Saturday 15 May 2010

Drogba aipa Ze Bluzi FA CUP!
Didier Drogba ni Shujaa wa Chelsea baada ya kufunga goli muhimu na la pekee na kuwapa ushindi wa kutwaa Kombe la FA dhidi ya Portsmouth leo Uwanjani Wembley.
Ushindi huu umehitimisha Msimu Bora katika historia ya Chelsea kwani hii ni mara ya kwanza kutwaa Vikombe viwili katika Msimu mmoja.
Portsmouth wangeweza kupata bao walipopewa penalti baada ya Arunda Dindane kuangushwa na Juliano Belleti lakini Boateng akashindwa kufunga.
Ndipo, mara baada ya tukio hilo, Drogba akafunga bao kwa frikiki.
Frank Lampard angeweza kuipatia Chelsea bao la pili kwa penalti alipoangushwa na Michael Brown ndani ya boksi lakini alipopiga tuta hilo likaenda nje.
Wigan yamchota Mchezaji wa Paraguay
Wigan imemsajili Beki wa Kimataifa wa Paraguay Antolin Alcaraz kutoka Klabu ya Ubelgiji Club Brugge na habari hizi zimethibitishwa na Meneja wa Wigan Roberto Martinez.
Alcaraz, miaka 27, amewahi kuchezea Klabu za Fiorentina ya Italia na SC Beira Mar ya Ureno.
Mchezaji huyo ambae ndie usajili wa kwanza wa Wigan kwa Msimu ujao atajiunga na Klabu yake mpya mara baada Fainali za Kombe la Dunia ambako Nchi yake Paraguay inashiriki.
Leonardo kutimka AC Milan
Bosi wa AC Milan Leonardo, ambae ni Staa wa zamani wa Brazil na alikuwemo Timu iliyotwaa Ubingwa wa Dunia 1994, ametangaza kuwa amekubaliana na Uongozi wa Klabu hiyo kuachia ngazi.
Leonardo, miaka 40, alipewa wadhifa wa Umeneja mwezi Mei mwaka jana alipoondoka Carlo Ancelotti kwenda Chelsea na kabla ya hapo alikuwa ni Mkurugenzi wa Ufundi Klabuni hapo.
Msimi huu ameiwezesha AC Milan kunyakua nafasi ya 3 ingawa Ligi inakwisha wikiendi hii kwa vile Timu ya 4, Sampdoria, wako nyuma yao kwa pointi 3 na tofauti ya magoli kwao ni kubwa mno hivyo Sampdoria hawawezi kuwashika.
Pia, AC Milan hawawezi kupanda nafasi ya pili kwa vile AS Roma wako mbele yao kwa pointi 10 na Inter Milan wako pointi 12 mbele.

Friday 14 May 2010

KWINGINEKO ULAYA: Kitimtim Italia, Spain wikiendi hii!!
Ligi za Ujerumani na England zilimalizika wikiendi iliyopita na wikiendi hii Ligi za Italia, Spain na Ufaransa zinafikia tamati.
Huko Ufaransa tayari Marseille wameutwaa Ubingwa wa Ligue 1 baada ya kuukosa tangu 1992 lakini huko Italia na Spain Bingwa bado hajapatikana na atajulikana baada ya mechi za mwisho wikiendi hii.
Ifuatayo ni hali halisi na jinsi kitimtim kilivyo:
LA LIGA: Nani Bingwa Barca au Real?
Ni Mabingwa Watetezi FC Barcelona au Real Madrid ndio watavikwa Ubingwa wikiendi hii ingawa Barcelona ndie mwenye nafasi kubwa kwa vile yuko pointi moja mbele ya Real Madrid na hata akifungwa mechi yake ya mwisho na Real kutoka sare, na hivyo Timu hizo kufungana pointi, bado Barca wana nafasi kwa sababu tu waliwafunga Real mechi zote mbili za La Liga Msimu huu.
Barca wako nyumbani Nou Camp kucheza na Valadolid ambao wako hatarini kuteremshwa Daraja na Real wako safarini nyumbani kwa Malaga ambao pia wako hatarini.
SWALI:
Je Barca watatwaa Ubingwa kwa mara ya 20 au Real ndio Bingwa kwa mara ya 32?
MSEMO:
“Nimefurahia Msimu huu! Ni kampeni bora lakini si lazima tuwe Mabingwa ingawa upo uwezekano!” Cristiano Ronaldo wa Real Madrid.
SERIE A: Inter mbioni kutwaa Mataji Matatu!!
Baada ya kunyakua Coppa Italia wiki iliyopita na kuwemo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI watakapoivaa Bayern Munich wiki ijayo, Jumapili Inter Milan, chini ya Kocha machachari na mwenye vituko, Jose Mourinho, wanaweza kutwaa Kombe lao la pili ikiwa wataifunga Siena, Timu ambayo tayari ishaporomoshwa toka Serie A,na kutwaa Ubingwa wa Serie A.
Lakini ikiwa Inter Milan watateleza na AS Roma kuifunga Chievo Verona basi AS Roma watatwaa Ubingwa wa Serie A.
MSEMO:
“Ni ngumu kuifikiria Siena wakati tuna Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI siku chache baadae! Nataka Wachezaji wangu wawe Mabingwa wa Ulaya!” Jose Mourinho, Meneja wa Inter Milan.
Kipa wa Man United njiani kwenda Birmingham
Birmingham wako mbioni kumsaini Kipa wa Akiba wa Manchester United Ben Foster na inasemekana Klabu hizo mbili zishakubaliana kuhusu uhamisho huo na kilichobaki ni Kipa huyo kukubaliana maslahi yake binafsi na Birmingham.
Birmingham wamelazimika kutafuta Kipa baada ya Kipa wao Nambari wani, Joe Hart, ambae alikuwa hapo kwa mkopo kutoka Manchester City, kumaliza Mkataba wa huo mkopo uliodumu hadi mwishoni mwa Msimu uliokwisha Jumapili iliyopita na hivyo kutakiwa kurudi Man City.
Ben Foster amekuwa akitaka kuondoka Man United kwa kukosa namba ya kudumu hapo na hilo limesababisha hata asichukuliwe Kikosi cha England cha Kombe la Dunia ingawa kawaida alikuwemo Kikosi cha England na badala yake amechukuliwa Joe Hart.
Wakala wa Foster, Lee Payne, amethibitisha kuwa wapo kwenye hatua za mwisho za majadiliano na Birmingham.
CAF yathibitisha Togo huru
CAF leo imetangaza rasmi kuifungulia Togo toka kifungo chake cha kutocheza Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 na 2014 kufuatia kujitoa Fainali za mashindano kama hayo yaliyofanyika Nchini Angola mwezi Januari baada ya Basi lao kushambuli kwa risasi na Waasi wa Jimbo la Angola la Cabinda na kumuua Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa Togo.
Kufunguliwa kwa Togo kunafuatia usuluhishi wa Sepp Blatter, Rais wa FIFA, ambae aliombwa na CAS [Court of Arbitration for Sports], Mahakama ya Usuluhisho kwa Michezo, kusuluhisha baada ya Togo kukata rufaa kwao.
Leo, CAF, baada ya Kikao cha Kamati Kuu yao huko Cairo, Misri, imetangaza rasmi kufunguliwa kwa Togo na kuthibitisha Togo watashirikishwa kwenye Mchujo wa kuingia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za Mwaka 2012 zitakazofanyika Nchini Gabon na Equtorial Guinea kwa pamoja.
FAINALI: Kesho Portsmouth v Chelsea
Jumamosi, Mei 15
Wembley Stadium, Saa 11 jioni, bongo taimu
HISTORIA:
Hii ni Fainali ya 129 ya Kombe la FA na hii ni mara ya kwanza kwa Chelsea na Portsmouth kukutana kwenye hatua hii ya Fainali ingawa zimewahi kucheza mara 3 kwenye hatua za awali za Kombe hili na kila Timu ilishinda mara moja na sare moja.
Chelsea ndio Mabingwa wa Ligi Kuu Msimu huu na Portsmouth ndio Timu iliyoshika mkia na hivi kuporomoshwa kucheza Daraja la chini Msimu ujao.
Portsmouth hawajahi kuwafunga Chelsea katika mechi zao 27 za mwisho walizocheza na mara ya mwisho kuwafunga Chelsea ilikuwa Desemba1960 Portsmouth waliposhinda 1-0.
Katika mechi hizo 27 tangu Portsmouth washinde, Chelsea wameshinda mechi 21 na sare 6.
Msimu huu kwenye Ligi Kuu, Chelsea waliibamiza Portsmouth bao 5-0 huko Fratton Park na kushinda mechi ya pili 2-0 Uwanjani Stamford Bridge.
Hii ni Fainali ya 10 kwa Chelsea na wameshinda 5 na kufungwa 4.
Kwa Portsmouth, itakuwa ni Fainali yao ya 5 na wameshinda mbili, mwaka 2008 walipoitoa Cardiff City na mwaka 1939 walipoibwaga Wolves, na zile walizopoteza ni mbili za mwaka 1934 walipocheza na Manchester City na mwaka 1929 walipoivaa Bolton.
Timu zote hizi Jezi zao za kawaida ni Bluu hivyo imeamuliwa kwenye Fainali ya kesho Chelsea watavaa Jezi za Bluu, juu na chini, na stokingi nyeupe na Portsmouth watavaa juu nyeupe na chini, bukta na stokingi, rangi ya kahawia.
NINI WANASEMA:
-Mchezaji wa Portsmouth, Tal Ben-Haim: “Sijapata kuona Mashabiki kama hawa ambao hata mkifungwa na kucheza vibaya na mabaya yote yaliyotukuta Msimu huu lakini wao wameendelea kuja kutushangilia! Kama tutaweza kuwafurahisha hiyo ni zawadi tosha kwao!”
-Nahodha wa Chelsea John Terry: “Hakuna kitu kitafuta majonzi yetu ya kufungwa Moscow na Man United na wao kutwaa UEFA CHAMPIONS LIGI labda tufanikiwe kutwaa Kombe hilo la Ulaya! Lakini tuna nafasi ya kuweka historia katika Historia ya Klabu hii kwa kutwaa Vikombe viwili Msimu mmoja-kile cha Ubingwa Ligi Kuu na FA Cup!”
VIKOSI VINAVYOTEGEMEWA:
Chelsea (Fomesheni, 4-3-3): Cech; Ivanovic, Alex, Terry, A Cole; Kalou, Ballack, Lampard; Malouda, Drogba, Anelka.
Portsmouth (Fomesheni, 4-5-1): James; Finnan, Mokoena, Rocha, Mullins; Boateng, Brown, Hughes Yebda, Dindane; Piquionne
Refa: Chris Foy
Marefa Wasaidizi: John Flynn na Shaun Procter-Green
Refa wa Akiba: Andre Marrrine
NJIA WALIYOFIKA FAINALI:
Chelsea
Raundi ya 3: Chelsea 5 Watford 0
Raundi ya 4: Preston 0 Chelsea 2
Raundi ya 5: Chelsea 4 Cardiff 1
Raundi ya 6: Chelsea 2 Stoke 0
Nusu Fainali: Aston Villa 0 Chelsea 3
Portsmouth
Raundi ya 3: Portsmouth 1 Coventry 1
Marudio Raundi ya 3: Coventry 1 Portsmouth 2 (Baada ya dakika 30 za nyongeza)
Raundi ya 4: Portsmouth 2 Sunderland 1
Raundi ya 5: Southampton 1 Portsmouth 4
Raundi ya 6: Portsmouth 2 Birmingham 0
Nusu Fainali: Portsmouth 2 Tottenham 0
WAFUNGAJI KOMBE LA FA:
Chelsea: Sturridge 4, Lampard 3, Malouda 2, Drogba 2, Anelka 1, Ballack 1, Kalou 1, Terry 1, Goli la kujifunga wenyewe 1.
Portsmouth: Piquionne 3, Boateng 2, Utaka 2, Belhadj 1, Dindane 1, Mokoena 1, O'Hara 1, Owusu-Abeyie 1, Goli la kujifunga wenyewe 1.
FIFA kupokea Maombi ya Uenyeji Kombe la Dunia 2018 & 2022 leo!!
  • 2018 WAOMBAJI: Australia, England, Ubelgiji na Uholanzi [Ubelgiji na Uholanzi zitaendesha Fainali kwa pamoja] Urusi, Spain na Ureno [Spain na Ureno zitaendesha Fainali kwa pamoja], USA [pia wameomba 2022].
  • 2022 WAOMBAJI: Japan, Korea ya Kusini, USA na Qatar.
Leo FIFA itapokea rasmi maombi ya Waombaji wa kuwa Wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 na 2022.
Fainali za mwaka 2014 tayari wameshapewa Brazil.
Fainali za 2010 zitaanza huko Afrika Kusini kuanzia Juni 11 hadi Julai 11.
Maombi ya England yatawasilishwa Makao Makuu ya FIFA huko Zurich, Uswisi na Supastaa David Beckham huku akibeba Buku lenye kurasa 1752 likichambua Maombi ya England.
Beckham amesema: “Tuna Viwanja vizuri, Viwanja vya Mazoezi bora, Usafiri na Mahoteli ya uhakika!”
Kila Nchi Mwombaji imetakiwa kuwasilisha Maombi yao yakichambua Miji na Viwanja vitakavyochezwa mechi, Miundombinu na Makaridio ya gharama za uendeshaji na mategemeo ya mapato.
Baada ya FIFA kupokea Maombi hayo watayachambua na kisha Wakaguzi watatembelea kila Nchi na kuwasilisha Ripoti zao kwa Kamati Kuu ya FIFA yenye Watu 24 ambayo ndio itaamua nani atakuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 na 2022.
Uamuzi huo unategemewa kutolewa Desemba 2, 2010.

Thursday 13 May 2010

Berbatov ajiuzulu Bulgaria, kuendelea Man United
Straika wa Manchester United Dimitar Berbatov amepuuza habari kuwa atahama Manchester United kabla Msimu ujao kuanza na badala yake amesema atabaki Klabuni hapo kupigania namba.
Berbartov, miaka 29, pia ametangaza kujiuzulu kuichezea Timu ya Taifa ya Nchi yake Bulgaria, yeye akiwa Nahodha, ambayo haikufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwezi ujao na ipo Kundi moja na England kwenye Mchujo wa EURO 2012.
Berbatov ametamka: “Siende popote, nipo Man United! Nimefika nilipopataka na hapa ni kileleni!”
Berbatov alijiunga na Man United mwaka 2008 kutoka Tottenham na katika mechi 65 alizocheza amefunga bao 26 lakini amekuwa akipondwa na baadhi ya Washabiki wa Klabu hiyo wakidai si mhangaikaji na anakosa bao nyingi.
Kuna vyanzo vya habari vimedai Berbatov atahamia Bayern Munich au AC Milan au hata kurudi Tottenham.
Lakini mwenyewe amedai: “Man United ni Klabu kubwa kabisa na ntapigana kubaki hadi Mkataba wangu uishe!”
Mkataba wa Berbatov unakwisha mwaka 2012.
Gallas mguu nje Ze Gunners
William Gallas, ambae Mkataba wake unakwisha kabla Msimu ujao kuanza, huenda asipate nyongeza ya Mkataba wake kufuatia kung’ang’ania kuongezwa Mshahara pamoja na nyongeza hiyo ya Mkataba ya mwaka mmoja.
Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood, amedai: “Tunataka abaki lakini madai yake ni makubwa mno na sisi hatuwezi kukubali. Ni Mchezaji mzuri lakini hatuna uwezo wa kumlipa zaidi. Akipata Klabu nyingine bora aende alipwe zaidi!”
FIFA yatangaza Wachezaji wa Timu zote Kombe la Dunia
FIFA imetoa majina ya Vikosi vya Awali vyaWachezaji 30 wa Nchi mbalimbali zitakazoshiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa huko Afrika Kusini kuanzia Juni 11 hadi Julai 11.
Kila Nchi inatakiwa iwasilishe Listi yao mwisho ya Wachezaji 23 hapo Juni 1.
Kuna baadhi ya Nchi hazikupeleka namba kamili ya Wachezaji 30 ya Vikosi vyao vya awali kama vile Ujerumani yenye Wachezaji 27, Mexico na Uruguay 26, Slovakia 29.
Lakini, Korea ya Kaskazini wao tayari washapeleka Kikosi chao cha mwisho cha Wachezaji 23.
Katika majina hayo yaliyopokelewa FIFA, Wachezaji Chipukizi kabisa ni Vincent Aboubakar wa Cameroun, Christian Eriksen wa Denmark na Nassim Ben Khalifa wa Uswisi na wote wana umri wa miaka18.
Wachezaji ‘Vinjeba’ ni Makipa wa Holland Sander Boschker na David James wa England na wote wana miaka 39.
Katika majina hayo huko FIFA, Wachezaji 139 wanacheza Soka lao England, 93 Italia, 94 Ujerumani, 74 Spain na 12 Scotland.
LISTI KAMILI YA FIFA BOFYA HAPA
Wenger aungama Difensi mbovu
Arsene Wenger amethibitisha atamnunua Difenda kabla Msimu mpya kuanza baada ya kukiri Difensi yake ilikuwa mbovu kwenye Msimu uliomalizika hivi karibuni.
Katika Misimu mitano sasa Arsenal imeambulia patupu bila ya kutwaa Kombe lolote na hilo limemfanya akiri kuwa ingawa Fowadi yake ni nzuri lakini ni Difensi ambayo ilifungwa mabao 41 kwenye Ligi Kuu iliyomalizika Jumapili iliyopita ndio iliyo wakosesha Vikombe.
Inasemekana Masentahafu wa Fulham, Brede Hangeland na Yule wa Senegal Pape Diakhate ndio analenga kuwanunua.
Pia, haja ya kununua Madifenda imeongezeka kwa vile Sol Campbell, Mikel Silvestre na William Gallas Mikataba yao inakwisha na bado haijazungumzwa kama itaongezwa au vipi.
Fergie asifu wasaidizi wake
Sir Alex Ferguson amewasifu na kuwashukuru Wasaidizi wake wote kwa kazi njema na msaada wao mkubwa kwa Msimu wote ulioisha Jumapili iliyopita ambao Manchester United walimudu kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, kutwaa Carling Cup na kufika hatua ya Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Ferguson alisema walikabiliwa na majeruhi kwa Wachezaji 16 wa Timu ya Kwanza na kukaa nje kwa zaidi ya Wiki 6 lakini Wasaidizi hao, wakiwemo wale wa Idara ya Matibabu, waliwahudumia vyema na kuhakikisha kila wakati wapo Wachezaji walio fiti kucheza.
Ferguson alisema: “Nasikia fahari kuwa na Wasaidizi hawa. Wale wa Matibabu walitoa huduma bora na wale Makocha walihakikisha Timu yeyote tunayoitupa Uwanjani imetayarishwa vyema!”
Kuna wakati, Difensi nzima ilikuwa majeruhi kuanzia Kipa Edwin van der Sar, Mabeki Garry Neville, Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Jonny Evans na Wes Brown na kubaki Beki mmoja tu, Patrice Evra, alie fiti na hivyo kulazimisha Viungo Darren Fletcher na Michael Carrick kucheza kama Masentahafu.
Sir Alex Ferguson anasaidiwa na Meneja Msaidizi Mike Phelan ambae aliwahi kuwa Mchezaji wa Man United aliponunuliwa mwaka 1989 kutoka Norwich City na alianza kazi hiyo ya Umeneja Msaidizi Septemba 2008.
Msaidizi mwingine wa Ferguson ni Kocha wa Timu ya Kwanza Rene Meulensteen kutoka Uholanzi aliechukua wadhifa huo Septemba 2008.
Timu ya Akiba, Rezevu, ipo chini ya Staa wa zamani Ole Gunnar Solksjaer.
Pichani Ferguson akiwa na Mike Phelan kulia kwake na Rene Meulensteen kushoto.
Ni Cardiff City au Blackpool kupanda LIGI KUU!!
Jana Cardiff City walifanikiwa kuwabwaga Leicester City licha ya kufungwa na hivyo kuingia Fainali kucheza na Blackpool hapo Mei 22 kuamua Timu ipi itaungana na Newcastle United na West Bromwich Albion kucheza Ligi Kuu Msimu ujao.
Katika mechi ya jana Cardiff City walifungwa 3-2 na Leicester City na kuifanya mechi iamuliwe kwa penalti kwa vile wao walishinda 1-0 kwenye mechi ya kwanza.
Katika mikwaju hiyo ya penalti Cardiff City walitoka kidedea kwa bao 4-3.
Atletico Bingwa!
Bao mbili toka kwa Diego Forlan zimewapa Atletico Madrid Ubingwa wa Kombe la Kwanza la EUROPA LIGI kwa kuwatoa Fulham kwa bao 2-1 katika mechi ilyoenda dakika 120 baada ya kuwa droo 1-1 katika 90 za kawaida.
Diego Forlan, Mchezaji wa zamani wa Manchester United, alifunga bao la kwanza kwa Atletico dakika ya 33 na Simon Davies akasawazisha dakika ya 37.
Ndipo katika kipindi cha pili cha nyongeza ya dakika 30, kwenye dakika ya 115, Diego Forlan akamalizia kazi nzuri ya mkwe wa Diego Maradona, Sergio Aguero, kwa kufunga bao la pili.
VIKOSI:
Atletico Madrid: De Gea, Ujfalusi, Perea, Dominguez, Antonio Lopez, Reyes, Paulo Assuncao, Raul Garcia, Simao, Forlan, Aguero.
AKIBA: Joel, Valera, Camacho, Jurado, Salvio, Juanito, Cabrera.
Fulham: Schwarzer, Baird, Hughes, Hangeland, Konchesky, Duff, Etuhu, Murphy, Davies, Gera, Zamora.
AKIBA: Zuberbuhler, Pantsil, Nevland, Riise, Dempsey, Greening, Dikgacoi.
REFA: Nicola Rizzoli (Italy)

Wednesday 12 May 2010

Meneja amwakia Capello, adai ni chuki kumwacha Kipa wake!
Bosi wa Blackburn Sam Allardyce amemshambulia Fabio Capello kwa kutomchagua Kipa wake Paul Robinson kwenye Timu ya England inayojitayarisha kwa Kombe la Dunia.
Robinson aliwahi kuwa Kipa nambari wani wa England kwa kipindi kirefu lakini hakuwemo kwenye Kikosi cha Wachezaji 30 alichokitangaza Capello hapo jana na badala yake kuna Makipa watatu ambao ni Robert Green wa West Ham, David James wa Portsmouth na Joe Hart wa Birmingham City [yupo kwa mkopo toka Man City].
Allardyce amelalamika: “Nimestushwa! Nadhani ni uamuzi mbovu! Ukiangalia fomu yake na Blackburn hakuna Kipa Bora England kama Robinson! Tizama ana rekodi ya kutofungwa goli katika mechi 13 za Ligi Kuu! Capello ameaahidi kuchagua Wachezaji kwa kuzingatia fomu zao sasa kutomchukua mtu bora hamna sababu labda ana chuki binafsi!”
Boateng ruksa kucheza Ghana
Ghana imetangaza kuwa imeruhusiwa kumchezesha Kombe la Dunia Kiungo Kevin Prince Boateng, miaka 23, ambae alizaliwa Ujerumani na kuzichezea Timu za Taifa za Vijana za Ujerumani.
Boateng, anaechezea Portsmouth, alitajwa kwenye Kikosi cha Wachezaji 30 na Kocha Milovan Rajevac ingawa bado walikuwa hawajaruhusiwa na FIFA kumchezesha Ghana kwa vile ni Raia wa Ujerumani.
Boateng, ambae Baba yake ni Mghana, aliamua miaka miwili iliyopita kuichezea Ghana.
Siku hizi FIFA imeondoa kile kikomo cha umri wa miaka 21 cha Wachezaji kuruhusiwa kubadili ‘Utaifa’ kwenye Soka ikiwa wameshachezea Timu za Vijana.
Fowler: ‘Rafa afunge virago Liverpool!!’
Staa wa zamani wa Liverpool, Robbie Fowler, amesema anaamini wakati umefika kwa Meneja wa Liverpool Rafael Benitez kuondoka Klabuni hapo.
Hatma ya Benitez imekuwa ya utata na mjadala mkubwa kwa Wadau wa Liverpool hasa baada ya Liverpool kumaliza Msimu huu wakiwa nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na hivyo kukosa kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Huku Wamiliki wa Klabu hiyo, Wamarekani George Gillet na Tom Hicks, wakihaha kila kukicha kutafuta mnunuzi wa Klabu hiyo, Liverpool imekumbwa na hali tata na Fowler, ambae alirudishwa kuichezea Liverpool na Benitez miaka minne iliyopita, anahisi sasa ni wakati muafaka kwa Benitez kung’oka.
Fowler amesema: “Ingawa moyo wangu ni mkunjufu kwa Rafa kwa kunirudisha kucheza Klabu ninayoipenda ukweli ni kwamba Liverpool ni Klabu kubwa na hakuna mtu mkubwa kupita Klabu!”
Fowler, ambae sasa anachezea Soka lake huko Australia na Timu ya Perth Glory, amesema ili Liverpool iwe na uwezo kutwaa Vikombe ni lazima mabadiliko yafanyike .
FAINALI: Fulham v Atletico Madrid
HSH Nordbank Arena, Hamburg, Ujerumani
SAA 3 DAKIKA 45 USIKU [Bongo Taimu]
Ni hatua ya kushangaza kwa Fulham leo kutinga Fainali ya EUROPA LIGI kwa kucheza na Atletico Madrid Uwanjani HSH Nordbank Arena Mjini Hamburg, Ujerumani.
Ni hatua ya kushangaza kwa vile hakuna alietegemea Fulham watafika Fainali kwa kuwabwaga Vigogo wa Italia Juventus, Mabingwa Watetezi wa UEFA CUP ambalo Msimu huu ndio linachezwa kwa mara ya kwanza kama EUROPA LIGI, Shakhtar Donetsk, na pia kuwasimamisha Hamburg kwenye Nusu Fainali wakati ilikuwa wazi kabisa Fainali hii itachezwa nyumbani kwa Hamburg Uwanja wa HSH Nordbank Arena.
Kwa kuipa Fulham mafanikio haya, Meneja wao Roy Hodgson, amepewa Tuzo ya Meneja Bora wa Msimu na LMA, Chama cha Mameneja wa Ligi hasa wakitambua Hodgson alitua katikati ya Msimu wa 2007/8 huku Timu ikiwa mkiani lakini akainusuru kushushwa Daraja.
Leo Fulham wanapambana na Timu yenye uzoefu kupita wao, Atletico Madrid iliyo chini ya Meneja Quique Sanchez Flores, ambayo ina Wachezaji mahiri kina Diego Forlan, Sergio Aguero na Jose Antonio Reyes.
Atletico Madrid hawajapata Vikombe vikubwa tangu washinde Ligi pamoja na Kombe la Mfalme huko kwao mwaka 1996 na mara ya mwisho kufanikiwa Ulaya ni mwaka 1962 walipotwaa Kombe la Washindi.
Kila Timu inategemewa kuwakilishwa na Mastaa wao huku Fulham wanategemewa kumchezesha Mfungaji wao mahiri Bobby Zamora akiwa amedungwa sindano ya maumivu na anategemewa kufanyiwa upasuaji mguu baada ya mechi hii ya Fainali na operesheni hiyo imemfanya akose kuitwa kwenye Kikosi cha England cha Kombe la Dunia.
Blackpool Fainali kuingia LIGI KUU
Blackpool, wakiwa ugenini Uwanja wa City, katika mechi ya marudiano, waliweza kuwafunga wenyeji wao Nottingham Forest bao 4-3 na kutinga Fainali ya kupata Timu moja itakayoungana na Newcastle United na West Bromwich Albion ambazo tayari zishapanda Daraja kuingia Ligi Kuu Msimu ujao.
Kwenye mechi ya kwanza, Blackpool walishinda 2-1 na hivyo wamefuzu kuingia Fainali kwa jumla ya bao 6-4.
Hapo jana, Mabao ya Forest yalifungwa na Earnshaw, dakika ya 66,7, Adebobala, 90 na yale ya Blackpool yalifungwa na Campbell, dakika ya 56, 76 na 79, na Dobbie, 72.
Blackpool watacheza Fainali na mshindi wa mechi ya leo kati ya Cardiff City na Leicester City.
Kwenye mechi ya kwanza Cardiff City walishinda bao 1-0 ugenini.
Ufaransa yawatupa nje Viera, Nasri & Benzema
Kocha wa Ufaransa, Raymond Domenech, ametangaza Kikosi chake cha awali cha Wachezaji 30 watakaojitayarisha kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini na Kikosi hicho kinabidi kipunguzwe na kuwasilishwa FIFA majina 23 tu ifikapo Juni 1.
Habari kubwa kuhusu Kikosi hicho ni kutemwa kwa Wachezaji Samir Nasri wa Arsenal, Patrick Viera wa Manchester City na Karim Benzema wa Real Madrid.
Vilevile, kivutio ni kuchaguliwa kwa Thierry Henry wa Barcelona na William Gallas wa Arsenal licha ya kuwa na Msimu wa kusuasua kwa Henry kupigwa benchi huko Barcelona kila mechi na Gallas kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Katika Fainali za Kombe la Dunia, Ufaransa wapo Kundi moja na Wenyeji Afrika Kusini, Mexico na Uruguay.
Kikosi kamili:
MAKIPA: Hugo Lloris (Olympique Lyon), Steve Mandanda(Olympique Marseille), Cedric Carrasso (Girondins Bordeaux), Mickael Landreau (Lille)
WALINZI: Bacary Sagna (Arsenal), Patrice Evra (Manchester United), William Gallas (Arsenal), Eric Abidal (Barcelona), Rod Fanni (Stade Rennes), Sebastien Squillaci (Sevilla), Adil Rami (Lille), Marc Planus (Girondins Bordeaux), Gael Clichy(Arsenal), Anthony Reveillere (Olympique Lyon)
VIUNGO: Lassana Diarra (Real Madrid), Alou Diarra(Girondins Bordeaux), Jeremy Toulalan (Olympique Lyon), Florent Malouda (Chelsea), Yoann Gourcuff (Girondins Bordeaux), Abou Diaby (Arsenal), Yann M'Vila (Stade Rennes)
MAFOWADI: Thierry Henry (Barcelona), Nicolas Anelka (Chelsea), Andre-Pierre Gignac (Toulouse), Franck Ribery (Bayern Munich), Sidney Govou (Olympique Lyon), Djibril Cisse (Panathinaikos), Hatem Ben Arfa (Olympique Marseille), Mathieu Valbuena (Olympique Marseille), Jimmy Briand (Stade Rennes)
McClaren Bosi mpya Wolfsburg
Kocha wa zamani wa England Steve McClaren amesaini Mkataba wa miaka miwili na Klabu ya Ujerumani VfL Wolfsburg mara tu baada ya kuiwezesha Klabu ya Uholanzi FC Twente kutwaa Ubingwa wa Uholanzi Msimu huu kwa mara ya kwanza katika miaka 45 ya historia yao.
McClaren, miaka 49, alitimuliwa kama Kocha wa England mwaka 2007 aliposhindwa kuipeleka England Fainali za EURO 2008.
Wolfsburg ndio walikuwa Mabingwa wa Ujerumani mwaka 2009 .
McClaren alikuwa Meneja Msaidizi huko Derby County na Manchester United, chini ya Sir Alex Ferguson, na kisha kuhamia Middlesbrough kama Meneja kamili na kuifanya Klabu hiyo inyakue Carling Cup mwaka 2004 na kuipeleka Fainali ya UEFA Cup mwaka 2006.
Alichaguliwa kama mrithi wa Kocha wa England, Sven-Goran Eriksson, Agosti 2006.
Rufaa ya Ribery yapangiwa tarehe
Fowadi wa Bayern Munich, Franck Ribery, atajua siku 4 kabla ya Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI kama ataweza kucheza Fainali hiyo itakayochezwa Mei 22 huko Santiago Bernabeau kati ya Timu yake, Bayern, na Inter Milan wakati CAS, Mahakama ya Usuluhishi Michezoni itakapokaa kujadili rufaa yake ya kufungiwa mechi 3 na UEFA itakaposikilizwa.
Ribery alitolewa kwa Kadi Nyekundu katika mechi ya Nusu Fainali na Lyon alipomchezea rafu Lisandro Lopez na baadae UEFA ikamwongezea adhabu kwa kumfungia mechi 3.
Bayern wakakata rufaa kwa UEFA ambao waliitupilia mbali rufaa hiyo na ndipo Bayern wakaamua kukata rufaa CAS ambao waitajadili na kutoa uamuzi Mei 18.

Tuesday 11 May 2010

Ronaldinho, Adriano nje Brazil!!
Dunga, Kocha wa Brazil, hakuwaita Wachezaji Ronaldinho na Adriano kwenye Kikosi chake cha Fainali za Kombe la Dunia alipoitaja Timu yake ambayo haikuleta maajabu yeyote kwa Wadau kwani amechukua Wachezaji walewale waliokuwa wakitegemewa.
Kikosi kamili:
MAKIPA: Julio Cesar (Inter Milan), Doni (AS Roma), Gomes (Tottenham Hotspur)
MABEKI: Maicon (Inter Milan), Daniel Alves (Barcelona), Michel Bastos (Olympique Lyon), Gilberto (Cruzeiro), Lucio (Inter Milan), Juan (AS Roma), Luisao (Benfica), Thiago Silva (AC Milan)
VIUNGO: Gilberto Silva (Panathinaikos), Felipe Melo (Fiorentina), Ramires (Benfica), Elano (Galatasaray), Kaka (Real Madrid), Julio Baptista (Roma), Kleberson (Flamengo), Josue (VfL Wolfsburg).
MASTRAIKA: Robinho (Santos), Luis Fabiano (Sevilla), Nilmar (Villarreal), Grafite (VfL Wolfsburg).
Fabio amrudisha kundini Carragher lakini Scholes agoma!!
Kocha wa England, Fabio Capello, leo ametoboa kuwa alijaribu kumshawishi Kiungo wa Manchester United Paul Scholes ili arudi tena kuichezea England aliyoistaafu mwaka 2004 lakini hakufanikiwa.
Capello alisema: "Ndio niliongea nae lakini akajibu hapana! Anapendelea zaidi kuwa na Familia yake! Lakini nilijaribu kumshawishi.”
Hata hivyo, Capello amefanikiwa kumrudisha kwenye Timu ya England Beki wa Liverpool, Jamie Carragher, aliestaafu mwaka 2007.
KESHO FAINALI: Fulham v Atletico Madrid
Uwanja wa HSH Nordbank Arena, Hamburg, Ujerumani
SAA 3 DAKIKA 45 USIKU [Bongo Taimu]


NJIA YA FAINALI KWA FULHAM
Kundi E
Fulham walianza Kundi hili kwa sare ya 1-1 na PFC CSKA Sofia na kisha kushinda 1-0 dhidi ya FC Basel.
Mechi iliyofuata AS Roma walifunga bao dakika za majeruhi na kufanya Fulham 1 AS Roma 1 lakini katika marudiano ya Timu hizi AS Roma ilitoka kidedea.
katika mechi iliyofuata Fulham waliibwaga CSKA bao 1-0 na ilibidi washinde mechi yao ya mwisho ya Kundi hili ili wasonge mbele na walimudu kuifunga FC Basel 3-2.
Raundi ya Timu 32
Fulham v FC Shakhtar Donetsk [Jumla ya Mabao 3-2]
Fulham walishinda mechi ya kwanza 2-1 na marudio ilikuwa sare 1-1.
Raundi ya Timu 16
Fulham v Juventus [Jumla ya Mabao 5-4]
Katika mechi ya kwanza huko Turin, Fulham walichapwa 3-1 na Juventus na kwenye mechi ya marudiano Uwanjani Craven Cottage, Fulham walijikuta wako nyuma kwa bao la David Trezeguet na kila mtu alijua Fulham wako nje.
Lakini, Juventus wakapata pigo pale Nahodha wao Fabio Cannavaro alipotolewa nje kwa Kadi Nyekundu na mabao kutoka kwa Bobby Zamora, Gera, bao mbili, na Clint Dempsey yaliwapa ushindi mnono wa bao 4-1 na kusonga mbele.
Robo Fainali
Fulham v VfL Wolfsburg [Jumla ya Mabao 3-1]
Fulham walishinda mechi zote mbili kwa bao 2-1 na 1-0 na walikuwa Mastraika wa Fulham, Damien Duff na Bobby Zamora, ndio Mashujaa kwa kufunga mabao hasa katika mechi ya pili ugenini Uwanjani VfL Wolfsburg Arena pale Bobby Zamora alipopachika bao pekee na la ushindi sekunde 25 tu tangu mechi ianze.
Nusu Fainali
Fulham v Hamburg [Jumla ya Mabao 2-1]
Uwanja wa Hamburg ndio ulipangwa kufanywa Fainali ya EUROPA LIGI, Uwanja wa HSH Nordbank Arena, na Wadau walitegemea Hamburg watajitutumua ili kucheza Fainali ‘homu graundi’ na kutwaa Kombe kilaini.
Lakini, Fulham walimudu kutoka sare 0-0 hapo Allianz Arena na kuitwanga Hamburg 2-1 huko Craven Cottage kwa bao za Simon Davies na Gera.
NJIA YA FAINALI KWA ATLETICO MADRID
UEFA CHAMPIONS LIGI Kundi D
Atletico Madrid walianzia kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI wakiwa Kundi moja na APOEL, FC Porto na Chelsea lakini walimaliza Kundi hili wakiwa nafasi ya 3 na kutupwa nje na kuchomekwa kwenye EUROPA LIGI.
Raundi ya Timu 32
Atletico Madrid v Galatasaray [Jumla ya Mabao 3-2]
Atletico walitoka sare na Galatasaray Uwanjani kwao Vicente Calderon ya 1-1 lakini katika mechi ya marudiano huko Uturuki, Diego Forlan alifunga bao la pili na la ushindi dakika ya 90 na kuwapa Atletico ushindi wa 2-1.
Raundi ya Timu 16
Atletico Madrid v Sporting Lisbon [Jumla ya Mabao 2-2, Atletico wasonga kwa mabao ya ugenini]
Baada ya sare ya 0-0 nyumbani, Sporting Lisbon na Atletico Madrid zilitoka sare 2-2 huko Ureno na kuifanya Atletico isonge kwa bao za ugenini.
Robo Fainali
Atletico Madrid v Valencia [Jumla ya Mabao 2-2, Atletico wasonga kwa mabao ya ugenini]
Kwa mara nyingine tena, Atletico Madrid walinufaika kwa mabao ya ugenini baada ya suluhu ya 0-0 nyumbani na 2-2 ugenini.
Nusu Fainali
Atletico Madrid v Liverpool [Jumla ya Mabao 2-2, Atletico wasonga kwa mabao ya ugenini]
Diego Forlan alifunga bao na kuwapa ushindi Atletico wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool na katika marudiano huko Anfield, Liverpool walishinda 2-1.
Huko Anfield, Liverpool walipata bao kupitia Alberto Aquilani na kufanya ngoma iende dakika 30 za nyongeza na katika kipindi hicho Yossi Benayoun aliifungia Liverpool bao la pili lakini alikuwa Diego Forlan tena aliefunga bao moja na kuiwezesha, kwa mara nyingine tena, Atletico isonge kwa bao la ugenini.
Capello atangaza Kikosi cha England cha Kombe la Dunia
Kocha wa England Fabio Capello amewatangaza Wachezaji 30 kikiwa ni Kikosi cha awali kitakachoingia kambini kujitayarisha na Fainali za Kombe la Dunia na baadae kupunguzwa hadi Wachezaji 23 watakaowasilishwa FIFA ifikapo Juni 1.
Katika majina hayo 30 yapo majina kadhaa yaliyowastukiza Wadau wakiwemo Adam Johnson na Michael Dawson , ambao hawajahi kuichezea England.
Pia yumo Beki Mkongwe wa Liverpool, Jamie Carragher, aliestaafu kuichezea England na Beki wa Tottenham, Ledley King, ambae huwa hawezi kucheza mechi mfululizo kwa kuwa ana matatatizo kwenye goti.
England itapiga Kambi ya mazoezi huko Austria ambako itakwenda Jumamosi na wanategemewa kucheza mechi mbili za kujipima nguvu, moja ikiwa Mei 24 watakapocheza na Mexico Uwanjani Wembley na nyingine na Japan itakayochezwa huko Graz, Austria.
MAKIPA: Joe Hart, David James, Robert Green.
WALINZI: Leighton Baines, Jamie Carragher, Ashley Cole, Michael Dawson, Rio Ferdinand, Glen Johnson, Ledley King, John Terry, Matthew Upson, Stephen Warnock.
VIUNGO: Gareth Barry, Michael Carrick, Joe Cole, Steven Gerrard, Tom Huddlestone, Adam Johnson, Frank Lampard, Aaron Lennon, James Milner, Scott Parker, Theo Walcott, Shaun Wright-Phillips.
MAFOWADI: Darren Bent, Peter Crouch, Jermain Defoe, Emile Heskey, Wayne Rooney.
Zola afukuzwa West Ham
West Ham imemtimua kazi ya Umeneja Gianfranco Zola baada ya kuitumikia Klabu hiyo tangu Septemba, 2008 alipochukua wadhifa huo kutoka kwa Alan Curbishley.
Katika Msimu wake wa kwanza na West Ham Zola aliweza kuifanya Timu hiyo imalize ikiwa nafasi ya 9 lakini Msimu huu wamefanya vibaya na kumaliza nafasi ya 17 wakiwa pointi 5 tu na nafasi moja tu juu ya Timu 3 za mkiani zilizoshushwa Daraja.
Mpaka sasa haijajulikana nani atachukua nafasi ya Zola ingawa wanatajwa kina Slaven Bilic, Kocha wa Croatia aliewahi kuichezea West Ham hapo nyuma, Bosi wa Portsmouth, Avram Grant na Kocha wa zamani wa Manchester City, Mark Hughes.
Zola amekuwa hana uhusiano mzuri na Wamiliki wapya wa West Ham, David Gold na David Sullivan, walioitwaa Klabu hiyo Januari mwaka huu.
Ancelotti ataka Chelsea itawale lakini................... Fergie adai: “TUTARUDI!”
Bosi waChelsea, Carlo Ancelotti, ana mipango kamambe ya kuwafanya Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu kwa Msimu wa 2009/10 wawe wanatawala Soka la England.
Ancelotti, miaka 50, amesema: “Ntakuwa hapa kwa muda mrefu na nategemea kushinda Ubingwa mara nyingi. Tuna Kikosi imara kwa mwaka ujao na mingine.”
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Chelsea, Ron Gourlay, amemuunga mkono Ancelotti na kusema: “Tuna Wachezaji 28 wenye umri wa wastani wa miaka 27 na hivyo si Wazee!”
Ancelotti ameongeza kuwa lengo lao kwa sasa ni kulitwaa Kombe la FA ambalo watacheza Fainali na Portsmouth Jumamosi Mei 15 Uwanjani Wembley.
Ancelotti pia amedai kuwa atafanya alichokifanya Meneja wa Chelsea wa zamani, Jose Mourinho, kwa kuchukua Ubingwa mara mbili mfululizo pale alipotwaa Taji la Ligi Kuu mwaka 2005 na 2006.
Ingawa Mourinho alichukua Mataji mawili mfululizo hakuwezi kuutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu na pia Kombe la FA katika Msimu mmoja kitu ambacho Ancelotti anaweza kukitimiza Msimu huu ikiwa watasishinda Portsmouth kwenye Fainali.
Wakati Chelsea wanajipongeza kwa Ubingwa, Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amedai wataibuka upya Msimu ujao na kuurudisha nyumbani Ubingwa wao.
Ferguson ametamka: “Ni lazima tutarudi tena Msimu ujao na kutwaa Ubingwa! Hii ni asili na tabia ya Manchester United! Tutalirudisha Taji kwenye sehemo inayostahili, sehemu bora Duniani!”
Hata hivyo, Ferguson aliwapongeza Chelsea na kusema wamestahili kuwa Mabingwa.
Ferguson amesema: “Hii ni Ligi ngumu Duniani! Kwa Carlo, namwambia hongera!”
Hodgson wa Fulham ateuliwa Bora na Wenzake
Roy Hodgson ameshinda Tuzo ya Meneja Bora wa Mwaka iliyotolewa na Chama cha Mameneja wa Ligi [LMA=League Managers Association] kwa kuiwezesha Klabu yake Fulham ishike nafasi ya 12 kwenye Ligi Kuu England na pia kuiingiza Fainali ya EUROPA LIGI ambapo Mei 12 watacheza na Atletico Madrid huko Hamburg, Ujerumani.
Harry Redknapp wa Tottenham ndie alienyakua Tuzo ya Meneja Bora wa Ligi Kuu, tuzo inayotolewa na Wadhamini wa Ligi Kuu Barclays.
Rooney ndie Mchezaji Bora Ligi Kuu
Straika wa Manchester United na England Wayne Rooney ametunukiwa Tuzo ya Barclays ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu.
Rooney alifunga goli 26 kwenye Ligi na Tuzo hii inafuatia Tuzo za PFA [Chama cha Wachezaji Soka wa Kulipwa] na ile ya Waandishi wa Soka.
Uteuzi wa Mchezaji Bora wa Barclays hufanywa na Jopo la Viongozi wa Vyama vya Soka, Waandishi na Mashabiki.
Wakati huohuo, Fabio Capello, Meneja wa England, amesema Rooney atakuwa fiti kwa ajili ya Kambi ya Timu hiyo itakayoanza Jumamosi huko Austria.
Capello anategemewa kukitangaza Kikosi cha awali cha Wachezaji 30 watakaoingia kambini leo Jumanne.
Rooney amekuwa akikumbwa na majeruhi mwishoni mwa Msimu huu uliokwisha Jumapili ya juzi na siku hiyo, akicheza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Klabu yake Manchester United ilipoifunga Stoke City bao 4-0, alilazimika kutoka nje baada ya kusikia maumivu.
Lakini Capello ameondoa wasiwasi kwa kusema Rooney atarudi uwanjani ndani ya wiki mbili.

Monday 10 May 2010

Ancelotti: ‘Kuifunga Man United kulitupa Ubingwa!’
Carlo Ancelotti amesema kuifunga Manchester United mara mbili kwenye Ligi Kuu Msimu huu ndio kumewapa Ubingwa ingawa kambi ya Man United bado inaamini mechi zote hizo mbili Chelsea walishinda kwa kubebwa na Marefa.
Chelsea imemaliza Msimu ikiwa pointi moja mbele ya Manchester United na kunyakua Ubingwa kwa mara ya kwanza tangu 2006.
Ingawa Chelsea inasemwa ina Wachezaji ‘Wazee’, Ancelotti amesema: “Hii Klabu inayo hatima nzuri muda ujao kwa sababu Wachezaji wetu si wazee!”
Evra ajuta!
Beki wa Manchester United Patrice Evra amebeba mzigo mkubwa wa majuto wa kuukosa Ubingwa baada ya Chelsea kuubeba hapo jana walipoitandika Wigan 8-0.
Evra ametamka: “Siku zote nimesema tusipochukua Ubingwa nakuwa nimeiangusha Man United! Hii ni mara ya kwanza sijachukua Ubingwa! Ndio kuwa wa pili ni nzuri lakini si stahili yetu!”
Evra ndie Mchezaji aliecheza mechi nyingi Manchester United Msimu huu kwa kucheza mechi 51.

Sunday 9 May 2010

Ze Bluzi BINGWA!!
Ni goli 8 na Ubingwa uko Stamford Bridge!!!
Mvua ya magoli ilishuka Stamford Bridge ya goli 8-0, hii ikiwa ni mara ya 4 Msimu huu kwa Chelsea kushusha kipigo cha aina hiyo Uwanjani kwao baada ya kushinda 7-0 mara 3 Msimu huu.
VIKOSI VILIKUWA:
Chelsea: Cech, Ivanovic, Alex, Terry, Ashley Cole, Lampard, Ballack, Malouda, Kalou, Drogba, Anelka.
Akiba: Hilario, Joe Cole, Zhirkov, Paulo Ferreira, Sturridge, Matic, Belletti.
Wigan: Pollitt, Melchiot, Gohouri, Caldwell, Figueroa, Boyce, McCarthy, Watson, Diame, N'Zogbia, Rodallega.
Akiba: Stojkovic, Thomas, Scharner, Scotland, Moses, Cywka, Mostoe.
Refa: Martin Atkinson
Zimebaki Siku 2 Capello kuitangaza England
Gumzo, mijadala na minong’ono ipo kila kona Wadau wakimsubiri Fabio Capello, Meneja wa England, kutangaza Kikosi cha awali cha England cha Wachezaji 30 ili hatimaye kipunguzwe na kuwakilishwa FIFA hapo Juni 1.
Capello anategemewa kuwatangaza Wachezaji hao 30 siku ya Jumanne na Kikosi hicho kitaruka kwenda Austria Jumamosi ijayo ili kupiga kambi ya mazoezi.
England itacheza mechi za kirafiki na Mexico Mei 25, Uwanjani Wembley, na Japan, huko Austria, Mei 30
Fergie: ‘Bado nipo labda afya igome!’
Sir Alex Ferguson amedai ni afya yake tu ndio itaamua kama atang’oka au la kama Meneja wa Manchester United.
Ferguson, miaka 68, yupo Old Trafford kwa miaka 24 na na bado ana njaa ya ushindi.
Mwenyewe anasema: “Sidhani nitabadilika kadri nnavyozeeka. Mie ni mtu yule yule. Ninachoomba ni afya yangu iendelee kuwa nzuri.”
Ferguson aliingia Man United Novemba 1986 na ilimchukua hadi 1990 ili kushinda Kombe lake la kwanza aliponyakua FA Cup lakini amekiri kuwa sasa ni vigumu Mameneja kupewa muda mrefu kama huo ili kuonyesha mafanikio.
Ferguson amelalamika: “Klabu nyingi hutafuta Meneja mwenye mafanikio lakini wakimchukua akikaa muda mfupi bila mafanikio huonekana si Meneja mwenye mafanikio tena!”
Fergie akaongeza: “Ni mchezo mbaya kabisa, utamaduni wa fani hii sasa ni mafanikio tu! Kama alivyosema Roberto Mancini, ukipoteza gemu tatu tu huko Italia, basi kazi huna!”
Ferguson akamalizia kwa kukumbusha jinsi walivyotimuliwa Peter Reid, Ruud Gullit na Bobby Robson wakati Msimu mpya umeanza tu na hata hawajapata muda wa kujenga Timu zao na kuponda hatua hii kwa kudai: “Ukifika hatua ya kufukuza Mameneja siku chache baada ya Msimu kuanza basi wewe hujui kabisa namna ya kuiendesha Klabu ya Soka!”
BINGWA NANI??????

Leo saa 12 jioni, saa za Bongo, Timu zote 20 za Ligi Kuu zitaingia Viwanja mbalimbali kucheza mechi zao za mwisho za Ligi Kuu Msimu wa 2009/10 lakini ni mechi mbili tu ndizo zenye msisimko mkubwa kwa vile zitaamua Bingwa nani.
=============================
RATIBA:
Jumapili, 9 Mei 2010
[saa 12 jioni]
Arsenal v Fulham
Aston Villa v Blackburn
Bolton v Birmingham
Burnley v Tottenham
Chelsea v Wigan
Everton v Portsmouth
Hull v Liverpool
Man United v Stoke
West Ham v Man City
Wolves v Sunderland
========================
Chelsea wakiwa pointi moja mbele ya Mabingwa Watetezi Manchester United watakuwa Mabingwa wapya leo wakiifunga Wigan Uwanjani Stamford Bridge na huu utakuwa ni Ubingwa wao wa kwanza tangu 2006.
Lakini Chelsea wakijikwaa tu na kutoka sare au kufungwa na Wigan na Manchester United wakiifunga Stoke City huko Old Trafford, Man United watakuwa Mabingwa kwa mara ya 4 mfululizo, ikiwa ni rekodi, na pia kwa mara ya 19, ikiwa pia ni rekodi ambayo sasa inashikiliwa na wao na Liverpool kwa pamoja kwa vile kila Klabu imchukua Ubingwa mara 18
Arsenal wataitwaa nafasi ya 3 wakiifunga Fulham huko Emirates lakini wakiteleza tu na Tottenham kuifunga Burnley basi Tottenham wataitwaa nafasi ya 3 na hii inamaanisha wataingia moja kwa moja hatua za makundi ya UEFA CHAMPIONS LIGI.
Timu inayoshika nafasi ya 4 inacheza pia UEFA CHAMPIONS LIGI lakini inaanza hatua za awali za Mchujo.
Wakati Bosi wa Chelsea Carlo Ancelotti amewaonya Wachezaji wake kutulia na kutokuwa na hofu, Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema ni upuuzi kutegemea msaada wa Chelsea ingawa ana mategemeo makubwa Wigan watajitahidi.
Wigan iliitandika Chelsea bao 3-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu na Bosi wa Wigan Roberto Martinez amesema wao watacheza Soka bora ili kulinda heshima ya Soka.
Ingawa wengi wanahisi mbali ya kitimtim cha nani Bingwa, Timu nyingine hazina kitu wanachogombea kwa vile pia Timu 4 za juu zitakazocheza UEFA CHAMPIONS LIGI [Chelsea, Man United, Arsenal na Tottenham] na zile zilizoshushwa [Hull City, Burnley na Portsmouth] tayari zishajulikana, lakini ukweli ni kuwa Timu ikipanda nafasi katika msimamo wa Ligi pia inajiongezea pato la Pauni 800,000 kwa kila nafasi nah ii ni sababu tosha kwa Timu kujikakamua leo.
MSIMAMO LIGI KUU:
[Kila Timu imecheza Mechi 37 na kubakisha moja]
1. Chelsea pointi 83===  KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
2. Man United pointi 82=KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
3. Arsenal pointi 72===  KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
4. Tottenham 70=====  KUCHEZA UEFA CHAMPIONS LIGI
--------------------------------------
5. Man City 66====EUROPA LIGI
6. Aston Villa 64==  EUROPA LIGI
7. Liverpool 62===  EUROPA LIGI
----------------------------------------------------
8. Everton 58
9. Birmingham 50
10.Stoke City 47
11.Blackburn 47
12.Fulham 46
13.Sunderland 44
14.Bolton 36
15.Wigan 36
16.Wolves 35
17.West Ham 34
----------------------------------------------------
18.Hull 29======= IMESHUSHWA DARAJA
19.Burnley 27==== IMESHUSHWA DARAJA
20.Portsmouth 19 = IMESHUSHWA DARAJA
KWINGINEKO ULAYA:
BUNDESLIGA: Bayern Munich Bingwa!!
Jana, rasmi Bayern Munich walitwaa Ubingwa wa Ujerumani walipoifunga ugenini Hertha Berlin, ambayo tayari ishashuka Daraja, kwa bao 3-1.
Huu ni Ubingwa wa 22 kwa Bayern Munich.
LA LIGA: Mgoma mgumu hadi Wikiendi ijayo!!
Huko Spain, Bingwa bado hajapatikana na atajulikana wikiendi ijayo kwenye mechi za mwisho za La Liga baada ya wagombea Ubingwa wawili, Real Madrid na Barcelona, kushinda mechi zao za jana.
Barcelona waliipiga Sevilla 3-2 na walimaliza mechi hiyo kwa hekaheka licha ya kuongoza kwa bao 3-0, kwa bao za Messi, Bojan na Pedrito, kwani Sevilla walipata bao mbili kupitia Kanoute na Luis Fabiano na kuufanya mwisho uwe mshikemshike.
Huko Santiago Bernabeau, Real Madrid waliishinda Athletic Bilbao 5-1 na kuwafanya wawe pointi moja nyuma ya Barcelona.
Real walipata bao la kwanza kwa penlti iliyomfanya Amorebieta wa Bilbao atolewe kwa Kadi Nyekundu na Cristiano Ronaldo kufunga.
Bilbao walisawazisha kupitia Yeste lakini kipindi cha pili Real waliangusha mvua ya magoli kupitia Gonzalo Higuain, Sergio Ramos, Karim Benzema na Marcello.
Mechi za mwisho, Barcelona wako nyumbani kuikaribisha Real Vallodolid na Real Madrid watakuwa ugenini kuikwaa Malaga.
Powered By Blogger