Wednesday 12 May 2010

Meneja amwakia Capello, adai ni chuki kumwacha Kipa wake!
Bosi wa Blackburn Sam Allardyce amemshambulia Fabio Capello kwa kutomchagua Kipa wake Paul Robinson kwenye Timu ya England inayojitayarisha kwa Kombe la Dunia.
Robinson aliwahi kuwa Kipa nambari wani wa England kwa kipindi kirefu lakini hakuwemo kwenye Kikosi cha Wachezaji 30 alichokitangaza Capello hapo jana na badala yake kuna Makipa watatu ambao ni Robert Green wa West Ham, David James wa Portsmouth na Joe Hart wa Birmingham City [yupo kwa mkopo toka Man City].
Allardyce amelalamika: “Nimestushwa! Nadhani ni uamuzi mbovu! Ukiangalia fomu yake na Blackburn hakuna Kipa Bora England kama Robinson! Tizama ana rekodi ya kutofungwa goli katika mechi 13 za Ligi Kuu! Capello ameaahidi kuchagua Wachezaji kwa kuzingatia fomu zao sasa kutomchukua mtu bora hamna sababu labda ana chuki binafsi!”
Boateng ruksa kucheza Ghana
Ghana imetangaza kuwa imeruhusiwa kumchezesha Kombe la Dunia Kiungo Kevin Prince Boateng, miaka 23, ambae alizaliwa Ujerumani na kuzichezea Timu za Taifa za Vijana za Ujerumani.
Boateng, anaechezea Portsmouth, alitajwa kwenye Kikosi cha Wachezaji 30 na Kocha Milovan Rajevac ingawa bado walikuwa hawajaruhusiwa na FIFA kumchezesha Ghana kwa vile ni Raia wa Ujerumani.
Boateng, ambae Baba yake ni Mghana, aliamua miaka miwili iliyopita kuichezea Ghana.
Siku hizi FIFA imeondoa kile kikomo cha umri wa miaka 21 cha Wachezaji kuruhusiwa kubadili ‘Utaifa’ kwenye Soka ikiwa wameshachezea Timu za Vijana.
Fowler: ‘Rafa afunge virago Liverpool!!’
Staa wa zamani wa Liverpool, Robbie Fowler, amesema anaamini wakati umefika kwa Meneja wa Liverpool Rafael Benitez kuondoka Klabuni hapo.
Hatma ya Benitez imekuwa ya utata na mjadala mkubwa kwa Wadau wa Liverpool hasa baada ya Liverpool kumaliza Msimu huu wakiwa nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na hivyo kukosa kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Huku Wamiliki wa Klabu hiyo, Wamarekani George Gillet na Tom Hicks, wakihaha kila kukicha kutafuta mnunuzi wa Klabu hiyo, Liverpool imekumbwa na hali tata na Fowler, ambae alirudishwa kuichezea Liverpool na Benitez miaka minne iliyopita, anahisi sasa ni wakati muafaka kwa Benitez kung’oka.
Fowler amesema: “Ingawa moyo wangu ni mkunjufu kwa Rafa kwa kunirudisha kucheza Klabu ninayoipenda ukweli ni kwamba Liverpool ni Klabu kubwa na hakuna mtu mkubwa kupita Klabu!”
Fowler, ambae sasa anachezea Soka lake huko Australia na Timu ya Perth Glory, amesema ili Liverpool iwe na uwezo kutwaa Vikombe ni lazima mabadiliko yafanyike .

No comments:

Powered By Blogger