Friday, 9 January 2009

DEFOE ARUDI TENA TOTTENHAM

Jermaine Defoe amekamilisha taratibu zote za uhamisho toka Klabu yake Portsmouth na sasa yuko huru kuichezea Tottenham siku ya Jumapili dhidi ya Wigan kwenye pambano la LIGI KUU England.
Defoe alichezea Tottenham kati ya 2004 na 2008 na kuhama kwenda Portsmouth mwaka jana baada ya kuchukuliwa na aliekuwa Meneja wa Portsmouth wakati huo Harry Redknapp.
Akiwa na Tottenham, Defoe alicheza mechi 177 na kufunga mabao 64.
Kwa sasa Harry Redknapp ndie Meneja wa Tottenham na ndio maana imekuwa rahisi kwa Defoe kurudi tena hapo klabuni alipohama takriban mwaka mmoja ulioisha.


LIGI KUU ENGLAND: MECHI ZA WIKIENDI NA TAARIFA ZA WACHEZAJI

Beki wa Manchester United Patrice Evra amemaliza adhabu yake ya kifungo cha mechi nne na sasa anaweza kucheza kwenye mechi ya Jumapili dhidi ya Chelsea.
Evra alifungiwa baada ya kuhusika kwenye ugomvi uliotokea baada ya mechi ya Chelsea na Man U iliyochezwa Stamford Bridge mwezi Aprili.

Na nguzo kubwa ya Mabingwa Man U, Rio Ferdinand, amepona tatizo la mgongo na atakuwepo uwanjani Old Trafford Jumapili kuwakabili Chelsea.
Rio amekosa mechi 4 zilizopita za Man U.
Nae Kepteni wa Chelsea John Terry pamoja na mwenzie Michael Ballack wamemaliza adhabu zao baada ya kulimwa Kadi na wanaruhusiwa kucheza mechi hiyo ya Jumapili huko Old Trafford dhidi ya Mabingwa Man U.
Liverpool ambao ndio vinara wa LIGI KUU England wanamkaribisha uwanjani Straika wao mahiri Fernando Torres ambae hajacheza mechi ya LIGI KUU tangu Novemba baada ya kuwa majeruhi wakati Liverpool watakaposafiri kwenda kukutana na Stoke City siku ya Jumamosi.
Torres aliingizwa kipindi cha pili kwenye mechi ya FA Cup Jumamosi iliyopita wakati Liverpool waliwafunga Preston North End.
Mchezaji mwingine wa Liverpool Xabi Alonso huenda akaikosa mechi hiyo dhidi ya Stoke baada ya kuumia mguu.
Nao Arsenal wanaoshikilia nafasi ya 5 kwenye msimamo wa LIGI KUU itabidi wacheze mechi ya Jumamosi dhidi ya Bolton Wanderers uwanjani kwao Emirates bila ya Walinzi William Gallas na Mikael Silvestre kwani wote ni majeruhi.
Inategemewa majeruhi wengine Kiungo Denilson na Beki Kolo Toure huenda wakacheza baada ya kupata nafuu.

No comments:

Powered By Blogger