Muda: Jumamosi, Mei 22 saa 3 dakika 45 usiku
Wakati Bayern Munich wanasaka Taji lao la 5 la Ulaya, Inter Milan wanatafuta Taji lao la kwanza la Ulaya katika Miaka 45.
Msimu huu, kwenye michuano hii ya UEFA CHAMPIONS LIGI, Bayern Munich tayari wameshazifunga Timu mbili za Italia, Juventus na Fiorentina.
Washindani hawa wanaongozwa na Makocha Stadi huko Ulaya ambao wakati mmoja waliwahi kuwa pamoja.Kocha machachari na mwenye vituko wa Inter Milan, Jose Mourinho, aliwahi kuwa Msaidizi wa Kocha wa Bayern Munich Louis van Gaal huko Barcelona kati ya Mwaka 1997 na 2000.
Makocha wote hao wawili wameshawahi kulitwaa Kombe hili la UEFA na yeyote atakaeshinda atakuwa ameingia kwenye kile Kitabu maalum cha kulishinda Kombe hilo wakiwa na Vilabu tofauti.
Inter Milan na Bayern Munich zimeshakutana mara 4 huko Ulaya na mara ya mwisho ilikuwa ni Msimu wa 2006/7 kwenye Makundi ya UEFA CHAMPIONS LIGI walipotoka sare 1-1 huko Munich kwa bao la dakika za mwishini la Patrick Viera kuiokoa Inter.
Katika mechi ya kwanza Msimu huo, Bayern ilishinda 2-0.
Mwaka 1988/9, katika Kombe la UEFA, Inter waliifunga Bayern 2-0 huko Ujerumani lakini Bayern wakaipiga Inter 3-1 huko Italia na kusonga kwa mabao ya ugenini.
Katika Fainali za Ulaya, rekodi ya Bayern ni ushindi mara 4 na kufungwa 3.
Walishinda Fainali hizo dhidi ya: Atletico Madrid [1974], Leeds United [1975], St-Etienne [1976], Valencia [2001].
Walifungwa: Aston Villa [1982], FC Porto [1987], Manchester United [1999].
Bayern Munich pia wameshashinda Ulaya Makombe mengine ikiwa Mwaka 1967 Kombe la Washindi la UEFA na Mwaka 1996 UEFA CUP.
Inter Milan watakuwa wakiomba washinde Kombe lao la kwanza Ulaya tangu waifunge Benfica Mwaka 1964.
Lakini, Mwaka 1967 walifungwa na Celtic na 1972 walitolewa na Ajax.
Inter wameshashiriki Fainali 4 za UEFA CUP na kushinda za Miaka ya 1991, 1994 na 1998 na kufungwa ile ya Mwaka 1997.
MASTAA NJE
Timu zote, Inter na Bayern, zitawakosa Wachezaji wao muhimu ambao wanatumikia kifungo baada ya kulambwa Kadi.
Inter watamkosa Thiago Motta na Bayern hawatakuwa na Mfaransa Franck Ribery waliediriki kukata Rufaa hadi CAS, Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, ambako Rufaa hiyo ilibwagwa.
REKODI
Ikiwa Bayern Munich watatwaa Kombe, watajumuika na Liverpool kwa kulitwaa mara 5 na kufungana pamoja kwa kuwa Timu za 3 nyuma ya AC Milan waliotwaa mara 7 na vinara Real Madrid walioshinda mara 9.
Vikosi vinavyotegemewa:
Bayern Munich: (Fomesheni 4-4-2) Butt; Lahm, Badstuber, Van Buyten, Contento; Altintop, Van Bommel, Schweinsteiger, Robben; Olic, Muller.
Inter Milan: (Fomesheni 4-2-3-1) Cesar; Maicon, Lucio, Samuel, Zanetti; Cambiasso, Pandev; Eto’o, Sneijder, Chivu; Milito.
Refa: Howard Webb (England).
No comments:
Post a Comment