Moyes adai Man City wanakosa heshima!!
Bosi wa Everton David Moyes amedai Manchester City hawaonyeshi heshima inayostahili kwa jinsi wanavyoendelea kumfukuzia Beki wa Everton Joleon Lescott ambae wameshatoa ofa mbili za kumnunua na zote zimekataliwa na sasa kuna taarifa kwamba watapandisha ofa yao hadi Pauni Milioni 22 huku pia Lescott atadai kuhama kwa maandishi.
Moyes, akionyesha masikitiko, alilalamika: “Wanatakiwa watuheshimu! Nina hakika kama ningekuwa Mark Hughes [Bosi wa Man City] nikiwa na pesa zote alizokuwa nazo ningetaka kununua Wachezaji bora lakini nisingetumia njia yao! Ningewasiliana na Mameneja wenzangu na kujadiliana! Hii ni kama tulivyokuwa tukifanya tangu zamani, tunapata kinywaji baada ya mechi, tunapigiana simu na kuulizana kuhusu Wachezaji tunaowataka! Sio haya!”
Toure: “Arsenal haina uongozi!’
Beki mpya wa Manchester City, Kolo Toure, amesema aliamua kuhama Arsenal kwa sababu Klabu hiyo ilikosa mwelekeo baada ya kushindwa kuimarisha Kikosi chake.
Toure, ambae amenunuliwa na Man City kwa Pauni Milioni 16, amesema ule msimamo wa kutegemea tu Wachezaji Chipukizi na Vijana umesababisha Klabu ikose Wachezaji wenye uzoefu na Viongozi bora.
Toure, mwenye miaka 28, anadai: “Ukiitazama Arsenal utaona Wachezaji wote Wakubwa na wazoefu wamehama! Thierry Henry, Patrick Viera na Ray Parlour hawapo! Hao ni Viongozi! Tumepoteza waongozaji wengi!’
Msimu uliokwisha, Arsenal iliongozwa na Manahodha wawili, huku Cesc Fabrega akimbadilisha William Gallas [pichani], baada ya Beki huyo kutoka Ufaransa kuwaponda Wachezaji wenzake.
Toure akaongeza: “Watu kama Thierry Henry, Patrick Viera na Ray Parlour walileta mafanikio Arsenal! Nadhani hapo nilipofikia ni bora kwangu kuhama!”
Toure akamalizia: “Timu bora ziko juu kwa sababu tu wana Wachezaji bora na kuwapata Wachezaji hao bora lazima utumie pesa! Huwezi kufanikiwa kwenye Soka kama huna pesa!”
Msimu uliokwisha Arsenal ilimaliza Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya 4 na haijatwaa Kombe lolote tangu mwaka 2005 iliposhinda Kombe la FA.
Man U imekataa “kuiba” mtoto!!!
Manchester United imepinga madai ya Klabu ya Ufaransa Le Havre kwamba “imemuiba” Chipukizi wao Kiungo Paul Pogba, mwenye umri wa miaka 16, baada ya kuwarubuni Wazazi wake.
Manchester United imepinga habari hizo kwa kusema imemsajili kinda huyo kwa kufuata misingi yote ya UEFA.
Le Havre imedai ilikuwa na makubaliano na Wazazi wa Pogba kwamba Kijana huyo abaki Le Havre hadi msimu wa 2009/10 umalizike lakini kwa sababu Manchester United imeingilia Wazazi hao wamegoma kuyafuata makubaliano hayo.
Le Havre inasifika kwa kuwa na Chuo bora cha Vijana Chipukizi na baadhi yao ambao wamehitimu hapo na kujipatia sifa ni pamoja na Kiungo wa Real Madrid, Lassana Diarra, Mchezaji wa Wigan Charles N’Zogbia pamoja na Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool ambae sasa yuko Atletico Madrid Florent Sinama-Pongolle.
Chipukizi huyo Paul Pogba ndie Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa ya Vijana wa chini ya miaka 16.
Hii si mara ya kwanza kwa Klabu za Ulaya kulalamika Man U kuwachota Chipukizi wao kwani mara tu alipoibuka Federico “Kiko” Macheda kama lulu pale alipoipa ushindi Man U katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa, Klabu iliyomlea ya Lazio ya Italia nayo ilililalamika.
No comments:
Post a Comment