Thursday 17 September 2009

Adebayor akiri kwa FA ‘kumtimba’ van Persie!!!
Emmanuel Adebayor pamoja na Klabu yake Manchester City zimekubali kwa ‘shingo upande’ kosa la aliloshitakiwa na FA la kutaka kumuumiza Mchezaji wa Arsenal Robin van Persie kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi iliyopita Uwanjani City of Manchester ambayo Man City waliishinda Arsenal 4-2.
Refa wa mechi hiyo Mark Clattenburg hakuona kosa hilo lakini amekiri kwa FA, baada ya kushuhudia marudio ya video, kuwa angemlima Adebayor Kadi Nyekundu kama angeliona.
Adebayor alipewa mpaka jana Jumatano ajitetee lakini ameamua kutofanya hivyo na kukubali kosa na adhabu atakayopewa ambayo inategemewa kuwa ni kufungiwa mechi 3 ya kwanza ikiwa ile ya Jumapili Man City watakapocheza na Man U.
Adhabu hiyo itajulikana leo kesi hiyo itakaposikilizwa.
Adebayor anakabiliwa na kosa jingine nalo ni la kuonyesha mwenendo usiokubalika wakati akishangilia goli lake siku hiyo hiyo Man City walipocheza na Arsenal na kwenda kuwachokoza Mashabiki wa Arsenal.
Uamuzi wa kosa hili utajulikana Septemba 30.

Bosi Kenyon abwaga manyanga Chelsea!!!
Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Chelsea, Peter Kenyon, ametangaza kuachia ngazi wadhifa huo kuanzia mwishoni mwa Oktoba baada ya kukalia kiti hicho kwa miaka mitano.
Kabla ya kuwa Chelsea, Kenyon, alishika wadhifa kama huo Manchester United.
Ingawa Kenyon anaachia ngazi ya ubosi, atabaki kuwa Mkurugenzi wa kawaida kwenye Klabu hiyo na kuiwakilisha kwenye vikao mbalimbali vya soka huko Ulaya.
Chelsea bado haijatangaza mrithi wake.
Timu za England zapeta!!! Eto’o, Ibrahimovic ngoma droo!!!
Timu za England zimeendeleza wimbi la ushindi kwenye mechi zao za kwanza kwenye Makundi UEFA CHAMPIONS LEAGUE baada ya Liverpool kushinda 1-0 dhidi ya Debrecen ya Hungary Uwanjani Anfield na Arsenal, waliojikuta wako nyuma 2-0 baada ya dakika 4 tu za mchezo, kuibuka na ushindi wa 3-2 huko Ubelgiji walipokwaana na Standard Liege.
Jumanne, Chelsea na Manchester United zilipata ushindi wa 1-0 kwa kila Timu baada ya Chelsea kuibwaga FC Porto Stamford Bridge na Man U kuishinda Besiktas ugenini Uwanjani Inonu huko Instanbul, Uturuki.
Bao la ushindi kwa Liverpool lilifungwa na David Kuyt baada ya mkwaju wa Torres kutemwa na Kipa wa Debrecen.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Bendtner, Vermaelen na Eduardo.
Katika ‘Bigi Mechi’, huku Dunia nzima ikawakazia macho Washambuliaji Samuel Eto’o wa Inter Milan na Zlatan Ibrahimovic wa FC Barcelona, timu hizo zilitoka suluhu 0-0 zilipocheza nyumbani kwa Inter Milan Uwanjani San Siro.
Kivutio kwa Washambuliaji hao kimekuja baada ya Mastaa hao kubadilishana Timu Eto’o akitoka Barca kwenda Inter na Ibrahimovic toka Inter kwenda Barca.
Ingawa mechi ilitawaliwa na Mabingwa Watetezi Barca na Ibrahimovic kukosa nafasi mbili tatu, matokeo hayo huenda yakawaridhisha Makocha Jose Mourinho wa Inter na Gurdiola wa Barca hasa kwa vile Timu hizi ndizo zinazotegemewa kusonga mbele toka Kundi hili.
MATOKEO KAMILI MECHI ZA UEFA CHAMPIONS LEAGUE:
Jumatano, 16 Septemba 2009
Dynamo Kiev 3 v v Rubin Kazan 1
Inter Milan 0 v Barcelona 0
Liverpool 1 v Debrecen 0
Lyon 1 v Fiorentina 0
Olympiakos 1 v AZ Alkmaar 0
Sevilla 2 v Unirea Urziceni 0
Standard Liege 2 v Arsenal 3
VfB Stuttgart 1 v Rangers 1

MECHI ZIJAZO UEFA CHAMPIONS LEAGUE:
Jumanne, 29 Septemba 2009
AZ Alkmaar v Standard Liege
Arsenal v Olympiakos
Barcelona v Dynamo Kiev
Debrecen v Lyon
Fiorentina v Liverpool
Rangers v Sevilla
Rubin Kazan v Inter Milan
Unirea Urziceni v VfB Stuttgart
Jumatano, 30 Septemba 2009
AC Milan v FC Zurich
Apoel Nicosia v Chelsea
Bayern Munich v Juventus
Bordeaux v Maccabi Haifa
CSKA Moscow v Besiktas
FC Porto v Atletico Madrid
Man U v Wolfsburg
Real Madrid v Marseille
EUROPA LIGI LEO:
[Kuna jumla ya mechi 24 na hapa zinatajwa mechi zinazohusu Timu za Uingereza tu]
Alhamisi, 17 Septemba 2009
Hapoel Tel Aviv FC V Celtic
PFC CSKA Sofia v Fulham
Everton v AEK Athens
LIGI KUU ENGLAND WIKIENDI HII:
[saa za bongo]
Jumamosi, 19 Septemba 2009
[saa 8 dak 45 mchana]
Burnley v Sunderland
[saa 11 jioni]
Bolton v Stoke
Hull v Birmingham
[saa 1 na nusu usiku]
West Ham v Liverpool
Jumapili, 20 Septemba 2009
[saa 9 na nusu mchana]
Man U v Man C
[saa 10 jioni]
Wolves v Fulham
[saa 11 jioni]
Everton v Blackburn
[saa 12 jioni]
Chelsea v Tottenham

Wednesday 16 September 2009

Klabu za LIGI KUU kuwa na Kikosi chenye Wachezaji 25 tu!!
Klabu za Ligi Kuu England zimepiga kura na kukubaliana kuwa kuanzia msimu ujao Klabu zinatakiwa ziwe na Kikosi cha Wachezaji 25 tu na kati yao si zaidi ya Wachezaji 17 wanatakiwa wawe na umri wa zaidi ya miaka 21 na wanaweza kutoka nje ya England na Wales.
Wachezaji wanane kwenye Kikosi hicho cha Wachezaji 25 ni wale waliofundishwa ndani ya Klabu hizo ama popote ndani ya England na Wales na wawe chini ya miaka 21 na wamefunzwa ndani ya England na Wales kwa muda usio chini ya miaka mitatu.
Hata hivyo Klabu zimeruhusiwa kuwa na Wachezaji zaidi ya 25 ili mradi Wachezaji zaidi ya hao 25 wawe na umri chini ya miaka 21.
Kila Klabu inatakiwa kuwasilisha Vikosi vyao mwishoni mwa mwezi Agosti dirisha la uhamisho linapofungwa na wanaweza kuwasilisha tena marekebisho ya Vikosi vyao baada ya kipindi kingine cha uhamisho mwishoni mwa Januari Dirisha la Uhamisho linapofungwa.
Scholes aipa ushindi Man U ugenini, Anelka aipaisha Chelsea kwao!!
Jana kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Klabu za England zilianza vyema kampeni zao za kutwaa Ubingwa wa Ulaya baada ya kushinda mechi zao za kwanza kwenye Makundi huku Manchester United wakishinda bao 1-0, bao lililofungwa na Paul Scholes dakika ya 77, wakiwa ugenini Instanbul, Uturuki walipocheza na Besiktas na Chelsea, wakiwa nyumbani Stamford Bridge, walipata ushindi kupitia Nicolas Anelka goli 1-0 dhidi ya FC Porto ya Ureno.
Leo, Klabu nyingine za England, Arsenal na Liverpool, zitatinga uwanjani kufungua kampeni zao za Ulaya na Liverpool watakuwa nyumbani Anfield kuikaribisha Debrecen ya Hungary wakati Arsenal watasafiri hadi Ubelgiji kucheza na Standard Liege.

MATOKEO KAMILI MECHI ZA JANA:
Atletico Madrid 0 v Apoel Nicosia 0
Besiktas 0 v Man U 1
Chelsea 1 v FC Porto 0
FC Zurich 2 v Real Madrid 5
Juventus 1 v Bordeaux 1
Maccabi Haifa 0 v Bayern Munich 3
Marseille 1 v AC Milan 2
Wolfsburg 3 v CSKA Moscow 1
MECHI ZA LEO Jumatano, 16 Septemba 2009
[saa 3 dak 45 usiku]
Dynamo Kiev v Rubin Kazan
Inter Milan v Barcelona
Liverpool v Debrecen
Lyon v Fiorentina
Olympiakos v AZ Alkmaar
Sevilla v Unirea Urziceni
Standard Liege v Arsenal
VfB Stuttgart v Rangers

Tuesday 15 September 2009

Besiktas v Manchester United
Manchester United, leo ugenini ndani ya Inonu Stadium huko Uturuki, itavaana na Besiktas ikiwa ni siku 111 tangu wafungwe 2-0 Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na FC Barcelona huko Rome.
Man U, wakiongozwa na Meneja wao Sir Alex Ferguson pamoja na Wachezaji wao Maveterani, wamekiri kipigo cha Rome kimewakera sana na sasa wanaomba wakutane tena na Barcelona ili walipe kisasi.
Man United wanasafiri kwenda Uturuki mara baada ya ushindi mtamu wa ugenini kwenye LIGI KUU England walioupata baada ya kuichabanga Tottenham mabao 3-1 huku wakitandaza ‘Soka Tamu!’
Man United wako Kundi moja na Besiktas, CSKA Moscow na VfB Wolfsburg.
Besiktas, wakiongozwa na Kocha Mustafa Denizli, wataingia uwanjani leo mara tu baada ya kupigwa mabao 3-0 na Mahasimu wao wa Mjini Instanbul Timu ya Galatasaray siku ya Jumamosi.
Huko Uturuki, Timu zinazonguruma sana ni Fenerbahce na Galatasaray lakini msimu huu ni Besiktas pekee ndio wamo UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mechi ya leo itamkutanisha Kipa wa zamani wa Uturuki, Rustu Recber, na Wayne Rooney kwa mara ya kwanza tangu Rooney amtoboe Recber kwa bao 3 mguuni kwake kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa Old Trafford mwaka 2004 kati ya Man United na Fenerbahce na Rustu Recber akiwa Kipa wa Fenerbahce na Rooney akiichezea Man U mechi yake ya kwanza tangu anunuliwe toka Everton. Man U walishinda mechi hiyo 6-2.
Waamuzi wa mechi hii ni kutoka Italia watakaoongozwa na Refa Nicola Rizzoli.
Chelsea v FC Porto
Chelsea wanaanza kampeni ya kutwaa Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE, ambalo hawajawahi kulitwaa, wakiwa nyumbani Stamford Bridge kwa kucheza na FC Porto ya Ureno.
Chelsea, katika misimu miwili iliyopita, walikaribia mno kutwaa Kombe hilo lakini kwa mara zote walibwagwa kwa uchungu.
Msimu wa 2007/8 walifika Fainali na kutolewa na Manchester United kwa penalti na hivyo kulikosa Kombe.
Msimu uliopita, baada ya kutoka suluhu 0-0 ugenini na Barcelona katika Nusu Fainali, walibwagwa kwao Stamford Bridge wakiwa wanaongoza 1-0 hadi dakika za majeruhi ndipo Andres Iniesta wa Barcelona akasawazisha bao na kuwaingiza Barcelona Fainali kwa goli la ugenini.
Uchungu na hasira ya kubwagwa mechi hiyo iliwasababisha Wachezaji wa Chelsea, Didier Drogba na Jose Bosingwa, wapandwe jazba na kumzonga, kumtukana na kumkashifu Refa.
UEFA iliwafungia Drogba na Bosingwa kwa vitendo hivyo na wataikosa mechi ya leo.
Kwa sasa Chelsea wanae Meneja mpya msimu huu, Mtaliana Carlo Ancelotti, ambae ameshawahi kuuchukua Ubingwa wa Ulaya akiwa na Klabu ya AC Milan.
Msimu huu, Chelsea wamecheza mechi 5 za LIGI KUU na kushinda zote.
FC Porto, chini ya Meneja Jesualdo Ferreira, msimu uliokwisha kwenye Kombe hili walitolewa Robo Fainali na Manchester United kwa jumla ya mabao 3-2.
Msimu huu, FC Porto, huko kwao, wameshacheza mechi za Ligi 4 na kutofungwa mpaka sasa.
Waamuzi wa mechi ya leo wanatoka Austria na Refa ni Konrad Plautz.
Adebayor ana mashtaka mawili FA, atakiwa kujibu kabla kesho!!!!
Mshambuliaji wa Manchester City, Emmanuel Adebayor, leo amepewa rasmi mashtaka yake mawili kutokana na vitendo vyake katika mechi ya Jumamosi iliyopita ya LIGI KUU kati ya Man City na Arsenal ambayo Man City walishinda 4-2.
Shtaka la kwanza ni la kutaka kumuumiza Robin van Persie kwa makusudi na la pili ni la kuonyesha mwenendo usiokubalika wakati akishangilia goli lake na kwenda kuwachokoza Mashabiki wa Arsenal.
Adebayor amepewa mpaka Jumatano saa 2 usiku saa za bongo kutoa utetezi wake.
Akipatikana na hatia kwa kosa la kutaka kumuumiza van Persie kwa makusudi basi atafungiwa mechi 3 na adhabu hii itaanza mara moja ikimaanisha mechi ya kwanza kuikosa ni ile ya LIGI KUU ya Jumapili pale Man City watakapoenda Old Trafford kukwaana na Mahasimu wao Manchester United.
FA imesema Refa Mark Clattenburg alisema hakuona Adebayor akimtimba van Persie lakini amethibitisha endapo angeliona tukio hilo basi angemtoa Adebayor kwa Kadi Nyekundu.
Adhabu ya kosa la pili, ikiwa atapatikana na hatia, itatangazwa baadae.
UEFA yafuta kifungo cha Eduardo, huru kucheza kesho UEFA CHAMPIONS LEAGUE!!!
Rufaa ya Arsenal waliyokata kwa UEFA kupinga kwa adhabu ya Mshambuliaji wao mwenye asili ya Brazil lakini ni raia wa Croatia, Eduardo, aliyopewa kwa kumhadaa Refa Manuel Gonzalez katika mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Celtic hapo Agosti 26, imekubaliwa na UEFA na sasa adhabu ya kufungiwa mechi mbili imefutwa.
Eduardu sasa ni ruksa kucheza mechi ya kesho ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ugenini Ubelgiji wakati Arsenal watakapokwaana na Standard Liege Uwanja wa Maurice Dufrasne.
Nahodha wa Everton Phillip Neville nje muda mrefu!!
Nahodha wa Everton, Phillip Neville, ambae ni mdogo wake Nahodha wa Manchester United, Gary Neville, atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuumia goti walipogongana na Dickson Etuhu wa Fulham katika mechi ya LIGI KUU siku ya Jumapili Uwanjani Craven Cottage na Fulham kushinda 2-1.
Meneja wa Everton David Moyes amethibitisha habari hizo na kusema Neville ataenda kwa Wataalam Jijini London kwa uchunguzi zaidi na hapo ndipo watajua kwa uhakika muda gani atakosekana.
Man City wasubiri litakalomkuta Adebayor!!! Shabiki amlalamikia van Persie Polisi!!
Manchester City wanasubiri kujua hatima ya Mchezaji wao Emmanuel Adebayor kufuatia matukio mawili yanayomhusu yeye yalyotokea kwenye mechi ya LIGI KUU Jumamosi iliyopita ambayo Man City waliifunga Arsenal bao 4-2 Uwanjani City of Manchester.
Tukio la kwanza ni ushangiliaji wa Adebayor alipofunga bao la 3 na kwenda kushangilia mbele ya Washabiki wa Arsenal ambao walikasirika na kutaka kuvamia uwanja lakini wakadhibitiwa na Walinzi pamoja na Polisi.
Katika tukio hilo Mlinzi mmoja alipigwa kichwani na kupoteza fahamu kwa dakika 5 na Polisi wa Manchester wamesema Adebayor ndie chanzo cha fujo hizo.
Refa Mark Clattenburg alimpa Adebayor Kadi ya Njano kwa tukio hilo.
Tukio la pili ni pale Adebayor alipomgusa usoni Robin van Persie kwa buti na ingawa Refa hakuchukua hatua yeyote kwa Adebayor, van Persie alidai Adebayor alikusudia kumuumiza.
Adebayor mwenyewe amekana hilo na kusema alimwomba radhi van Persie ambae amepinga hakuombwa radhi.
FA wanatakiwa kutoa uamuzi kabla ya leo [Jumanne] saa 2 usiku [saa za bongo] kama watachukua hatua zozote kwa Adebayor na baada ya hapo Klabu inapewa masaa 24 kuamua kukata rufaa ikiwa adhabu imetolewa.
Wakati huo huo, ameibuka Shabiki mmoja aliewakilisha malalamiko yake kwa Polisi kuwa van Persie aliwatukana alipokwenda mbele ya Mashabiki wa Man City baada ya kuifungia Arsenal goli dakika ya 62.
Polisi wamesema wanachunguza malalamiko hayo.

Monday 14 September 2009

Park apewa Mkataba mpya wa miaka mitatu!!
Kiungo wa Manchester United kutoka Korea Park Ji-sung inasemekana amesaini Mkataba mpya wa miaka mitatu kufuatana na taarifa alizotoa Wakala wake aitwae Kim Jung-Soo.
Park alijiunga na Manchester United mwaka 2005 akitokea Klabu ya PSV Eindhoven na sasa atabaki Old Trafford hadi 2012.
Park ndie Mchezaji wa kwanza kutoka Bara la Asia kucheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE alipocheza mechi ya Fainali dhidi ya Barcelona mwezi Mei mwaka huu.
Benki ya Standard Chartered yawa Mfadhili mpya Liverpool
Standard Chartered Bank itakuwa ndio Mfadhili mpya wa Liverpool baada ya kusaini mkataba wa miaka minne utakaoanza Julai mwakani na kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2013/14.
Kwa kusaini mkataba huo wenye thamani ya Pauni Milioni 80, Liverpool watatengana na Mfadhili wao mkuu Kampuni ya Bia ya Carlsberg ambae walikuwa nae kwa miaka 17.
Hivi karibuni Manchester United nao walipata Ufadhili mkubwa kutoka Kampuni kubwa ya Kimarekani iitwayo Aon na wao pia mkataba utaanza mwakani.
UEFA CHAMPIONS LEAGUE KESHO:
[mechi zote saa 3 dak 45 usiku bongo taimu]
Jumanne, 15 Septemba 2009
Atletico Madrid v Apoel Nicosia
Besiktas v Man U
Chelsea v FC Porto
FC Zurich v Real Madrid
Juventus v Bordeaux
Maccabi Haifa v Bayern Munich
Marseille v AC Milan
Wolfsburg v CSKA Moscow
Jumatano, 16 Septemba 2009
Dynamo Kiev v Rubin Kzan
Inter Milan v Barcelona
Liverpool v Debrecen
Lyon v Fiorentina
Olympiakos v AZ Alkmaar
Sevilla v Unirea Urziceni
Standard Liege v Arsenal
VfB Stuttgart v Rangers
Chelsea yakana madai Abramovich alianguka na kutojiweza akipanda Mlima Kilimanjaro!!!!
Klabu ya Chelsea imekana vikali taarifa kuwa Mmiliki wake Roman Abramovich [pichani akiwa na Kocha Hiddink] alianguka na kutojiweza wakati akipanda Mlima Kilimanjaro Nchini Tanzania wiki iliyopita.
Ilidaiwa kuwa Abramovich alipata matatizo ya kutopumua vizuri alipofika Futi 15,000 juu na hivyo kushindwa kufika kileleni ambako ni zaidi ya Futi 19,000 na kuwaacha baadhi ya watu kwenye msafara wake waendelee juu.
Chelsea imepinga taarifa hizo na pia kusema aliekuwa Kocha wao hivi karibuni Guus Hiddink hakuwamo kwenye msafara huo kama ilivyodaiwa kwani alikuwa Uingereza na Timu ya Taifa ya Urusi, akiwa ndie Kocha wake, iliyocheza na Wales kwenye mechi ya Kombe la Dunia wiki iliyopita.

Klabu ya Chelsea vilevile imekana kuwa Abramovich ilibidi atibiwe na Madaktari kwa matatizo hayo.
Chelsea ilikuwa ikijibu tuhuma zilizozagaa kuwa msafara wake haukujitayarisha vyema hasa kupata uzoefu wa hali ya hewa ya hapo Kilimanjaro na hasa kukabili upungufu wa hewa ya Oksijeni kwenye mwinuko mkubwa.
POLISI wamlaumu Adebayor kwa fujo za Mashabiki!! Kwa kumpiga buti van Persie huenda akaikosa Man U Jumapili!!
Mshambuliaji wa Manchester City, Emmanuel Adebayor, sasa yuko matatani kwa vitendo vyake viwili alivyovitenda kwenye mechi ya LIGI KUU Jumamosi ambayo Man City waliifunga Arsenal 4-2.
Adebayor alipofunga goli la 3 alikimbia hadi kwa Mashabiki wa Arsenal na kushangilia na Mashabiki hao walipandwa hasira na kutaka kuvamia uwanja lakini Walinzi na Polisi waliokuwepo walidhibiti fujo hizo. Refa Mark Clattenburg alimpa Adebayor Kadi ya Njano kwa kitendo hicho.
Hata hivyo Mlinzi mmoja alijeruhiwa na kupoteza fahamu kwa dakika 5.
Polisi wa Manchester wamesema ni ushangiliaji wa Adebayor ndio uliosababisha fujo hizo na wameliacha suala hilo kwa Man City na FA kuamua nini cha kufanya.
FA imeshatamka inachunguza tukio hilo.
Lakini huenda Adebayor akachukuliwa hatua za haraka na kufungiwa mechi 3 na hivyo kuikosa ‘BIGI MECHI’ ya Manchester kati ya Man U v Man City Jumapili ijayo baada ya Adebayor kumkanyaga usoni Robin van Persie wa Arsenal kitendo ambacho Mchezaji huyo wa Arsenal amesema kilikuwa kusudi ingawa Adebayor anadai ni bahati mbaya na alimwomba radhi van Persie.
Refa hakuona tukio hilo.
LIGI KUU England: Fulham 2 Everton 1
Wakiwa nyumbani uwanjani Craven Cottage, Fulham walijikuta wako nyuma kwa bao 1-0 hadi mapumziko kwa bao la Tim Cahill wa Everton aliloingiza dakika ya 33.
Kipindi cha pili Fulham walikaza buti na kufunga bao mbili kupitia Konchesky dakika ya 57 na Winga Damien Duff aliwapa ushindi dakika ya 79.
Mpaka sasa baada ya mechi 4 Fulham wana pointi 6 na Everton pointi 3.

Sunday 13 September 2009

Kipa wa Besiktas Rustu Recber augwaya Mpira wa Adidas unaotumika Ulaya!!!
Adai unawasaidia sana Washambuliaji kuliko Makipa!!!

Kipa wa Besiktas ya Uturuki, Rustu Recber, ambae alikuwa Kipa nambari wani Timu ya Taifa ya Uturuki, amedai mpira uliotengenezwa na Kampuni ya Adidas unaoitwa ‘Finale 9’ ambao hauna maungio kwani umeumbwa kwa utaalam wa hali ya juu wa kisasa, unawasaidia sana Washambuliaji kwa vile huwezi kutabiri utaruka vipi na kwenda wapi.
Mpira huo ndio utatumika huko Ulaya kwenye mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mpira huo ‘Finale 9’ ulitumika kwa mara ya kwanza kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu uliokwisha kati ya Manchester United na FC Barcelona.
Recber amesema: “Tangu 2002 mipira yote iliyotengenezwa na Adidas hubadili spidi na mwelekeo ikiwa hewani baada ya kupigwa shuti! Hii ni ngumu kwa Makipa lakini ni furaha kwa Washambuliaji na UEFA kwani wanataka magoli mengi kuwafurahisha Washabiki!”
Maoni hayo ya Recber yameungwa mkono na Kipa wa Spain anaedakia Real Madrid Iker Casillas.
Besiktas siku ya Jumanne watakuwa wenyeji wa Manchester United kwenye mechi ya kwanza ya Kundi lao kwenye ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

Birmingham 0 Aston Villa 1
Goli la dakika ya 85 la Gabriel Agbonlahor limewapa ushindi Aston Villa waliokuwa wakicheza ugenini Uwanja wa St Andrews na kuwaua Mahasimu wao Birmingham katika mechi ya leo ya LIGI KUU ENGLAND iliyozikutanisha Timu mbili zilizo mji mmoja wa Birmingham.
Birmingham walijitahidi kutaka kulipa kisasi cha kipigo cha 5-1 walichokipata toka kwa Aston Villa mara ya mwisho Timu hizi zilipokutana lakini mechi ilikuwa ngumu kwa kila upande na nafasi zilikuwa za shida.
FA kuchunguza matukio ya Adebayor mechi ya Man City v Arsenal!!!
Bosi wa FA, Chama cha Soka England, Ian Watmore amesema watachunguza matukio mawili yanayomhusu Mshambuliaji wa Manchester City Emmanuel Adebayor yaliyotendeka kwenye mechi ya jana ya LIGI KUU ambayo Manchester City waliwafunga Arsenal 4-2.
Adebayor, baada ya kufunga bao la 3, alikimbia mita zaidi ya 90 kuwafuata Washabiki wa Arsenal na kushangilia. Kitendo hicho kiliwaudhi Washabiki hao na ikabidi Walinzi pamoja na Polisi wafanye kazi ya ziada kuwatuliza wasilete fujo. Refa Mark Clattenburg alimpa Kadi ya Njano Adebayor kwa kosa hilo.
Lakini, baada ya mechi, Mshambuliaji wa Arsenal, Robin van Persie, alidai alitimbwa makusudi usoni na Adebayor na Adebayor mwenyewe amekiri buti yake ilimpiga van Persie usoni lakini ilkuwa bahati mbaya na alimwomba msamaha van Persie ingawa Mchezaji huyo alikataa kuwa aliombwa msamaha na akabaki aking’ang’ania Adebayor alikusudia.
Adebayor pia aliomba msamaha kuhusu ushangiliaji wake na kudai alipandwa na furaha baada ya kufunga goli hivyo hakufikiria kile anachotenda.
Tottenham 1 Manchester United 3
Manchester United, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu England, jana wakiwa ugenini mjini London Uwanjani White Hart Lane nyumbani kwa Tottenham, timu ambayo ilikuwa haijafungwa hata mechi moja msimu huu wa Ligi, jana mbali ya kujikuta iko nyuma kwa bao 1-0 lilofungwa sekunde ya 51 tangu mechi ianze na Jermaine Defoe na baadae ikijikuta inacheza watu 10 baada ya Mchezaji wao Mkongwe Paul Scholes kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu, ilitoa somo la hali ya juu ya jinsi ‘Soka Bora na Tamu” linavyochezwa.
Baada ya Manchester United kufungwa bao hilo moja walitulia na kutandaza soka la hali ya juu na kusawazisha bao hilo kupitia Mkongwe Ryan Giggs aliefunga kwa frikiki murua ambayo sasa itawafanya Washabiki wake wamsahau mpigaji frikiki wao wa kawaida Cristiano Ronaldo.
Mbrazil Chipukizi Anderson, alieonyesha ukomavu mkuu katika kiungo, aliipatia Man U bao la pili na la kwanza kwake kwenye Ligi Kuu tangu ajiunge Man U.
Hadi mapumziko Tottenham 1 Man U.
Kipindi cha pili ndipo, Paul Scholes, baada ya tayari kuwa na Kadi moja ya Njano, alipewa Kadi ya pili ya Njano baada ya kuonekana amemchezea Rafu Tom Huddlestone ingawa marudio ya video yalionyesha ni Mchezaji wa Spurs ndie aliecheza rafu. Hiyo ilikuwa dakika ya 59 na Scholes akapewa Kadi Nyekundu.
Hata hivyo, dakika ya 79, Wayne Rooney alifunga bao zuri baada ya kuihadaa ngome na Kipa Cudicini wa Spurs.
Tottenham: Cudicini, Corluka, King, Bassong, Assou-Ekotto, Lennon, Huddlestone, Palacios, Defoe, Crouch, Keane. Akiba: Gomes, Hutton, Bentley, Jenas, Pavlyuchenko, Naughton, Kranjcar.
Man Utd: Foster, O'Shea, Ferdinand, Vidic, Evra, Fletcher, Scholes, Anderson, Giggs, Berbatov, Rooney. Akiba: Kuszczak, Owen, Carrick, Nani, Fabio Da Silva, Jonathan Evans, Valencia.
Fergie akerwa na Refa kumtoa Scholes
Sir Alex Ferguson ameeleza kuwa Refa Andre Marriner kumpa Kadi Nyekundu Paul Scholes katika mechi ya jana Manchester United waliyoifunga Tottenham ni kitendo ‘kibaya sana’ na hakikustahili.
Schools alipewa Kadi mbili za Njano, na ya pili ikiwa dakika ya 59 walipovaana na Tom Huddlestone na hivyo kupata hiyo Nyekundu.
Ferguson alilalamika: “Ni makosa kumtoa! Na tungeweza kuathirika, tuko ugenini tunaongoza 2-1 dakika ya 59 na tunabakishwa mtu 10! Hakumgusa! Nimetizama video ile mara 2 na pengine ni Huddlestone aliecheza rafu!”
Van Persie adai Adebayor alimtimba makusudi amuumize!!!
=Adebayor huenda akasulubiwa na FA kwa ushangiliaji!!!
Emmanuel Adebayor, aliefunga bao moja dhidi ya Timu yake ya zamani Arsenal katika mechi ya jana ambayo Manchester City iliipiga Arsenal 4-2, huenda akawa matatani na FA hasa baada ya kufunga goli hilo la 3 na kisha kukimbia nusu ya Uwanja na kwenda mbele ya Mashabiki wa Arsenal kushangilia kitendo ambacho Refa alimpa Kadi ya Njano.
Mashabiki hao wa Arsenal walichukizwa sana na kitendo hicho na ilibidi Polisi na Walinzi wawatulize.
Ndani ya uwanja, Mchezaji wa Arsenal, Robben van Persie amedai Adebayor alimkanyaga usoni makusudi ingawa Adebayor mwenyewe amekiri hilo lakini amesema ni bahati mbaya na alimwomba radhi van Persie.
Kitendo hicho hakikuonekana na Refa lakini van Persie amepinga kuwa Adebayor alimwomba radhi na aliendelea kung’ang’ania alitimbwa kusudi
.
Powered By Blogger