Saturday 1 November 2008

MECHI ZA LEO!

Meneja mpya wa Tottenham, Harry Redknapp, ambae katika mechi zake mbili za kwanza amewafunga Bolton na kuwatia kiwewe Arsenal kwa kulazimisha sare, sasa anapambana na timu ambayo haijafungwa na ndiyo inayoongoza LIGI KUU, Liverpool, itakayotua White Hart Lane baada ya kuipachika timu yake ya zamani ya Portsmouth bao 1-0 kwenye mechi iliyokwisha.
Nao Portsmouth watawakaribisha Wigan kwao Fratton Park ikiwa ni mechi ya pili kwa Meneja mpya Tony Adams wakijaribu kukwepa kufungwa mechi ya 5 mfululizo kwenye ligi huku Wigan, baada ya kuanza vema msimu, wamejikuta wakipata vipigo mfululizo kutoka kwa Fulham, Aston Villa, Liverpool na Middlesbrough na kuwafanya wateremka na kuwa miongoni mwa timu 3 za mwisho kwenye msimamo wa ligi.
Bolton ni timu nyingine inayoporomoka kadri ligi ikiendelea baada ya kupata vipigo vinne katika mechi zao 6 za mwisho na sasa wako nafasi ya 19 yaani nafasi moja juu ya timu ya mwisho kwenye msimamo wa ligi. Sasa wanakutana na Manchester City timu nyingine kigeugeu kwenye ligi kwani haitabiriki.
Everton, mpaka sasa washashinda mechi 3 za ligi na zote wameshinda ugenini. Nyumbani, Uwanja wa Goodison Park, hawajashinda hata mechi moja katika mechi 5 za ligi walizocheza hapo msimu huu. Everton watawakaribisha Fulham ambao juzi waliwafunga Wigan.
Chelsea, waliopoteza rekodi yao ya kutofungwa katika mechi 86 za ligi nyumbani Stamford Bridge baada ya kupigwa 1-0 na Liverpool, wanawakaribisha Sunderland kwenye hiyo ngome iliyopenywa ya Stamford Bridge.
Nao Arsenal, baada ya kupokwa tonge mdomoni na Tottenham ambao walilazimisha sare ya 4-4 wakati Arsenal walikuwa wakiongoza kwa bao 4-2 hadi dakika ya 88, wanasafiri kwenda kukutana na timu iliyopanda daraja msimu huu Stoke City ambao silaha yao kubwa ni Mchezaji wao Rory Delap ambae ni spesho kwa mipira ya kurusha inayofanya kila mara Stoke City wapate bao.
Ukichukulia jinsi mechi ya Arsenal na Tottenham ilivyoisha, taarifa za ngumi kwenye chumba cha Arsenal baada ya mechi hiyo na jinsi defensi ya Arsenal inavyoyumba, basi bila shaka Arsenal lazima wagwaye mipira ya kurusha golini atakayorusha Rory Delap.
West Ham waliochabangwa bao 2 na Ronaldo wakati walipotembelea Old Trafford kukutana na Mabingwa Manchester United wanasafiri tena kwenda Riverside kukutana na Middlesbrough waliowakung'uta Manchester City juzi.,
Kwenye Uwanja wa Hawthorns, West Brom watawakarbisha Blackburn huku timu zote zikitoka kwenye vipigo. West Brom walifungwa 2-1 na Newcastle huku Blackburn walitandikwa 3-2 na Aston Villa.
Hull City, timu iliyopanda daraja msimu huu na iliyoleta msisimko sana msimu huu baada ya kuzifunga Arsenal, Tottenham na Newcastle, itatua Old Traford kupambana na Mabingwa wenyewe Manchester United baada ya juzi kupigwa 3-0 na Chelsea.
Kuna kila dalili Manchester United na hasa Cristiano Ronaldo sasa wanaanza kupamba moto. Ronaldo ndie aliewapa ushindi baada ya kufunga bao 2 dhidi ya West Ham.
Hull City inaongozwa na Meneja Phil Brown ambae mwenyewe amekiri Sir Alex Ferguson ndie aliemsaidia kupata kazi ya Umeneja huko Derby County miaka mitatu iliyopita.
Phil Brown anasema: 'Alimpigia simu Mwenyekiti wa Derby. Sidhani kama angempigia kama angeona sifai. Namshkuru ni mtu mwema sana!'
Wenger adharau ripoti ngumi zilifumuka kati ya Wachezaji wake baada ya sare na Tottenham!

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amekanusha ripoti zilizozagaa kwamba Wachezaji wake waligombana katika chumba cha kubadilishia nguo uwanjani kwao Emirates Stadium mara baada ya mechi na Tottenham ambayo iliisha suluhu 4-4 baada ya Tottenham waliokuwa nyuma kwa bao 4-2 kusawazisha dakika za mwisho.
Taarifa zilizigaa kuwa Wachezaji waligombana na sasa nyufa zimeanza kujitokeza kwenye timu kitu ambacho Arsene Wenger anabisha.
Baada ya mechi, staa wao Adebayor alikaririwa akidai Arsenal hawawezi kuchukua ubingwa.
Wenger amekanusha kama kuna mifarakano kwa kusema: 'Sote tulisononeka kwa droo ile. Kwenye chumba cha kubadilishia nguo, kila mmoja alivunjika moyo na alikuwa haamini nini kilitokea. Lakini, sisi ni wamoja na tutaibuka na ushindi!'
Arsenal haijatwaa Kombe lolote tangu iliposhinda FA CUP mwaka 2005.

Friday 31 October 2008

NI RASMI: BECKHAM ATUA AC MILAN KWA MKOPO!!!

AC Milan ya Italy imethibitisha kuwa David Beckham atajiunga na klabu hiyo kwa mkopo kuanzia Januari 7, 2009.
Beckham, mwenye miaka 33, ni mchezaji wa Klabu ya Marekani ya LA Galaxy ya huko Marekani ambako kwa sasa msimu wa ligi umeisha na utaanza upya mwakani mwezi Aprili.
Ili kujiweka fiti, Beckham ameamua kujiunga na Klabu hiyo ya Italia aweke uhai matumaini yake ya kuendelea kuichezea Timu ya Taifa ya Uingereza ambayo mpaka sasa ameshaiwakilisha mara 108.
Meneja wa England, Fabio Capello, ambae aliwahi kuwa na AC Milan kwa vipindi viwili vya kati mwaka 1991-1996 na 1997-1998 ameunga mkono hatua hiyo ya Beckham kwa kusema: 'Milan wamepata mchezaji bora'
Vilevile Capello aliongeza: 'Nilipokuwa nae Real Madrid alisaini mkataba na LA Galaxy na nikamuacha kwenye kikosi changu lakini kila siku alikuja kufanya mazoezi kwa bidii tu, nikamrudisha! Ni mtu makini sana, mwenye bidii na ingawa watu wanafikiri ni pleiboi nje ya uwanja lakini hilo si kweli hata chembe!'
MECHI ZIJAZO ZA LIGI KUU UINGEREZA

Jumamosi, 1 Novemba 2008

[saa 9 dak 45 mchana]

Everton v Fulham

[saa 12 jioni]

Chelsea v Sunderland

Man U v Hull City

Middlesbrough v West Ham

Portsmouth v Wigan

Stoke City v Arsenal

West Brom v Blackburn

[saa 2 na nusu usiku]

Tottenham v Liverpool

Jumapili, 2 Novemba 2008

[saa 1 usiku]

Bolton v Man City

Jumatatu, 3 Novemba 2008

[saa 5 usiku]

Newcastle v Aston Villa
Gallas majeruhi!

Nahodha wa Arsenal William Gallas ataikosa mechi ijayo na Stoke City siku ya Jumamosi baada ya kuumia kufuatia habari alizozitoa Meneja wake Arsene Wenger ambae pia amethibitisha nae Eboue ni majeruhi.

Carvalho nje!

Beki wa kutumainiwa wa Chelsea Ricardo Carvalho atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu baada ya kuumia goti katika mechi timu yake iliyoishinda Hull City juzi kwa mabao 3-0.

Tevez ni muhimu kwetu-Sir Alex Ferguson!

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ametamka Carlos Tevez ni bado mchezaji muhimu sana kwa timu yake ingawa hajaanza mechi nyingi hivi karibuni.
Katika mechi ya juzi ambayo Man U waliifunga West Ham 2-0, Tevez alianza na Rooney alikuwa benchi.
Sir Alex Ferguson amesisitiza ni bado muhimu sana na kwamba kwa sasa tatizo ana mastraika watatu na ni wawili tu ndio wanaoweza kucheza kwa wakati mmoja, bila shaka, akimaanisha mastraika hao ni Berbatov, Rooney na Tevez.

Adebayor akiri: 'Hatuwezi kuwa mabingwa!'

Baaada ya kuona timu yake Arsenal ikiporwa pointi sekunde ya mwisho ya mechi na Tottenham wakati zilipotoka sare ya bao 4-4 baada ya Aaron Lennon wa Tottenham kuisawazishia, Adebayor amelalamika: 'Huwezi kuwa bingwa namna hii!! Huu ni ukweli!'

Thursday 30 October 2008

MATOKEO LIGI KUU:

Arsenal 4 Tottenham 4

Aston Villa 3 Blackburn 2

Bolton 0 Everton 1

Fulham 2 Wigan o

Hull City 0 Chelsea 3

Liverpool 1 Portsmouth 0

Manchester United 2 West Ham 0

Middlesbrough 2 Manchester City 0

Stoke City 1 Sunderland 0

Wednesday 29 October 2008

TONY ADAMS AWA MENEJA MPYA PORTSMOUTH

Tony Adams, mwenye umri wa miaka 42 na ambaye alikuwa Mchezaji wa zamani wa Arsenal na Timu ya Taifa ya Uingereza, ametangazwa kuwa ndie Meneja mpya wa Portsmouth kuchukua nafasi ya Harry Redknapp aliehamia Tottenham.
Kabla uteuzi huu Tony Adams alikuwa ndie Meneja msaidizi hapo hapo Portsmouth chini ya Harry Redknapp na alianza kazi hiyo mwaka 2006.
Tony Adams aliichezea Arsenal kama beki wa kati kuanzia mwaka 1983 hadi 2002 na alikuwa Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Uingereza kuanzia 1987 hadi 2000 na alicheza mechi 66 zikiwemo Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998.
Newcastle 2 West Brom 1

Mchezaji Joey Barton, akianza mechi yake ya kwanza tangu atoke jela, alifunga bao la kwanza kwa Newcastle kwa penalti na Obefami Martins akaongeza la pili na kuwapatia Newcastle ushindi wa kwanza kwenye LIGI KUU tangu Meneja Joe Kinnear ashike hatamu hapo klabuni.
Ishmael Miller wa West Brom alifunga bao moja la West Brom.
Ushindi huo wa jana umewakwamua Newcastle kutoka mkiani ambako walikuwa ni moja ya timu tatu za mwisho kwenye ligi.

LEO LIGI KUU INAENDELEA KWA MECHI ZIFUATAZO:

[saa 4 dakika 45 usiku]
Aston Villa v Blackburn

Hull City v Chelsea

Stoke City v Sunderland

[saa 5 usiku]

Arsenal v Tottenham

Bolton v Everton

Fulham v Wigan

Liverpool v Portsmouth

Man U v West Ham

Middlesbrough v Man City

Monday 27 October 2008

Sir Alex Ferguson: 'Ronaldo atazidi kuwa bora!'

Baada ya Crsitiano Ronaldo kushinda TUZO YA FifPro WORLD FOOTBALLER OF THE YEAR 2008, Sir Alex Ferguson ametamba Ronaldo atazidi kuwa bora zaidi kwa kuwa bado ana umri mdogo.
Msimu huu, Sir Alex Ferguson ametabiri Ronaldo atafunga magoli 25 kwa kuwa ameanza msimu akitokea kwenye operesheni ya enka. Msimu uliokwisha, Ronaldo alifunga mabao 42.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 23, nae amekiri: 'Bosi wangu Sir Alex Ferguson ni mtu muhimu kwangu. Nipo klabu hii kwa sababu yake! Alinichukua wakati nina miaka 18 tu na amenisaidia sana! Anaheshimu wachezaji wote, anajua kuongea na wachezaji na hiyo ni muhimu. Asilimia 99 ya wachezaji wana uhusiano mzuri na yeye! Ni mtu bora sana! Ni sifa kubwa sana kuwa Manchester United pamoja na yeye, yeye ameshinda kila kitu kwa klabu hii!'
Sir Alex Ferguson alimsifia vilevile Rio Ferdinand ambae pamoja na Ronaldo wapo kwenye TIMU BORA YA 2008 YA FifPro kwa kusema: 'Rio si mlinzi bora tu bali ana uwezo mkubwa wa kugeuza ulinzi kuwa mashambulizi! Hilo alikuwa nalo lakini kwa sasa ni ule uwezo wa kuwa kiongozi na kuwa mstari wa mbele kuhamasisha timu kwa kila kitu!'
WAFUNGAJI BORA:

Baada ya kila Timu LIGI KUU kucheza mechi 9, kasoro Mabingwa Man U na Fulham wenye mechi ya kiporo kati yao, huku ligi ikongozwa na Liverpool wakifuatiwa na Chelsea kisha Hull City, Arsenal, Aston Villa na Man U, Mfungaji Bora mpaka sasa ni Mshambuliaji toka Afrika Amr Zaki kutoka Misri [pichani] anaechezea Klabu ya Wigan mwenye magoli 7.
Anaefuta ni Mbrazil Robinho wa Man City mwenye goli 6 huku Agbonlahor na Carew wa Aston Villa pamoja na Defoe wa Portsmouth na Torres wa Liverpool wakifuatia wakiwa na magoli matano kila mmoja.
Adebayor [Arsenal], Anelka [Chelsea], Bent [Tottenham], Crouch [Portsmouth], Davies [Bolton], Geovanni [Hull] na Van Persie [Arsenal] wana goli 4 kila mmoja.
Mfungaji Bora wa msimu uliopita Cristiano Ronaldo wa Manchester United, alieanza kucheza hivi karibuni baada ya operesheni ya enka, ana goli 2.
RONALDO ATWAA TUZO YA FifPro WORLD FOOTBALLER OF THE YEAR!!!




Cristiano Ronaldo wa Manchester United leo ameshinda Tuzo ya kuwa MCHEZAJI BORA WA DUNIA kwa mwaka huu iliyotolewa na FifPro ambacho ni Chama cha Wachezaji wa Kulipwa Duniani.
Ronaldo amewashinda kina Lionel Messi, Fernando Torres, Xavi na Mchezaji mwenzake wa Manchester United Rio Ferdinand katika kinyang'anyiro hiki ambacho Wachezaji wa Kulipwa kutoka zaidi ya Vyama 40 duniani vilimpigia kura.
Ronaldo ambae msimu uliokwisha alifunga jumla ya mabao 42 aliweza kuisaidia Timu yake Manchester United kutwaa Ubingwa wa LIGI KUU UINGEREZA na wa Ulaya mpaka sasa ameshatwaa Tuzo za Mchezaji na Mfungaji Bora LIGI KUU UINGEREZA pamoja na Mchezaji na Mfungaji Bora wa Klabu za Ulaya ya UEFA.
Ronaldo ametoa shukrani zake kwa FifPro kwa kutamka: 'Kutambuliwa na Wachezaji wenzangu wa kulipwa zaidi ya 50,000 duniani kote ni maajabu! Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Wachezaji wenzangu wa Manchester United, Makocha wangu wa Klabuni na Timu ya Taifa, familia yangu na marafiki zangu!'
Alimalizia kwa kusema: 'FifPro naipongeza kwa kazi nzuri ya kutetea na kuboresha maslahi ya Wachezaji wa kulipwa. Nawashkuru kwa Tuzo hii!'
Ronaldo vilevile yuko kwenye kinyang'anyiro cha kugombea Mpira wa Dhahabu [yaani Ballon d'Or] na Tuzo ya MCHEZAJI BORA DUNIANI YA FIFA 2008.
Vilevile FifPro imeitangaza Timu yake Bora ya Mwaka 2008:
KIPA– Iker Casillas (Spain/ Real Madrid) WALINZI– Sergio Ramos (Spain/ Real Madrid), John Terry (England/ Chelsea), Carles Puyol (Spain/ Barcelona) and Rio Ferdinand (England/ Manchester United) VIUNGO- Steven Gerrard (England/ Liverpool), Xavi (Spain/ Barcelona) and Ricardo Kaká (Brazil/AC Milan). WASHAMBULIAJI– Lionel Messi (Argentina/ Barcelona), Fernando Torres (Spain/ Liverpool), and Cristiano Ronaldo (Portugal/ Manchester United)

LIGI KUU UINGEREZA itaendelea kesho usiku kwa mechi moja na Jumatano timu zote nyingine zitacheza.
Kuanzia Jumapili taimu huko Uingereza imebadilika na hivyo tofauti ya wakati kati ya bongo na huko sasa inakuwa masaa matatu kufuatia kuingia majira ya baridi.
Hivyo mtaona tofauti katika taimu mechi zinapochezwa.
Tulizoea kuona mechi zinaanza saa 3 dakika 45 usiku lakini sasa zitaanza saa 4 dakika 45 usiku na zile za mchana badala ya kuanza saa 11 jioni bongo taimu sasa zitaanza saa 12 jioni.

Jumanne, 28 Oktoba 2008

Newcastle v West Brom [saa 4 dakika 45 usiku]

Jumatano, 29 Oktoba 2008

[saa 4 dakika 45 usiku]

Aston Villa v Blackburn

Hull City v Chelsea

Stoke City v Sunderland

[saa 5 usiku]

Arsenal v Tottenham

Bolton v Everton

Fulham v Wigan

Liverpool v Portsmouth

Man U v West Ham

Middlesbrough v Man City

KWA UFUPI TU TOKA LIGI KUU UINGEREZA:


Liverpool sasa inaongoza LIGI KUU kwa kuwa na pointi 23 kwa mechi 9 ilizocheza, Chelsea na Hull City ni za pili na za tatu zote zikiwa na pointi 20 kwa mechi 9 ingawa Chelsea iko mbele kwa magoli.
Ya nne ni Arsenal ikiwa na pointi 19 kwa mechi 9 ikifuatiwa na Aston Villa yenye pointi 17 kwa mechi 9.
Mabingwa Man U ni wa 6 wakiwa na pointi 15 kwa mechi 8, mechi moja pungufu kupita timu nyingine.
Mkiani wako Stoke nafasi ya 18 na wana pointi 7, Newcastle nafasi ya 19 kwa pointi 6 na wa mwisho ni Tottenham wana pointi 5.
Liverpool wameweza kuongoza ligi baada ya kuivunja ngome ya Chelsea walipowatwanga bao 1-0 nyumbani kwao Stamford Bridge ambako walikuwa hawajafungwa tokea Februari, 2004 na kwa mechi jumla ya mechi 86 za ligi.

Benitez ajigamba!

Meneja wa Liverpool Rafael Benitez amejigamba sasa kwamba kwa kuwa wameshazifunga Man U na Chelsea basi kila mtu ajue wao wanaweza kuchukua ubingwa.

Redknapp aanza vizuri!!!

Nae Harry Redknapp, Meneja mpya wa Tottenham, ameanza enzi yake mpya hapo Tottenham kwa kuipa klabu hiyo ushindi wake wa kwanza wa ligi msimu huu pale walipoifunga Bolton ba0 2-0.
Nayo klabu aliyotoka Rednapp, Portsmouth, imeanza ngwe bila ya Meneja huyo aliyeiwezesha klabu hiyo kunyakua Kombe la FA msimu uliopita, kwa sare ya 1-1 dhidi ya Fulham.

Robinho apachika 3!!

Robinho wa Man City alipachika mabao matatu mguuni kwake na kuiwezesha Man City kuifunga Stoke mabao 3-0.

Ronaldo kimwili na kiroho yuko Man U!!

Siku chache baada ya Rais wa Real Madrid Ramon Calderon kutamka klabu hiyo haina haja ya Ronaldo tena, Mchezaji huyo ameibuka na kusisitiza atabaki Manchester United kwa muda mrefu.
Ronaldo amekaririwa akisema: 'Sasa naelewa nimefanya uamuzi sahihi! Mie nipo Manchester kimwili na kiroho!

Sunday 26 October 2008

MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU LEO:

Tottenham 2 Bolton 0

West Ham 0 Arsenal 2

Man City 3 Stoke City 0

Wigan 0 Aston Villa 4
Chelsea 0 Liverpool 1

Ile rekodi ya Chelsea ya kutokufungwa mechi 86 za LIGI KUU kwenye ngome yao, uwanja wa nyumbani Stamford Bridge, leo imekwenda na maji baada ya kufungwa na Liverpool bao 1-0.
Mara ya mwisho kwa Chelsea kufungwa hapo kwao ilikuwa ni Februari, 2004 walipofungwa na Arsenal.
Sasa Liverpool wanaongoza ligi wakiwa na pointi 23.
Bao la ushindi la Liverpool lilifungwa na Xabi Alonso kwenye dakika ya 10 baada ya shuti lake kumbabatiza Beki wa Chelsea Bosingwa na kumpoteza maboya Kipa Petr Cech.
Mwenyekiti wa Tottenham atetea uamuzi wa kumtimua Ramos na kumchukua Redknapp

Mwenyekiti wa Tottenham Hotspurs Daniel Levy [pichani kushoto akiwa na Ramos] ametoa utetezi wake kumfukuza kazi Meneja Juande Ramos kwa barua ya wazi iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Klabu ya Tottenham.
Daniel Levy ameeleza uamuzi wa kumtimua Ramos pamoja na Mkurugenzi wa Michezo Damien Comoli [pichani kulia Comoli na Ramos] na kumuajiri Meneja wa Portsmouth Harry Rednapp [pichani chini kulia] umefanywa ili klabu irudi katika utawala wa asilia wa klabu za soka Uingereza.
Washabiki wengi walikuwa wanamponda Mkurugenzi wa Michezo Damien Comoli kwa ushauri na shindikizo bovu la usajili wa Wachezaji. Damien Levy anajitetea: 'Katika miaka mitatu iliyopita tulitumia Pauni Milioni 175 kusajili Wachezaji kufuatia ushauri mbovu! Sasa tutamwachia masuala yote ya usajili Meneja Harry Redknapp ambae ataiarifu bodi chaguo lake la wachezaji anaowataka!'
Vilevile Mwenyekiti Levy aligusia kwa nini Robbie Keane na Dimitar Berbatov waliuzwa kwa kutamka kuwa Robbie Keane alitaka mwenyewe kwenda Liverpool kwa madai ni klabu aliyoipenda tangu yuko mdogo ingawa wao walitegemea angebaki Tottenham hadi anastaafu.
Levy anaongeza: 'Kwa ushauri wa Makocha tuliona Keane hawezi tena kukaa hapa Tottenham kwani ataleta kutoelewana. Tukakubali kumuuza.'
'Lakini Berbatov ni suala jingine! Levy aliendelea. 'Yeye alipofika tu hapa Tottenham msimu wa kwanza tu akataka ahamie Manchester United. Tulikataa lakini kila ukija wakati wa uhamisho aliendelea kudai kuhama. Tukaona atatuvuruga tukamuuza!'
Menyekiti huyo aliendelea utetezi wake kwa kuwajulisha Washabiki kuwa yeye daima anajali maslahi ya Tottenham na ameahidi ikifika Januari, wakati msimu wa uhamisho wa Wachezaji utakapofunguliwa tena, basi Meneja mpya Harry Redknapp atapewa fungu nono la kununua Wachezaji wapya.
Tottenham wamtimua Ramos na kumchukua Redknapp!

Tottenham Hotspur wamemfukuza kazi Meneja wao Juande Ramos pamoja na Mkurugenzi wa Michezo Damien Comolli na wamemteua Meneja wa Portsmouth Harry Redknapp kuwa Meneja mpya.
Tottenham vilevile imewaachisha kazi Makocha Gus Poyet na Marcos Avarez.
Mechi ya leo ambayo Spurs inacheza na Bolton Makocha Wasaidizi Clive Allen na Alex Inglethorpe ndio watakaosimamia timu.
Mpaka sasa Tottenham ndiio wanashika mkia kwenye LIGI KUU wakiwa na pointi 2 tu katika mechi 8 walizocheza.
Juande Ramos alijiunga na Tottenham Oktoba 2007 akitokea klabu ya Sevilla ya Spain baada ya kufukuzwa kwa Meneja Mholanzi Martin Jol.

MAN U WAKANUSHA KUWA MAZUNGUMZO NA MOURINHO

Manchester United wameziponda taarifa kwamba wapo kwenye mazungumzo na Jose Mourinho ili awe Meneja wao baada ya kustaafu kwa Meneja wa sasa Sir Alex Ferguson.
Jose Mourinho mwenyewe ametamka wiki hii kwamba angependa kurudi tena kwenye LIGI KUU UINGEREZA mkataba wake na Inter Milan ukimalizika mwaka 2011 ingawa hakutaja klabu angeyopenda kwenda.
Nae Sir Alex Ferguson alishatamka kuwa hategemei kuendelea kuwa Meneja wa Man U baada ya mwaka 2010 wakati huo atakuwa ametimiza miaka 24 ya kuwa Meneja wa Man U.
Msemaji wa Manchester United ametamka: ‘Kama tulivyosema mara nyingi, hakuna mazungumzo yeyote ya nani atamrithi Sir Alex Ferguson akistaafu
.’

WALIO KILELENI KUKUMBANA LEO!

Timu za Chelsea na Liverpool zinazoongoza LIGI KUU zikiwa zote zina pointi 20 INGAWA Chelsea yuko mbele kwa idadi makubwa ya magoli zinapambana Stamford Bridge kwenye ngome ya Chelsea.
Stamford Bridge hakika ni ngome kwa Chelsea kwani mpaka sasa hawajafungwa hapo katika mechi 86 za LIGI KUU. Nao Liverpool, mbali ya kuhofia rekodi hiyo ya Chelsea, wao wenyewe wana rekodii mbaya ya kucheza hapo katika mechi za LIGI KUU kwani katika mechi 16 za ligi walizocheza hapo ni mechi moja tu walishinda.
Msimu huu Liverpool wamesha jizolea sifa ya kuwa mafundi wa kushinda mechi wanazotangulia kufungwa kama vile walivyofanya katika mechi zao na Middlesbrough, Manchester United, Manchester City na Wigan.
Nahodha wa Chelsea John Terry aemesema wao wana usongo wa kukata maini Liverpool ili kudhihirisha wao ndio wanaostahili kuwa Mabingwa.
Timu zinaweza kuchaguliwa kutoka kwa Wachezaji wafuatao:
Chelsea:
Cech, Bosingwa, Carvalho, Terry, Bridge, Mikel, Lampard, Deco, Malouda, Anelka, Kalou.
Liverpool: Reina, Arbeloa, Carragher, Agger, Dossena, Riera, Alonso, Mascherano, Gerrard, Kuyt, Keane.

MECHI NYINGINE ZA LEO JUMAPILI 26 OKTOBA 2008:

[saa 12 jioni]

Man City v Stoke City

Tottenham v Bolton

Wigan v Aston Villa

[saa 1 usiku]

West Ham v Arsenal

[saa 2 usiku]

Portsmouth v Fulham

Alex Ferguson adai alimtoa Rooney ili asipewe kadi nyekundu!

Sir Alex Ferguson amedai ilibidi ambadilishe Wayne Rooney katika mechi waliyotoka suluhu na Everton ili kumuokoa asipewe kadi nyekundu na Refa Alan Wiley ambae muda mfupi kabla ya hapo alimpa kadi ya njano Rooney kwa rafu dhidi ya Mikel Arteta, kadi ambayo Ferguson vilevile alidai haikustahili na Refa aliitoa kwa sababu ya shindikizo la watazamaji.
Wayne Rooney ambae alikuwa Mchezaji wa Everton kabla ya kujiunga na Man U kuna wakati alionekana akishika jezi yake na kuibusu huku akiwapungia mashabiki waliokuwa wakimzomea.
Powered By Blogger