Saturday 22 May 2010

Blackpool yatinga LIGI KUU baada ya kupotea Miaka 39!!!!
Blackpool leo Uwanjani Wembley imekamilisha idadi ya Timu 3 zilizopanda Daraja kutoka Coca Cola Championship na kuingia Ligi Kuu baada ya kuifunga Cardiff City kwa bao 3-2 katika Fainali ya Mchujo maalum kuungana na Mabingwa wa Ligi hiyo, Newcastle, na Timu iliyoshika nafasi ya pili, West Bromwich Albion, kuingia Ligi Kuu Msimu ujao.
Timu za Newcastle na WBA zimepandishwa moja kwa moja na Timu zilizoshika nafasi ya 3 hadi ya 6 ndizo zilicheza Mchujo maalum.
Alikuwa ni Brett Ormerod aliewapandisha Daraja Blackpool baada ya kufunga bao la 3 dakika ya 46 ya Kipindi cha Kwanza.
Cardiff City ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kigongo cha Michael Chopra dakika ya 9 lakini Blackpool wakasawazisha kwa frikiki ya Charlie Adam kutoka umbali wa mita 25 kwenye dakika ya 13.
Joe Ledley akaifungia Cardiff bao la pili dakika ya 37 na dakika 4 baadae Blackpool wakasawazisha tena kupitia kichwa cha Gary Taylor-Fletcher.
Ndipo kwenye dakika za majeruhi za Kipindi cha Kwanza Brett Ormerod akafunga bao la 3 na la ushindi na kuirudisha Blackpool Ligi ya juu kabisa England baada ya kutokuwepo huko kwa Miaka 39
FAINALI: Nini cha kuangalia Leo!!!
Stadio Santiago Bernabeau

Inter Milan (Mabingwa Mara mbili: 1963/64 & 1964/65)
Inter Milan inaongozwa na Kocha machachari na mwenye majivuno, Jose Mourinho, ambae ameshawahi kutwaa Kombe hili akiwa na FC Porto Mwaka 2004.
Mfungaji Bora: Diego Milito [Argentina]
Mechi bora kwa Milito ilikuwa ni Nusu Fainali ya kwanza Inter walipoivaa Barcelona huko San Siro alipofunga bao la kwanza na kuzitengeneza bao mbili nyingine katika ushindi wa 3-1.
Milito ameshafunga bao 4 kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu.
Mchezaji anaeweza kuwika: Mario Balotelli [Italy]
Tineja huyu mara nyingi huonekana mapepe lakini akitulia ni Mchezaji hatari mno na mara nyingi Mourinho humwingiza toka Benchi kuchukua namba ya Samuel Eto’o au Milito.
Nguvu ya Inter: Mtu 4 za Difensi yao zenye uzoefu- Javier Zanetti, Maicon, Lucio & Walter Samuel
Bayern Munich (Mabingwa Mara 4: 1973/74, 1974/75, 1975/76 & 2000/01)
Bayern Munich iko chini ya Kocha toka Udachi, Louis van Gaal, ambae alikuwa Bosi wa Mourinho walipokuwa wote FC Barcellona kati ya Mwaka 1997 na 2000.
Mfungaji Bora: Ivica Olic [Croatia]
Ni mhangaikaji mkubwa uwanjani na ameshafunga bao 7 kwenye Kombe hili Msimu huu.
Mchezaji anaeweza kuwika: Arjen Robben [Udachi]
Amefunga bao 4 katika mechi zake 5 za mwisho za Kombe hili na hivyo Difensi ya Inter Milan itabidi imchunge.
Changamoto kwa Robben ni kufunga bao katika Uwanja wa Timu iliyo mkataa na kumtupa nje- Real Madrid.
Pigo kwa Bayern: Kumkosa Franck Ribbery
Ingawa Inter Milan nao watamkosa Thiago Motta aliefungiwa kama Frank Ribery lakini pengo kubwa inaelekea litakuwa kwa Bayern kwa vile Ribery ndie injini yao kubwa.
Rafa atetea rekodi yake Liverpool, ageuka Mhasibu!!
Rafael Benitez amejitetea kuhusu rekodi yake Klabuni Liverpool huku tetesi zikizidi kumwandama kuwa yuko mbioni kuihama Timu hiyo.
Benitez amehusishwa na kuhamia Klabu kadhaa ikiwemo Inter Milan ambayo Meneja wake Jose Mourinho anadaiwa atakwenda Real Madrid kwa Msimu ujao.
Ingawa mwenyewe Benitez anadai bado yuko na furaha kubakia Anfield lakini Wadau wanamkandya kufuatia Msimu mbovu waliomaliza wakiwa nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na hivyo kukosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Lakini Benitez bado anang’ang’ania utawala wake hapo Liverpool ni wa mafanikio na amesema: “Kuna hoja hatujashinda Vikombe vingi. Chelsea na Man United wameshinda Vikombe 10 kila mmoja katika miaka 6 nikiwa hapa Liverpool. Arsenal, Spurs na Portsmouth Kikombe kimoja moja tu. Liverpool wameshinda Vikombe Vinne na tumefika Fainali 3 nyingine!”
Benitez amepuuza hoja ya kuwa Liverpool yake haijachukua Ubingwa wa England kwa kudai hilo si lazima.
Vilevile, amedai Nchini England Mameneja wanakosa uwezo wa kuamua kuhusu Bajeti na ununuzi wa Wachezaji na hilo ndio jibu lake kwa tuhuma juu yake za kuwa katika wakati wake hapo Liverpool ametumia zaidi ya Pauni Milioni 280 kununua Wachezaji bila mafanikio ya kuwa Bingwa wa England.
Benitez anadai ametumia Pauni Milioni 220 tu lakini pia ameuza Wachezaji na kuingiza Pauni Milioni 160 na hivyo ni Pauni Milioni 60 tu ndizo alizotumia kununua Wachezaji katika Miaka yake 6 ya Umeneja hapo Anfield.
Anasema: “Ukichukua mapato tuliyovuna wakati tunacheza UEFA CHAMPIONS LIGI ya Pauni Milioni 120 katika kipindi hicho cha Miaka 6 ni wazi nimeleta faida ya Pauni Milioni 60!”
LEO NDIO LEO NDIO FAINALI!!!!
Mabaki ya Real yatua Real: Robben v Sneijder
Leo ni Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI inayochezwa Stadio Santiago Bernabeau, Uwanja maarufu wa Real Madrid, ambao walikuwa na ndoto kubwa yakucheza Fainali hii nyumbani kwao pale walipovunja Benki zote za Spain na kutumia zaidi ya Euro Milioni 200 kuwanunua Masupastaa Cristiano Ronaldo, Kaka, Xabi Alonso na Karim Benzema na kuwabwaga Wachezaji, miongoni mwa wengine, Arjen Robben na Wesley Sneijder.
Lakini leo si Real Madrid na Masupastaa wake ndio wako Fainali, leo ni Timu ya Bayern Munich ya Arjen Robben na Inter Milan ya Wesley Sneijder ndio wako Fainali nyumbani kwa Real Madrid.
Walipotimuliwa Real Madrid mwanzoni mwa Msimu uliokwisha juzi hakuna alieota ‘Takataka’ hizo za Real Madrid ndizo zitaongoza Timu zao kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI ndani ya Stadio Santiago Bernabeau.
Kwa namna moja au nyingine Sneijder na Robben, ambao wote ni Wadachi, ndio walioziongoza Timu zao na kuzifikisha Fainali.
Robben ndie aliefunga magoli muhimu katika mechi dhidi ya Fiorentina na Manchester United na kuhakikisha Bayern Munich inasonga mbele.
Sneijder ndie ‘akili’ ya Inter Milan kwa pasi zake na frikiki zake.
Robben amesema: “Mie na Sneijder tulitaka kubakia Real! Lakini ilibidi tuondoke. Ndoto ya Real ilikuwa kucheza Fainali hii Uwanjani kwao! Sisi tuliondoka, tumepata Klabu mpya na sasa tumerudi hapa tuko Fainali!”
Mshindi leo kuziiga Barca na Man United!!!
Katika Fainali ya leo ya UEFA CHAMPIONS LIGI, Mshindi kati ya Bayern Munich na Inter Milan atakuwa ameingia kwenye historia iliyowekwa na Klabu za Manchester United na FC Barcelona ya kutwaa Mataji Matatu kwa mpigo katika Msimu mmoja.
Mwaka 1999, Manchester United ilitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England, FA CUP na UEFA CHAMPIONS LIGI na Msimu uliokwisha FC Barcelona ilifanya hivyo kwa kushinda La Liga, Copa del Rey na UEFA CHAMPIONS LIGI.
Msimu huu, huko kwao, tayari Inter Milan na Bayern Munich zimeshatwaa Ubingwa wa Nchi zao na pia Vikombe vya Nchi zao na Timu yoyote ikishinda leo itakuwa inatwaa Taji la 3.
Makocha Mourinho na Van Gaal kuweka Historia!!!
Msisimko mwingine kwenye Fainali ya leo ni ule ukweli kuwa Makocha wote wa Inter Milan, Jose Mourinho, na wa Bayern Munich, Louis van Gaal, wameshawahi kushinda Kombe hili la UEFA CHAMPIONS LIGI wakiwa na Klabu nyingine.
Mourinho alitwaa Kombe hili Mwaka 2004 akiwa na FC Porto na Van Gaal alishinda Mwaka 1995 akiwa na Ajax.
Kocha atakaeshinda leo ataingia kwenye ile Orodha iliyotukuka ya Makocha walioshinda Kombe hili wakiwa na Vilabu tofauti ambayo kwa sasa wamo Ottmar Hitzfield [Akiwa na Borrussia Dortmund Mwaka 1997 na Bayern Munich Mwaka 2001] na Ernst Happel [Feyenoord Mwaka 1970 na Hamburg Mwaka 1983].
Chamakh rasmi Ze Gunners
Arsenal wamethibitisha kumsaini Mchezaji wa Kimataifa kutoka Morocco, Marouane Chamakh, ambae ni Mchezaji huru baada ya Mkataba wake na Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa kumalizika.
Wenger amesema: “Tuna furaha kumchukua. Ni Mchezaji tuliekuwa tukimtaka kwa muda mrefu.”
Mwenyewe Chamakh, miaka 26, amesema: “Hii ni ndoto yangu. Lengo langu lilikuwa kucheza Ligi Kuu na Arsenal ni chaguo langu!”

Friday 21 May 2010

Ze Gunners hawajateta na Barca kuhusu Fabregas
Arsenal wametamka hawajazungumza lolote na Barcelona kuhusu uhamisho wa Nahodha wao Cesc Fabregas ambae yuko kambini na Timu ya Spain iliyo kwenye matayarisho ya Kombe la Dunia.
Wiki hii kumekuwa na taarifa kuwa Barcelona, ambao wamekuwa wakimwinda Fabregas kwa muda mrefu, wameongeza kasi baada ya kuripotiwa Fabregas mwenyewe amemjulisha Wenger nia yake ya kuhamia Barcelona.
Mchezaji huyo mwenye miaka 23 alianza Soka lake na Timu za Vijana huko Nou Camp na kuhamia Arsenal akiwa tineja ambako kipaji chake kiliongezeka maradufu chini ya Wenger.
Lakini, kufuatia Msimu mwingine tena ambao Ze Gunners wametoka kapa, inadaiwa Fabregas amechoshwa na anataka kuhama huku kukiwa na ripoti kuwa Arsenal watamruhusu ikiwa Barcelona watatoa Pauni Milioni 39.
Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood, ameeleza wao hawajasikia chochote toka Barcelona.
Fergie: Berbatov si biashara!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesisitiza Klabu yao haina nia ya kumuuza Straika Dimitar Berbatov kama inavyovumishwa na Vyombo vya Habari.
Ferguson ametamka: “Hapana hauzwi! Ni Mchezaji mzuri sana na atakuwa nasi Msimu ujao.”
Ferguson amesema tetesi zinazozagaa kila siku ni tatizo kwa Klabu kubwa kama yao kwa vile Wadau wana matarajio mengi na Vyombo vya Habari siku zote vinawakazia macho.
Binafsi, Berbatov ameshatamka yeye atabaki Manchester United na kupigania namba yake kwa vile kuna uwezekano mkubwa Man United ikaongeza Straika mmoja.
MECHI YA PAUNI MILIONI 90: Blackpool v Cardiff City
Kesho Uwanjani Wembley zitashuka Timu mbili za Daraja la Coca Cola Championship, Blackpool na Cardiff City, ambazo ndizo ziko Fainali ya Mchujo maalum kupata Timu moja itakayoungana na Newcastle United na West Bromwich Albion kucheza Ligi Kuu England Msimu ujao.
Newcastle na WBA zilimaliza Ligi ya Coca Cola Championship zikiwa nafasi za kwanza na za pili na hivyo kuingia Ligi Kuu moja kwa moja lakini Timu za nafasi za 3 hadi za 6, yaani Blackpool, Cardiff, Leicester na Nottingham Forest, zilicheza Mchujo maalum na Blackpool na Cardiff ndizo zimetinga Fainali.
Blackpool waliwatoa Nottingham kwa jumla ya bao 6-4 katika mechi mbli na Cardiff waliwabwaga Leicester kwa penalti 4-3 baada ya mechi mbili kwisha kwa sare ya jumla ya bao 3-3.
Fainali hii ya Blackpool v Cardiff City imebatizwa ‘Mechi ya Pauni Milioni 90’ kwa vile Mshindi, yaani Timu itakayopanda Daraja kuingia Ligi Kuu itavuna kitita hicho kama mapato ya kucheza Ligi Kuu.
Mara ya mwisho Blackpool kucheza Ligi ya juu kabisa England ilikuwa Mwaka 1971 ilipocheza Divisheni ya Kwanza.
Na Cardiff nao hawajacheza Ligi ya juu ya England tangu walipocheza Divisheni ya Kwanza Mwaka 1962.
Newcastle, WBA na Mshindi kati ya Cardiff na Blackpool zitachukua nafasi za Burnley, Hull City na Portsmouth zilizoporomka Daraja toka Ligi Kuu.
FAINALI: Bayern Munich v Inter Milan
Santiago Bernabéu, Madrid, Spain
Muda: Jumamosi, Mei 22 saa 3 dakika 45 usiku
Wakati Bayern Munich wanasaka Taji lao la 5 la Ulaya, Inter Milan wanatafuta Taji lao la kwanza la Ulaya katika Miaka 45.
Msimu huu, kwenye michuano hii ya UEFA CHAMPIONS LIGI, Bayern Munich tayari wameshazifunga Timu mbili za Italia, Juventus na Fiorentina.
Washindani hawa wanaongozwa na Makocha Stadi huko Ulaya ambao wakati mmoja waliwahi kuwa pamoja.
Kocha machachari na mwenye vituko wa Inter Milan, Jose Mourinho, aliwahi kuwa Msaidizi wa Kocha wa Bayern Munich Louis van Gaal huko Barcelona kati ya Mwaka 1997 na 2000.
Makocha wote hao wawili wameshawahi kulitwaa Kombe hili la UEFA na yeyote atakaeshinda atakuwa ameingia kwenye kile Kitabu maalum cha kulishinda Kombe hilo wakiwa na Vilabu tofauti.
Inter Milan na Bayern Munich zimeshakutana mara 4 huko Ulaya na mara ya mwisho ilikuwa ni Msimu wa 2006/7 kwenye Makundi ya UEFA CHAMPIONS LIGI walipotoka sare 1-1 huko Munich kwa bao la dakika za mwishini la Patrick Viera kuiokoa Inter.
Katika mechi ya kwanza Msimu huo, Bayern ilishinda 2-0.
Mwaka 1988/9, katika Kombe la UEFA, Inter waliifunga Bayern 2-0 huko Ujerumani lakini Bayern wakaipiga Inter 3-1 huko Italia na kusonga kwa mabao ya ugenini.
Katika Fainali za Ulaya, rekodi ya Bayern ni ushindi mara 4 na kufungwa 3.
Walishinda Fainali hizo dhidi ya: Atletico Madrid [1974], Leeds United [1975], St-Etienne [1976], Valencia [2001].
Walifungwa: Aston Villa [1982], FC Porto [1987], Manchester United [1999].
Bayern Munich pia wameshashinda Ulaya Makombe mengine ikiwa Mwaka 1967 Kombe la Washindi la UEFA na Mwaka 1996 UEFA CUP.
Inter Milan watakuwa wakiomba washinde Kombe lao la kwanza Ulaya tangu waifunge Benfica Mwaka 1964.
Lakini, Mwaka 1967 walifungwa na Celtic na 1972 walitolewa na Ajax.
Inter wameshashiriki Fainali 4 za UEFA CUP na kushinda za Miaka ya 1991, 1994 na 1998 na kufungwa ile ya Mwaka 1997.
MASTAA NJE
Timu zote, Inter na Bayern, zitawakosa Wachezaji wao muhimu ambao wanatumikia kifungo baada ya kulambwa Kadi.
Inter watamkosa Thiago Motta na Bayern hawatakuwa na Mfaransa Franck Ribery waliediriki kukata Rufaa hadi CAS, Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, ambako Rufaa hiyo ilibwagwa.
REKODI
Ikiwa Bayern Munich watatwaa Kombe, watajumuika na Liverpool kwa kulitwaa mara 5 na kufungana pamoja kwa kuwa Timu za 3 nyuma ya AC Milan waliotwaa mara 7 na vinara Real Madrid walioshinda mara 9.
Vikosi vinavyotegemewa:
Bayern Munich: (Fomesheni 4-4-2) Butt; Lahm, Badstuber, Van Buyten, Contento; Altintop, Van Bommel, Schweinsteiger, Robben; Olic, Muller.
Inter Milan: (Fomesheni 4-2-3-1) Cesar; Maicon, Lucio, Samuel, Zanetti; Cambiasso, Pandev; Eto’o, Sneijder, Chivu; Milito.
Refa: Howard Webb (England).
Maradona amsaga na Gari Mpigapicha
Kocha wa Argentina Diego Maradona ameelezwa kuwa alimtukana Mpigapicha mara baada ya kuukanyaga mguu wake na gari lake kwa bahati mbaya wakati akienda kutangaza Kikosi chake cha mwisho cha Wachezaji 22 wa Fainali za Kombe la Dunia.
Mpigapicha huyo alipondwa na Gari la Maradona alipokuwa akiingia nalo ndani ya Viwanja vya Mazoezi vya Chama cha Soka cha Argentina Mjini Buenos Aires, Argentina.
Mara baada ya kumuunda Mpigapicha huyo, Maradona akamtukana na kuhoji kwanini aliweka mguu wake chini ya tairi.
Mpigapicha huyo alipewa huduma ya kwanza hapohapo kisha kukimbizwa Hospitalini.
Grant atimka Pompey
Avram Grant ameachia ngazi kama Meneja wa Portsmouth na kuna tetesi huenda akatua West Ham.
Ingawa Portsmouth imeshushwa Daraja toka Ligi Kuu kwa kumaliza ikiwa mkiani Msimu uliokwisha Mei 9, Grant aliipeleka Timu hiyo, iliyokumbwa na balaa kubwa la kifedha na hata kunusurika kuwa mufilisi na kuwekwa chini ya Msimamizi maalum, Fainali za Kombe la FA na kutolewa kwa mbinde na Mabingwa wa England, Chelsea, kwa bao 1-0 Mei 15.
Grant alichukuwa wadhifa wa Meneja toka kwa Paul Hart Novemba mwaka jana lakini Klabu ikaingia kipindi kigumu cha fedha na mwishowe kupokwa pointi 9 na Wasimamizi wa Ligi Kuu kwa kuwekwa chini ya Msimamizi maalum ili kuinusuru isifilisiwe.
Grant ametoa shukrani zake za dhati kwa Mashabiki wa Pompey na amesema Klabu hiyo ilimfanya ajisikia nyumbani wakati yuko mbali na kwao Uyahudi.
Grant alisema: “Siwezi kulipa imani na fadhila za Mashabiki, Wachezaji na Wafanyakazi wa Pompey! Nawashukuru sana kwa kunipa nafasi na heshima ya kuwa sehemu ya Mji wenu spesheli na Klabu hii iliyotukuka!”

Thursday 20 May 2010

Spain yatangaza Mtu 23 kwa Fainali Kombe la Dunia
Kocha wa Spain Vicente del Bosque ametangaza Kikosi chake cha mwisho cha Wachezaji 23 cha Fainali za Kombe la Dunia na majina hayo yatawsilishwa FIFA.
Kila Nchi itakayocheza Fainali hizo huko Afrika Kusini kuanzia Juni 11 zimetakiwa kufikisha FIFA Vikosi vyao vya Wachezaji 23 si zaidi ya terehe 1 Juni.
Katika Kikosi hicho wapo Mastaa Cesc Fabregas, Andres Iniesta na Fernando Torres ambao wote ni majeruhi.
Pia wamo Wachezaji watatu ambao hawajawahi kuichezea Spain nao ni Kipa Victor Valdes na Pedro wa Barcelona na Javi Martinez wa Athletic Bilbao.
Spain wapo Kundi H pamoja na Uswisi, Chile na Honduras na mechi yao ya kwanza ni Mjini Durban Juni 16 watakapocheza na Uswisi.
Spain wanategemea kucheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya Saudi Arabia, Korea Kusini na Poland kabla kwenda Afrika Kusini.
Kikosi kamili:
MAKIPA: Iker Casillas (Real Madrid), Jose Manuel 'Pepe' Reina (Liverpool), Victor Valdes (Barcelona).
WALINZI: Raul Albiol (Real Madrid), Alvaro Arbeloa (Real Madrid), Joan Capdevila (Villarreal), Carlos Marchena (Valencia), Gerard Pique (Barcelona), Carles Puyol (Barcelona), Sergio Ramos (Real Madrid).
VIUNGO: Xabier Alonso (Real Madrid), Sergio Busquets (Barcelona), Cesc Fabregas (Arsenal), Andres Iniesta (Barcelona), Javier Martinez (Athletic Bilbao), David Silva (Valencia), Xavi Hernandez (Barcelona).
MAFOWADI: Jesus Navas (Sevilla), Juan Manuel Mata (Valencia), Pedro Rodriguez (Barcelona), Fernando Llorete (Athletic Bilbao), Fernando Torres (Liverpool), David Villa (Valencia).
Sevilla yanyakua Copa del Rey
Atletico Madrid 0 Sevilla2
Jana Sevilla waliweza kuwafunga Atletico Madrid 2-0 Uwanja wa Nou Cam katika Fainali ya Kombe la Mfalme huko Spain, maarufu kama Copa del Rey.
Mabao ya Sevilla yalifungwa na Diego Capel dakika ya 5 na la pili na Jesus Navas kwenye dakika ya 90.
Webb kuchezesha Fainali ya UEFA
Refa wa Ligi Kuu Howard Webb ndie atakaechezesha Fainali ya Jumamosi ya UEFA CHAMPIONS LIGI huko Stadio Santiago Bernabeau kati ya Inter Milan na Bayern Munich.
Refa huyu mwenye miaka 38 pia yumo kwenye Kundi la Marefa watakaochezesha Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini.
Msimu huu, Webb amechezesha mechi 6 za UEFA CHAMPIONS LIGI ikiwemo ile ya Robo Fainali ya kwanza kati ya Inter Milan na CSKA Moscow.
Webb atasaidiwa na Waingereza wenzake Michael Mullarkey na Darren Cann na Refa wa 4 [wa Akiba] Martin Atkinson.
Villa wakataa Pauni Milioni 20 kwa Milner
Aston Villa wameikataa ofa ya Pauni Milioni 20 ya Manchester City ya kumnunua Mchezaji wao James Milner ambae sasa yupo Kikosi cha England kilichopiga Kambi huko Austria kwa ajili ya Kombe la Dunia
Klabu ya Aston Villa imesema imekataa ofa hiyo kwa vile wanataka kukaa chini na Milner mara baada ya Kombe la Dunia kumalizika ili kuuboresha na kuurefusha Mkataba wa Milner.
Hivi karibuni, Milner, mwenye miaka 24, ndie alieshinda Tuzo ya PFA ya Mchezaji Bora Kijana kwa Msimu wa 2009/10 na alinunuliwa na Villa toka Newcastle mwaka 2008 kwa Pauni Milioni 12 kwa Mkataba wa Miaka minne.
Bifu la Boateng na Ballack
Kiungo wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng amedai Michael Ballack alimzaba kibao na hilo ni jambo baya kupita rafu aliyocheza yeye na kumuumiza na kumkosesha Fainali za Kombe la Dunia.
Ballack ameripotiwa kumlaumu sana Boateng ambae alizaliwa Ujerumani na kuichezea Nchi hiyo Timu zake za Vijana lakini kwenye Kombe la Dunia ameamua kuchezea Ghana ambako Baba yake ndiko anakotoka.
Boateng amedai Ballack analalamika sana lakini amesahau kuwa yeye Ballack aliwahi kupigwa kibao na Mchezaji mwenzake wa Ujerumani Lukas Podolski na akaligeuza tukio hilo nongwa kwa kulalamika kwa wiki kadhaa.
Boateng amesema inashangaza kumwona Ballack akilalamikia kitu ambacho yeye mwenyewe ni kawaida kufanya.
Boateng vilevile amemponda Kocha wa Ujerumani Joachim Low kwa kusema rafu ya Boateng kwa Ballack ilistahili Kadi Nyekundu.
Boateng amehoji: “Nikisikia hilo naona wao ni ndumilakuwili! Je Nahodha wake anaweza kumzaba mtu amtakae kibao na asichukuliwe hatua? Ningefanya mimi hilo ningefungiwa kwa miaka! Ndio maana nimegoma kuchezea Ujerumani na kuichagua Ghana!”
Ghana na Ujerumani zipo Kundi D kwenye Fainali za Kombe la Dunia na zitacheza Juni 23 Mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kingine chenye mvuto kwenye sakata la Boateng na Ujerumani ni kuwa mdogo wake, Beki Jerome Boateng, yupo kwenye Kikosi cha Ujerumani.

Wednesday 19 May 2010

Barca wamnasa Villa
David Villa atatangazwa rasmi kama Mchezaji wa Barcelona siku ya Ijumaa baada ya kufanikiwa kumnunua kutoka Valencia kwa dau la Pauni Milioni 34.
Villa, miaka 28, amesaini Mkataba wa Miaka minne na Barcelona na kesho atapimwa afya yake.
Mchezaji huyo ambae ni mmoja wa Mastaa wakubwa wa Spain ameongeza joto kwa Mafowadi wa Barca hasa Thierrry Henry ambae sasa anaonekana kama ziada.
Man United kuchukua Mchezaji mmoja tu!!
Sir Alex Ferguson amepasua kuwa Manchester United inategemea kuongeza Mchezaji mmoja tu kabla Msimu ujao haujaanza na kauli hii imezua mjadala kwa Wadau wanaohisi Wamarekani Wamiliki wa Klabu hiyo, Familia ya Glazer, haitaki kutoa bulungutu kununua Wachezaji.
Hata hivyo, David Gill, Mkurugenzi Mtendaji, amekanusha hayo na kusema fedha zipo wakati wowote ule ila tatizo ni Soko la Wachezaji kupotoshwa kwa kupandishwa bila msingi thamani za Wachezaji.
Tayari Manchester United imeshawachukua kwa ajili ya Msimu ujao Wachezaji Chipukizi kutoka Mexico, Javier Hernandez, na Beki wa Fulham, Chris Smalling.
Ferguson ametamka: “Soko la sasa ni gumu lakini hata hivyo Kikosi chetu kina uwiano mzuri na kuna Vijana wengi tu!”
Kugushia wakati wa penalti marufuku!
Wapigaji penalti kuanzia sasa hawaruhusiwi kukimbia kisha kugushi na kusimama wakifika kwenye mpira na kisha kuupiga na Mchezaji akifanya hivyo atatwangwa Kadi ya Njano na penalti kurudiwa.
Mabadiliko hayo yamefanywa na Bodi ya Chama cha Soka cha Kimataifa [IFAB=The International Football Association Board] ambao ndio wenye mamlaka ya kubadili sheria za Soka na Bodi hiyo hujumuisha FIFA pamoja na Vyama vya Soka vya England, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini ambao ndio Waanzilishi wa Soka Duniani.
FIFA imesema Mchezaji anaruhusiwa kugushi akiwa anakimbia lakini akifika kwenye mpira haruhusiwi.
Vilevile, IFAB imesema Yule Refa wa 4 [Refa wa Akiba] ambae kawaida husimamia ubadilishaji Wachezaji, nyongeza ya muda na kuzuia benchi la kila Timu kuingilia mchezo, sasa ataruhusiwa kuingia Uwanjani kumsaidia Refa katika maamuzi wakati wa mchezo.
Mabadiliko haya yanategemewa kuonekana kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini.

Tuesday 18 May 2010

Fabregas awambia Ze Gunners naenda Barca!
Kuna ripoti zimeibuka kwamba Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas leo amemjulisha Meneja wake Arsene Wenger anataka kuondoka kurudi Timu yake ya utotoni FC Barcelona.
Fabregas, ambae yuko Spain akitibiwa goti lake, inasemekana leo aliongea na simu na Wenger.
Habari za kutaka kuondoka kwa Mchezaji huyo zimepata nguvu zaidi baada ya Makamu wa Rais wa Barcelona, Rafael Yuste, kuongea na Radio Ona FM ya huko Spain na kusema kuwa Fabregas amewajulisha azma yake kuhama Arsenal.
Hata hivyo Yuste alikiri suala la Fabregas lazima likubaliwe na Klabu zao mbili ingawa alikiri mazungumzo yanaenda vizuri.
Fabregas alianza Soka lake pamoja na Lionel Messi kwenye Timu ya Vijana ya Barcelona na akahamia Arsenal Septemba 2003.
Kipa wa Man United auzwa Birmingham
Kipa wa Manchester United Ben Foster, miaka 27, leo alitegemewa kupimwa afya yake huko Birmingham ili kukamilisha uhamisho wake baada ya Man United kulikubali dau la Pauni Milioni 6.
Birmingham wamelazimika kumchukua Foster kufuatia kuondoka kwa Kipa wao namba moja Joe Hart ambae walimchukua kwa mkopo kutoka Manchester City kurudi Klabuni kwake.
Nae Foster amelazimika kuhama Man United baada ya kukosa namba ya kudumu huko Man United ambako aliuanza Msimu wa 2009/10 vizuri tu alipopata mamba kufuatia kuumia kwa Kipa namba moja Edwin van der Sar lakini akawa anafanya makosa uwanjani hasa kwenye mechi za Ligi Kuu dhidi ya Manchester City na Sunderland na alipopona Van der Sar akapigwa tena benchi na hilo limemfanya aikose namba kwenye Kikosi cha England cha Kombe la Dunia.
Neville ahoji uteuzi wa Capello
Gary Neville ameutia walakin uteuzi wa Kocha wa England Fabio Capello hasa kwa kumchukua Beki mmoja tu wa kulia Glen Johnson wa Liverpool katika Kikosi chake kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Neville amesema: “Nashangaa kuona Beki mmoja tu wa kulia!”
Kwa mtazamo wa Neville, yeye alitaka achukuliwe Mchezaji mwenzake wa Manchester United Wes Brown ambae pia hucheza kama Beki wa Kulia lakini Capello amemchukua Sentahafu wa Liverpool, Jamie Carragher, ambae pia huweza kucheza kama Beki wa Kulia.
Carragher alikuwa ameshaamua kustaafu kucheza mechi za Kimataifa lakini Capello akamshawishi kurudi kilingeni.
Hata hivyo, Capello alishindwa kumshawishi Kiungo wa Man United, Paul Scholes, aliestaafu arudi kuchezea England tena.
Neville aliongeza: “Binafsi sijuti kukosa kuitwa ingawa nilidhani kuna nafasi ya hilo lakini nadhani kutochukuliwa Wes Brown kunashangaza!”
Neville ameshaichezea England mara 85.
Boateng amtaka radhi Ballack kumkosesha Kombe la Dunia
Kiungo wa Portsmouth Kevin-Prince Boateng amemwomba radhi Nahodha wa Ujerumani kwa kumuumiza na hata kumsababisha akose Kombe la Dunia.
Boateng alimuumiza Ballack katika Fainali ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Portsmouth Jumamosi iliyopita.
Boateng ametamka: “Sina cha kufanya ila kumwomba radhi tu. Niliuchelewa mpira na nikamvaa. Nilimwomba radhi mara mbili Uwanjani!”
Ingawa amezaliwa na kuwahi kuzichezea Timu za Taifa za Vijana za Ujerumani, Boateng ameamua kuchezea Ghana ambako Baba yake anatoka lakini mdogo wake, Jerome Boateng, ni Mchezaji wa Ujerumani.
Kwenye Fainali za Kombe la Dunia, Ujerumani na Ghana, zimo Kundi moja.
Mwenyewe Ballack amekaririwa akisema: “Nimechukizwa na kuvunjika moyo. Sitaki kusema chochote. Inaumiza roho kwa vile Kombe la Dunia lipo karibu lakini hii ni Soka na maisha yanaendelea!”
Chamakh atua London, yuko mezani na Ze Gunners
Marouane Chamakh yupo Jijini London kujadiliana na Arsenal kuhusu maslahi yake ili ajiunge nao kufuatia kumalizika kwa Mkataba wake na Klabu ya Ufaransa Bordeaux ambao unamfanya awe Mchezaji huru.
Mchezaji huyo wa Kimataifa toka Morocco, mwenye umri wa miaka 26, amekuwa akiripotiwa atajiunga na Arsenal tangu Msimu uliopita.
Chamakh, ambae ni Fowadi, ataacha majonzi huko Bordeaux kwani Klabu hiyo ilijaribu sana kuongeza Mkataba wake lakini walishindwa.
Rais wa Bordeaux Jean-Louis Triaud amelalamika: “Tulijaribu kuongeza Mkataba wake. Yeye amesema hajaongea na Wenger lakini ajabu anajiunga na Klabu bila kuongea na Wenger! Tangu niwe hapa nimepata matatizo kwenye uhamisho wa Wachezaji wawili, Wiltord na Chamakh, na wote wanahamia Arsenal!”
Hata hivyo Triaud amesema anamtakia kila la heri Chamakh kwani ni Kijana mzuri na Mpiganaji hodari.
Nyota AC Milan kucheza bureeeeee!!
Difenda wa AC Milan, anaechezea USA, Oguchi Onyewu, ameipa ofa Klabu yake AC Milan ya kucheza mwaka mmoja bure bila malipo ikiwa kama fidia ya kushindwa kucheza Msimu wote wa 2009/10 kwa sababu ya kuumia goti na ofa hiyo imekubaliwa.
Onyewu, miaka 28, alijiunga na AC Milan kutoka Standard Liege na akacheza mechi moja tu kisha akaumia goti katika mechi ya mchujo wa Kombe la Dunia kati ya Nchi yake USA na Costa Rica.
Mkataba wa Mchezaji huyo na Milan ulikuwa ni wa miaka mitatu na unatakiwa kumalizika 2012 lakini mwaka mmoja mzima kati ya hiyo mitatu alishindwa kucheza na hivyo kwa ridhaa yake mwenyewe ameomba nyongeza ya kuanzia Juni, 2012 hadi Juni, 2013 acheze bure.
Onyewu sasa amepona na yumo kwenye Kikosi cha USA cha Kombe la Dunia linaloanza Afrika Kusini Juni 11.
FIFA kumchunguza kibopa toka England
Kamati ya Maadili ya FIFA itachunguza kauli zinazodaiwa kutolewa na Lord Triesman aliekuwa Kiongozi wa Maombi ya England kuwa Mwenyeji Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 na pia wa FA ya England, nyadhifa ambazo zote amelazimika kujiuzulu kufuatia kuvuja kwa kauli hizo zinazodaiwa alizitoa kuhusu rushwa kwa Vyama vya Soka vya Spain na Urusi kuhusiana na uombaji wa kuwa Wenyeji wa Kombe la Dunia.
Jumapili iliyopita FA ilimbadili Lord Triesman na kumweka Geoff Thompson kama Mwenyekiti wa FA England.
Geoff Thompson ni Makamu wa Rais wa FIFA.
Inadaiwa Lord Triesman alimwambia Msaidizi wake mmoja wa zamani kuwa Spain inapanga kuwahonga Marefa kwenye Fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu na wataisaidia Urusi kushinda Uenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2022 ikiwa Urusi itaisaidia Spain kufanikisha wao kuwa Wenyeji mwaka 2018.
Kamati ya Maombi ya Uenyeji wa Kombe la Dunia ya England imeshapeleka kwa Vyama vya Soka vya Spain na Urusi taarifa za kuomba radhi kwa mkanganyiko uliotokea.

Monday 17 May 2010

CAS yasema Ribery ng’o Fainali UEFA!!!
Winga wa Bayern Munich Franck Ribery ataikosa Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI Jumamosi hii inayokuja, Mei22, wakati Timu yake itakapokutana na Inter Milan baada ya Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, CAS [Court of Arbitration for Sports] kuitupilia mbali rufaa yake ya kupinga kufungiwa mechi 3 adhabu aliyopewa na UEFA.
Ribery alitolewa nje kwa Kadi Nyekundu kwenye mechi ya Nusu Fainali kati ya Bayern Munich na Lyon alipomchezea rafu mbaya Lisandro Lopez na baadae UEFA ikamfungia mechi 3 lakini akakata rufaa UEFA ambayo iliitupa rufaa hiyo na ndipo akaamua kukata kwenda CAS.
CAS imetangaza uamuzi huo leo kutoka Makao Makuu yao Nchini Uswisi baada ya Jopo la Watu watatu kupitia rufaa hiyo lakini imesema sababu za kuikataa rufaa hiyo zitatangazwa baada ya siku chache.
Jopo lilikuwa na Bernhard Welten, kama Rais, Dr Stephan Netzle na Dr Andras Gurovits wote raia wa Uswisi.
Ballack bai bai Kombe la Dunia
Nahodha wa Ujerumani Michael Ballack hatacheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini zinazoanza Juni 11 baada ya kuthibitishwa enka aliyoumia kwenye Fainali ya FA Cup hapo Jumamosi Chelsea walipoifunga Portsmouth 1-0 inahitaji wiki 8 ili apone na kuanza mazoezi.
Ballack aliumizwa na Mchezaji wa Portsmouth, Kevin-Prince Boateng, ambae ni mzaliwa wa Ujerumani lakini Baba yake anatoka Ghana na yeye mwenyewe ameamua kuchezea Ghana kwenye Fainali hizo za Kombe la Dunia na ameribakiwa na FIFA kuichezea Ghana licha ya kucheza Timu za Taifa za Vijana za Ujerumani.
Kwenye Fainali hizo za Kombe la Dunia Ujerumani na Ghana wapo Kundi D pamoja na Serbia na Australia.
Ancelotti ataka kudumu Chelsea
Carlo Ancelotti anapendelea abaki Chelsea kwa muda mrefu kufuatia kuiongoza kushinda Makombe mawili kwa mpigo Msimu uliokwisha majuzi, Makombe ya Ligi Kuu na FA.
Ancelotti amesema: “Ikiwa kila Msimu utakuwa kama huu uliopita ningependa nikae miaka 10! Niko tayari kusaini Mkataba mpya!”
Mtaliana huyo ambae alikaa na AC Milan kwa miaka minane amekiri kuongoza England ni kazi rahisi mno kwani hupewa kila kitu na ushirikiano mkubwa.
Kuhusu Msimu ujao, Ancelotti amesema mpaka sasa hajajua aongeze Wachezaji gani na wa idara ipi hasa kwa vile Wachezaji majeruhi wa muda mrefu, Jose Bosingwa na Michael Essien, watarudi upya uwanjani baada ya kupona.
Pia, Ancelotti amepinga tetesi kuwa Frank Lampard yumo mbioni kuhama Chelsea na ameng’ang’ania kuwa Lampard atabaki Klabuni hapo.
Ufaransa yapunguza Kikosi cha Kombe la Dunia
Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech amekipunguza Kikosi alichokitangaza wiki iliyopita kutoka Wachezaji 30 hadi 24 na ameahidi kutaja Timu yake ya Wachezaji 23, wanaotakiwa kuwasilishwa FIFA ifikapo Juni 1, Mei 27.
Wachezaji 6 waliopigwa panga ni Hatem Ben Arfa wa Marseille, Kipa Mickael Landreau na Beki Adil Rami, wote wa Lille, na Wachezaji watatu toka Rennes, Rod Fanni, Yann M’Vila na Jimmy Briand.
Timu hiyo inategemewa kuanza mazoezi Ufaransa kisha kwenda kupiga kambi Nchini Tunisia.
Ufaransa ipo Kundi A pamoja na Mexico, Afrika Kusini na Uruguay.
Kikosi kamili:
MAKIPA: Hugo Lloris (Lyon ), Steve Mandanda (Marseille), Cedric Carrasso (Bordeaux);
WALINZI: Eric Abidal (Barcelona), Gael Clichy, William Gallas, Bakary Sagna (Wote wa Arsenal), Patrice Evra (Manchester United ), Marc Planus (Bordeaux), Anthony Reveillere (Lyon), Sebastien Squillaci (Sevilla);
VIUNGO: Abou Diaby (Arsenal), Lassana Diarra (Real Madrid), Alou Diarra, Yoann Gourcuff (Wote toka Bordeaux), Florent Malouda (Chelsea), Franck Ribery (Bayern Munich ), Jeremy Toulalan (Lyon);
MASTRAIKA: Nicolas Anelka (Chelsea), Thierry Henry (Barcelona), Andre-Pierre Gignac (Toulouse), Sidney Govou (Lyon), Djibril Cisse (Panathinaikos), Mathieu Valbuena (Marseille).
LA LIGA: Barca Bingwa!!
FC Barcelona waliitandika Real Valladolid bao 4-0 na kuwashusha Daraja na pia wao kutwaa Ubingwa wa Spain kwa mara ya pili mfululizo huku Wapinzani wao wa jadi, Real Madrid, wakitoka sare na Malaga kwa bao 1-1.
Barcelona waliianza mechi hii wakiwa nyumbani Nou Camp kwa mchecheto pengine wakijua ni lazima washinde ili wawe Mabingwa, walituliza boli pale Luis Prieto alipojifunga mwenyewe na kuwapa Barce bao la kwanza.
Kisha Pedro Rodriguez akapachika bao la pili na kuifanya Barca iwe 2-0 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili, Barcelona waliongeza bao mbili kupitia Staa Lionel Messi na kuifanya iibuke na ushindi mnono wa 4-0 na Ubingwa wa La Liga.
Huko Malaga, Real Madrid walilazimishwa sare ya 1-1 ambayo iliwanusuru Malaga kushushwa Daraja na pia kufanya kibarua cha Kocha wa Real, Manuel Pellegrini, kiwe kwenye utata mkubwa.
Kabla kuanza Msimu huu uliokwisha jana, Real Madrid walitumia zaidi ya Pauni Milioni 200 kuwanunua Nyota Cristiano Ronaldo, Kaka, Karim Benzema na Xabi Alonso lakini mwishoni mwa Msimu wameambulia patupu.
Real Madrid imethibitisha watakaa chini na kuangalia nini cha kufanya.
Timu ambazo zimeporomoka Daraja kutoka La Liga ni Real Valladolid, Tenerife na Xerez.
Kombe la Mataifa Afrika kuchezwa Miaka Tasa!
CAF imethibitisha kuwa kuanzia Mwaka 2013, Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitafanyika katika Miaka isiyogawanyika ili isiwe ikichezwa Mwaka mmoja pamoja na Fainali za Kombe laDunia.
Mabadiliko haya yanamaanisha Fainali za 2012 ambazo zitachezwa kwa pamoja katika Nchi mbili, Gabon na Equtorial Guinea, zitafuatiwe na zile zitakazochezwa Libya Mwaka 2013 hii ikiwa ni baada ya miezi 12 tu badala ya kila Miaka miwili kama ilivyo kawaida na baada ya hapo Fainali nyingine zitakuwa Mwaka 2015.
CAF pia imetangaza kuwa yale Mashindano kwa Wachezaji wa Ndani ya Nchi, CHAN [Championship of African Nations], yatakuwa yakifanyikakila baada ya Miaka miwili katika miaka inayogawanyika na mbili kuanzia Fainali za Libya Mwaka 2014 na Fainali inayofuata itakuwa 2016.
Fainali za Kombe la Afrika, tangu 1968, zimekuwa zikifanyika kila Miaka miwili ingawa Mashindano ya kwanza yalifanyika Sudan 1957.

Sunday 16 May 2010

SERIE A: Inter Milan Bingwa!!
Jose Mourinho leo ameiongoza Timu yake Inter Milan kutwaa Kombe kubwa la pili Msimu huu, la kwanza likiwa Coppa Italia wiki iliyokwisha, na leo wameutwaa Ubingwa baada ya kuifunga Siena bao 1-0 kwa bao la dakika ya 57 Mfungaji akiwa Diego Alberto Milito.
Jumamosi ijayo Inter wanaweza kutwaa Kombe la 3 wakiifunga Bayern Munich kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI inayochezwa huko Madrid, Spain Uwanja wa Real Madrid, Santiago Bernabeau.
Wapinzani wao wa karibu kwenye SERIE A, AS Roma, wameifunga Chievo Verona bao 2-0 na hivyo kushika nafasi ya 2.
MATOKE0 MECHIZA LEO:
Parma 4 Livorno 1
Cagliari 1 Bologna 1
Catania1 Genoa 0
Chievo Verona 0 AS Roma 2 [41, Mirko Vucini & 45 Daniele De Rossi]
Siena 0 Inter Milan 1 [57, Diego Alberto Milito]
AS Bari 2 Fiorentina 0
Atalanta 1 Palermo 2
Sampdoria 1 Napoli 0
LA LIGA: Leo kindumbwendumbwe!!
Barcelona v Real Valladolid na Malaga v Real Madrid
Huko Spain, leo kuanzia saa 2 usiku saaza bongo, mechi za mwisho za La Liga zitachezwa na mechi zenye mvuto mkubwa ni zile za FC Barcelona watakapo wakaribisha Real Valladolid Uwanjani Nou Camp na ile ya ugenini ya Real Madrid wanaosafiri kwenda kucheza na Malaga ambazo ndizo zitaamua Bingwa ni nani.
Barcelona wako pointi moja mbele ya Real Madrid na wakishinda mechi yao watafanikiwa kutetea tena Ubingwa wao lakini hata wakifungwa na ikiwa Real atatoka sare Timu hizo zitalingana pointi lakini kwa sheria za Spain Barcelona atakuwa Bingwa kwa vile tu Timu hizo zilipokutana mara zote mbili kwenye Ligi Barca aliibuka Mshindi.
Powered By Blogger