Ze Gunners hawajateta na Barca kuhusu Fabregas
Arsenal wametamka hawajazungumza lolote na Barcelona kuhusu uhamisho wa Nahodha wao Cesc Fabregas ambae yuko kambini na Timu ya Spain iliyo kwenye matayarisho ya Kombe la Dunia.
Wiki hii kumekuwa na taarifa kuwa Barcelona, ambao wamekuwa wakimwinda Fabregas kwa muda mrefu, wameongeza kasi baada ya kuripotiwa Fabregas mwenyewe amemjulisha Wenger nia yake ya kuhamia Barcelona.
Mchezaji huyo mwenye miaka 23 alianza Soka lake na Timu za Vijana huko Nou Camp na kuhamia Arsenal akiwa tineja ambako kipaji chake kiliongezeka maradufu chini ya Wenger.
Lakini, kufuatia Msimu mwingine tena ambao Ze Gunners wametoka kapa, inadaiwa Fabregas amechoshwa na anataka kuhama huku kukiwa na ripoti kuwa Arsenal watamruhusu ikiwa Barcelona watatoa Pauni Milioni 39.
Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood, ameeleza wao hawajasikia chochote toka Barcelona.
Fergie: Berbatov si biashara!
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesisitiza Klabu yao haina nia ya kumuuza Straika Dimitar Berbatov kama inavyovumishwa na Vyombo vya Habari.
Ferguson ametamka: “Hapana hauzwi! Ni Mchezaji mzuri sana na atakuwa nasi Msimu ujao.”
Ferguson amesema tetesi zinazozagaa kila siku ni tatizo kwa Klabu kubwa kama yao kwa vile Wadau wana matarajio mengi na Vyombo vya Habari siku zote vinawakazia macho.
Binafsi, Berbatov ameshatamka yeye atabaki Manchester United na kupigania namba yake kwa vile kuna uwezekano mkubwa Man United ikaongeza Straika mmoja.
MECHI YA PAUNI MILIONI 90: Blackpool v Cardiff City
Kesho Uwanjani Wembley zitashuka Timu mbili za Daraja la Coca Cola Championship, Blackpool na Cardiff City, ambazo ndizo ziko Fainali ya Mchujo maalum kupata Timu moja itakayoungana na Newcastle United na West Bromwich Albion kucheza Ligi Kuu England Msimu ujao.
Newcastle na WBA zilimaliza Ligi ya Coca Cola Championship zikiwa nafasi za kwanza na za pili na hivyo kuingia Ligi Kuu moja kwa moja lakini Timu za nafasi za 3 hadi za 6, yaani Blackpool, Cardiff, Leicester na Nottingham Forest, zilicheza Mchujo maalum na Blackpool na Cardiff ndizo zimetinga Fainali.
Blackpool waliwatoa Nottingham kwa jumla ya bao 6-4 katika mechi mbli na Cardiff waliwabwaga Leicester kwa penalti 4-3 baada ya mechi mbili kwisha kwa sare ya jumla ya bao 3-3.
Fainali hii ya Blackpool v Cardiff City imebatizwa ‘Mechi ya Pauni Milioni 90’ kwa vile Mshindi, yaani Timu itakayopanda Daraja kuingia Ligi Kuu itavuna kitita hicho kama mapato ya kucheza Ligi Kuu.
Mara ya mwisho Blackpool kucheza Ligi ya juu kabisa England ilikuwa Mwaka 1971 ilipocheza Divisheni ya Kwanza.
Na Cardiff nao hawajacheza Ligi ya juu ya England tangu walipocheza Divisheni ya Kwanza Mwaka 1962.
Newcastle, WBA na Mshindi kati ya Cardiff na Blackpool zitachukua nafasi za Burnley, Hull City na Portsmouth zilizoporomka Daraja toka Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment