Scolari akubali lawama za kubamizwa na Man U, amtema Drogba mechi ya leo!!
Wataalam wachambua kipigo!!
Mourinho awaponda Chelsea!!!
Luiz Felipe Scolari, Meneja wa Chelsea, amekubali kubeba lawama za kufungwa 3-0 na Manchester United siku ya Jumapili lakini amedai watarudi tena wakiwa imara. Na ili kuonyesha nia yake kuibadili timu, amemtema Didier Drogba kwenye kikosi cha leo kinachorudiana na Southend kwenye mechi ya Kombe la FA watakayocheza na Southend ugenini baada ya kutoka sare ya 1-1 huko Stamford Bridge.
Amekiri alifanya kosa kwa kuifungua midifildi yake kwenye mechi na Manchester United pale alipoamua kumtoa nje Kiungo Deco wakati wa mapumziko na kumwingiza Anelka ambae ni Mshambuliaji ili aanze kipindi cha pili na kuifanya Chelsea icheze mfumo wa 4-4-2 badala ya 4-5-1 walioanza nao.
Lee Dixon, Beki wa zamani wa Arsenal, katika tathmini yake ya mechi hiyo ya Man U na Chelsea, amesema nguvu ya Chelsea ni kwenye Kiungo ambako siku hiyo waliaanza na mfumo wa 4-5-1 huku Mabeki wakiwa ni Bosingwa, Carvalho, Terry na Ashley Cole wakiwa ndio mstari wa mtu 4 nyuma wakifuatiwa na Viungo watano ambao walikuwa ni nanga Mikel Obi aliesimama katikati mbele ya Defensi hiyo ya watu wanne kisha Michael Ballack, Frank Lampard na Deco wakitawanyika mbele ya Obi huku Joe Cole akikamilisha idadi ya Viungo hao watano na ila alimiliki nafasi ya mbele zaidi ili kumpa sapoti Mshambuliaji pekee wa siku hiyo ambae ni Didier Drogba.
Ili mfumo huo wa 4-5-1 ufanye kazi yake vyema ilibidi Mabeki wa pembeni Bosingwa na Ashley Cole wapande pembeni kama Mawinga na kuongeza mashambulizi.
Wakati Chelsea walianza na 4-5-1, Manchester United walitumia 4-4-2 kwa mechi nzima.
Mabeki wao wanne wa nyuma walikuwa pembeni ni Neville na Evra na katikati Vidic na Evans.
Viungo wanne wa Man U walikuwa ni Ronaldo na Park, waliocheza pembeni kama Mawinga, na katikati Fletcher na Giggs.
Washambuliaji wawili ni Berbatov na Rooney.
Ingawa Rooney alikuwa ni Mshambuliaji anaemsaidia Berbatov yeye alipewa jukumu kubwa la kushuka kwenye kiungo hasa Chelsea wanapomiliki mpira ili kumkaba Kiungo wa Chelsea Obi asianzishe kilaini kujenga mashambulizi ya Chelsea.
Lee Dixon amechambua kwa kukiri kuwa Bosingwa na Cole walishindwa kupanda mbele kuongeza mashambulizi kwani Man United walihakikisha Ronaldo na Park, waliokuwa wakibadilishani wingi kila mara, wako huko kwenye wingi wakiendelea kushambulia.
Huo ukawa mwisho wa Cole na Bosingwa kwenda mbele kushambulia.
Dixon amesema kwa sababu Chelsea walikuwa na Mshambuliaji mmoja tu mbele, Drogba, ilikuwa rahisi kwa Mabeki wa Kati Vidic na Evans kummudu na vilevile wao kutoa pasi bila presha kwa Fletcher na Giggs kuanza mashambulizi.
Vilevile, Dixon akafafanua, kwa sababu Ashley Cole na Bosingwa walibanwa na kushindwa kupanda mbele kushambulia kwa sababu ilibidi wafanye kazi ya ziada ya kuwakaba Mawinga wa Man U, Ronaldo na Park, hilo lilitoa mwanya kwa Mabeki wa pembeni wa Man U, Evra na Neville, kupanda kirahisi kushambulia. Hili lilidhirika pale Ronaldo alipohadaa na kumpa pasi tamu Evra aliepanda kwenye kibendera cha kona na kuteremsha krosi safi iliyomaliziwa na Rooney na kuwa bao la pili.
Uwanjani hapo Old Trafford siku ya mechi hiyo kwenye jukwaa la Waheshimiwa walikuwa watu maarufu kadhaa wakiwemo Diego Maradona ambae ni Bosi wa Timu ya Taifa ya Argentina, Carlos Quieroz, aliekuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson na sasa ni Meneja wa Ureno, Fabio Capello wa England na Jose Mourinho, Meneja wa zamani wa Chelsea ambae sasa ni Meneja wa Inter Milan timu ambayo itapambana na Manchester United kwenye UEFA Champions League mwezi ujao.
Baada ya mechi Waandishi wakamzonga Jose Mourinho azungumzie mechi.
'Sikuwaona Chelsea' Alikebehi Jose Mourinho. 'Niliwaona watu kutoka Chelsea kabla ya mechi, kwenye mapumziko na mwisho wa mechi!! Ila sikuwaona Chelsea uwanjani, niliwaona Man U tu!'
No comments:
Post a Comment