Saturday, 22 May 2010

Rafa atetea rekodi yake Liverpool, ageuka Mhasibu!!
Rafael Benitez amejitetea kuhusu rekodi yake Klabuni Liverpool huku tetesi zikizidi kumwandama kuwa yuko mbioni kuihama Timu hiyo.
Benitez amehusishwa na kuhamia Klabu kadhaa ikiwemo Inter Milan ambayo Meneja wake Jose Mourinho anadaiwa atakwenda Real Madrid kwa Msimu ujao.
Ingawa mwenyewe Benitez anadai bado yuko na furaha kubakia Anfield lakini Wadau wanamkandya kufuatia Msimu mbovu waliomaliza wakiwa nafasi ya 7 kwenye Ligi Kuu na hivyo kukosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao.
Lakini Benitez bado anang’ang’ania utawala wake hapo Liverpool ni wa mafanikio na amesema: “Kuna hoja hatujashinda Vikombe vingi. Chelsea na Man United wameshinda Vikombe 10 kila mmoja katika miaka 6 nikiwa hapa Liverpool. Arsenal, Spurs na Portsmouth Kikombe kimoja moja tu. Liverpool wameshinda Vikombe Vinne na tumefika Fainali 3 nyingine!”
Benitez amepuuza hoja ya kuwa Liverpool yake haijachukua Ubingwa wa England kwa kudai hilo si lazima.
Vilevile, amedai Nchini England Mameneja wanakosa uwezo wa kuamua kuhusu Bajeti na ununuzi wa Wachezaji na hilo ndio jibu lake kwa tuhuma juu yake za kuwa katika wakati wake hapo Liverpool ametumia zaidi ya Pauni Milioni 280 kununua Wachezaji bila mafanikio ya kuwa Bingwa wa England.
Benitez anadai ametumia Pauni Milioni 220 tu lakini pia ameuza Wachezaji na kuingiza Pauni Milioni 160 na hivyo ni Pauni Milioni 60 tu ndizo alizotumia kununua Wachezaji katika Miaka yake 6 ya Umeneja hapo Anfield.
Anasema: “Ukichukua mapato tuliyovuna wakati tunacheza UEFA CHAMPIONS LIGI ya Pauni Milioni 120 katika kipindi hicho cha Miaka 6 ni wazi nimeleta faida ya Pauni Milioni 60!”

No comments:

Powered By Blogger