Thursday, 6 August 2009

Arsenal kujua Mpinzani wake UEFA CHAMPIONS LEAGUE kesho!!!
Kesho Ijumaa mchana huko Nyon, Switzerland, Makao Makuu ya UEFA, Chama cha Soka cha Ulaya, kutafanyika dro ya kupanga Timu zipi zinakutana kwenye Raundi ya mwisho ya Mtoano wa Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Kwenye dro hiyo kuna jumla ya Timu 20 zinazowania nafasi 10 ili kujumuika na Timu 22 kufanya jumla ya Timu 32 zitakazogawanywa Makundi Manane ya Timu 4 kila moja zitakazocheza kwa mtindo wa ligi wa mechi za nyumbani na ugenini.
Timu hizi 20 zimegawanywa Makundi mawili ya timu 10 kila moja huku Arsenal ikiwa Kundi la “sio mabingwa” ambalo lina Makapu mawili.
Kundi jingine linaitwa “mabingwa” [Hivi ni Vilabu vilivyonyakuwa Ubingwa Nchini kwao lakini Nchi hizo hazikuingizwa moja kwa moja kwenye Makundi yatayocheza kwa Ligi kwa sababu Nchi zao ziko nafasi ya chini ya Ubora HUKO Ulaya].
Arsenal yuko Kapu la kwanza lenye Timu za Arsenal, Olympique Lyonnais [Ufaransa], Sporting Lisbon [Ureno], Panathinaikos [Ugiriki] na Vfb Stuttgart [Ujerumani].
Kapu la pili ziko ACF Fiorentina [Italia], Atletico Madrid [Spain], Celtic [Scotland], Anderlecht [Ubelgiji] na Timisoara [Romania].
Timu za Kapu la Kwanza zitacheza na Mpinzani toka Timu za Kapu la Pili.
Hivyo Mpinzani wa Arsenal anaweza kuwa mmoja kati ya ACF Fiorentina [Italia], Atletico Madrid [Spain], Celtic [Scotland], Anderlecht [Ubelgiji] au Timisoara [Romania].
Kundi la “mabingwa” nalo pia limegawanywa Makapu mawili ya Timu tano kila moja na Timu ya Kapu la Kwanza itapambanishwa na Timu toka Kapu la Pili.
Kapu la Kwanza zipo Olympiacos [Ugiriki], FC Kobenhavn [Denmark], PFC Levski Sofia [Bulgaria] na Maccabi Haifa [Israel].
Kapu la Pili zipo FC Salzburg [Austria], Apoel FC [Cyprus], FK Ventspils [Latvia], Debreceni VSC [Hungary] na FC Sheriff [Marcedonia].
Mechi hizi za Raundi hii ya Mtoano zitachezwa tarehe 18 na 19 Agosti 2009 na marudiano tarehe 25 na 26 Agosti 2009.
Mechi za Kwanza za Ligi kwenye Makundi Manane ya Timu 4 kila moja zitachezwa tarehe 15 na 16 Septemba 2009.
Ligi Kuu kumpa heshima Robson
Ligi Kuu England inayoanza Jumamosi tarehe 15 Agosti 2009 imetoa maelekezo kuwa kabla ya mechi zitakazochezwa hiyo Jumamosi na siku inayofuata Jumapili kutakuwa na dakika moja ya kushangilia ikiwa ni kutoa heshima na kumbukumbu kwa Sir Bobby Robson aliefariki hivi karibuni.
Sir Bobby Robson alikuwa Meneja wa England, Newcastle na Ipswich Town na pia Klabu za PSV Eindhoven, Sporting Lisbon, Porto na Barcelona.

Mwaka 1990 aliifikisha England Nusu Fainali ya kombe la Dunia huko Italia lakini ikakosa kuingia Fainali baada ya kubwagwa kwa penalti na Ujerumani.
Mbali ya heshima hiyo ya dakika moja, Viwanja vyenye TV kubwa vimeagizwa kuonyesha mkanda maalum wa Sir Bobby Robson
.
UHAMISHO………kwa ufupi!!!!!!!!!
-AC Milan imemchukua Mshambuliaji wa Kidachi kutoka Real Madrid, Klaas-Jan Huntelaar, umri miaka 26, kwa mkataba wa miaka minne.
Huntelaar alijiunga na Real mwezi Januari mwaka huu na kufunga bao 8. Kabla ya hapo alikuwa Timu ya Uholanzi Ajax kwa muda wa miaka mitatu huku akifunga mabao 76 katika mechi 92 alizocheza.
-Burnley, Klabu iliyopanda Daraja kuingia Ligi Kuu England, imemchukua kwa mkopo Winga kutoka Nchi ya Ecuador, Fernando Guerrera, miaka 19, kutoka Klabu ya Independientede Valle.
-Hull City imewachukua Wachezaji wawili, kutoka Stoke City Mnigeria Seyi Olofinjana , miaka 29, na kutoka Villareal imembeba Mshambuliaji wa USA, Jozy Altidore, kwa mkopo.
-Wigan imemsaini Winga wa Chelsea, Scott Sinclair, miaka 20, kwa mkopo utakaodumu msimu mmoja. Msimu uliokwisha Sinclair alikuwa Birmingham kwa mkopo ambako aliisaidiaTimu hiyo kupanda Daraja kuingia Ligi Kuu.
Man U 2 Valencia 0
Akicheza mechi yake ya kwanza ndani ya Jezi maarufu Nambari 7, mbele ya Washabiki zaidi ya 70,000, Uwanjani Old Trafford, akishuhudiwa pia na Meneja wa England Fabio Capello, Mshambuliaji Michael Owen, aliepata nafasi zaidi ya 3 za wazi, alishindwa kupata bao.
Na ilikuwa ni juu ya Nyota Wayne Rooney na Chipukizi Tom Cleverley kupachika mabao yaliyowapa ushindi Manchester United wakicheza mechi yao ya kwanza Uwanja wa nyumbani kabla msimu mpya kuanza dhidi ya Klabu ngumu kutoka Spain Valencia iliyokuwa na Nyota kama Villa na Silva.
Akicheza pia mechi yake ya kwanza mbele ya Mashabiki wa Man U hapo Old Trafford, Mchezaji mpya Winga Luis Antonio Valencia aling’ara sana na kuwapa matumaini makubwa Washabiki hao baada ya kuwa mpishi murua wa mabao yote hayo mawili kwa kufanya kazi nzuri winga ya kulia na kutoa krosi tamu kwa wafungaji zilizowafanya Washabiki kukumbuka enzi za David Beckham.
Jumapili, ndani ya Wembley Stadium, Jijini London, Mabingwa Manchester United watajimwaga kucheza na Mabingwa wa Kombe la FA Chelsea ikiwa mechi ya “ Fungua Pazia” msimu mpya ya kugombea Ngao ya Hisani.
MATOKEO JANA MECHI ZA MTOANO UEFA CHAMPIONS LEAGUE: [matokeo mechi ya awali kwenye mabano]
BATE 2 v FK Ventspils 1, (0-1),

Debrecen 1 v FC Levadia Tallinn 0, (1-0),
Dinamo Moscow 0 v Celtic2, (1-0),
Levski Sofia 2 v FK Baku 0, ( 0-0),
NK Maribor 0 v FC Zurich 3, (3-2),
Olympiacos 2 v Slovan Bratislava 0, ( 2-0),
Partizan Belgrade 1 v Apoel Nicosia 0, ( 0-2),
Politehnica Timisoara 0 v Shakhtar Donetsk 0, ( 2-2),
Slavia Prague 1 v FC Sheriff Tiraspol 1, (0-0),
Stabaek 0 v FC Copenhagen 0, (1-3),
Chelsea yamkera Mourinho!!
Bosi wa Inter Milan Jose Mourinho ameishambulia Klabu yake ya zamani Chelsea kwa kutia ngumu kwa yeye kumsaini Sentahafu wa Chelsea Ricardo Carvalho.
Mourinho amedai Chelsea imeongeza dau la Carvalho baada ya kugundua wao Inter Milan wanamtaka.
Mourinho ameonyesha nia ya kuwachukua Wachezaji wake wa zamani aliokuwa nao huko Ureno na Klabu ya FC Porto Deco na Carvalho ambao sasa wako Chelsea.
Lakini Mourinho ameonyeshwa kukerwa na Chelsea na ametamka: “Ni ngumu kwa sasa kumchukua Mchezaji toka Chelsea. Kila wakigundua nina nia na Mchezaji wao mambo hubadilika ghafla! Tuliambiwa Deco yuko huru kuja kwetu lakini wiki mbili baadae, walipogundua tuna nia ya kweli, dau likatoka sifuri hadi Milioni 5! Carvalho likapanda toka Milioni 5 hadi 15!”
EUROPA LEAGUE: Marudiano leo Fulham v FK Vetra
Fulham, baada ya kupata ushindi mnono wa bao 3-0 ugenini, leo wakiwa nyumbani wanarudiana tena na FK Vetra ya Lithuania uwanjani kwao Craven Cottage.
Endapo Fulham watashinda leo wataingia Raundi ya mwisho ya Mtoano ya EUROPA LEAGUE na kucheza na Timu watakayopangiwa kwenye dro hapo Ijumaa kwa mtoano kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na wakifuzu hapo ndipo watakuwa kwenye hatua ya Makundi itakayochezwa kwa mtindo wa Ligi.
Katika Raundi ijayo ya Mtoano Klabu nyingine za Ligi Kuu England zitakazojumuika na Fulham ikifuzu ni Aston Villa na Everton.
Timu hizi mbili zitaanzia Raundi hii kwa vile zilimaliza Ligi nafasi ya 5 na 6.

Fulham ilimaliza ya 7.
Kikosi cha leo Fulham kintatokana na: Stockdale, Schwarzer, Zuberbuhler, Baird, Konchesky, Hangeland, Hughes, Pantsil, Kelly, Stoor, Andranik, Seol, Zamora, Nevland, Gera, Etuhu, Murphy, Dempsey, E Johnson, A Johnson.

Wednesday, 5 August 2009

MTOANO UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Celtic wasonga mbele, washinda ugenini 2-0!
Baada ya kuchapwa 1-0 kwao mjini Glasgow, leo Celtic wameshinda ugenini mjini Moscow, Urusi baada ya kuinyuka Dinamo Moscow bao 2-0 huku mkombozi akiwa Mchezaji wao wa Kigiriki Georgios Samaras aliepachika bao la pili dakika za majeruhi.
Samaras aliingizwa kipindi cha pili kumbadili Mchezaji Scott MaCdonald aliefunga bao la kwanza kipindi cha kwanza.
Huku mechi ikielekea kwenda muda wa nyongeza wa nusu saa na pengine penalti kama matokeo yangebaki Dinamo Moscow 0 Celtic 1, ndipo Samaras alipopachika bao la pili na kuipeleka Celtic kwenye Raundi ya mwisho ya Mtoano kabla Ligi ya Makundi kuanza.
MADENI YAKWAMISHA KUANZA MSIMU ARGENTINA!!!
Kuanza kwa msimu mpya wa soka huko Nchini Argentina kumekwama kufuatia kwa Klabu nyingi kukumbwa na madeni.
Msimu mpya ulitakiwa uanze Agosti 14 lakini Chama cha Soka cha Argentina [AFA] kimesema Klabu nyingi hazina pesa kuwalipa Wachezaji na sasa hali ni ngumu sana.

Rais wa AFA, Julio Grondona, amesema hali inatisha na hata Ligi Daraja la Pili iliyokuwa ianze wiki iliyokwisha imesimama na wao sasa wanatafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kubwa.
Hata hivyo Rais huyo amesema ushiriki wa Argentina kwenye mashindano na Nchi nyingine za Marekani ya Kusini, kama vile Kombe la Sudamericana, na pambano la kirafiki la Timu ya Taifa ya Argentina na Urusi hapo Agosti 12, yataendelea kama yalivyopangwa.
Hali hiyo ya ngumu kwa Klabu za Argentina imechangiwa sana na hali tata ya uchumi duniani na pia kutopanda kwa mapato toka kwenye haki za maonyesho ya mipira kwenye Televisheni.
Liverpool wamsaini Aquilani toka AS Roma!!
Baada ya kumuuza Xabi Alonso kwa Real Madrid, Liverpool haraka haraka wamejaribu kuziba pengo lake kwa kutangaza kuwa wamemchukua Kiungo wa AS Roma ya Italia, Alberto Aquilani, Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Italia.
Inaaminika dau la ununuzi wake ni Pauni Milioni 20 na inasadikiwa baadae wiki hii Aquilani ataenda Liverpool kukamilisha uhamisho ikiwa pamoja na kupimwa afya yake.
Ferguson: “Liverpool hawana nafasi Ubingwa!’
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amewakata maini Mahasimu wao wa Jadi Liverpool kwa kuwaambia hawana nafasi yeyote ya kuchukua Ubingwa wa Ligi Kuu England wakati wao wanawania kuuchukua kwa mara ya 4 mfululizo na kwa mara ya 19 kwa ujumla ili kuwapiku Liverpool ambao wamefungana nao kwa kuwa Timu zilizonyakua Ubingwa huo mara 18 kila mmoja zikiwa ni mara nyingi kupita Klabu nyingine yeyote.
Ferguson alitamka: “Pengine msimu uliokwisha kwa Liverpool ulikuwa bora kupita mwingine wowote kwa miaka 20 iliyopita! Waliumaliza wakiwa na pointi 86, pointi 4 nyuma yetu na itakuwa ngumu kufikia tena hapo na pengine hawataweza kuyapita mafanikio hayo! Timu nyingine sasa zimeshaisoma Liverpool na kuijua vizuri!”
Alipoulizwa ikiwa Liverpool itaathirika kwa kuuzwa Kiungo wao Xabi Alonso kwa Real Madrid, Ferguson alijibu kuwa Alonso hawezi kuleta pengo kwa Liverpool kwa kuwa tegemezi kubwa la Liverpool ni Nahodha wao Steven Gerrard na Mshambuliaji Fernando Torres.
Ferguson ameonyesha kuitilia wasiwasi Chelsea kuwa pengine ndie mshindani wao mkuu huku wakiwa na Meneja mpya Carlo Ancelotti ambae ni Mshindi wa Makombe mawili ya Ulaya na Ubingwa wa Serie A akiwa na AC Milan.
“Ni Chelsea! Ancelotti ataibadili Chelsea uchezaji wake na watapata magoli mengi kupitia Didier Drogba na Nicolas Anelka!” Ferguson aliongezea.
Hata hivyo Ferguson amekiri kuwa Man U itakuwa na pengo kwa kumkosa Ronaldo lakini ana uhakika Chipukizi wa Timu yake watasimama kidete. Ferguson amekiri pia kuwa hawawezi kumpata Mchezaji mwingine atakaekuwa kama Ronaldo.
Ferguson amesema: “Watu watasema mengi, kwangu mimi Ronaldo ni Mchezaji Bora Duniani! Ukiwa na Mchezaji Bora ni vigumu kumpata mwingine kama yeye! Na wakati ukijua huwezi kumpata mwingine wa kuziba pengo lake, kilichobaki ni kutazama njia mbadala! Watu wanakosea na kudharau uwezo wetu wa kukuza vipaji. Tuna matumaini makubwa kwa Chipukizi wetu Evans, Welbeck, Gibson, Macheda na Pacha Da Silva. Nani na Anderson wameshaonyesha vitu vizuri na watapanda chati msimu ujao!”
Van der Sar nje wiki 8!!!
Wakati huo huo, Kipa Veterani, Edwin van der Sar, atakosa wiki nane za mwanzo wa msimu ujao unaoanza Agosti 9 kwa mechi ya “fungua pazia” kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea baada ya kufanyiwa opersheni kutibu kidole cha mkononi kilichovunjika pamoja na mfupa mkono wake wa kushoto.
Van der Sar, miaka 38, aliumia akiokoa penalti kwenye mechi na Bayern Munich wiki iliyokwisha.
Makipa wa akiba Ben Foster na Tomasz Kuszczak wanategemewa kuchukua nafasi yake kwenye hiyo ya Ngao ya Hisani dhidi ya Chelsea.
Wachezaji Portsmouth watwangana kambini Ureno, warudishwa England!!!
Klabu ya Portsmouth imewatwanga Wachezaji wake wawili, David Nugent na Marc Wilson, faini ya mishahara ya wiki mbili na kuwafungisha virago warudi jijini Portsmouth kutoka kwenye kambi ya mazoezi huko Ureno baada ya kupigana makonde.
Katika taarifa yake, Klabu ya Portsmouth imesema Wachezaji hao walifanya utovu wa Nidhamu na wameadhibiwa kufuatana na kanuni za Klabu hiyo.
UEFA CHAMPIONS LEAGUE MTOANO: MATOKEO MECHI ZA MARUDIANO JANA:
FC Twente 1 v Sporting 1, (Sporting Lisbon yasonga mbele)

Maccabi Haifa 4 v FC Aktobe 3, (Haifa imefuzu),
Panathinaikos 3 v Sparta Prague 0, (Panathinaikos yasonga),
Sivasspor 3 v Anderlecht 1, (Anderlecht imepita),
MECHI ZA LEO: [KWENYE MABANO MATOKEO MECHI YA AWALI]
BATE v FK Ventspils, (0-1),
Debrecen v FC Levadia Tallinn, (1-0),
Dinamo Moscow vCeltic, (1-0),
Levski Sofia v FK Baku, ( 0-0),
NK Maribor v FC Zurich, (3-2),
Olympiacos v Slovan Bratislava, ( 2-0),
Partizan Belgrade v Apoel Nicosia, ( 0-2),
Politehnica Timisoara v Shakhtar Donetsk, ( 2-2),
Slavia Prague v FC Sheriff Tiraspol, (0-0),
Stabaek v FC Copenhagen, (1-3),

Tuesday, 4 August 2009

REAL NA LIVERPOOL WAKUBALIANA KWA ALONSO!!
Liverpool imethibitisha kuwa wamefikia makubaliano na Real Madrid kuhusu kuuzwa kwa Xabi Alonso.
Alonso, umri miaka 27, amekuwa akiwindwa na Real kwa muda mrefu ingawa Liverpool imekuwa ikigoma kumuuza hasa ukitilia manani Kiungo wao mwingine Mascherano nae ameeleza matakwa yake kuhama.
Liverpool, ikithibitisha kuuzwa kwa Alonso aliehamia Anfield mwaka 2004 akitokea Real Sociedad na kucheza mechi 127, imesema dau na mkataba wa uhamisho hautangazwi.
Mameneja LIGI KUU wafungwa midomo!!!
Kuanzia msimu ujao, Mameneja wa Ligi Kuu England wamepigwa marufuku na FA, Chama cha Soka England, kuzungumzia chochote kabla ya mechi kuhusu Refa aliepangwa kuchezesha mechi hiyo na endapo Meneja yeyote atakiuka agizo hilo basi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Tamko la FA lilisema: “Vilabu vimeshauriwa kwamba matamshi yeyote ya Mameneja, Wachezaji na Viongozi wengine wa Klabu kuhusu Waamuzi wa mechi kabla ya mechi husika hayaruhusiwi na ukiukwaji wake utashughulikiwa ipasavyo. Lakini, baada ya mechi, Klabu zinaruhusiwa kuongelea kuhusu Waamuzi na matukio ya mechi ili mradi tu yasiwahusishe binafsi au kuhusisha upendeleo au kushambulia hadhi ya Marefa au kudhalilisha soka.”
Tukio kubwa linalokumbukwa msimu uliokwisha ni lile la Meneja wa Everton, David Moyes, kuhoji uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA kati ya Everton na Manchester United wakati yeye aliambiwa Refa huyo ni shabiki wa Manchester United.
Baada ya mechi hiyo, Sir Alex Ferguson, alisema matamshi ya Moyes pengine yalimfanya Refa Mike Riley awanyime penalti wakati Danny Welbeck alipochezewa faulo ya dhahiri na Phil Jagielka ndani ya boksi.
Everton walishinda mechi hiyo kwa matuta baada ya mechi kwenda suluhu dakika 120.
Kwa sasa Mike Riley ndie alieteuliwa kuwa Mkuu wa Marefa wa Ligi Kuu England.
FA pia imeongeza kipengele kingine cha kanuni zake na kuanzia msimu ujao endapo Wachezaji watatu au zaidi wakimzonga Refa kwa “jazba” basi Klabu husika itashtakiwa.

Hapo nyuma Klabu zilikuwa zikikumbana na mashtaka pale tu Refa aliechezesha mechi akiripoti kuandamwa na Wachezaji.
Nyota wa Bondeni kucheza Fulham
Nyota wa Afrika Kusini, Kagiso Dikgacoi, amesema amekamilisha taratibu za kujiunga na Klabu ya Ligi Kuu England, Fulham.
Mchezaji huyo wa Bafana Bafana mwenye umri wa miaka 24 anaechezea Klabu ya Golden Arrows huko Bondeni kama Kiungo alipimwa afya yake wiki iliyopita baada ya kumaliza majaribio Klabuni hapo.
Kagiso Dikgacoi, alieng’ara kwenye michuano ya Kombe la Mabara iliyomalizika hivi karibuni akichezea Timu ya Taifa ya Afrika ya Kusini Bafana Bafana, amerudi kwao Afrika Kusini kwa muda mfupi kabla ya kujiunga tena na Klabu yake mpya Fulham.
MECHI ZA MTOANO LEO UEFA CHAMPIONS LEAGUE-Marudiano [magoli mechi ya kwanza kwenye mabano]
FC Twente v Sporting, (0-0)
Maccabi Haifa v FC Aktobe, (0-0),
Panathinaikos v Sparta Prague, (1-3),
Sivasspor v Anderlecht, (0-5),
HALI YA KIFEDHA KLABU ZA ENGLAND ZAITIA KIWEWE UEFA!!!
Chama cha Soka cha Ulaya, UEFA, kimeeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kifedha ya Klabu za Ligi Kuu England huku Katibu Mkuu wa UEFA, David Taylor, akionya kuwa kuna baadhi ya Klbu zitaangamia kwa kile alichokiita ‘kuishi nje ya uwezo wao”.
Taylor ametamka kuwa mfano bora ni ule yaliyowapata Leeds United.
Mwaka 2001 Leeds ikiwa Ligi Kuu England ilifanikiwa kucheza UEFA CHAMPIONS LEAGUE lakini msimu uliofuatia walishindwa kupata nafasi ya kucheza Ulaya na hivyo kukosa mapato na Klabu ikaingia matatani na kulazimika kuwauza Wachezaji wao nyota ili kufidia mapato.

Mwaka 2003 Leeds waliponea chupuchupu kuteremshwa Daraja lakini wakaporomoka msimu uliofuata na huo ukawa mwanzo wa kuangamia.
Leeds ikadidimia zaidi na kulazimika kuuza Uwanja wao Elland Road pamoja na viwanja vya mazoezi na wakazidi kuporomoka na mpaka sasa wako Daraja la tatu chini na Klabu imetangazwa mufilisi.
Mpaka sasa Klabu ya Liverpool iliyonunuliwa na Wamarekani wawili ipo kwenye deni kubwa.

Hata Wamiliki wa Manchester United, Familia ya Glazer, wameitumbukiza Klabu hiyo iliyokuwa na mahesabu safi na kutokuwa na chembe ya deni kwenye deni ingawa wenyewe kina Glazer wanatamba hawapo hatarini.
Lescott anataka kuhama Everton
Mlinzi wa Everton Joleon Lescott ameiambia Klabu yake kuwa dhamira yake ni kuhama ingawa mpaka sasa hajatoa maombi maalum ya kutaka kuhama huku Manchester City ikimfukuzia na iko tayari kuilipa Everton Pauni Milioni 18.
Everton mpaka sasa imegoma kumuuza Lescott lakini kuna dalili kuwa huenda wakalazimika kufanya hivyo kwani imeshadhihirika kuwa wapo kwenye mazungumzo na Arsenal ili wamchukue Mlinzi Philippe Senderos ili azibe pengo la Lescott.
Lescott alijiunga na Everton mwaka 2006 kutoka Wolverhampton kwa ada ya Pauni Milioni 5.
Wenger ang’ang’ana haongezi dau kumnunua Chamakh!!!
Arsene Wenger ametoboa kuwa hayuko tayari kuongeza dau la kumnunua Mchezaji wa kutoka Morocco, Marouane Chamakh kutoka Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa, kwa zaidi ya Pauni Milioni 5 alizotoa ofa.
Bordeaux mpaka sasa wanataka dau liongezwa huku zikitajwatajwa Pauni Milioni 15 kama ndio wanazozitaka kwa Mchezaji huyo.
Arsene Wenger ametamka: “Katika miezi mitano ijayo, endapo Chamakh hataongeza mkataba wake na Bordeaux, atakuwa huru kuongea na Klabu yeyote! Baada ya hapo Bordeaux hawatapa senti hata moja! Sina papara ya kumchukua kwa zaidi ya ofa tuliyotoa kwanza nnao Mafowadi wengine kama Walcott, Bendtner, Van Persie, Arshavin na Eduardo!”
Safari ya Alonso Real yanukia!!
Liverpool imethibitisha wako kwenye mazungumzo na Real Madrid kuhusu uhamisho wa Mchezaji wao Xabi Alonso ambae mwenyewe alitoa kimaandishi maombi rasmi ya kutaka kuhama Liverpool.
Ingawa Liverpool ilikuwa haitaki kumruhusu Alonso kuhama na hata kufikia hatua ya kupandisha ada yake ya uhamisho ili kuwakatisha tamaa Real lakini msimamo wa Alonso wa kudai uhamisho ndio umeifanya Klabu hiyo kuzungumza na Real.
Bent kwenda Sunderland
Mshambuliaji wa Tottenham, Darren Bent, amefanyiwa upimaji afya huko Sunderland na endapo mambo yote yatakamilika atahamia Klabu hiyo iliyo chini ya Meneja mpya Steve Bruce ambae mpaka sasa ameshawachukua Wachezaji wapya Lorik Cana, Frazier Campbell na Paulo Da Silva.
Imeripotiwa kuwa ada ya Bent kwenda Sunderland ni Pauni Milioni 14.
Chamakh atua London kutafuta Klabu!!
Mshambuliaji kutoka Morocco, Marouane Chamakh, anaecheza Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa inasemekana yuko London kusaka Klabu ya kuhamia na mpaka saa Klabu za Sunderland na Arsenal ndizo zilizotoa ofa kwa Bordeaux kumnunua ingawa Klabu hiyo ya Ufaransa inadai dau kubwa.
Inasemekana Arsenal imetoa ofa ya Pauni Milioni 5 kumnunua Chamakh, miaka 25, ofa ambayo Rais wa Bordeaux Jean-Louis Triaud ameiita “si haki” na inadaiwa Bordeaux wanataka si chini ya mara mbili ya pesa hizo.
Pia Sunderland walitoa ofa kubwa zaidi ya Arsenal lakini Klabu ya Bordeaux ikaikataa kwa madai Sunderland hawana hadhi ya kumnunua Chamakh, kauli ambayo ilithibitishwa na Meneja wa Bordeaux, Laurent Blanc, kuwa Chamakh ni “Mchezaji mzuri sana kujiunga Sunderland!”.
Chamakh mwenyewe ameelekea kukerwa na msimamo wa Klabu yake Bordeaux na ameripotiwa kutamka: “Nimekasirika! Tangu lini Klabu inaamua maisha ya baadae ya Mchezaji? Sunderland wametoa ofa, wakaambiwa sistahili kwenda huko! Arsenal wametoa ofa, sasa wanataka pesa nyingi!”
Mutu kwenda Mahakamani!
Baada ya kushindwa rufaa yake iliyobwagwa na Korti ya Masuala ya Michezo [CAS= Court of Arbitration for Sport] na kumtaka ailipe Chelsea Pauni Milioni 14 ikiwa ni fidia ya kukiuka mkataba kama ilivyoamuliwa na FIFA, Adrian Mutu, umri miaka 30, ameuita uamuzi huo ni “uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu” na sasa yuko tayari kuiburuza Chelsea na FIFA Mahakama za kiraia.
Mshambuliaji huyo kutoka Rumania alieigharimu Chelsea Pauni Milioni 15 mwaka 2003 alifukuzwa Chelsea mwaka mmoja baadae baada ya kugundulika anatumia cocaine na kufungiwa miezi 7 kutocheza soka.FIFA iliamua Mutu ailipe Chelsea pesa hizo zikiwa ni fidia lakini Mutu alikata rufaa kupinga uamuzi huo kwa Korti ya Masuala ya Michezo [CAS= Court of Arbitration for Sport].
Mutu amesema: “Hii ni gharama ninayoilipa kwa kosa la kijinga la kitoto! Lakini sasa nimenadilika! Chelsea hawana haki kulipwa, ni wao walionifukuza! Mie ni Mwanamichezo lakini vile vile raia wa Ulaya na haki lazima itendeke!”
Baada ya kutimuliwa Chelsea, Mutu alijiunga na Juventus Januari 2005 na msimu mmoja baadae akaenda Fiorentina ambako yuko mpaka leo.
Mashabiki wa Urusi watakiwa kupiga wiski ili kupambana na “Homa ya Mafua ya Kitimoto!’
Kiongozi wa Chama cha Mashabiki wa Soka huko Urusi, Alexander Shprygin, amewataka Mashabiki wote wa Urusi watakaoenda Nchini Wales kuishabikia Timu ya Taifa ya Urusi itakayocheza na Wales mwezi ujao katika mchujo wa kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 washindilie wiski kwa wingi ili kukabiliana na Homa ya Mafua ya Kitimoto ambayo imepamba moto huko Wales na Uingereza kwa jumla.
Katika Kundi lao, Ujerumani ndie anaongoza akiwa na pointi 16 kwa mechi 6, Urusi anafuata pointi 15 na Wales ni wa 4 wakiwa na pointi 9.

Sunday, 2 August 2009

KOMBE LA EMIRATES: Arsenal wabeba Kombe lao, nyumbani kwao!
Leo, Arsenal wameibandika Glasgow Rangers mabao 3-0 Uwanjani Emirates katika mashindano ya kugombea Kombe la Emirates na kubeba Kombe hilo huku magoli mawili ya kwanza yakifungwa ndani ya dakika 10 za kwanza kupitia kwa Kijana hatari Jack Wilshere dakika ya pili na Eduardo Da Silva dakika ya 10.
Jack Wilshere tena alipachika bao la 3 dakika ya 72.
Mechi hii ilitanguliwa na mechi kati ya PSG na Atletico Madrid iliyomalizika suluhu 1-1.
Katika mechi hii Madrid walipata bao la kwanza baada ya Mlinzi wa PSG Baning kutoa penalti na kutwangwa Kadi Nyekundu kwenye dakika ya 40 na penalti hiyo ikafungwa na Serigo Leonel Aguero.
PSG, wakicheza mtu 10, walisawazishi kipindi cha pili dakika ya 71 kupitia Mchezaji wa zamani wa Barcelona Ludovic Giuly.
Moyes adai Man City wanakosa heshima!!
Bosi wa Everton David Moyes amedai Manchester City hawaonyeshi heshima inayostahili kwa jinsi wanavyoendelea kumfukuzia Beki wa Everton Joleon Lescott ambae wameshatoa ofa mbili za kumnunua na zote zimekataliwa na sasa kuna taarifa kwamba watapandisha ofa yao hadi Pauni Milioni 22 huku pia Lescott atadai kuhama kwa maandishi.
Moyes, akionyesha masikitiko, alilalamika: “Wanatakiwa watuheshimu! Nina hakika kama ningekuwa Mark Hughes [Bosi wa Man City] nikiwa na pesa zote alizokuwa nazo ningetaka kununua Wachezaji bora lakini nisingetumia njia yao! Ningewasiliana na Mameneja wenzangu na kujadiliana! Hii ni kama tulivyokuwa tukifanya tangu zamani, tunapata kinywaji baada ya mechi, tunapigiana simu na kuulizana kuhusu Wachezaji tunaowataka! Sio haya!”
Toure: “Arsenal haina uongozi!’
Beki mpya wa Manchester City, Kolo Toure, amesema aliamua kuhama Arsenal kwa sababu Klabu hiyo ilikosa mwelekeo baada ya kushindwa kuimarisha Kikosi chake.
Toure, ambae amenunuliwa na Man City kwa Pauni Milioni 16, amesema ule msimamo wa kutegemea tu Wachezaji Chipukizi na Vijana umesababisha Klabu ikose Wachezaji wenye uzoefu na Viongozi bora.
Toure, mwenye miaka 28, anadai: “Ukiitazama Arsenal utaona Wachezaji wote Wakubwa na wazoefu wamehama! Thierry Henry, Patrick Viera na Ray Parlour hawapo! Hao ni Viongozi! Tumepoteza waongozaji wengi!’
Msimu uliokwisha, Arsenal iliongozwa na Manahodha wawili, huku Cesc Fabrega akimbadilisha William Gallas [pichani], baada ya Beki huyo kutoka Ufaransa kuwaponda Wachezaji wenzake.
Toure akaongeza: “Watu kama Thierry Henry, Patrick Viera na Ray Parlour walileta mafanikio Arsenal! Nadhani hapo nilipofikia ni bora kwangu kuhama!”
Toure akamalizia: “Timu bora ziko juu kwa sababu tu wana Wachezaji bora na kuwapata Wachezaji hao bora lazima utumie pesa! Huwezi kufanikiwa kwenye Soka kama huna pesa!”
Msimu uliokwisha Arsenal ilimaliza Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya 4 na haijatwaa Kombe lolote tangu mwaka 2005 iliposhinda Kombe la FA.
Man U imekataa “kuiba” mtoto!!!
Manchester United imepinga madai ya Klabu ya Ufaransa Le Havre kwamba “imemuiba” Chipukizi wao Kiungo Paul Pogba, mwenye umri wa miaka 16, baada ya kuwarubuni Wazazi wake.
Manchester United imepinga habari hizo kwa kusema imemsajili kinda huyo kwa kufuata misingi yote ya UEFA.
Le Havre imedai ilikuwa na makubaliano na Wazazi wa Pogba kwamba Kijana huyo abaki Le Havre hadi msimu wa 2009/10 umalizike lakini kwa sababu Manchester United imeingilia Wazazi hao wamegoma kuyafuata makubaliano hayo.
Le Havre inasifika kwa kuwa na Chuo bora cha Vijana Chipukizi na baadhi yao ambao wamehitimu hapo na kujipatia sifa ni pamoja na Kiungo wa Real Madrid, Lassana Diarra, Mchezaji wa Wigan Charles N’Zogbia pamoja na Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool ambae sasa yuko Atletico Madrid Florent Sinama-Pongolle.
Chipukizi huyo Paul Pogba ndie Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa ya Vijana wa chini ya miaka 16.
Hii si mara ya kwanza kwa Klabu za Ulaya kulalamika Man U kuwachota Chipukizi wao kwani mara tu alipoibuka Federico “Kiko” Macheda kama lulu pale alipoipa ushindi Man U katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa, Klabu iliyomlea ya Lazio ya Italia nayo ilililalamika.
KOMBE LA EMIRATES: Magoli mechi ya Arsenal na Atletico Madrid yapatikana dakika 5 za mwisho!
Jana, kwenye Uwanja wao wa Emirates, Arsenal walikumbana na Atletico Madrid ya Spain na magoli ya mechi hiyo yalipatikana dakika 5 za mwisho za mechi pale Andre Arshavin wa Arsenal alipofunga goli dakika ya 86, Atletico wakasawazisha kupitia Pacheco dakika ya 88 lakini Arshavin tena akafunga la pili dakika ya 89 na kuwapa Arsenal ushindi.
Katika mechi nyingine ya awali hapo jana Glasgow Rangers iliifunga PSG kutoka Ufaransa kwa bao moja kwa bila.
Leo ni PSG na Atletico na baadae Arsenal na Rangers.
Powered By Blogger