Yanga wajikita kileleni
Alhamisi, Septemba 23
Yanga leo wamejichimbia kileleni mwa LIGI KUU VODACOM baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 2-0 katika Uwanja wa Jamhuri huko Morogoro.
Wafungaji wa Yanga walikuwa ni Jerry Tegete na Mghana Ernest Boarkye.
Kwa ushindi huo, Yanga wamejikita kinarani kwa pointi 4 mbele wakiwa na pointi 13 kwa mechi 5.
Simba, ambao wako nafasi ya pili, wanacheza Jumamosi na Toto African huko Mwanza.
MAKUNDI/RATIBA KOMBE LA KINAMAMA TAYARI!!!!
• Twiga Stars Kundi Gumu!
Jumatano, Septemba 22
TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ itaanza kampeni zake za Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa kumenyana na Wenyeji wa michuano hiyo, Afrika Kusini maarufu kama Banyana Banyana na Timu nyingine kwenye Kundi A ni Mali na Nigeria.
Kundi B wapo Bingwa Mtetezi Equatorial Guinea, Ghana, Cameroon na Algeria.
Michuano hiyo itaanza Mwezi ujao Oktoba 29 na kumalizika Novemba 14 Bingwa pamoja na Mshindi wa Pili watashiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake zitakazofanyika Ujerumani Mwakani.
Katika timu hizo nane, Tanzania ndio inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.
Twiga Stars ilishacheza mechi ya kirafiki na Banyana Banyana takriban mwezi mmoja na nusu uliopita na kufungwa mabao 6-0.
Timu hiyo pia ilifanya ziara huko Marekani ambapo walikaa kambini kwa wiki tatu na kucheza mechi kadhaa za kirafiki
Yanga kulipa Wachezaji Milioni 250?
Alhamisi, Septemba 2
Kuna hatari kubwa Klabu ya Yanga ikalazimika kuwalipa Wachezaji wake wanne iliyowakata bogi fidia ya Shilingi Milioni 250 kufuatia malalamiko ya Wachezaji hao yaliyowasilishwa TFF na Chama cha Kutetea Maslahi ya Wanakandanda Tanzania.
Wachezaji hao wanne waliotemwa na ambao wanadai Mikataba yao ilivunjwa kinyume cha sheria ni Steven Malashi, Wisdom Ndhlovu, Ally Msigwa na John Njoroge.
Malashi, ambae inadaiwa alikuwa na Mkataba hadi Msimu wa 2012/13, anadai fidia ya Shilingi 37,500,000/-, Beki kutoka Malawi Ndhlovu, ambae inasemekana Mkataba wake ungeisha 2012, anadai 82,000,000/-, Msigwa, mwenye kudai alikuwa na Mkataba hadi 2012/13, anadai 89,700,000/- na Beki wa Kenya Njoroge anadai 44,000,000/-.
Hata hivyo taarifa ndani ya Yanga zimesema Wachezaji hao hawakusajiliwa na TFF hivyo wao hawawajibiki kwa lolote kuhusu Wachezaji hao.
Simba kuhamia CCM Kirumba
Jumanne, Agosti 31
Baada ya Uwanja wa Uhuru kufungwa Wiki iliyopita kwa ajili ya matengenezo ya Miezi mitatu, Klabu ya Simba imeamua kuhamishia Mechi zake za nyumbani za LIGI KUU VODACOM huko Mwanza na kuutumia Uwanja wa CCM Kirumba.
Timu zenye makazi Jijini Dar es Salaam, Yanga, Simba, Azam FC, JKT Ruvu na African Lyon, huutumia Uwanja wa Uhuru kama wa nyumbani.
Timu hizo zimekuwa zikijaribu kuishawishi Serikali iruhusu Uwanja mpya, Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuchukua Watazamaji Elfu 60, lakini inaelekea hilo limegonga mwamba.
LIGI KUU VODACOM ilianza Agosti 21.
Mbali ya Simba, Timu nyingine zilizoathirika na kufungwa Uwanja wa Uhuru hazijatangaza zitatumia Viwanja vipi.
Ngorongoro Heroes nje CECAFA U-20
Jumanne, Agosti 24
Timu ya Taifa ya Tanzania ya Vijana chini ya Miaka 20, Ngorongoro Heroes, imeifunga Sudan 1-0 lakini hata hivyo imetolewa nje ya Mashindano.
Kwenye Kundi lao ni Wenyeji Eritrea na Kenya ndizo zilizosonga mbele.
Kundi B ni Uganda na Rwanda ndizo zimetinga Nusu Fainali.
Kwenye hiyo Nusu Fainali Eritrea itacheza na Rwanda na Uganda itakumbana na Kenya.
Katika Mashindano hayo Ngorongoro Heroes ilifungwa 1-0 na Eritrea, kutoka sare 1-1 na Somalia na kuchapwa 3-0 na Kenya.
Wakati huo huo, Timu ya Zanzibar kwenye Mashindano hayo imepatwa na skandali baada ya CECAFA kubaini kuwa Mchezaji wao Said Mussa Shaban ana utata wa umri wake huku Pasi yake ikionyesha kazaliwa Aprili, 1989 na Kadi ya Usajili kuonyesha kazaliwa 5 Desemba 1993.
Kanuni za Mashindano hayo inaruhusu Wachezaji wale tu waliozaliwa tarehe 1 Januari 1991 au baada ya hapo.
Kwa kosa hilo, Zanzibar ilifutiwa ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Yemen na kuhesabiwa imefungwa 3-0 na pia Kamati Kuu ya CECAFA itakaa kuamua adhabu gani ya ziada ipewe Zanzibar.
Poulsen ataja Kikosi cha Taifa Stars kucheza na Algeria
Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Jan Polsen, ameteua Wachezaji 26 watakaoingia kambini na baadae kuchujwa kufikia 20 ili kwenda kupambana na Algeria mapema Mwezi ujao kwa ajili ya Mechi za Mtoano za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Timu nyingine kwenye Kundi la Taifa Stars ni Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Miongoni mwa Wachezaji hao walioteuliwa ni pamoja na Kipa Juma Kaseja alieumia mkono na ambae inasemekana hataweza kucheza mechi hiyo na Algeria.
Pamoja na Kaseja wapo Makipa Jackson Chive toka Azam na Shaaban Hassan wa Mtibwa Sugar.
Wachezaji wengine ni: Shadrack Nsajigwa (Yanga), Salum Kanoni (Simba), Aggrey Morris (Azam FC), Erasto Nyoni (Azam FC), Nadir Haroub (Yanga), Kevin Yondani (Simba), Stephano Mwasika (Yanga), Juma Jabu (Simba), Henry Joseph ( Kongsivinger ya Norway), Jabir Aziz (Azam FC), Athumani Idd (Yanga), Nurdin Bakari (Yanga), Abdulhalim Humoud (Simba), Abdi Kassim (Yanga), Seleman Kassim (Azam Fc), Idrisa Rajabu (Sofapaka ya Kenya), Uhuru Suleiman (Simba), Danny Mrwanda (anaecheza Nchini Vietnam), Nizar Khalfan (Vancouver White Caps ya Canada), Mrisho Khalfan Ngassa (Azam), Mussa Hassan Mgosi (Simba), John Bocco, (Azam FC) na Jerson Tegete (Yanga).
LIGI KUU VODACOM Msimu 2010/11: Kuanza leo!
Jumamosi, Agosti 21
Baada ya Yanga na Simba kuanua pazia la Msimu mpya wa 2010/11 kwa kugombea Ngao ya Hisani ambapo Yanga waliinyuka Simba kwa mikwaju 3-1 ya penalti, leo Timu zote 12 za LIGI KUU VODACOM zinatinga dimbani kuanza kampeni zao za Msimu mpya.
RATIBA:
Simba v African Lyon
Polisi Dodoma v Yanga
Majimaji Songea v Mtibwa Sugar
Kagera Sugar v JKT Ruvu
AFC Arusha v Azam FC
Ruvu Shooting v Toto African
Taifa Stars v Mafarao Agosti 11
Jumamosi, Julai 31
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itacheza Mechi ya kirafiki na Egypt huko Cairo hapo Agosti 11.
Habari hizo zimetolewa na TFF ambao wamesema Mechi hiyo ipo kwenye Kalenda ya FIFA ya Mechi za Kimataifa.
Hii itakuwa Mechi ya kwanza kwa Kocha mpya wa Taifa Stars anaetoka Denmark, Jan Poulsen.
Poulsen ametwaa wadhifa huo baada ya Mbrazi Marcio Maximo kumaliza Mkataba wake.
Taifa Stars inategemewa kucheza Mechi za Mchujo kuwania kuingia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazochezwa huko Gabon na Equatorial Guinea Mwaka 2012 na itacheza ugenini Mwezi ujao na Algeria na Oktoba itapambana na Morocco.
Rage akerwa na Phiri
Jumapili, Julai 25
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phri hajarudi toka kwao Zambia na hali hiyo imemtibua Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, ambae ameamua kumwandikia barua akitaka maelezo kwa nini ana tabia ya kuchelewa kuripoti kazini kila anapoenda likizo.
Rage amesema wamechoshwa na vitendo hivyo ambavyo huathiri programu za mazoezi yao.
Tayari Simba imeshaanza mazoezi bila ya Phiri wakiwa chini ya Supa Kocha Syllersaid Mziray kwa ajili ya Msimu ujao wa Ligi Kuu Vodacom unaoanza Agosti 21 lakini Agosti 14 wana kindumbwendumbwe cha mechi ya fungua pazia kugombea Ngao ya Hisani dhidi ya Mahasimu wao wakubwa Yanga.
Rage, akitoa mfano wa Phiri kuchelewa kurudi na kuwafanya wacheze na Yanga Aprili 18 bila ya yeye, amesema wameomba ushauri wa Wakili Jijini Dar es Salaam ili aupitie Mkataba wa Phiri na kuangalia jinsi ya kuutengua.
Banyana Banyana 6 Twiga Stars 0
Jumapili, Julai 25
Jana, Timu ya Taifa ya Wanawake wa Tanzania, Twiga Stars, imetandikwa bao 6-0 huko Afrika Kusini ilipoenda kucheza mechi moja na wenzao, Banyana Banyana.
Hadi mapumziko, Twiga Stars walikuwa nyuma kwa bao 3-0.
Mwezi Oktoba, Twiga Stars itarudi tena Afrika Kusini kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.
Twiga Stars wanategemewa kurudi Dar es Salaam leo na kisha kuendelea na kambi yao tayari kwa safari ya mazoezi huko Marekani.
Uongozi mpya Yanga wateua Kamati mbalimbali
Ijumaa, Julai 23
Mwenyekiti mpya wa Yanga, Lloyd Nchunga, ametangaza kuwa Mchezaji wao wa zamani, Salvatory Edward, ameteuliwa kuwa Kocha Msaidizi chini ya Kocha Mkuu Papic.
Na aliekuwa Meneja wa Klabu hiyo, Kenneth Mkapa, amepewa wadhifa wa kuwa Kocha Mkuu wa Timu B.
Vile vile, Nchunga alitangaza uteuzi wa Kamati mbali mbali za kuusaidia uongozi wake na baadhi ya Viongozi wa zamani wamechomekwa kwenye hizo Kamati.
Kamati ya Utendaji itakuwa na Seif Said, Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga.
Kamati ya Nidhamu itaongozwa na Wakili Mark Antony akisaidiwa na Wakili mwingine Rogers Ishengoma, Mwamuzi Msafiri Mkeremi na Mbunge wa huko Zanzibar Jimbo la Dimani, Hafidh Ali.
Kamati ya Mipango ni Mwenyekiti Charles Mgondo akisadiwa na Salum Rupia, David Mataka, Isaac Mazwile, Michael Malebo na Abel Mtaro.
Kamati ya Ufundi Mwenyekiti ni Mohamed Bhinda na wengine ni Ally Mayai 'Tembele', Sekilojo Chambua, Paul Malume, Edgar Chibura, Maneno Tamba na Abeid Abeid 'Falcon'
Kamati ya Mashindano itaundwa na Seif Seif 'magari', Majid Seif, Abdallah Binkreb, Muzamili Katunzi, Albert Marwa, Moses Katabaro na Lameck Nyambaya.
Kamati ya kuratibu shuguli za Matawi itaundwa na Tito Osoro, Kibwana Matokeo, Ali Kamtande, Theonest Rutashoborwa, Mzee Yusuf, Sarah Ramadhan na Athuman Fumo.
Kamati pekee ambayo haikuguswa na itabaki kama Uongozi mpya walivyoikuta ni Kamati ya Uchaguzi na itaendelea kuongozwa na Jaji John Mkwawa, Makamu Mwenyekiti ni Ridhiwani Kikwete na wengine ni Philemon Ntahilaja, Yusuf Mzimba na Angetile Oseah.
Viongozi wapya Yanga waanza kwa suluhu!
Jumatano, Julai 21
Mwenyekiti mpya wa Yanga, Lloyd Nchunga, ameanza rasmi wadhifa wake kwa nia njema ya kutaka kuleta umoja na maelewano pale alipomwandikia barua Francis Kifukwe, ambae ni Rais wa zamani wa Yanga na aliekuwa Mgombea wa Uenyekiti kwenye Uchaguzi wa Jumapili lakini akajitoa sekunde za mwisho kwa madai ya mizengwe, na kumwomba awe mmoja wa Wadhamini wa Yanga.
Barua hiyo ya Mwenyekiti wa Yanga imewataja Wadhamini wengine wa Klabu hiyo kuwa ni Mfadhili wao Mkuu, Yusuf Manji, na Mama Fatma Karume, ambae ni Mama Mzazi wa Rais wa Zanzibar, Abeid Karume.
Inasemekana Kifukwe amekubali kuwa amepokea barua hiyo na baada ya muda ataijibu ipasavyo.
Katika Uchaguzi wa Jumapili, Lloyd Nchunga alishinda kwa kishindo uchaguzi na kuchukua wadhifa wa Uenyekiti na Makamu wake ni Davies Mosha.
LIGI KUU BARA: Ratiba nje!
Jumanne, Julai 20
Ratiba ya LIGI KUU BARA imetolewa leo na sokomoko litaanza Agosti 21 kwa Mabingwa Watetezi Simba kucheza na African Lyon Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam na Yanga kucheza ugenini huko Dodoma dhidi ya Polisi, Timu ambayo imepanda Daraja.
Mechi nyingine siku hiyo hiyo ni AFC Arusha v Azam, huko Arusha Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Majimaji v Mtibwa Sugar huko Songea, Toto African v Ruvu Shooting, Kagera Sugar v JKT Ruvu.
BIGI MECHI ni Okotoba 16 Simba v Yanga na watarudiana Machi 5 Mwakani.
Lakini, Agosti 14, Mahasimu hao wakubwa, Yanga v Simba, watakuwa na mechi ya fungua pazia ya Msimu mpya kugombea Ngao ya Hisani.
Hatimaye Yanga yapata Viongozi
Jumatatu, Julai 19
Jana kwenye Uchaguzi Mkuu wa Yanga uliofanyika Ukumbi wa PTA Jijini Dar es Salaam, Wanachama wa Yanga licha ya kukumbwa na mizengwe mingi iliyofikia hadi Mgombea wa Uenyekiti, Francis Kifukwe kujitoa hapo hapo uchaguzini, waliweza kumchagua Mwenyekiti mpya, Makamu wake na Wajumbe wa Kamati ya Utendaje.
Loyd Nchunga ndie aliechaguliwa Mwenyekiti mpya na Makamu wake ni David Mosha.
Mgombea ambae alipewa nafasi kubwa ya kunyakua kiti cha Uenyekiti, Francis Kifukwe, alijitoa hapo hapo kwenye Ukumbi wa PTA dakika za mwisho kabla Uchaguzi haujaanza kwa madai kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki.
Licha ya kusihiwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, aliekuwa hapo kama Mgeni rasmi, Kifukwe aligoma kushiriki kwenye Uchaguzi huo.
Ijumaa, Julai 2
Kocha Maximo aagwa
Kocha wa Taifa Stars kutoka Brazil, Marcio Maximo, ameagwa rasmi katika sherehe fupi ambazo TFF iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake Fredrick Mwakalebela zilizofanyika Mikocheni.
Maximo alitoa shukrani zake kwa Viongozi wa Tanzania kwa kumpa kila msaada katika Miaka minnne aliyokuwa Tanzania na pia kumtakia kila la kheri Kocha mpya kutoka Denmark, Jan Poulsen, atakaeanza kazi Agosti 1.
Katika sherehe hizo Wadhamini wakubwa wa Taifa Stars, Kampuni ya Bia ya Serengeti na Benki ya NMB, waliwakilishwa.
Serikali iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Seth Kamuhanda.
Wachezaji wa Taifa Stars waliwakilishwa na Nahodha wao Shadrack Nsajigwa.
Jumatano, Juni 30
Wanne wapigwa shoka Yanga!!
Kamati ya Uchaguzi ya Yanga imewapiga panga Wagombea wanne baada ya kuwekewa pingamiza akiwemo Francis Kifukwe, aliekuwa Rais wa zamani wa Yanga, ambae safari hii alitaka kugombea Uenyekiti.
Wengine waliokatwa ni Katibu mkuu wa zamani wa FAT, Ali Mwanakatwe, Abeid Abeid aka Falcon na Hashim Lundenga.
Uchaguzi wa Yanga utafanyika Julai 18.
Baada ya kukatwa Kifukwe, Wagombea waliobaki nafasi ya Mwenyekiti ni Lloyd Mchunga, Mbaraka Igangula na Edgar Chibula
Wagombea wa Makamu Mwenyekiti ni Constatine Marigo, Ayubu Nyenza na David Mosha.
Jumanne, Juni 29
Wabunge waombwa kuchangia Twiga Stars
Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, ambayo imefuzu kuingia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake yatayofanyika Oktoba huko Afrika Kusini, imepigiwa chapuo huko Bungeni Dodoma ili Wabunge waichangie.
Ombi la kuichangia Timu hiyo itakayoingia kambini hivi karibuni lilitolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera.
Twiga Stars itashiriki Fainali hizo pamoja na Mali, Senegal, Nigeria, Algeria, Equatorial Guines, Ghana na Wenyeji Afrika Kusini.
Waziri Bendera pia alisema Makocha wa Timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake Mohammed ‘Adolf’ Rishad, watazunguka Nchi nzima kusaka Wanawake wenye vipaji ili kuimarisha Timu hiyo.
Ijumaa, Juni 24
UCHAGUZI YANGA: Kifukwe awekewa pingamizi
Francis Kifukwe, aliewahi kuwa Kiongozi Yanga, anaegombea nafasi ya Uenyekiti kwenye Uchaguzi Mkuu Yanga utakaofanyika Julai 18, amewekewa pingamizi na Mwanachama mmoja wa Yanga, Selemani Kato wa Kariakoo.
Wanachama wa Yanga wanaruhusiwa kutoa pingamizi zao hadi Jumamosi Juni 26 kwa Mgombea yeyote na Kifukwe amekuwa Mgombea wa kwanza kupingwa.
Madai ya Mwanachama huyo kumpinga Kifukwke yanahusu kushindwa kwake kutoa Mahesabu ya Mapato na Matumizi wakati wa Uongozi wake hapo nyuma na pia kushindwa kwake kuumaliza mgogoro mkubwa ulioikumba Yanga wakati wake uliozua Makundi ya ‘Yanga Asili’ na ‘Yanga Kampuni’.
Wagombea wengine wa nafasi ya Uenyekiti ni Ally Mwanakatwe, Lyod Mchunga, Mbaraka Igangula, Edgar Chibula na Abeid Abeid.
Jumamosi, Juni 19
TFF kudhibiti Wageni Ligi Kuu Bara
Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, limesisitiza kuwa uamuzi wa kila Klabu Ligi Kuu Bara kutosajili zaidi ya Wachezaji watano toka nje ya Nchi uko palepale kwa vile sheria hiyo ilishakubalika na Klabu zote tangu Mwaka jana na pia ilikubaliwa ianze kutumika Msimu wa 2010/11.
Inadaiwa Klabu vigogo, Yanga na Simba, hawaitaki sheria hiyo kwa vile tayari washawachukua Wageni zaidi ya watano na hivyo wanataka kuleta shinikizo ifutwe.
Alhamisi, Juni 17
Memba Yanga wagwaya kugombea!!!
Ikiwa imebaki siku moja tu kabla kufungwa kwa uchukuaji fomu kwa ajili ya kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Yanga utakaofanyika Julai 18 ni Wanachama 20 tu wamechukua fomu na kati yao ni wawili tu ndio wanagombea uongozi wa juu na huku 18 wakiwania Ujumbe wa Kamati Kuu.
Wagombea hao wawili wanaowania nafasi za juu ni Baraka Igangula anaegombea Uenyekiti na Ayoub Nyenza anaewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Hata hivyo katika duru za Yanga kuna minong’ono ya Majina makubwa kuchukua fomu dakika za lala salama na yanayotajwa ni Viongozi wa zamani Francis Kifukwe na Jamal Malinzi huku Mfadhili Mkuu Yusuf Manji akitajwa kwamba atawania Uenyekiti.
Pia, minong’ono hiyo inawataja Mwenyekiti wa zamani FAT, Muhidin Ndolanga na hata Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa, Idd Kipingu, anahusishwa.
Baadhi ya Watu waliochukua fomu kugombea Ujumbe ni Omary Ndulla, Yusuf Yassin, Atufigwegwe Mwakatumbula, Mwinyi Mangale, Lameck Nyambea, Robert Kasela, Tito Oselo, Dr Evans Matee na Seif Mohamed.
Inategemewa Majina ya Wagombea rasmi itatangzwa Jumatatu ijayo baada ya Kamati ya Uchaguzi chini ya Jaji John Mkwawa kuyapitia.
Jumamosi, Juni 12:
CHALENJI 2010 ni Bongo!!
TFF imetoa Kalenda yake ya Msimu wa 2010/11 na imethibitisha kuwa Tanzania ndio watakuwa Wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, yaani CECAFA Senior Challenge Cup.
Mashindano hayo yatachezwa kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 5, 2010.
Mwaka 2009, Kenya ndio walikuwa Wenyeji wa Mashindano hayo ambayo Uganda ndio waliibuka kidedea kwa kuchukua Ubingwa.
Katika Kalenda hiyo ya TFF kuna Ligi ya Vijana chini ya Miaka 20 itakayoaanza Mwezi Novemba.
Pia TFF imeweka kwenye Kalenda Ligi za Wanawake kuanzia ngazi za Wilaya, Mikoa na Taifa.
TFF bado yamtambua Madega
Kwa mujibu wa TFF, Imani Madega bado ni Mwenyekiti wa Yanga licha ya kudaiwa kuondolewa na Wanachama wa Yanga.
Hapo Juni 6 kwenye Mkutano Mkuu wa Yanga uliofanyika Bwalo la Polisi, Oyster Bay, Jijini Dar es Salaam, Wanachama walidai muda wa Madega ulikwisha Mei 30 hivyo wakamng’oa na kumweka Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Jaji John Mkwawa, kama Kiongozi wa muda mwenye jukumu la kuitisha Uchaguzi Juni 27.
TFF imedai kuwa Madega bado ni halali na ndie mwenye jukumu la kusaini mabadiliko ya Katiba kama yavyotakiwa na TFF na kuyarudisha TFF kwa kupitiwa na kupitishwa.
Jumanne, Juni 8
Dunga aisifia Tanzania
Baada ya kuipiga Taifa Stars mabao 5-1 hapo jana Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Kocha wa Brazil Dunga aliimwagia sifa Timu ya Tanzania.
Dunga alisema: ‘Ilikuwa ni majaribio mazuri kwa Brazil kwani Tanzania ni Timu nzuri sana waliojipanga vizuri. Nia yetu ilikuwa kucheza na Timu zenye kasi, nguvu na kwa hiyo ni vizuri tumecheza na Tanzania na Zimbabwe.”
Dunga alimaliza kwa kusema yeye kama Wabrazil wote anataka kushinda Kombe la Dunia.
Katika mechi ya jana, Mabao ya Brazil yalifungwa na Robinho na Ramirez, waliofunga bao 2 kila mmoja, na moja alifunga Kaka.
Bao la Taifa Stars lilifungwa na Jabir Aziz.
Twiga Stars kwenda USA
Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, ambayo imefuzu kuingia Fainali za Kombe la Afrika kwa Wanawake baada ya kuwabwaga Eritrea, itapelekwa Marekani na Mlezi wa Timu hiyo Bibi Rahma Al-Kharoosi ili ikafanye mazoezi ya Wiki mbili baada ya kuwaahidi tripu hiyo ikiwa watashinda.
Twiga Stars iliitoa Eritrea kwa jumla ya Mabao 11-4 baada ya kushinda Mechi ya kwanza Jijini Dar es Salaam kwa bao 8-1 na kutoka sare 3-3 huko Asmara, Eritrea.
Wakiwa huko Marekani watacheza Mechi 4 za kirafiki.
Maximo kurithiwa na Kocha toka Denmark
Jan B Poulsen, Miaka 64, anaetoka Denmark ndie atarithi nafasi ya Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Marcio Maximo, kuanzia Julai kwa Mkataba wa Miaka Miwili.
Habari hizo za uteuzi wa Kocha huyo mpya zimethibitishwa na TFF ambao wamesema jumla ya Makocha 59 waliomba nafasi hiyo.
Poulsen, mwenye sifa za Ukocha zinazotambuliwa na FIFA, ameshashika nyadhifa mbalimbali zikiwemo za kuwa Kocha Msaidizi wa Denmark na pia kuifundisha Timu ya Taifa ya Singapore.
Ijumaa, Juni 4
Taifa Stars v Brazil: Ulinzi mkali!!
Jeshi la Polisi limeahidi ulinzi mkali kwenye ziara ya Brazil Nchini Tanzania wanaotegemewa kutua Dar es Salaam Jumapili usiku wakitokea Afrika Kusini waliko kwa ajili ya Kombe la Dunia na Jumatatu jioni kucheza na Taifa Stars Uwanjani Uhuru kisha kuondoka kurudi Afrika Kusini mara baada ya mechi hiyo.
Polisi wamesema Siku ya Jumamosi watafanya zoezi maalum Uwanja wa Uhuru ili kuhakikisha Siku ya Jumatatu mambo yanaenda sawa.
Jumatano Brazil walienda Harare, Zimbabwe kucheza na Nchi hiyo na kushinda kwa bao 3-0 kwa mabao ya Bastos, Robinho na Elano.
NGAO YA HISANI: Simba v Yanga, Agosti 14
Pazia la kufungua rasmi Msimu wa Mwaka 2010/11 wa Soka Tanzania Bara litafunguliwa Agosti 14 kwa mechi ya kugombea Ngao ya Hisani kati ya Mabingwa wa Bara, Simba, na Washindi wa Pili, Yanga.
Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza hapo Agosti 21.
Simba yamsaini Mganda wa St George
KIUNGO wa Saint George ya Ethiopia, Patrick Ochan kutoka Uganda amesaini Mkataba wa Miaka miwili kuichezea Simba.
Ochan pia huichezea Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes.
Alhamisi, Juni 3
Taifa Stars v Brazil: Kiingilio kuanzia Laki 2 hadi Elfu 30!!
Mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Magwiji wa Soka Duniani, Brazil, itakayochezwa Juni 7 Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam imepangiwa Viingilio malum ambavyo ni vya kihistoria na kiingilio cha juu kabisa ni Shilingi Laki 2 na cha chini ni Shilingi Elfu 30.
Mechi hiyo pia itaonyeshwa moja kwa moja kwenye TV na kupeperushwa kwenda zaidi ya Nchi 160 Duniani kote.
Hii ni mechi ya pili ya majaribio kwa Brazil Barani Afrika na jana walikuwa Mjini Harare, Zimbabwe na waliifunga Timu ya Zimbabwe kwa bao 3-0 Wafungaji wakiwa Bastos, Robinho na Elano.
Brazil wapo Afrika Kusini tayari kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 huko huko Afrika Kusini.
Siku moja kabla ya mechi hiyo, Taifa Stars watakuwa Nchini Rwanda watakaporudiana na Rwanda ili kupata Timu itakayocheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN.
Katika mechi ya kwanza Jijini Dar es Salaam, Timu hizo zilitoka sare 1-1.
[PATA HABARI/MAKALA NYINGINE www.sokainbongo.com]
Jumatatu, Mei 30
KILI TAIFA CUP: Singida ndio Wafalme!!
Mkoa wa Singida umeibuka kidedea walipoitandika Lindi bao 3-0 katika Fainali ya Kombe la Taifa iliyochezwa Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam hapo jana.
Ushindi Kindai Shooting Stars ulitokana na Chipukizi wa Klabu ya Simba, Kelvin Chale, aliepachika bao mbili na Kiula kufunga moja.
Kwa ushindi huo, Singida wamenyakua kitita cha Shilingi Milioni 35 toka kwa Wadhamini ambao ni TBL, wanaotengeneza Bia maarufu ya Kilimanjaro.
Lindi walipewa Milioni 20 na Ilala waliomaliza nafasi ya 3 walipata Milioni 10.
Arusha walipewa Milioni 5 kwa kushika nafasi ya 4.
Zawadi nyingine zilikwenda kwa Morogoro kupata Milioni 2 kwa kuwa na nidhamu bora.
Kwa Wachezaji, Hassan Hatibu wa Singida, alishinda Tuzo za Mchezaji Bora wa Fainali na kupewa Elfu 50 na pia kwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano kwa jumla alipata Milioni 2.
Kipa wa Lindi, Mohamed Ally, alipata Milioni 2 kwa kuwa Kipa Bora na Mfungaji Bora ni Amani George kwa kuwa na goli 9 na alipata Milioni 2.
Refa Bora ni Hashim Abdallah aliepewa Milioni 2.
KAGAME CUP: APR Bingwa!!
APR ya Rwanda imenyakua Ubingwa wa Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuinyuka St George ya Ethiopia bao 2-0 Uwanja wa Amahoro Mjini Kigali, Rwanda siku ya Jumamosi.
Timu hizo zilikuwa 0-0 hadi dakika 90 kwisha na ndipo Chiukepo Msowoya na Victor Nyirenda, wote Wachezaji kutoka Malawi, walipoifungia APR mabao dakika ya 92 na 98 katika dakika 30 za nyongeza.
Hii ni mara ya 3 kwa APR kuwa Bingwa baada ya kushinda Mwaka 2004 na 2007.Mchezaji wa APR, Chiukepo Msowoya, alinyakua Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora wa Mashindano hayo kwa kupachika bao 7.
Kabla ya Fainali hiyo, Sofapaka ya Kenya iliibuka Mshindi wa 3 walipoifunga Atraco ya Rwanda kwa bao 2-1.
Rais Paul Kagame wa Rwanda, aliekuwepo Uwanjani [Pichani pa moja na Rais wa TFF Leodegar Tenga] alikabidhi Zawadi ya Dola 30,000 kwa APR, Dola 20,000 kwa St George na Dola 10,000 kwa Sofapaka.
Jumamosi, Mei 29
Memba Yanga kuingia Brazil dezo!
Mfadhili Mkuu wa Yanga, Yusuf Manji, ameahidi kuwapa tiketi za bure za mechi ya Taifa Stars na Brazil ya Juni 7 Wanachama wote wa Yanga watakaohudhuria Mkutano Mkuu wa Klabu hiyo utakaofanyika Jumapili Mei 30 kwenye Bwalo la Polisi, Oyster Bay, Jijini Dar es Salaam.
Vile vile, Manji ameahidi kugharimia kila kitu kinachohusiana na Mkutano huo ikiwa pamoja na usafiri wa Wanachama toka Makao Makuu ya Klabu Mtaa wa Jangwani na Twiga hadi huko Bwalo la Polisi, kulipia Ukumbi na posho za Wasimamizi.
Simba yajipanga
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, ambae amechaguliwa hivi karibuni, ametangaza Kamati mbalimbali zitakazoongoza kwa Miaka Minne ijayo.
Kamati hizo ni za Usajili wa Wachezaji, Kamati ya Fedha na Kamati ya Mashindano.
Kamati ya Usajili itaongozwa na Zakaria Hanspoppe na Mlamu Ng’ambi atakuwa Katibu. Wanachama wake watakuwa Swedi Nkwabi, Azim Dewji, Patric Paul, Salim Abdallah, Musle Ruhei, Godfrey Iriki Nyange na Kassim Dewji.
Kamati ya Fedha itakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godrey Nyange, akisaidiwa na Joseph Itang’ire Kinesi na Katibu atakuwa Onesmo Waziri. Wanachama wa Kamati hiyo ni Adam Mgoi, Jerre Yambi, Seleman Zakazaka, Hassan Bantu na Gerald Lukumai.
Kamati ya Mashindano itaongozwa na Hassan Hassanoo huku Katibu akiwa Damian Manembe.
Wakati huo huo, Aden amesema wamefikia makubaliano na Mmiliki wa Kiwanja cha Kinesi cha huko Ubungo, Jijini Dar es Salaam ili wakikarabati na kukitumia kama Makao Makuu yao ya kufanyia mazoezi.
Kiwanja hicho kinachomilikiwa na Mwanachama wa Simba, Joseph Itang’ire Kinesi, ambae ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, kitajengewa Jim na kuwekewa nyasi mpya ambazo huenda zikawa za bandia.
Matengenezo ya Uwanja huo yanategemewa kumalizika kabla Msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kuanza.
KAGAME CUP: Fainali APR v St George
Leo ni Fainali ya Kagame Cup, Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, itakayofanyika Mjini Kigali, Rwanda kati ya APR ya Rwanda na St George ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Amahoro.
St George, wanaofundishwa na Kocha wa zamani wa Yanga Milutin Sredojevic “Micho’, waliwabwaga Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo Atraco ya Rwanda bao 3-1 kwenye Nusu Fainali.
APR wametinga Fainali kwa kuifunga 1-0 Sofapaka ya Kenya.
Mshindi wa Fainali ya leo atanyakua Dola 35000, Mshindi wa Pili Dola 20,000 na wa Tatu Dola 10,000.
Akaunti za Simba zakwanguliwa!!!
Uongozi mpya wa Simba utawaweka Wakaguzi wa Mahesabu ili kupitia Hesabu za Klabu hiyo na kuainisha Mapato na Matumizi yaliyofanywa chini ya Uongozi uliopita uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa zamani Hassan Dalali baada ya kugundulika Akaunti zote za Klabu hiyo hazina hata salio na nyingine kuchotwa fedha siku chache baada ya Uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage kuingia madarakani.
Inadaiwa Simba ilikuwa na Akaunti 3 na zote hazina hata senti.
Uongozi huo mpya wa Simba umezisimamisha Akaunti zote hizo na kuamua pia kuanzia sasa Mapato yote ya Mechi zote lazima yapitie Benki.
Pia Klabu imesema itapitia upya Mikataba yote ya Wapangaji wa Majengo mawili ya Klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi Jijini Dar es Salaam.
Ijumaa, Mei 28
Mo aahidi Milioni 5 kwa Singida
Shabiki mkubwa wa Soka, Mbunge wa Singida, Mohammed Dewji, ametoa ahadi kutoa zawadi ya shilingi milioni 5 kwa Wachezaji wa Mkoa wa Singida endapo watafanikiwa kunyakuwa ubingwa wa mashindano ya Kili Taifa Cup siku ya Jumapili.
Singida walifuzu kuingia Fainali kwa kuitoa Arusha 3-2 na watamenyana na Lindi waliowabwaga Mabingwa Watetezi Ilala kwa bao 3-0 hapo jana.
Mshindi wa Fainali hiyo kati ya Singida na Lindi atazawadiwa Shilingi Milioni 35 zilizotolewa na Wadhamini wa Mashindano, Bia maarufu ya Kilimanjaro.
Supersport kurusha Ligi Kuu Bara
Ligi Kuu ya Bara itaonyeshwa moja kwa moja na Kituo cha TV Supersport kuanzia Msimu ujao na hilo limethibitishwa na Barbara Kamogi, Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania ambao ndio wenye Supersport.
Kwa sasa Supesport inaonyesha mechi za Ligi Kuu za Kenya, Zambia, na Afrika Kusini.
Katika Msimu wa 2007/8 Kampuni ya GTV ya Uingereza ilianza kuonyesha Mechi za Ligi Kuu Bara lakini Kampuni hiyo ikafilisika.
Alhamisi, Mei 27
KILI TAIFA CUP: Fainali ni Singida v Lindi
Leo Lindi iliwabwaga Mabingwa Watetezi wa Taifa Cup, Ilala, kwa bao 3-0 katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam hii ikiwa ni Nusu Fainali ya Pili.
Jana, Singida waliitoa Arusha bao 3-2.
Fainali itakuwa Jumapili kati ya Lindi na Singida.
Jumanne, Mei 25
Brazil kutua Bongo njiani kwenda Bondeni?
Kuna taarifa kuwa Brazil watapita na kucheza mechi moja Mjini Dar es Salaam wakiwa njiani kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11.
Rais wa TFF Leodegar Tenga ametamka kuwa wanafanya mazungumzo na uongozi wa Brazil ili kukamilisha mpango huo na Tenga ametoa matumaini kufanikisha ziara hiyo kwa vile mazungumzo yapo hatua za juu kabisa na uhakika utapatikana siku chache zijazo.
Katika Fainali za Kombe la Dunia Brazil wapo Kundi G pamoja na Korea Kaskazini, Ivory Coast na Ureno.
Brazil watacheza mechi ya kwanza Juni 15 na Korea Kaskazini Mjini Johannesburg Uwanja wa Ellis Park.
KILI TAIFA CUP: Nusu Fainali ni:
Ilala v Lindi & Arusha v Singida
Mabingwa Watetezi Ilala wamefuzu kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Taifa la Kili baada ya kuwatoa Iringa kwa mikwaju ya penalti 5 kufuatia sare ya dakika za kawaida 90.
Ilala, walioshinda penalti 5-3, watakutana na Lindi Nusu Fainali.
Lindi waliwapiga Kilimanjaro bao 3-1.
Nusu Fainali nyingine itakuwa kati ya Arusha na Singida.
Arusha waliitoa Mwanza kwa penalty 6-5 na Singida walifunga Temeke 3-2.
Nusu Fainali zitachezwa kesho na kesho kutwa na Fainali ni Jumapili Mei 30.
Kombe hili la Taifa limedhaminiwa na Bia maarufu ya Kilimanjaro.
Jumatatu, Mei 24
Simba nje Kagame, yapigwa 2-1!!!
Katika mechi iliyochezwa Kigali, Rwanda ya Kombe la Kagame, Simba walifungwa 2-1 na Wenyeji APR ya Rwanda na kutupwa nje ya Kombe hilo.
Simba walianza vizuri katika Mashindano hayo kwa kuifunga Atraco ya Rwanda 2-1 lakini wakafungwa mechi mbili za Makundi zilizofuata na Sofapaka ya Kenya kwa bao 1-0 na URA ya Uganda ikawachapa 2-1.
Leo walikuwa wakicheza hatua ya Mtoano baada ya kufika hapo kama Washindi wa 3 wa Kundi lao.
Twiga Stars 8 Eritrea 1
Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salam, Timu ya Kina Mama, Twiga Stars, iliinyuka Timu ya Taifa ya Eritrea kwa bao 8-1 katika mechi ya kwanza ya kugombea kuingia Fainali za CAF za Wanawake.
Timu hizi zitarudiana huko Eritrea mwezi ujao na endapo Twiga Stars watapata matokeo mazuri watafuzu kuingia Fainali.
Jumapili, Mei 23
KILI TAIFA CUP: Robo Fainali kuanza kesho
Robo Fainali za Kili Taifa Cup zitaanza kesho Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kwa mechi mbili kila siku.
Ratiba ni:
Mei 24:
Singida v Temeke [saa 8 mchna]
Mwanza v Arusha [saa 10 jioni]
Mei 25;
Iringa v Ilala [saa 8 mchana]
Lindi v Kilimanjaro [saa 10 jioni]
NUSU FAINALI: Mei 26 na 27
FAINALI: Mei 30
Jumamosi, Mei 22
KAGAME CUP: Simba 1 URA 2
Licha ya kupata kipigo chao cha pili ndani ya siku 3 walipofungwa 2-1 hapo jana huko Kigali, Rwanda na URA ya Uganda katika mechi ya Kundi C ya Kombe la Kagame, Simba wamefanikiwa kusonga mbele katika Mashindano haya ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Juzi Simba walifungwa 1-0 na Sofapaka ya Kenya.
Katika mechi ya kwanza Simba waliifunga Atraco ya Rwanda 2-1.
Mabao ya jana yalifungwa na Nsumba Augustine na Kaweesa Manco kwa URA na la Simba alifunga Ramadhani Chombo.
Simba wamesonga mbele kama Washindi wa 3 wa Kundi C na Jumanne watacheza na APR ya Rwnada au TP Mazembe ya DR Congo.
Wachezaji wa Simba walikuwa: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Nyosso, Joseph Owino, Abdulhalim Humoud/ Jerry Santo, Uhuru Selemani, Jabir Aziz, Emmanuel Okwi/Robert Ssentongo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ and Ramadhan Chombo/ Mike Barasa.
Yanga yakubali Milioni 58 kumuuza Ngassa
Yanga imekubali dau la Shilingi Milioni 58 kutoka kwa Klabu ya Azam kwa ajili ya kumnunua Straika Mrisho Ngassa ingawa awali waligoma kumuuza.
Huenda mabadiliko ya Yanga yamekuja baada ya Mchezaji huyo kutaka kuuzwa na kutangaza kwenye Vyombo vya Habari nia yake ya kuhama.
Ijumaa, Mei 21
KAGAME CUP: Mafunzo Zenji yafunzwa adabu!!
TIMU ya Mafunzo ya Zanzibar jana ilifunzwa katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kupata kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa St. Georges ya Ethiopia huko Kigali, Rwanda.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Mafunzo tangu iwasili mjini Kigali karibu wiki moja sasa kufuatia mabadiliko ya Ratiba baada ya kujitoa kwa Timu ya kualikwa Heartland ya Nigeria na hivyo CECAFA kulazimika kubadili ratiba.
Timu nyingine iliyopo Kundi B pamoja na Mafunzo na St. Georges ni Wenyeji Rayon Sport ambayo kesho itacheza na Mafunzo.
Mabao ya washindi yalifungwa na Saladin Said dakika ya saba, Adame Girma dakika ya 14 na 35, Mohammed Marmo dakika ya 65 na Elias Marmo dakika ya 79.
TAIFA CUP: Robo Fainali Jumatatu, Mara yatolewa!!
WAKATI hatua ya Robo Fainali ya michuano ya kuwania Kombe la Taifa ikitarajiwa kuanza Jumatatu jijini Dar es Salaam, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeiondoa Timu ya Mkoa wa Mara katika Mashindano hayo na nafasi yake kuchukuliwa na Kilimanjaro baada ya kugundua kuwa Mara ilimchezesha Ludenzi Kilinga kinyume na kanuni za mashindano hayo.
Mchezaji huyo aliichezea Timu ya Polisi Morogoro katika Mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kutokana na kauni za mashindano hayo, Mchezaji huyo hakuruhusiwa kuuchezea mkoa wa Mara bali alitakiwa kuuchezea Mkoa wa Morogoro ambao ndio uliomsajili.
Wakati huohuo, TFF imeipiga faini ya Shilingi Milioni 2 Timu ya Mkoa wa Kagera, Lweru Eagles, kwa kutofika uwanjani katika mchezo wao wa mwisho wa Makundi dhidi ya Tabora.
Alhamisi, Mei 20
Simba 0 Sofapaka 1
Mchezaji wa zamani wa Yanga, John Barasa, aliipa ushindi Sofapaka ya Kenya alipofunga bao pekee kwenye dakika ya 30 na kuitoa Simba kwa bao 1-0 huko Kigali, Rwanda katika Mashindano ya Kombe la Kagame ambalo ndilo Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Simba juzi waliifunga Atraco ya Rwanda bao 2-1 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C.
Ili kutinga Robo Fainali Simba lazima waifunge URA ya Uganda katika mechi yao ya mwisho hapo kesho.
Jumatatu, Mei 17
KAGAME CUP: Simba 2 Atraco 1
Leo huko Kigali, Rwanda, Simba iliichapa Atraco ya Rwanda kwa bao 2-1 katika mechi yake ya kwanza ya Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame.
Mabao ya Simba yalifungwa na Mussa Mgosi na Sentongo.
Simba ipo Kundi C pamoja na Sofapaka ya Kenya, URA ya Uganda na Atraco ya Rwanda.
Hapo jana, mbele ya Rais wao Paul Kagame, APR ya Rwanda iliwafunga jirani zao toka Burundi Vitalo kwa bao 2-1 katika mechi iliyokumbwa na mvua kubwa.
Mabao ya APR yalifungwa na Haruna Ninyonzima na Sebanani Emanuel.
Bao la Vitalo lilifungwa na Bolima Matembe.
Jumamosi, Mei 15
FIFA yaiteua Tanzania kufanya utafiti
Tanzania ni miongoni mwa Nchi 5 zilizochaguliwa na FIFA kufanya utafiti
Kama vipimo vya MRI [Magnetic Resonance Imaging] vinaweza kutumika ili kuthibitisha umri wa Wachezaji Chipukizi kwenye Mashindano ya Vijana wa Kike.
FIFA imemleta Mtaalam, Daktari Yacine Zerguini wa Algeria, Tanzania kufanya utafiti huo na ametamka: “Tatizo la udanganyifu kwenye Mashindano ya U-17 [Chini ya Miaka 17] na U-20 [Chini ya Miaka 20] ni sugu na ndio maana tunatafuta ufumbuzi. Utafiti huu unafanywa kwenye Mabara matano Duniani.”
Dr Zerguini aliongeza kuwa MRI hutumika kupima mifupa ya mkononi na hugundua kama mtu yuko zaidi ya miaka 17 na hili limekuwa likifanyika kwa Vijana wa Kiume na sasa ndio wanajaribu kwa Wasichana.
Nchi nyingine ambazo utafiti huu unafanywa ni Brazil, Canada, Thailand na Belgium.
Yanga yaipongeza Simba
Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, amempongeza Ismail Aden Rage kwa kuchaguliwa Mwenyekiti mpya wa Simba kwenye uchaguzi uliofanyika Mei 9 na kumtaka kuondoa vikundi Klabuni hapo.
Madega aliongezea kuwa Simba nzuri ndio Yanga nzuri na hivyo akautaka Uongozi mpya wa Simba usimamie vizuri maslahi ya Klabu hiyo.
Wachezaji Simba watakiwa Misri
Kuna taarifa kuwa Wachezajiwa Simba, Uhuru Selemani na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ wanatakiwa wakapimwe afya zao katika Klabu ya Misri Haras El Hodood ambayo iliichapa Simba 5-1 huko Alexandria hivi majuzi na kuitoa nje ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Inasemekana Wachezaji hao wanatakiwa warudi Misri Juni 1 ingawa hamna taarifa kama Klabu hizo mbili zimefikia makubaliano ya kuuziana Wachezaji hao.
Simba kwenda Kigali leo
Simba inaondoka leo kwenda Kigali, Rwanda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, ambayo inaanza kesho kwa mechi kati ya Vitalo ya Burundi na APR ya Rwanda.
Msafara huo wa Simba una Wachezaji 20 na Viongozi watano wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti mpya Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Simba ipo Kundi C pamoja na Sofapaka ya Kenya, URA ya Uganda na Atraco ya Rwanda.
Alhamisi, Mei 13
KOMBE LA TAIFA: 8 zaingia ROBO FAINALI
Mikoa minane imefanikiwa kuingia Robo Fainali za Kombe la Taifa, mahsusi kwa jina la Kili Taifa Cup 2010, baada ya hatua za Makundi kumalizika hapo jana kutoka vituo mbalimbali.
Timu hizo 8 zitatua Dar es Salaam kwa Robo Fainali zitakazoanza Mei 22 na kuchezwa Uwanja wa Uhuru.
Mikoa niyo minane ni Mabingwa Watetezi, Ilala, Arusha, Iringa, Singida, Mwanza, Temeke, Mara na Lindi.
Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, ilishiriki ikiwa kituo cha Dodoma lakini haikufuzu baada ya kushinda mechi moja na sare mbili.
Jumatano, Mei 12
Ngassa ang'ang'ania kuhama Yanga!
Straika mahiri wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Ngassa, ambae yuko Kigali, Rwanda kwa majadiliano na Klabu ya APR ya Rwanda ili kuhamia huko ameiomba Klabu yake ya Yanga ambayo ana Mkataba wa mwaka mmoja nayo imruhusu kuhama ili ajiunge na APR wakifikia makubaliano ama na Klabu nyingine ya Tanzania ambayo inamtaka kwa dau kubwa.
Jumatatu, Mei 10
Rage Mwenyekiti Simba
Ismail Aden Rage jana alichaguliwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba na Makamu wake ni Godfrey Nyange 'Kaburu'.
Uchaguzi huo ulifanyika jana Bwalo la Polisi huko Oyster Bay na Rage alipata kura 785 na mpinzani wake Hassanol alipata kura 435.
Jumapili, Mei 9
Simba yaangushiwa kipondo huko Misri!!
Yabondwa 5-1
Mjini Allexandria, Misri hapo jana, Simba ilifungwa bao 5-1 na Haras El Hodood ya Misri na kutupwa nje ya Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya bao 6-3.
Simba walishinda mechi ya kwanza Jijini Dar kwa bao 2-1.
Hadi mapumziko hapo jana Simba walikuwa wameshapigwa 3-1.
UCHAGUZI SIMBA: Mahakama yaamua ufanyike leo!
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeamuru Uchaguzi Simba uliopangwa kufanywa leo uendelee baada ya kuondoa amri ya kuuzuia Uchaguzi huo iliyowekwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuatia kufunguliwa kesi na kundi la Michael Wambura, alieenguliwa kugombea.
KOMBE LA TAIFA: Laanza jana!
KITUO CHA MTWARA:
-Mtwara 1 Ilala 2
-Lindi 3 Ruvuma Warriors 1
KITUO CHA ARUSHA:
-Mount Warriors 3 Manyara 0
-Mara 3 Kilimanjaro Stars 2
KITUO CHA TANGA:
-Temeke 1 Pwani 0
-Tanga 0 Morogoro 0
KITUO CHA DODOMA:
-Dodoma 2 Kigoma 1
-Ngorongoro Heroes 0 Singida 0
Jumamosi, Mei 8
Ngassa Mchezaji bora Ligi Kuu VODACOM
Mchezaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya VODACOM kwa Msimu wa 2009/10.
Tuzo hiyo imetolewa na wadhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya VODACOM.
Mussa Mgosi wa Simba ndie aliepata Tuzo ya Mfungaji Bora.
Marudiano: Haras El Hodood v Simba
Leo saa 2 usiku saa za bongo, Simba inashuka dimbani huko Mjini Alexandria, Misri kurudiana na Haras El Hodood katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Simba ilishinda bao 2-1.
Simba walikuwa Jijini Cairo tangu Jumapili iliyopita wakijifua na juzi ndio walielekea Alexandria.
Ijumaa, Mei 7
Mahakama yapiga stopu Uchaguzi, Simba yampiga stopu Wambura
Wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesimamisha Uchaguzi wa Klabu ya Simba kufanyika Mei 9, uongozi wa Klabu hiyo umewasimamisha uanachama Michael Wambura na Juma Mtemi kufuatia kufunguliwa kesi hiyo Mahakamani.
Mahakama ya Kisutu imesimamisha Uchaguzi huo ili kutoa nafasi kesi ya msingi ya Wambura isikilizwe.
Nao Uongozi wa Simba umedai uchaguzi utafanyika Mei 9 kwa vile Mahakama imemshitaki Mwenyekiti wa Simba na si Kamati ya Uchaguzi ambayo ndio inayoendesha uchaguzi huo.
Yanga yaitaka Simba iwe na busara!
Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Imani Madega, amewataka Simba watumie busara katika sakata lao la uchaguzi ili kuinusuru soka ya Tanzania isiingizwe mashakani.
Madega aliwaasa Wanachama Simba watambue masuala ya michezo hupelekwa CAS [Court of Arbitration for Sports] ambayo ni Mahakama ya Usuluhisho ya Michezo na si Mahakama za kawaida za kisheria.
Alhamisi, Mei 6
Sakata la uchaguzi Simba: Wambura yuko Mahakamani!!
Mgombea Uenyekiti Klabuni Simba, Michael Wambura, ambae alienguliwa kugombea amefungua kesi Mahakamani akitaka Uchaguzi usimamishwe na pia ameandika barua FIFA kuwaelezea uamuzi wake.
Hatua hii ya Wambura kwenda Mahakamani huenda ikazua mtafaruku mkubwa kwa Tanzania toka kwa FIFA kwa vile FIFA haitaki masuala ya soka yaende Mahakamani.
Jumatano, Mei 5
Makocha Wabongo hawafai Taifa Stars
TFF imewatosa Makocha Wabongo walioomba kugombea nafasi kumrithi Mbrazil Marcio Maximo na kuwapitisha Makocha toka nje tu kwa Waombaji wa nafasi hiyo.
Miongoni mwa Wabongo walioomba nafasi hiyo ni Charles Boniface ambae alikuwa miongoni mwa Makocha 53 wanaoitaka nafasi hiyo.
TFF imepitisha Makocha watano toka Bulgaria, Ureno, Poland, Serbia na Denmark kwa ajili ya intavyu.
Jumapili, Mei 2
Taifa Stars 1 Amavubi 1
Jana Timu ya Taifa ya Tanzania ilijiweka nafasi mbovu ya kufuzu kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN, walipotoka sare 1-1 na Timu ya Rwanda Jijini Dar es Salaam.
Timu hizi zitarudiana mwezi Juni huko Kigali, Rwanda na droo ya 0-0 ni tosha kwa Rwanda kwenda Fainali kwa goli la ugenini.
Rwanda ndio walitangulia kupata bao lakini Mrisho Ngassa ndie aliewatoa Wabongo kimasomaso.
Jumamosi, Mei 1
Ngorongoro Heroes yasonga!!
Timu ya Taifa ya Vijana Chini ya Miaka 20, Ngorongoro Heroes, jana kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, iliwafunga wenzao toka Malawi bao 3-1 na kufuzu kusonga raundi ijayo watakayokutana na Ivory Coast ili kuingia Fainali za Vijana wa Afrika zitakazochezwa Libya mwakani.
Timu hizi mbili zilitoka sare 2-2 huko Malawi wiki mbili zilizopita hivyo Mashujaa wa Ngorongoro wameshinda kwa jumla ya bao 5-3.
Mashujaa hao walipata bao la kwanza dakika ya pili tu Mfungaji akiwa Ulimwengu na bao la pili alifunga Seme dakika ya 30.
Malawi walipata bao lao kwa njia ya penalti lakini muda mfupi baadae Mashujaa wakaongeza bao la 3 Mfungaji akiwa tena ni Ulimwengu.
Ijumaa, Aprili 30
UCHAGUZI SIMBA: Wagombea wapigwa makwanja, wengine kwenda Mahakamani!!
Uchaguzi wa Simba uliopangwa kufanyika Mei 9 huenda ukavurugika baada ya kuondolewa kwa baadhi ya Wagombea kufuatia pingamizi mbalimbali juu yao na huenda ukaangukia Mahakamani.
TFF, chini ya Kamati yake Maalum, ilitangaza kuondolewa Wagombea wanne akiwemo yule wa Uenyekiti, Michael Wambura, ambae amesema huenda akafika kwa Pilato.
Majina mengine yaliyopigwa panga ni Zacharia Hanspoppe, aliekuwa akigombea Uenyekiti, Mwina Kaduguda, ambae ni Katibu Mkuu wa sasa wa Simba aliekuwa akigombea Makamu Mwenyekiti, na Chano Almas aliekuwa akigombea Ujumbe.
TFF ilitangaza kuwa Kamati yake chini ya Jaji John Mkwawa iliridhika na pingamizi hizo ambapo Wambura alikatwa kwa misingi ya ‘uaminifu’ na ‘utendaji’, Hanspoppe aliondolewa kwa sababu aliwahi kufungwa kwa kosa la uhaini na Kaduguda alipigwa shoka kwa kutomiza wajibu wake akiwa Kiongozi wa Simba.
Chano Almas, alieondolewa kwa kutotimiza masharti ya Katiba ya Simba, amesema yeye atawaachia Wanachama wa Simba kutoa uamuzi.
Kamati hiyo ya TFF ilimpitisha Ismail Aden Rage licha ya pingamizi kuwa aliwahi kufungwa kwa vile Mahakama Kuu ilimsafisha kwa kumuona hana hatia kwa makosa yaliyomfunga.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Simba, Damas Ndumbaro, amesema Uchaguzi utafanyika Mei 9 kama ulivyopangwa.
Kufuatia mchujo huo, Nafasi ya Mwenyekiti ina Wagombea wawili tu nao ni Hassan Othman ‘Hassanol’ na Ismail Aden Rage.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ina Mgombea mmoja tu nae ni Geoffrey Nyange.
Jumatano, Aprili 28
TFF yatoa ofa kwa Watazamaji: KIINGILIO bure!!!
TFF imetoa ofa ya Watazamaji kuingia bure ila wale wa Jukwaa la Bluu watalipa Elfu 10 na wale wa Jukwaa la Kijani watalipa Elfu 5 ili kushuhudia mechi kati ya Timu ya Vijana wa Chini ya Miaka 20, Ngorongoro Heroes, watakapocheza na Malawi Siku ya Ijumaa Aprili 30 Uwanja wa Taifa.
Hiyo ni mechi ya marudiano baada ya kutoka sare huko Malawi kwa bao 2-2 na mshindi atacheza na Ivory Coast ili kuwania kuingia Fainali za Afrika kwa Vijana wa Chini ya Miaka 20.
Kocha wa Ngorongoro Heroes, Rodrigo Stockler, amesema Timu yake iko imara na wana matumaini ya kusonga mbele.
Jumapili, Aprili 25
Simba 2 Haras El-Hodood 1
Mabao ya Okwi na Mgosi yamewapa Simba ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Haras El-Hodood ya Misri katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Jijini Dar es Salaam.
Timu hizi zitarudiana Mjini Alexandria, Misri baada ya wiki mbili.
MATOKEO KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
Coton Sport FC [Cameroun] 1 v CD 1 de Agosto [Angola] 0
Simba [Tanzania] 2 v Haras El Hedoud [Misri] 1
Alamal Atbar [Sudan] 1 v CR Belouizdad [Algeria] 0
Petrojet [Misri] 1 v Club Sportif Sfaxien [Tunisia] 1
FUS Rabat [Morocco] 2 v Stade Malien de Bamako [Mali] 0
Warri Wolves [Nigeria] 2 v Caps United FC [Zimbabwe] 1
AS-FAN [Niger] 1 v Daring Club Motema Pembe [DR Congo] 0
AS Vita Club [DR Congo] 3 v Enyimba International FC [Nigeria] 0
Jumamosi ,Aprili 24
Haras El-Hodood wagomea Karume
WAPINZANI wa Simba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Haras El-Hodood ya Misri, wamegoma kufanya mazoezi kwenye Viwanja vya nyasi bandia vya Karume walivyopangiwa kufanyia mazoezi.
Timu hiyo iliamua kurudi Hotelini kwao Movenpick bila kufanya mazoezi.
Nae mmoja wa Maafisa wa Timu hiyo kutoka Misri amedai anaifahamu vizuri Simba na alipokuwa mmoja wa Viongozi wa Ismailia pia ya huko Misri waliwahi kucheza na Simba na kutoka sare 1-1 Mjini Dar es Salaam na wao kuifunga 2-0 huko Misri.
Ratiba kamili ya Raundi ya Timu 16 ya Kombe la Shirikisho Afrka ni:
Jumapili, Aprili 25
Coton Sport FC [Cameroun] v CD 1 de Agosto [Angola]
Simba [Tanzania] v Haras El Hedoud [Misri]
Alamal Atbar [Sudan] v CR Belouizdad [Algeria]
Petrojet [Misri] v Club Sportif Sfaxien [Tunisia]
FUS Rabat [Morocco] v Stade Malien de Bamako [Mali]
Warri Wolves [Nigeria] v Caps United FC [Zimbabwe]
AS-FAN [Niger] v Daring Club Motema Pembe [DR Congo]
Ngorongoro Heroes kucheza Aprili 30 na Malawi
TFF imebadili ratiba ya mechi ya Timu ya Taifa ya Vijana Chini ya Miaka 20, Ngorongoro Heroes, dhidi ya Malawi ikiwa ni marudiano baada kutoka 2-2 huko Malawi na sasa itachezwa Aprili 30 badala ya Mei mosi Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Ijumaa, Aprili 23
Taifa Stars yatajwa
KOCHA wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo ametangaza Kikosi cha Wachezaji 27 watakaokuwa kambini kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Rwanda “Amavubi” kuwania kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) ambao umepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam Mei Mosi.
Katika Kikosi hicho wamo baadhi ya Vijana wa Timu ya U-20, Ngorongoro Heroes.
Kikosi kamili ni:
Makipa Shaaban Kado na Jackson Chove.
Walinzi wa wapemben ini Shadrack Nsajigwa, Salum Kanoni, Juma Jubu na Stephano Mwasika.
Walinzi wa Kati: Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, David Naftari na Dickson Daudi.
Viungo ni Erasto Nyoni, Nurdin Bakari, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Kigi Makasi, Shaaban Nditi, Abdi Kasim, Uhuru Selemani na Chipukizi Selemani Kasim.
Washambuliaji ni Mrisho Ngassa, John Boko, Mussa Hassan Mgosi, Jerson Tegete, Michael Mgimwa, Yusuph Soka na Jonas Kajuna.
Wapinzani wa Simba Haras El-Hodood kutua Dar
WAPINZANI wa Simba, Haras el-Hodood, yenye maskani yake kwenye mji wa Alexandia Nchini Misri, wanawasili leo Jijini Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumapili Uwanja wa Taifa.
Mabingwa hao wa Tanzania wa mwaka huu, waliitoa Lengthens ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-1, kwa kushinda katika mchezo wa kwanza mabao 3-0 huko Harare, Zimbabwe na kuifunga mabao 2-1 Jijini Dar es Salaam.
Haras el-Hodood, iliitoa Ethiopian Banks ya Ethiopia kwa kuifunga jumla ya mabao 6-1. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Timu hizo zilitoka sare bao 1-1.
Haras el-Hodood wilishinda mchezo wa marudiano kwa mabao 5-0 Mjini Alexandria, Misri.
Alhamisi, Aprili 22
Prisons, Manyema zawafuata chini Moro United
Ligi Kuu Tanzania Bara ilikwisha rasmi hapo jana, na wakati tayari Bingwa, Simba, na Timu moja iliyoporomoka, Moro United, zilikwishajulikana, jana Prisons na Manyema ziliungana na Moro United kucheza Daraja la chini baada ya kushushwa rasmi.
Prisons, waliokuwa wakihitaji ushindi dhidi ya Yanga, walikuwa wakiongoza bao 1-0 hadi dakika ya 87 huko Mbeya, ndipo Steven Bengo wa Yanga akasawazisha na kuibwaga Prisons.
Nao, Manyema, waliokuwa wakihitaji ushindi kujinusuru, walitoka sare na Azam na hivyo pia kuporomoka.
Timu zilizopanda Daraja na zitacheza Ligi Kuu Msimu ujao ni AFC Arusha, Polisi Dodoma na Ruvu Shooting.
Jumatano, Aprili 21
Klabu Bingwa Afrika Mashariki: Makundi yapangwa
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba, wamepangwa katika Kundi C la Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ijulikanayo kama Kagame Cup, itakayoanza Mei 15 na kumalizika Mei 29 huko Kigali, Rwanda.
Timu nyingine kwenye Kundi C ni Atraco FC ya Rwanda, Uganda Revenue Authority [URA] na Sofapaka ya Kenya.
Kundi A ni APR ya Rwanda, TP Mazembe ya DRC, Vitalo (Burundi) na Telkom (Djibouti).
Kundi B ni Rayon Sports ya Rwanda, kutoka Ethiopia ni St George, Heartland ya Nigeria na Mafunzo ya Zanzibar.
Timu za Heartland ya Nigeria na TP Mazembe ya DRC ni Wageni Waalikwa.
KILI TAIFA CUP: Ratiba nje!
Ratiba ya Kilimnjaro Taifa Cup, inayodhaminiwa na Bia maarufu ya Kilimanjaro, imetolewa na Makundi ya mechi za awali yametajwa huku Mabingwa Watetezi, Mkoa wa Ilala, watakuwa Kundi F na wataanza mechi na Mtwara mwezi ujao.
Timu nyingine kwenye Kundi F ni Lindi, Ruvuma na Mtwara ndio Wenyeji wa Kundi hili.
Timu ya Taifa ya Vijana wa Chini wa Miaka 20, Ngorongoro Heroes, ambao wameingizwa kwenye michuano hii ili kupata mazoezi na kujipima nguvu wapo Kundi A pamoja na Singida, Kigoma na Dodoma ambao ni Wenyeji wa Kundi hili.
Kundi B, litakalocheza mechi Mjini Tanga, lina Timu za Tanga, Morogoro, Pwani naTemeke
Kundi C litakuwa Mjini Mwanza likiwa na Timu za Mwanza, Kagera, Shinyanga na Tabora.
Arusha ndio Wenyeji wa Kundi D na timu nyingine ni Mara, Manyara na Kilimanjaro.
Kundi E, litachezwa Iringa, na lina Timu za Iringa, Mbeya, Rukwa na Kinondoni.
Mshindi wa kila Kundi ataingia Robo Fainali.
Mshindi wa Kili Taifa Cup atanyakua Donge la Shilingi Milioni 35.
Mshindi wa pili atapata Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 10 na wa 4 Sh Milioni 5.
Mchezaji Bora atapewa Milioni 2 na pia Refa, Kipa, Kocha na Mfungaji bora watapata Milioni 2 kila mmoja.
Jumanne, Aprili 20
Dalali atupwa nje kwenye Uchaguzi Simba
Mwenyekiti wa sasa wa Simba, Hassan Dalali, ameondolewa kama Mgombea wa Kiti hicho kwenye Uchaguzi Mkuu hapo Mei 9 kwa kukosa elimu inayostahili kwa mujibu wa Katiba ya Simba.
Inaaminiki Dalali alishindwa kuwakilisha Cheti cha Elimu ya Sekondari.
Kabla ya Dalali kuwakilisha fomu zake kugombea nafasi ya Uenyekiti, Mwanachama wa Simba, Seydou Rubeya, alitamka atamwekea pingamizi Dalali akigombea kwa kukosa elimu inayotakiwa.
Mgombea mwingine alietupwa nje kwa sababu ya elimu ni Mohammed Nanyali.
Wagombea ambao pingamizi zao zimetupiliwa mbali ni Ismail Aden Rage na Michael Wambura wanaogombea Uenyekiti.
Wengine waliosafishiwa njia kwa kutupwa pingamizi ni Hassan Othman ‘Hassanol’ na Zacharia Hanspope wanaogombea Uenyekiti.
Pia, pingamizi dhidi ya Wagombea Makamu Mwenyekiti, Mwina Kaduguda na Geofrey “Kaburu” Nyange, zimetupwa.
Wagombea Ujumbe walioenguliwa kwa kukosa elimu stahili ni Josiah Jackson, Said Kubenea, Hamis Sued, Abdallah Mzenga, Shaaban Geva na Jasmin Badawi Soud.
Jumapili, Aprili 18
Simba 4 Yanga 3
Simba leo wamehitimisha Ubingwa wao wa Ligi Kuu kwa kuwafunga Mahasimu wao Yanga kwa bao 4-3 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.
Kadi Nyekundu ziltembea kwa wingi katika mechi hii huku Wachezaji wawili wa Yanga na mmoja wa Simba wakilambwa Kadi hizo.
Mabao ya Simba yalifungwa na Mgosi bao 3 na Hilal Echesa ndie aliefunga bao moja na la ushindi kwenye dakika ya 94.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Jerry Tegete bao 2 na Kigi Makasi bao moja.
Ngorongoro droo huko Malawi
TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (U-20), Ngorongoro Heroes imetoka sare na Malawi kwa mabao 2-2 hapo jana huko Nchini Malawi katika mechi ya kuwania kuingia Fainali za Kombe la Afrika.
Malawi walianza kufunga kupitia kwa Lucas Milanzi dakika ya 40 na dakika ya 46, Mbwana Samatta aliisawazishia Ngorongoro.
Ngorongoro walipata bao la pili dakika ya 48 Mfungaji akiwa Rajabu Abdallah lakini Malawi wakarudisha kwenye dakika ya 67.
Mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili zinazokuja Jijini Dar es Salaam ma Mshindi atasonga mbele kupambana na Ivory Coast.
Leo ni leo: Yanga v Simba
Wakati Simba inataka kufurahia Ubingwa wao kwa kuwaua Wapinzani wao wa Jadi, Yanga wanalilia kulinda heshima na pia kuwaharibia furaha katika mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam leo jioni.
Yanga haijaifunga Simba kwa muda mrefu kwenye mechi za Ligi isipokuwa mwishoni mwa mwaka jana, Desemba 24, iliposhinda kwa mabao 2-1 katika michuano ya Tusker.
Pia, Yanga itataka kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu uliochezwa Oktoba 31.
Yanga na Simba zitamaliza mechi zao za Ligi kwa samba kucheza na Mtibwa Mjini Morogoro na Yanga kucheza na Prisons Jijini Dar es Salaam.
Alhamisi, Aprili 15
Uchaguzi Simba: Dalali awekewa pingamizi
Katibu Mwenezi wa zamani wa Simba, Said Rubeya 'Seydou' ametimiza azma yake kwa kumwekea pingamizi mgombea Uenyekiti anayetetea kiti chake, Hassan Dalali.
Seydou aliahidi wiki iliyopita kuwa ikiwa Dalali atagombea tena uongozi Simba yeye ataweka pingamizi kwa madai kuwa Dalali hana elimu ya kumwezesha kugombea Uenyekiti kama Katiba ya Simba invyotaka.
Ngorongoro Heroes safarini Malawi
Kikosi cha Wachezaji 20 wa Timu ya Taifa ya Vijana wa Chini ya Miaka 20 cha Tanzania, Ngorongoro Heroes, kinaelekea Malawi kucheza na Timu ya Nchi hiyo siku ya Jumapili ili kuwania kuingia Fainali za Vijana huko Afrika Kusini.
Msafara wa Timu hiyo una jumla ya Watu 27 na Kocha wa Timu hiyo, Rodrigo, ameahidi ushindi kwa vile wako fiti.
Ngorongoro Heroes majuzi walicheza mechi ya kujipima nguvu na Vijana wa Kenya na kushinda 4-3 Mjini Dar es Salaam
Jumatano, Aprili 14
Kilimanjaro Taifa Cup Mei 8
Mashindano ya Taifa Cup, yanayojulikana rasmi kama Kilimanjaro Taifa Cup kwa sababu Mdhamini ni Bia Maarufu ya Kilimanjaro, yataanza Mei 8 kwa kushindaniwa na Timu za Mikoa na Mshindi atanyakua donge la Shilingi Milioni 35.
Ili kufanikisha Mashindano hayo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, ametangaza kuwa Waandishi wa Michezo watafanyiwa Semina maalum ili kuwaongezea ujuzi.
Wadhamini wa Kombe hilo, Tanzanian Breweries Limited, wameongeza udhamini wao kutoka Milioni 650 za mwaka jana hadi Milioni 850 kwa Mashindano ya mwaka huu.
Pamoja na udhamini kwa kila Timu na zawadi za donge nono kwa washindi wa kwanza hadi wanne, pia kuna zawadi kwa Mchezaji Bora, Refa Bora, Kipa, Kocha na Mfungaji Bora.
Kauli mbiu ya Mashindano hayo ya mwaka huu ni ‘Kupeleka Soka ya Tanzania Kilele cha Mafanikio’.
Hatua za awali zitaanza Mei 8 hadi 15 na kuhusisha Timu 24 katika vituo 6 ambavyo ni Mtwara, Arusha, Dodoma, Tanga, Iringa na Mwanza.
Mshindi wa Kila Kituo ataingia Robo Fainali.
Hatua za mwisho za Mashindano hayo zitafanyika Dar es Salaam kati ya Mei 22 hadi 30.
Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela, amesema kila Mkoa utasajili Wachezaji 20 lakini kati ya hao ni wa 5 tu ndio wanaruhusiwa kutoka Timu za Ligi Kuu ili kutoa nafasi kwa wachezaji Chipukizi kucheza.
Vilevile, Katibu Mkuu huyo amesema Wachezaji wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, hawataruhusiwa kucheza kwa vile watakuwepo kwenye maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN.
Pia, Timu ya Taifa ya Vijana wa Chini ya Miaka 20, Ngorongoro Heroes, watashiriki Mashindano hayo kama sehemu ya mazoezi yao kujitayarisha na Mchujo wa Michezo ya Olimpiki.
Lakini ikiwa Ngorongoro Heroes watafanikiwa kuingia Fainali na kushinda hawatapewa zawadi ya Mshindi ambayo itachukuliwa na Timu nyingine itakayocheza nayo Fainali hiyo.
Mwaka jana, Mkoa wa Ilala ulikuwa ndio Mabingwa walipowafunga Temeke 1-0.
Jumanne, Aprili 13
Bongo: Kwa ufupi…………
-Yanga, Simba zote Visiwani!
Wakati Simba iko Zanzibar kwa wiki mbili ikifanya mazoezi kujitayarisha kwa pambano lao na Yanga hapo Aprili 18, Yanga ilikwenda Visiwani huko kwa ziara ya siku moja tu ili kwenda kupata Baraka za Mama Fatma Karume ambae ni mlezi wa Klabu hiyo.
Mama Karume wiki iliyopita alikwenda Dar es Salaam akiongoza msafara uliotembelea Klabu ya Yanga na alipokuwa hapo alikabidhiwa Kadi mpya ya Uanachama.
-Wafungaji Bora Ligi kuu ni Watatu!
Ligi Kuu inaelekea ukingoni na mpaka sasa hajapatikana Mfungaji Bora na wapo Wachezaji watatu waliofungana kwa wote kufunga mabao 14 kila mmoja.
Watatu hao ni John Bocco wa Azam, Musa Hassan Mgosi wa Simba na Mrisho Ngassa wa Yanga.
-African Lyon yajinusuru
African Lyon imetoka sare 2-2 na Azam na hivyo kujihakikishia kutoshuka Daraja kutoka Ligi Kuu.
Azam wapo nafasi ya 3 kwenye Ligi hiyo.
Tayari Moro United washashushwa Daraja na Timu zilizo juu yao na ambazo zipo hatarini kushushwa nao ni Prison na Toto African zenye pointi 20 kila mmoja.
Juu ya Timu hizo 3 za chini ni Manyema wenye pointi 22.
Timu zilizopanda Daraja na zitacheza Ligi kuu Msimu ujao ni AFC Arusha, Polisi Dodoma na Ruvu Shooting.
Jumatatu, Aprili 12
Yanga, Simba Usiku
Mechi ya Watani wa Jadi, Yanga na Simba, iliyoahirishwa hadi Aprili 18 baada ya mkanganyo wa Kiwanja kipi kichezewe, sasa itachezwa siku hiyo hiyo lakini usiku kuanzia saa 2 kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.
Mara ya mwisho kwa Yanga na Simba kucheza mechi nyakati za usiku ni mwaka 1992 katika Fainali ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki huko Zanzibar Uwanja wa Amani na Simba ikashinda kwa matuta 6-5.
Sababu hasa iliyofanya mechi hii ichezwe usiku ni kuwa Aprili 18 ni Siku ya Maji Duniani na Serikali pamoja na Benki ya Exim zimeandaa mbio fupi kwa ajili ya kuchangia fedha za upatikanaji wa maji Tanzania ambazo zitaanzia nje ya Uwanja wa Taifa.
Viingilio vya mchezo huo vimepangwa kwa watakaokaa viti vya VIP A kulipa Sh 40,000, VIP B ni Sh 30,000 na VIP C ni Sh 20,000. Viti vya rangi mkabala na magoli ni Sh 15,000 na vile vya rangi ya machungwa nyuma ya magoli ni Sh10,000, viti vya bluu ni Sh 7,000 na viti vya kijani ni Sh 5,000.
Jumapili, Aprili 11
Uchaguzi Mkuu Simba: Wagombea wafikia 33
Wagombea 33 ndio waliochukua na kurudisha fomu za kugombea Uongozi Klabuni Simba katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Mei 9.
Kwenye nafasi ya Uenyekiti wapo Hassan Dalali, ambae ndie Mwenyekiti wa sasa, wengine ni Zacharia Hanspope, Hassan Othman Hassanol, Michael Wambura, Ismail Aden Rage, Andrew Ditta Tupa na Mohammed Nanyali.
Kwenye Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wapo Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwina Kaduguda.
Katika nafasi za Wajumbe wapo Watu 26 waliorudisha fomu kugombea nafasi 7 na kati ya hizo 7 kiti kimoja ni maalum kwa Wanawake.
Wagombea kwa Wanaume ni Said Pamba, Suleiman Zakazaka, Sheikh Shughuli Sheikh, Sued Fikirini Mkwabi, Hamis Sued, Khamis Mkoma, Boniface Wambura, Titus Lipagile, Saed Kubenea, Yasin Mweta, Mohammed Mjenga, Francis Mdenda,Shaaban Gervas, Hassan Myenye, Charles Hamka, Hassan Mtenga, Joseph Kinesi, Ibrahim Masoud, Damian Manembe, Chano Almasi, Maulid Abdallah, Bundallah Kabulwa, Josiah Jackson na Zuberi Magoha.
Wagombea wa Kiti kimoja cha Kinamama ni wawili nao ni Zuwena Matibwa na Jasmin Badawi Soud.
Inategemewa Majina ya Wagombea itatangazwa Jumanne na wale wataokatwa Majina yao watapewa siku mbili baada ya hapo ili kukata rufaa.
Jumamosi, Aprili 10
Simba, Yanga yaahirishwa!!!!
Sakata la Kiwanja kipi kichezewa pambano la Mahasimu wakubwa, Simba na Yanga, limefanya mechi hiyo iliyokuwa ichezwe kesho kuahirishwa hadi Jumapili Aprili 18 na hivyo pia Ligi kusogezwa mbele na kumalizika Aprili 21.
Kwa wiki nzima sasa kumekuwa na mkanganyiko wapi mechi hiyo ichezwe, Uwanja wa Taifa au Uhuru, kutokana na pande zote kutoridhishwa na gharama na pia uwezo wa Viwanja hivyo kuingiza Watazamaji.
Kiwanja cha Taifa kinaingiza Watazamaji 60,000 lakini gharama zake ni kubwa na kile cha Uhuru ni nafuu lakini kinachukua Watazamaji 19,000 tu.
Wakati Klabu hizo na TFF wakiendelea maandalizi ili pambano hilo lichezwe Uwanja wa Uhuru, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo baada ya majadiliano na pande zote, imetamka kuwa pambano hilo litaahirishwa hadi Aprili 18 na kuchezwa Uwanja wa Taifa na pia suala la gharama za Uwanja huo zitatolewa maamuzi wiki ijayo.
Wadau wanahisi uamuzi wa Serikali unatokana na hofu ya usalama wa watu kwani kungekuwa na msongamano mkubwa kwenye Uwanja huo mdogo.
Ijumaa, Aprili 9
Moro United yateremka!
Moro United leo imefungwa na Manyema Rangers bao 2-0 na kuwa Timu ya kwanza kuteremshwa Daraja huku kukiwa bado kuna mechi moja mkononi.
Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na mabao ya Manyema yalifungwa kipindi cha pili na Yusuf Nguya na Ali Mohamed.
Ushindi huo umeiwezesha Manyema kuponyoka kutoka zile Timu 3 za mwisho zinazoshuka Daraja na kuzivuta chini Prison na Toto African.
Manyema sasa wana pointi 22, Prison na Toto African pointi 20 kila mmoja wakiwa juu ya Timu ya mwisho Moro United ambayo sasa tayari imeshashuka.
Timu zilizopanda Daraja ni AFC Arusha, Polisi Dodoma na Ruvu Shooting.
Mgombea Simba ataka kashfa ziachwe
Michael Wambura, anaegombea nafasi ya Uenyekiti Klabuni Simba katika uchaguzi utakaofanyika Mei 9, amewataka Wana Simba kuacha kashfa na badala yake wazungumzie sera za maendeleo.
Wambura alitangaza kugombea huku akinadi mambo 18 ya maendeleo atakayoyafanya Simba akichaguliwa Mwenyekiti.
Simba v Yanga Jumapili, Kiwanja hakijulikani!
Lile pambano la Watani wa Jadi, Simba na Yanga, litakalochezwa Jumapili mpaka sasa haijulikani litachezwa wapi baada ya TFF kusema bado inajadiliana na Serikali ili ipunguze gharama inazotoza kwa kuutumia Uwanja wa Taifa ambazo ni asilimia 40 ya mapato.
TFF na Klabu husika zinataka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa ambao unachukua Watazamaji 60,000 wakati ule wa zamani, unaoitwa Uwanja wa Uhuru, unapakia watu 19,000 tu.
TFF imesema uamuzi wa Uwanja upi utatumiwa utajulikana leo.
Hanspope ajikita Uchaguzi Simba
Yule Mwanachama maarufu wa Simba na mmoja wa Kikundi chenye nguvu Klabuni hapo, ‘Friends of Simba’, Zakaria Hanspope ameingia kwenye kimasomaso cha kugombea Uenyakiti kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Mei 9.
Hanspope anakuwa Mgombea wa 6 wa Uenyekiti wengine wakiwa Mwenyekiti wa sasa Hassan Dalali, Ismail Aden Rage, Michael Wambura, Andrew Dita Tupa na Mohammed Nyangamala.
HABARI ZA AWALI:
Mechi Simba na Yanga kupigwa mnada!
Mechi ya wa Watani wa Jadi, Yanga na Simba imeingizwa sokoni ili kutafutiwa wanunuzi kwa Shilingi Milioni 300 kama litachezwa Uwanja wa Taifa na Shilingi Milioni 200 ikiwa utachezwa Uwanja wa Uhuru.
Habari hizi zimetangazwa na Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, ambae pia amesema viwango hivyo vimeafikiwa na Viongozi wa Klabu hizo mbili.
Uamuzi huo umefikiwa ikiwa ni moja ya mbinu ya kuhakikisha mapato mazuri nay a uhakika na pia kuwakwepa wale wavunaji wa ‘Shamba la Bibi”.
Mwakalebela alisema iwapo hakutakuwa na Mdau yoyote ambae atajitokeza kununua pambano hilo, mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru kwa kuwa Uwanja wa Taifa gharama zake ni kubwa.
Alifafanbua kuwa ikiwa mechi Uwanja wa Taifa imeingiza Milioni 100, Milioni 40 ni za Uwanja, NA Milioni 60 ndizo watakazogawana BMT, DRFA, TFF na Vilabu.
Wakati huo huo, Hassan Dalali, Mwenyekiti wa sasa wa Simba, amechukua fomu ya kugombea tena uongozi wa Klabu hiyo.
Kuingia kwa Dalali kumefikisha idadi ya Wagombea wa nafasi hiyo kuwa watano. Wengine ambao wameshachukua fomu hizo ni Andrew Dita Tupa, Mohammed Nyangamala, Aden Rage na Michael Wambura.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti waliochukua fomu ni Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Mwina Kaduguda na Godfrey Nyange 'Kaburu.
Wanaoomba nafasi ya Ujumbe ni Shehe Jumbe, Swed Kisilini Mkwabi, Hamis Yusuph Swed na Hamis Ramadhan Mkoma.
Yanga v Simba Jumapili
- Viongozi hawataki Wajanja kuvuna 'Shamba la Bibi!'
Wakati kila Klabu imeweka Timu zao kambini, Viongozi wa pande hizo mbili wanahaha kutafuta njia muafaka ili kudhibiti mapato yatakayotokana na viingilio vya milangoni ambayo mara nyingi huishia kwa wajanja na kufanya Uwanja huo ubatizwe jina “ Shamba la Bibi!”
Wakati wadau wa Simba na Yanga wakiingojea BIGI MECHI, wadau wa Simba wako kwenye kampeni za Uchaguzi wao Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mei 9 na tayari kumeibuka vijembe na kashfa za kila aina.
Imeripotiwa, Katibu Mwenezi wa Simba wa zamani, Said Rubeya ' Seydou' amemtaka Mwenyekiti wa sasa, Hassan Dalali, kutochukua fomu ya kugombea uongozi kwa kuwa hana sifa.
Inadaiwa Rubeya alisema kuwa Dalali hana elimu ya Kidato cha Nne kama kanuni za uchaguzi zinavyotaka na pindi akichukua fomu tu atamkatia rufaa.
Yanga yachuja Wachezaji
Yanga imetangaza kuwatema Wachezaji watano katika mchujo wa awali katika kufanikisha usajili wao kwa Msimu ujao.
Kutemwa Wachezaji hao watano kumetobolewa na Kocha wao kutoka Serbia, Kosta Papic, ambae amesema wanaweza kuihama Yanga hata sasa na pia hawatakuwemo kwenye Kikosi kitakachopambana na Watani wao wa Jadi, Simba, wikiendi ijayo katika mechi ya Ligi ya kukamilisha ratiba tu kwa vile Simba tayari ni Bingwa..
Papic aliwataja Wachezaji hao kuwa ni Robert Jama Mba, Honore Kabongo, Steven Bengo, Hamisi Yusufu na Moses Odhiambo.
Wambura nae achukua fomu Simba
Kiongozi wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania, Michael Wambura, ambae pia aliwahi kuwa kiongozi Simba amechukua fomu Klabuni hapo kugombea nafasi ya Uenyekiti.
Uchaguzi Mkuu wa Simba unatarajiwa kufanyika Mei 9.
Wambura ameungana na Aden Rage aliyechukua fomu mwishoni mwa wiki naye pia akiwania Uenyekiti nafasi inayoshikiliwa na Hassan Dalali.
Akizungumza na waandishi wa Habari hapo jana Jijini Dar es Salaam, Wambura, alitangaza mambo 18 ambayo anataka kuyafanya katika klabu hiyo endapo atachaguliwa na miongoni mwa mambo hayo ni kuhakikisha rasilmali na mali za klabu zinasimamiwa vizuri huku akiifanya Simba ijiendeshe kibiashara zaidi kwa mfumo wa kampuni na pia kutoa ajira za kudumu kwa wanachama .
KOMBE LA SHIRIKISHO LA AFRIKA: Simba kuanza nyumbani na Haras El Hedoud ya Misri
Simba ya Tanzania itachuana na Klabu ya Misri Haras El Hadoud Jijini Dar es Salaam hapo Aprili 25 katika Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya Kombe la Shirikisho la Afrika na marudiano ya Timu hizo ni huko Misri Jumapili, tarehe 9 Mei.
Simba imeingia Raundi hiyo ya Timu 16 baada ya kuichapa Lengthens ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-1 waliposhinda 3-0 huko Harare, Zimbabwe na 2-1 Dar es Salaam.
Nayo, Haras El Hedoud ilitoka sare 1-1 na Ethiopian Banks Nchini Ethiopia na kuichapa Timu hiyo mabao 5-0 ziliporudiana Nchini Misri hapo jana Jumapili Aprili 4.
Ratiba kamili ya Raundi ya Timu 16 ni:
Aprili 25
Coton Sport FC [Cameroun] v CD 1 de Agosto [Angola]
Simba [Tanzania] v Haras El Hedoud [Misri]
Alamal Atbar [Sudan] v CR Belouizdad [Algeria]
Petrojet [Misri] v Club Sportif Sfaxien [Tunisia]
FUS Rabat [Morocco] v Stade Malien de Bamako [Mali]
Warri Wolves [Nigeria] v Caps United FC [Zimbabwe]
AS-FAN [Niger] v Daring Club Motema Pembe [DR Congo]
AS Vita Club [DR Congo] v Enyimba International FC [Nigeria]
Simba 2 Lengthens 1
Simba leo kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wameweza kusonga mbele kuingia Raundi nyingine ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuichapa Lengthens ya Zimbabwe bao 2-1.
Hii ni mechi ya marudiano baada ya Simba kushinda mechi ya awali huko Harare, Zimbabwe kwa bao 3-0 mechi iliyochezwa wiki mbili zilizopita.
Katika Raundi inayofuata, Simba itacheza na Mshindi kati ya Haras El Hedoud ya Misri na Ethiopian Banks ya Ethiopia ambazo zinarudiana leo huko Misri baada ya kutoka sare 1-1 huko Ethiopia.
Wafungaji wa mabao ya Simba ni Mgosi na Nico Nyagawa.
Kipa Mzungu wa Yanga yuko Bondeni!
SuperSport United ya Afrika Kusini wako mbioni kumsajili Kipa Obren Circovic kutoka Serbia ambae amekuwa akiichezea Yanga kwa miaka miwili baada ya kufanya vizuri kwenye majaribio ya wiki kadhaa hivi karibuni huko Afrika Kusini.
Kocha wa Matsatsantsa, hilo ni jina maarufu la SuperSport United, Gavin Hunt, amesema wameamua kumbakisha Kipa huyo wa Yanga baada ya kuridhika na Uchezaji wake akiwa hapo.
Hunt amesema: “Anafanya vizuri. Tutazidi kumwangalia kabla hatujatoa uamuzi wa mwisho.”
Kipa Circoviv amesema anafurahishwa na hali ilivyo hapo Matsatsantsa na yuko tayari kuichezea Klabu hiyo iliyotwaa Ubingwa wa Bondeni mara 3 mfululizo.
Yanga yamliza Tegete
Imedaiwa Mchezaji wa Yanga, Jerry Tegete, alilia alipopata taarifa kuwa Klabu yake imemnyima ruhusa ya kuchezea Dalkurd ya Sweden kwa mkopo wa miezi mitatu kwa sababu tu wanataka arudi bongo kucheza mechi na Simba Aprili 11, mechi ambayo ni ya kukamilisha ratiba tu kwa vile Simba tayari ni Bingwa.
Tegete alifuzu majaribio ya wiki mbili huko Sweden na alitakiwa aanze mkataba wa Miezi mitatu kuanzia Jumatano iliyopita.
Wakala wa Tegete, Damas Ndumbaro, amesema Tegete atarudi Dar es Salaam kwa vile wameshindwa kukubaliana na Yanga.
Habari kutoka Yanga zimedai kuwa wameshindwa kufikia makubaliano kwa vile mkataba haukuwa wazi, ni wa mkopo na tena wa muda mfupi.
Rage kugombea Uenyekiti Simba
Ismael Aden Rage, aliewahi kuwa Makamu wa Pili wa TFF [Shirikisho la Soka Tanzania], amechukua fomu kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Simba katika Uchaguzi Mkuu wa Simba unaotarajiwa kufanyika Mei 9.
Mwenyekiti wa sasa wa Simba ni Hassan Dalali.
Aden aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba mwaka 1982 na kuiongoza Timu hiyo vizuri ikiwemo kuipeleka Simba Brazil, kuleta Makocha toka Brazil na Klabu kujiendesha yenyewe bila kutembeza kofia kuomba michango ya Wanachama.
Aden pia ashawahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Soka zikiwemo kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Dar es Salaam[ DRFA], Katibu Mkuu FAT [Chama cha Soka Tanzania] na Rais wa Klabu ya Moro United.
Kwa sasa, Ismael Aden Rage ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora.
Watu wengine waliochukua Fomu kugombea nyadhifa Simba ni Geofrey Nyange “Kaburu” na Mwina Kaduguda wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Makamu Mwenyekiti wa sasa ni Omar Gumbo.
AFRICAN CONFEDERATIONS CUP 2010:
Simba v Lengthens
Jumapili, Aprili 4
Maandalizi ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho la Afrika kati ya Simba ya Tanzania na Lengthens ya Zimbabwe yamekamilika ikiwa pamoja na kutangazwa viingilio vya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam hapo Jumapili
Katika pambano la kwanza wiki mbili zilizopita Jijini Harare, Zimbabwe, Simba ilishinda mabao 3-0 na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano.
Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela, alivitaja viingilio hivyo kuwa ni Sh, 30,000 kwa viti maalumu vya rangi ya bluu wakati katika jukwaa kuu viti vya rangi nyekundu na njano kiingilio kitakuwa Sh 20,000.
Alisema kiingilio katika jukwaa la kijani kitakuwa Sh 10,000 wakati katika eneo la mzunguko kiingilio kitakuwa Sh, 5,000.
Mwakalebela pia amesema Marefa watatoka Uganda nao ni Ali Kayango, Kitti Kahaya na Mussa Ngobi.
Alisema: “Mwamuzi wa nne ni Israel Nkongo, toka Tanzania na Kamishna ni Andre Mtine kutoka Zambia.”
Simba wakifuzu kupita watapambana na Mshindi kati ya Haras El Hedoud ya Misri au Ethiopian Banks ya Ethiopia ambazo pia zitarudiana Jumapili baada ya kutoka 1-1 huko Ethiopia katika mechi ya awali.
Nae Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda, amewataka Wana Simba kushikama ili kuhakikisha ushindi katika mechi hiyo.
Tenga aionya Simba
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania [TFF], Leodegar Tenga, ameionya Klabu ya Simba isibweteke na ushindi wao wa 3-0 walioupata ugenini huko Harare walipoichapa Lengthens ya Zimbabwe wakati watakaporudiana Siku ya Jumapili katika Mashindano ya CAF mjini Dar es Salaam.
Ingawa Kocha Msaidizi wa Lengthens Paul ‘Popo’ Chimalizeni amekiri ni kazi kubwa kuupindua ushindi huo wa 3-0, Tenga amewaambia Simba: “Ushindi wa 3-0 ni mkubwa lakini wasibweteke! Wasidhani wameshaitoa Timu hiyo ya Zimbabwe! Katika Soka kuumwaga ushindi wa 3-0 si kitu kisichowezekana!”
Tenga amesema alikutana na Viongozi wa Simba na kuwapa mawaidha hayo na kuwataka waitayarishe vizuri Timu yao.
Simba ndio Timu ya kwanza Tanzania kufika Fainali za Kombe la CAF mwaka 1993 walipofungwa 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Straika wa Yanga, Tegete, aula Sweden!
Mchezaji wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Jerry Tegete, amefuzu majaribio yake kwenye Klabu ya Daraja la Kwanza la Sweden Dalkurd.
Wakala wa Mchezaji huyo, Damas Ndumbaro, amesema Dalkurd itamchukua Tegete kwa mkopo wa Miezi mitatu baada ya kupasi majaribio ya wiki mbili na Klabu hiyo.
Hata hivyo inaelekea kuna mvutano kati ya upande wa Tegete na Yanga kwani Klabu hiyo inamtaka Tegete arudi nyumbani ili acheze mechi ya Ligi na Mahasimu wao wakubwa Simba hapo Aprili 11 lakini upande wa Mchezaji huyo unataka aendelee na kibarua kipya huko Sweden.
Mechi hiyo ya Simba na Yanga ni ya kukamilisha ratiba tu kwani Simba ameshanyakua Ubingwa.
No comments:
Post a Comment