Tuesday, 4 August 2009

Mameneja LIGI KUU wafungwa midomo!!!
Kuanzia msimu ujao, Mameneja wa Ligi Kuu England wamepigwa marufuku na FA, Chama cha Soka England, kuzungumzia chochote kabla ya mechi kuhusu Refa aliepangwa kuchezesha mechi hiyo na endapo Meneja yeyote atakiuka agizo hilo basi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Tamko la FA lilisema: “Vilabu vimeshauriwa kwamba matamshi yeyote ya Mameneja, Wachezaji na Viongozi wengine wa Klabu kuhusu Waamuzi wa mechi kabla ya mechi husika hayaruhusiwi na ukiukwaji wake utashughulikiwa ipasavyo. Lakini, baada ya mechi, Klabu zinaruhusiwa kuongelea kuhusu Waamuzi na matukio ya mechi ili mradi tu yasiwahusishe binafsi au kuhusisha upendeleo au kushambulia hadhi ya Marefa au kudhalilisha soka.”
Tukio kubwa linalokumbukwa msimu uliokwisha ni lile la Meneja wa Everton, David Moyes, kuhoji uteuzi wa Refa Mike Riley kuchezesha mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA kati ya Everton na Manchester United wakati yeye aliambiwa Refa huyo ni shabiki wa Manchester United.
Baada ya mechi hiyo, Sir Alex Ferguson, alisema matamshi ya Moyes pengine yalimfanya Refa Mike Riley awanyime penalti wakati Danny Welbeck alipochezewa faulo ya dhahiri na Phil Jagielka ndani ya boksi.
Everton walishinda mechi hiyo kwa matuta baada ya mechi kwenda suluhu dakika 120.
Kwa sasa Mike Riley ndie alieteuliwa kuwa Mkuu wa Marefa wa Ligi Kuu England.
FA pia imeongeza kipengele kingine cha kanuni zake na kuanzia msimu ujao endapo Wachezaji watatu au zaidi wakimzonga Refa kwa “jazba” basi Klabu husika itashtakiwa.

Hapo nyuma Klabu zilikuwa zikikumbana na mashtaka pale tu Refa aliechezesha mechi akiripoti kuandamwa na Wachezaji.

No comments:

Powered By Blogger