Saturday 10 January 2009

LIVERPOOL WAANZA KUWEWESEKA: Meneja Benitez ashangaza dunia kwa kumshambulia Ferguson!

Rafa Benitez ameushangaza ulimwengu wa soka kwa kumshambulia Sir Alex Ferguson na kumtuhumu anaua Marefa.
Meneja huyo wa Liverpool inasadikiwa ameanza kuonyesha dalili za kuchanganyikiwa kwa presha kali ya LIGI KUU England kwa kuingilia kitu ambacho wadau wanahisi hakikumhusu na kutoa maneno makali huku akinukuu vitu alivyoandika kwenye karatasi zake alizoshika mkononi kitu kinachoonyesha alikusudia.
Wiki iliyokwisha Sir Alex Ferguson alikaririwa akitoa tathmini ya Manchester United kwa mwaka 2008 na alisema kuwa timu yake iliathirika kwa kucheza mechi nyingi ugenini hasa baada ya kucheza mechi za UEFA CHAMPIONS LEAGUE nje ya nchi na kujikuta mechi zinazofuata ni za ugenini hasa na timu ngumu za LIGI KUU.
Ukweli ni kwamba Manchester United washacheza na Liverpool, Arsenal, Chelsea, Aston Villa na Everton mechi zote zikiwa ugenini na zote zilifuata baada ya kuwa nje ya nchi.
Timu hizo zote sasa zinatakiwa ziende nyumbani kwa Man U uwanjani Old Trafford.
Rafa Benitez alitoa msisitizo wa kauli zake za ajabu huku akinukuu vikaratasi vyake kwa kudai: 'Ferguson ni Meneja pekee anaua Marefa na haadhibiwi!'
Pengine ni dalili ya kuchanganyikiwa kwa Rafa Benitez kwani amesahau au hataki kukumbuka kwamba Sir Alex Ferguson alipigwa faini ya Pauni Elfu 10 na kufungiwa mechi 2 mwezi Novemba, 2008 kwa kulalamika kuhusu Refa Mike Dean.
Wadau wengi wa Soka England wanamkumbuka Kevin Keagan mwaka 1996, wakati huo akiwa Meneja wa Newcastle na wakati huo ulikuwa kipindi kama cha sasa na walikuwa wakiongoza LIGI KUU kwa pointi 14, akapanda jazba na kulipuka kama Benitez.
Mwisho wa msimu huo, Sir Alex Ferguson na Manchester United ndio waliokuwa Mabingwa!

Friday 9 January 2009

DEFOE ARUDI TENA TOTTENHAM

Jermaine Defoe amekamilisha taratibu zote za uhamisho toka Klabu yake Portsmouth na sasa yuko huru kuichezea Tottenham siku ya Jumapili dhidi ya Wigan kwenye pambano la LIGI KUU England.
Defoe alichezea Tottenham kati ya 2004 na 2008 na kuhama kwenda Portsmouth mwaka jana baada ya kuchukuliwa na aliekuwa Meneja wa Portsmouth wakati huo Harry Redknapp.
Akiwa na Tottenham, Defoe alicheza mechi 177 na kufunga mabao 64.
Kwa sasa Harry Redknapp ndie Meneja wa Tottenham na ndio maana imekuwa rahisi kwa Defoe kurudi tena hapo klabuni alipohama takriban mwaka mmoja ulioisha.


LIGI KUU ENGLAND: MECHI ZA WIKIENDI NA TAARIFA ZA WACHEZAJI

Beki wa Manchester United Patrice Evra amemaliza adhabu yake ya kifungo cha mechi nne na sasa anaweza kucheza kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Chelsea.
Evra alifungiwa baada ya kuhusika kwenye ugomvi uliotokea baada ya mechi ya Chelsea na Man U iliyochezwa Stamford Bridge mwezi Aprili.

Na nguzo kubwa ya Mabingwa Man U, Rio Ferdinand, amepona tatizo la mgongo na atakuwepo uwanjani Old Trafford Jumapili kuwakabili Chelsea.
Rio amekosa mechi 4 zilizopita za Man U.
Nae Kepteni wa Chelsea John Terry pamoja na mwenzie Michael Ballack wamemaliza adhabu zao baada ya kulimwa Kadi na wanaruhusiwa kucheza mechi hiyo ya Jumapili huko Old Trafford dhidi ya Mabingwa Man U.
Liverpool ambao ndio vinara wa LIGI KUU England wanamkaribisha uwanjani Straika wao mahiri Fernando Torres ambae hajacheza mechi ya LIGI KUU tangu Novemba baada ya kuwa majeruhi wakati Liverpool watakaposafiri kwenda kukutana na Stoke City siku ya Jumamosi.
Torres aliingizwa kipindi cha pili kwenye mechi ya FA Cup Jumamosi iliyopita wakati Liverpool waliwafunga Preston North End.
Mchezaji mwingine wa Liverpool Xabi Alonso huenda akaikosa mechi hiyo dhidi ya Stoke baada ya kuumia mguu.
Nao Arsenal wanaoshikilia nafasi ya 5 kwenye msimamo wa LIGI KUU itabidi wacheze mechi ya Jumamosi dhidi ya Bolton Wanderers uwanjani kwao Emirates bila ya Walinzi William Gallas na Mikael Silvestre kwani wote ni majeruhi.
Inategemewa majeruhi wengine Kiungo Denilson na Beki Kolo Toure huenda wakacheza baada ya kupata nafuu.

Thursday 8 January 2009

RUSHWA SOKA LA ITALIA: Bosi wa zamani wa Juventus jela miezi 18!!!

Meneja Mkuu wa zamani wa Klabu kongwe Italia Juventus, Luciano Moggi, amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela baada ya kupatikana na hatia ya rushwa iliyohusu upangaji matokeo wa mechi huko Italia.
Moggi alifungiwa kushiriki kwenye soka huko Italia mwaka 2006 kwa muda wa miaka mitano wakati huo akiwa tayari kiongozi wa Juventus kwa miaka 12.
Mtoto wa Luciano Moggi anaeitwa Alessandro nae amefungwa miezi 14 kuhusiana na kashfa hiyohiyo.
Juventus walivuliwa ubingwa mwaka 2005/6 na kushushwa daraja kuhusiana na kashfa hiyohiyo ya rushwa.
Kwa sasa Juventus wamesharudi daraja la juu liitwalo SERIE A huko Italia.

RATIBA LIGI KUU ENGLAND

Jumamosi, 10 Januari 2009
[saa 9 dak 45 mchana]

Aston Villa v West Brom

[saa 12 jioni]
Arsenal v Bolton
Everton v Hull
Fulham v Blackburn
Middlesbrough v Sunderland
Newcastle v West Ham
Portsmouth v Man City

[saa 2 na nusu usiku]
Stoke v Liverpool

Jumapili, 11 Januari 2009
[saa 10 na nusu jioni]

Wigan v Tottenham

[saa 1 moja usiku]

Man U v Chelsea

Jumatano, 14 January 2009
[saa 5 usiku]

Man U v Wigan

FERRARI YA RONALDO ILIVYOBAMIZWA!!
Cristaiano Ronaldo leo asubuhi akiwa njiani kwenda mazoezini alipata ajali wakati akiendesha gari lake la thamani aina ya Ferrari [pichani].
Ingawa yeye mwenyewe hakuumia gari lake hilo la kifahari limeharibiwa vibaya.
Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara ya chini ya ardhi inayopita chini ya Uwanja wa Ndege wa Manchester.
Wakati ajali hiyo ikitokea Mchezaji mwenzake wa Man U Kipa Edwin van der Sar alikuwa akija na gari lake nyuma yake nae pia alikuwa akienda mazoezini.
Polisi waliofika mara baada ya ajali walimpima Ronaldo kama alikuwa amelewa au la na walithibitisha vipimo havikuonyesha kama alikuwa na ulevi wa aina yeyote mwilini mwake.
Baadae, Ronaldo aliweza kushiriki mazoezi kama kawaida pamoja na wenzake.
Man U yafungwa na Derby kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali Carling Cup!!
Ronaldo apata ajali na gari lake la kifahari Ferrari, hakuumia ila gari nyang'anyang'a!
Ferguson adai watashinda mechi ya marudiano na Derby huko Old Trafford!!

Mabingwa Manchester United, wakichezesha kikosi hafifu kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Carling walipigwa bao 1-0 na timu hafifu na inayosuasua kwenye Ligi ya daraja la chini ya LIGI KUU, Derby County kwenye mechi iliyofanyika Pride Park uwanjani kwa Derby.
Timu hizi zitarudiana tarehe 20 Januari 2009 huko Old Trafford na mshindi atapambana na mshindi wa Nusu Fainali nyingine iliyochezwa juzi kati ya Tottenham na Burnsley ambako Tottenham alishinda 4-1 uwanjani kwake.
Marudiano kati ya Burnsley na Tottenham ni Januari 21.
Fainali ya Kombe la Carling ni tarehe 1 Machi 2009.
Wakati huohuo, nyota wa Man U, Cristiano Ronaldo, aligongesha gari lake la bei mbaya ya aina ya Ferrari kwenye ukuta wa pembeni wa daraja la chini ya ardhi lakini yeye hakujeruhiwa ila gari liliharibika vibaya.
Ajali hii ilitokea karibu na Uwanja wa Ndege wa Manchester.
Nae Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson amekiri timu yake ilicheza vibaya na ilistahili kufungwa ingawa amesema ni furaha kwao kufungwa goli moja tu kwani katika mechi ya marudiano kazi itakuwa laini kidogo kwani watachezea nyumbani kwao Old Trafford.

Wednesday 7 January 2009

CARLING CUP: Tottenham 4 Burnley 1

Tottenham jana waliikung'uta Burnley, timu ya Daraja dogo, mabao 4-1 katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling iliyochezwa White Hart Lane nyumbani kwa Tottenham.
Timu hizi zitarudiana Januari 21, nyumbani kwa Burnley.
Leo saa 4 dakika 45 usiku, saa za kibongo, Derby County wanawakaribisha Manchester United kwenye Nusu Fainali nyingine ya Kombe hili.
Mechi ya marudiano ya timu hizi itafanyika Januari 20 huko Old Trafford nyumbani kwa Manchester United.
Powered By Blogger