Thursday, 17 September 2009

Adebayor akiri kwa FA ‘kumtimba’ van Persie!!!
Emmanuel Adebayor pamoja na Klabu yake Manchester City zimekubali kwa ‘shingo upande’ kosa la aliloshitakiwa na FA la kutaka kumuumiza Mchezaji wa Arsenal Robin van Persie kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi iliyopita Uwanjani City of Manchester ambayo Man City waliishinda Arsenal 4-2.
Refa wa mechi hiyo Mark Clattenburg hakuona kosa hilo lakini amekiri kwa FA, baada ya kushuhudia marudio ya video, kuwa angemlima Adebayor Kadi Nyekundu kama angeliona.
Adebayor alipewa mpaka jana Jumatano ajitetee lakini ameamua kutofanya hivyo na kukubali kosa na adhabu atakayopewa ambayo inategemewa kuwa ni kufungiwa mechi 3 ya kwanza ikiwa ile ya Jumapili Man City watakapocheza na Man U.
Adhabu hiyo itajulikana leo kesi hiyo itakaposikilizwa.
Adebayor anakabiliwa na kosa jingine nalo ni la kuonyesha mwenendo usiokubalika wakati akishangilia goli lake siku hiyo hiyo Man City walipocheza na Arsenal na kwenda kuwachokoza Mashabiki wa Arsenal.
Uamuzi wa kosa hili utajulikana Septemba 30.

Bosi Kenyon abwaga manyanga Chelsea!!!
Mkurugenzi Mkuu wa Klabu ya Chelsea, Peter Kenyon, ametangaza kuachia ngazi wadhifa huo kuanzia mwishoni mwa Oktoba baada ya kukalia kiti hicho kwa miaka mitano.
Kabla ya kuwa Chelsea, Kenyon, alishika wadhifa kama huo Manchester United.
Ingawa Kenyon anaachia ngazi ya ubosi, atabaki kuwa Mkurugenzi wa kawaida kwenye Klabu hiyo na kuiwakilisha kwenye vikao mbalimbali vya soka huko Ulaya.
Chelsea bado haijatangaza mrithi wake.

No comments:

Powered By Blogger