Friday 13 February 2009

Scolari: 'Timu ilikosa 'Mchawi', walizoea soka la 'Umangimeza!''

Luiz Felipe Scolari, alietimuliwa kazi na Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich siku ya Jumatatu, alitoboa siri ya kudebweda Chelsea alipofanya mahojiano na Gazeti la Ufaransa 'France Football' wiki iliyokwisha wakati hajui hatima yake nini!
Scolari alikiri Chelsea haina ubunifu na Wachezaji kama Florent Malouda, Didier Drogba na Salomon Kalou viwango vyao vimeshuka sana na vinatisha.

Scolari alitamka: 'Hapa Chelsea hatuna Mchezaji mbunifu anaeweza kuleta 'uchawi' na kuibadilisha mechi sekunde moja! Zamani alikuwepo Arjen Robben na aliweza kubadilisha mechi kwa uwezo wake binafsi! Robinho angekuwa hapa angeweza kufanya hivyo, haogopi kupiga chenga na hushambulia bila woga. Mimi kama Mbrazil napenda hilo! Timu yangu si ya Kibrazil! Ni timu inayocheza soka la 'Umangimeza' haina Wachezaji wabunifu! Ndio maana naamini Robinho angefanya mengi kwa timu hii!'
Alipoulizwa kwa nini hakuwa anawechezesha Didier Drogba na Nicolas Anelka kama Washambuliaji wawili kwenye Fomesheni ya 4-4-2, Scolari alijibu: 'Sina Wachezaji wanaoweza kubadilika kumudu mfumo huo. Ilikuwa ngumu wao kucheza pamoja. Sina Wachezaji wa kucheza Wingi. Kalou anaweza kucheza kwenye 4-3-3 lakini 4-4-2 hawezi, ingawa anaweza kucheza Winga kulia kwa sababu tukishambuliwa hana uwezo mzuri kurudi nyuma kusaidia ulinzi! Na nani atacheza Winga ya kushoto?'
Scolari aliendelea: 'Hata tukicheza 4-4-2 nani viungo? Tutazidiwa kwenye midifildi! Inabidi nichague mmoja acheze Drogba au Anelka. Lakini Drogba baada ya kuumia hayupo kwenye fomu, anakosa kujiamini. Malouda wa Chelsea si Malouda wa Lyon'
Scolari alimaliza mahojiano hayo na Gazeti 'France Football' kwa pengine, bila kujijua, kutoa utabiri wake: 'Chelsea ndio walinipa kazi mwanzoni mwa msimu uliokwisha. Huo ulikuwa uamuzi wao. Sasa, wakitaka kunifukuza, huo uamuzi wao. Mimi nafanya kazi yangu tu!'
Kutoka Urusi na.......mapenzi!!!!

Meneja wa Timu ya Taifa ya Urusi na ambae pia ndie Meneja mpya wa Chelsea, Guus Hiddink [pichani na tajiri Abramovich], anaamini Chelsea bado wana nafasi nzuri kwani bado wamo kwenye mapambano ya kugombea Vikombe vitatu.
Hiddink amesema: 'Kuna Kombe la FA, Kuna Ubingwa wa Ulaya na ipo LIGI KUU! Ndio tuko pointi 10 nyuma kwenye ligi lakini lolote linaweza kutokea!'
Guus Hiddink mwenyewe amekiri bila ya uswahiba mkubwa na mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, ambae pia ndie mfadhili mkubwa wa soka ya Urusi, asingekubali kwenda Chelsea.
Inaaminika kazi ya ukocha wa Urusi Guus Hiddink amepewa na Abramovich na inasadikiwa Mrusi huyo tajiri ndie anaemlipa mshahara wa kuwa Meneja wa Urusi.
Hakika, NI KUTOKA URUSI.........NA MAPENZI!!!!!!

Giggs asaini mkataba mpya Man U!!

Ryan Giggs [35] amesaini nyongeza ya mwaka mmoja kwenye mkataba wake ambao sasa utamweka Manchester United hadi msimu ujao utakapoisha katikati ya mwaka 2010.
Winga veterani Giggs, ambae ameshachezea mechi 787 hapo Man U ikiwa ni rekodi kwa Mchezaji kucheza mechi nyingi klabuni hapo, alianza kuwachezea Mabingwa hao mwaka 1991.
Giggs ndie Mchezaji alieshinda Vikombe vingi hapo Man U kupita mwingine yeyote na ameshachukua Ubingwa wa LIGI KUU England mara 10, UEFA Champions League mara 2, FA Cup mara 4 na Kombe la Ligi [sasa linaitwa Carling Cup] mara 2.
Goli lake la ushindi Jumamosi iliyopita wakati Man U walipowafunga West Ham 1-0 kwenye LIGI KUU limemfanya awe Mchezaji pekee aliefunga bao kila msimu kwa misimu 17 mfululizo tangu LIGI KUU England ianzishwe.

Straika Mahakamani kwa 'Shambulio la Ngono'!!

Mshambuliaji wa Wigan, Marlon King [28], ambae yupo kwa mkopo Middlesbrough atafikishwa Mahakamani tarehe 25 Februari 2009 akishtakiwa kosa la 'Shambulio la Ngono' na kumjeruhi mwanamke mwenye umri wa miaka 20 kwenye Baa moja huko Soho jijini London.
Tukio hilo inasemekana lilitokea Desemba 7 mwaka jana na kusababisha mwanamke huyo avunjike pua na kupasuka mdomo.
Marlon King pia ni Mcchezaji wa Timu ya Jamaica.

Thursday 12 February 2009

MECHI ZIJAZO

Wikiendi hii kutakuwa na mechi moja tu ya LIGI KUU England na zilizobaki zote ni za Raundi ya 5 kugombea Kombe la FA isipokuwa Jumatatu kuna mechi ya marudiano ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA baada ya Cardiff kutoka sare na Arsenal kwenye mechi ya kwanza.
Jumatano Mabingwa Manchester United wanacheza ile mechi yao ya kiporo ya LIGI KUU kwa kupambana na Fulham hapo kwao Old Trafford.
Mechi hii ilikuwa ichezwe mwaka jana lakini ikaahirishwa kwa kuwa Man U alikuwa akicheza UEFA Super Cup.
RATIBA KAMILI: [Saa ni Bongo Taimu]
Jumamosi, 14 Februari 2009
LIGI KUU England
Portsmouth v Man City [saa 12 jioni]
FA Cup
Swansea v Fulham [saa 9.45 mchana]
[saa 12 jioni]
Blackburn v Coventry
Sheffield United v Hull City
West Ham v Middlesbrough
[saa 2.30 usiku]
Watford v Chelsea
Jumapili, 15 Februari 2009
FA Cup
[saa 11.30 jioni]
Everton v Aston Villa
[saa 1.30 usiku]
Derby v Man United
Jumatatu, 16 Februari 2009
[saa 4.45 usiku]
Arsenal v Cardiff
Jumatano, 18 Februari 2009
LIGI KUU England
Man United v Fulham
Spain 2 England 0

Jana England ilichapwa mabao 2-0 na Spain kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa nchini Spain.
Mabao ya Spain yalifungwa na David Villa dakika ya 36 na Llorente dakika ya 82.
David Beckham aliingizwa dakika ya 46 na hiyo ikawa ni mechi yake ya 108 kuichezea England ikiwa ni sawa na rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Bobby Moore kucheza mechi nyingi.

MATOKEO MECHI NYINGINE ZA KIRAFIKI:

France 0 Argentina 2
Germany o Norway 1
Portugal 1 Finland 0
Tunisia 1 Holland 1
Tanzania 0 Zimbabwe 0
Brazil 2 Italy 0

Chelsea wathibitisha Hiddink Meneja mpya

Chelsea imetangaza Guus Hiddink ndie Meneja mpya atakaechukua nafasi ya Luiz Felipe Scolari alietimuliwa.
Hiddink ataendelea pia kuwa Meneja wa Timu ya Taifa ya Urusi na inaaminika nafasi yake hapo Chelsea ni mpaka mwisho wa msimu huu.


Adebayor MCHEZAJI BORA AFRIKA

Mshambuliaji wa Togo na Arsenal Emmanuel Adebayor ametunukiwa na CAF, Chama cha Soka cha Afrika, tuzo ya MCHEZAJI BORA AFRIKA 2008.K
Ameshinda tuzo hiyo baada ya kura iliyopigwa miongoni mwa Makocha wa Timu za Taifa za Afrika na Adebayor alipata pointi 74 na mpinzani wake mkubwa Mohammed Aboutrika wa Misri alipata pointi 53.

Washindi wa Tuzo nyingine za CAF ni:

Mchezaji Bora wa Klabu: Aboutrika [AL AHLY]
Timu Bora ya Taifa: Misri
Klabu Bora: Al Ahly
Mchezaji Bora Kijana: Salomon Kalou
Mchezaji Bora Wanawake: Alice Mattlou [Afrika Kusini]
Kocha Bora: Hassan Shehata

Meneja Newcastle Kinnear kufanyiwa operesheni ya moyo

Joe Kinnear [62] Meneja wa Newcastle ambae yuko hospitalini tangu Jumamosi inabidi afanyiwe opersheni ya moyo na huenda akaukosa msimu wote uliobaki.
Kinnear alichukua hatamu hapo Newcastle Septemba 2008 baada ya Kevin Keagan kutimka.

Tuesday 10 February 2009

Edwin Van der Sar na Ngome yake: Dakika 1212 haijafungwa!!! Ni REKODI!!

Nae Ryan Giggs aweka rekodi: NI MCHEZAJI PEKEE ALIEFUNGA GOLI KILA MSIMU WA LIGI KUU TANGU IANZISHWE MIAKA 17 ILIYOPITA!!!

Kipa Edwin Van der Sar na Beki Nemanja Vidic ndio Wachezaji pekee waliocheza mechi zote 13 zilizoweka rekodi mpya, zenye jumla ya Masaa 20 na dakika 12 ikiwa ni sawa na dakika 1212, bila ya kufungwa hata goli moja kwenye mechi za LIGI KUU England.
Mara ya mwisho Man U kufungwa goli ilikuwa ni Novemba 8 mwaka jana wakati Sami Nasri alipoifungia Arsenal huko Emirates Stadium kwenye ushindi wao wa 2-1.
Mwezi uliokwisha, wakicheza na West Bromwich, Man U waliweka rekodi mpya ya LIGI za England ya kutofungwa muda mrefu.
Jumapili walipocheza na West Ham wameipita rekodi iliyowekwa na Aberdeen ya Scotland na kuwa Klabu ya kwanza Uingereza yote kutokufungwa goli kwenye LIGI za Uingereza [Uinigereza ikimaanisha Visiwa vya Uingereza yaani Scotland, Wales, Ireland pamoja na England].
Rekodi hiyo ya Aberdeen huku Kipa akiwa Bobby Clark iliwekwa kwenye Ligi ya Scotland msimu wa mwaka 1970/71 mwaka aliozaliwa Van der Sar!!!
Endapo Manchester United wataweza kuwazuia Fulham kufunga bao kwa Dakika 64 ya mechi yao ya kiporo ya LIGI KUU itakayochezwa Old Traford nyumbani kwa Mabingwa hao Jumatano ijayo tarehe 18 Februari, basi Manchester United wataivunja rekodi ya dunia inayoshikiliwa na aliekuwa Kipa wa Atletico Madrid Abel Renso ya kutokufungwa kwa Dakika 1275 katika mechi za Ligi.
RYAN GIGGS na rekodi yake!!!
Wakati Edwin Van der Sar anaweka rekodi akisaidiwa na Ngome yake ya Man U ikiongozwa na Nemanja Vidic kwenye mechi hiyo ya Jumapili waliyoishinda West Ham bao 1-0 goli lililofungwa na Ryan Giggs, nae Ryan Giggs kwa bao hilo aliweka rekodi mpya kwenye LIGI KUU England ya kuwa Mchezaji pekee alieweza kufunga goli kila msimu wa LIGI KUU hiyo tangu ianzishwe miaka 17 iliyopita.
LIGI KUU England ilianza rasmi tarehe 15 Agosti 1992.
Ryan Giggs alianza kuichezea Man U tangu Timu za Watoto lakini alianza kucheza Timu ya Kwanza rasmi tarehe 2 Machi 1991 akiwa na miaka 17 tu alipoingizwa kwenye mechi kumbadilisha Veterani Dennis Irwin Man U walipocheza na Everton.
Ryan Giggs kwa kucheza mechi hiyo ya juzi na West Ham amefikisha mechi 787 kwa Manchester United akiwa ni Mchezaji anaeongoza kwa kucheza mechi nyingi Manchester United.
Harakati za Chelsea kutafuta Mrithi wa Scolari: Meneja wa Timu ya Taifa ya Urusi Guus Hiddink aanza mazungumzo na Chelsea!!

Guus Hiddink [62], raia wa Uholanzi [pichani], ambae kwa sasa ni Meneja wa Timu ya Taifa ya Urusi, amefuatwa na Klabu ya Chelsea, iliyomtimua Meneja wake Mbrazil Luiz Felipe Scolari hapo jana, ili kuiongoza hadi mwishoni mwa msimu huu.
Guus Hiddink ambae ana uhusiano wa karibu na Mmiliki wa Chelsea tajiri wa Kirusi Roman Abramovich na ambae ndie aliesababisha Hiddink apewe kazi ya Umeneja wa Urusi mwaka 2006, amesema: 'Ingekuwa Klabu nyingine nisingesita kusema hapana lakini Chelsea ni tofauti kwa sababu ya uhusiano wangu mzuri na mwenye mali.'
Chelsea imeshapewa kibali na FUR ambacho ndicho Chama cha Mpira cha Urusi kuzungumza na Guus Hiddink na habari hizi zimethibitishwa na Tovuti ya Chelsea.
Roman Abramovich ndie mfadhili mkuu wa FUR na pia anaekiendesha Chuo cha Mafunzo ya Soka huko Urusi.
Chelsea imetamka makubaliano yakifikwa basi Guus Hiddink atakuwa hapo klabuni hadi mwisho wa msimu lakini vilevile ataendelea kuwa Meneja wa Urusi.
Kwa sasa Chelsea iko chini ya usimamiza wa Meneja Msaidizi Ray Wilkins.
Guus Hiddink ameshawahi kuwa Kocha wa PSV Eindhoven, Real Madrid pamoja na Timu za Taifa za Netherlands, South Korea and Australia.

Sir Alex Ferguson ataja Kikosi chake kilichosajiliwa UEFA Champions League

Meneja wa Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametaja Kikosi cha Wachezaji 30 waliosajiliwa kwa UEFA kwa ajili ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16 inayoanza kuchezwa wiki mbili zijazo.
Kufuatana na Kanuni za UEFA, Kikosi cha Wachezaji 30 kinakuwa na Makundi mawili ya Wachezaji na la kwanza huitwa 'Listi A' ambayo ndiyo listi kuu na huwa na Wachezaji 25.
'Listi B' ni ile ya nyongeza ambayo ina majina ya Wachezaji watano waliozaliwa tarehe 1 Januari 1987 au baada ya hapo.
Mabadiliko kwenye Listi A ya Man U ni kukosekana kwa Owen Hargreaves ambae ni majeruhi na Manucho kwa sababu yuko Hull City kwa mkopo.
Nafasi zao zimechukuliwa na Federico Macheda na Davide Petrucci wote wakiwa Wachezaji chipukizi toka Timu ya Akiba ya Man U.
Mchezaji mpya aliesajiliwa Januari kutoka Serbia Zorin Tosic hayumo kwa sababu haruhusiwi kucheza kwa vile alishaechezea Klabu yake ya zamani Partizan Belgrade kwenye UEFA Champions League msimu huu pale walipofungwa na Fenerbahce kwenye Raundi ya 3.
Listi A [Na Namba zao za Jezi]:
Makipa: 1. Van der Sar, 12. Foster, 29. Kuszczak
Walinzi: 2. Neville, 3. Evra, 5. Ferdinand, 6. Brown, 15. Vidic, 20. Fabio, 21. Rafael, 22. O'SheaViungo: 8. Anderson, 11. Giggs, 13. Park, 16. Carrick, 17. Nani, 18. Scholes, 24. Fletcher, 34. Possebon, 43. Petrucci
Washambuliaji: 7. Ronaldo, 9. Berbatov, 10. Rooney, 32. Tevez, 41. Macheda
Listi B: Ben Amos, Richard Eckersley, Jonny Evans, Darron Gibson and Danny Welbeck.
Wakala wa Scolari adai: 'Ametimuliwa na Mwenye Mali Abramovich!!'
Ferguson astushwa, asema ni alama za nyakati!!


Baada ya Luiz Felipe Scolari kufukuzwa na Chelsea kama Meneja na kazi hiyo kupewa kwa muda Ray Wilkin aliekuwa msaidi wake, Wakala wa Scolari ametangaza uamuzi wa kumtimua umefanywa na Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich ambae alikerwa sana na mwendo mbaya wa Chelsea.
Chelsea mpaka sasa wako nafasi ya 4 kwenye LIGI KUU England wakiwa pointi 7 nyuma ya vinara Man U na wamecheza mechi moja zaidi ya Man U.

Hata hivyo, Chelsea bado wamo kwenye vindumbwembwe wa Vikombe vya FA na UEFA Champions League.
Jumamosi walitoka sare 0-0 nyumbani kwao Stamford Bridge na Timu 'dhaifu' Hull City na kundi la Mashabiki lilimzomea Scolari na kubwata: 'Hajui afanyalo!' huku baadhi wakiinua bango kubwa lililoandikwa: 'Mfukuzeni kazi!'.
Msimu huu, Chelsea wamekuwa na rekodi mbaya kwenye LIGI KUU hasa walipocheza na vigogo wenzao kwani walifungwa nyumbani na ugenini na Liverpool, wakafungwa na Arsenal hapo kwao Stamford Bridge, wametoka suluhu Stamford Bridge na Man U lakini wakabamizwa bao 3-0 na Man U kwenye marudiano huko Old Trafford.
Wakala wa Scolari, Acaz Felleger, amesema: 'Uamuzi ni wa Abramovich. Scolari hakuwa kwenye nafasi nzuri ingawa Bodi na Wachezaji walikuwa wakimsapoti. Alirithi kikosi cha Wachezaji 'wazee' na juhudi zake za kuleta damu changa zilishindikana!'
Nae Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United ambae ndie anashikilia rekodi ya kudumu muda mrefu kazini kwa kuwepo zaidi ya miaka 22 na kuwa na mafanikio makubwa, amenena: 'Nimesikitika! Nimestuka sana! Hii ni alama ya nyakati! Dunia haina tena uvumilivu! Huyu amekuwa na timu miezi 7 tu na ukweli ni kwamba ni mwezi uliokwisha tu ndio timu ililegalega. Tatizo ni kuwa Chelsea wana matumaini makubwa sana!'
Tangu Roman Abramovich ainunue Chelsea mwaka 2003, Mrusi huyo tajiri sana ameshawatimua Mameneja wannne, wa kwanza alikuwa Claudio Ranieri mwaka 2004, akafuata Jose Mourinho Septemba 2007, kisha Avram Grant Mei 2008 na jana Scolari.

RATIBA MECHI ZA KESHO:

Jumatano, 11 Februari 2009
MECHI ZA KIMATAIFA ZA KIRAFIKI
Andorra v Lithuania,
Austria v Sweden,
Belgium v Slovenia,
Cameroon v Guinea,
Colombia v Haiti,
Egypt v Ghana,
Estonia v Kazakhstan,
FYR Macedonia v Moldova,
France v Argentina, [SAA 5 USIKU]
Germany v Norway,
Greece v Denmark,
Iceland v Liechtenstein,
Israel v Hungary,
Latvia v Armenia,
Morocco v Czech Republic,
Nigeria v Jamaica,
Portugal v Finland,
Romania v Croatia,
South Africa v Chile,
Spain v England, [SAA 6 USIKU]
Switzerland v Bulgaria,
Tunisia v Netherlands,
Turkey v Ivory Coast,
Venezuela v Guatemala,
Wales v Poland,

Monday 9 February 2009

Scolari afukuzwa Chelsea!!!

Klabu ya Chelsea imetangaza kupitia tovuti yake kuwa Meneja wao Luiz Felipe Scolari amefukuzwa kazi ili Klabu ipate changamoto mpya ya kugombea Vikombe ambavyo Timu hiyo ina nafasi ya kuvichukua.
Scolari, ambae alishinda Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa Meneja wa Brazil, aliteuliwa kuwa Meneja wa Chelsea mwaka jana kabla msimu huu haujaanza na alichukua nafasi ya Avram Grant ambae nae alitimuliwa.
Chelsea imetangaza atakaekaimu nafasi hiyo ni Meneja Msaidizi Ray Wilkins.

Tony Adams atimuliwa toka Portsmouth!!

Klabu ya Portsmouth imethibitisha kuwa imemwachisha kazi aliekuwa Meneja wao Tony Adams kufuatia mwenendo mbaya wa Timu.
Tony Adams, aliekuwa Nahodha wa zamani wa Arsenal na Timu ya Taifa ya England, aliteuliwa kuwa Meneja wa Portsmouth mwishoni mwa Oktoba mwaka jana kufuatia kuondoka kwa Harry Redknapp aliehamia Tottenham.
Lakini tangu wakati huo Portsmouth imecheza mechi 16 za LIGI KUU na kushinda 2 tu na kuifanya Timu iwe pointi moja tu juu ya timu zilizo kwnye zoni ya kushuka daraja.
Vilevile, Portsmouth ambao ndio walikuwa Mabingwa Watetezi wa Kombe la FA walitolewa nje ya Mashindano hayo walipofungwa na Timu ya Daraja la chini Swansea kwa bao 2-0.
Jumamosi Portsmouth walifungwa nyumbani kwao na Liverpool kwa bao 3-2 katika mechi waliyokuwa wakiongoza 2-1 huku zimesalia dakika 5 tu!
Portsmouth imetangaza aliekuwa Mkurugenzi wa Vijana Paul Hart ndie atakuwa Meneja wa muda wa klabu wakati wakianza kusaka mtu mpya.

Shaun Wright-Phillips afungiwa Mechi 3!!!

Mchezaji wa Manchester City Shaun Wright-Philips amefungiwa kucheza Mechi 3 na FA baada ya kupatikana na hatia ya kulipiza kisasi kwa kumpiga teke Rory Delap wa Stoke katika mechi Man City walifungwa 1-0.
Kwenye mechi hiyo Rory Delap alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu kumpiga na mpira Shaun Wright-Phillips lakini Refa hakuona jinsi Mchezaji huyo wa Man City alivyolipa kisasi lakini baada ya mechi Refa Martin Atkinson alikiri kama angemwona Shaun Wright-Phillips basi angempa Kadi Nyekundu.
Sasa Shaun Wright-Phillips atazikosa mechi za Timu yake dhidi ya Portsmouth, Liverpool na West Ham

Sunday 8 February 2009

Veterani Giggs afunga goli tamuuu, Man U wavunja rekodi Dakika 1193 bila nyavu zao kutikiswa na hizo ni Mechi 13!!

Mabingwa Manchester United wamerudi tena kileleni baada ya kushinda ugenini Upton Park bao 1-0 na kuwaliza wenyeji West Ham timu ambayo wakiwa hapo kwao kawaida huwatoa nishai Man U.
Ni veterani Ryan Giggs aliefunga goli tamu sana dakika ya 61 kufuatia kona aliyopiga mwenyewe na kuokolewa na West Ham lakini ikamkuta Paul Scholes katikati ya uwanja na akatoa pasi ndefu kwa Giggs aliekuwa wingi ya kushoto aliempiga chenga Carlton Cole na kumhadaa Noble kisha akapiga shuti kwa mguu wake dhaifu wa kulia na kufunga goli ambalo bila shaka linaweza kuwemo kwenye listi ya magoli bora ya msimu!

Kwa ushindi huu ambao hawakufungwa goli sasa Man U wamevunja rekodi ya Uingereza kwa kucheza muda mrefu bila nyavu zao kuguswa ikiwa ni dakika 1193 sawa na mechi 13!
Sasa Man U wana pointi 56 kwa mechi 24, huku Liverpool ni wa pili akiwa na pointi 54, Villa wa tatu pointi 51 akifuata Chelsea pointi 49 na Arsenal ni wa 5 pointi 44 timu zote hizi zikiwa zimecheza mechi 25, mechi moja zaidi ya Man U.
Vikosi vilivyoanza:
West Ham:
Green, Neill, Collins, Upson, Ilunga, Behrami, Parker, Noble, Collison, Cole, Di Michele.
Akiba: Lastuvka, Nsereko, Boa Morte, Kovac, Spector, Tristan, Sears.
Man Utd: Van der Sar, Rafael Da Silva, Ferdinand, Vidic, O'Shea, Ronaldo, Scholes, Carrick, Giggs, Tevez, Berbatov.
Akiba: Foster, Park, Nani, Welbeck, Fabio Da Silva, Fletcher, Eckersley.

Mtu 10 Arsenal wajitutumua na kutoka droo na Tottenham!!
Nyota Adebayor aumia kuwa nje wiki 6!!!!


Arsenal wakiwa ugenini White Hart Lane nyumbani kwa majirani na mahasimu wao wakubwa Tottenham wamefanikiwa kutoka sare ya 0-0 huku wakicheza watu 10 tu kwa muda mwingi wa gemu hii baada ya Mchezaji wao Eboue kutolewa nje dakika ya 38 ya kipindi cha kwanza kufuatia kupewa Kadi ya pili ya Njano baada ya kumkwatua Luka Modric.
Eboue alipewa Kadi ya kwanza ya Njano dakika ya 19 ya mchezo kwa kumletea ubishi Refa Mike Dean.
Ingawa Tottenham walitawala mchezo walishindwa kuipasua ngome ya Arsenal iliyoongozwa vizuri na Gallas na Kolo Toure huku Kipa Alumnia akiwa makini sana.
Katika mechi hii Mshambuliaji Staa wa Arsenal Adebayor, alieumia musuli ya nyuma ya paja kwenye dakika ya 38 na akaingizwa Bendtener, atakuwa nje kwa wiki 6 habari zilizothibitishwa na Meneja Arsene Wenger.

Hivyo Adebayor atazikosa mechi za Arsenal dhidi ya Cardiff, ikiwa mechi ya marudiano Kombe la FA, mechi za LIGI KUU dhidi ya Sunderland na Fulham, na ile ya UEFA Champions League watakayocheza na AS Roma.
Vikosi vilivyoanza vilikuwa:
Arsenal wanabaki nafasi ya 5 wakiwa na pointi 44 pointi 5 nyuma ya Timu ya 4 Chelsea na pointi 10 nyuma ya Liverpool inayoongoza ligi.
Tottenham wako nafasi ya 15.
Tottenham: Cudicini, Corluka, Dawson, Woodgate, Assou-Ekotto, Lennon, Jenas, Palacios, Modric, Pavlyuchenko, Keane.
Akiba: Gomes, Bale, Zokora, Huddlestone, Bent, Taarabt, Chimbonda.
Arsenal: Almunia, Sagna, Toure, Gallas, Clichy, Eboue, Song Billong, Denilson, Nasri, Adebayor, Van Persie.
Akiba: Fabianski, Eduardo, Ramsey, Djourou, Arshavin, Bendtner, Gibbs.

Benitez ang'ang'ania uteuzi wake wa Timu ni sawa tu!!

Washabiki wengi wa Liverpool na hata watu wa pembeni mara nyingi hushangazwa na jinsi Meneja wa Liverpool Rafael Benitez anavyopanga Timu yake.
Jana haikuwa tofauti wakati, kwa mara nyingine tena, alipowashangaza wengi kwa kuwaacha nyota kama Dirk Kuyt na Fernando Torres kwenye mechi ya jana na Portsmouth na kuuamua tu kuwaingiza dakika za mwisho wakati Liverpool ishafungwa na Wachezaji hao hawakufanya ajizi wakafunga mabao yaliyowapa ushindi wa 3-2.
Mwenyewe Benitez anatetea: 'Torres ni mmoja kwenye kikosi na wapo wengine wanaofanya timu iwe imara! Tungefungwa lakini tumeshinda!!'


Wilkins amtetea Scolari!!

Meneja msaidizi wa Chelsea, Ray Wilkins, amejitokeza kumtetea Bosi wake Luiz Felipe Scolari ambae jana alizomewa na Mashabiki wa Chelsea uwanjani kwao Stamford Bridge mara baada ya kutoka suluhu ya 0-0 na Hull City kwenye mechi ya LIGI KUU.
Mashabili hao walizomea huku wakibwata:'Hujui unachokifanya!'
Wilkins amesema: 'Wakitaka kuzomea shauri yao lakini wasiseme hajui anachokifanya kwani Scolari ana mafanikio makubwa kwenye soka.'
Scolari aliiongoza Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2002 lakini tangu atue hapo Chelsea imeshapoteza pointi 16 hapo Stamford Bridge kwenye LIGI KUU wakati hapo kulikuwa ndio ngome yao kuu.
Baadhi ya Mashabiki kwenye mechi hiyo ya jana waliinua bango kubwa lililoitaka Chelsea imfukuze kazi Scolari. Bango hilo lilionyeshwa pale Scolari alipofanya uamuzi wa kumbadilisha Mchezaji mpya Ricardo Quaresma na kumwingiza Didier Drogba.

Beckham yumo Kikosi cha England kupambana na Spain Jumatano

Meneja wa England Fabio Capello amemwita kikosini David Beckham ambae kwa sasa yuko kwa mkopo AC Milan kutoka Klabu yake ya Marekani LA Galaxy na endapo atacheza mechi ya kirafiki na Spain hapo Jumatano huko Spain atakuwa amefungana na Bobby Moore kwa kuchezea mechi 108 Timu ya Taifa ya England ikiwa ni rekodi ya Mchezaji wa mbele kucheza mechi nyingi Timu ya England.
Wachezaji Carlton Cole wa West Ham na James Milner wa Aston Villa pia wamo kikosi hicho ikiwa ni mara yao ya kwanza kuitwa Timu ya Taifa.
Wayne Rooney wa Manchester United hayumo kwenye kikosi hicho kwa kuwa alikuwa majeruhi.
Vikosi vya Timu hizo ni kama ifuatavyo:
England:

Makipa: Robert Green (West Ham), Joe Hart (Man City), David James (Portsmouth).
Walinzi: Wayne Bridge (Man City), Ashley Cole (Chelsea), Rio Ferdinand (Man Utd), Phil Jagielka (Everton), Glen Johnson (Portsmouth), John Terry (Chelsea), Matthew Upson (West Ham), Luke Young (Villa).
Viungo: David Beckham (LA Galaxy), Gareth Barry (Villa), Michael Carrick (Man Utd), Stewart Downing (Middlesbrough), Frank Lampard (Chelsea), James Milner (Villa), Shaun Wright-Phillips (Man City), Ashley Young (Villa).
Washambuliaji: Gabriel Agbonlahor (Villa), Carlton Cole (West Ham), Peter Crouch (Portsmouth), Emile Heskey (Villa).
Spain:
Makipa: Iker Casillas (Real Madrid), Pepe Reina (Liverpool).
Walinzi: Raul Albiol (Valencia), Carlos Marchena (Valencia), Alvaro Arbeloa (Liverpool), Joan Capdevila (Villarreal), Juan Gutierrez (Real Betis), Gerard Pique (Barcelona), Carles Puyol (Barcelona), Sergio Ramos (Real Madrid).
Viungo: Xabi Alonso (Liverpool), Albert Riera (Liverpool), Sergi Busquets (Barcelona), Santiago Cazorla (Villarreal), Marcos Senna (Villarreal), Xavi Hernandez (Barcelona), Andres Iniesta (Barcelona), David Silva (Valencia).
Washambuliaji: Daniel Guiza (Fenerbahce), Fernando Llorente (Athletic Bilbao ), Fernando Torres (Liverpool), David Villa (Valencia).
Powered By Blogger