!!
Chelsea wameukwaa tena uongozi wa Ligi Kuu kwa kuwapiga Birmingham City mabao 3-0 huku Aston Villa na Arsenal wakitoka suluhu ya 0-0.
Everton, wakiwa kwao Goodison Park, waliwabutua Sunderland 2-0 na kuendeleza kwao wimbi la matokeo mazuri.
Nao Blackburn wamezidi kujikongoja kujinasua toka eneo la hatari la mkiani kwenye msimamo wa Ligi kwa kuifunga Wigan 2-1.
Ushindi wa Chelsea uliowapa uongozi wa Ligi Kuu uliletwa na mabao ya Malouda na Lampard aliefunga mawili.
Arsenal walibanwa na Aston Villa na hivyo kushindwa kuipiku Manchester United toka nafasi ya pili na sasa wamebaki wakiwa wa 3 wakiwa pointi moja nyuma Man U kwa mechi sawa zilizochezwa.
Pia, Arsenal wamepata pigo kubwa kwenye mechi hiyo baada ya kuumia kwa Beki wao alionyesha umahiri mkubwa Msimu huu, Thomas Vermaelen, ambae inahofiwa amevunjika mfupa mguuni.
Man United waifumua Man City na kutinga Fainali!!!!
• Ni Rooney aleta ushindi!!!!
Huku ngoma ikiwa suluhu kwa jumla ya magoli 3-3, Wayne Rooney alichomeka bao la ushindi dakika za majeruhi na kuwanyamazisha mahasimu wao wakubwa Manchester City na pia kuipeleka Manchester United Fainali ya Kombe la Carling huko Wembley hapo Febryari 28 watakapocheza na Aston Villa.
Bao la Wayne Rooney liliipa ushindi Man U wa bao 3-1 hapo jana kwao Old Trafford.
Man City walishinda mechi ya kwanza 2-1 na hivyo wametolewa kwa jumla ya bao 4-3.
Man City waliingia kwenye mechi hiyo wakiwa mbele kwa bao 2-1 na majigambo yao, wakiongozwa na kidomodomo cha Tevez, lakini walisahau kuwa wao kwa mara ya mwisho kutinga Fainali yeyote ilikuwa ni mwaka 1981 na tangu wakati huo mpaka sasa Manchester United wameshacheza Fainali 21 na kutwaa Ubingwa wa England mara 11.
Hadi mapumziko bao zilikuwa 0-0.
Paul Scholes alifunga bao la kwanza dakika ya 51 na Michael Carrick akapachika la pili dakika ya 71 lakini Tevez akawapa City matumaini alipofunga bao dakika ya 75.
Huku ngoma ikitaka kwenda dakika 30 za nyongeza ndipo Rooney akaonyesha ushujaa wake kwa mara nyingine tena.
MATOKEO MECHI ZA Jumatano, Januari 27
Caling Cup
Man United 3 v Man City 1 [Man U aingia Fainali kwa jumla ya bao 4-3]
LIGI KUU
Aston Villa 0 v Arsenal 0
Chelsea 3 v Birmingham 0
Blackburn 2 v Wigan 1
Everton 2 v Sunderland 0
Basturk asaini Blackburn
Mchezaji wa Kimataifa wa Uturuki, Yildiray Basturk, miaka 31, ambae ni Mzaliwa wa Ujerumani amehamia Klabu ya Ligi Kuu England Blackburn Rovers kutoka Klabu ya Bundesliga huko Ujerumani ya Stuttgart.
Basturk, ambae ni Kiungo, ameshaichezea Timu ya Taifa ya Uturuki mara 49 na amesema alidokezwa kuwa Blackburn ni Klabu nzuri na Mchezaji wa zamani wa Blackburn Mturuki Tugay ambae amestaafu.
Basturk amesaini mkataba wa kuichezea Blackburn hadi mwishoni mwa Msimu huu.
Rio akana shitaka la FA
Mchezaji wa Manchester United Rio Ferdinand amekana shitaka lake la kucheza vibaya na kumshambulia Mchezaji wa Hull City Craig Fagan analodaiwa na FA kulitenda kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi iliyokwisha ambayo Man United walishinda 4-0.
Refa Steve Bennett hakuona kitendo cha Rio lakini alimpa Fagan Kadi ya Njano mara baada ya Rio kuonekana akitenda kosa hilo.
Kwa kukanusha kosa, Rio yuko huru kucheza mechi ya Nusu Fainali ya Carling dhidi ya Manchester City na jopo litasikiliza kesi yake Alhamisi Januari 28 na endapo atapatikana na hatia atafungiwa mechi 3 na hivyo kuikosa mechi ya Jumapili na Arsenal, mechi ya Februari 6 na Portsmouth na ile dhidi ya Aston Villa siku 4 baadae.

Wednesday 27 January 2010

Carling Cup: Leo moto kuwaka Old Trafford??
• Marudio Man United v Man City
FA imetoa onyo kali kwa Mameneja, Wachezaji na Washiriki wote wa Klabu mbili za Jiji la Manchester, Manchester United na Manchester City, kabla ya pambano lao la Jumatano Januari 27 la marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling Uwanjani Old Trafford, ili kuepusha mtafaruku kati ya Mashabiki wa Timu hizo mbili ambao ni Mahasimu wakubwa.
Katika mechi ya kwanza wiki iliyopitwa iliyochezwa nyumbani kwa Man City Uwanjani City of Manchester Wenyeji waliwafunga Man United 2-1.
Lakini katika pambano hilo kulitokea kitendo ambacho kimekuwa gumzo kubwa pale Carlos Tevez, aliekuwa Mchezaji wa Man United kabla kwenda Man City, ambae ndie aliifungia Man City bao zao 2 kwenda mbele ya benchi la Man United kila alipofunga bao kuwakejeli na mwenyewe Tevez anadai yeye alikuwa akimdhihaki Nahodha wa Man United Gary Neville aliekuwa benchi kwa kauli yake kuwa Tevez hana thamani ya Pauni Milioni 25 zilitokiwa kumbakisha Man United na ndio maana klabu hiyo haikumbakisha.
Inasemekana kejeli za Tevez zilimfanya Neville amwonyeshe Tevez ishara ya kidole kimoja ambacho wengi hutafsiri ni matusi.
Wachezaji hao wawili wamepewa onyo kali na la mwisho na FA kutorudia vitendo hivyo.
FA imeshawasiliana na Polisi wa Manchester ambao wataimarisha ulinzi na ambao watawasachi Washabiki wote watakaoingia Uwanjani kuhakikisha hawabebi silaha.
Pia imefafanunuliwa kuwa endapo mechi hiyo itamalizika huku idadi ya magoli iko sawa hadi dakika 90 zikiisha magoli ya ugenini hayatahesabiwa kama mawili na mechi itaingia muda wa nyongeza wa dakika 30 na hizo zikiisha huku idadi ya magoli ipo sawa basi hapo ndipo magoli ya ugenini yatahesabiwa kama mawili ili kumpata Mshindi.
Ikiwa pia Timu zitafungana kwa magoli hayo ya ugenini basi itapigwa mikwaju mitano ya penalti ili kumpata Mshindi atakeingia Fainali kucheza na Aston Villa aliemtoa Blackburn kwenye Nusu Fainali kwa jumla ya mabao 7-4.
Chipukizi wa Fulham kutua Man United?
Fulham inasemekana imekubali ofa ya Manchester United ya kumnunua Mlinzi Chipukizi ambae pia ni Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana wa chini ya miaka 21 ya England, Chris Smalling.
Mchezaji huyo amekuwa akiwaniwa na Klabu kadhaa ikiwemo Arsenal lakini inaelekea Man United ndio itafuzu kumnyakua.
Smalling alijiunga na Fulham mwaka 2008 na alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu tarehe 28 Desemba 2009 Fulham ilipoivaa Chelsea.
MATOKEO LIGI KUU Jumanne, Januari 26
Portsmouth 1 v West Ham 1
Tottenham 2 v Fulham 0
Wolves 0 v Liverpool 0
Bolton 1 v Burnley 0

Tuesday 26 January 2010

Kandanda wiki hii:
Jumanne, Januari 26
LIGI KUU
[saa 4 dak 45 usiku]
Portsmouth v West Ham
Tottenham v Fulham
Wolves v Liverpool
[saa 5 usiku]
Bolton v Burnley
Jumatano, Januari 27
Caling Cup
[saa 5 usiku]
Man United v Man City
LIGI KUU
[saa 4 dak 45]
Aston Villa v Arsenal
Chelsea v Birmingham
[saa 5 usiku]
Blackburn v Wigan
Everton v Sunderland
Alhamisi, Januari 28
Kombe la Mataifa ya Afrika-Nusu Fainali
[saa 1 usiku]
Ghana v Nigeria
[saa 4 na nusu usiku]
Algeria v Misri
LIGI KUU
Jumamosi, Januari 30
[saa 12 jioni]
Birmingham v Tottenham
Fulham v Aston Villa
Hull v Wolves
Liverpool v Bolton
West Ham v Blackburn
Wigan v Everton
[saa 2 na nusu usiku]
Burnley v Chelsea
LIGI KUU
Jumapili, Januari 31
[saa 10 na nusu jioni]
Man City v Portsmouth
[saa 1 usiku]
Arsenal v Man United
LIGI KUU
Jumatatu, Februari 1
[saa 5 usiku]
Sunderland v Stoke

LIGI KUU
Jumanne, Februari 2
[saa 4 dak 45]
Hull v Chelsea
LIGI KUU
Jumatano, Februari 3
Fulham v Portsmouth
Shearer: “Rooney anaibeba Man United”
Alan Shearer, Mshambuliaji wa zamani wa England ambae pia alikuwa Meneja wa Newcastle, ametamka kuwa Wayne Rooney ndio anaibeba Manchester United na bila yake Klabu hiyo ingeyumba.
Shearer amesema: “Wasingekuwa walipo kwenye Ligi bila Rooney.”
Rooney ndie anaeongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye Ligi Kuu na anazo goli 19.
Hata hivyo Shearer amekiri kuwika kwa Rooney ni manufaa makubwa kwa England hasa kwa sababu Kombe la Dunia lipo karibuni.
Rio ashitakiwa na FA!!
Sentahafu wa Manchester United, Rio Ferdinand, ameshitakiwa na FA kwa kosa la mchezo mbaya na wa fujo baada ya kunaswa na kamera akimpiga Mshambuliaji wa Hull City Craig Fagan katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Old Trafford Jumamosi iliyopita ambapo Man United waliifunga Hull mabao 4-0.
Kitendo cha Rio hakikuonekana kwa Refa Steve Bennett na badala yake alimpa Kadi ya Njano Fagan muda mfupi baada ya tukio hilo.
Rio Ferdinand alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza baada ya miezi mitatu kwa sababu alikuwa kaumia.
Ferdinand amepewa mpaka Jumatano kujibu mashitaka hayo na anaweza kukubali kosa na hivyo kutumikia kifungo cha mechi 3 au kukana na kesi hiyo ikaanza kusikilizwa Alhamisi.
Akikubali kosa hiyo Jumatano atakuwa huru kucheza Mechi ya siku hiyo hiyo usiku ya Nusu Fainali ya Carling Cup dhidi ya Manchester City na adhabu yake ya mechi 3 itaanza Jumapili Man United watakapocheza na Arsenal.
KOMBE LA AFRIKA: Nigeria yaitoa Zambia kwa matuta!!
Ni mechi ambayo ni lazima Zambia wataiota kwa muda mrefu sana kwani ushindi ulikuwa mweupe kwao baada ya kuutawala mchezo na kukosa nafasi nyingi sana.
Zambia, wakiwa na Vijana wadogo kiumri kama vile Mbola mwenye miaka 16 tu na wengi wenye maumbo madogo tu, waliwafunika Masupastaa wa Nigeria akina Shittu, Etuhu, Mikel, Odemwingie, Yakubu na Martins.
Licha ya kumiliki mechi yote na pia Nigeria kucheza mtu 10 kipindi cha pili cha nyongeza ya dakika 30 baada ya Apam kutolewa kwa Kadi Nyekundu, Zambia walishindwa kupata goli.
Ndipo ikaja mikwaju mitano ya penalti na Zambia wakakosa moja iliyookolewa na Kipa Enyeama.
Nusu Fainali Nigeria watacheza na Watani wao wa Jadi Ghana.
Vikosi vilivyoanza:
Zambia: Mweene, Musonda, Sunzu, Himonde, Mbola, Chris Katongo, Nyirenda, Njobvu, Felix Katongo, Chamanga, Mulenga
Nigeria: Enyeama, Mohammed, Apam, Shittu, Echiejile, Etuhu, Kaita, Mikel, Odemwingie, Yakubu, Obasi
Nusu Fainali Alhamisi Januari 28
[saa 1 usiku]
Ghana V Nigeria
[saa 4 na nusu usiku]
Algeria V Misri

Monday 25 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Mafarao Nusu Fainali kuwakwaa wabaya wao Algeria!!!
Misri leo wameichabanga Cameroun mabao 3-1 katika mechi ya Robo Fainali iliyochezwa dakika 120 baada ya kuwa suluhu 1-1.
Cameroun walitangulia kufunga dakika ya 26 wakati kona ya Emana iliposindikizwa na Kepteni wa Misri Ahmed Hassan kwa kichwa wakati akigadi posti.
Lakini Ahmed Hassan, aliekuwa akicheza mechi yake ya 170 kwa Timu ya Taifa ikiwa ni rekodi, alisahihisha makosa hayo kwa kufumua shuti toka umbali wa Mita 34 na mpira kudunda mbele ya Kipa Kameni na kutikisa nyavu.
Hadi dakika 90 kumalizika mechi ilikuwa 1-1 na ndipo nusu saa ikaongezwa.
Dakika moja tu baada ya muda wa nyongeza kuanza, Fulbeki wa Cameroun, Geremi Njitap, alifanya kosa kubwa kwani mpira wake aliotaka kumrudishia Kipa wake ulikuwa mfupi na Gedo akaunasa na kuchomeka bao la pili.
Dakika 3 baadae, frikiki ya Kepteni wa Misri, Ahmed Hassan, ilipanguliwa na Kipa Kameni na kugonga mwamba wa juu kisha kudunda chini dhahiri ikiwa nje ya goli lakini Refa toka Afrika Kusini, Jerome, kimakosa akawapa Misri bao la 3 na kuwakata maini Cameroun.
Sasa Misri siku ya Akhamisi itacheza Nusu Fainali na Algeria Nchi ambayo wana uhasama wa jadi na wa kutisha na ambayo ndiyo iliwazuia kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini baada ya kuwafunga 1-0 katika mechi ya marudio huko Khartoum, Sudan iliyochezwa Novemba mwaka jana.
Muda si mrefu kuanzia sasa Robo Fainali ya mwisho kati ya Zambia na Nigeria itaanza na Mshindi wake atapambana na Ghana Nusu Fainali.
RATIBA: NUSU FAINALI
Alhamisi, Januari 28:
Ghana V Zambia/Nigeria
Algeria V Misri
KWA UFUPI TU………………..
• Gerrard yuko fiti
Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard amepona maumivu yake ya musuli wa mguu na kesho huenda akaonekana dimbani kucheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Wolves.
Gerrard aliumia Januari 13 kwenye mechi ya Kombe la FA waliyofungwa na Reading na kutolewa nje ya mashindano hayo.
• Kinda wa Man U aenda kwa Mwana wa Fergie!!!
Danny Welbeck, miaka 19, ambae ni Straika wa Manchester United amechukuliwa kwa mkopo na Preston North End hadi mwishoni mwa Msimu huu.
Preston ipo Daraja la Championship ambalo liko chini tu ya Ligi Kuu na Meneja wao ni Mtoto wa Sir Alex Ferguson aitwae Darren Ferguson.
• Ronaldo afunga 2, alambwa Nyekundu!
Cristiano Ronaldo hapo jana alifunga bao zote 2 za ushindi wa Real Madrid dhidi ya Malaga kwenye La Liga lakini akapewa Kadi Nyekundu dakika ya 70 baada ya mkono wake kumpiga Patrick Mtiliga wa Malaga na kumvunja pua.
• Mchezaji wa Paraguay ala shaba Mexico!!
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Paraguay anaecheza soka huko Mexico na Club America, Salvador Cabanas, miaka 29, amepigwa risasi kichwani na hali yake ni tete.
Cabanas aliwahi kuwa Mchezaji Bora wa Marekani Kusini mwaka 2007.
Dabi ya Milan: Mtu 9 Inter yawabwaga AC Milan!!
Inter Milan wamejivuta hadi pointi 9 mbele ya Mahasimu wao AC Milan baada ya kuwachapa 2-0 hapo jana kwenye mechi ya Serie A.
Inter ilibidi wacheze muda mwingi wa mechi hiyo wakiwa mtu 10 baada ya Wesley Sneijder kutwangwa Kadi Nyekundu na katika dakika 5 za mwisho walibaki mtu 9 baada ya Beki Lucio kutolewa kwa Kadi Nyekundu.
Mmoja wa watu walioshuhudia mechi hiyo ni Sir Alex Ferguson ambae alikuja kuwacheki wapinzani wao wa mwezi ujao kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE ACMilan.
Inter Milan walipata bao la kwanza kupitia Diego Milito na Goran Pandev akafunga bao la pili.
Ronaldinho aliwakosesha AC Milan bao wakati penalti yake iliyotolewa baada ya Mbrazil mwenzake Beki wa AC Milan Lucio kuunawa na hivyo kulambwa Kadi Nyekundu kuokolewa na Kipa wa Brazil Cesar.
Pengine Ferguson atapata moyo mkubwa kwa kuiona AC Milan butu lakini Chelsea watapata kiwewe kwa kuwaona wapinzani wao wa UEFA CHAMPIONS LEAGUE Inter Milan wakiwa wakali kama mbwa mwitu!
KOMBE LA AFRIKA: Leo Robo Fainali tena!!
Misri v Cameroun
Huko Benguela, Angola Uwanjani Ombaka, Mabingwa Watetezi Misri watajimwaga kuchuana na Timu ngumu Cameroun katika mechi ya kwanza ya leo ya Robo Fainali.
Mechi hii itaanza saa 1 kamili saa za bongo.
Zambia v Nigeria
Robo Fainali hii ya pili kwa leo itachezwa Uwanja wa Tundavala huko Lubango na itaanza saa 4 na nusu usiku saa za bongo.
Katika mechi ya leo Nigeria itamkosa Nahodha Joseph Yobo na Zambia itawakosa Kiungo Kalaba Rainford na Beki Kampamba Chintu ambao wamesimamishwa kwa kuwa na Kadi.
Algeria yawatoa Masupastaa kina Drogba!!!
• Algeria 3 Ivory Coast 2
Wengi walidhani Ivory Coast wametinga Robo Fainali pale Keita alipoingiza bao dakika ya 89 na kufanya gemu kuwa 2-1 lakini Algeria wakasawazisha dakika ya 90 kupitia Bougherra na ngoma ikaingizwa kwenye muda wa nyongeza wa nusu saa na ndipo Algeria wakaibuka kidedea baada ya Mchezaji wa Klabu ya Blackpool ya England, Bouazza, kupachika bao la 3 na la ushindi dakika ya 93.
Ivory Coast ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 4 Mfungaji akiwa Kalou na Algeria wakarudisha dakika ya 40 kwa bao la Matmour.
Algeria atacheza Nusu fainali na Mshindi wa leo kati ya Misri na Cameroun.
Wenger ajibebesha lawama!!
Arsene Wenger amekubali kuwa lawama zote za kutupwa nje ya Kombe la FA baada ya kuchapwa 3-1 na Stoke City hapo jana ni za kwake yeye baada ya kupanga Kikosi dhaifu.
Wenger amesema alikuwa hana njia ila kupanga Timu ya aina hiyo kwa vile wanakabiliwa na mechi ngumu mfululizo dhidi ya Aston Villa, Manchester United, Chelsea na Liverpool ndani ya siku 14 zijazo wakianzia Jumatano hii.

Sunday 24 January 2010

FA Cup: Raundi ya 5 tayari, mechi Februari 12 & 13
Mabingwa Watetezi wa Kombe la FA Chelsea wamepangwa kucheza nyumbani Stamford Bridge na watakumbana na Timu ya Daraja la chini Cardiff City.
Mpambano pekee uliothibitika wa Timu za Ligi Kuu ni ule wa kati ya Manchester City, watakaokuwa nyumbani, watakapocheza na Stoke City.
Mechi pekee ya Timu za Madaraja ya chini ni ile ya Reading v West Brom huku mechi nyingine zikitegemea nani atakuwa Mshindi wa mechi za marudiano kwa Timu zilizotoka sare Raundi ya 4.
RATIBA KAMILI:
[Timu inayotajwa kwanza ipo nyumbani]
Southampton v Portsmouth
Reading v West Bromwich Albion
Fulham v Notts County au Wigan Athletic
Chelsea v Cardiff City
Bolton Wanderers v Tottenham Hotspur au Leeds United
Derby County v Birmingham City
Manchester City v Stoke City
Wolverhampton Wanderers au Crystal Palace v Aston Villa
KOMBE LA AFRIKA: Wenyeji Angola waaga!!
Bao la dakika ya 16 la Asamoah Gyan limewaliza Angola na kuwatoa nje ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika mechi ya Robo Fainali iliyofanyika Mjini Luanda, Angola Uwanja wa Novemba 11 mbele ya halaiki ya Waangola waliohuzunika.
Baada ya bao la Gyan, Angola walifanya wimbi kufuatia wimbi la mashambulizi lakini umaliziaji wao ulikuwa dhaifu hasa Mshambuliaji Manucho aliepata nafasi kadhaa za wazi na pia umahiri wa Kipa wa Ghana Kingston ndio uliowaua Angola.
Ghana wameingia Nusiu Fainali na watakutana na Mshindi kati ya Zambia au Nigeria na mechi hiyo ya Nusu Fainali itachezwa Alhamisi tarehe 28 Januari.
Baada ya muda mfupi ujao, Ivory Coast wataingia dimbani kucheza na Algeria kwenye mechi ya pili ya Robo Fainali ya leo.
Rooney awania kuvunja rekodi yake!!
Wayne Rooney anapigania kuivunja rekodi yake ya kufunga Magoli 23 kwa Msimu aliyoiweka huko nyuma na mpaka sasa ameshafunga Mabao 19 yakiwemo mabao manne aliyofunga jana kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Old Trafford dhidi ya Hull City.

Rooney, miaka 24, ametamka: “Ni mara yangu ya kwanza kufunga bao 4 kwenye mechi moja katika mpira wa kulipwa! Nataka nizipiku goli 23 nilizowahi kufunga Msimu mmoja na sasa nina goli 19 na bado mechi kama 20 hivi!”
Rooney akaongeza: “Tofauti Msimu huu ni kuwa naingia sana ndani ya boksi na nakuwepo kwenye nafasi za kufunga magoli!”
Hata Meneja wa Hull City, Phil Brown, amekiri: “Ni wazi ni Straika bora duniani! Ana uwezo wa kufunga ukimpa nusu upenyo tu! Hii ni hali nzuri kwa England kwenye Fainali za Kombe la Dunia!”
WAFUNGAJI BORA LIGI KUU:
1 Wayne Rooney Magoli 19
2 Jermaine Defoe 14
3 Didier Drogba 14
4 Darren Bent 14
5 Fernando Torres 12
6 Carlos Tevez 12
7 Louis Saha 11
8 Cesc Fabregas 11
9 Gabriel Agbonlahor 8
10 Carlton Cole, Arshavin, Berbatov, Cole, Kuyt Goli 7 kila mmoja
FA Cup: Arsenal nje!!!
• Stoke City 3 Arsenal 1
Sol Campbell leo ameanza kibarua chake Arsenal kwa kipigo kwenye Uwanja wa Britannia cha 3-1 na Stoke City kwenye mechi ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA na hivyo kubwagwa nje ya Mashindano hayo.
Arsenal wakichezesha Kikosi cha mchanganyiko cha Maveterani kama kina Campbell na Silvestre na Chipukizi kina Eastmond, Coqquelin na Vela walijikuta wako nyuma baada ya dakika moja tu mechi kuanza baada ya silaha yao kubwa ya Stoke City ya mipira ya kurushwa ya Rory Delap kutumika na mpira huo wa kurusha kumkuta Straika Ricardo Fuller ndani ya boksi  aliemaliza kwa kichwa.
Arsenal walisawazisha dakika ya 44 baada ya frikiki ya Fabregas kupasiwa Denilson aliefumua shuti lililobabatiza Wachezaji wawili wa Stoke na kumhadaa Kipa Sorensen na kutikisa nyavu.
Alikuwa Fuller tena aliepachika bao la pili dakika ya 77 baada ya Sidibe kumfunga tela Denilson winga ya kulia na kutia krosi iliyopigwa kichwa na Fuller.
Dean Whitehead akapigilia nsumari wa mwisho dakika ya 86 kwa bao tamu na kuifanya Arsenal kujumuika na Manchester United na Liverpool kuwa Watazamaji maarufu wa FA Cup.
Vikosi vilivyoanza:
Stoke: Sorensen, Huth, Shawcross, Higginbotham, Collins, Delap, Whitehead, Whelan, Etherington, Sidibe, Fuller.
Akiba: Simonsen, Lawrence, Beattie, Pugh, Diao, Sanli, Wilkinson.
Arsenal: Fabianski, Coquelin, Campbell, Silvestre, Traore, Eastmond, Denilson, Fabregas, Walcott, Emmanuel-Thomas, Vela.
Akiba: Mannone, Rosicky, Eduardo, Ramsey, Arshavin, Bartley, Frimpong.
Refa: Martin Atkinson
FA Cup: Dro ya Raundi ya 5 kufanyika leo usiku!!
Mabingwa Watetezi Chelsea pamoja na Timu nyingine 11 za Ligi Kuu wanasubiri kujua watapangiwa kucheza na nani katika mechi za Raundi ya 5 ya Kombe la FA zitakazochezwa Februari 12 na 13.
Dro ya mechi hizo inafanyika leo Jumapili Januari 24 saa 3 usiku saa za bongo.
Timu zitakazopigiwa kura ni:
1 Southampton
2 Reading
3 Derby County
4 Cardiff City
5 Stoke City
6 Notts County au Wigan Athletic [mechi inarudiwa]
7 Scunthorpe United au Manchester City [mechi inachezwa saa hizi]
8 West Bromwich Albion
9 Birmingham City
10 Fulham
11 Bolton Wanderers
12 Portsmouth
13 Chelsea
14 Aston Villa
15 Wolverhampton Wanderers au Crystal Palace [mechi inarudiwa]
16 Tottenham Hotspur au Leeds United [mechi inarudiwa]
Hamburg wamchota Van Nistelrooy
Mshambuliaji wa Real Madrid Ruud van Nistelrooy amejiunga na Hamburg ya Ujerumani kwa mkataba wa miezi 18-month.
Veterani huyo mwenye umri wa miaka 33 alihusishwa na kuhamia England aidha West Ham au Tottenham lakini Tottenham ikajitoa kumchukua walipoona hawatomudu Mshahara wake wakati Mchezaji mwenyewe aliikataa West Ham.
Van Nistelrooy amekuwa hapati namba Real na kuhama kwake ni kutafuta namba ya kudumu ili apate nafasi ya kuchukuliwa Timu ya Taifa ya Uholanzi kuchezea Kombe la Dunia mwezi Juni huko Afrika Kusini.
KOMBE LA AFRIKA: Robo Fainali zaanza leo!!!
Angola v Ghana
Leo Robo Fainali ya kwanza itakayoanza saa 1 usiku saa za bongo ni ile itakayopigwa Uwanja wa Novemba 11 huko Luanda, Angola na ni kati ya Wenyeji Angola na Ghana.
Angola watafarijika na kupata morali kubwa kwa habari kuwa Flavio ambae ndie Mfungaji Bora wa Mashindano haya mpaka sasa yuko fiti kucheza.
Flavio hakucheza mechi ya mwisho Angola walipokutana na Algeria.
Wakati Ghana walipata shida kutinga Robo Fainali baada ya kupigwa 3-1 na Ivory Coast na kisha kuifunga Burkina Faso 1-0, Wenyeji Angola kwao ilikuwa nafuu kidogo kwani walitoka sare 4-4 na Mali, wakaifunga Malawi 2-0 na kutoka sare 0-0 na Algeria.
Ivory Coast v Algeria
Huko Cabinda, Angola Uwanja wa Taifa wa Chiazi, Ivory Coast na Algeria zitashuka kukwaana katika mechi ya Robo Fainali huku wengi wakiwapa Ivory Coast wenye Mastaa wakubwa kina Drogba na Ndugu wawili Kolo Toure na Yaya nafasi kubwa ya ushindi.
Lakini Algeria si Timu ya mchezo na wengi watakumbuka walivyoiadhiri Misri na kuwabwaga nje ya Kombe la Dunia.
Ivory Coast walikuwa na njia nyepesi kuingia Robo Fainali kwani walicheza mechi mbili tu baada ya Togo kujitoa toka Kundi lao kufuatia maafa waliyopata na katika mechi hizo walitoka droo na Burkina Faso na kisha kuwafunga Ghana 3-1.
Algeria wao walipigwa mechi ya kwanza 3-0 na Malawi, wakafufuka na kuwakung’uta Mali 2-0 na kisha kutoka sare 0-0 na Wenyeji Angola.
Everton wambeba Senderos kwa mkopo
Everton na Arsenal zimekubaliana Mchezaji Philippe Senderos aende Everton kwa mkopo hadi mwishoni mwa Msimu huu.
Mlinzi huyo wa Arsenal kutoka Uswisi mwenye umri wa miaka 24, amekuwa hana namba Arsenal na Everton wamelazimika kumchukua baada ya kupata pengo kufuatia kuhama kwa Beki wao Lucas Neill aliehamia Klabu ya Uturuki Galatasaray.
Senderos alijunga Arsenal mwaka 2003 kutoka Klabu ya Uswisi Servette na ameichezea Arsenal mechi 117 lakini Msimu uliokwisha alipelekwa AC Milan kwa mkopo na tangu arudi hapo Klabuni amekuwa hapewi namba.
Senderos amesema: “Nataka niondoke! Nataka niwe nacheza ili niwe fiti kwa Fainali za Kombe la Dunia!”
Powered By Blogger