Saturday, 17 January 2009
Manchester United, Mabingwa Watetezi wa LIGI KUU England, wakicheza ugenini na Bolton Wanderers walishinda kwa goli la dakika ya 90 lililofungwa na Dimitar Berbatov na kuwafanya waongoze kwa mara ya kwanza tangu msimu uanze.
Man U wako na pointi 47 kwa mechi 21 wakifuatiwa na Liverpool pointi 46 mechi 21 na watatu ni Chelsea pointi 45 mechi 22, Aston Villa pointi 44 mechi 22 na watano Arsenal pointi 41 mechi 22.
Liverpool anacheza Jumatatu saa 5 usiku [bongo taimu] na Watani wake wa jadi watoto wa mji mmoja Liverpool, Timu ya Everton na mechi hii haitabiriki.
Na hata Liverpool akishinda mechi hiyo atakuwa mbele ya Manchester United kwa sababu ya kucheza mechi moja mbele.
MATOKEO KAMILI:
Bolton 0 v Man U 1
Chelsea 2 v Stoke 1
Man City 1 v Wigan 0
Sunderland 1 v Aston Villa 2
West Brom 3 v Middlesbrough 0
Hull 1 v Arsenal 3
NI ZAIDI YA PAUNI MILIONI 100!!!
Nia ya Klabu ya Manchester City kutaka kumnunua Kaka kwa Pauni Milioni 100 na kumlipa Mshahara wa Pauni Laki 500 kwa wiki, zote zitakuwa ni rekodi za dunia kwa mbali kabisa, imewashangaza wadau wengi wa soka huko Ulaya.
Angalia watu muhimu wanavyochukulia taarifa hizo za uhamisho wa Kaka.
-Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson:
'Inakuwa ngumu kwangu kuelewa hilo! Inashangaza lakini soka ni soka na wakati mwingine unapata mistuko na maajabu na hili lazima limemshangaza kila mtu! Sidhani kama uhamisho huu utatudhuru sisi lakini hilo dau halieleweki!'
-Meneja wa Arsenal Arsene Wenger:
'Sijiskii wala sihisi kama Man City wako dunia hii kwa sababu sisi tuko kwenye klabu ya soka iliyo kwenye dunia ya kikweli. Uhamisho huu utaleta madhara makubwa kwenye soko la uhamisho wa Wachezaji. Utapandisha bei wakati kote duniani bei zinaporomoka! Sisi tupo kwenye dunia ya soka inayotegemea mapato yake yote kutoka kwa viingilio mlangoni, wadhamini wa matangazo na mapato kwenye matangazo ya TV!'
-Meneja wa AC Milan Carlo Ancelotti:
'Tegemeo langu ni kumfundisha Kaka kwa miaka mingi zaidi lakini lazima tukubali ukweli na tathmini iliyofanya AC Milan kwenye dau lilopendekezwa! Nadhani kuna makubaliano klabu itafanya pamoja na Kaka. Lakini nia yetu siku zote, tuwe na Kaka au tusiwe nae, ni kushindana na kushinda.'
-Alan Shearer, Mchezaji wa zamani wa England:
'Tunazungumzia Mchezaji Bora duniani lakini huwezi kuniambia yeye ana thamani hiyo! Dau hilo ni kitu hakijawahi kuonekana! Kwangu mimi, medali ni kitu muhimu kuliko pesa kwa Mchezaji!
Huwezi kuniambia Robinho ameenda Manchester City kupata medali kwani timu hiyo haiwezi kushinda chochote! Nadhani yuko huko kufuata pesa tu!!'
-Scolari wa Chelsea:
'Hii ni soka na Kaka ni Mchezaji wa kulipwa! Labda wanataka Man City iwe Klabu kubwa.'
-Clarence Seedorf, Mchezaji mwenzake Kaka huko AC Milan:
'Hilo dau ni kama sinema ya Hollywood! Pengine Man City wanatuma ujumbe kuionyesha dunia wanataka kuwa klabu kubwa duniani!'
-Rodney Marsh, Mchezaji staa wa zamani Man City:
'Inastusha! Ni dili kubwa sana, sana!! Lakini swali kubwa ni je hii itaisaidia Man City kuwa Timu bora LIGI KUU? Sidhani hata chembe!!!!'
SCOLARI: 'Ntawauza wote!!'
Meneja wa Chelsea Luiz Felipe Scolari amembwaga Didier Drogba nje ya kikosi chake kinachocheza leo nyumbani Stamford Bridge na Stoke City kwenye ya mechi ya LIGI KUU na pia kumwambia hata asikanyage uwanjani hapo.
Mbali ya kumtema Drogba kwa mechi mbili mfululizo ya kwanza ikiwa ile ya Jumatano Chelsea walipocheza ugenini na Southend na kushinda 4-1 katika mechi ya mashindano ya Kombe la FA, Scolari amewatisha Wachezaji wake wote na kuwaambia anaetaka kuhama hii ni nafasi yake kabla dirisha la uhamisho halijafungwa mwishoni mwa Januari.
Msimamo huu mkali wa Scolari unafuatia kipigo kitakatifu walichoangushiwa Chelsea Jumapili iliyopita na Mabingwa Manchester United waliposhindiliwa mabao 3-0.
Scolari alibwaka: 'Huu ni wakati wa kila Mchezaji kucheza kitimu, kwa moyo na mapenzi kwa Chelsea. Huwezi ondoka klabu, badilisha, nafasi iko wazi mpaka mwisho wa mwezi!'
Friday, 16 January 2009
BLACKBURN v NEWCASTLE
Mshambuliaji wa Blackburn Roque Santa Cruz na Kiungo David Dunn wanategemewa kuwa ulingoni baada ya kupona majeraha. Santa Cruz hajacheza mechi nne sasa na Dunn ameshakosa mechi mbili.
Meneja mpya wa Blackburn Sam Allardyce atakuwa akiomba alinde rekodi yake ya kutofungwa mechi 3 sasa tangu apate kazi ya Umeneja hapo na kesho anacheza dhidi ya timu iliyomfukuza kazi mwaka mmoja uliokwisha.
Blackburn wanategemea kuchezesha kikosi toka hawa: Robinson, Ooijer, Samba, Nelsen, Warnock, Emerton, Tugay, Mokoena, Andrews, Dunn, Pedersen, McCarthy, Santa Cruz, Derbyshire, Roberts, Brown, Khizanishvili, Treacy.
Meneja wa Newcastle Joe Kinnear ana mlolongo wa majeruhi.
Miongoni mwao ni Steven Taylor, Andy Carroll, Geremi, ambae inasemekana anahamia Besiktas ya Uturuki, Enrique, Joey Barton, Claudio Caçapa, Shola Ameobi, Obafemi Martins, Habib Beye na Alan Smith.
Timu ya Newcastle itatokana na: Given, Harper, Bassong, Coloccini, Taylor, Edgar, Kadar, Butt, Guthrie, N'Zogbia, Duff, Gutiérrez, Donaldson, Godsmark, Owen, Xisco, Carroll, LuaLua, Ranger.
BOLTON v MAN U
Bolton watawakosa Nahodha Kevin Nolan [adhabu ya kuwa na Kadi], Gavin McCann [majeruhi] na John Elmander [majeruhi].
Timu inategemewa kuwa: Jaaskelainen, Hunt, Shittu, Cahill, A O'Brien, Samuel, Riga, Muamba, Taylor, Davies, Gardner, Obadeyi, Bogdan, Smolarek, Fojut, Basham, Puygrenier.
Manchester United watawakosa Wayne Rooney, Patrice Evra na Rio Ferdinand.
Kikosi kitatokana na: Van der Sar, Kuszczak, Foster, Neville, Rafael, Vidic, Evans, Chester, O'Shea, Ronaldo, Nani, Scholes, Gibson, Anderson, Carrick, Fletcher, Giggs, Park, Berbatov, Tevez, Welbeck.
CHELSEA v STOKE CITY
Didier Drogba anarudi kundini baada ya kutemwa na Florent Malouda amepona ila Joe Cole na Deco wako nje baada ya kuumia.
Kikosi ni: Cech, Cudicini, Hilario, Ferreira, Bosingwa, Terry, Ivanovic, Alex, Carvalho, A Cole, Belletti, Lampard, Ballack, Mikel, Kalou, Stoch, Anelka, Drogba, Malouda, Di Santo, Mineiro, Mancienne.
Nao Stoke wana Mshambuliaji mpya James Beattie aliehamia hapo kutoka Sheffield United.
Beattie alishacheza LIGI KUU zamani alipokuwa na Southampton.
Mshambuliaji wao wa kawaida Ricardo Fuller amefungiwa baada ya kula Kadi Nyekundu pale alipomzaba kibao Nahodha wa timu yake Andy Griffins kwenye mechi waliyofungwa 2-1 na West Ham.
Kikosi: Sorensen, Griffin, Abdoulaye Faye, Shawcross, Higginbotham, Delap, Amdy Faye, Whelan, Diao, Etherington, Beattie, Cresswell, Kitson, Simonsen, Wilkinson, Olofinjana, Lawrence, Tonge, Sonko, Pugh.
HULL CITY v ARSENAL
Hull watakuwa na Mchezaji mpya Kevin Kilbane aliehamia kutoka Wigan na inawezekana pia Straika toka Angola Manucho aliejumuika hapo leo kutoka Manchester United kwa mkopo akacheza.
Hull watawakosa George Boateng [majeruhi], Kamil Zayate [adhabu] na Paul McShane alierudi Klabu yake Sunderland baada ya kumaliza mkataba wake wa kuchezea Hull kwa mkopo.
Kikosi: Myhill, Ricketts, Turner, Gardner, Dawson, Ashbee, Mendy, Barmby, Geovanni, Kilbane, King, Garcia, Fagan, Halmosi, Folan, Marney, Cousin, Manucho, Doyle, Giannakopoulos, Duke.
Arsenal watakuwa bila ya Song [ingawa anaweza kuonekana endapo atapasi testi ya kuwa fiti kabla ya mechi], William Gallas na Mikael Silvestre ikiwa pamoja majeruhi wa muda mrefu akina Eduardo, Fabregas na Rosicky.
Kikosi: Almunia, Sagna, Touré, Djourou, Clichy, Eboué, Diaby, Denilson, Nasri, Adebayor, Van Persie, Fabianski, Wilshere, Bischoff, Gibbs, Bendtner, Vela, Ramsey, Song.
MANCHESTER CITY v WIGAN
Man City watawakosa Stephen Ireland [Kadi] na Dietmar Hamann kwa kuwa majeruhi.
Kikosi: Hart, Schmeichel, Zabaleta, Onuoha, Richards, Dunne, Bridge, Ball, Ben Haim, Garrido, Wright-Phillips, Kompany, Fernandes, Elano, Robinho, Vassell, Jo, Caicedo, Sturridge, Berti.
Wigan wana kikosi kamili kitakachotokana na: Kirkland, Melchiot, Bramble, Scharner, Figueroa, Valencia, Cattermole, Palacios, Taylor, Heskey, Zaki, Boyce, Brown, Koumas, Edman, Camara, Pollitt, De Ridder, Kapo.
SUNDERLAND v ASTON VILLA
Sunderland watamkosa Kiungo Steed Malbranque kwani amefungiwa pamoja na majeruhi George McCartney na Craig Gordon.
Kikosi: Fulop, Colgan, Bardsley, Chimbonda, Ferdinand, Nosworth Collins, Whitehead, Richardson, Tainio, Leadbitter, Edwards, Miller, Yorke, Reid, Henderson, Diouf, Cissé, Jones, Murphy, Healy, Chopra.
Aston Villa wanamkaribisha tena Mshambuliaji hatari John Carew ingawa inasemekana nafasi yake kucheza mechi hii ni finyu.
Kikosi: Friedel, Guzan, Reo-Coker, Cuéllar, Laursen, Davies, Knight, L Young, Shorey, Milner, Petrov, Barry, Sidwell, A Young, Osbourne, Gardner, Salifou, Agbonlahor, Harewood, Delfouneso.
WEST BROMWICH v MIDDLESBROUGH
West Brom wana kikosi chao kamili: Carson, Kiely, Zuiverloon, Hoefkens, Olsson, Barnett, Donk, Robinson, Cech, Greening, Koren, Valero, Brunt, Teixeira, Kim, Dorrans, Simpson, Fortune, Moore, Beattie, Pele.
Na Middlesbrough nao hawana tatizo: Turnbull, Jones, McMahon, Bates, Riggott, Huth, Wheater, Taylor, Emnes, Tuncay, O'Neil, Arca, Digard, Johnson, Downing, Porritt, Alves, Mido.
-Benitez aukataa mkataba mpya Liverpool
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, ameukataa mkataba mpya ambao ungemweka Liverpool kwa miaka mitano zaidi kwa sababu haumpi uhuru na madaraka ya kuchukua Wachezaji anaowataka na badala yake madaraka na uamuzi wa mwisho unabaki kwa wamiliki wa Klabu hiyo ambao ni Wamarekani wawili waitwao Tom Hicks na George Gillette.
Benitez amekuwa Liverpool tangu Juni 2004.
-Manucho aenda Hull City kwa mkopo
Fowadi kutoka Angola Manucho ambae ni Mchezaji wa Manchester United ameenda Klabu ya Hull City kwa mkopo hadi msimu huu utakapoisha.
Msimu uliokwisha Manucho alikuwa Panathinaikos vilevile kwa mkopo na tangu arejee Manchester United amecheza mechi moja tu na uhamisho wake kwenda Hull City ni kumpa nafasi ya kupata uzoefu wa kucheza LIGI KUU kwani akibaki Man U ni vigumu kuwapiku akina Rooney, Berbatov na Tevez na kupata namba.
-Pennant njiani kuhamia Portsmouth
Winga Jermaine Pennant wa Liverpool ambae kwa sasa hana namba kwenye kikosi hicho yuko mbioni kuhamishiwa Portsmouth.
Pennant alijiunga na Liverpool Julai 2006 akitokea Arsenal na ameshaichezea Liverpool mechi 81 na sasa atajiunga na Timu inayoongozwa na Meneja Tony Adams ambae wanafahamiana tangu walipokuwa wote Arsenal wakati huo Tony Adams akiwa ndie Nahodha wa timu hiyo.
-Mukukula atua Bolton
Ariza Mukukula, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwa sasa ni raia wa Ureno, amehamia Bolton Wanderers kwa mkopo akitokea Klabu ya Ureno Benfica.
Mukukula, umri miaka 27, amekuwa hana namba ya kudumu hapo Benfica msimu huu na ameshawahi kuichezea Timu ya Taifa ya Ureno mara 4. Vilevile amewahi kushinda Kombe la UEFA mwaka 2006 alipokuwa akichezea Sevilla ya Spain.
-Rais wa Real Madrid Ramon Calderon ajiuzulu baada ya kugundulika aliiba kura za uchaguzi wake!!!!
Rais wa Klabu ya Spain Real Maldrid, Ramon Calderon, amelazimika leo kujiuzulu baada ya kugundulika aliiba kura wakati wa uchaguzi wa kuthibitisha nafasi yake kama Rais wa klabu hiyo hapo Desemba pale alipowapenyeza watu kumpigia kura wakati walikuwa hawana sifa za kupiga kura kufuatana na kanuni za klabu hiyo.
Baada ya kuibuka kashfa hiyo siku chache zilizopita, Calderon alijitetea hawajui watu hawo na akachukua hatua ya kumfukuza kazi Mkurugenzi aitwae Luis Barcena aliesimamia na kuendesha uchaguzi huo lakini Gazeti la Spain lenye kuaminika huko liitwalo Marca lilitoa picha zinazoonyesha baadhi ya wapigaji kura hao wasio halali wakiwa na Kaka wa Calderon aitwae Ignaciao na mtoto wa Calderon, Jamie.
Calderon alishinda Urais huo wa Real Madrid kwa kuahidi kuwanunua Wachezaji nyota Cristiano Ronaldo wa Manchester United, Fabregas wa Arsenal na Arjen Robben.
Mpaka sasa ameweza kutimiza ahadi ya kumchukua Robben tu na kushindwa kuwapata hao wengine wawili.
Hivi majuzi tu wakati Rais huyo wa Real Madrid akimtambulisha Mchezaji mpya toka Holland, Klaas-Jan Huntelaar, mashabiki waliojazana hapo walimpigia kelele na kumzomea Ramon Calderon: 'Yuko wapi Ronaldo!!!!'.
Thursday, 15 January 2009
-Man City waendelea kumsaka Kaka!
Klabu ya Manchester City kupitia Meneja wao Mark Hughes wamesema bado wana nia ya kumchukua staa wa Brazil Kaka kutoka AC Milan ya Italia na mazungumzo bado yanaendelea ingawa uamuzi haujafikiwa.
Inasemekana dau la kumuhamisha Kaka litazidi Pauni Milioni 100 na hii itakuwa rekodi ya dunia kwa uhamisho.
-Drogba bado anahitajika Chelsea
Meneja msaidizi wa Chelsea Ray Wilkins amesema Klabu ya Chelsea bado inamhitaji Didier Drogba na hatua ya kumtema jana kwenye kikosi kilichoenda kucheza mechi ya Kombe la FA na Southend ambako waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 ni uamuzi wa Meneja Luiz Felipe Scolari wa kubadilisha Wachezaji na wala si hatua ya kumwondoa Chelsea.
Hivi karibuni kumekuwa na tetesi nzito kwamba Drogba ataenda Italia kuungana na aliekuwa Meneja wa Chelsea Jose Mourinho ambae kwa sasa yuko Inter Milan.
-Wenger bado ana matumaini ya kumsaini Arshavin
Arsene Wenger wa Arsenal ametamka kuwa majadiliano bado yanaendelea na Klabu ya Kirusi Zenit St Petrsburg ya kumsaini nyota wa Urusi Andrei Arshavin.
Wenger alisema: 'Pengine si leo ila tunazungumza na ikiwezekana sawa isipowezekana basi! Hatuwezi kukiuka misimamo yetu!'
-Rooney nje wiki 3!!
Nyota wa Mabingwa Manchester United Wayne Rooney anategemewa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki kama 3 baada ya kuumia mara tu baada ya kufunga bao la ushindi kwenye mechi ya jana ya LIGI KUU dhidi ya Wigan iliyochezwa Old Trafford.
Rooney alifunga bao hilo kwenye sekunde ya 53 tu ya mchezo na akatoka nje ya uwanja dakika ya 6 tu ya mchezo.
Ikiwa atakuwa nje wiki hizo 3 basi Rooney atazikosa mechi zijazo dhidi ya Bolton [LIGI KUU], Derby [CARLING CUP], Tottenham [FA CUP], West Bromwich na Everton [zote za LIGI KUU].
MECHI ZIJAZO ZA LIGI KUU: [saa za kibongo]
Jumamosi, 17 Januari 2009
[saa 12 jioni]
Blackburn v Newcastle]
Bolton v Man U
Chelsea v Stoke
Man City v Wigan
Sunderland v Aston Villa
West Brom v Middlesbrough
[saa 2 na nusu usiku]
Hull v Arsenal
Jumapili, 18 Januari 2009
[saa 10 na nusu jioni]
West Ham v Fulham
Tottenham v Portsmouth
Jumatatu, 19 Januari 2009
[saa 5 usiku]
Liverpool v Everton
Mabingwa watetezi wa LIGI KUU England Manchester United wamewafunga Wigan goli 1-0 goli lililofungwa na Wayne Rooney sekunde ya 53 tu tangu mechi ianze baada ya pasi yenye akili toka kwa Mchezaji Bora Duniani Cristiano Ronaldo.
Rooney hakucheza muda mrefu baada ya hapo kwani alitolewa dakika ya 6 ya mchezo baada ya kupata maumivu.
Sasa Manchester United wako nafasi ya pili katika msimamo wa LIGI KUU England wakiwa na pointi 44 baada ya kucheza mechi 20.
Vinara Liverpool wana pointi 46 kwa mechi 21.
Timu ya tatu ni Chelsea wana pointi 42 kwa mechi 21 na Aston Villa ni wanne wakiwa na pointi 41 kwa mechi 21.
Arsenal ni wa tano wakiwa na pointi 38 kwa mechi 21.
Manchester United wanacheza ugenini na Bolton Wanderers siku ya Jumamosi inayokuja na endapo watashinda mechi hiyo watachukua uongozi wa LIGI KUU kwani Liverpool anacheza Jumatatu na watani wake wa jadi wenzake wa mji mmoja, mji wa Liverpool, Klabu iitwayo Everton.
Hii ni mechi isiyotabirika.
MATOKEO MECHI ZA FA CUP:
Southend 1 Chelsea 4
Newcastle 0 Hull City 1
Crystal Palace 2 Leicester 1
Wednesday, 14 January 2009
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, alietumia wiki yote iliyokwisha kwa kuishambulia Manchester United alipodai Sir Alex Ferguson 'anaua' Marefa na haadhibiwi na kisha kumrukia Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United David Gill ambae pia yuko kwenye Bodi ya FA, Chama cha Soka England, na kudai Manchester United wanamiliki kila kitu, amerudishwa tena hospitali kufanyiwa operesheni ya tatu ili kuondoa vijiwe kwenye figo zake.
Mwezi Desemba, 2008 alifanyiwa operesheni kwa tatizo hilohilo.
Baada ya kuanza kumshambulia Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson alijibu kwa ufupi na kusema: 'Ni upuuzi! Huyu ni mtu mwenye hasira! Nadhani kuna kitu kinamsumbua!'
David Gill, Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, akiwa ziarani Mashariki ya Mbali huko Macau, alijibu tuhuma za Benitez kwa kueleza: 'Kauli za Benitez hazina ukweli hata chembe! Ukweli ni kwamba kwenye Bodi ya FA kuna Wawakilishi Watatu wa Klabu za LIGI KUU-yuko Mwenyekiti Dave Richards, yupo Mwenyekiti wa Klabu ya Bolton Wanderers Phil Gartside na mimi. Sote tunachaguliwa kila mwaka na Klabu zote za LIGI KUU ikiwemo Liverpool! Mimi nipo Bodi hiyo huu ukiwa mwaka wa pili na nikiwa kule siwakilishi Manchester United bali Klabu zote za LIGI KUU!!'
Gill akamalizia: 'Ukitazama ukweli kuhusu maamuzi ya FA na kila kitu kinachoihusu Manchester United utaona hamna upendeleo na badala yake ni tofauti! Huyu anatushangaza wote!!'
Refa Howard Webb aomba msamaha kwa kusaidia kufunga goli!!
Refa Howard Webb [pichani] ambae sasa anasifika ndie bora na juzi Jumapili ndie aliechezesha 'BIGI MECHI' kati ya Manchester United na Chelsea ambapo Man U waliibuka kidedea kwa bao 3-0, jana alichezesha mechi ya Kombe la FA kati ya Birmingham na Wolves ambayo Wolves walishinda ugenini bao 2-0.
Lakini, Refa Howard Webb ilibidi aombe msamaha kwa Klabu ya Birmingham baada ya kutibua pasi ya Radhi Jaidi wa Birmingham iliyomgonga kwa bahati mbaya na kumkuta Mshambuliaji wa Wolves Andy Keogh aliempasia Sam Vokes aliepachika bao la pili.
Howard Webb alisikitika: 'Sikufurahia na niliwaomba msamaha Birmingham! Walinielewa!'
Sheria za Soka hazimlazimshi Refa kusimamisha mechi endapo mpira unamgusa.
Wataalam wachambua kipigo!!
Mourinho awaponda Chelsea!!!
Luiz Felipe Scolari, Meneja wa Chelsea, amekubali kubeba lawama za kufungwa 3-0 na Manchester United siku ya Jumapili lakini amedai watarudi tena wakiwa imara. Na ili kuonyesha nia yake kuibadili timu, amemtema Didier Drogba kwenye kikosi cha leo kinachorudiana na Southend kwenye mechi ya Kombe la FA watakayocheza na Southend ugenini baada ya kutoka sare ya 1-1 huko Stamford Bridge.
Amekiri alifanya kosa kwa kuifungua midifildi yake kwenye mechi na Manchester United pale alipoamua kumtoa nje Kiungo Deco wakati wa mapumziko na kumwingiza Anelka ambae ni Mshambuliaji ili aanze kipindi cha pili na kuifanya Chelsea icheze mfumo wa 4-4-2 badala ya 4-5-1 walioanza nao.
Lee Dixon, Beki wa zamani wa Arsenal, katika tathmini yake ya mechi hiyo ya Man U na Chelsea, amesema nguvu ya Chelsea ni kwenye Kiungo ambako siku hiyo waliaanza na mfumo wa 4-5-1 huku Mabeki wakiwa ni Bosingwa, Carvalho, Terry na Ashley Cole wakiwa ndio mstari wa mtu 4 nyuma wakifuatiwa na Viungo watano ambao walikuwa ni nanga Mikel Obi aliesimama katikati mbele ya Defensi hiyo ya watu wanne kisha Michael Ballack, Frank Lampard na Deco wakitawanyika mbele ya Obi huku Joe Cole akikamilisha idadi ya Viungo hao watano na ila alimiliki nafasi ya mbele zaidi ili kumpa sapoti Mshambuliaji pekee wa siku hiyo ambae ni Didier Drogba.
Ili mfumo huo wa 4-5-1 ufanye kazi yake vyema ilibidi Mabeki wa pembeni Bosingwa na Ashley Cole wapande pembeni kama Mawinga na kuongeza mashambulizi.
Wakati Chelsea walianza na 4-5-1, Manchester United walitumia 4-4-2 kwa mechi nzima.
Mabeki wao wanne wa nyuma walikuwa pembeni ni Neville na Evra na katikati Vidic na Evans.
Viungo wanne wa Man U walikuwa ni Ronaldo na Park, waliocheza pembeni kama Mawinga, na katikati Fletcher na Giggs.
Washambuliaji wawili ni Berbatov na Rooney.
Ingawa Rooney alikuwa ni Mshambuliaji anaemsaidia Berbatov yeye alipewa jukumu kubwa la kushuka kwenye kiungo hasa Chelsea wanapomiliki mpira ili kumkaba Kiungo wa Chelsea Obi asianzishe kilaini kujenga mashambulizi ya Chelsea.
Lee Dixon amechambua kwa kukiri kuwa Bosingwa na Cole walishindwa kupanda mbele kuongeza mashambulizi kwani Man United walihakikisha Ronaldo na Park, waliokuwa wakibadilishani wingi kila mara, wako huko kwenye wingi wakiendelea kushambulia.
Huo ukawa mwisho wa Cole na Bosingwa kwenda mbele kushambulia.
Dixon amesema kwa sababu Chelsea walikuwa na Mshambuliaji mmoja tu mbele, Drogba, ilikuwa rahisi kwa Mabeki wa Kati Vidic na Evans kummudu na vilevile wao kutoa pasi bila presha kwa Fletcher na Giggs kuanza mashambulizi.
Vilevile, Dixon akafafanua, kwa sababu Ashley Cole na Bosingwa walibanwa na kushindwa kupanda mbele kushambulia kwa sababu ilibidi wafanye kazi ya ziada ya kuwakaba Mawinga wa Man U, Ronaldo na Park, hilo lilitoa mwanya kwa Mabeki wa pembeni wa Man U, Evra na Neville, kupanda kirahisi kushambulia. Hili lilidhirika pale Ronaldo alipohadaa na kumpa pasi tamu Evra aliepanda kwenye kibendera cha kona na kuteremsha krosi safi iliyomaliziwa na Rooney na kuwa bao la pili.
Uwanjani hapo Old Trafford siku ya mechi hiyo kwenye jukwaa la Waheshimiwa walikuwa watu maarufu kadhaa wakiwemo Diego Maradona ambae ni Bosi wa Timu ya Taifa ya Argentina, Carlos Quieroz, aliekuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson na sasa ni Meneja wa Ureno, Fabio Capello wa England na Jose Mourinho, Meneja wa zamani wa Chelsea ambae sasa ni Meneja wa Inter Milan timu ambayo itapambana na Manchester United kwenye UEFA Champions League mwezi ujao.
Baada ya mechi Waandishi wakamzonga Jose Mourinho azungumzie mechi.
'Sikuwaona Chelsea' Alikebehi Jose Mourinho. 'Niliwaona watu kutoka Chelsea kabla ya mechi, kwenye mapumziko na mwisho wa mechi!! Ila sikuwaona Chelsea uwanjani, niliwaona Man U tu!'
Jumatano, 14 Januari 2009 [saa za bongo]
LIGI KUU England
Man U v Wigan [saa 5 usiku]
FA Cup [Marudiano]
Crystal Palace v Leicester [saa 5 usiku]
Newcastle v Hull [saa 4 dak 45 usiku]
Southend v Chelsea [saa 5 dak 10 usiku]
Matokeo mechi za jana za Kombe la FA
Birmingham 0-2 Wolverhampton
Bristol City 0-2 Portsmouth
Burnley 2-1 QPR [baada ya dakika za nyongeza 30]
Cheltenham 0-0 Doncaster
Crew 2-3 Millwall
Histon 1-2 Swansea
LeytonOrient 1-4 Sheffield United
Norwich 0-1 Charlton
Peterborough 0-2 West Brom
HABARI KWA UFUPI:
Evra kuwa nje kwa wiki 4!
Patrice Evra, beki mahiri wa Man u, atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki 3 au 4 baada ya kuumia mguu wakati akipiga krosi iliyomuunganisha Rooney aliefunga bao la pili katika ushindi wa 3-0 wa Man U dhidi ya Chelsea siku ya Jumapili iliyopita.
Man City wapo katika mazungumzo na AC Milan ili wamnunue Kaka!
Taarifa zisizothibitishwa zinadai Manchester City ipo mbioni kumnunua Kaka kutoka kwa AC Milan kwa kitita kitakachovunja kila aina ya rekodi. Inadaiwa dau la ununuzi ni Pauni Milioni 100 na Mshahara wake utakuwa Pauni Laki 5 kwa wiki!!
Mabingwa Watetezi wa Kombe la FA Portsmouth waingia Raundi ya 4!!
Bao tata la Straika Peter Crouch na lingine la Niko Kranjcar limeipa ushindi Portsmouth ambao ndio Mabingwa wa FA Cup msimu uliopita wa 2-0 hapo jana walipocheza na Timu ya Daraja la chini Bristol City.
Mkurugenzi Mtendaji wa Man U David Gill amkandya Benitez!!
Davidi Gill, Mkurugenzi Mtendaji wa Man U na ambae pia ni mmoja wa viongozi wa juu wa FA, ameziita kauli za Meneja wa Liverpool zilizohoji kuwepo kwake FA ni za kupotosha na kuficha ukweli.
Benitez alimkurupukia Gill mara tu baada ya kumwandama Sir Alex Ferguson ambae alijibu mapigo kwa mkato pale alipombandika jina la 'mpuuzi' Benitez.
David Gill amesema kuwapo kwake pale FA ni baada ya kuchaguliwa na Klabu zote za LIGI KUU na ndio taratibu za England za wao kusimamia masuala ya kibiashara na mapato huku Kamati mbalimbali zikiiendesha FA katika shughuli zake za kila siku na haziingiliwa hata chembe na wao.
David Gill yeye ni mmoja tu wa viongozi wa FA ambao wanatoka na waliwahi kutoka Klabu kadhaa za LIGI KUU.
Tuesday, 13 January 2009
Wakati Mchezaji nyota wa Liverpool, Fernando Torres anakiri Manchester United wana nafasi nzuri kutetea vyema taji lao la Ubingwa wa LIGI KUU England, Meneja wake Rafa Benitez ambae alimshambulia Sir Alex Ferguson hivi juzi tu, sasa ameelekeza mtutu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manchester United, David Gill, ambae pia ni mmoja wa viongozi wa FA, Chama cha Soka cha England.
Torres alikaririwa akisema: 'Man U wana nafasi kubwa, ni timu bora, ngumu na kwa miaka mingi wameonyesha wako madhubuti sana! Tena wana mechi mbili mkononi!'
Torres anakiri kuwa mechi kati ya Manchester United na Liverpool itakayochezwa Old Trafford Machi 14 ndio itatoa mwelekeo nani Bingwa.
Wakati huohuo, Meneja wake Rafa Benitez ameendelea kuishambulia Manchester United na safari hii amempiga kwanja mtendaji wa juu wa Klabu hiyo David Gill ambae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Man U na vilevile ana wadhifa kwenye FA kwa kuhoji kuweko kwake kwenye FA.
Ni kawaida kwa viongozi wa Klabu huko England vilevile kushika nyadhifa kwenye FA na hasa wakisimamia upande wa biashara, mapato na mgawanyo wa mapato hasa urushaji matangazo kwenye TV.
Kwa miaka kadhaa hapo nyuma, David Dean aliekuwa Makamu Mwenyekiti wa Arsenal alikuwa kiongozi wa juu huko FA.
Sir Alex Ferguson alijibu shutuma dhidi yake kwa kuziita ni upuuzi.
Stoke wamsaini James Beattie.
Timu ya Stoke City imemchukua Mshambuliaji James Beattie kutoka Timu ya Daraja la chini Sheffield United kwa dau la Pauni Milioni 3 na nusu na kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.
James Beattie, mwenye miaka 30, aliwahi kuchezea LIGI KUU akiwa na Timu ya Southampton.
Monday, 12 January 2009
Meneja wa Chelsea, Luis Felipe Scolari, amekiri kipigo cha 3-0 walichokipata Old Trafford kutoka kwa Mabingwa Manchester United kimewaumiza vibaya ingawa bado anadai lolote linaweza kutokea kwani wamebakiza mechi 17.
'Manchester United walikuwa bora kupita sisi!' Scolari alikiri 'Lakini sasa ni wakati wa kufikiria nini cha baadae, inabidi tujikaze kama wanaume na tuwe bora zaidi.'
Ferguson: 'Benitez ni mpuuzi!'
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amemwita Meneja wa Liverpool Rafa Benitez mpuuzi kufuatia tuhuma dhidi yake.
Ferguson, aliehojiwa jana na Waandishi wa Habari, hakutaka kuingia ndani juu ya tuhuma hizo na alijibu kifupi: 'Maneno yake yalikuwa na sumu kali! Lakini akikaa chini na kutafakari atajiona ni mpuuzi! Nadhani ni mtu mwenye hasira! Kuna kitu kinamsumbua!'
Wenger asikitishwa na mbinu za Timu za LIGI KUU
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, anakerwa sana na mbinu za Timu za LIGI KUU za kujihami kwa kupindukia.
Juzi Arsenal ilibidi wasubiri hadi dakika ya 84 ili wapate bao la ushindi lililofungwa na Bendtner dhidi ya Bolton waliocheza defensi ya watu 10 muda wote wa mchezo.
Wenger alisema: 'Miaka 10 iliyopita nilipofika hapa England kila timu ilicheza 4-4-2 lakini sasa ni timu chache sana zinakuja kucheza na Washambuliaji wawili! Kila timu inajihami na hata hao Manchester United wenye Washambuliaji hodari wanapata taabu kufunga! Lakini mbinu hizo za kujihami zitashindwa tu kwani sasa wanatufanya tutilie mkazo mbinu za kuwa na wepesi wa kubadili nafasi kwa haraka, ubunifu na kasi ya mchezo!'
Sunday, 11 January 2009
Chelsea walipata kipigo kitakatifu ndani ya Old Trafford baada ya kubamizwa magoli 3-0 na Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia Manchester United.
Kwenye mechi ambayo magazeti ya Uingereza yaliwekea bango kauli za ajabu za Meneja wa Liverpool Rafa Benitez za kumshambulia Sir Alex Ferguson ambae hakujibu chochote, sasa majibu yametoka Uwanjani!
Msimu wote huu Chelsea hawajahi kufungwa ugenini na leo kilikuwa kipigo chao cha kwanza.
Goli la kwanza la Man U lilifungwa na Vidic baada ya kona ya Giggs.
La pili alifunga Rooney kufuatia gonga murua kati ya Ronaldo na Evra kwenye wingi ya kushoto.
Berbatov alipachika bao la 3 kufuatia frikiki safi ya Ronaldo.
TIMU ZILIKUWA:
Man Utd: Van der Sar, Neville, Vidic, Evans, Evra (O'Shea 66), Ronaldo, Fletcher, Giggs (Carrick 79), Park, Berbatov, Rooney.
Akiba hawakucheza: Kuszczak, Anderson, Scholes, Welbeck, Tevez.
Kadi: Ronaldo, Rooney, Park.
Magoli: Vidic 45, Rooney 63, Berbatov 87.
Chelsea: Cech, Bosingwa (Belletti 64), Carvalho, Terry, Ashley Cole, Mikel, Joe Cole (Di Santo 85), Lampard, Ballack, Deco (Anelka 46), Drogba.
Akiba hawakucheza: Cudicini, Ivanovic, Ferreira, Kalou.
Kadi: Lampard, Bosingwa, Carvalho, Terry, Belletti.
Watazamaji: 75,455
Refa: Howard Webb
Wanaoongoza ligi, Liverpool jana walitoka suluhu ya 0-0 walipocheza ugenini na Stoke.
Nazo Timu zinazokamiani kuwania nafasi za Juu, Arsenal na Aston Villa waliibuka washindi katika mechi zao.
Arsenal, wakicheza nyumbani Uwanja wa Emirates, ilibidi wasubiri hadi dakika ya 84 ndipo Mshambuliaji wao Niklas Bendtner alipopachika bao lao moja la ushindi dhidi ya Bolton Wanderers.
Aston Villa waliwafunga West Bromwich Albion mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa Villa Park nyumbani kwa Aston Villa.
Matokeo mengine ni:
Everton 2 Hull o
Middlesbrough 1 Sunderland 1
Newcastle 2 West Ham 2
MECHI ZA LEO:
Wigan v Tottenham
Man U v Chelsea