Saturday, 24 April 2010

Ze Gunners kwisha kazi!!!
-Msimu mwingine tena patupuuuuu!!!
Leo wakiwa kwao Emirates, Arsenal rasmi wamemaliza matumaini yao ya kutwaa Ubingwa na kupata Kikombe cha kwanza tangu 2005 walipotoka sare 0-0 na Manchester City kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Kwa sare ya leo, Arsenal wamefikisha pointi 72 na wamebakisha mechi mbili wakati Man United wanaoongoza Ligi tayari wana pointi 79.
Pia, sare hii ya leo imewafanya Man City wang’ang’anie nafasi ya 5 pointi moja nyuma ya Tottenham waliofungwa mechi ya awali leo na Man United bao 3-2.
Mechi ya leo ni rahisi kuisahau kwa kukosa msisimko wowote labda kuzomewa kwa Emmanuel Adebayor wa Man City alieingizwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Patrick Viera ambae alikuwa akishangiliwa na Washabiki wa Arsenal.
Arsenal: Fabianski, Sagna, Campbell, Silvestre, Clichy, Song, Diaby, Walcott, Nasri, Rosicky, van Persie.
Vikosi vilivyoanza:
Akiba: Mannone, Eduardo, Vela, Eboue, Traore, Eastmond, Bendtner.
Man City: Given, Zabaleta, Toure, Kompany, Bridge, De Jong, Vieira, Barry, Adam Johnson, Bellamy, Tevez.
Akiba: Nielsen, Richards, Onuoha, Ireland, Wright-Phillips, Santa Cruz, Adebayor.
Refa: Mike Dean
Maporomoko yawanukia Hull, West Ham wajinasua polepole!!!!
MATOKEO LIGI KUU:
Jumamosi, 24 Aprili 2010
Man United 3 v Tottenham 1
Bolton 2 v Portsmouth 2
Hull 0 v Sunderland 1
West Ham 3 v Wigan 2
Wolves 1 v Blackburn 1
West Ham 3 Wigan 2
West Ham leo wamegangamara katika vita yao kujihakikishia wanabaki Ligi Kuu walipowafunga Wigan, Timu nyingine ambayo pia bado haijapona, kwa bao 3-2.
West Ham waliianza mechi hii kwa balaa baada ya Beki wao Jonathan Spector kujifunga mwenyewe kwenye dakika ya 4 tu. Lakini dakika ya 31 Ilan akasawazisha kufuatia krosi ya Carlton Cole na Radoslav Kovac akawapachikia West Ham bao la pili dakika ya 45.
Wigan wakaifanya gemu iwe 2-2 kupitia Rodallega kwenye dakika ya 52.
Scott Parker, Kiungo anaeibeba West Ham karibu kila mechi, ndie aliekuwa mkombozi alipofunga bao la ushindi dakika ya 77 kwa kigongo kutoka mita 25.
Kutokana na matokeo haya na pia leo Hull City kuchapwa 1-0 na Sunderland, huku kukiwa kumebaki mechi mbili tu, West Ham sasa wako pointi 6 juu ya Hull City walio Timu ya 3 toka mkiani na hivyo wana nafasi kubwa kupuruchuka kushushwa Daraja balaa ambalo linawakabili Hull City na Burnley ilio chini ya Hull.
Chini ya Hull na Burnley, kwenye nafasi ya mwisho, wapo Portsmouth ambao tayari washashuka Daraja.
Ikiwa kesho Burnley watafungwa na Liverpool, West Ham na Wigan watapata uhakika wa kubaki Ligi Kuu.
Hull City 0 Sunderland 1
Hull City walikosa penalti, Mchezaji wao Jozy Altidore, pamoja na Alan Hutton wa Sunderland, walitolewa kwa Kadi Nyekundu na wakafungwa bao 1-0 na hivyo safari ya kwenda kucheza Daraja la chini imeanza kuiva hasa baada ya Timu iliyo juu yao West Ham kuifunga Wigan 3-2 na kufanya pengo kati yao kuwa pointi 6 huku mechi zimebaki mbili tu.
Kichwa cha Darren Bent baada ya pasi ya Kenwyne Jones dakika ya 7 ndio kimewaua Hull City.
Rooney nje mechi za Man United
Straika wa Manchester United Wayne Rooney huenda akazikosa mechi za Timu yake zilizobaki za Msimu huu baada ya kuumia nyonga mazoezini siku ya Alhamisi lakini atakuwa fiti kuichezea England kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Habari za kuumia kwake zimethibitishwa na Kocha wake Sir Alex Ferguson na leo hakucheza kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Tottenham kwenye mechi ya LigI Kuu.
Hivi karibuni Rooney amekuwa akikumbwa na majeruhi na aliumizwa kwenye mechi zote mbili za Robo Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI Man United walipocheza na Bayern Munich.
Mechi za Man United za Ligi Kuu zilizobaki ni za wiki ijayo na Sunderland na ya mwisho ni Mei 9 na Stoke City.
Kwa England, Rooney, ambae ameifungia Klabu yake bao 34 Msimu huu na England bao 8, ni ufunguo wa mafanikio yao.
England itacheza mechi za kirafiki na Mexico Mei 24 Uwanjani Wembley na Japan huko Graz, Austria Mei 30.
Mechi ya kwanza kwa England kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ni Juni 12 dhidi ya USA Mjini Rustenburg.
Man United wadandia kilele!!!!
Katika mechi ya Ligi Kuu iliyoanza mapema leo, Manchester United wakiwa kwao Old Trafford, wamemudu kuwabamiza Wababe wa Chelsea na Arsenal, Tottenham, kwa bao 3-1 na kutwaa uongozi wa Ligi wakiwa pointi 2 mbele ya Chelsea ambao wanacheza kesho na Stoke City.
Wakicheza bila ya Mfungaji wao mkuu, Wayne Rooney, Manchester United walifunga bao zao 3 kipindi cha pili.
Bao la kwanza lilifungwa kwa penalti na Ryan Giggs baada ya Beki wa Spurs Assou-Ekotto kumkata Evra aliekuwa akichanja mbuga kufuatia pande la kisigino toka kwa Berbatov.
Hii ilikuwa dakika ya 58.
Tottenham walisawazisha dakika ya 70 baada ya kona ya Bale kumaliziwa kwa kichwa na Ledley King.
Kwenye dakika ya 82, gonga tamu kati ya Darren Fletcher, Kiko Macheda, alieingia kuchukua nafasi ya Rafael,na Nani ilimaliziwa kwa ufundi wa hali ya juu na Nani alieubetua mpira kwa ustadi mkubwa kumpita Kipa Gomes na kuandika bao la pili.
Man United wakapata penalti yao ya pili dakika ya 85 baada ya Wilson Palacios kumuangusha Nani ndani ya boksi na Refa Andre Marriner kuamua ni penalti.
Mkongwe Ryan Giggs, kwa utulivu mkubwa, akaupachika mpira kulia mwa Kipa Gomes na kuifanya Man United iwe mbele kwa bao 3-1.
Vikosi vilivyoanza:
Man United: Van der Sar, Rafael Da Silva, Vidic, Jonathan Evans, Evra, Fletcher, Scholes, Giggs, Valencia, Berbatov, Nani.
Akiba: Kuszczak, Hargreaves, Brown, Carrick, O'Shea, Macheda, Gibson.
Tottenham: Gomes, Assou-Ekotto, Dawson, King, Bale, Bentley, Huddlestone, Palacios, Modric, Defoe, Pavlyuchenko.
Akiba: Alnwick, Kaboul, Lennon, Jenas, Crouch, Gudjohnsen, Bassong.
Refa: Andre Marriner
KWA UFUPI Tu……………..
Rangers kuukwaa Ubingwa Scotland?
Klabu Kongwe huko Scotland, Rangers, huenda wakaunasa Ubingwa wa Nchi hiyo kwa mara ya pili mfululizo hapo Jumapili wakiifunga Hibernian.
Lakini Rangers pia wana nafasi kubwa ya Kuwa Mabingwa kabla ya mechi yao ya Jumapili ikiwa Mahasimu wao wakubwa Celtic wanaocheza na Dundee United mapema watashindwa kushinda.
Bosi wa Rangers, Walter Smith, ameitaka Timu yake itulie na ifanye kazi yao ipasavyo.
Zaki arudishwa Misri
Straika wa Misri Amr Zaki ameondolewa kutoka Timu ya Hull City alipokuwepo kwa mkopo na kurudishwa kwenye Klabu yake Zamalek ya Misri kwa sababu ni majeruhi.
Zaki, miaka 27, Msimu uliokwisha alicheza Wigan kwa mkopo na Msimu huu mwezi Januari alijiunga na Hull City kwa mkopo ambao ungedumu hadi mwishoni mwa Msimu.
Zaki alicheza mechi 6 za Hull bila ya kufunga goli na mwezi uliokwisha aliumia goti ambalo hawezi kupona kabla Ligi kumalizika.
Ligi Kuu inatazamiwa kumalizika Mei 9.
FIFA na Tiketi za Kombe la Dunia
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, amedai Viwanja huko Afrika Kusini kwenye mechi za Fainali ya Kombe la Dunia litalochezwa Juni 11 hadi Julai vitakuwa na Watazamaji asilimia 95 katika kila mechi.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa mechi kutokuwa na Watazamaji kutokana na kulegalega katika mauzo ya tiketi lakini tangu tiketi hizo zianzwe kuuzwa kwenye Masupamaketi Aprili 14 huko Nchini Afrika Kusini, mauzo yamechanganya mno.
Valcke amesema hadi sasa kuna tiketi 300,000 zimebaki lakini hazitagawiwa bure.
Awali FIFA na waandalizi wa huko Afrika Kusini walikuwa wakiuuza tiketi kwa kutumia mtandao lakini wakagundua kuwa huko Bondeni Watu wengi hununua tiketi za mechi kwenye Supamaketi na mara nyingi huwa ni siku ya mechi tu ndio Watu hufurika kukata tiketi.
Ni mechi ya Fainali ya Julai 11 ndio tiketi zote zimeuzwa. 
LIGI KUU: NDOTO ZA FISI????
Ukiachia Timu chache, Timu nyingi kwenye Ligi Kuu zimebakisha mechi 3 kumaliza Ligi na kileleni wapo Chelsea walio mbele ya Manchester United kwa pointi moja tu.
Nyuma ya Man United wapo Arsenal walio pointi 5 nyuma.
Kimahesabu, ni Chelsea, Man United na Arsenal ndizo zinaweza kutwaa Ubingwa ingawa nafasi kubwa ni ya Chelsea kwa vile tu yuko pointi moja mbele na akishinda mechi zake 3 zilizobaki ni Bingwa.
Hivyo, kwa Man United na Arsenal, ni ile hadithi ya Fisi kuufuata mkono wa Binadamu kungoja udondoke.
Lakini ni nani anajua kama ipo siku utadondoka?
RATIBA:
[Saa za Bongo]
_____________________________________
Jumamosi, 24 Aprili 2010
[saa 8 dak 45 mchana]
Man United v Tottenham
[saa 11 jioni]
Bolton v Portsmouth
Hull v Sunderland
West Ham v Wigan
Wolves v Blackburn
[saa 1 na nusu usiku]
Arsenal v Man City
________________________________________
Jumapili, 25 Aprili 2010
[saa 8 mchana]
Aston Villa v Birmingham
[saa 11 jioni]
Burnley v Liverpool
Everton v Fulham
[saa 12 jioni]
Chelsea v Stoke
------------------------------------------------
MSIMAMO LIGI KUU
[Aprili 24]:
1. Chelsea mechi 35 pointi 77
2. Man United mechi 35 pointi 76
3. Arsenal mechi 35 pointi 71
4. Tottenham mechi 34 pointi 64
5. Man City mechi 34 pointi 62
6. Aston Villa mechi 35 pointi 61
7. Liverpool mechi 35 pointi 59
8. Everton mechi 35 pointi 54
9. Birmingham mechi 35 pointi 47
10.Fulham mechi 34 pointi 43
11.Stoke mechi 34 pointi43
12.Blackburn mechi 35 pointi 43
13.Sunderland mechi 35 pointi 41
14.Bolton mechi 35 pointi 35
15.Wigan mechi 35 pointi 35
16.Wolves mechi 35 pointi 34
17.West Ham mechi 35 pointi 31
18.Hull mechi 35 pointi 28
19.Burnley mechi 35 pointi 27
20.Portsmouth mechi 35 pointi 15
MECHI ZA JUMAMOSI:
Manchester United v Tottenham
Baada ya kuzitandika Chelsea na Arsenal ndani ya siku 4, Tottenham wako safarini hadi Old Trafford kuwakwaa Mabingwa Watetezi Manchester United na hii ni mechi yenye uzito mkubwa kwa Timu zote mbili.
Man United wakishinda watachukua uongozi wa Ligi Kuu japo kwa masaa 24 tu ikiwa Chelsea atashinda mechi yake ya Jumapili atakapocheza na Stoke City.
Tottenham, walio nafasi ya 4 pointi 2 mbele ya Manchester City, wanataka kuendeleza ushindi ili wajikite vizuri nafasi hiyo itakayowapeleka Ulaya Msimu ujao.
Lakini, Man United wana rekodi nzuri ya kutofungwa Old Trafford na Tottenham kwenye Ligi Kuu na wameshinda mechi 14 kati ya 17 walizocheza pamoja.
Katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Msimu huu, Man United waliifunga Tottenham 3-1 huko White Hart Lane.
Arsenal v Man City
Mara nyingi Arsenal wakikumbana na kipigo, huibuka na kupata ushindi mnono lakini kile kipigo cha Wigan cha dakika 10 za mwisho kiliwastua wengi na Jumamosi wanakutana na Man City Timu inayowania nafasi ya 4 na yenye Wachezaji kadhaa waliotokea Arsenal kama vile Adebayor, Kolo Toure na Viera.
Mbali ya wachezaji hao wa zamani wa Arsenal, pia mechi hii inangojewa kwa hamu kwa vile Man City waliitwanga Arsenal 4-2 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Msimu huu.
Hull City v Sunderland
Hull City wako kwenye balaa la kushushwa Daraja wakiwa Timu ya 3 toka mkiani na wanakutana na Sunderland Timu ambayo tayari imepona balaa hilo.
Zikiwa zimebaki mechi 3 tu ni dhahiri mechi zinakwisha haraka kwa Hull kujinusuru.
West Ham v Wigan
Kudidimia kwa Hull City kumewapa ahueni kidogo West Ham walio pointi 3 mbele ya Hull na pambano lao na Wigan ni mechi muhimu kwao na pia kwa Wigan ambao kidogo walipata afueni walipoifunga Arsenal kimiujiza mechi ya wikiendi iliyopita.
Wolves v Blackburn
Ushindi kwa Wolves katika mechi hii na Blackburn utawahakikishia wanabaki Ligi Kuu.
Bolton v Portsmouth
Kwa Bolton, ushindi kwenye mechi hii dhidi ya Portsmouth ambayo tayari imeshashushwa, una maana watabaki Ligi Kuu.
MECHI ZA JUMAPILI:
Chelsea v Stoke City
Chelsea wako nyumbani Stamford Bridge kucheza na Stoke siku ya Jumapili na inawezekana wakati wanaanza mechi hii Man United atakuwa kileleni ikiwa watamfunga Tottenham siku ya Jumamosi.
Stoke wanaingia kwenye mechi hii bila ya woga wowote kwa vile wako salama kwenye Ligi Kuu.
Aston Villa v Birmingham
Hii ni dabi ya Timu za Midlands na Aston Villa bado wana matumaini ya kunyakua nafasi ya 4 ingawa kidogo iko mbali kwao kwani wako nafasi ya 6 pointi 3 nyuma ya Tottenham na wamecheza mechi moja zaidi.
Birmingham wao wanaelea tu kwenye Ligi Kuu na mechi hii kwao ni ya kulinda heshima kwa vile ni dabi.
Burnley v Liverpool
Baada ya safari ndefu ya ardhini hadi huko Spain walipofungwa 1-0 na Atletico Madrid kwenye Nusu Fainali ya EUROPA LIGI, Liverpool wanasafiri hadi Turf Moor kucheza na Burnley ambao wako nafasi moja toka mkiani.
Liverpool wako nafasi ya 7 na kimahesabu bado wako kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya 4.
Everton v Fulham
Uwanjani Goodison Park, Everton wanaikaribisha Fulham ambayo ndio kwanza imerudi toka Ujerumani walikotoka droo 0-0 na Hamburg kwenye Nusu Fainali ya EUROPA LIGI.

Friday, 23 April 2010

Wenger amlinda Adebayor
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ametoa wito kwa Mashabiki wa Arsenal kumheshimu Emmanuel Adebayor wakati Arsenal na Manchester City zitakapocheza kesho Jumamosi Uwanjani Emirates kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Wito wa Wenger unafuatia vitendo alivyofanya Adebayor, aliekuwa Mchezaji wa Arsenal kabla kuhamia Man City, katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu iliyochezwa Septemba na Man City kuifunga Arsenal 4-2 na Adebayor kwenda kushangilia kwa kejeli mbele ya Mashabiki wa Arsenal.
Kitendo hicho kilimpatia onyo kali toka kwa FA lakini pia katika mechi hiyo hiyo Adebayor alimtimba Robin van Persie na FA ikamfungia mechi 3.
Wenger ametamka: “Bila kujali kilichotokea mechi iliyopita ni muhimu kila mtu awe na nidhamu. Mtu hufanya makosa ambayo hujutia. Si kwa Adebayor tu hata kwa Viera na Toure- wote tunawakaribisha na tunaheshimu mchango wao kwa Arsenal.”
Kolo Toure, ambae ni Mchezaji mwenzake Adebayor Klabuni Man City na wote wametokea Arsenal, amemtaka Adebayor awe mtulivu na kutumia akili kwenye mechi na Arsenal.
Fergie azicheka kauli za kustaafu kwake
Sir Alex Ferguson ameziita kauli za kwamba atastaafu kuwa Meneja wa Manchester United mwishoni mwa Msimu wa 2010/11 kuwa ni za kipuuzi na kuzicheka.
Ferguson amesema: “Ni upuuzi mtupu! Hamna ukweli! Sina nia ya kustaafu na hata nikitaka kustaafu Watu ntakaowajulisha ni David Gill [Mkurugenzi Mtendaji wa Man United] na Familia ya Glazer.”
Ferguson amesisitiza kitu pekee kitakachoamua atabaki Manchester United au la ni afya yake na kwa sasa bado ni nzuri tu.
Huu ni mwaka wa 23 kwa Sir Alex Ferguson, mwenye umri wa miaka 68, kuwa Bosi wa Manchester United na ndie Meneja anaesifika wa kuwa na mafanikio makubwa mno katika historia ya kandanda ya huko Uingereza.
Msimu huu, Manchester United inawania kutwaa Ubingwa wa England kwa mara ya 4 mfululizo ikiwa ni kutaka kuweka historia kwa kuwa Klabu ya kwanza kuweza kufanya hivyo.
Hata hivyo, Man United wapo nafasi ya pili pointi moja nyuma ya Chelsea huku mechi zimebaki 3.
Man United ni KLABU TAJIRI!!!
Gazeti kubwa lenye hadhi, kusifika na kutambulika Ulimwenguni kote katika masuala ya biashara, Forbes, limetoa listi ya Klabu za Soka Tajiri Duniani na Manchester United ndio inaongoza ikifuatiwa na Real Madrid.
Forbes imetoa thamani ya Man United kuwa ni Pauni Bilioni 1.19, Real Madrid Pauni Milioni 859 na Arsenal, wakiwa nafasi ya 3, Pauni Milioni 767.
Forbes katika kutathmini hutumia takwimu zinazotokana na haki za matangazo, udhamini na mauzo ya tiketi na bidhaa mbalimbali za Klabu.
Katika listi hiyo ya Forbes yenye Timu 20, Barcelona iko nafasi ya 4 na zipo Klabu za Ligi Kuu England 6 pamoja na Newcastle United iliyocheza Daraja la Chini la Coca Cola Championship Msimu huu.
Katika 10 Bora pia zipo Chelsea, Liverpool na AC Milan ingawa thamani za Klabu hizo zimeporomoka kidogo.
LISTI KAMILI:
1. Manchester United
2. Real Madrid
3. Arsenal
4. Barcelona
5. Bayern Munich
6. Liverpool
7. AC Milan
8. Juventus
9. Chelsea
10. Inter Milan
11. Schalke 04
12. Tottenham Hotspur
13. Olympique Lyonnais
14. Hamburg SV
15. AS Roma
16. Werder Bremen
17. Olympique Marseille
18. Borussia Dortmund
19. Manchester City
20. Newcastle United
Mchezaji wa Man United awaua Liverpool!!
Atletico Madrid 1 Liverpool 0
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Diego Forlan, alifunga bao dakika ya 9 na kuihakikishia Atletico Madrid ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya kwanza ya EUROPA LIGI iliyochezwa Uwanjani Vicente Calderon Mjini Madrid, Spain.
Liverpool walionekana wachovu pengine ni sababu ya safari ya umbali wa maili 1200 kwa njia za Treni, Basi na Ndege kutokana na balaa la Majivu ya Volcano ya huko Iceland.
Timu hizi zitarudiana Anfield Alhamisi ijayo Aprili 29.
Ingawa Atletico Madrid wameshinda lakini pengine watajuta kwa kukosa bao kadhaa za wazi na labda kumkosa kwa Straika wao mwingine, Kun Aguero kutoka Argentina, kumechangia hilo.
Aguero hakucheza kwa vile kafungiwa lakini mechi ijayo yupo huru kucheza.
Nao Liverpool walionekana wazi pengo la Fernando Torres, ambae ni Mchezaji wa zamani wa Atletico Madrid, linawaletea kasoro.
Pia, katika mechi nzima Mawinga wa Atletico, Simao na Antonio Reyes, Mchezaji wa zamani wa Arsenal, waliwachachafya sana.
Vikosi vilikuwa:
Atletico Madrid: De Gea, Antonio Lopez, Ujfalusi, Dominguez, Perea, Raul Garcia, Paulo Assuncao, Simao [Valera 77], Forlan [Eduardo Salvio] 85], Jurado, Reyes [Camacho 90].
Liverpool: Reina, Johnson, Agger, Kyrgiakos, Carragher, Gerrard, Benayoun [El Zhar], Mascherano, Lucas, Kuyt, Ngog [Babel 64]
Hamburg 0 Fulham 0
Kwenye Nusu Fainali nyingine ya EUROPA LIGI, Fulham wakicheza ugenini huko Ujerumani walimudu kutofungwa na Hamburg na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri Timu hizi zitakaporudiana huko Craven Cottage Alhamisi ijayo Aprili 29.
Fulham, wakicheza fomesheni ya 4-5-1 huku Bobby Zamora akiwa ndie Straika pekee mbele, walipata pigo pale Zamora alipoumia na kutolewa dakika ya 52 na kuingizwa Clint Dempsey.
Nao Hamburg, walikosa bao pale Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy, aliposhindwa kufunga.
Katika mechi yote, Fulham walisimama ngangari katika ulinzi.
Vikosi vilikuwa:
Hamburg: Rost, Mathijsen, Boateng, Demel [Rincon 82], Aogo, Ze Roberto, Jarolim, Trochowski, Pitroipa, Guerrero [Petric 72], Ruud van Nistelrooy
Fulham: Schwarzer, Konchesky, Hangeland, Baird, Hughes, Gera, Murphy, Duff, Etuhu, Davies, Zamora [Dempsey 52]

Thursday, 22 April 2010

Mchezaji alieiua Arsenal akamatwa!!
Mchezaji wa Wigan Charles N'Zogbia amekamatwa kwa madai kuwa alimkodi Mtu mwingine amfanyie Testi yake ya nadharia ya kupata Leseni ya Kuendesha Gari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 mwenye Uraia wa Ufaransa lakini mwenye asili ya Congo alikamatwa na Polisi mara baada ya kuwasili kwenye Kituo cha kufanyia Testi ya Vitendo.
N’Zogbia yuko nje kwa dhamana hadi Juni 3.
Jumapili iliyopita N’Zogbia ndie alieifungia Wigan bao la 3 na la ushindi dakika za majeruhi na kuiua Arsenal 3-2.
Meneja wa Wigan Roberto Martinez amesema: “Nadhani ni kosa la kijinga! Tutaangalia kila kitu na kujua nini tumsaidie!”
Liverpool wataka bao la ugenini huko Vicente Calderon
Liverpool leo wako huko Spain Uwanja wa Vicente Calderon kuivaa Atletico Madrid katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya EUROPA LIGI na Meneja wao Rafa Benitez anahisi ni muhimu kufunga bao la ugenini.
Liverpool waliwasili Madrid kwa njia ya mzunguko wakitumia Basi, Treni na Ndege kwa hatua ya mwisho kufuatia kusimama kwa safari za Ndege kwa sababu ya mlipuko wa Volcano ya Iceland iliyosambaza Majivu.
EUROPA LIGI ndio nafasi ya mwisho kwa Liverpool kutwaa Kombe.
Liverpool leo watamkosa Mchezaji wao ambae kabla alikuwa Mchezaji na Kipenzi cha Atletico Madrid, Fernando Torres, ambae ameumia goti.
Ingawa Benitez anataka goli la ugenini lakini Meneja wa Atletico Madrid, Quique Sanchez Flores ana maoni kuwa Mshindi atajulikana baada ya mechi ya marudiano huko Anfield wiki ijayo.
Adebayor aonywa kuhusu mechi Jumamosi huko Emirates
Straika wa Manchester City ambae alitokea Arsenal, Emmanuel Adebayor, ameambiwa ni wajibu wake kutumia akili wakati Timu yake Manchester City watakapokuwa Wageni wa Timu yake ya zamani Arsenal Uwanjani Emirates kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi hii inayokuja.
Adebayor alikumbana na kashkash ya FA na kupewa onyo kali aliposhangilia goli lake mbele ya Mashabiki wa Arsenal mwezi Septemba Timu hizo zilipocheza mechi ya Ligi na Man City kuifunga Arsenal 4-2 Uwanjani City of Manchester na ushangiliaji huo ulizua hasira toka kwa Mashabiki wa Arsenal.
Mchezaji mwenzake wa Man City ambae pia alitokea Arsenal, Kolo Toure, amemtaka Adebayor apunguze mzuka na alisema kuwa kitendo cha Adebayor katika mechi ya kwanza hakikuwa kizuri.
Mbali ya ushangiliaji wake uliompa onyo la FA, Adebayor pia alifungiwa mechi 3 kwa kitendo chake cha kumtimba Robin van Persie katika mechi hiyo.
Mechi ya Jumamosi ni muhimu mno kwa Man City ambao wako nafasi ya 5 pointi 2 nyuma ya Tottenham walio nafasi ya 4 kwani Timu itakayomaliza nafasi ya 4 inaungana na Timu 3 za juu kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Kwa Arsenal nao kimahesabu bado wanaweza kuwa Mabingwa kwani wako pointi 6 nyuma ya vinara Chelsea huku zimebaki mechi 3.
NUSU FAINALI: Leo Atletico Madrid v Liverpool & Hamburger SV v Fulham
Baada ya kusafiri kwa ‘Madaladala’ hadi Spain na Ujerumani, leo usiku Timu za Liverpool na Fulham ziko ugenini kucheza mechi za kwanza za Nusu Fainali za EUROPA LIGI wakati Liverpool atakapomenyana na Atletico Madrid na Fulham wataivaa Hamburger.
Marudio ya mechi hizo ni Alhamisi ijayo Aprili 29.
Bayern Munich 1 Lyon 0
Wakiwa kwao Uwanja wa Allianz Arena, Bayern Munich walimpoteza Staa wao Franck Ribery aliewashwa Kadi Nyekundu na Refa kutoka Italia Roberto Rosetti baada ya kumtimba Cris kwenye dakika ya 37 lakini wakaibuka washindi kwa shuti la Staa wao mwingine Arjen Robben lililomparaza Muller kichwani na kumbabaisha Kipa Lloris na kutinga wavuni kwenye dakika ya 69 kuwapa Bayern ushindi wa bao 1-0.
Lyon pia walimpoteza Mchezaji wao Toulalan aliepewa Kadi mbili za Njano na kutolewa dakika ya 54 lakini walinusurika athari zaidi ya kukosa Wachezaji kwenye mechi ya marudiano wiki ijayo baada ya Wachezaji wao wengine kukwepa Kadi kwani walikuwa na Wachezaji 7 tayari wana Kadi na kama wangepata Kadi ya Njano wasingecheza marudiano.
Vikosi vilivyoanza:
Bayern Munich: Butt, Lahm, Van Buyten, Demichelis, Contento, Robben (Altintop 85), Schweinsteiger, Pranjic (Gomez 63), Ribery, Muller, Olic (Tymoschuk 46).
Akiba hawakucheza: Rensing, Gorlitz, Klose, Alaba.
Lyon: Lloris, Reveillere, Cris, Toulalan, Cissokho, Gonalons, Kallstrom, Ederson (Michel Bastos 71), Pjanic (Makoun 55), Delgado (Govou 79), Lopez. Akiba hawakucheza: Vercoutre, Gomis, Anderson, Gassama.
Hull City 0 Aston Villa 2
Aston Villa wameendelea kuweka hai matumaini yao ya kunyakua nafasi ya 4 kwenye Ligi Kuu walipoichapa Hull City bao 2-0 kwenye Uwanja wa KC.
Bao la kwanza la Villa lilipatikana dakika ya 13 baada ya Beki Paul McShane kuokoa butu na mpira kumfikia Straika wa Villa John Carew aliemsogezea Gabriel Agbonlahor na kufunga.
James Milner akaipatia Villa bao la pili kwa penalti dakika ya 76 baada ya yeye mwenyewe kuangushwa na George Boateng.
Obi kwaheri Msimu!!!
Kiungo wa Chelsea kutoka Nigeria, John Obi Mikel, yumo hatarini kuzikosa mechi zilizobaki za Ligi Kuu Msimu huu baada ya kuumia goti na kuambiwa anahitaji wiki 3 ili kupona.
Obi alitoka nje dakika ya 33 huko White Hart Lane Chelsea walipofungwa na Tottenham 2-1 wikiendi iliyokwisha na kubadilishwa na Michael Ballack.
Mechi zinazofuata za Chelsea za Ligi Kuu ni Jumapili watakapocheza na Stoke City, tarehe 1 Mei na Liverpool na tarehe 9 Mei, Ligi itakapokwisha, watamaliza na Wigan.
Mei 15, Chelsea wapo Wembley kucheza Fainali ya FA Cup na Portsmouth.

Wednesday, 21 April 2010

Nasri: ‘Inakera hatuna Kombe Msimu huu!!!’
Samir Nasri anaamini si haki kabisa kwa Timu yake Arsenal kukosa Kikombe kwa mara nyingine tena Msimu huu wakibaki wakiuendeleza ukame wa Vikombe tangu mwaka 2005 ingawa anaamini tatizo lao kubwa lilikuwa kukabiliwa na majeruhi wengi.
Wengi wanahisi nafasi ya Arsenal ya mwisho kupata Kombe ilipotezwa pale walipoumwaga uongozi wa bao 2-0 huku dakika zimebaki 10 tu na kujikuta wakichapwa 3-2 na Wigan kwenye mechi ya Ligi Kuu wikiendi iliyopita na kuwafanya wawe nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi 6 huku mechi zimebaki 3.
Staa wa zamani wa Arsenal Ian Wright ametamka kuwa Klabu hiyo inahitaji mabadiliko makubwa ikiwa wanataka kurudia mafanikio ya enzi zao.
Lakini Samir Nasri anadai, chini ya Wenger, Timu ina mwelekeo mzuri na alisisitiza: “Inakera! Tunafanya kazi kubwa lakini hatupati mafanikio, hatushindi Vikombe! Si haki kwani sisi tunastahili sana kupita wale wanaojenga Timu kwa kutumia pesa nyingi!”
Nasri anaamini kama wasingekuwa na majeruhi wengi Msimu wote lazima wangepata mafanikio.
Kwa nyakati tofauti, Arsenal walikumbwa na kuumia kwa Mastaa kama vile Robin van Persie, Nahodha Cesc Fábregas, Andrey Arshavin na Theo Walcott.
Hata mwenyewe Nasri alikumbwa na balaa la kuvunjika mguu kabla Msimu huu haujaanza.
Wadau wengi wanahisi ni wajibu wa Wenger kukiimarisha Kikosi chake, hasa Defensi, kwa vile Wakongwe kina Sol Campbell, William Gallas na Mikaël Silvestre watakuwa wamemaliza Mikataba yao mwishoni mwa Msimu huu.
Lakini mpaka sasa hakuna anaejua kinachoendelea labda ule ‘uhakika’ wa Straika toka Morocco anaechezea Bordeaux ya Ufaransa, Marouane Chamakh, kutua Arsenal.
UEFA CHAMPIONS LIGI: Leo Bayern Munich v Lyon
Leo usiku, huko Munich, Ujerumani Uwanja wa Allianz Arena, Wababe wa Manchester United, Bayern Munich, watakuwa dimbani kuwakwaa Lyon ya Ufaransa katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya pili ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Jana, Inter Milan waliifunga Barcelona 3-1 katika Nusu Fainali nyingine.
Kutokana na tatizo la usafiri wa anga lililoikumba Ulaya kufuatia Majivu ya Volcano iliyolipuka huko Iceland, Lyon ilibidi waazime ‘Vipanya’ 10 ili wasafirie kwenda Ujerumani.
Wenyeji Bayern Munich watawakosa Wachezaji wao Mark van Bommel na Holger Badstuber ambao wana Kadi.
Lyon watawakosa majeruhi Jean Makoun, Mathieu Bodmer na Jean-Alain Boumsong.
Pia, Lyon watacheza mechi hii huku Wachezaji wao 7 wako hatarini kuikosa mechi ya marudiano Aprili 27 endapo leo watapata Kadi za Njano.
LIGI KUU England: Leo ni Hull City v Aston Villa
Hull City, ambao wako taabani kwenye eneo la kushushwa Daraja wakiwa pointi 3 nyuma ya Timu zilizo salama, leo wako nyumbani kucheza na Timu ngumu Aston Villa kwenye mechi pekee ya Ligi Kuu.
Hull City wana mechi moja mkononi ukilinganisha na Timu zilizoizunguka na hilo huenda likawapa motisha zaidi ili leo wajitutumue.
Aston Villa wako pointi 6 nyuma ya Timu ya 4, Tottenham, na kimahesabu wanaweza wakainyaka nafasi hiyo inayogombewa pia na Manchester City na Liverpool ili kucheza Ulaya Msimu ujao.
Vikosi vinaweza kuwa:
Hull City: Myhill, McShane, Sonko, Mouyokolo, Dawson, Fagan, Cairney, Bullard, Boateng, Kilbane, Vennegoor of Hesselink.
Aston Villa: Friedel, Cuellar, Dunne, Collins, Warnock, Downing, Milner, Petrov, Ashley Young, Carew, Agbonlahor.
Mourinho achekelea na kuiponda Barca!!!
Jose Mourinho amewaponda Barcelona kwa kuwa wasahaulifu na kuanza kulaumu kunyimwa penalti katika kipigo cha 3-1 jana Uwanjani San Siro mikononi mwa Timu yake Inter Milan katika Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Mourinho alisema: “Inasikitisha. Mwaka jana Chelsea walikuwa wanalia na Barca wakawa wanacheka na Refa. Walikuwa wanacheka kwa sababu Refa aliwanyima Vijana wangu wa Chelsea haki yao.”
Mourinho, ambae alikuwa Bosi wa Chelsea na kuondoka Septemba 2007, alikuwa akikumbushia Nusu Fainali ya Msimu uliopita ya UEFA CHAMPIONS LIGI kati ya Chelsea na Barcelona ambayo Barcelona walishinda kwa goli la ugenini baada ya Andres Iniesta kusawazisha dakika za majeruhi katika mechi ambayo Refa Tom Ovrebo aliwanyima Chelsea penalti kibao.
Katika mechi ya jana, Mchezaji wa Barca Daniel Alves alitwangwa Kadi ya Njano baada ya kujidondosha kwenye boksi huku Barca wakidai ilikuwa ni penalti.
Mourinho alikisifia Kikosi chake kwa kucheza kwa ustadi na kuifunga ‘Timu Bora Duniani.’
Nae Kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, alikataa kutoa kisingizio cha uchovu kwa kusafiri kutoka Spain hadi Italia kwa Mabasi kufuatia kusimama kwa safari za anga huko Ulaya baada ya kukumbwa na balaa la majivu kutoka Volcano ya Iceland.
Guardiola amesema: “Hii hutokea kwenye Nusu Fainali ukicheza na Timu ngumu kama Inter. Najua Wachezaji wamechoka lakini hio sio sababu. Huko Barcelona, tutashambulia! Tutamwagia maji kiwanja ili mpira uwe unateleza haraka kwenye nyasi jambo ambalo hapa hawakufanya!”
Liverpool watua Madrid kwa ‘Daladala!”
Liverpool wamewasili Mjini Madrid huko Spain kwa ajili ya pambano lao la Nusu Fainali ya EUROPA LIGi la kesho watakapocheza na Atletico Madrid baada ya safari ya zaidi ya Maili 1200 kwa kutumia Treni, Basi na Ndege.
Usafiri huo mgumu umesababishwa na athari ya Majivu ya Volcano kutoka Iceland iliyolipuka na kutapakaza Majivu yaliyosimamisha safari za Ndege eneo kubwa la Ulaya.
Liverpool walianza safari yao Siku ya Jumanne.
Na wenzao Fulham ambao pia wanacheza Nusu Fainali ya EUROPA LIGI hapo kesho huko Ujerumani watakapokutana na Hamburg wamelazimika pia kusafiri kwa usafiri wa ardhini .
Inter Milan 3 Barcelona 1
Inter Milan, wakiwa bao moja nyuma, walifanikiwa kuilaza Barcelona mabao 3-1 Uwanjani San Siro kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Barca walipata bao lao kupitia Pedro baada ya krosi ya Maxwell.
Inter walisawazisha pale Wesley Sneijder alipofunga kufuatia pasi ya Diego Milito na ni Milito tena aliemtengenezea Maicon kufunga bao la pili.
Na ni Milito alieifungia Inter bao la 3.
Katika mechi hii Inter walimudu kuwabana Barca ambao nyota wao Lionel Messi alionekana kupwaya.
Mechi ya marudiano ni wiki ijayo Aprili 28 huko Nou Camp.
Leo ni Nusu Fainali ya pili kati ya Bayern Munich na Lyon.

Tuesday, 20 April 2010

Inter Milan v Barcelona
Leo saa 3 dakika 45 usiku, saa za bongo, Nusu Fainali ya kwanza ya UEFA CHAMPIONS LIGI itachezwa huko Uwanjani San Siro, nyumbani kwa Inter Milan, kwa Wenyeji hao kuwakaribisha Mabingwa Watetezi, Barcelona, waliolazimika kusafiri kutoka kwao Spain kwa njia ya barabara kufuatia kusimama kwa Usafiri wa Anga kufuatia kusambaa kwa Majivu kutoka Volcano iliyolipuka huko Iceland.
Msimu huu, Timu hizi mbili zimeshawahi kukutana mara mbili kwenye Michuano hii katika hatua za awali za Makundi na mechi ya kwanza Uwanjani San Siro ilikuwa 0-0 na marudiano huko Nou Camp Barca walishinda 2-0.
Katika mechi ya leo, Barca wataikosa Injini yao moja ya Kiungo, Andres Iniesta, ambae ni majeruhi.
Inter, safu yao ya mashambulizi, itaongozwa na Mchezaji wa zamani wa Barca, Samuel Eto’o,
Mechi ya marudiano itafanyika Nou Camp Aprili 28.
Kesho kutakuwa na mechi ya Nusu Fainali ya pili kati ya Bayern Munich na Lyon.
Newcastle Mabingwa
Newcastle United, ambao tayari wamefuzu kupanda Daraja pamoja na West Bromwich Albion na kurudi Ligi Kuu England, baada ya Msimu mmoja tu kwenye Coca Cola Championship, jana walifanikiwa kuutwaa Ubingwa wa Daraja lao la Coca Cola Championship walipowafunga Plymouth bao 2-0.
Mabao ya Newcastle yalifungwa na Andy Carroll na Routledge.
Liverpool 3 West Ham 0
Katika mechi ya Ligi Kuu hapo jana, Liverpool walimudu kuichapa West Ham bao 3-0 na kushika nafasi ya 6 wakiwa na pointi 59 kwa mechi 35 na juu yao kwenye nafasi ya 5 wako Man City wenye pointi 62 kwa mechi 34 na nafasi ya 4 ni Tottenham waliocheza mechi 34 na wana pointi 64.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Yossi Benayoun, David Ngog na Sotiros Kyrgiakos.
Mutu kifungo Miezi 9
Straika wa Romania, Adrian Mutu, ameendelea kukumbwa na mabalaa ya kufumaniwa akitumia madawa marufuku na hivyo kufungiwa kwa mara ya pili na safari hii amekikwaa kifungo cha Miezi 9 kilichotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Italia alipogunduliwa kutumia dawa marufuku Mwezi Januari katika mechi kati za Timu yake Fiorentina dhidi ya Bari na nyingine na Lazio na atatumikia kifungo hicho hadi Oktoba 29.
Mwaka 2004, akiwa Chelsea, alikikwaa kifungo baada ya kugunduliwa akitumia kokeni.

Monday, 19 April 2010

Ligi Kuu basi kwa Torres
Mshambuliaji wa Liverpool Fernando Torres ameshaiaga Ligi Kuu Msimu huu pale alipofanyiwa upasuaji wa goti lake siku ya Jumapili na Madaktari wanasema kupona atachukua wiki 6 na hii ina maana hawezi kucheza tena Ligi kwa vile inamalizika Mei 9.
Hata Timu yake ya Taifa Spain itakuwa ikimtazama kwa wasiwasi kwani Timu zinatakiwa kuwasilisha kwa FIFA Listi zao za mwisho za Wachezaji 23 Juni 1.
Kwenye Ligi Kuu, Liverpool bado ina nafasi finyu ya kuipata nafasi ya 4 itakayowawezesha kucheza Ulaya Msimu ujao.
Alhamisi, Liverpool wapo Spain kucheza mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya EUROPA LIGI na Atletico Madrid.
Pompey 1 Villa 2
Nathan Delfouneso aliingizwa kama Mchezaji wa Akiba kipindi cha pili na kufunga bao la ushindi kwa Aston Villa dhidi ya Portsmouth ambayo tayari ishashuka Darajana kuyaweka hai matumaini ya kuipata nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyochezwa Fratton Park, Pompey walikuwa wa kwanza kupata bao Mfungaji akiwa Michael Brown dakika ya 10 na Villa wakasawazisha kwa bao la John Carew dakika ya 16.
Papa Bouba Diop akawapa Villa zawadi pale chenga zake ndani ya boksi zilipomfanya acheze rafu aliponyang’anywa mpira na kutolewa penalty ambayo ilipigwa na John Carew lakini Kipa wa Pompey David James akapangua.
Dakika ya 82 ndipo Delfouneso akafunga bao la pili na la ushindi na kuwafanya Villa wafikishe pointi 58 wakiwa nafasi ya 6, juu yao wapo Man City wenye pointi 62 na Spurs wako nafasi ya 4 wakiwa na pointi 64.
Timu hizi zote zimebakisha mechi 4.

Sunday, 18 April 2010

Wenger awaka!
Baada ya kipigo cha bao 3-2 toka kwa Wigan wakiwa wanaongoza 2-0 na dakika zikiwa zimebaki 10, Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, amehuzunishwa na kukasirishwa na kushindwa mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyowapotezea matumaini ya kuuonja Ubingwa.
Wenger alilalamika: “Siwezi kusema jinsi kushindwa huko kunavyokera!”
Wenger pia alikiri Kipa wake Fabianski alikuwa na makosa alipofungwa bao la pili lililofanya mechi iwe 2-2.
Wenger alikubali kuwa, kimahesabu, hata Manchester City na Tottenham, zinaweza kuwakuta na kuwapiku kutoka nafasi ya 3 na hivyo ni muhimu kwao kushinda mechi inayofuata.
Alipoulizwa nani sasa atakuwa Bingwa kati ya Chelsea na Manchester United, Wenger alijibu kimkato: “Haipo akilini na wala sijali! Ninachojua ni kwamba tungeshinda leo bado tungekuwa kwenye kinyang’anyiro cha Ubingwa!”
MAJIVU KUTIBUA MECHI ZA ULAYA WIKI HII?
Ulaya imekumbwa na balaa la majivu yatokayo kwenye Volcano iitwayo Eyjafjallajoekul ya huko Iceland na kutapakaa Nchi kadhaa huko Ulaya na kusababisha kusimama kwa safari za Ndege kwa vile majivu hayo huzidhuru Ndege na hatari kubwa ni kuweza kuzifanya Injini za Ndege kuzimika.
UEFA imekuwa ikifuatalia matatizo hayo kwa karibu kwani wiki hii ipo michuano ya Ulaya nayo ni ile ya Nusu Fainali za UEFA CHAMPIONS LIGI Siku za Jumanne na Jumatano.
Alhamisi ni Nusu Fainali za EUROPA LIGI.
Barcelona watasafiri hadi Italia kwa barabara kucheza na Inter Milan kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI siku ya Jumanne na Jumatano Timu ya Ufaransa Lyon watakuwa Ujerumani kucheza na Bayern Munich na wataenda huko kwa usafiri wa barabara.
Lakini mechi za EUROPA LIGI za Nusu Fainali za Liverpool na Fulham ndizo zenye matatizo makubwa ya usafiri kwani Liverpool wanatakiwa kusafiri hadi Spain kucheza na Atletico Madrid na Fulham wanatakiwa kwenda Ujerumani kucheza na Hamburg.
Ze Gunners watwangwa!!!
Dakika 10 za mwisho zilizaa mabao matatu ya Wigan waliokuwa nyuma kwa bao mbili na kuweza kuitwanga Arsenal bao 3-2 na kuifanya Arsenal ipoteze matumaini ya Ubingwa.
Theo Walcott aliipa Arsenal bao la kwanza na Mikael Silvestre akapachika bao la pili kwa kichwa kufuatia kona.
Lakini Wigan ambao bado walikuwa kwenye wimbi la hatari ya kushuka walijitutumua na katika dakika 10 za mwisho wakafunga bao 3.
Ben Watson akaipatia Wigan bao la kwanza na Kipa wa Arsenal Lukasz Fabianski akafanya uzembe uliomruhusu Titus Bramble kupiga kichwa na kufunga.
Kwenye dakika za majeruhi huku bao zikiwa 2-2, Charles N’Zogbia akafumua fataki nje ya boksi na mpira kugonga mwamba na kutinga wavuni.
Bao hilo pengine ndio limeua matumaini yote ya Arsenal ya kutwaa Ubingwa kwani wamekwama wakiwa nafasi ya 3, mechi zimebaki 3 na wana pointi 71.
Juu yao wapo Manchester United wenye pointi 76 na Chelsea ndio vinara wenye 77 na Timu zote hizo zimebakisha mechi 3.
Fergie kicheko, Wataliana wawili kilio!!!
Mancini akasirika, Ancelotti ataka Timu isiingiwe hofu!!
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amechukizwa na kuvunjwa moyo na kufungwa 1-0 na Manchester United hapo jana kwa bao la Paul Scholes katika dakika za majeruhi.
Matokeo hayo yameifanya Manchester United wawe pointi 1 tu nyuma ya Chelsea ambao baadae hapo jana walifungwa 2-1 na Tottenham.
Kipigo hicho cha Man City na ushindi kwa Tottenham kimewafanya Man City wawe nafasi ya 5 pointi 2 nyuma ya Tottenham ambao sasa wanashikilia ile nafasi ya 4 ambayo inagombaniwa ili Timu itakayoipata icheze UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao pamoja na Timu 3 za juu, Chelsea, Man United na Arsenal.
Mancini alisema mechi yao na Tottenham mwezi ujao ndio itakayoamua nani anachukua nafasi ya 4.
Nae Sir Alex Ferguson aliushangilia ushindi wa jana wa Timu yake kwa kusema ingekuwa ngumu mno kwao kuwaza Ubingwa kama wasingeshinda jana.
Ferguson alisema mwishoni mwa mechi alimtaka Paul Scholes acheze mbele zaidi ili kutafuta goli: “Scholes ana kipaji! Ni Mchezaji bora sana!”
Ferguson pia aliwasifia Wakongwe wengine, Ryan Giggs na Gary Neville, kwa kusema katika mechi ngumu hasa za dabi uzoefu ni kitu muhimu.
Huko Chelsea, Bosi wao, Carlo Ancelotti, amewataka Wachezaji wake wasivunjike moyo kufuatia kufungwa 2-1 na Tottenham.
Ancelotti amesema: “Tunajua nini tufanye mechi zilizobaki. Hamna haja ya kupatwa hofu! Tuna mechi 3 zimebaki.”
Kuhusu kutolewa kwa Kadi Nyekundu kwa Nahodha wake John Terry ambae ataikosa mechi moja ya Ligi, Ancelotti hakutaka kuzungumza lolote kuhusu hilo.
Powered By Blogger