Saturday, 24 April 2010

KWA UFUPI Tu……………..
Rangers kuukwaa Ubingwa Scotland?
Klabu Kongwe huko Scotland, Rangers, huenda wakaunasa Ubingwa wa Nchi hiyo kwa mara ya pili mfululizo hapo Jumapili wakiifunga Hibernian.
Lakini Rangers pia wana nafasi kubwa ya Kuwa Mabingwa kabla ya mechi yao ya Jumapili ikiwa Mahasimu wao wakubwa Celtic wanaocheza na Dundee United mapema watashindwa kushinda.
Bosi wa Rangers, Walter Smith, ameitaka Timu yake itulie na ifanye kazi yao ipasavyo.
Zaki arudishwa Misri
Straika wa Misri Amr Zaki ameondolewa kutoka Timu ya Hull City alipokuwepo kwa mkopo na kurudishwa kwenye Klabu yake Zamalek ya Misri kwa sababu ni majeruhi.
Zaki, miaka 27, Msimu uliokwisha alicheza Wigan kwa mkopo na Msimu huu mwezi Januari alijiunga na Hull City kwa mkopo ambao ungedumu hadi mwishoni mwa Msimu.
Zaki alicheza mechi 6 za Hull bila ya kufunga goli na mwezi uliokwisha aliumia goti ambalo hawezi kupona kabla Ligi kumalizika.
Ligi Kuu inatazamiwa kumalizika Mei 9.
FIFA na Tiketi za Kombe la Dunia
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, amedai Viwanja huko Afrika Kusini kwenye mechi za Fainali ya Kombe la Dunia litalochezwa Juni 11 hadi Julai vitakuwa na Watazamaji asilimia 95 katika kila mechi.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa mechi kutokuwa na Watazamaji kutokana na kulegalega katika mauzo ya tiketi lakini tangu tiketi hizo zianzwe kuuzwa kwenye Masupamaketi Aprili 14 huko Nchini Afrika Kusini, mauzo yamechanganya mno.
Valcke amesema hadi sasa kuna tiketi 300,000 zimebaki lakini hazitagawiwa bure.
Awali FIFA na waandalizi wa huko Afrika Kusini walikuwa wakiuuza tiketi kwa kutumia mtandao lakini wakagundua kuwa huko Bondeni Watu wengi hununua tiketi za mechi kwenye Supamaketi na mara nyingi huwa ni siku ya mechi tu ndio Watu hufurika kukata tiketi.
Ni mechi ya Fainali ya Julai 11 ndio tiketi zote zimeuzwa. 

No comments:

Powered By Blogger