KOMBE LA AFRIKA: Mafarao Nusu Fainali kuwakwaa wabaya wao Algeria!!!
Misri leo wameichabanga Cameroun mabao 3-1 katika mechi ya Robo Fainali iliyochezwa dakika 120 baada ya kuwa suluhu 1-1.
Cameroun walitangulia kufunga dakika ya 26 wakati kona ya Emana iliposindikizwa na Kepteni wa Misri Ahmed Hassan kwa kichwa wakati akigadi posti.
Lakini Ahmed Hassan, aliekuwa akicheza mechi yake ya 170 kwa Timu ya Taifa ikiwa ni rekodi, alisahihisha makosa hayo kwa kufumua shuti toka umbali wa Mita 34 na mpira kudunda mbele ya Kipa Kameni na kutikisa nyavu.
Hadi dakika 90 kumalizika mechi ilikuwa 1-1 na ndipo nusu saa ikaongezwa.
Dakika moja tu baada ya muda wa nyongeza kuanza, Fulbeki wa Cameroun, Geremi Njitap, alifanya kosa kubwa kwani mpira wake aliotaka kumrudishia Kipa wake ulikuwa mfupi na Gedo akaunasa na kuchomeka bao la pili.
Dakika 3 baadae, frikiki ya Kepteni wa Misri, Ahmed Hassan, ilipanguliwa na Kipa Kameni na kugonga mwamba wa juu kisha kudunda chini dhahiri ikiwa nje ya goli lakini Refa toka Afrika Kusini, Jerome, kimakosa akawapa Misri bao la 3 na kuwakata maini Cameroun.
Sasa Misri siku ya Akhamisi itacheza Nusu Fainali na Algeria Nchi ambayo wana uhasama wa jadi na wa kutisha na ambayo ndiyo iliwazuia kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini baada ya kuwafunga 1-0 katika mechi ya marudio huko Khartoum, Sudan iliyochezwa Novemba mwaka jana.
Muda si mrefu kuanzia sasa Robo Fainali ya mwisho kati ya Zambia na Nigeria itaanza na Mshindi wake atapambana na Ghana Nusu Fainali.
RATIBA: NUSU FAINALI
Alhamisi, Januari 28:
Ghana V Zambia/Nigeria
Algeria V Misri
No comments:
Post a Comment