Sunday 13 September 2009

Birmingham 0 Aston Villa 1
Goli la dakika ya 85 la Gabriel Agbonlahor limewapa ushindi Aston Villa waliokuwa wakicheza ugenini Uwanja wa St Andrews na kuwaua Mahasimu wao Birmingham katika mechi ya leo ya LIGI KUU ENGLAND iliyozikutanisha Timu mbili zilizo mji mmoja wa Birmingham.
Birmingham walijitahidi kutaka kulipa kisasi cha kipigo cha 5-1 walichokipata toka kwa Aston Villa mara ya mwisho Timu hizi zilipokutana lakini mechi ilikuwa ngumu kwa kila upande na nafasi zilikuwa za shida.
FA kuchunguza matukio ya Adebayor mechi ya Man City v Arsenal!!!
Bosi wa FA, Chama cha Soka England, Ian Watmore amesema watachunguza matukio mawili yanayomhusu Mshambuliaji wa Manchester City Emmanuel Adebayor yaliyotendeka kwenye mechi ya jana ya LIGI KUU ambayo Manchester City waliwafunga Arsenal 4-2.
Adebayor, baada ya kufunga bao la 3, alikimbia mita zaidi ya 90 kuwafuata Washabiki wa Arsenal na kushangilia. Kitendo hicho kiliwaudhi Washabiki hao na ikabidi Walinzi pamoja na Polisi wafanye kazi ya ziada kuwatuliza wasilete fujo. Refa Mark Clattenburg alimpa Kadi ya Njano Adebayor kwa kosa hilo.
Lakini, baada ya mechi, Mshambuliaji wa Arsenal, Robin van Persie, alidai alitimbwa makusudi usoni na Adebayor na Adebayor mwenyewe amekiri buti yake ilimpiga van Persie usoni lakini ilkuwa bahati mbaya na alimwomba msamaha van Persie ingawa Mchezaji huyo alikataa kuwa aliombwa msamaha na akabaki aking’ang’ania Adebayor alikusudia.
Adebayor pia aliomba msamaha kuhusu ushangiliaji wake na kudai alipandwa na furaha baada ya kufunga goli hivyo hakufikiria kile anachotenda.

No comments:

Powered By Blogger