Sunday 18 April 2010

Fergie kicheko, Wataliana wawili kilio!!!
Mancini akasirika, Ancelotti ataka Timu isiingiwe hofu!!
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amechukizwa na kuvunjwa moyo na kufungwa 1-0 na Manchester United hapo jana kwa bao la Paul Scholes katika dakika za majeruhi.
Matokeo hayo yameifanya Manchester United wawe pointi 1 tu nyuma ya Chelsea ambao baadae hapo jana walifungwa 2-1 na Tottenham.
Kipigo hicho cha Man City na ushindi kwa Tottenham kimewafanya Man City wawe nafasi ya 5 pointi 2 nyuma ya Tottenham ambao sasa wanashikilia ile nafasi ya 4 ambayo inagombaniwa ili Timu itakayoipata icheze UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao pamoja na Timu 3 za juu, Chelsea, Man United na Arsenal.
Mancini alisema mechi yao na Tottenham mwezi ujao ndio itakayoamua nani anachukua nafasi ya 4.
Nae Sir Alex Ferguson aliushangilia ushindi wa jana wa Timu yake kwa kusema ingekuwa ngumu mno kwao kuwaza Ubingwa kama wasingeshinda jana.
Ferguson alisema mwishoni mwa mechi alimtaka Paul Scholes acheze mbele zaidi ili kutafuta goli: “Scholes ana kipaji! Ni Mchezaji bora sana!”
Ferguson pia aliwasifia Wakongwe wengine, Ryan Giggs na Gary Neville, kwa kusema katika mechi ngumu hasa za dabi uzoefu ni kitu muhimu.
Huko Chelsea, Bosi wao, Carlo Ancelotti, amewataka Wachezaji wake wasivunjike moyo kufuatia kufungwa 2-1 na Tottenham.
Ancelotti amesema: “Tunajua nini tufanye mechi zilizobaki. Hamna haja ya kupatwa hofu! Tuna mechi 3 zimebaki.”
Kuhusu kutolewa kwa Kadi Nyekundu kwa Nahodha wake John Terry ambae ataikosa mechi moja ya Ligi, Ancelotti hakutaka kuzungumza lolote kuhusu hilo.

No comments:

Powered By Blogger