Tuesday, 4 August 2009

Safari ya Alonso Real yanukia!!
Liverpool imethibitisha wako kwenye mazungumzo na Real Madrid kuhusu uhamisho wa Mchezaji wao Xabi Alonso ambae mwenyewe alitoa kimaandishi maombi rasmi ya kutaka kuhama Liverpool.
Ingawa Liverpool ilikuwa haitaki kumruhusu Alonso kuhama na hata kufikia hatua ya kupandisha ada yake ya uhamisho ili kuwakatisha tamaa Real lakini msimamo wa Alonso wa kudai uhamisho ndio umeifanya Klabu hiyo kuzungumza na Real.
Bent kwenda Sunderland
Mshambuliaji wa Tottenham, Darren Bent, amefanyiwa upimaji afya huko Sunderland na endapo mambo yote yatakamilika atahamia Klabu hiyo iliyo chini ya Meneja mpya Steve Bruce ambae mpaka sasa ameshawachukua Wachezaji wapya Lorik Cana, Frazier Campbell na Paulo Da Silva.
Imeripotiwa kuwa ada ya Bent kwenda Sunderland ni Pauni Milioni 14.
Chamakh atua London kutafuta Klabu!!
Mshambuliaji kutoka Morocco, Marouane Chamakh, anaecheza Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa inasemekana yuko London kusaka Klabu ya kuhamia na mpaka saa Klabu za Sunderland na Arsenal ndizo zilizotoa ofa kwa Bordeaux kumnunua ingawa Klabu hiyo ya Ufaransa inadai dau kubwa.
Inasemekana Arsenal imetoa ofa ya Pauni Milioni 5 kumnunua Chamakh, miaka 25, ofa ambayo Rais wa Bordeaux Jean-Louis Triaud ameiita “si haki” na inadaiwa Bordeaux wanataka si chini ya mara mbili ya pesa hizo.
Pia Sunderland walitoa ofa kubwa zaidi ya Arsenal lakini Klabu ya Bordeaux ikaikataa kwa madai Sunderland hawana hadhi ya kumnunua Chamakh, kauli ambayo ilithibitishwa na Meneja wa Bordeaux, Laurent Blanc, kuwa Chamakh ni “Mchezaji mzuri sana kujiunga Sunderland!”.
Chamakh mwenyewe ameelekea kukerwa na msimamo wa Klabu yake Bordeaux na ameripotiwa kutamka: “Nimekasirika! Tangu lini Klabu inaamua maisha ya baadae ya Mchezaji? Sunderland wametoa ofa, wakaambiwa sistahili kwenda huko! Arsenal wametoa ofa, sasa wanataka pesa nyingi!”
Mutu kwenda Mahakamani!
Baada ya kushindwa rufaa yake iliyobwagwa na Korti ya Masuala ya Michezo [CAS= Court of Arbitration for Sport] na kumtaka ailipe Chelsea Pauni Milioni 14 ikiwa ni fidia ya kukiuka mkataba kama ilivyoamuliwa na FIFA, Adrian Mutu, umri miaka 30, ameuita uamuzi huo ni “uonevu na ukiukwaji wa haki za binadamu” na sasa yuko tayari kuiburuza Chelsea na FIFA Mahakama za kiraia.
Mshambuliaji huyo kutoka Rumania alieigharimu Chelsea Pauni Milioni 15 mwaka 2003 alifukuzwa Chelsea mwaka mmoja baadae baada ya kugundulika anatumia cocaine na kufungiwa miezi 7 kutocheza soka.FIFA iliamua Mutu ailipe Chelsea pesa hizo zikiwa ni fidia lakini Mutu alikata rufaa kupinga uamuzi huo kwa Korti ya Masuala ya Michezo [CAS= Court of Arbitration for Sport].
Mutu amesema: “Hii ni gharama ninayoilipa kwa kosa la kijinga la kitoto! Lakini sasa nimenadilika! Chelsea hawana haki kulipwa, ni wao walionifukuza! Mie ni Mwanamichezo lakini vile vile raia wa Ulaya na haki lazima itendeke!”
Baada ya kutimuliwa Chelsea, Mutu alijiunga na Juventus Januari 2005 na msimu mmoja baadae akaenda Fiorentina ambako yuko mpaka leo.
Mashabiki wa Urusi watakiwa kupiga wiski ili kupambana na “Homa ya Mafua ya Kitimoto!’
Kiongozi wa Chama cha Mashabiki wa Soka huko Urusi, Alexander Shprygin, amewataka Mashabiki wote wa Urusi watakaoenda Nchini Wales kuishabikia Timu ya Taifa ya Urusi itakayocheza na Wales mwezi ujao katika mchujo wa kuwania kuingia Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwaka 2010 washindilie wiski kwa wingi ili kukabiliana na Homa ya Mafua ya Kitimoto ambayo imepamba moto huko Wales na Uingereza kwa jumla.
Katika Kundi lao, Ujerumani ndie anaongoza akiwa na pointi 16 kwa mechi 6, Urusi anafuata pointi 15 na Wales ni wa 4 wakiwa na pointi 9.

No comments:

Powered By Blogger